Na. Furaha Venance
Mwaka 2015
Kazi
hii tumeigawa katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo tutatoa
fasili za usimulizi kwa mujibu wa
wataalamu mbalimbali na namna wataalamu hao wanavyoainisha aina za usimulizi.
Sehemu ya pili ambayo ndiyo kiini cha kazi hii, tutatumia riwaya ya Vuta n’Kuvute
iliyoandikwa na Shafi, A. Shafi kubainisha kauli za usimulizi na usimulizi unaojitokeza
katika riwaya husika. Sehemu ya mwisho itakuwa ni hitimisho.
Usimulizi
umefasiliwa kwa namna mbalimbali na wataalamu tofauti tofauti. Mathalani, Mohochi
(2000:50) akiwanukuu Attenbernd na Lewis (1963) anasema, usimulizi ni mkabala
ambao hutuwezesha kuyatizama yanayotendeka na kusikia yanayozungumzwa katika
kazi ya fasihi. Kanar (2001) akinukuliwa na Burundi na wenzake (2014:74)
anasema kuwa, usimulizi ni mtindo wa mpangilio unaotumiwa na mwandishi wa hotuba,
habari na utanzu wa kibunilizi kuelezea matukio. Mawazo ya mtaalamu huyo
hayapishani sana na mawazo ya Wamitila (2003:325) anayesema kuwa usimulizi ni
uelezeaji wa matukio katika hadithi. Hawa wote wanaona kuwa usimulizi ni namna
ya kuyaeleza matukio katika habari au hadithi.
Kwa
maana hiyo tunaweza kusema, usimulizi ni namna mwandishi anavyotumia kauli
mbalimbali za usimulizi na mbinu za usimulizi katika kuelezea visa na matukio
kwa jinsi alivyopangilia katika bunilizi yake ya riwaya. Ama kuhusu kauli za
usimulizi na mbinu za usimulizi wataalamu mbalimbali wamekuwa wakizitumia dhana
hizi kwa namna moja ingawa kiuhalisia kwa mawazo yetu tunaona kama
zinatofautiana. Kwa mfano, Mazrui na Syambo (1992) akinukuliwa na Burundi na
wenzake (wameshatajwa, 75) wanaeleza aina zifuatazo za usimulizi; Usimulizi wa
mwandishi mwenyewe akitumia viambishi nafsi ya tatu, aina ya pili ni usimulizi
wa mmoja wa wahusika akitumia viambishi vya nafsi ya tatu. Aina ya tatu ni usimulizi wa
mwandishi akitumia viambishi vya nafsi ya tatu. Wakitofautisha aina hii na ile
ya kwanza, wanatueleza kuwa katika aina hii, msimulizi huwa haelezi yale ambayo wahusika
hawayakudhihirisha katika vitendo au maneno, kwa maana kuwa msimulizi anakuwa
hayajui yale yaliyofichika ndani tofauti na aina ya kwanza ambapo msimulizi
anajua kila kitu hata yaliyo mawazoni mwa mhusika. Na aina ya nne wanatueleza
ni usimulizi wa mmoja wa wahusika akitumia viambishi vya nafsi ya kwanza.
Kama
tutachunguza vizuri, aina hizi kama zilivyoainishwa na Mazrui na Syambo,
tutagundua kuwa, aina hizi zinaangukia katika aina za kauli za usimulizi, wao
wamezitaja nne lakini kimsingi zinapaswa kuwa mbili ambazo ni usimulizi wa
kutumia viambishi nafsi ya tatu na usimulizi wa kutumia viambishi vya nafsi ya
kwanza, kwani aina ya kwanza, ya pili na ile ya tatu wamezitenganisha ili hali
zote zina fanana. Zote zinatumia
viambishi nafsi ya tatu hivyo zilitakiwa kuwekwa katika kundi moja kama kauli
ya usimulizi nafsi ya tatu.
