Ndugu waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu kuwa Baraza la Vijana la
Chadema Taifa (BAVICHA), limefanya kikao cha kawaida cha Kamati Tendaji, juzi 5
Januari 2013, katika Hotel ya Benzi Garden jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja
na mambo mengine, kilijadili masuala matatu mazito.
Kwanza, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina suala la kuporomoka kwa
elimu nchini, ambapo serikali imepunguza alama za viwango vya kufaulu, jambo
ambalo limesababisha mamia ya wanafunzi waliochaguliwa kutokuwa na sifa.
Pili, Kamati Tendaji ilijadili jinsi Bavicha itakavyoshiriki katika
maandilizi ya utekelezaji wa maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema yalioeleza kuwa
mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma.
Tatu, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina “Tuhuma za usaliti na njama za
kuvuruga chama, kutukana viongozi wakuu wa chama na kuvuruga wanachama wa
Chadema na Baraza kwa ujumla.”
Ndugu waandishi wa habari, yapo baadhi ya vyombo vya habari jana na leo
vimeripoti kwa upotoshaji mkubwa wa baadhi ya masuala yaliyojadiliwa na kikao
hicho.
Kwa mfano, gazeti moja la kila siku limemtaja mwanachama wetu mmoja kuwa
ndiye aliyekuwa mtoa taarifa wetu muhimu na kusema mbunge mmoja wa CHADEMA
alijadiliwa katika kikao hicho kuwa ni miongoni mwa kundi hili la MASALIA na
kufika mbali zaidi kwa kusema, “…sasa amekalia kuti kavu.”
Lakini ukweli wa kilichojadiliwa kikaoni ni huu ambao tunaueleza sasa:
Kwanza, kuhusu ajenda ya kuporomoka kwa elimu: Kamati Tendaji imeagiza kuwa
utafiti uliofanywa na BAVICHA katika ngazi ya sekondari, ambao umegundua madudu
mbalimbali, uongezwe hadi shule za Msingi na taarifa yake ililetwe kwenye kikao
kijacho cha Kamati Tendaji.
Kwenye ajenda ya pili: Kamati ya Utendaji BAVICHA, ilipokea na kujadili agizo
la Kamati Kuu ya Chama iliyoeleza kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma.
Katika ajenda ya tatu juu ya tuhuma za usaliti na njama za kuvuruga chama,
kutukana viongozi wakuu wa chama na kuvuruga wanachama wa CHADEMA, na Baraza,
Kamati ya Utendaji ilipokea taarifa ya Kamati Ndogo ya Kamati Tendaji iliyoundwa
Septemba mwaka jana kwenye kikao chake kilichofanyika mjini Morogoro. Kamati
ilipewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha kazi hii.
Katika hili, watuhumiwa wakuu walikuwa ni kama ifuatavyo:
1. Juliana Shonza, Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa
2. Habib Mchange, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
3. Mtela Mwampamba, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
4. Gwakisa Burton Mwakasendo, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
5. Joseph Kasambala, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
Aidha, baada ya Kamati iliyoundwa kuwahoji baadhi ya watuhumiwa na wanachama
wengine mbalimbali, ilibaini kwamba wapo baadhi ya wanachama wa BAVICHA ambao
wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika tuhuma hizi. Hao ni pamoja na
Ben Saanane – maarufu kama Eight Oclock.
Katika orodha hiyo, wakatajwa pia Exaud Mamuya lakini kamati ikashindwa
kumpata Mamuya kwa kuwa hakukuwa na mawasiliano ya kutosha.
Ndugu waandishi wa habari, hizi sasa ni tuhuma za kila mmoja:
Ndugu Juliana Shonza:
Alituhumiwa akiwa katika nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA, amekuwa
akishirikiana na baadhi ya watu kupanga njama na kufanya usaliti dhidi ya
Baraza, Chama na vijana wenzake wapenda mabadiliko nchini.
Amekuwa akifanya mikutano na vikao vya siri, kwa manufaa ya CCM, akiwakusanya
vijana wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa masomo au kufukuzwa
vyuoni kwa kutimiza wajibu wao wa kudai haki zao za msingi na uwajibikaji wa
serikali na ambao ni wanachama wa CHASO.
