Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Sunday, January 13, 2013

Dr. SLAA AFAFANUA CHIMBUKO LA MKATABA KATI YA SERIKALI NA MAKANISA [MOU]

Dr. Willibroad Peter Slaa
 
KWA mara ya kwanza, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ameweka bayana chimbuko la mkataba wa makubaliano kati ya serikali na makanisa, huku akiwasihi Watanzania kujiepusha na malumbano yenye hisia za udini.
 
Dk. Slaa alitoa tahadhari hiyo jana katika ufafanuzi wake aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forum, kuhusu mkataba huo (Memorandum of Understanding - MOU) kati ya Baraza la Kikristo Tanzania, Baraza la Maaskofu Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
 
Alisema kuwa amelazima kutoa ufafanuzi baada ya kuona mkataba huo umewekwa kwenye mtandao wa kijamii, huku watu wengi wakiwa wanauzungumzia kwa kupotosha ukweli wa jambo hilo, na kulihusisha na masuala ya udini.
 
 
“Kama mnavyoona, mimi nilikuwa nafahamu historia yote, nafahamu MOU, lakini sikuwa nayo. Mtu huwezi kujua kila kitu, na au kuwa na kila kitu, ‘we need to complement each other’.
 
 
“Ninarudia kuwaomba wenzangu, tumetumia muda mrefu sana kujadiliana kwa hisia ya aina mbalimbali. Watanzania hatukuzoea huko nyuma kuulizana dini zetu, wala kabila, wala ukanda. Haya mambo tukiyaendekeza taifa letu litakuwa hatarini,” alisema.
 
 
Alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa, kubomoa ni kazi nyepesi, lakini kujenga tena inachukua muda mrefu, na ni kazi ngumu, na wakati mwingine hata ukifanikiwa huwezi kujenga kama ilivyokuwa.
 
 
Akifafanua historia ya jinsi na kwanini MOU hiyo ilizaliwa, Dk. Slaa alisema kuwa huko nyuma serikali ilitaifisha shule nyingi za madhehebu ya dini.
 
 
Kwamba utaifishaji huo uliendana pia na ardhi, hasa ikizingatiwa kuwa wakati huo shule zilijengwa kwenye maeneo ya madhehebu ya dini na papo hapo kukiwa na kanisa, nyumba za mapadre na vitu vingine.
 
 
Alisema kuwa kwenye miaka ya 1980, madhehebu yakataka warudishiwe ardhi yao, hasa ambayo ina majengo mengine yasiyohusiana na shule hizo.
 
 
Dk. Slaa alifafanua kuwa, mchakato wa mjadala ulishika kasi mwaka 1986 Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), lilipopitisha azimio rasmi na kumtaka Katibu Mkuu, awasiliane na serikali kuanzisha mchakato wa kufanya upembuzi na kutenga ardhi ya shule rasmi, kutoka kwenye ardhi inayotumika kwa huduma nyinginezo za madhehebu ya dini.
 
 
“Wakati huo mimi (Dk. Slaa), ndiye nilikuwa Katibu Mkuu wa TEC baada ya kupokea rasmi kazi hiyo Desemba1985. Wakati huo madhehebu yaliishakudai yarudishiwe shule zao kwa kuwa zimegeuka kuwa aibu kwa kukosa ukarabati, na ziko kwenye hali mbaya sana,” alisema.
 
 
Aliongeza kuwa serikali ilikuwa imekataa ombi hilo kwa lengo la kuwa, shule hizo zinawahudumia Watanzania wote bila ubaguzi, jambo ambalo ndilo lilikuwa lengo kuu la utaifishaji, na sababu ya utaifishaji ilikuwa bado inaendelelea.
 
 
Dk. Slaa aliongeza kuwa, mawasiliano yalipoanza na serikali, wakati huo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu, serikali iliomba TEC na madhehebu ya dini kwa ujumla, kama yanaweza kusaidia ukarabati wa shule hizo kwa kuwa ziko kwenye hali mbaya na hali ya uchumi wa nchi haikuwa nzuri.
 
 
“Wakati mchakato huo kwa upande wa elimu umeanza, kulikuwa pia na mgogoro kati ya serikali na TEC baada ya serikali kuichukua Hospitali ya Bugando kwa utaratibu huo huo wa kuitaifisha,” alibainisha.
 