Mohochi
(2000:) anaainisha aina tatu za usimulizi ambazo anaziita kama mitindo ya
usimulizi, aina hizo ni, usimulizi maizi pia anauita usimulizi mwakote, aina
nyingine ni usimulizi wa nafsi ya tatu na usimulizi wa nafsi ya kwanza. Wamitila
(2003:325-328) anabainisha aina zifuatazo za usimulizi, usimulizi anuwai,usimulizi
ngazi,usimulizi maizi, usimulizi penyezi au dukizi, usimulizi sawia, usimulizi
tangulizi, usimulizi ki-itimamu, usimulizi wa kiutendi, usimulizi kirejeshi,
usimulizi wa kiutomaji, usimulizi wa nafsi ya pili na usimulizi wa nafsi ya
tatu.
Ama
kwa hakika tukiangalia aina hizi za usimulizi kama zilivyoanishwa na wataalamu
hao ni wazi kuwa wapo wanaona aina za usimulizi ni zile kauli zinazotumia
viambishi vya nafsi na wengine wanachanganya kwa kutumia kigezo cha matumizi ya
viambishi vya nafsi na kigezo ambacho kwetu tunaona ni kigezo cha mitindo ya
usimulizi au usimuliaji kama inavyojitokeza kwa Mohochi naWamitila.
Katika
mjadala huu, tutatumia vigezo vya kauli za usimulizi na mbinu za usimulizi kwa
namna tofauti, tukiwa na maana, kauli za usimulizi ni ule usimulizi wa matukio au
visa katika bunilizi ya hadithi au riwaya kwa kutumia viambishi vya nafsi.
Katika aina hii tunapata kauli zifuatazo za usimulizi, usimulizi kauli nafsi ya
kwanza, usimulizi kauli nafsi ya pili na usimulizi kauli nafsi ya tatu, wakati
mbinu za usimulizi tunaweza kusema kuwa ni namna mwandishi ama mtunzi
anavyotumia mitindo na mbinu mbalimbali za kuyasimulia na kupangilia matukio na
visa kwa namna anayoona inafaa katika bunilizi ya hadithi au riwaya. Katika
aina hii tunapata aina zifuatazo za usimulizi, usimulizi anuwai, usimulizi
ngazi,usimulizi maizi, usimulizi penyezi au dukizi, usimulizi sawia, usimulizi
tangulizi, usimulizi ki-itimamu, usimulizi wa kiutendi, usimulizi kirejeshi na usimulizi
wa kiutomaji (pia angalia Wamitila uk. 325-328 keshatajwa).
Hivyo
basi kwa kutumia riwaya ya Vunta N’kuvute
iliyoandikwa na Shafi Adam Shafi tunaweza kuangalia na kubainisha kauli za
usimulizi na mbinu za usimulizi zinaojitokeza katika riwaya hii. Tukianza na
kauli za usimulizi. Kama tulivyoona hapo awali, kuwa katika kauli za usimulizi
kuna aina tatu za usimulizi, aina zinazojitokeza katika riwaya hii ni:
Kwa
kiasi kikubwa, riwaya hii inatumia kauli ya usimulizi nafsi ya tatu. Mazrui na
Syambo (wameshatajwa,) wanaeleza kuwa, huu ni usimulizi unaomwezesha mtunzi
kusimulia matukio yote pamoja na matokeo yake popote. Aina hii ya usimulizi
hutumia kiambishi awali cha a katika umoja au wa
katika wingi. aina hii ya usimulizi tunaweza kuiona ukurasa wa 1 msimulizi
anaposema;
“Mara tu baada ya kuvunja
ungo, Yasmin aliozwa mume. Alikuwa mume wa jamii yake ya
Ithnasharia ambaye alikuwa akiishi jirani naye hapo Mtendeni.
Alikuwa ni mume asiyelingana naye hata kidogo.”
Hapa
mwandishi anatusimulia juu ya binti mdogo kulazimishwa kuolewa na mzee wa miaka
52. Viambishi vilivyoandikwa kwa hati ya kukolezwa ni viambishi vinvyodokeza
kuwa kauli husika ni kauli simulizi nafsi ya tatu.
Aidha wakati mwingine msimulizi anaweza kumwachia mhusika katikati
ya usumulizi wake naye akatumia kauli simulizi nafsi ya tatu kama
inavyojitokeza katika kazi hii. Mwandishi anapomtumia mhusika Koplo Matata
anaposema;
Denge anakwenda kuvua kama kisingizio tu,
lakini ana mambo anayoyafanya, tena mambo mabaya sana,
mambo ambayo yanaweza kumfanya aende
jela, yeye na kila anayemjua kama vile wewe na Mwajuma (Uk.
