Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Sunday, January 25, 2015

MATUMIZI YA SITIARI NA ISHARA KATIKA NGANO

                                                                        Mwaka 2015

Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi, ambapo katika sehemu hii, tutaangalia maana ya sitiari, ishara na maana ya ngano, sehemu ya pili ni kiini cha swali, hapa tutaangalia sitiari na maana zake  na ujumbe unaotokana na sitiari hizo, pia tutaangalia ishara maana zake katika ngano na ujumbe unaotokana na ishara hizo. Na sehemu ya mwisho ni hitimisho na kiambatanisho cha ngano tulizozitumia kama mifano katika kazi yetu (kiambatanisho hicho kinapatikana kuanzia ukurasa wa 8-20.

Utangulizi
Kabla hatujaingia katika kiini cha swali letu, kwanza tuangalie maana ya istilahi muhimu katika mada hii. Tukianza na maana ya Sitiari, Mulokozi, M.M. na Kahigi, K.K. (1979:38) wanasema sitiari ni tamathali ambayo athari yake hutegemea uhamishaji wa maana na hisi kutoka katika kitu au dhana moja hadi kitu au dhana nyingine tofauti. Vitu hivyo viwili vyenye kuhusishwa kwa kawaida huwa havina uhusiano wa moja kwa moja.

Wamitila, K.W. (2003:202) anasema, Sitiari ni tamathali ya semi ielezeayo sifa za kitu Fulani kwa kusema kingine anaendelea kufafanua kuwa, sitiari huhusisha vitu viwili ambavyo ni tofauti kitabia na kimaumbile.

Mulokozi, M.M. (2002:171) Sitiari ni tamathali ya semi (maneno,kirai au miundo) inayotumika kuumba picha fulani inayoamsha mwitiko fulani kutoka kwa hadhira.
Method, S. (2013:97) anasema, tamathali hii ya usemi huitwa pia istiara, istiari au jazanda. Tamathali hii haina tofauti na tashibiha, kwani kama ilivyo tashibiha, sitiari pia hulinganisha vitu viwili. Tofauti pekee ni kuwa, katika sitiari, vitu tofauti hulinganishwa kana kwamba ni vitu vilivyo sawa kabisa.
Hivyo, kwa ujumla tunaweza sema kuwa, sitiari ni tamathali ya semi inayozungumzia kitu au dhana moja huku ikimaanisha kitu au dhana nyingine. Mfano wa sitiari ni kama vile, baba ni simba, juma amepata jiko. Dunia mti mkavu.
Maana ya ishara
Mulokozi,M.M.(1979:39) wanasema ishara ni sitiari ambamo kitu kimoja kinawakilisha kitu kingine kwa sababu ya kuhusiana nacho. Wamitila,K.W. (2003:68) anasema, isharahutumiwa kuelezea kitu fulani katika kazi ya kifasihi ambacho huwakilisha kitu kingine. Kuwakilisha huku kuaweza kutokana na uhusiano uliopo kati ya vitu hivyo viwili au uwezo wake wa kuibua fikra fulani katika akili ya msomaji.
Kwa ujumla tunaweza sema kuwa, ishara ni matumizi ya kitu, dhana, au kitendo kuwakilisha jambo au kitu kingine. Mfano wa ishara ni kama vile:
Maji.....................uhai
Damu...................kifo/machafuko
Bundi...................uchuro/mikosi
Paka mweusi.........ushirikina
Milima na mabonde.....matatizo au vikwazo

Kitu muhimu katika ishara ni kuwa, maana ya ishara zinafungamana na utamaduni wa jamii husika, hivyo ishara huweza kuwa, matendo, vitu au dhana ambazo hutumika na jamii wa utamaduni fulani kuashiria matendo, vitu au dhana fulani. Kwa maana hiyo basi ishara za jamii moja zinaweza kutofautiana na ishara za jamii nyingine. Ikumbukwe kuwa, matendo, dhana au kitu kinapotumika kuwakilisha matendo, vitu au dhana fulani hiyo ni ishara wakati matendo, vitu au dhana fulani inapotumika kwa kufananishwa au kuhusishwa na sifa au tabia na dhana, kitu au matendo mengine hiyo ni sitiari.

Maana ya ngano
Senkoro (2011:53) anasema, ngano  ni utanzu wa kifasihi simulizi ambao ulipitishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. King’ei  (2005:65)  anasema  ngano  kuwa  ni  hadithi  fupi  na  zenye   masimulizi    yasiyo    ya  kishairi. Kwa upande wake,Wamitila, K.W. (2003:165) anasema  ngano ni hadithi  ya kale ambayo ni moja kati ya tanzu maarufu za fasili simulizi.  Ni moja kati ya vipera au vitanzu vya hadithi au simulizi. Ngano nyingi huwa na mwanzo wa hapo zamani za kale.

Kwa fasili yetu, tunaweza kusema kuwa, ngano ni utanzu wa hadithi fupi fupi ambazo huelezea/kusimulia matukio mbalimbali yanayoleta mafunzo katika jamii husika na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Kiini cha swali
Tunakubaliana na hoja hii inayosema kuwa, bila kuelewa sitiari na ishara katika ngano ni vigumu kumuuliza mtoto hadithi hii amejifunza nini? Ni hii ni kwa sababu ngano/hadithi nzima hujengwa na sitiari na ishara ambazo kama hazitaeleweka vizuri itakuwa vigumu kuielewa ngano husika inahusu nini. Hivyo katika sehemu hii tutaangalia baadhi ya sitiari na ishara zinazojitokeza katika baadhi ya ngano na kuzitolea maana zake na jinsi tunavyoweza kupata ujumbe kutokana na kuzielewa sitiari na ishara hizo, lakini kabla hatujajikita huko tuangalie mifano ya ngano tutakazozitumia katika mjadala wetu. (rejea Kiambatanisho cha ngano kuanzia ukurasa wa 8-20.

Sitiari katika ngano, katika ngano sitiari huweza kujitokeza kwa namna tatu, kwanza huweza kujitokeza kwa wahusika wanaotumika kisitiari. Mulokozi na Kahigi (1979:39), wanaziita sitiari za aina hii kuwa ni istiara, ambapo muhusika au wahusika wakuu katika hadithi huweza kuwa ni mwakilishi wa tabia na vitendo vya kundi fulani la watu. Njia ya pili ni kwa njia ya hadithi nzima, hapa ni kwamba hadithi nzima hujengwa kisitiari, kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho wa hadithi na matukio yanayoambatana na matendo katika ngano hujengwa kwa kuhusishwa au kufananishwa na matendo au matukio katika ulimwengu halisi. Na njia ya tatu kwa kwa kutumia matumizi ya lugha, yaani vitu viwili tofauti hufananishwa au kulinganishwa bila kutumia maneno ya kuanganisha. Mfano, matumizi ya sentensi kama vile, baba ni simba, dunia uwanja wa fujo, kilimo ni uti wa mgongo wa taifa, maji ni uhai n.k. lakini kwa kiasi kikubwa sitiari katika ngano hujitokeza katika njia mbili yaani njia ya kwanza na njia ya pili ambazo ndizo tutazitumia. Katika mifano tuliyoitoa (rejea Kiambatanisho cha ngano kuanzia ukurasa wa 8-20.) sitiari zinazojitokeza hapo ni:

Sungura amatumika kisitiari kwa kufananiishwa na mtu mwenye tabia za ujanja na hila, kwa mfano katika hadithi ya CHUI, PONGO,SUNGURA NA BUIBUI tunamuona Sungura akitumia ujanja kuwaokoa watoto wa Pongo wasiuwawe na Chui, lakini pia tumwona Sungura akitumia ujanja huo huo kujinasua kutoka katika hatari ya kukamatwa na Chui. Hadithi nyingine zinazomtumia Sungura kisitiari kumfananisha na mtu mwenye tabia za ujanja ujanja ni hadithi ya, Sungura na Fisi, Sungura Aoa pia angalia hadithi ya Je, Kuna Wema Duniani?