Kwamba hospitali hiyo ilikuwa kwenye awamu ya pili ya ujenzi kwa msaada mkubwa wa Shirika la la Maendeleo la Baraza la Maaskofu Katoliki la Ujerumani (Misereor).
 
Alisema kuwa Katibu Mkuu wa TEC alipowasiliana na wahisani, walikataa katakata kujihusisha tena na ujenzi au ukarabati wa shule au hospitali, vituo vya afya na zahanati, kwa kuhofia kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikitaifisha huduma hizo bila majadiliano ya aina yoyote.
 
Wahisani hao walisema hawawezi kuwekeza fedha za walipakodi wao (Ujerumani), lakini walikuwa tayari kuendelea na huduma mbalimbali za kusaidia dawa na elimu kwa shule ambazo bado ziko chini ya madhehebu ya dini kwa kuwa hawawezi kuwaadhibu wananchi na watoto.
 
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kwa kuwa shughuli zote za Bugando zilikuwa zinaelekea kusimama, na kulikuwa na mgomo kila siku kwa madaktari, manesi na watumishi, serikali ikaomba wajadiliane upya juu ya mambo makubwa mawili.
 
Mambo hayo ni utoaji huduma katika sekta za huduma za jamii, na kuwa na chombo cha mawasiliano na majadiliano kati ya Ikulu na madhehebu ya dini.
 
Lakini kwa kuwa madhehebu ni mengi, wakaomba chombo hicho kiundwe na viongozi wakuu wa madhehebu yaliyokuwa yanajulikana kwa mujibu wa sheria.
 
Hivyo, Waislamu wakawakilishwa na Bakwata, TEC na CCT (kwa madhehebu zaidi ya 60 yaliyoko chini ya Christian Council of Tanzania), na baada ya mashauriano waliunda chombo hicho.
 
Alifafanua kuwa kutokana na hali mbaya ya shule, serikali iliomba madhehebu ya dini kusaidia ukarabati kwa zile zilizoonekana zitafungwa kutokana na hali mbaya.
 
“Nasi kwa upande wetu, kwa nia njema ya kuisaidia serikali, lakini pia kuwahudumia Watanzania, tuliwasiliana na wahisani ambao walikazia msimamo wao kuwa hawako tayari kuingia kwenye shughuli za ujenzi wala ukarabati kwa kukosa msimamo wa wazi na wa kisheria wa Serikali ya Tanzania kuhusiana na utaifishaji wa huduma hizo,” alisema.
 
Katibu huyo aliongeza kuwa, serikali ilipojulishwa ilichukua hatua ya kuanzisha mchakato mzima wa kupata suluhu ya jambo hilo. Ndipo akapewa jukumu hilo, Anne Makinda, wakati huo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.
 
“Hatimaye, serikali ilikubali kuwa haitataifisha tena na kwa kuthibitisha hivyo, ikawa tayari kuwekeana mkataba na madhehebu ya dini. Ndipo tukaanzisha mchakato wa majadiliano na wahisani, nao katika umoja wao kati ya dhehebu la kikatoliki Ujerumani na Kilutheri pia la Ujerumani, tukaanzisha mchakato wa namna bora ya kutoa huduma za jamii,” alisema.
 
Hatimaye, makubaliano yalifikiwa na ndipo kikazaliwa chombo kipya, Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), chenye sekretarieti yake, hivyo huduma ya Christian Medical Board ya TEC na CCT, ikavunjwa na kuwekwa chini ya CSSC.
 
Dk. Slaa aliongeza kuwa, kwa upande wa serikali aliweka saini Edward Lowassa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu wakati huo. Kwamba TEC na CCT nazo zikawekeana na wahisani mikataba yao ya ndani ili kupata misaada ya ujenzi, ukarabati na uendelezaji wa huduma zote za jamii.
 
Chanzo: Tanzania Daima au Tembelea www.freemedia.co.tz

HONGERA SUGU! TUKIANZISHA MIFUKO KAMA HII TUNAWEZA KUINUA KIWANGO CHA ELIMU KATIKA MAJIMBO YETU NA WILAYA ZETU

Matokeo mabaya ya mitihani kwa shule zetu za serikali huwa mabaya kwa sababu viongozi wetu waliowengi wamezitelekeza shule hizi. na kama wadau mbalimbali wataamua kuwa na mikakati ya maana tunaweza kuinua kiwango chetu cha elimu katika wilaya zetu, majimbo yetu, mikoa yetu na hata taifa letu kwa ujumla!
 