99-100).
Usimulizi
wa kauli nafsi ya kwanza pia unajitokeza katika kazi hii ingawa kwa kiasi
kidogo. Wamitila(keshatajwa, uk.327) anaeleza, ni usimulizi wa hadithi
unaofanywa na mhusika kwa nafsi ya kwanza. Mhusika huyo anaweza kuwa mshiriki
wa matukio au matendo ya hadithi au asiwe mshiriki. Mazrui na Syambo
(washatajwa,) wanasema huu ni usimulizi wa mmoja wa wahusika akitumia viambishi
vya nafsi ya kwanza. Kwa kuwa kauli usimulizi nafsi ya kwanza Tofauti na Wamitila
anavyodai kuwa katika kauli hii, msimulizi anaweza kuwa mshiriki wa matukio au
matendo ya hadithi au asiwe mshiriki kwa hakika linahitaji kuangaliwa vizuri. hutumia
viwakilishi au viambishi nafsi vya mimi,
ni, katika umoja na si, sisi na tu katika wingi ni dhahili kuwa
msimulizi ni lazima atakuwa mshiriki wa matendo na matukio katika hadithi
husika.
Tukirejea
katika riwaya yetu ya Vuta n’kuvute, mwandishi kuna sehemu huwaachia wahusika
wake kusimulia au kuelezea na kujieleza ndipo kauli hii nafsi ya kwanza inapojitokeza
kama mwandishi anavyotuambia:
Denge
alikuwa ametulia kimya, anamsikiliza kwa makini kabisa. “Yasmini mimi najua kama
unanipenda, na mimi nakupenda vile
vile, lakini kuna kitu kimoja, (Uk. 145).
Hapa
tunamwona mwandishi anatumia nafsi ya tatu katika kuelezea matukio na matendo
lakini pia anatoa nafasi kwa wahusika kueleza na kusimulia kama tunavyoweza
kuona hapo juu mhusika Denge akimweleza Yasmini.
Kwa
upande mwingine, usimulizi maizi unapewa nafasi na mwandishi. Mohochi (2000:50)
anaeleza kuwa, katika mbinu hii mwandishi huieleza hadithi ambayo mara nyingi
yeye haimhusu; yaani haishiriki lakini, akiwa muumbi wake, anaelewa kila kitu
kinachotendeka hadithini. Mawazo haya ya Mohochi yanaelekea kuungwa mkono na
Wamitila (2003:326) anasema, hii ni aina ya usimulizi unaotambulishwa na
ufahamu wa kila kitu. Katika aina hii ya usimulizi, Msimulizi anakuwa na uwezo wa kupenya na kuingia katika fikra za
wahusika wake na kujua na kutueleza kile wanachowaza, wanachofikiria kukifanya
hata kabla hakidhihirika wazi kwa vitendo. Sifa hizi za usimulizi maizi
Hawthorn (1985) anaona kuwa, huenda mbinu hii ilikuwa tokeo la mojawapo ya sifa
za Mungu ya kujua kila kitu. Usimulizi wa aina hii unajitokeza katika ukurasa
wa 17 msimulizi anapotueleza yale yanayowazwa mawazoni na mhusika Yasmin kama
anavyotuambi;
Mawazo yake yalikuwa
mbali na pale kilipo kiwiliwili chake na alikuwa akiwaza na kujiuliza, “Nende
wapi saa hizi?” alijiuliza na kujishauri moyoni mwake, “Nende kwa mama?
Hapa
msimulizi ameingia hadi akilini mwa mhusika Yasmin na kujua kile anachowaza,
maswali anayojiuliza au yanayomtatiza mawazoni. Aina hii ya usimulizi pia
tunaona inajotokeza msimulizi kwa wakati mmoja akisimulia tukio linalotokea
Unguja na wakati huo huo anaelezea tukio linalotokea Tanga Rejea ukurasa wa 214
msimulizi anapotupa habari na matendo yanayofanyika unguja na Zanzibar kwa
wakati mmoja; katika hali ya kawaida sifa ya mtu kujua mambo yanayotendeka kwa
wakati mmoja sehemu mbili tofauti ni jambo ambalo Mungu peke yake ndiye
anayeweza.
