Hussein Bashe
MGOGORO wa makada wawili wa CCM; Benard Membe na Hussein Bashe umechukua sura mpya, baada ya mbunge huyo wa Mtama, kukiomba chama hicho tawala kuingilia kati ili kuupatia suluhu.
Mvutano wa Bashe na Membe ulianza wakati wa kampeni za uchaguzi wa ndani wa CCM hasa uchaguzi wa NEC baada ya Bashe kumtuhumu Membe kwa mambo mbalimbali ikiwamo kukigawa chama.
Kauli hiyo ya Bashe ilimkera Membe ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza kuwa atamshughulikia mwanasiasa huyo chipukizi wa CCM ili amtambue.
“Nitashughulika na Bashe ndani ya chama kwa maana ya kumfikisha kwenye kamati zetu, ili ayaeleze vizuri ambayo amenipakazia na kunichafua sana… Lakini mambo mengine ambayo yamekaa kijinai sasa hayo ndiyo nitakayoyapeleka mahakamani,” alisema Membe baada ya taarifa hizo.
Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Membe amemwandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kumwomba amtake Bashe athibitishe kauli zake mbalimbali dhidi yake.
Moja ya mambo Membe anamtaka Bashe ayathibitishe ni kwamba waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuwahi kusema kuwa akiwa Rais, atawafukuza watu kumi na moja nchini ambao anaamini kuwa siyo Watanzania.
“Barua hii ina tuhuma nyingi, lakini kikubwa mheshimiwa huyo (Membe) amekiomba chama kimtake Bashe athibitishe tuhuma zake dhidi yake, ikiwamo hili la kuwafukuza Watanzania 11,” kilidokeza chanzo chetu cha habari ndani ya CCM.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa baada ya makamu mwenyekiti huyo kupata barua ya Membe, ameipeleka katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa hatua zaidi.
Habari zimeeleza kuwa tayari Kinana ameifanyia kazi barua hiyo kwa kumwandikia barua Bashe ili ajibu tuhuma zinazomkabili ifikapo kesho Januari 10.
Nakala ya barua hiyo ya Kinana imetumwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega ambako Bashe anatokea akiwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kupitia wilaya hiyo.
“Tayari Bashe ameandikiwa barua na CCM kumtaka ajibu malalamiko hayo ya mwenzake Membe,” kilieleza chanzo hicho cha habari.
Membe hakupatikana kwa siku tatu mfululizo, ili azungumzie suala hilo baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana na taarifa zilizopatikana ofisini kwake, zimeeleza kuwa yuko likizo jimboni kwake Mtama, Lindi.
Bashe hakuthibitisha wala kukanusha kupata barua hiyo ya CCM inayomtaka ajibu madai ya Membe, badala yake akasema: “Membe aliahidi kunishughulikia na mimi ninangoja anishughulikie.”
Mangula alipotafutwa juzi kuzungumzia suala hilo alisema asingeweza kusema chochote kwa kuwa alikuwa hajafika ofisini tangu alipokwenda kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Sijajua chochote kilichoendelea ofisini kwa sababu nilikuwa kijijini kwangu kwa ajili ya Sikukuu ya Krimasi na Mwaka Mpya. Nikiingia ofisini naweza kuwa katika nafasi ya kujua kilichoendelea,” alisema Mangula. Hata hivyo, alipopigiwa simu jana, iliita bila kupokewa na baadaye ikazimwa kabisa.
Kinana naye hakupatikana jana baada ya simu yake pia kuita na kupokelewa na mtu mwingine mara kadhaa ambaye alieleza kuwa alikuwa mkutanoni siku nzima.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alijibu kwa kifupi na kukata simu,” Sijapata wala kuona barua ya malalamiko ya Membe kwa Bashe.”
Mgororo ulikoanzia
Novemba 10, mwaka jana Bashe akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, alimtuhumu Membe akidai kuwa ndiye anayehusika na vipeperushi vya kumhujumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete vilivyokuwa vimetawanywa na watu wasiojulikana siku chache kabla ya uchaguzi wa mwenyekiti na nafasi nyingine kufanyika.
Chanzo cha habari: http://www.mwananchi.co.tz [Gazeti la Mwananchi 09/01/2013]
No comments:
Post a Comment