 
Wapo watu/viongozi ambao kwa namna moja ama nyingine wanajitahidi kubuni na kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha wanainua kiwango cha elimu na ufaulu kwa wanafunzi wao, mifano iko, kwa mfano mbunge wa Bumbuli huko Tanga January Makamba ameanzisha mfuko maalum wa elimu jimboni mwake lengo la mfuko huo ni kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika jimbo lake.
 
 
mwingine ni mbunge wa Ubongo ndugu John Mnyika naye ameanzisha mfuko wa namna hiyo ukiwa na lengo la kuzisaidia shule, wanafunzi wasiojiweza n.k lakini pia mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi naye ameanzisha mfuko wa namna hiyo pia, na wadau mbalimbali wameweza kujitokeza na kutoa michango yao kwa ajili ya kusaidia katika elimu jimbo hilo la mbeya mjini na kuwasaidia watoto wasio na uwezo!
 
 
je swali la kujiuliza wabunge wengine katika maeneo yetu wanasubiri nini kufanya hivyo? wakuu wa wilaya katika wilaya zao wamefanya nini kusaidia sekta ya elimu katika wilaya zao!
 
 
Je! tunasubiri mpaka rais Kikwete afanye hili katika wilaya zetu/majimbo yetu! watoto wangapi katika wilaya zetu, majimbo yetu, mikoa yetu wanashindwa kuanza na kidato cha kwanza kwa kukosa pesa za kulipa ada, kutengeneza au kununua madawati na michango mingine mingi tu kwa sababu ya umaskini wa wazazi wao?
 
 
walimu na viongozi wa kisiasa wakiamua kushirikiana kwa dhati kabisa tunaweza kuzifanya shule za serikali kuwa kimbilio la watanzania tofauti na hali ilivyo sasa! shule hizi wanasoma watoto ambao wazazi wao hana uwezo wa kuwasomesha katika shule zingine.
 
 
tufanye kama akina Joseph Mbilinyi, kwa mfano leo katika ukurasa wake wa facebook, Mbunge wa mbeya mjini Joseph Mbilinyi  ameandika  kitu kama hiki:
 
 
"SHUKRANI: MH JOSEPH O. MBILINYI (MP),MBUNGE WA MBEYA MJINI NA MWENYEKITI WA MFUKO WA ELIMU MBEYA-(MBEYA EDUCATION TRUST FUND) PAMOJA NA BODI YETU YA WADHAMINI TUNAPENDA KUTOA SHUKRANI ZETU ZA DHATI KWA MAKAMPUNI YAFUATAYO YA MJINI MBEYA KWA KUCHANGIA MFUKO WETU, COCA COLA (5,000,000/-), LAFARGE-MBEYA CEMENT (2, 000, 000/-), TBL (1,OOO,OOO/-) CRDB BANK-MBEYA BRANCH (200,000/-), MWAKIMOMO STORE (150,000/-), NA ACCESS COMPUTERS WALIOTUPATIA COMPUTER MOJA KWA AJILI YA MATUMIZI YA OFISI YA MBETF ILIYOPO KATA YA NZOVWE...
 

 WITO: EWE MWANA-MBEYA NA RAFIKI WA MBEYA POPOTE ULIPO,TAFADHALI CHANGIA MFUKO WA ELIMU ILI TUFIKIE MALENGO YA KUPELEKA SEKONDARI WATOTO WASIO NA UWEZO(UNDERPRIVILEDGED) WAPATAO 360 KWA MWAKA HUU 2013...A/C YETU NI -01J50421214700 CRBD BANK MWANJELWA BRANCH- KWA JINA LA MBEYA EDUCATION TRUST FUND.


TUNATANGULUZA SHUKRANI KWA WOTE WATAKAOTUCHANGIA...
 