Aidha
usimulizi wa kirejeshi unajitokeza katika riwaya hii, Wamitila (keshatajwa, uk.
327) anatueleza kuwa, usimulizi kirejeshi ni aina ya usimulizi ambao unategemea
wakati uliopita hasa kumfanya msimulizi kutafakari kuhusu yaliyotokea na
kubainisha tofauti zilizopo kati ya jana na wakati uliopo. Katika sura ya nne
mwandishi anatuonesha Denge akiwa Unguja na akiendesha harakati zake za
kimapinduzi usimulizi kirejeshi unajitokeza sura ya sita mwandishi
anapotusimulia au kuturudisha nyuma matukio ya kutuelezea habari za Denge za
huko nyuma ambazo mwanzo hazikuonesha.
“Denge alimaliza darasa
la nne skuli ya Gulioni na alifuzu vizuri mtihani wake. Aliingia daraa la tisa
Government Secondary School. Alimaliza darasa la 12 na alishinda mtihani wa
Cambridge daraja la kwanza.
Hata
hivyo usimulizi wa Ki-itimamu pia unajitokeza katika riwaya hii. Wamitila
(keshatajwa) anasema usimulizi wa aina hii unaweza kupatikana pale ambapo pana
matumizi ya barua hasa katika riwaya za aina hiyo. Riwaya hii si ya kibarua
kama ilivyo katika riwaya ya Barua Ndefu
Kama Hii iliyoandikwa na Mariam Ba. Matumizi ya mbinu hii inajitokeza
katika ukurasa 168-169. Mbinu hii imetumika kama mbinu moja wapo ya kuipamba
kazi yake na kumchota msomaji kihisia.
Hitimisho,
ama kwa hakika tukitaza usimulizi wa kutumia viambishi vya nafsi ya tatu bila
shaka utagundua kuwa aina hiyo ya usimulizi kwa kiasi kikubwa huingiliana ama
kuhusiana na mbinu ya usimulizi maizi ambayo nayo hutumia viambishi vya nafsi
ya tatu katika usimulizi wake. Tofauti yake ni kwamba usimulizi wa nafsi ya
tatu kwa mujibu wa mjadala wetu mwandishi si lazima ajue kile kitu hata yale
ambayo hayakudhihirishwa na muhusika wakati, katika usimulizi maizi msingi wake
mkubwa ni mwandishi kuwa na sifa za kimungu, kujua hata yale ambayo hayakudhihirishwa
na muhusika. Kwa hakika, katika riwaya ya Vuta
n’kuvute mwandishi ametumia kauli na mbinu mbalimbali za usimulizi,
tulizoziangalia hapa ni baadhi tu. Matumizi ya mbinu hizo katika bunilizi ya
riwaya nikutupa picha kuwa ni nani anayesimulia, nani anasimuliwa (mhusika),
anayesimuliwa anafanya nini, amefanya nini au atafanya nini lini na wapi.
Kumbuka mpangilio mzuri wa usimulizi katika bunilizi huweza kuifanya kazi
husika kupendeza na kuvutia kwa msomaji.
MAREJEO
Burundi,
R.N, Mukuthuria, M. na Matundura, E.S. (2014) “Usimulizi katika Utenzi wa Swifa
ya Nguvumali.” Katika Kioo cha Lugha: Jarida la Taasisi ya Taaluma
za Kiswahili. Juz 12:
Uk.73-86.
Dar es Salaam. TATATKI.
Mohochi,
E.S. (2000), “Usimulizi wa Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini.” katika Nordic Journal of
African Studies 9 (2): 49-59.
Shafi,
A,S. (1999) Vuta n’Kuvute. Dar es
Salaam. Mkuki na Nyota Publisher.
Wamitila,
K.W. (2008) Kanzi ya Fasihi: Misingi ya
Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi.
Vide-Muwa Publishers Limited.
Wamitila,
K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi: Istilahi na
Nadharia. Nairobi.Focus Publications
Ltd.
Simu 0715335558 (whatsapp) na 0755440699
Facebook: Furaha Venance
instagram: fullraha17