Funzo: katika hadithi hizi, kutumika kwa Sungura kisitiari, ukimuuliza mtoto hadithi hii inatufunza nini? Atakwambia kuwa, tunajifunza kuwa kutumia akili katika kukabiliana na matatizo katika jamii ni njia bora kuliko kutumia nguvu.

Chui pia katika hadithi hiyo ametumika kisitiari kuwakilisha tabia za watu wabinafsi, wanaotumia nguvu walizonazo kuwaonea watu wanyonge, lakini pia kuwakilisha tabia za watu wanaotumia nguvu kuliko akili katika kufanya maamuzi. Katika hadithi hiyo, tunamwona Chui akitumia hila kuwachukua watoto wa Pongo ili awafanye kitoweo. Lakini pia anaonesha tabia za watu wabinfsi kwani kwa kumuonesha kuwa anapenda kuwafanyia ubaya wenzake lakini anapofanyiwa yeye huwa mbogo.
Funzo, funzo tunalolipata kutokana na Chui kutumika kisitiari, tunajifunza kuwa, ubaya mwisho wake ni aibu, ujumbe huu tunaupata kutokana na kitendo cha Chui kumfanyia ubaya Pongo kwa kuwachukua watoto wake kuwa kitoweo lakini mwisho wake watoto wanaofanywa kitoweo ni watoto wake mwenyewe na hivyo kuishia katika aibu, lakini pia tunapata ujumbe mwingine kuwa tenda wema kadili na wewe unavyotaka kutendewa wema, tunamwona Chui akiwatendea wenzake ubaya lakini anapotendewa ubaya anakuwa mbogo na hii kufanya ionekane kuwa mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu.

Fisi pia ni mnyama mwingine anayetumika kisitiari katika ngano nyingi za Kiswahili kuwakilisha tabia za watu waroho, walafi, wajinga au wapumbavu katika jamii, kwa mfano rejea hadithi ya Sungura Aoa. Katika hadithi hii tunamwona fisi akiwa na tabia za kiroho na wizi, akiiba mbuzi wa binadamu na kuwasingizia wenzake lakini kutokana na ujinga wake hila zake hizo zinagunduliwa na Sungura.
Funzo tunalolipata kutokana na hadithi hii ni, tama mbele mauti nyuma, tunamwona Fisi tamaa yake humwingiza katika matatizo na kukosa mke.

Dege katika hadithi ya DEGE pia ametumika kisitiari katika hadithi hiyo akihusishwa na watu wenye kukemea uovu unaofanyika sirini, pia kubashiri matukio ya mbele, pia katika Hadithi ya Mama Mgumba tunamwona ndege huyo akitoa siri ya Mama Mgumba aliyoitoa kwa rafiki yake jinsi alivyopata mtoto.

Funzo tunalolipata hapa, ni kuwa duniani hakuna siri ya watu wawili. Unapokuwa na jambo ambalo unaona halitakiwi kujulikana na watu wengine ni vema siri hiyo ukabaki nayo mwenyewe kuliko kumweleza mtu mwingine. Akiingilia mtu wa pili hiyo siyo siri tena.

Mfalme katika hadithi ya Saidi na Rafiki yake Muhamed pia kuna sitiari za wahusika zinajitokeza, kwa mfano, Mfalme, ametumika kisitiari akihusishwa na viongozi wabinafsi, na wenye tama ya kupata kila kitu kwa nafasi zao, lakini  tabia yake ya hiyo inamponza mfalme kwa kurubuniwa na Muhamed na hatimaye Mfalme ananyongwa yeye. Hivyo kutokana na maana hiyo ya sitiari, ukimuuliza mtoto, hadithi hii inatufundisha nini, atakwambia kuwa, hadithi hii inatufundisha kuwa, tamaa mbele mauti nyuma. Kwa mfano tunamuona Mfalme, tamaa yake ya kutaka kwenda peponi kama alivyodanganywa na Muhamed inasababishwa Mfalme ananyongwa na kufariki.

Muhusika Kichwa kidogo katika hadithi hiyo hiyo ya Saidi na Rafiki yake Muhammed pia ametumika kisitiari akihusishwa na watu wanyonge, watu wanaokandamizwa katika jamii kutokana unyonge wao wa kutokujua sheria, kwa mfano tunaona Kichwa Kidogo ni mtu mnyonge hana hasiyekuwa na hatia lakini hakimu anataka kumdhulumu haki yake kwa sababu ya maumbile yake tu. Lakini Kichwa kidogo hanasi kitanzini anatoka na kuokoka.

Baada ya kupata maana ya sitiari hii, ukimuuliza mtoto hadithi hii inatufundisha nini, mtoto atakujibu kuwa hadithi hii inatufundisha, fimbo ya mnyonge hulipwa na Mungu.

Hakimu pia katika hadithi hiyo, ametumika kisitiari akihusishwa na mahakimu au wawakilishi wa mfumo ambao unaendeshwa na watu wasio na elimu na waliojaa inda, choyo na dhuluma. Kwa mfano katika hadithi hii ya Saidi na Rafiki yake Mohammedi. (Uk. 13-14) hakimu anamuhumu Kichwa kidogo kunyongwa hadi kufa ili hali hajafanya kosa lolote.

Kwa sitiari hii ukimuuliza mtoto hadithi hii inatufundisha nini, atakujibu kuwa hadithi hii inatufundisha kuwa si kila anayehukumiwa kufungwa jela ana hatia, wengine hufungwa kutokana na uelewa mdogo wa watu waliopewa dhamana ya kusimamia sheria, lakini inda na dhuluma.

Sitiari nyingine zinazojitokeza katika ni safari,mabonde, mito, misitu na nyika. Safari katika ngano hutumika katika ngano kuhusisha na mchakato wa makuzi, yaani kuzaliwa, kukua hadi kufa, wakati, mabonde, mito, misitu na nyika huusishwa na matatizo au vikwazo katika maisha, ambavyo binadamu anatakiwa kivivuka ili kupata mafanio. Kwa mfano rejea hadithi ya “DEGE” (uk. na KAZI KWA MFALME

Kwa sitiari hizi, ukimuuliza, mtoto hadithi hii imetufundisha nini, atakujibu kuwa hadithi hii inatufundisha kuwa maisha ni safari ndefu iliyojaa changamoto na vikwazo vingi ambavyo hatuna budi kupambana navyo ili kufanikiwa katika maisha.