Mwisho wa kunukuu. wengine tuige huu mfano. umefika wakati sasa wa kuacha kulaumiana kila mtu atimize wajibu wake kwa nafasi yake na kwa uwezo wake. na hii chini ndo nembo inayotumiwa na huo mfuko wa elimu mbeya [Mbeya Education Trust Fund]
Photo
Kama na wewe katika wilaya yako au jimbo lako kuna mifuko ya aina hii unaweza kutujulisha kwa kuandika hapo chini sehemu ya kuandika comment au kunitumia kwa anuani zetu hapo juu ukitaja jimbo, wilaya jina la mfuko na aliyeuanzisha au anayeusimamia na malengo ya huo mfuko kwa ajili ya kutumia hizo data katika makala yangu nitakayoiandika na kuchapwa katika gazeti la Mwananchi pindi itakapokuwa imekamilika.
 
Imeandikwa na Mwl. Furaha Venance
simu 0715 33 55 58 /0787 33 55 53
 
 
 

Saturday, January 12, 2013

YULE MWANAJESHI FEKI ALIYEPIGA PICHA NA LEMA JELA MIAKA 2



 
MTU aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema akiwa amevalia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela.
 


Abubakari Kikulu (29), alipiga picha na mbunge huyo Desemba 23 mwaka jana, baada ya Lema kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara eneo la Mererani, ikiwa ni sehemu ya mikutano aliyoifanya kutokana na Mahakama ya Rufani Tanzania kumrejeshea ubunge wake.
 


Mbali na kupiga picha hiyo na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari, kijana huyo alionekana katika picha hiyo akionyesha vidole viwili, ambayo ni alama ya Chadema.
 


Hata hivyo, baada ya picha hiyo, JWTZ lilimtilia shaka kijana huyo na kutangaza rasmi kumsaka, ili lijiridhishe kama ni mmoja wa wanajeshi wake.

Baada ya kumsaka kwa takriban siku 12, kijana huyo alikamatwa Januari 13, katika Mji wa Bomang’ombe wilayani Hai na baada ya kupekuliwa alikutwa na sare hizo.
 


Jana, Kikulu alifikishwa mahakamani mjini Moshi, akiwa chini ya ulinzi wa polisi na kusomewa mashtaka mawili, ambayo yote alikiri kuyafanya kama ilivyodaiwa mahakamani.
 

Baada ya kukiri kosa hilo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Kilimanjaro, alimhukumu kifungo cha miaka minne jela, ili iwe fundisho wa wakosaji wengine wa aina hiyo.


Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka alimsomea mshtakiwa huyo mashitaka yake mawili, likiwamo la kujifanya Ofisa wa Jeshi, wakati akijua ni uongo.
Wakili huyo alidai mahakamani kuwa Januari 3, mwaka huu katika eneo la Bomang’ombe wilayani Hai, mtuhumiwa huyo alijitambulisha kama mtumishi wa umma.

 

Katika shtaka la pili, wakili huyo alidai siku hiyo hiyo katika Mtaa wa Msikitini, eneo hilo la Bomang’ombe, mtuhumiwa alipatikana na sare za JWTZ kinyume cha sheria.
 


Sare hizo ni pamoja na suruali moja, mashati mawili na kofia mbili, vyote vikiwa na alama za Jeshi la Wananchi wa Tanzania la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 

Baada ya Hakimu Kobelo kumuuliza mshtakiwa kama ni kweli alitenda makosa anayoshitakiwa, mshtakiwa huyo alikiri makosa yake katika hali ambayo haikutarajiwa.


Kutokana na kukiri kwake makosa hayo, Hakimu Kobelo alimhukumu kifungo cha miaka miwili kwa kosa la kwanza la kujifanya Ofisa wa JWTZ na miaka mingine miwili kwa kosa la pili.
Hata hivyo, Hakimu Kobelo alisema kuwa kwa kuwa adhabu hizo zinakwenda kwa pamoja (concurrent), mshtakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.
 


Kwa mujibu wa hakimu huyo, kosa alilolifanya mtuhumiwa huyo ni baya na linastahili adhabu kali, ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotumia vibaya sare za majeshi nchini.
 
Chanzo: Mwananchi

Friday, January 11, 2013

MATOKEO KIDATO CHA PILI WANAFUNZI 136,923 KATI YA 386,271 WAMEFELI

 
SERIKALI imetangaza matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka 2012, takwimu zikionesha kuwa nusu ya watahiniwa wameshindwa kupata alama 30, huku shule kumi za mikoa ya Lindi na Mtwara zikishika mkia.
 