Juliana alifanya kazi yake hiyo kwa ushawishi wa hongo, ili wakubali kuitisha
mkutano na waandishi wa habari, watoe matamko machafu dhidi ya CHADEMA na
viongozi wake wakuu, akiwamo Dk. Willibrod Slaa na Freeman Mbowe.
Mfano dhahiri hapa ni kikao alichofanya Baa ya Highland iliyoko maeneo ya
Makumbusho, majira ya saa 9 hadi saa 11, ambapo aliwaita viongozi wa CHASO,
akawashawishi kuwa watakuwa na maisha mazuri, watarudishwa vyuoni na kutunzwa
vizuri hapa mjini kama anavyoishi yeye, endapo tu watakubali kufanya press
conferences na kuisema CHADEMA kuwa inawavuruga vijana walioko vyuoni.
Tarehe 6, Desemba, 2012 Hotel MIC, kuanzia saa 10 hadi saa 12, aliwaita
baadhi ya vijana ambapo yeye na wenzake walipanga njama za kukichafua chama na
kutukana viongozi, kwa manufaa ya CCM.
Ifuatayo hapa chini ni moja ya sms ambazo Juliana Shonza alikuwa akiwaandikia
vijana katika ushawishi wake wa usaliti kwa mapambano haya ambayo chama chetu
kinafanya, kuwapigania Watanzania maskini na wanyonge katika nchi yao;
“jembe chukua bodaboda basi jamaa washatia timu hela yako yakulinda mfuko wako utaikuta tumempa eddo mnaetoa naye tamko tutalindana tu jembe usijali.”
“jembe chukua bodaboda basi jamaa washatia timu hela yako yakulinda mfuko wako utaikuta tumempa eddo mnaetoa naye tamko tutalindana tu jembe usijali.”
Huu ni moja tu kati ya ushahidi mwingi, wa meseji, simu, sauti, video, picha
na vikao kadhaa katika maeneo mbalimbali, unaomwingiza Shonza na wenzake wengine
katika sifa mbaya ya usaliti wa chama, baraza na viongozi wake na wanachama
wenzao na umma wa Watanzania kwa ujumla.
Hapo alikuwa akimwandikia mmoja wa viongozi wetu ili ashiriki katika press
conference ambayo yeye Makamu Mwenyekiti kwa kushirikiana na wenzake wengine,
walikuwa wameiandaa kwa nia ya kuchafua chama, kulichafua baraza, kutukana
viongozi waandamizi pamoja na kuvuruga na kuchonganisha wanachama wa CHADEMA.
Matokeo ya kikao hicho cha MIC Hotel, yalionekana siku moja baada ya kikao
hicho, ambapo mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Edo Mwamalala, aliyeshiriki
kikao hicho cha MIC Hotel, aliitisha mkutano na waandishi wa habari,
akijitambulisha kuwa ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA, cheo ambacho hakuwa
nacho.
Aidha, Shonza amekuwa akikutana na kufanya vikao vya siri na wenzake,
wakipanga njama za kufanya kazi na majukumu ya CCM kuhujumu BAVICHA pamoja na
CHADEMA. Mikakati ya kuvuruga baraza, kuchonganisha wanachama na kutukana chama
na viongozi wakuu, kwa siri na hadharani, imekuwa ikipangwa katika vikao hivi.
Amebainika kukiuka kipengele cha 10.1(x) cha Maadili ya Viongozi, cha Katiba
toleo la mwaka 2006, kinachomtaka kiongozi yeyote asitoe tuhuma zozote juu ya
viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali, kwa kuzingatia taratibu na kanuni
za chama.
Ameonesha ubaguzi wa kikabila na kikanda kupitia maandiko yake kwenye mtandao
kwa kutumia jina lake, anapungukiwa na sifa muhimu na mahsusi za kuwa kiongozi,
kwa mujibu wa kipengele cha 10.1(iv) kinachomtaka kiongozi yeyote asijihusishe
na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini au ukanda vinavyolenga kuleta
ubaguzi ndani ya chama.