Funzo lingine tunaloweza kulipata kutokana na sitiari ya safari, mabonde, mito, misitu na nyika ni kuwa, mtaka cha uvunguni sharti ainame, hii ina maana muwa mtu kama unataka mafanikio katika jambo lolote basi mtu huyo hana budi kuvumilia shida, matatizo na vikwazo vyote atakavyokumbana navyo na si kukata tamaa.

Matumizi ya Ishara.
Baada ya kuzivunja na kuzifafanua sitiari na jinsi tunavyoweza kupata ujumbe kutokana na sitiari hizo sasa tuangalie ishara, hapa pia tutaangalia maana ya ishara kama zilivyojitokeza katika ngano tunazozitumia lakini pia tutaeleza kwa namna gani mtoto anaweza kupata funzo kutokana na kuzielewa ishara hizo. Tukianza na;

Bundi, bundi hutumika kiishara kuashiria uchuro, mikosi, ushirikina, kwa mfano katika hadithi ya “Je, Duniani kuna Wema?” tunamuona muhusika baba mmoja kabla hajaenda kutafuta chakula usiku  anasikia sauti ya bundi, ambaye anaashiria balaa, nuksi au mikosi na huko mbele ya safari huyo baba anakutana na balaa la kutaka kuuwawa na jinni aliyekuwa amehifadhiwa kwenye chupa.
Matumizi ya ishara kama hizi, mtoto akizielewa maana yake na ukamuuliza hadithi hii inatufundisha nini? Atakujibu kuwa hadithi hii inatufundisha kuwa dalili ya mvua mawingu, hivyo tunapoona dalili fulani ni bora kuchukua hatua mapema kabla ya hatari kutokea.

Chupa, katika hadithi hiyo, “Je, Duniani kuna Wema?” imetumika kiishara kuashiria gereza au kifungo. Na tunamuona jini akiwekwa ndani ya chupa kutokana na uovu aliomfanyia bosi wake. Lakini jini huyo anapookolewa na binadamu kwa kutolewa ndani ya chupa jini linataka kumuua binadamu kwa kutaka kumfanya kitoweo.
Funzo, matumizi ya ishara ya chupa, na jini kuwekwa ndani ya chupa ni ishara inayotupa funzo kuwa, dawa ya moto ni moto, ikiwa na maana kuwa haifai kuwahurumia watu wanaohalifu sheria katika jamii, sharti wapewe adhabu kali kama tulivyoona adhau aliyopewa jini.
Safari, katika hadithi ya DEGE na ‘Saidi na rafiki yake Muhamed’ pia imetumika kiishara, safari imetumika kiishara kuashiria kuwa maisha ni safari ndefu yenye vingi vikwazo, kwa mfano katika hadithi ya ‘Saidi na rafiki yake Muhammed’  tunawaona akina Saidi wakisafiri kwa nia ya kutafuta elimu na katika hadithi ya DEGE tunamwona kijana akitoka nyumbani na kusafiri kwa lengo la kutafuta binti ampendaye (Kipepeo) .

Funzo, hadithi hii inatufundisha kuwa, elimu ni ufunguo wa maisha hivyo tunakiwa kuitafuta popote pale inapoweza kupatikana ili iweze kutusaidia katika maisha yetu. Lakini pia funzo lingine tunaloweza kulipata hama ni kuwa mtaka cha uvunguni sharti ainame, ikiwa na maana kuwa jambo lolote tunalolitafuta ili tuweze kulipata hatuna budi kuvumilia shida, matatizo na vikwazo mbalimbali. Hadithi nyingine zinazotumia safari kama ishara ni pamoja na Kazi kwa Mfalme, Kitambi cha Pembemauli, n.k.
Mifupa, maji na maziwa, pia hutumika kiishara kuashiria uhai, katika ngano nyingi za Kiswahili mifupa, maji au maziwa ni vitu vinavyotumika kiishara kuashiria uhai, kwa mfano katika hadithi ya “Mama Mgumba” mama Mgumba anapewa masharti na bibi Kizee ili aweze kupata mtoto achukue mfupa na kuuweka kwenye chungu na kuumwagilia maziwa, Mama Mgumba anapofanya hivyo anapata mtoto.
Kilemba pia katika hadithi ya “Kazi Kwa Mfalme.” Imetumika kiishara, atakayeweza masharti ya mfalme, mfalme atavua kilemba, hapa kilemba kinaashiria Utawala au uongozi. Na katika hadithi hiyo, mtoto anafanikiwa kwenda kuwatafuta ndugu zake na kuweza kujibu vitendawili vyote alivyotegewa na Mfalme na mfalme kumpa kilemba kama ishara ya kuumpa uongozi.
Funzo: kama mtoto ataulizwa hadithi hii inatufundisha nini? Anaweza kujibu kuwa hadithi hii inatufundisha kuwa baada ya dhiki faraja. Pamoja na matatizo ya kuwapoteza ndugu zake, wazazi kuwapoteza watoto wao hatimaye baadaye familia inaungana na kuishi maisha ya raha na faraja.
Vilevile kitendo cha jini kuokolewa kutoka ndani ya chupa na binadamu na kutaka kumuua binadamu kwa kumfanya kitoweo na kitendo cha binadamu kuokolewa na Sungura asiuawe na Jini lakini baada ya kuokolewa anaamua kumuua Sungura na kumfanya kitoewo ni kitendo cha kiishara linachoashiria kutendeana wema na tusifanyiane ubaya. rejea shairi la “Je, Duniani kuna Wema?” 

Funzo, funzo tunalolipata hapo ni kuwa shukrani ya punda mateke au tenda wema nenda zako usingoje shukrani. Na hii inatokana na sababu kuwa Jina anataka kulipa ubaya kwa wema aliofanyiwa vilevile Sungura anafanyiwa ubaya kwa wema aliomfanyia binadamu.

Hitimisho
Kama tulivyoona katika sehemu iliyotangulia, tumeziona sitiari na ishara jinsi zinavyoweza kutumika na maana zake, na matumizi ya sitiari na ishara katika ngano hutumika ili kuepusha udhibiti wa jamii, kuepusha migogoro katika jamii ambayo ingeweza kutokea kama ngano zingekuwa zinaelezea mambo waziwazi, vilevile hutumika kuifikirisha hadhira iweze kufikiria na kutafakari yale yanayojitokeza katika ngano na hivyo kukuza uelewa wao na uwezo wa kudadisi lakini pia matumizi ya sitiari na ishara huijengea jamii utu.