Licha ya watahiniwa hao kushindwa kupata alama hizo, zile za ufaulu zimeongezeka kutoka asilimia 45.40 mwaka 2011 hadi kufikia 64.55 kwa mwaka 2012.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema kuwa watahiniwa 136,946 walioshindwa kupata alama 30 na wengine 23 walioonekana kudanganya watalazimika kukariri kidato cha pili mwaka huu.
 
Mulugo alisema kuwa watahiniwa 249,325 wataendelea na masomo ya kidato cha tatu.
 
“Ni vema ikaeleweka kuwa kukariri kidato sio adhabu bali ni kutoa fursa nyingine kwa wanafunzi hao kuweza kupata maarifa, stadi na ujuzi wa elimu ya sekondari kidato cha kwanza na pili kwa kiwango kizuri,” alisema.
 
Ufaulu wa watahiniwa
Kwa ipande wa ufaulu wa watahiniwa Mulugo alisema kuwa watahiniwa 249,325 sawa na asilimia 64.55 walifaulu huku wasichana wakiwa 113,213 na wavulana 136,112 kiwango kikipanda kwa asilimia 19.15.
 
“Watahiniwa waliofaulu kwa kiwango cha A, B na C walikuwa 127,981 sawa na asilimia 33.13 na waliofaulu kwa kiwango cha D ni 121,344 na alama ya juu ya ufaulu ilikuwa ni asilimia 92,” alisema.
Shule zilizofanya vizuri
Mulugo alizitaja shule za serikali kumi zilizoongoza ni Mzumbe, Tabora wavulana, Ilboru, Kibaha, Iyunga, Msalato, Malangali, Ifunda Ufundi, Samora Machel na Kilakala.
Kwa upande wa shule zisizo za serikali, Mulugo alizitaja kuwa ni Kaizerege, Marian wavulana, St Francis, Don Bosco, Bethel SABS, Marian wasichana, Don Bosco Moshi, Cannosa, St Joseph Iterambogo na Carmel.
Shule zilizofanya vibaya
 
Kwa upande wa shule za serikali zilizofanya vibaya ni Mihambwe, Dinduma, Kiromba, Marambo, Mbembaleo, Kinjumbi, Litipu, Luagala, Miguruwe na Napacho ambazo zote ni kutoka mikoa ya kusini – Mtwara na Lindi.
 
Kwa upande wa shule zisizo za serikali ni Mfuru, Pwani, Doreta, Kigurunyembe, Ruruma, At-taaun, Jabal hira, Mkono wa Mara, Kilepile na Kiuma.
Wanafunzi waliofanya vizuri
Mulugo aliwataja wanafunzi walioongoza katika mtihani huo na shule wanazotoka katika mabano kuwa ni Magreth Kakoko (St Francis) Queen Masiko (St Francis), Lukundo Manase (Kaizerege), Frank Nyamtarila (Kaizerege), Grace Msovella (St Francis), Harieth Makireye (St Francis) Robinnancy Mtitu (St Francis), Humrath Lusheke (St Francis), Mukhsin Hamza (Kaizerege) na Anastazia Kabelinde (Kaizerege).
Walimu shule za mijini
Katika hatua nyingine, Mulugo alisema kuwa kuanzia mwaka huu hakuna mwalimu atakayepangwa shule za mjini.
 
 
Hatua hiyo imetokana na ukosefu wa walimu ulioko vijijini na tabia ya walimu wengi kupenda kuishi mijini.
 
 
Akizungumza na viongozi wa kanda mbalimbali kutoka Jumuia ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Tahliso), Mulugo alisema kuwa mwalimu yeyote ambaye hataripoti katika kituo chake cha kazi ndani ya wiki mbili atakuwa amejipotezea ajira yake mwenyewe.
 
Akitoa nasaha kwa viongozi hao wa Tahliso, Mulugo aliwataka kuachana na tabia ya kuingiza siasa katika mambo ya elimu kwani husababisha migogoro.
 
 
Mulugo alisema kuwa zinapotokea changamoto zozote vyuoni, ni vyema wanafunzi kukubali kukaa meza moja ya mazungumzo badala ya kusisitiza migomo na maandamano ya yasiyoleta tija ambayo huaribu mfumo.
 
Naye mwenyekiti wa Tahliso, Amn Chakushemeire, aliwataka wanafunzi wa vyuo vyote kuacha kutumika na wanasiasa ikiwemo kuondoa chuki za itikadi za vyama vya siasa ndani ya vyuo vyao.