Kwa kushiriki vikao vya kuanzisha chama kipya kinachoitwa CHAUMMA, kushiriki
katika makundi yaitwayo MASALIA na PM7 ambayo yote yalikuwa na lengo la kuvuruga
chama na wanachama, kukosanisha na kutukana viongozi wa chama, ndugu Shonza
amevunja kipengele cha 10.1(i),(viii)(ix) na ibara ya 10.2(iv).
Kwa kushiriki vikundi hivyo hapo juu, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya
BAVICHA wamejiridhisha pasi na shaka kuwa Shonza haendani na katiba, falsafa,
sera na maadili ya chama makini na tumaini la watu, CHADEMA. Hivyo kwa mujibu wa
ibara ya 5.1.4 na 5.1.5 anakosa sifa za kuwa mwanachama wa Baraza la Chama.
Kwa kutoa tuhuma za uongo dhidi ya wanachama na viongozi wenzake, ameendelea
kuvunja kanuni za uendeshaji kazi za chama ibara ya 10.1(viii).
Amehusika katika kuanzisha, kujihusisha na kuratibu moja kwa moja kundi la
vijana waliokuwa wakizunguka mikoani na kushawishi viongozi wa vijana kutoa
matamko kwa kutumia jina la CHADEMA kufanya kazi na majukumu ya CCM ya
kukichafua chama, kugombanisha wanachama na kumtukana Katibu Mkuu kwa kutumia
propaganda za CCM.
Kamati Ndogo ilimuita Ndugu Shonza ili kumhoji. Lakini aligoma kwa madai kuwa
haitambui kamati hiyo na wala hajui kuwa kuna mgogoro, jambo ambalo
limetushangaza wengi kwa kuwa Ndugu Shonza alikuwapo katika kikao cha Morogoro
kilichounda Kamati hii.
Ndugu Shonza pia hakuhudhuria kikao cha Kamati Tendaji cha juzi kwa madai
kuwa amebanwa na shughuli za familia. Baada ya kupitia maelezo yote hayo, Kamati
Tendaji iliamua yafuatayo:
Ndugu Juliana Shonza, amepoteza sifa na uhalali wa kuwa mwanachama wa Chadema
kwa kukiuka ibara ya 5.3.4 na ibara ya 10.1(ix) ya katiba ya CHADEMA na hivyo
imeamua kumuondoa katika nafasi yake ya makamu mwenyekiti na kumfuta uwanachama
wake.
Hivyo basi, kwa maamuzi hayo ya Kikao cha Kamati ya Utendaji ya BAVICHA,
kuanzia juzi tarehe 5 Januari 2013, Ndugu Juliana Shonza, si mwanachama wa
BAVICHA na hivyo moja kwa moja amepoteza sifa za kuwa kiongozi wa baraza na kwa
nafasi yake aliyokuwa nayo ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.
Habib Mchange:
Huyu alituhumiwa kutoa tuhuma za uongo, zikiwemo za mauaji, kinyume na
maadili ya Wanachama (kipengele cha 10.3(3); kuunda vikundi vinavyojulikana kwa
majina ya MASALIA na PM7 – Pindua Mbowe.
Pia Ndugu Mchange alituhumiwa kuwavuruga wanachama, kuwachonganisha na
kuwatukana viongozi, kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine cha siasa
cha CHAUMMA.
Alituhumiwa pia kupotosha maamuzi halali ya vikao vya chama na Baraza hivyo
kuendelea kukipaka chama matope.
Kamati ilimuita Mchange, na kumhoji juu ya tuhuma zinazomkabili. Hakufika.
Badala yake, aliandika barua kueleza kuwa hana imani na kamati:
Aidha, pamoja na Mchange kugoma kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Kamati Tendaji,
Sekretarieti ya Kamati Tendaji Taifa, ilimuita Ndugu Mchange kuhudhudhuria
mkutano wa Kamati Tendaji ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Mwaliko huu ulifanywa kwa njia ya barua na simu. Njia hizo ndio zilizotumika
kualika wahusika wote wakiwamo wajumbe wa Kamati Tendaji,
Ndugu waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu kwamba Ndugu Mchange
alikuwa miongoni mwa wanachama wa BAVICHA waliotaka kuwania nafasi ya uenyekiti
wa taifa wa baraza hili. Jina lake liliondolewa na Kamati Kuu ya CHADEMA,
kutokana na kukosa maadili ya uongozi.
Kamati Tendaji baada ya kusikiliza hoja yake hii, ikajiridhisha kuwa
mtuhumiwa ameamua kuibuka hoja hiyo ili kutaka Kamati Tendaji isimjadili ili
aendeleze mradi wake wa kukichafua chama akiwa ndani ya chama.
Hivyo Kamati Tendaji imefanya yafuatayo: Imempata na hatia ya kuvunja ibara
ya 10.3(iii) na kwenda kinyume na kanuni za uendeshaji wa chama ibara ya
10.3(4), kinyume na Maadili ya Wanachama (kipengele cha 10.3(3); uendeshaji wa
chama ibara ya 10.3(4) na kwamba mambo yote haya yanadhihirisha kuwa Ndugu
Mchange hayuko tayari kushirikiana na viongozi wake kama mwanachama, hivyo
kukiuka katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na kuafikiwa uamuzi wa kumfukuza
uwanachama wa Bavicha na Chadema.
Mtela Mwampamba:
Huyu ametuhumiwa kutoa tuhuma nzito za uongo hadharani, zikiwemo za mauaji,
kinyume kabisa na Maadili ya Wanachama (kipengele 10.3(3).
Kuvunja katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na Kanuni za Uendeshaji kazi za chama
Ibara ya 10.3(4) kwa kupotosha maamuzi halali ya vikao vya chama na baraza na
kukipaka matope chama pamoja na kudhihirisha kuwa hayuko tayari kushirikiana na
viongozi wake kama mwanachama.
3. Amevunja Katiba ya CHADEMA ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 kwa kutoa kauli za
kichochezi dhidi ya chama, kuwachonganisha wanachama na kuwatukana viongozi.
4. Kwa kujiunga na vikundi vinavyoitwa MASALIA NA PM7 na baadae kushiriki
vikao vya kuanzisha chama cha CHAUMMA, Ndugu Mwampamba amevunja ibara ya
10.3(iii).
5. Kinyume na ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 ya Katiba ya CHADEMA na Ibara ya 4.3(g)
na (i) ya kanuni za BAVICHA, zinazopinga ubaguzi wa aina yoyote ile, Ndugu
Mwampamba ameonesha hisia za ubaguzi wa kikabila na kikanda.
Gwakisa Burton Mwakasendo:
Huyu amekuja kwenye kikao na kukiri kutenda makosa yake ambayo takriban yote
ni sawa yanayowahusu watuhumiwa waliotangulia hapo juu. Mbele ya kikao cha
Kamati ya Utendaji alikiri kushiriki vikao, akisema kuwa ‘lakini’ alilazimika
‘kuikimbia’ dhambi kwa kuondoka katika baadhi ya mikutano na watu hao, wakati
mwingine hata nyumbani kwake hakuweza kulala akihisi ‘dhambi’ hiyo anayoikimbia
itamfuata nyumbani.
Kamati Tendaji, iliamua kumpa adhabu ya kuwekwa chini ya uangalizi kwa mwaka
mzima, katika wakati wote huo amezuiwa kugombea nafasi yoyote ndani ya BAVICHA
na onyo kali la barua.
Ben Saanane:
Huyu pamoja na kwamba hakuwa miongoni mwa watuhumiwa alipewa adhabu ya onyo
kali na uangalizi wa miezi 12, kutokana na makosa yafuatayo. Kutoa tuhuma nzito,
zinazomhusu pia Kiongozi wa juu mwandamizi wa chama, Ben amekiuka Maadili ya
Wanachama (kipengele 10.3(3).
Kukiri kuwa mmoja wa waanzilishi wa vikundi vinavyoitwa MASALIA na PM7 na
kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine cha CHAUMMA, amevunja ibara ya
10.3(iii), kwa nia ya kuvuruga chama na kutukana viongozi wake:
Mbele ya Kamati Tendaji, Ben alikiri makosa na akaomba radhi.
Aidha, Ben alitoa ushirikiano mkubwa kwa Kamati Ndogo jinsi ya kupatikana kwa
taarifa na ushahidi wa namna wanachama wa BAVICHA walivyokuwa wanafanya kazi za
kundi hili la MASALIA na PM 7 na hasa juu ya majina wanayotumia katika mitandao
mbalimbali ya kijamii, wakifanya juhudi za kuivuruga CHADEMA, kuvuruga BAVICHA,
kutukana viongozi na kuwavuruga wanachama, lakini kikubwa wakionesha kila dalili
ya tabia ya usaliti.
Exaud Mamuya:
Huyu hajapata nafasi ya kusikilizwa kwenye vikao. Hivyo suala lake
litaendelea kufanyiwa kazi na uongozi wa BAVICHA.
Aidha, kikao cha Kamati ya Utendaji pia kilipitisha kwa kauli moja, moja ya
maazimio ya BAVICHA Mkoa wa Mwanza, waliopendekeza kufukuzwa uanachama kwa
aliyekuwa Katibu wa Mkoa wa Mwanza, Salvatory Magafu, kwa tuhuma za kukiuka
Kanuni ya 10.1(xii) kwa kutoa tamko kwenye vyombo vya habari kwa nia ya
kumfarakanisha Katibu Mkuu na wanachama wa CHADEMA na umma wa Watanzania, ikiwa
ni sehemu ya uratibu wa kundi lililokuwa likiendeshwa na watuhumiwa wengine hapo
juu.
Kamati ya Utendaji pia ilimkuta na makosa ya kiuongozi katika tuhuma
zilizowasilishwa vikaoni na kufanyiwa kazi na Kamati Ndogo, Mwenyekiti wa Vijana
Mkoa wa Mbeya, Joseph Kasambala na hivyo amepewa adhabu ya onyo kali.
Hitimisho
Tunaomba kuwahakikishia vijana wenzetu wa CHADEMA na wengine wote wapenda
mabadiliko nchini, hakuna kijana mwanachama wa BAVICHA, atafanya kazi za
kuhujumu baraza na chama kwa ujumla na kusaliti matumaini pekee ya Watanzania,
akifanya kazi za mahasimu wetu, kisha akaachwa.
Ni lazima na muhimu tuoneshe kuwa tuna uthubutu kwa kuchukua hatua kadri
inavyotakiwa, pale panapotakiwa. Tuliopewa dhamana za uongozi, tutatimiza wajibu
kuhakikisha hakuna mtu ataonewa wala kupunjwa haki yake katika kusimamia
utendaji na utoaji utumishi bora wa baraza kwa wanachama wake na chama kwa
ujumla.
Daima tutasimamia katiba ya chama, maadili, kanuni, taratibu, itifaki na
miongozo ya mabaraza. Baraza hili halitakuwa tayari kuwa sehemu ya kuruga
matumaini makubwa ya Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA.
Baraza liko imara. Wanachama wetu wasifadhaishwe na upotoshaji unaofanywa na
wasaliti kuwa tumevurugika au ‘kumechafuka’. Hatuwezi kuchafuka wala kuvurugika
kwa kuchukua maamuzi dhidi ya watu wabinafsi wanaotaka kukwamisha mapambano ya
awamu ya pili, kupigania mabadiliko ya kweli ya kimfumo na kiutawala, kwa ajili
ya Watanzania.
Historia inatuonesha kuwa mara zote ambapo mapambano yamefikia hatua ya juu
ya kutimiza malengo, ndipo ambapo wasaliti hujitokeza. Hivyo vikwazo hivi vya
baadhi yetu kuanza kugeuka nyuma ni dalili za mwisho mwisho kuwa ushindi
unakaribia. Ni lazima kama vijana tuendelee kujenga imani na matumaini ya
Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA kutukabidhi dola mwaka 2015.
Mwisho
Imetolewa leo Januari 7, 2013, Dar es Salaam na;
John Heche
Mwenyekiti wa Taifa, Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA)
No comments:
Post a Comment