              KIAMBATANISHO CHA NGANO ZILIZOTUMIKA KAMA MIFANO

CHUI, PONGO,SUNGURA NA BUIBUI
Nakandai!
Nakaicha
Hapo zamani sana chui, pongo, sungura na buibui walikuwa marafiki, wakubwa. Siku moja chui alitaka kwenda kuwatembelea wazazi wake. Kabla ya kuondoka lakini aliwatwaa watoto wa Pongo na kuwafunga katika pakacha. Kasha akawaita Pongo, Sungura na Buibui na kuwaambia, “Leo ninakwenda kuwaamkia wazazi wangu. Hivyo ningependa mje pamoja name.” Wote wakakubali.
Wakaanza safari yao huku Pongo amelibeba lile pakacha.walipokuwa njiani walikutana na watu, wa wakamsalimia Chui.

“Mama Chui, HUJAMBO?” Chui akaitika, “Sijambo, wenzangu. Ila ninawadanganya wajinga , waliopeleka wenzao kuliwa.” Kusikia jibu hilo Sungura akauliza, “Maana yake nini Chui kusema hivyo?” basi, akawaomba Pongo na Buibui kwa siri, “Tufungue pakacha, tuone kilichomo.” Kwa hiyo wamwacha Chui atangulie.

Chui alipotangulia kidogo kulingana na desturi yake ya kujidai ukubwa, Sungura na wenzake walifungua pakacha. La haula! Ni watoto wa Pongo ndani: wote hai. Pale pale Pongo aliwachukua watoto wake na kuwaficha. Kasha aliwaendea watoto wa Chui na kuwaambia, “Twendeni haraka, mama yenu anawaita.” Akawaleta hadi kwa Sungura na Buibui. Buibui mara ile akawatia watoto wa chui katika pakacha , akalifunga imara kama alivyofunga mama Chui hapo awali.
Kasha fanya hivyo Pongo, Sungura na Buibui wakapiga mbio hadi kumfikilia Chui. Wakaendelea na safari huku wanapigiana vitendawili.
Baada ya muda walikutana tena na watu. Wale watu walipomsalimia chui, mama Chui aliitikia kwa kauli ile ile yake. “Ninawadanganya wajinga , waliopeleka wenzao kuliwa .” Watu hao walipomsalimai Sungura, Sungura alijibu, “Nitambua kilichomo katika pakacha ambalo sikulifunga .” naye Pongo aliposalimiwa alijibu, “Hatua moja kuficha watoto, ya pili kuchukua watoto, ya tatu kati ya wenzangu.” Naye Buibui alijibu, “Ninaufunga mzigo kama aliyeufunga.”

Waliendelea na safari. Jioni jioni walifika nyumbani kwa wazazi wa Chui. Wageni wote walipokelewa vizuri sana. Wakaonyeshwa kibanda pa kujipumzishia. Alivyojidai ni mjanja sasa, baada ya kupumzika kidogo tu, Chui alimwambia Sungura, “Nenda kwa mama yangu na mweleze apike nyama iliyomo katika pakacha bila wasiwasi.”

Mama chui alipokea pakacha, akasikiliza na maelekezo ya Sungura aliyoagizwa na Chui. Haraka bila kusita, Chui mzee akalitenga pakacha jikoni. Nyama ikatokota. Kisha akalifungua pakacha. “Loo!” alishangaa Chui mzee. Akamuliza Sungua, “Mbona hii nyama inafanana na watoto wa Chui?” Sungura akajibu, “Ndivyo yeye alivyoniagiza. Pika tu wala usisitesite.”
Hata chakula kilivyokuwa tayari wageni wote walikaribishwa mezani. Sima na nyama mbele yao. Baada ya kula tonge mbili tatu Sungura akasema, “Ama kweli watoto wa Chui watamu sana.” Chui akagutuka, “Umesemaje, Sungura?” Sungura akaitika, “Nasema hivi: Ama kweli nyama ya chumvi tamu sana.” Wakaendelea kula.

Punde si punde Sungura akatamka tena, “Utadhani tunakula nyama ya Pongo, kumbe vitoto vya mama chui.”

Hapo mama Chui alichukua kipande cha nyama na kukiangalia vizuri. La haula! Ni kichwa cha mwanaye. Vurumai na rabsha zikaanza mara. Buibui alipanda haraka kwenye paa la nyumba. Pngo na Sungura wakakurupuka nje, mbio. Chui akawaandama hawa wawili. Ndipo Pongo akakimbilia upande mmoja na sungura upande wa pili.Chui akaamua kumfuata Sungura. Sungura alipiga chenga huku na kule mpaka mwisho akawa karibu akamatwe. Kwa bahati njema Sungura akaona, mara akajitia ndani.

Karibu na hilo shimo kulikuwa na mzee Chura. Kuona Chui jinsi alivyohangaika sana, Chura alimpa Chui ushauri, “Mama Chui, hivi hivi tu huwezi kumpata Sungura . bali ukalete jembe pamoja na moto kishaye chimba  na kulifukizia moshi. Haraka sana moshi utamtoa Sungura nje.”
Shauri hili lilimpendeza sana mama Chui. Akamwambia Chura, “Tafadhli nilindie hili shimo, nikachukue haraka jembe na moto.”

Chui alipoondoka, Sungura alichungulia mlangoni na kumwangalia Chura. Kisha akamwambia, “Mzee Chura, kodoa macho nikutupie njugu.” Chura kusikia habari za njugu akatoa macho pima. Sungura haraka alizoa mchanga na kumtia Chura machoni. Chura akashindwa kuona. Ndipo Sungura akatoka shimoni na kukimbia kabisa.

Hata mama Chui aliporudi na jembe na moto, alimwuliza Chura, “Sungura bado angali ndani?” Chura huku amefikicha macho yake hata yakamvimba mfano wa njugu alijibu, “Yumo.” Mara kazi ikaanza ya kuchimba shimo na kufukizia moshi ili kumkamata Sungura.
Alichimba na kufukua, akafukizia na moshi kufa na kupona. Mwisho akaufikia mwisho wa shimo, lakini Sungura hayumo.

Mama Chui alikasirika sana kuona hata Chura amemdanganya. Alimgeukia mara akamkamata Chura na kumwambia, “sasa  hivi nitakutupa motoni ufe.” Chura akajibu , “Wanyama wote walinichoma moto wala sikudhurika. Huoni haya malengelenge?”

Mama chui akaendelea, “Kwanini umenidanganya. Basi nitakuponda ufe.” Chura akajibu huku ametulia tu, “Oo! Wanyama wote walijaribu kuniponda lakini sikufa.”