Chanzo: Tanzania Daima

Tuesday, January 8, 2013

MAGAZETI YA LEO JUMATANO 09/01/2013

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
MAGAZETI YA UDAKU
 
 
 
 

CCM WAANZA KUMSHUGHULIKIA BASHE.

                                                                      Hussein Bashe
 
MGOGORO wa makada wawili wa CCM; Benard Membe na Hussein Bashe umechukua sura mpya, baada ya mbunge huyo wa Mtama, kukiomba chama hicho tawala kuingilia kati ili kuupatia suluhu.
 

Mvutano wa Bashe na Membe ulianza wakati wa kampeni za uchaguzi wa ndani wa CCM hasa uchaguzi wa NEC baada ya Bashe kumtuhumu Membe kwa mambo mbalimbali ikiwamo kukigawa chama.
 


Kauli hiyo ya Bashe ilimkera Membe ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza kuwa atamshughulikia mwanasiasa huyo chipukizi wa CCM ili amtambue.
 


“Nitashughulika na Bashe ndani ya chama kwa maana ya kumfikisha kwenye kamati zetu, ili ayaeleze vizuri ambayo amenipakazia na kunichafua sana… Lakini mambo mengine ambayo yamekaa kijinai sasa hayo ndiyo nitakayoyapeleka mahakamani,” alisema Membe baada ya taarifa hizo.
 


Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Membe amemwandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kumwomba amtake Bashe athibitishe kauli zake mbalimbali dhidi yake.
 


Moja ya mambo Membe anamtaka Bashe ayathibitishe ni kwamba waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuwahi kusema kuwa akiwa Rais, atawafukuza watu kumi na moja nchini ambao anaamini kuwa siyo Watanzania.


“Barua hii ina tuhuma nyingi, lakini kikubwa mheshimiwa huyo (Membe) amekiomba chama kimtake Bashe athibitishe tuhuma zake dhidi yake, ikiwamo hili la kuwafukuza Watanzania 11,” kilidokeza chanzo chetu cha habari ndani ya CCM.

 

Chanzo hicho kimeeleza kuwa baada ya makamu mwenyekiti huyo kupata barua ya Membe, ameipeleka katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa hatua zaidi.
Habari zimeeleza kuwa tayari Kinana ameifanyia kazi barua hiyo kwa kumwandikia barua Bashe ili ajibu tuhuma zinazomkabili ifikapo kesho Januari 10.

 

Nakala ya barua hiyo ya Kinana imetumwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega ambako Bashe anatokea akiwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kupitia wilaya hiyo.
“Tayari Bashe ameandikiwa barua na CCM kumtaka ajibu malalamiko hayo ya mwenzake Membe,” kilieleza chanzo hicho cha habari.
 


Membe hakupatikana kwa siku tatu mfululizo, ili azungumzie suala hilo baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana na taarifa zilizopatikana ofisini kwake, zimeeleza kuwa yuko likizo jimboni kwake Mtama, Lindi.
Bashe hakuthibitisha wala kukanusha kupata barua hiyo ya CCM inayomtaka ajibu madai ya Membe, badala yake akasema: “Membe aliahidi kunishughulikia na mimi ninangoja anishughulikie.”


Mangula alipotafutwa juzi kuzungumzia suala hilo alisema asingeweza kusema chochote kwa kuwa alikuwa hajafika ofisini tangu alipokwenda kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Sijajua chochote kilichoendelea ofisini kwa sababu nilikuwa kijijini kwangu kwa ajili ya Sikukuu ya Krimasi na Mwaka Mpya. Nikiingia ofisini naweza kuwa katika nafasi ya kujua kilichoendelea,” alisema Mangula. Hata hivyo, alipopigiwa simu jana, iliita bila kupokewa na baadaye ikazimwa kabisa.

 

Kinana naye hakupatikana jana baada ya simu yake pia kuita na kupokelewa na mtu mwingine mara kadhaa ambaye alieleza kuwa alikuwa mkutanoni siku nzima.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alijibu kwa kifupi na kukata simu,” Sijapata wala kuona barua ya malalamiko ya Membe kwa Bashe.”