Chui kuona hana la kufanya . akamwuliza Chura, “Basi nifanye nini nikitaka kukuua?” Mzee Chura akamjibu mara moja, “Sikufichi neno mama Chui. Ukitaka kuniua, nitupe kwa nguvu zako zote .” hapo Chui alimwinua mzee Chura kwa chuki na ghadhabu, kwa nguvu zote akamtupa kwenye dimbwi la maji. Kwa furaha kubwa mzee Chura aliogelea majini hadi ukingo wa pili. Ndipo aliposimama na kumwambia mama Chui, “Bibi mkuki kwa nguruwe kwa binadamu haramu!
Ndio mwisho wa hadithi. Chanzo (Nkwera, F.K. (hakina mwaka) uk. 36-39)

SAIDI NA RAFIKI YAKE MUHAMMED
Paukwa
Pakawa
Mwanangu mwanasiti
Kijiwe kama chikichi ehe!
Basi alikuwepo mtu mmoja, anaitwa Saidi na Muhammed mtu na rafiki yake. Mohammed akamwambia rafiki yangu Saidi tusafiri tukatafute elimu, Wakakubari wakafanya safari. Hata wakafika nchi moja ambayo nchi hiyo. Maisha ya pale ni kuwa kila kitu kinauzwa riale moja. Ukitaka nyumba riale moja, ukitaka owa riale moja, ukitaka kununua mbuzi riale moja. Ukitaka kununua kuku riale moja, muradi kula kitu ni riale moja. Kwa hivyo Saidi yule, Muhammed akamwambia la, hapa mie sipakai, bora mie ntaendelea mbele. Na Saidi yule akasema la, mimi siwezi kuendelea, ntakaa hapa hapa. Kwa hivyo maisha hapa naona mazuri ntafanya biashara. Muhammed akafunga safari kuendelea mbele. Saidi yule yue akakaa akanunua nyumba, akaoa mke, ikawa anafanya biashara, muradi mambo yakamfanikia vizuri. Pale katika mtaa ule. Palielemewa na mtu na nyumba, palikuwa na nyumba moja inajengwa , kwa bahati mbaya akafa.ikawa akakatwa yule alojenga yule tajiri mwenye kujenga nyumba ile, kwamba umemuu mtu. Tajiri yule akasema, la miye si makosa yangu, nimepata mtu kotrakti, yaani mtu kutengeneza nyumba hii. Nimempa fundi kwa kazi zote miye juu yangu kutoa fedha basi ikiwa kosa kakosa huyo fundi. Akakamatwa fundi yule, kashtakiwa. Aliposhtakiwa fundi akasema la, mie si makosa yangu. Miye ndo niliyetia mafundi wadogo wadogo ili kuitengeneza nyumba hiyo. Wao ndio waliosababisha ukuta huu kuanguka kumuelemea mtu ukamuua. Ikenda kesi ikajiri mafundi wale waliojenga wakamatwe. Fundi yule mmoja alipokamatwa akasema, la si miye Abadan, mimi nilikuwa nikijenga vizuri, lakini hawa vibarua wakiuponda udongo wakaufanya laini sana. Kwa hivyo udongo ulikuwa tepetepe nyumba isijiweze hii ikaanguka ikamwelemea mtu.

Sasa ikawa wakamatwe vibarua wale walioponda udongo, vibarua walipokamatwa kwenda kwenye kesi wakasema, la, sisi kweli tumeponda udongo lakini alipita mmoja ana kichwa kidogo. Huyo kichwa kidogo huyo ikawa sote twamtizama na huku twatia maji twatizama, kutahamaki udongo umekwisha kuwa laini. Kwa hiyo tusiweze  kuunanihii tukaupeleka hivo hivo, nyumba ikawa majenzi yake laini, imeanguka nyumba. Sasa, sasa atafutwe Kichwa Kidogo yule akatafutwa akakamatwa, ikenda hukumu, akaona sasa lazima Kichwa Kidogo auliwe, hapana jambo lolote, sasa akatengenezewa kitanzi yule, ikatoka hukumu kuwa atiew kitanzi, alivyokwenda kwenda tiwa kitanzi yule Kichwa Kidogo kikawa kitanzi hakikamati, kila akitiwa chatoka. Kila akitiwa akifatuliwa atoka Kichwa Kidogo. Sasa akenda akaambiwa Hakimu bwana tumejaribu kumuua Kichwa Kidogo lakini katushinda. Kwa sasa  kila tukimtia kitanzi kichwa chake kinapenya kidogo.

Hakimu akasema, mtafuteni mtu yoyote mumuue. Kwa bahati akapita Saidi enda sokoni na Saidi kanenepa alikuwa kibaba. Wakaona huyu ndo anayefaa kuuliw huyu. Huku maadam jaji kasema auliwe huyu basi auliwe tu hapana maneno yoyote. Akakamatwa, akasema lakini miye sikufanya kitu, akaambiwa hukumu imekwishatoka uuliwe, uuliwe tu. Njoo hapa akaona hana njia ya kusema. Lakini akaomba, akasema mimi naomba, ikiwa mtaniuwa, yuko ndugu yangu Muhammed nimwagize. Maana yake nikishakufa aweze kwenda kusema kwetu na kuwapa wazee wangu mirathi. Muhammed akaagizwa yule kwa bahati akaja, alipokuja, akaambiwa Mohammed, huyu bwana imetoka hukumu hapa auliwe, kwa sababu tumepita mote tumeona hapana mtu wa kuuliwa isipokuwa yeye. Kichwa Kidogo hakufaa kitu, ambao hukumu ya mwisho kutoka kwa Kichwa Kidogo, Mohammed akasema miye nataka kuonana na Mfalme, akaambiwa, jee nini shida yako!

Shida yangu bwana mimi nna ndugu yangu hapa imetoka hukumu auliwe lakini kwa bahati naona bora niuliwe miye kuliko yeye. Kwa nini? Akamwambia siri kuwa huyo akiuliwa atakwendazake peponi. Kwa hivyo fursa hii naitaka miye, unisaidie niipate miye. Mfalme yule akafikiri akaona bai ikiwa enda peponi moja kwa moja huyu, bora niuliwe miye  nende zangu peponi. Kwa hiyo akakamatwa mfalme akakubali kwa hiari yake auliwe, mfale akauliwa. Alipkwishauliwa akamwambia jee si nimwkwambia miye saidi, tusikae nchi hii! Basi hii salama yetu, hii ni salama yako wewe kuuliwa. Sasa ninavyokueleza tenzetu unifuate huko niliko miye.

Siku ile ile wakafungafunga mizigo yao wakasafiri siku ile ile. Akamwambia hii sasa ndiyo hatari ya kukaa chi ambayo watu hawana elimu. Na hadithi yangu imeishia hapo. (Chanzo: Gibbe, A.G. na Mvungi, T.A. (1986:16-17)
MAMA MGUMBA
Hadithi hadithi1
Hadithi njoo!
1.      Katika nchi fulani ya mbali paliishi mtu na mkewe. Mama huyo alikuwa mgumba kwa siku nyingi, wala hakuzaa mtoto hata mmoja. Hali hii iliwahuznunisha sana watu hawa wawili. Walijaribu kila njia ili wapate watoto lakini hawakufanikiwa kabisa.

2.      Siku moja huyu mama alikwenda mtoni kuteka maji. Njiani alimkuta ajuza mmoja anang’oa nyasi za kulalia. Ajuza alikuwa amefunga mzigo mkubwa na mzito sana wa nyasi hata ukamshinda kujitwika peke yake. Akamwomba msaada huyu mama mgumba. Mama huyu hakusita. Wakaamkiana kiada. Kisha hapo ajuza na mama waliinua mzigo. Lakini badala ya kumtwika ajuza, mama mgumba akaomba aubebe yeye, kisha amchukuze walau njia yake. Ajuza akashukuru sana.

3.      Wakiwa njiani, ajuza aliuliza, “Mwanangu, una watoto wangapi?” mama mgumba akajibu, “Mamangu sina. Sina hata mmoja wa kumtuma maji.” Kusikia vile ajuza alihuzunika sana moyoni mwake na kumwambia, “Mama kadiri ulivyonitendea wema ndivyo name nitakufanyia wema. Basi, nenda ukachukue mfupa wowote utakaouona karibu na nyumba iliyohamwa na wenyeji wake. Ukisha uokota kauweke katika chungu nyumbani mwako. Kazi yako itakuwa kumwagilia maziwa huo mfupa kila siku. Bora zaidi uukamulie maziwa yako mwenyewe. Nawe utaona matokeo yake.

4.      Mama mgumba akafurahi sana kupata siri hiyo. Alipofika tu nyumbani kwake kutoka mtoni, alitua maji yake; mara akaanza kutekeleza agizo la ajuza. Aliokota mfupa kwenye nyumba iliyohamwa, akauweka ndani ya chungu chumbani mwake, akaukamulia maziwa kila siku. Baada ya siku saba mama mgumba alisikia mtoto analia ndani ya chungu. Akafurahi mno. Haraka alikifungua kile chungu akamtoa mtoto wa kiume, mchanga, mzuri ajabu. Furaha yake nay a mumewe ikawa kubwa sana.

5.      Mtoto alikuwa, naye akaoa.

6.      Ila, pamoja na hiyo siri ya mtoto ajuza alikuwa amemwagiza mama mgumba sharti moja, “Lolote litakalotokea usimweleze mtu yeyote.” Kumbe, ikaondokea katika furaha yake kubwa mama mtoto alisahau miko yote. Mama akamweleza jirani yake siri yote jinsi alivyompata huyo mtoto mzuri. Akiongea naye, mama alimsihi jirani yake, “Lakini nakuomba usimweleze mambo haya mtu yeyote.”

7.      Kumbe wakati hawa majirani wawili walipozungumza ile siri, kacheche (ndege mdogo sana) alikuwa ameatamia mayai yake kwenye upenu wa nyumba. Akasikia yote. Pitepite, kacheche alipomwona yule mtoto mzuri amekaa na mama yeke, akaanza kumhadithia mtoto mambo yote aliyozungumza mama mtu na jirani yake huku naye mama mwenyewe anayasikia. Mama akastaajabu sana. Pale pale mtoto wa ajabu huyo alianza kubadilika rangi na kudidimia ardhini taratibu hadi kutoweka kabisa.

8.      Mama akabaki analia na kufikiria nini atakachomweleza mume wake. Alihuzunika moyoni n kukumbuka neno la hayati bibi alilomwambia siku moja, “Mjukuu wangu kua ufikie uzee. Ila hamna siri ya watu watatu.”
(Chanzo: Nkwera, F.V (xx) uk.14-15)

SUNGURA AOA
Kwali murhu!
Dii!
Hapo kale Sungura, fisi, Chui na Ngiri waliishi nyumba moja. Walitembea pamoja na kufanya kazi pamoja; kila kitu walifanya pamoja.

Siku moja katika mazungumzo yao waliamua waoe mabinti wa watu. Baada ya makelele mengi walishindwa kuafikiana nani kati yao aanze kuoa. Hatimaye wakaamua, “Wote wane twende pamoja kutafuta mchumba. Huyo msichana atakayetupendeza sote wane, tumwachia yeye achague yupi kati yetu apenda kumwoa.

Baada ya makubaliano hayo wote wane walianza safari ya pamoja katika zunguka yao walikutana na kidosho. Kidosho, msichana mrembo aliwakata maini wote wanne.
Wote wanne walikaribishwa vizuri kwao kidosho, wakapikiwa chakula, wakala. Punde si punde wakatoa ombi lao kwa baba mtu. Baba mtu hakuwakatalia. Aliwaonyesha chumba kizuri ambamo watalala kwa siku nne; siku ya nne atawapa jibu.

Karibu na chumba walimokaribishwa wageni kulala, kulikuwa na zizi la mbuzi. Haraka fisi na chui walipata harufu ya mbuzi, wakawamezea mate. Hata ulipofika usiku wote walikwenda kulala. Katikati ya usiku mroho wa wote hakuweza kufumba macho zaidi. Fisi aliamka kwa siri, akaelekea kwenye zizi la mbuzi la yule baba mtu. Akaua mbuzi mmoja na kumla mzima. Kishaye alitwaa samadi kidogo na kuja nayo chumbani kwao. Alinyatia taratibu hadi alipolala chui na kumpaka ile samadi miguuni.
Kulipokucha baba mtu alishangaa kuona mbuzi mmoja ameliwa usiku. Alipowaangalia wageni wake alimwona chui ana samadi miguuni. Bila hili wala lile baba mtu alishika marungu na kumfukuza kabisa chui. Maskini chui alitimua mbio za kujisalimisha.
Huku nyuma fisi aliendelea na kazi yake ya usiku. Siku ya pili ngiri akafukuzwa kwa kosa hilo hilo la wizi. Sasa wakabaki Fisi na Sungura.

Sungura hakuchelewa. Aling’amua janja za fisi. Basi naye akabuni hila ya mwaka. Walipokwenda kulala usiku huo watu wa tatu, sungura alimwambia fisi, “Rafiki yangu, nakupa siri moja. Mimi ni mtu wa ajabu sana. Usiku nikilala natumbua macho, nikiwa macho nafumba kope!”

Aliposikia habari hiyo fisi alifurahi sana  moyoni mwake. Alidhani kwamba amefumbuliwa siri kubwa sana itakayomponza sungura.
Basi ilitimu usiku wa manane fisi akaamka. Kumbe sungura anamsikia, tena amefumbua macho aonekane yuko usingizini.

Fisi alikwenda zizini, akala beberu la mbuzi. Hata aliposhiba alirudi chumbani huku amechukua samadi ya kumpaka sungura . fisi alipomkaribia sungura na kumwona bado amefumbua macho kabisa kwa furaha alimsogelea ili ampake samadi. Kumbe, ghafula kabisa sungura alikurupuka na kuanza kumkemea fisi kwa sauti kali, “Fisi mwenzangu unadhani nimelala? Sikuoni? Nakuona. Wacha mchezo wako.” Basi sungura aliendelea kupiga kelele nay owe mpaka mwenye nyumba aliamka na kuja chumbani kwa wageni wake.

Ndipo sungura alimshtaki fisi uovu wake, “Baba mkwe, fisi siye wa kumwacha. Mwana haramu huyu astahili kabisa kirungu. Mwuaji, mwizi, hakuna alichobakiza.” Bila ya simile baba Kidosho alimshambulia fisi kwa kishindo kizito. Fisi alinusurika kufa. Alikimbia pasi na kuona nyuma, huku analia ovyo, “Huuuuuuuuwiii! Nimemkosa Kidosho.”

Huku nyuma, asubuhi na mapema sungura akapewa mke; akamwoa kidosho.
Mwisho wa hadithi. (Chanzo: Nkwera, F.V (xx) uk. 65-67)

JE, DUNIANI KUNA WEMA
Hadithi hadithi!
Hadithi njoo
Hapo zamani za kale palitokea baba mmoja na mkewe ambao walibahatika kuwa na watoto watatu. Katika nchi ile kulikuwa na neema nyingi yaani ardhi yenye rutuba, watu walijipatia mazao mengi na mifugo ya kutosha. Basi kiama kikaja bonge la njaa likaikumba nchi ile watu wakadhoofika kwa kukosa chakula, wanyama wengi wakaffa na wengine kudhoofika sana. Basi yule bwana akawaza na kuwazua akaona bora atafute jitihada za kuinusuru familia yake kwa kuwa kazi yake kubwa alikuwa mwindaji. Akaomba ushauri kwa mkewe naye hakuwa na kipingamizi alimruhusu.

Lakini kabla ya kuondoka usiku ule wakiwa wamelala yeye na mkewe mara wakasikia mlio wa bundi juu ya paa lake, uuuuuuuwi! Uuuuuuwi! Uuuuuwi! Basi wakafadhaika sana kwani walijua kuwa huo ni uchuro mkubwa sana. Mkewe akamwonya mumewe asiende kwani angeweza angeweza kukumbwa na mabalaa mengi huko aendako. Lakini yule baba hakuwa na namna ya kufanya kwani aliona hata akikaa na kuacha kwenda kutafuta chochote familia yake itaangamia.

Basi siku ya siku ikawadia safari ikaanza, akasafiri kwa masaa marefu sana bila ya mafanikio, lakini apiga moyo konde. Aliendelea na safari yake ya nyika na jangwa. Akafika sehemu yenye bonde kubwa sana akawaona wanyama wengi wakila majani kwa furaha kubwa. Bwana yule akaona atafute mbinu mbadala ya kuwapata, akaamua kutafuta ulimbo na majani ya miti akajigandisha mwili mzima ili wanyama wasiweze kujua kuwa ni adui yao. Katika harakati za kuwanyatia akajikuta katumbukia kwenye shimo, looo! Wanyama wakashtuka na kukimbia yule bwana akajuta sana kwa uamuzi alioufanya kwani hakuambulia chochote. Lakini hakukata tama akaendelea mbele na safari yake. Alipofika mbali sana aliona bonge la chupa ya dhahabu akafurahia sana, akaona sasa umaskini kwa heri na maisha ya neema yamekaribia. Kasogelea ile chupa akapata shauku ya kulifungua, alipofungua tu mara zimwi jinni hiloo! Loo! Bonge la jinni akatetemeka sana lakini hakuwa na ujanja.

Jini likamshika na kumwambia nashukuru sana kwa kunitoa kifungoni cha miaka saba. Nilimuuzi tajiri wangu naye akanipa kifungo hiki cha maisha. Sasa nashukuru sana kwa kunitoa na utakuwa kitoweo change maana sijala muda mrefu. Yule bwana kajaribu kujitetea lakini jinni halikuelewa somo. Mara Sungura huyo kapita pale kichakani kasikia mzozo uliopo baina ya binadamu na jinni, sungura akawauliza kulikoni.

Basi jini akamweleza sungura kesi yake, na binadamu naye akamweleza mwanzo na chanzo cha safari yake mpaka kukutana na mkasa huo. Basi sungura akaomba ili kila mmoja apate haki yake, kila mtu arudi alikotoka ili tuanze upya na utatuzi utapatikana na kila mmoja ataridhika na matokeo hayo. Basi Sungura akasema tuanze na wewe jinni urudi kwenye chupa tukufungie na binadamu arudi alikotoka na mimi nirudi nilikotoka ili tukirudi tutajua la kufanya, Jini akakubali. Mara tu Jini aliporudi akafungiwa ndani ya chupa, sungura akasema sasa kwa sababu wewe unajitia jeuri utaendelea kubaki humo humo ndani ya chupa kama tajiri yako alivyokusudia ufie ndani ya chupa.

Yule bwana kuona hali ile akamshukuru sana sungura kwa kumwokoa mikononi mwa yule jinni. Basi wakaagana ili binadamu aendelee na safari zake na sungura ashike zake. Yule bwna alipopiga hatua mbili akakumbuka kuwa nyumbani watu hawana kitoweo na anasubiriwa ili ainusuru familia yake, akageuka nyuma na kumwona mnyama aliyekaribu naye akiwa ni sungura, akampiga mshale pale pale, sungura akafa, binadamu akamchukua tayari kwa ridhiki ya siku hiyo.
Hadithi yangu imeishia hapo. (Chanzo: imesimuliwa na Magreth mwanafunzi wa M.A. Kiswahili 2014)

DEGE

Hapo zamani za kale waliondokea mtu, mkewe na mtoto wao wa kiume. Watu hao walikuwa na maisha mazuri tu ambayo hayana hitaji lisilokidhiwa.

Siku moja, majira ya asubuhi sana, yule mtoto mwanamume alikuwa nje akicheza. Mara hiyo akamwona kipepeo mzuri mmmmmno. Mwenye rangi mzomzo, zilizooana kwa urembo na ulimbo wa ajabu.

Yule mtoto akawa anajaribu kumkamata yule kipepeo kwa kuchupa na kumrukia kama sungura na zabibu.

Alichupaaaaaa, akaruka huyooo. Lakini kila akichupa na kuruka, utadhani waliagana na kipepeo yule, kwani kipepeo pia alichupa na kuruka. Mtoto alizidi kuchupa na kuruka, akiwa anamfuatia yule kipepeo. Yakawa ni mashindano ya kuchupa na kuruka. Haooooo! Msitu na nyika, msitu na nyika; hata kushtukia wako mbaliiii! Mtoto hajui mbele wala nyuma, hajui pa kupata njia wala pa kupotelea. Mradi tu alijikuta yuko pake yake, kachoka taabani wa Shaabani, kiu imemkamata kijana, ulimi nje nje kama wa mbwa. Na kipepeo naye nd'o hivo, haonekani tena.
Basi bwana! Kijana wetu huyo alikaa chini ya mti ambao ulikuwa umeambatana na mwamba uliokuwa katikati ya njia kubwa. Akawa anawaza ya nyumbani, lakini afanyeje masikini wa watu. Na jua nalo nd'o hivo linakwenda kama lilivyopangiwa. Njaa imembana, na kiu kimemkamata; afanye nini?
Ghafla, kijana wetu akaona matone yadondokayo kutoka kwenye mwamba. Matone yakazidi kudondoka, makubwa hayoo. Kijana akakurupuka huyoooo! Mbio kama vile kamwona tena yule kipepeo. Akaokota kifuu cha nazi, akayakinga yale matone. Akakinga weee! Hata wakati maji yale yanakaribia kujaa, akaona ayanywe kuituliza ile kiu yake kali. Akaelekeza kifuu chenye maji mdomoni mwake. Lakini, ghafla, likaja dege kubwa hilo! Dege lisilo na mfano. Mbawa zake zilikuwa zikipiga, na upepo karibu umwangushe kijana wetu. Hilooo, likakipiga kile kifuu na kuyamwaga yale maji yooote! Halafu likajiendea zake likimwacha kijana anahaha kwa kiu na woga. Lakini kijana wetu hakukata tamaa. Alikinga mara ya pili; tena akawa ameshikilia kifuu imara zaidi ya mara ya kwanza. Alipojaribu kunywa, lile dege hilooo! Likampokonya kile kifuu tena.

Mara ya tatu yalipotokea yale, kijana akaamua kwenda juu ya mwamba kuona kulikoni huko yanakotokea yale maji.Akapanda, akapanda, akapandaaaa! Halafu hukooo juu kabisa ya ule mwamba, kijana akalikuta joka! Joka joka hasaaa! Limelala utadhania limekufa, ijapokuwa macho yake makubwa kama nazi yalikuwa yakigeukageuka kama ya kinyonga. Kijana hakulikaribia dude lile; bali pale akagundua yalikokuwa yanatoka yale maji. Domo la joka lile lilikuwa wazi, na sumu yalo ikitiririka kama maji mferejini hadi kule chini ya mwamba. Kijana mwili ulimsisimka, moyo ukamchachatika. Alijua.

Ghafla, lile dege likaja tena. Mara hii si kwa kasi kama mwanzo. Masikini kijana wetu. Kule nyumbani wazazi wake wote wawili, wa kuukeni na wa kuumeni walikuwa wakikata roho kwa huzuni ya kumpoteza mtoto wao.

Lile dege likamjia yule mwanamume na kumchukua hangahanga, juu kwa juu. Likawa linampepea mwanamume yule asiungue jua. Lilipaaaaaaa. Halafu ghafla likaanza kushuka. Kijana mwanamume alipoangalia chini akajua kuwa karudishwa nyumbani kwao. Akafurahi, na hadithi yangu ikaishia hapo hapo. (Chanzo: Senkoro. F.E.M.K. 2014)

 KAZI KWA MFALME

Alikuwepo mtu na mumewe na watoto wao wawili.  Kutokana na hali ya maisha waliyonayo mtoto mkubwa aliamua kuondoka kwenda kutafuta kazi. Aliambiwa na watu kwamba kwa Mfalme kuna kazi, lakini kuna masharti yake, pindi ukishindwa utafungwa na ukimshinda mfalme atavua kilemba chake.  Masharti yenyewe ni: Mfalme atatoa vitandawili vyake uvijibu na wewe utowe vyako avijibu.
Siku ilipowadia mtoto alifika kwa mfalme na akapewa masharti na akayakubali.  Mtoto akaanza kutoa vitandawili vyake vikajibiwa vyote, zamu ya mfalme mtoto akashindwa na akapelekwa kufungwa.

Siku zilipita mtoto wa pili naye akaamua kumtafuta kaka yake.  Alipita njia ile ile na kupewa masharti yale yale.  Alishindwa na akafungwa.

Mama yao alijaaliwa kupata mtoto wa mwisho na kila siku mtoto yule akifanya kosa mama yake husema, "Wawili wamepotea na kwa hiyo si kitu."

Yule mtoto yalimuingia ndani ya kichwa maneno yale, akamuuliza baba yake. Baba yake akamwambia, "Nenda kamuulize mama yako!"  Mama alimuhadithia yote yale.  Mtoto akasema "Kesho kutwa nitakwenda kuwatafuta."  Mama alimkubalia, lakini baada ya kukaa na mumewe wakashauriana wakaona bora mtoto afe pale pale kuliko kufa kama walivyokufa wenziwe. Mtoto aliendelea kuwasihi mpaka wakamkubalia.

Siku ilipowadia mtoto alifunga mizigo yake tayari ili asubuhi sana aanze safari.  Wakati amelala mtoto alioteshwa kuwa mama yake anataka kumuuwa, ameweka kisu ili akenda kumuaga amchome nacho.  Usiku ule ule aliamka na kuchonga kisu cha bao na kukibadili na kile ambacho mama yake angeweza kumuuwa nacho. Kile kisu hasa akakichukua yeye.

Asubuhi alikwenda kumuaga. Alipogeuka nyuma mama alichukua kisu akamrushia, mtoto aligeuka nyuma na kumuuliza mama yake, "Nini hicho"?  Mama alisema "Ah nilikuwa nikijaribu tu sababu baba yako eti anataka kwenda kuwinda".  Mtoto kuona vile akavunja safari akamwambia mama yake kuwa safari itakuwa kesho yake.

Ilipofika usiku alioteshwa tena mama yake kaweka mshale, alikwenda akauondowa na akauweka wa mbao.  Alipokwenda kumuaga alfajiri alimrushia nao, alipogeuka alimueleza maneno yale yale, na mtoto alivunja tena safari. Ikawa siku iliyofuatia usingizini alioteshwa tena, lakini hakujua kuna nini. Alipoamka alimuaga mama na baba yake.  Alipewa chai na mkate na maandazi. Akanywa na kula, na mengine akafungiwa, mlikuwa mna maandazi yenye sumu.

Alianza safari yake ya kutwa nzima. Aliposikia njaa alitoa andazi lile lenye sumu, alitokea paka ikawa analia sana akamkatia andazi akampa, wakati paka anakula andazi yule mtoto anamtizama. Mara paka akawa anapepesuka; na mara akafa pale pale.  Akatokea mbwa nae akamla paka.  Mbwa baada ya muda akafa.  Wakaja nguruwe watatu, wakamla mbwa nao wakafa. Wakaja wasasi sita nao wakakatiana nguruwe. Watu wawili wakachoma wakala wakafa.

Mambo yote yale mtoto anayatizama akachukua mikuki yao yote sita na like andazi kipande akenda zake, Alikwenda hadi alipofika kwa mfalme.  Mfalme alimueleza yale yale aliyowaeleza kaka zake na alikubali.  Mfalme alitoa vitandawili vyake vitatu na mtoto akavijibu. 

Zamu ikafika kwa mtoto.  Alikumbuka yaliyomtokea, na baadaye akasema,  `Kitandawili!"
Akajibiwa, "Tega!"
"Nusu imeuwa moja, moja imeuwa tatu, tatu imeuwa sita.'
Mfalme akawaza, hakujuwa la kumjibu.  Hivyo alishindwa, na akavua kilemba chake akampa yule mtoto.  Mtoto akashika ufalme na akawafungua ndugu zake pamoja na wote waliofungwa.  Mfalme mpya alikaa na kaka zake kwa raha zote. (Chanzo: Senkoro. F.E.M.K. 2014)

Kazi imeandaliwa kwa pamoja na Venance, Furaha, Margareth Waivyala na Zuhura Katoto wanafunzi wa mwaka wa kwanza UDSM, M.A.KISWAHILI 2014/2015