Mgororo ulikoanzia
Novemba 10, mwaka jana Bashe akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, alimtuhumu Membe akidai kuwa ndiye anayehusika na vipeperushi vya kumhujumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete vilivyokuwa vimetawanywa na watu wasiojulikana siku chache kabla ya uchaguzi wa mwenyekiti na nafasi nyingine kufanyika.
 
Chanzo cha habari: http://www.mwananchi.co.tz     [Gazeti la Mwananchi 09/01/2013]
TANZIA: Msanii maarufu wa Mchiriku, Omari Omar amefariki dunia. Omar aliyetamba na wimbo wake maarufu wa "Kupata ni Majaliwa"
(audio Video-->http://bit.ly/XgL0ez) alifariki nyumbani kwao Temeke, saa chache baada ya kurejeshwa toka hospitali ya temeke alipokuwa amelazwa kwa siku kadhaa. Kwa habari zaidi na kusikiliza wimbo wake, click link ifuatayo-->http://bit.ly/XgL0ez

Msanii wa Bongo Fleva hususani miondoko ile ya Mchiriku Omary Omary amefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya kuugua kwa muda mrefu, msanii huyo aliyewahi kutamba na kibao chake cha "KUPATA NI MAJALIWA" Taarifa zinasema kuwa Omary Omary ameaga dunia saa chache huko kwake TEMEKE MIKORISHINI mara baada ya kurejea kutoka hospitali ya TEMEKE aalikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.

Taarifa zaidi tutakuwa tukiwaletea kadili tutakavyozipata
 
RIP OMARY OMARY

Monday, January 7, 2013

SHULE 24 ZA SEKONDARI KUTOA WANAFUNZI KUJIUNGA NA JKT MWAKA HUU

 
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limetaja shule 24 za sekondari ambazo zitatoa wanafunzi 5,000 waliomaliza kidato cha sita watakaojiunga na jeshi hilo.
 
 

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Raphael Mahuga alisema katika taarifa yake jana kuwa wanafunzi hao watatakiwa kujiunga na jeshi hilo ifikapo Machi 2, mwaka huu.
 
 

Shule hizo za sekondari ni Kibondo, Musoma, Kibaha, Ilboru, Bagamoyo, Jitegemee, Tabora Wavulana na Nganza.
 
 

Shule nyingine ni Mtwara Wasichana, Ihungo, Kilakala, Benjamin Mkapa, Maswa Wasichana, Dodoma, Tumain-Singida na Galanos.
 
 

Nyingine ni Ashira, Nangwa-Manyara, Iyunga, Mpanda, Lindi, Iringa Wasichana, Kawawa-Iringa na Ruhuwiko-Songea.
 

Taarifa hiyo ilisema maofisa wa JKT watakwenda kwenye shule hizo kuanzia Januari 9, mwaka huu kwa ajili ya kutoa utaratibu wa mafunzo na kambi ambazo watakwenda.
 

“Mkuu wa JKT kwa mamlaka aliyopewa kisheria ya mwaka 1964 na kufanyiwa mapitio mwaka 2002, chini ya kifungu cha sheria namba 5,” ilisema taarifa hiyo.
 
 

Iliongeza kuwa “Anawaita vijana watakaohitimu kidato cha sita mwaka 2013 kujiunga na JKT kwa mujibu wa sheria ifikapo terehe 2, Machi 2013.” Utaratibu wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria ulisimamishwa tangu mwaka 1994.
 

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Jeshi la Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Julai mwaka jana, Waziri wake, Shamshi Vuai Nahodha alisema kambi zilizopo za JKT zina uwezo wa kuchukua vijana 20,000 kwa wakati mmoja, lakini kutokana na ufinyu wa bajeti mwaka huu wataanza kwa majaribio na vijana 5,000.
 
 

Alisema wanafunzi 41,348 wanatarajiwa kuhitimu elimu ya kidato cha sita katika mwaka 2013 na kwamba vilikuwa vikiandaliwa vigezo ili kuwapata vijana 5,000 ili kujiunga na JKT.
 
 

Kwa mujibu wa jarida la JKT, mafunzo hayo yatakuwa ya miezi sita katika Kambi za JKT Bulombora na Kanembwa mkoani Kigoma.  Nyingine ni Mlale (Ruvuma), Mafinga (Iringa), Msange (Tabora) na Oljoro(Arusha).
 

MAGAZETI YA LEO JUMANNE 08/01/2013

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
HABARI ZA UDAKU
 
 
HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI