Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

KISWAHILI

UHAKIKI WA USHAIRI

DIWANI: FUNGATE YA UHURU, MWANDISHI: MOHAMED SEI KHATIBU


MCHAPISHAJI: MACMILLAN AIDAN, MWAKA: 2007 [TOLEO LA PILI]




MHAKIKI: MWL. FURAHA VENANCE  SIMU    0715- 33 55 58


                                                               Mwl. Furaha Venance

Tuanze uhakiki huu, kwa kuanza na :

KIPENGELE CHA MAUDHUI


Dhamira
Hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Na katika diwani hii kuna  dhamira kuu na dhamira ndogondogo ambazo zimejitokeza, kwa kuanza tunaanza na;
Dhamira kuu
Dhamira kuu ni wazo kuu linalojitokeza katika kazi za fasihi, na katika diwani hii, wazo kuu ni ukombozi wa jamii, sasa tuanzekuangalia ukombozi huo wa jamii, namna unavyojadiliwa katika diwani hii:


Ukombozi wa jamii
Dhamira kuu inayojitokeza katika diwani hii ni ukombozi wa jamii, mwandishi amejadili ukombozi huo katika Nyanja mbalimbali kama vile ukombozi wa kisiasa, kiuchumi na kiutamduni.
  
Ukombozi wa kisiasa

Kwa kiasi kikubwa mwandishi amejadili ukombozi wa kisiasa, mwandishi anaona kuwa ili jamii iweze kujikomboa kisiasa, jamii hiyo haina budi kuondokana na matatizo ya kiungozi [uongozi mbaya] uongozi ambao hauwajali wananchi zaidi ya kujali matumbo yao na maisha yao huku wakiwaacha wananchi waliowengi wakiishi maisha ya tabu na dhiki hu kundi hilo la viongozi wachache wakifaidi matunda ya uhuru, kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Fungate ya Uhuru" ubeti wa kwanza anaposema,


"Karamu za fahari, mabembe ya kupepea.
Na majumba mazuri, wamekwisha jijengea.
Watembea kawa magari, hivi zimewazowea." Uk.1



Katika shairi la Viongozi wa Afrika mwandishi pia anasema,


"Viongozo wa Afrika
Wanaotumia mapesa,
Wakaogelea anasa,
Nayo mitindo ya kisiasa,
Wakavamia kwa sesa.." Uk. 21






Vile vile mwandishi anaishauri jamii yake ili iweze kujikomboa kisiasa, jamii hiyo haina budi kufuata itikadi ya ujamaa ambayo mwandishi anaamini kuwa itikadi hii ni tumaini kwa wavuja jasho na wafanyakazi. Rejea shairi la ‘Ujamaa’ ubeti wa pili na tatu [uk. 30]




Mwandishi pia anaitaka jamii yake ili kujikomboa kisiasa, inatakiwa jamii hiyo kuondokana na kupiga viata ukoloni mamboleo, kama tunavyofahamu kuwa ukoloni mamboleo ni ile hali ya nchi kupata uhuru wa bendera lakini kiuchumi, kitamaduni na hata kujiamulia mambo yetu wenyewe kuwategema wakoloni au mataifa ya kimagharibi na Amerika.rejea katika shairi la "Afrika" Uk. 22-23



Masuala mengine ambayo mwandishi anayajadili katika ukombozi huu wa kisiasa ni pamoja na jamii kupinga utawala wa kidikteta unaokandamiza jamii kwa kutawala kimabavu, kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Viongozi wa Afrika"
"Viongozi wa Afrika, wanaotawala kwa mabavu,
Kujifanya ni washupavu,
Wao wachache ni werevu,
Na umma wote ni wapumbavu,
Wanafiki,
Wazandiki."



Katika shairi la "Maendeleo ya Umma" ukurasa wa 2-4 mwandishi anasisitiza hili la kupinga utawala wa kidekteta ili kujikomboa kisiasa anaposema katika ubeti wa nane [8]
Maendeleo ya umma
Watu kuwa na kauli
Katika zao shughuli
Vikaoni kijadili
Na mwisho kuyakubali
Maamuzi ya hali
Udikteta la!
Mwandishi naonesha njia za kuondokana na utawala wa aina hii ni kama vile, jamii kuungana na kupambana na hali hii, jamii kujitoa muhanga, kwa mfano mwandishi anaonesha haya katika shairi la "Unganeni!" anaposema;
Wafanyakazi wa Afrika, tuunganeni,
Na wakulima kadhalika, tushikaneni,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa Mapambano, yalo Marefu,
Ushindi ni wetu.



Pia rejea mashairi ya "Ningekuwa na sauti, Nikizipata Bunduki, Gorila,Afrika,Utawala, Ni vita Si Lelemama, Siku Itafika,Naona n.k" mashairi haya mwandishi anaelezea njia mbalimbali ambazo jamii ya kiafrika inaweza kuzitumia ili kujikomboa kisiasa kwa kuondoka na tawala dhalimu na za kidikteta.
Ukombozi wa Kiuchumi
Hii ni aina nyingine ya ukombozi amabao mwandishi Mohamed Seif Khatibu amelijadili katika diwani hii. Mwandishi anaonesha kuwa jamii ya kiafrika inatakiwa kujikomboa kichumi kwa wafanyakazi na wakulima kuungana kupambana na unyonyaji unaofanywa na mataifa ya Ulaya na Amerika ili kujikomboa kiuchumi, kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Afrika" ukurasa wa 22-23.
Bara la Amerika, Na Ulaya kadhalika,
"Wamestaarabika"
Kunyonya Afrika, Ni kwa mingi miaka,
Nasi tukafukarika.



Vilevile mwandishi anaonesha kuwa ili jamii iweze kojikomboa kiuchumi inatakiwa njia kuu za uzalishaji mali umilikiwe na dola/serikali na si kuwa mikoni mwa watu wachache tu, mwandishi anathibitisha hili katika shairi la "Maendeleo ya Umma" ukurasa wa 2-4 hususani katika ubeti wa tano [5] anaposema;
Maendeleo ya umma
Dola kuthibiti vitu
Vijapo nchini mwetu
Na kuwauzia watu
Toka nguo na sapatu
Pasibakishiwe na kitu
Huo usawa!



Lakini pia mwandishi anaiasa jamii yake kuwa maendeleo ya kiuchumi sit tu kuonekana kwa vitu madukani, kujaa kwa vitu maghalani, wa si vitu kuonekana kwa masoko yetu, bali ili jamii iweze kujikomboa kiuchumi maendeleo hayo ya kiuchumi ni lazima vitu hivyo vimilikiwe na wanyonge ambao ndiyo wengi katika jamii zetu, maisha ya watu wote bila kujali kipato chao, kuwa rahisi, rejea tena shairi la "Maendeleo ya Umma" ukurasa wa 2-



jamii kupinga matabaka amabayo husababisha watu wachache katika nchi za kiafrika kunufaika na rasilimali za nchi huku wakiwaacha wananchi waliowengi kuwa hoi kiuchumi, vilevile mwandishi anaitaka jamii yake kuchukua hatua kupambana na viongozi wezi, wanaondekeza maisha ya anasa na kujilimbikizia mali kuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya kiuchumi kwa jamii na nchi husika.
Ukombozi wa Kiutamaduni
Mwandishi pia amejadili suala la ukombozi wa kiutamaduni, mwandishi anaitaka jamii yake kujikomboa kiutamaduni kwa jamii kuwa na utamaduni wa kuheshimiana na kuwa waungwana kama ambavyo utamaduni wa kiafrika unavyotutaka kuishi kwa kuheshimiana na kuwa waungwana kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Maendeleo ya Umma" ubeti wa tisa [9]
Maendeleo ya Umma
Watu kuwa waungwana
Vijakazi na watwana
Nchini kuwa hakuna
Wote kuheshimiana
Wazee hata vijana
Wote ni sawa

Tofauti na sasa katika jamii yetu inayotuzunguka ambapo watu wamekuwa si waungwana, vijana kutokuwa na heshima kwa wazee n.k



Vilevile mwandishi anaitaka jamii yake kujikomboa kiutamaduni kwa kuithamini lugha yake kwa kuwa lugha ni nyenzo muhimu sana katika ukombozi wa kiutamaduni, katika diwani hii mwandishi anaitaka jamii ya kitanzania kuwa na utamaduni wa kuithamini na kuienzi lugha ya kiswahili kwa kuifananisha mgodiau zawadi/tunu isiyokwisha, kama ambavyo anasema katika shairi la "Dafina" ukurasa wa 8-10
Paa, ni kuruka angani, kama ndege na tiara.
Paa, ni mnyama porini,ni mwenye nyingi papara.
Paa,ni kuteka mekoni, moto uwake imara.
Paa, ni toa magambani, samaki atiye sura.
Paa, pia la nyumba, kmakuti au karara.
Dhamira ndogo ndogo
Usaliti

Suala la usaliti pia limepewa nafasi katika riwaya hii, mwandishi amejadili usaliti unaofanywa na viongozi wengi wa kiafrika wanaopewa dhamana za uongozi katika nchi zao. Kwa mfano wakati wa kudai uhuru viongozi waliuaminisha umma kuwa tukijatawala wenyewe kutakuwa na usawa kwa watu wote na maisha yatakuwa mazuri kwa kila mwananchi tofauti na maisha yalivyokuwa katika tawala za kikoloni, lakini mara baada ya kupata uhuru, viongozi hao hao wakausali umma kwa kuanza kujiangalia wao, kijitajirisha wao, kuwakandamiza na kuwanyonya wananchi, kuendekeza maisha ya anasa na starehe huku wananchi walio wengi wakiishi maisha ya tabu na dhiki, Mwandishi anaonesha usaliti katika shairi La "Fungate ya Uhuru" ubeti wa kwanza anaposema,;


"Karamu za fahari, mabembe ya kupepea.
Na majumba mazuri, wamekwisha jijengea.
Watembea kawa magari, hivi zimewazowea." Uk.1


Vilevile katika shairi la "Tumesalitiwa!" mwandishi anaendelea kuzungumzia suala hili la usaliti wa viongozi kwa umma anaposema;


Nikate tama?
Kwani tuendavyo hatufiki.
Vile ipasavyo, hayakamiliki.
Mambo yalivyo, ni unafiki.
Tumesalitiwa!

Lakini pia mwandishi anaonesha namna ambavyo usaliti lilivyokuwa ni tatizo kwa nchi nyingi za kiafrika, kwa mfano mwandishi anaonesha namna ambavyo viongozi wanavyozisaliti nchi zao kwa kuhongwa na mabepari bila kujali uhai wa mataifa yao, mwandishi anaonesha hili katika diwani yake katika shairi la "Viongozi wa Afrika" uk. 21-22 hususani katika ubeti wa 8 anaposema;



Viongozi wa Afrika,
Wanaohongwa na mabepari,
Kwa kuutaka utajiri,
Bila ya kujali hatari,
Nchi zao kuwa fakiri,
Majasusi,
Mafisadi.

Hivyo mwandishi anaitaka jamii yake kupambana na viongozi wasaliti kwa kuchukua hatua mbalimbali kama vile kuwakamata na kuwachukulia hatua kali, kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Nikipata Bunduki" uk. 11-12 hususani ubeti wan ne [4]






"Nikizipata shembea,
Takamata viongozi, wasaliti wa nchini,
Niwachinje kama mbuzi miiko wasoamini…"

Mashairi mengine yanayozungumzia dhamira hii ni pamoja na shairi la "Ni Vita Si Lelemama" uk. 34, "Wingu" uk. 35,



Ukigeukia katika jamii yetu, ni kweli usiopingika, viongozi wasaliti wapo, amabao wameamua kuusaliti umma kwa kuamua kujilimbikizia mali huku wanachi wakiishi maisha ya shida kwa kukosa huduma muhimu kama vile afya, elimu, maji n.k kwa sababu tu viongozi hujijali wao tu na si jamii inayowatawala na wengine kuhongwa na watu matajiri au mataifa mengine ili kuuza rasilimali za mataifa yao bila kujali hatari yoyote ile, huu ni usaliti na jamii inatakiwa kuupinga kwa nguvu zote.



Unafiki
Hii ni hali ya mtu kujifanya rafiki huku ni adui, au kutokuwa mkweli katika maneno yake na vitendo vyake, suala hili la unafiki pia limeshughulisha kalamu ya mwandishi kwa kuonesha namna ambavyo tabia ya unafiki ilivyoshamiri miongoni mwa watu tunaowaamini, kama vile viongozi wa serikali na hata viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini. Kwa mfano mwandishi anaonesha unafiki unaofanywa na viongozi wa serikali kwa kujifanya ni wafuasi wa mfumo na itikadi ya ujamaa huku wakitumia nguvu kubwa kuihubiri majukwaani ili hali matendo yao yakiwa ni ya kibepari, kama vile kujilimbikizia mali n.k. kama mwandishi anavyothibitisha hili katika shairi la "Nikizipata Bunduki" uk. 11-13 anaposema;
Nikipata mikuki,
Lazima ntawachoma, "wajamaa" wa zamani,
Mali nyingi walochuma, kwa hotuba jukwaani,
Ni dhahiri,
Watughuri, mabepari,
Matajiri,
Hubiri haziwalishi!



Vilevile mwandishi ameonesha unafiki unaofanywa na viongozi wetu wa dini, ambao madhabahuni katika makanisa ni misikiti wamekuwa wakihubiri watu kuacha dhambi kama vile wizi n.k. huku wao wakiishi maisha kama wacha Mungu kumbe nyuma ya pazia wamekubuhu kwa wizi tena hata kuwaibia waumini wao. Hili linathibitishwa na mwandishi katika shairi la "Wizi" uk.25 mwandishi anaposema;
Wizi umo;
Kanisani,
Msikitini,
Hekaluni,
Wanyang’anwao ni fukarini.
Vilevile mwandishi anaonesha namna vyombo vya dola kama vile polisi na majeshi mengine ambao jukumu lao kulinda watu na mali zao kinyume chake huwalinda wezi wanaowaibia wananchi, mwandishi anathibitisha hili katika shairi hilo hilo la "Wizi" [uk. 25] ubeti wa tano [5] anaposema;
Walinzi hawapo? La hasha!
polisi hulinda wezi,
majeshi huhalalisha wezi,
na dini zawabariki wezi.
Tukiangalia uhalisia wake haya yanayozungumzwa na mwandishi kwa jamii yetu inayotuzunguka, yana uhalisia kwani yanatokea katika jamii yetu, wapo viongozi wa dini ambao na waumini ambao kwa maneno hujifanya kama watu wema wakati matendo yao ni kinyume. Na hata vyombo hivyo vya dola katika jamii yetu, mchana wanajifanya kama walinzi wetu, usiku hushirikiana na wezi au viongozi wasiowaaminifu kuwaibia wananchi na taifa kwa ujumla, unafiki wa aina hii unatakiwa kupigwa vita.
Unyonyaji
Mwandishi hakuwa nyuma, kujadili suala la unyonyaji katika jamii yake, anaonesha namna ambavyo kundi moja huishi kwa kulinyonya kundi lingine, kwa mfano mwandishi, anaonesha namna ambavyo mataifa ya Ulaya na Amerika yanavyozinyonya rasilimali za nchi zinazoendelea hususani nchi za kiafrika na hivyo kuzifanya nchi hizo kuendelea kuwa masikini ingawa nchi hizo zina rasilimali za kutosha, mwandishi anathibitisha hili anaposema katika shairi la "Afrika" ukurasa wa 22-23.
Bara la Amerika, Na Ulaya kadhalika,
"Wamestaarabika"
Kunyonya Afrika, Ni kwa mingi miaka,
Nasi tukafukarika.
Vilevile mwandishi anaonesha namna ambavyo wakulima wakivuja jasho kwa kutumia nguvu nyingi kulima mazao mbalimbali lakini wanapovuna hayo mazao yao na kuyapeleka sokoni, huko hunyonywa kwa kwa kuuza bei ya chini thamani isiyolingana na nguvu waliyotumia kuzalisha. Hili mwandishi anathibitisha katika shairi la "Naona" uk. 41-42, anaposema;
Naona
Wanakwenda gulioni
Mazao kuyazabuni
Wanapata bei duni
Na kubaki maskini
Unyonge uleule.



Ili kuondokana na unyonyanyi wanaofanyiwa wakulima na wafanyakazi, mwandishi anawataka wafanyakazi na wakulima kote Afrika kuungana kupambana na tabaka linalowanyonya, kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Unganeni" uk. 1-2
Wafanyakazi wa Afrika, tuunganeni,
Na wakulima kadhalika, tushikaneni,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa Mapambano, yalo Marefu,
Ushindi ni wetu.






Mashairi mengine yanayozungumzia dhamira hii ya unyonyaji ni pamoja na, "Utawala"uk. 28-29, "Njama" uk.29, "Wengine" uk. 24, n.k
Hata tukiigeukia jamii yetu ya leo, bado mataifa ya Ulaya na Amerika yanazinyonya nchi za kiafrika kupitia mgongo wa viongozi wasiowaaminifu, nab ado tabaka la wafanyakazi na wakulima wanaendelea kunyonywa kwa malipo yasiyokidhi mahitaji yao huku wakiwatajirisha watu wachache. Hivyo tunatakiwa kupambana kupinga unyonyaji wa aina yoyote ile kama mwandishi anavyoasa.
Wizi wa mali za umma/ufisadi
Suala la wizi wa mali za umma au ufisadi kama inavyojulikana kwa sasa linajitokeza katika diwani hii, mwandishi anajadili namna ambavyo viongozi mbalimbali wa kiafrika wanavyojitajirisha kwa kuiba rasilimali za taifa na hivyo kuzifanya nchi zetu kuendelea kuwa nyuma kiuchumi, rejea katika shairi la "Fungate " ubeti wa kwanza anaposema,
"Karamu za fahari, mabembe ya kupepea.
Na majumba mazuri, wamekwisha jijengea.
Watembea kwa magari, hivi zimewazowea." Uk.1



Dhamira nyingine zinazojitokeza ni kama vile, kupiga vita rushwa, matabaka, kujitoa muhanga, umojana na mshikamano, ukabila n.k



VIPENGELE VYA FANI
MUUNDO
Katika utanzu wa ushairi, muundo tunaangalia idadi ya mistari katika beti, kama mwandishi katika diwani yake atatumia mistari miwili katika kila ubeti, basi tutasema kuwa mwandishi ametumia muundo wa tathnia, na kama atatumia mistari mitatu kwa kila ubeti, tutaseama kuwa mwandishi ametumia muundo wa tathilitha, na mistari mine ni muundo wa tarbia na mistari mitano na kuendelea utakuwa muundo wa takhmisa.



Kwa upande wake, mwandishi Mohamed Seif Khatibu katika diwani hii, ametumia muundo changamano kwani mashairi tunayoyaona katika diwani hii ametumia miundo zaidi ya mmoja. Kwa mfano kuna mashairi ya muundo wa:
Tathnia [Mistari miwili]
Mfano wa shairi lenye muundo huu ni shairi la "Mjamzito" uk. 7-8
Ubeti 1. Mjamzito, Amelazwa "thieta"
Lazima kupasuliwa.
Ubeti 2. Chake kitoto, tumboni kinatweta,
Hawezi kujifungua.
Ubeti 3. Mwili u moto, tumbo linamkeketa,
Kwa kite anaugua.

Tathilitha [mistari mitatu]
Mfano wa shairi lenye muundo huu ni shairi la "Waja wa Mungu" uk. 27
Ubeti 1. Dunia, vyakula hawavioni, mafakiri,
Lakini, vyakula kwao pomoni, mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu!
Ubeti 2. Duniani, wanalala majiani, mafakiri,
Lakini, wanalalaghorofani, mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu!
Ubeti 3. Duniani, nguo mbovu matakoni, mafakiri,
Lakini, nguo tele kabatini, mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu!
Mashairi mengine yenye muundo huu ni shairi la "Fungate" [uk, 1], "Nataka Kusema" [uk. 18], "Nia Yangu Sigeuzi" [uk. 46], "Uwapi Uzuri Wako" [UK.46-47], "Sakubimbi" [uk.44], "Paka Shume" [uk.45], "Wewe Peke Yako" [uk.45]

Tarbia [mistari minne]
Mfano wa shairi lenye muundo huu ni shairi la "Afrika" uk. 22-23
"Bara la Amerika, Na Ulaya kadhalika,
"Wamestaarabika"
Kunyonya Afrika, Ni kwa mingi miaka,
Nasi tukafukarika."



Mashairi mengine yenye muundo huu ni pamoja na shairi la "Nahodha Mtwesi" [uk.6], "Gorila" [uk.14], "Kunguru" [uk. 26], "Ua Si Ruwaza Njema" [uk.47-48]
Takhmisa/sabilia [Mistari mitano au zaidi]

Shairi lenye muundo huu ni shairi la "Unganeni" [uk. 1-2]
Wafanyakazi wa Afrika, tuunganeni,
Na wakulima kadhalika, tushikaneni,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa Mapambano, yalo Marefu,
Ushindi ni wetu.



Mashairi mengine yenye muundo huu, ni pamoja na "Dafina" [uk.8], "Ningekuwa na Sauti" [uk.10-11], "Utawala" [uk.28-29], "Njama" [uk. 29], "Ladha ya Maji Katani" [uk. 35-37] "Mkata" [uk.19], "Joka la Mdimu" [uk. 40] n.k
MTINDO
Mwandishi amatumia mtindo changamano yaani amechanganya mitindo yote ya aina mbili, yaani mtindo wa kimapokeo na mtindo wa kisasa [mambo leo].
Mtindo wa Kimapokeo
Mtindo wa kimapokeo ni mtindo unaofuata na kuzingatia urari wa vina na mizani , kuwa ni idadi ya mistari mine kwa kila ubeti na kuimbika kwa shairi. Mfano wa shairi la kimapokeo ni; "Kuntu Sauti ya Kiza" [uk. 33
"Nyuki ni mtanashati, umbo na zake tabia,
Yeye yukila wakati, Vichafu kuvikimbia,
Mchana na lailati, Hatui kwa kukosea,
Kuntu Sauti ya Kiza, nyuki hapendi vichafu."

Shairi hilo ni la kimapokeo kwakuwa kila ubeti katika shairi hilo lina mistari mine na kila mstari umeundwa na vipande viwili vya mstari, vilevile shairi hilo lina urari wa vina na mizani kwa kila mstari una silabi kumi na sita [16] na kuna vina vya kati na vina vya mwisho, katika ubeti wa kwanza vina vya kati ni ‘ti’ na vina vya mwisho ni "a"



Mashairi mengine ya kimapokeo ni kama vile, "Mcheza Hawi Kiwete" [uk. 37-38], "Ua Si Ruwaza Njema" [uk. 47-48]
Mtindo wa kisasa
Ni mashairi yasiyofuata urari wa vina na mizani, wala halizingatii idadi ya mistari katika beti na wala si lazima kuimbika. Mfano wa shairi la kisasa ni kama vile, shairi la "Naona" [uk. 41-42]
Naona
Wanakwenda gulioni
Mazao kuyazabuni
Wanapata bei duni
Na kubaki maskini
Unyonge uleule



Ukiliangalia shairi hili utaona kuwa halina urari wa vina na mizani, na mistari yake ni vipande hivyo shairi hilo ni la kisasa kwakuwa halijazingatia kanuni za wanamapokeo. Mashairi mengine ya kisasa ni kama vile, "Fungate" [uk. 1], "Unganeni" [uk. 1-2], "Maendeleo ya Umma" [uk. 2-4], "Tumesalitiwa!" [uk. 5], "Haki [uk.5] n.k
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi ametumia lugha sanifu ya Kiswahili yenye lahaja ya kiunguja iliyojaa lugha ya picha, taswira, misemo mbalimbali na tamathali za semi ni mbinu nyingine za kisanaa.
Lugha ya picha/taswira

Lugha ya picha iliyotumika ni pamoja na kunguru katika shairi la "Kunguru" [uk. 26-27], tunaposoma shairi hili tunapata picha kuwa, kunguru ni sawa na viongozi ambao tuliwachagua kuondoa matatizo katika jamii kinyume chake wao ndo wakazidi kuleta matatizo badala ya kuyaondoa kama walivyofanya kunguru weusi waliopandikizwa kuondoa uchafu badala yake wao ndo wamekuwa wakileta na kujaza uchafu na kuwa kero kwa jamii, mfano katika shairi hilo mwandishi anasema,
Kunguru walisafilishwa,
Nchini wakahaulishwa,
Na kazi ikatayarishwa,
Ili uchafu kuondoshwa.

Kunguru wakabadilika,
Uchafu wao wakaweka,
Maradhi yakaongezeka,
Ni badala ya kutoweka.



Lugha ya picha au Taswira nyingine iliyotumika ni jina la kitabu lenyewe, "Fungate ya Uhuru" taswira inayojengeka hapa ni kuwa, uhuru ni kama harusi na kama tunavyofahamu katika jamii yetu baada ya shamlashamla za harusi wanaenda fungate kwa mapumziko huku wakiendelea kula na kunywa bila kujali mzigo na uzito wa wale waliofanikisha shrehe yao kwa hali na mali, hivyo mwandishi anawafananisha hao maharusi sawa na viongozi ambao mara baada ya hekaheka za uhuru viongozi mpaka sasa wako katika mapumziko yanayotokana na heka heka za uhuru huo huku wakiendekeza anasa na starehe bila kujali wavuja shajo waliofanikisha uhuru huo. Mwandishi anathibitisha hilo anaposema, katika shairi la "Fungate ya Uhuru" ubeti wa kwanza anaposema,
"Karamu za fahari, mabembe ya kupepea.
Na majumba mazuri, wamekwisha jijengea.
Watembea kawa magari, hivi zimewazowea." Uk.1

Taswira nyingine zinazojitokeza katika diwani hii, ni ‘paka shume’ katika shairi la "Paka Shume" [uk.45] ambayo inajenga taswira ya viongozi au watu wadokozi.
Misemo
Misemo inayojitokeza katika diwani hii ni pamoja na:
Paka shume ukurasa wa 45 katika shairi la "Paka Shume" .
Utakiona cha Mtema kuni, Katika shairi la "Nyayo" uk. 31
Umelichimba kaburi, mzima utajizika, katika shairi la "Sakubimbi" uk. 44
Joka la mdimuni, ukurasa wa 40 katika shairi la "Joka la Mdimuni" uk. 40-41
Patashika na nguo kuchanika Katika shairi la "Joka la Mdimuni" [uk. 40-41]
Vishindo vya kufa na kupona katika shairi la "Kinyang’anyiro" [uk.43-44]
Hatwendi mrama katika shairi la "Nahodha Mtwesi" uk. 6-7
Ni wachapa kazi, kazi ni kilimo katika shairi la "Naona" uk. 41-42
Matumizi ya tamathali za semi
Tashibiha
Ama havikamatiki ni kama jinga la moto kama katika shairi la "Maendeleo ya Umma" [uk. 2-4]
Nabaki kugunaguna, kama nyani kwenye nyika katika shairi la "Ningekuwa na Sauti" [uk.10-11]
Niwachinje kama mbuzi, miiko wasoamini katika shairi la "Nikizipata Bunduki" [uk. 11-13]
Ulinijia mapema kama ukinda yatima katika shairi la "Si Wewe" [uk. 38-39]
Ni pomoni, mbu ndani, kama ndege za vitani, katika shairi la "Mkata" uk. 19-20
Matopeni, hujazika, mithili nimo karoni, katika shairi la "Mkata" uk. 19-20
Sitiari
Bao la mkahawani , kila mtu akalia, hapa mwandishi anamfanisha mwanamke malaya sawa na bao la mkahawani/mgahawani ambalo kila mtu hukalia, rejea shairi la "U wapi Uzuri Wako" [uk. 46-47]
Sasa jamvi la wageni, wajapo huwapokea, hapa mwandishi pia humfananisha mwanamke na jamvi/mkeka wa wageni kwa kila mgeni anayetokea yeye lazima atembee nao.
Mgodi wa Kiswahili, ni dafina isokwisha, mwandishi hapa anaifanani lugha ya kiswahili na mgodi wa madini, au kitu chenye thamani kubwa sana. Rejea shairi la "Dafina" [uk. 8-10]
Mashikoni, kibandani, vifaru vya panya ndani, mwandishi anafananisha panya na silaha ya kivita aina ya kifaru katika shairi la "Mkata" uk 19-20
Tashihisi
Na mauti yanamwita, katika shairi la "Mjamzito" uk. 7
Nyuki ni mtanashati, Umbo na zake tabia, katika shairi la "Kuntu Sauti ya Kiza" uk. 33
Ruya, umenigutusha, ukaniamsha, usingizini, katika shairi la "Ruya" uk. 13-14
Mbinu nyingine zilizotumika ni kama vile;
Takriri
Mbinu hii inajitokeza katika shairi la "Dafina" uk. 8-9 ambapo tunaona mwanzoni mwa kila mstari katika ubeti kuna maneno yanarudiwa rudiwa. Tazama ubeti ufuatao katika shairi hilo;
                                        "Paa, ni kuruka angani, kama ndege na tiara.
Paa, ni mnyama porini,ni mwenye nyingi papara.
Paa,ni kuteka mekoni, moto uwake imara.
Paa, ni toa magambani, samaki atiye sura.
Paa, pia la nyumba, kmakuti au karara.
Mgodo wa Kiswahili, ni dafina isokwisha."



Ukiangalia ubeti huo, utagundua kuwa kuwa neno ‘paa’ linajirudia rudia katika kila mstari wa ubeti, na mbinu hii imetuka katika shairi zima, shairi lingine lililotumia mbinu hii ni shairi la "Gorila" uk. 14-16 neno "gorila" linajirudia mstari wa mwanzo na mwisho kwa kila beti. Mashairi mengine ni, "Waja wa Mungu" uk. 27, sentensi, Abadani, hawa si waja wa Mungu! Inajirudia mwishoni mwa kila beti, rejea pia mashairi ya "Kunguru" uk. 26-27, "Utawala" uk. 28-29, "Wizi" uk. 25, "Maendeleo ya Umma" uk. 2-4 n.k
Lugha ya kejeli/dhihaka
Jina la kitabu "Fungate ya Uhuru" limetumika kidhihaka, mwandishi anawakejeli/dhihaki viongozi ambao wamewasahau wananchi na kujijali wao, kuishi maisha ya anasa na starehe huku wananchi wakitaabika kuwa wako katika fungate. Rejea pia shairi la "Fungate" uk. 1
Tafsida
Hawezi kujifungua badala ya kutumia neno hawezi kuzaa ambalo ni neno kali sana, katika shairi la "Mjamzito" uk. 7
Jina la shairi "Mjamzito" uk. 7 limetumika kitafsida kaepuka kutumia neno mimba
Vipengele vingine vya maudhui
FALSAFA YA MWANDISHI
Mwandishi Mohamed Seif Khatibu, falsafa yake anaamini katika ujamaa, anaona kuwa itikadi ya ujamaa ndiyo inayofaa kufuatwa na nchi za kiafrika ili kuleta usawa, haki na maendeleo ya watu wake, anaamini kuwa ujamaa unaweza kuondoa unyonyaji, matabaka na mambo yanayofanana na hayo katika jamii.



MTAZAMO

Mwandishi ana mtazamo wa kiyakinifu kwani anaamini kuwa matatizo yanayotokea katika jamii yake yanasababishwa na jamii yake, na mifumo iliyowekwa na watu, matatizo yote aliyoyajadili katika diwani hii mwandishi anaamini yanasababishwa na jamii, na jamii hiyo hiyo ndiyo inayoweza kuyaondoa hayo matatizo.                                        
MSIMAMO

Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi, anaitaka jamii yake ifanye mapinduzi kuondokana na mifumo mibovu na matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii yake kama vile uongozi mbaya, tattizo rushwa, usaliti, matabaka, unyonyaji n.k na kuonesha njia mbalimbali ambazo jamii yake inaweza kuzitumia ili kuondokana na matatizo hayo, miongoni, mwandishi ni mtaka mabadiliko katika jamii.
JINA LA KITABU

Jina la kitabu Fungate ya Uhuru linasadifu yale yote yaliyomo katika diwani hii. Jina hili la fungate ya Uhuru limetumika kikejeli, kiuhalisia neno fungate, linamaana ya tafrija, burudani, mapumziko, kula na kunya na kujiliwaza au kujipumbaza baada ya heka heka za harusi na hasa maharusi wawili yaani bwana harusi na bibi harusi, lakini katika diwani hii mwandishi ana maana ya viongozi ambao mara baada ya uhuru ambao uhuru huo watu wengi walijitoa kwa hali na mali, jasho kwa damu kupambana na dhuluma, manyanyaso na ubaguzi uliokuwa unafanywa na wakoloni, viongozi waliopata dhamana ya kutuongoza wamejisahau na kuwaacha wananchi na kuamua kujilimbikizia mali, kuishi maisha ya anasa, kuwanyonya wakulima na wafanyakazi, kukumbati rushwa na ukabila na hivyo kuwa katabaka ka watu wacheche wanaofaidi matunda ya uhuru kama maharusi walio katika fungate.
Hivyo mwandishi katika diwani hii, anazungumzia kwa kiasi kikubwa namna ambavyo viongozi hao, wameusaliti umma na wao kuwa wateule wachache wanaoishi maisha mazuri na ya anasa. Hivyo jina la kitabu kwa kiasi kikubwa linasadifu yale yote yanayozungumzwa katika diwani hii. [Rejea dhamira mbalimbali.



TATHMINI YA MHAKIKI
Kufanikiwa kwa mwandishi

Kwa kiasi kikubwa mwandishi amafaulu katika vipengele vyote vya fani na maudhui, kwa mfano, kimaudhui, amefanikiwa kuonesha matatizo mbalimbali yanaikabili jamii yake na kuipa njia jamii yake namna inavyoweza kuondokana na matatizo hayo. [rejea dhamira mbalimbali]
Kifani amefanikiwa, ametumia muundo changamani jambo ambalo linaweza kumsaidia msomaji wa kazi yake kujifunza namna ya kuandika mashairi yenye miundo tofauti tofauti, pia ametumia mtindo changamani yaani hakufungamana katika mtindo mmoja tu, ametumia mitindo yote, yaani mashairi ya kimapokeo na kisasa ambayo nayo huweza kumfanya msomaji wake, kuweza kujifunza namna ya kuandika na kutunga mashairi kwa mitindo yote hiyo.
Mapungufu
Kma ilivyo kawaida huwa hakuna kazi isiyo na mapungufu, hivyo hivyo katika diwani hii kuna mapungufu mbalimbali yanajitokeza ingawa si kwa kiwango kikubwa sana, kwa mfano, baadhi ya njia ambazo mwandishi anazitoa jamii kuzitumia ili kuondokana na matatizo zinaweza kuhamasisha jamii kujichukulia sheria mikononi wakati vipo vyombo vya kisheria vinavyopaswa kufanya hivyo, mfano rejea shairi la, "Ningekuwa na Sauti" uk. 10-11, na shairi la "Nikipata Bunduki" uk. 11, pia kutumia maneno makali kama vile matakoni badala ya kutumia tafsida makalioni pia ni mapungufu mengine yanayojitokeza katika kazi hii.






Kazi ya kufanya:



Ujumbe gani unajitokeza katika diwani ya Fungate ya Uhuru?
MWISHO

NADHARIA ZA CHIMBUKO LA NGANO/MASIMULIZI

Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu, ambazo ni, Utangulizi, katika sehemu hii tutatoa fasili ya nadharia na fasili ya ngano kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali. Sehemu ya pili itakuwa ni kiini cha swali ambapo tutajikita kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya fasihi simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka (1994/1999) na Finnegan (1970). Na sehemu  ya mwisho ni hitimisho.

Tukianza na fasili ya Nadharia, Massamba (2009:63) anasema, nadharia ni taratibu kanuni na misingi ambayo imejengwa katika muundo wa kimawazo kwa madhumuni ya kutumiwa kama kielelezo cha kuelezea jambo. Sarantakos (1997: 9) amefasili nadharia kama jambo linalofanywa na kuthibitishwa kwa utaratibu maalum kwa njia ya utafiti kwa ajili ya kuelezea jambo fulani katika jamii. Martin E. Amini (2005:10) anasema nadharia ni jumla ya mambo yote ambayo mtafiti amekusudia kuelezea, kuchambua, kuelewa au hata kutabiri jambo fulani kwa utaratibu maalum.

Hivyo basi, nadharia huchukuliwa kama dira au muongozo wa kumuongoza mtafiti/mchambuzi ili kulielezea vema jambo fulani kwa mtazamo unaotarajiwa kuwa imara zaidi kuliko mtazamo mwingine. Hivyo tunaweza kujumuisha kuwa nadharia ya fasihi simulizi ni chombo kinachotoa mwongozo kuhusu mwelekeo wa jamii fulani.
Maana ya ngano
Senkoro (2011:53) anasema, ngano  ni utanzu wa kifasihi simulizi ambao ulipitishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. King’ei  (2005:65)  anasema  ngano  kuwa  ni  hadithi  fupi  na  zenye   masimulizi    yasiyo    ya  kishairi. Kwa upande wake,Wamitila, K.W. (2003:165) anasema  ngano ni hadithi  ya kale ambayo ni moja kati ya tanzu maarufu za fasili simulizi.  Ni moja kati ya vipera au vitanzu vya hadithi au simulizi. Ngano nyingi huwa na mwanzo wa hapo zamani za kale.

Kwa fasili yetu, tunaweza kusema kuwa, ngano ni utanzu wa hadithi fupi fupi ambazo huelezea/kusimulia matukio mbalimbali yanayoleta mafunzo katika jamii husika na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Baada ya kuangalia fasili mbalimbali za nadharia na ngano, sehemu inayofuata ni kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya fasihi simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka (1994/1999) na Finnegan (1970). Tukianza na Okpewho (1992) ameanisha aina sita za nadharia zinazoelezea asili ya fasihi simulizi/masimulizi ambazo ni, nadharia ya mabadiliko, nadharia ya msambao, nadharia ya uamilifu, nadharia ya urasimi, nadharia ya Saikochanganuzi na mwisho ni nadharia ya Umuundo. Kwa upande wake, Miruka (1994) ameanisha aina tano za nadharia ambazo ni, nadharia ya Mabadiliko, nadharia ya msambao, nadharia ya urasimi, nadharia ya uamilifu na nadharia ya umuundo, wakati  Finnegan (1970) ameanisha aina tatu za nadharia ambazo ni nadharia ya Mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya Umuundo.

Tukiangalia uanishaji wa nadharia hizo za wataalamu hapo juu, tunaona kuwa, wataalamu hao wanatofautiana katika idadi ya nadharia hizo, lakini kimsingi wataalamu wote wanakubaliana kuhusu nadharia fulani fulani, mathalani, wote wanakubaliana uwepo wa nadharia ya mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya umuundo. Lakini Okpewho na Miruka wanakubaliana juu ya uwepo wa nadharia ya mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya umuundo, nadharia ya urasimi na nadharia ya uamilifu. Okpewho anainisha aina nyingine ya nadharia ya Saikochanganuzi ambayo haijitokezi kwa hao wataalamu wengine. Hivyo katika uwasilishaji wetu, tutazigawa nadharia hizo katika aina sita kama ifuatavyo:

Nadharia ya wanamabadiliko, nadharia hii iliasisiwa na Charles Darwin ambaye alikuwa mwana bailojia karne ya 19, alifanya utafiti kuhusu mabadiliko ya viumbe ambao waliishi miaka mamilioni iliyopita. Katika utafiti wake aligundua kuwa viumbe walioendelea kuishi  imewezekana tu kwa sababu ya kumudu mapambano dhidi ya uhaba wa vyakula, hivyo Darwin aliita jambo hili kama “Uhai kwa wanaofaa”. Pia aligundua viumbe walioendelea kuishi kwa sababu ya maumbo yao na mazingira yaliyosababisha wao kuwepo.
Mawazo ya utafiti wa Darwin yalishadadiwa na wanazuoni mbalimbali waliokuwa wanachunguza utamaduni wa binadamu, katika utafiti wao walikusanya simulizi kutoka jamii mbalimbali za Afrika, Asia na Amerika ambapo baada ya kukusanya simulizi hizo waligundua zilikuwa na ufanano wa kimaudhui. Wanamabadiliko wanaamini kuwa ngano/masimulizi tuliyonayo leo yana asili moja isipokuwa zimekuwa zikibadilika kutokana na mabadiliko ya wakati. Zaidi ya haya wanamabadiliko wanaamini kuwa viumbe wote tumetokea kwenye asili moja hivyo tuna uwezo wa akili sawa na maendeleo tutakuwa sawa.
Ubora wa nadharia hii, nadharia hii ndiyo msingi wa nadharia nyingine zilizofuata kama nadharia ya msambao, urasimi na uamilifu. Vilevile imesaidia kuelezea asili ya ngano/masimulizi hasa ngano zinazofanana kimaudhui, na mwisho nadharia imesaidia kuonesha kuwa ngano zina asili moja isipokuwa zinabadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na mazingira.

Mapungufu ya nadharia hii, wanamabadiliko waliamini kila kilichokusanywa katika fasihi simulizi kilihesabika kama masalia ya zamani/mabaki ya fasihi zilizotangulia, kwa maana kwamba kila kitu kilichosalia kitakuwa na dosari hakiwezi kuwa kitu halisi. Wanamabadiliko pia wameangalia tu upande wa maudhui na kuacha kipengele cha fani kama vile muundo na mitindo ya fani husika. Mwisho, pamoja na ufanano wa huo wa kimaudhui kuwa ngano zina asili moja lakini kuna tofauti kubwa hasa katika utendaji wa fanani hivyo fanani hutofautiana.

Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadharia hii inahusiana na ngano za Kiswahili katika sanaa za jadi ambayo ni elimu inayohusu asili ya binadamu pamoja na umuhimu wake ambao ilihusishwa na usimulizi wa ngano ambayo ilitokana na jamii husika katika shughuli mbalimbali za jamii kama vile jando na unyago, miviga, vyanzo vya vyakula, sherehe, matambiko kwa kutaja kwa uchache.

Nadharia ya msambao, nadharia hii imeasisiwa na wataalamu kama Jacob na Wilhem Grimm, baadaye mawazo yao yaliendelezwa na Maxmuller na Mmarekani Stere Thomson. Pamoja na kwamba kulikuwa na tofauti ndogondogo lakini wataalamu wa nadharia hii wanamwelekeo mmoja ambao wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ni moja lakini kutokana na maingiliano ya kijamii ndiyo yaliyosababisha kusambaa kwa hii ngano hasa kutoka katika jamii zilizostaarabika (Ulaya) kuja katika jamii zisizostaarabika (Afrika).

Okpewho anasema, wanamsambao walijishughulisha na kuhusianisha ngano za jamii mbalimbali na kugundua kuwa ngano zina ufanano unaokaribiana sana. Uhusiano huu unahusishwa na kipindi cha kihistoria ambacho kulikuwa na mawasiliano baina ya jamii moja hadi nyingine. Katika utafiti wao wanamsambao wamegawanywa katika shule mbili, kwanza ni kundi la shule ya India, kundi hili lilianzishwa na Jacob na Wilhelm ambapo walikusanya hadithi mbalimbali huko ujerumani na kwingineko barani Ulaya na kugundua kuwa ngano hizo zilikuwa na uhusiano na kuhitimisha kuwa ngano za Ulaya kama zilivyo lugha za Ulaya zimeonekana na rangi ya nasaba bora iliyopata kuishi huko kati ya kaskazini na Asia, rangi ya nasaba bora si rangi ya ngozi bali ni familia ya lugha ambayo lugha zote za Ulaya zinahusishwa nayo. Hivyo aligundua kuwa ngano zilikuwa zinasambaa na makundi ya wahamiaji. Wao waliona chimbuko la ngano ni huko India na zikafika huko Magharibi kwa njia ya msambao.

Kundi la pili ni kundi la shule ya Kifini, shule hii ilianzishwa na Eliasi Lonnrot ambaye mwaka 1825 alianza kukusanya ngano za mashujaa katika nchi ya Finland, kupitia maudhui yanayohusiana na kuziweka katika kundi moja.

Ubora wa nadharia hii, wanamsambao waliipa hadhi fasihi simulizi kwa kuchunguza muktadha kwa undani, vilevile, nadharia hii ilionekana kuwa ni ya kisayansi zaidi, hivyo inaweza kuchunguzika tofauti na wanamabadiliko kwani akili ya mtu haiwezi kuchunguzika.

Upungufu wa wa nadharia hii, kufikiria kuwa ngano zimeenea toka kundi moja la watu hadi kundi jingine, inaonesha kuwa jamii ya Kiafrika haikuwa na ngano. Nadharia hii inaona kuwa Afrika haikuwa na ngano kwani ngano zilitoka katika jamii zilizostaarabika (Ulaya) jambo ambalo si kweli kwani hata kabla ya ujio wa wakoloni Waafrika walikuwa na ngano zao. Vilevile, licha ya kuipa fasihi simulizi upekee katika kipengele cha muktadha lakini hawakuchunguza kwa undani vipengele vya kisanaa vya fasihi simulizi, mfano hawakuangalia vipengele muhimu vya fasihi simulizi ya Kiafrika hususani sanaa ya jadi kama vile, miviga, jando na unyago, matambiko, n.k.

Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, ukiangalia kwa jicho la ndani nadharia hii inasaidia kutambua kuwa mfanano wa ngano katika jamii nyingi za kiafrika ulitokana na maingiliano ya shughuli za kijamii kama vile, biashara, kilimo,ufugaji, uwindaji na kazi mbalimbali za jamii.
Nadharia ya umuundo, nadharia hii iliasisiwa na Claude Levis Strauses, alidai kuwa utamaduni unajumuisha vitu mbalimbali vinavyofanana, alichunguza visasili na kusema kuwa visasili hivyo vinatumika katika kuelezea na kutatua matatizo katika jamii. Hadithi hizo zilikuwa zinaelezea falsafa ya jamii husika, alidai kuwa visasili hivyo vilisaidia jamii katika kuyaelewa na kutatua matatizo ambayo yalileta mtanziko katika maisha ya binadamu, matatizo hayo ni kama vile, uhai na kifo.

Strauses, alidai kuwa muhusika wa ngano anajengwa katika kupambana na tatiziko ambalo anashindwa kulipatia majibu. Dominique Zahen aliongeza kuwa ngano  zinahusu uhai na kifo na ziishie kwa kuona kuwa uhai na kifo vimetoka kwa mungu (mfano: ngano inayoelezea namna kifo kilivyoingia duniani) (rejea Miruka 1994:138)

Ngano zinatakiwa kutazamwa kama mfumo wenye kanuni zake ambazo kila msanii anatakiwa kuelewa pia aelewe mfumo unavyoweza kutumiwa katika mawasiliano na hata kimuundo. Mfano katika ngano lazima kuangalia matumizi ya lugha na kaida zinazotawala utunzi huo.

Ubora wa nadharia hii, nadharia hii inasisitiza kuwepo kwa kanuni/kaida maalumu za kiutambaji, kiutunzi na matumizi ya lugha. Hapa wanaona kuwa ngano zisichukuliwe kama kitu pekepeke bali ni utanzu unaoongozwa na kaida maalumu katika uumbaji, kiutambaji na matumizi ya lugha. Hivyo kutakuwa na sifa zinazofanana katika ngano zote. Vilevile, inasaidia kujua chimbuko la ngano katika jamii fulani.

Udhaifu wa nadharia hii, kwanza kwa kutumia nadharia hii hatuwezi kupata kanuni rasmi ya kiutambaji, kiutunzi na matumizi ya lugha toka jamii moja hadi nyingine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kila jamii ina namna yake ya kuwasilisha ngano zao, kuziumba ngano zao na matumizi ya tofauti ya lugha. Mfano; maumbo ya ngano yanatofautiana toka jamii moja hadi nyingine, mfano, muingiliano wa tanzu moja katika nyingine, utambaji pia hutofautiana, mfano watambaji na tabaka tawala na watambaji na tabaka duni. Hata wahusika wa ngano pia hutofautina mhusika anaweza kuwa mtu duni kwenda bora au mtu bora kuwa mtu duni. Nadharia hii pia inatalia mkazo muundo kuliko dhima ya ngano katika jamii.

Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadhairia inasaidia wanafasihi kutambua/kuelewa ngano kama utanzu wa fasihi una muundo wake rasmi katika uumbaji, kiutambaji na matumizi ya lugha kiulemwengu lakini muundo huo si wa kimajumui kwa maana huweza kutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine.
Nadharia ya urasimi, nadharia hii iliasisiwa na mwanazuoni wa Kinesi Vladimir Propp (1928,1968) katika chake cha “The Morphology of the folktale.” Nadharia hii ilizuka ili kupinga mawazo ya wanamsambao hususani katika ugawaji wa ngano bila kuchunguza kwa umakini sifa ya kila kundi. Propp anaamini kuwa ili kuchunguza asili ya ngano ni vema kuanza kuchunguza aina za ngano kwa kuangalia maumbo ya ngano. Hivyo mtazamo huu unaangalia asili ya ngano kwa kuchunguza maumbo ya ngano husika.

Ubora wa nadhairia hii, nadharia hii inasaidia kujua aina za ngano kutokana na dhima zake, mfano ngano za urafiki, miadi, ukatili, ugunduzi na mwisho wa urafiki, (Alan Dunde’s)

Udhaifu wa nadharia, nadharia hii inaonekana kutomzingatia mtambaji ambaye ni sehemu ya ngano yenyewe ambaye anaweza kubadilisha umbo la ngano kadri ya utendaji wake.
Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadharia hii inatusaidia kuziweka ngano katika makundi kutokana na kazi zake. Mfano tunapata ngano zinazohusu wahusika wajanja mfano sungura na wahusika wasiowaelevu/wajinga mfano fisi.

Nadharia ya saiko-changanuzi, muasisi wa Nadharia hii ni Sigmund Freud raia wa Australia, mtaalamu huyu alikuwa tabibu wa magonjwa ya akili, alifanya uchunguzi wa nafsia, alichunguza hasa sehemu ya nafsi iliyofichika yaani sehemu ya ung’amuzi bwete ili kujua asili ya tatizo la mgonjwa husika, alieleza kuwa ung’amuzi bwete ni sehemu ya akili ya binadamu ambayo huhodhi fikra, mawazo, hofu na mitazamo hasi ambayo haiwezi kukubalika na jamii. Hofu na mawazo hayo hujitokeza kwa ndoto. Pia ung’amuzi bwete huhusisha matukio yaliyotendeka zamani lakini mgonjwa huyaingiza katika maongezi yake kama yanatendeka muda huo. Kutokana na utafiti wake aligundua kwamba ndoto zote husheheni ukweli kuhusu maisha ya mgonjwa.
Freud anaifananisha kazi ya fasihi na ndoto kwa kuwa visasili huwa ni hadithi za kubuni basi ubunifu huo unashabihi ndoto kwani wahusika wake na maudhui  yake kwa ujumla huwa katika ulimwengu wa kufikirika ambao ni kama ndoto katika ulimwengu halisi sawa sawa na mgonjwa wa akili anayeumba ulimwengu wake.

Freud alisisitiza mambo yote katika akili ya binadamu yanatawaliwa na ngono (libido). Mawazo yake yaliungwa mkono na mwanafunzi wake Carl Gustav Jung ambaye pia alifanya kazi pamoja na Freud katika kuwatibu wagonjwa wa akili kwa kutafsiri ndoto ingawa Gustav alitofautiana na Freud kwa msimamo wake kuwa akili ya binadamu inatawaliwa na ngono.

Carl Gustav Jung alifanya utafiti na kuunda dhana ya kikale ambayo ni mtiririko au picha kongwe inayojitokeza mara kwa mara katika tajriba anayopitia mwanadamu , alisema kuna sehemu ndani ya akili isiyokuwa na fahamu ya mtu mwenyewe lakini ina athira kubwa juu ya mawazo na matendo yake. Alitofautisha sehemu hiyo kama, sehemu ya kwanza ni sehemu binafsi inayofunza maarifa yaliyokusanywa na kila mtu katika maisha yake na sehemu ya pili ni sehemu ya kijamii inayofunza maarifa ya kibinadamu yaliyokusanywa na watu katika historia yao na kuendelezwa kwa karne nyingi. Anasema sehemu hii husika na matambiko muhimu ambayo mtu anapitia kama sherehe za kumpa mtu jina, sherehe za kuingia jandoni na unyagoni, sherehe zinazoigizwa wakati wa ndoa na hatimaye sherehe zinazohusu maziko ambazo sherehe zote hii ndizo huibua ngano.

Gustav alifafanua kwa undani masuala ya ngano katika tamaduni mbalimbali za dunia. Hivyo Freud na Gustav wanasema masimulizi ni kama ndoto au mvurugiko wa akili kwani picha, taswira na maudhui vyote ni vya kubuni havitoki katika ulimwengu halisi.

Ubora wa Nadharia hii, Nadharia hii inaonesha utofauti wa msimulizi mmoja hadi mwingine hutokana na historia ya mtu binafsi na uwezo wake binafsi hata kama kisa kitakachosimuliwa ni kimoja, hii imedhihirishwa kwa wagonjwa waliokuwa wanasimulia mambo yao kwa utofauti kutokana na historia zao. Lakini pia imesaidia kutuonesha chimbuko la ngano kwa miktadha tofauti tofauti kama sherehe za jando na unyago, sherehe za kutoa jina, n.k.

Upungufu wa Nadharia hii, Nadharia hii imesisitiza zaidi masuala ya hisia za kingono katika ubunifu wa masimulizi kitu ambacho hakina ushahidi wa kutosha kwani siyo kila hadithi inatarajia kujiridhisha kutoka hali ya ngono iliyofifizwa katika ung’amuzi bwete kama anavyosema Freud.

Nadharia ya kiuamilifu, Nadharia hii iliasisiwa karne ya 20 na Poland Bronislav Malinowsk. Uamilifu uliibuka kama njia yal kuyatazama maisha na utamaduni wa jamii, kwa kuchunguza dhima za vipengele vya kijamii pamoja na njia ambazo kwazo dhima hizi zinahakikisha uwepo wa jamii. Malinowsk alifanya utafiti Australia na kugundua kuwa ngano ni kumbukumbu za kweli za mila na desturi za jamii zilizopita, unyago, jando, mazishi, harusi, tohara, matambiko, kusalia miungu, n.k.
Ubora wa Nadharia hii, Nadharia hii imesaidia kuondoa mawazo kuwa chimbuko la fasihi mbalimbali zikiwemo ngano ni mahali fulani bali ni kila jamii imekuwa na simulizi ambazo zinasawiri tajriba (uzoefu) wao wa kila siku katika Nyanja mbalimbali kama vile, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii. Vilevile Nadharia hii, inatusaidia kujielewa na kuzielewa jamii zetu vizuri, kwa kuyaelewa mazingira ya mila na desturi zetu katika jimii.

Nafasi ya Nadharia hii katika ngano za Kiswahili, inatusaidia kujua tamaduni zetu katika somo la ngano, pia inatusaidia kujua kuwa kila jamii ilikuwa na tamaduni zao zenye kuwaongoza katika maisha yao ya kila siku kama vile, jando na unyago, harusi, matambiko, mazishi, miviga, kusalia miungu kuwa ndiyo chimbuko la ngano.


Hitimisho, kila nadharia tuliyoiangalia ina umuhimu wake katika kujifunza chimbuko la ngano, hivyo ni muhimu kila mwanataaluma wa ngano kuzisoma na kuzielewa nadharia zote zinazozungumzia chimbuko la ngano kwa sababu kila nadharia ina misingi yake ambayo kwa namna moja ama nyingine inatusaidia kujua na kuelewa chimbuko la ngano, Nadharia hizi ni muhimu pia kujifunza kwa sababu kuanzishwa kwa nadharia inategemea na upungufu unaojitokeza katika nadharia nyingine. Kwa ujumla licha ya mtenguo wa nadharia moja dhidi ya nyingine tunaona kuwa Nadharia hizi zinakamilisha, Nadharia moja inakamilisha Nadharia nyingine. Kwa maana hiyo, hatuwezi kujua au kuthibitisha chimbuka la ngano kwa kutumia nadharia moja.

MAREJEO
Finnegan, R. (1976) Oral Literature in Africa. Oxford University Press. Nairobi.
Kingei, K na Kisovi, C (2005), Msingi wa  Fasihi simulizi.  Nairobi: Kenya Literature  
                                                  Bureau.                
Martin E.Amin (2005),Social Science Researc Conception,Methodology and
                                    Analysis.Makerere University
Massamba (2009:63) Kamusi ya isimu na lugha, Falsafa ya Lugha. Dar es salaam.TUKI.
Mhando,J. na Balisidya, N. (1976) Fasihi , Tanzania Publishing House, Dar es salaam.
Miruka, O.S. (1994) Encounter with Oral Literature, East African Educational  
                                 Publisher.Nairobi. Kenya.
Muhando, P & Balisidya, N (1976) Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Tanzania Publishing     
                                                         House(TPH) Dar es Salaam.

Mulokozi, M.M. (1989:5) “Tanzu za Fasihi Simulizi” Katika MULIKA Na. 21, D.SM. TUKI
Nkwera, F.V. (xx) Tamrini za Fasihi Simulizi: Sekondari na Vyuo, Dar es Salaam: Business                               Printers Limited
Okpewho, I. (1992) African Oral Literature. Backgrounds, Character, and Continuity.
                                  Indiana  University Press: USA.
Sarantakos. S.(1997), Social Research. (2nd Edition) Palgrave Publisher Ltd (Formerly
                                   Macmillan Press Ltd)
Senkoro, F.E.M.K  (2011Fasihi. KAUTITU Limited. Dar es salaam.
Wamitila. K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi Istilahi na Nadharia. Focus Books.Nairobi.



Kwa kutumia nadharia za Turton (1975) na Barker (1848) kuthibitisha kuwa, hadi kufikia miaka 800 BK hadi 900 BK mijongeo ya wabantu ilikwashafika maeneo ya mito ya juba na tana


Na. Furaha Venance
M.A.KISWAHILI (UDSM)
2015
Ikisiri
Mijongeo ya Wabantu na kutamakani katika upwa wa Afrika Mashariki ni suala ambalo limewashughulisha wataalamu mbalimbali. Ama kwa hakika wataalamu walio wengi wanaelekea kukubaliana kuwa mpaka kufikia miaka 800 BK na 900 BK mijongeo ya Wabantu ilikuwa tayari imekwishafika maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Hivyo basi, katika makala haya tunakusudia kutumia nadharia ya Barker (1848) na nadharia ya Turton (1975) kuafiki kuwa, mpaka kufikia miaka 800BK na 900BK wabantu walishafika na kutamakani maeneo tajwa hapo juu. Ili kufikia lengo hilo, makala haya yamegwanyika katika sehemu tatu sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo kwa kifupi tutaeleza maana ya Wabantu, sehemu ya pili ambapo ndiyo kiini cha makala haya itakuwa na sehemu mbili, sehemu ya kwanza tutaanza kutalii mawazo ya baadhi ya wataalamu yanayodai kuwa mpaka kufikia miaka hiyo Wabantu walishajongea na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana na sehemu ya pili ya sehemu hii ndipo tutatumia nadharia ya Barker na Turton kuthibitisha ama kuafiki kuwa mpaka kufikia miaka ya 800 na 900BK Wabantu walishafika na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Sehemu ya tatu ambao ndiyo sehemu ya mwisho itakuwa ni hitimisho la makala haya.

1.0            Utangulizi
Katika lugha nyingi za kibantu neno bantu1 lina maana ya watu Mapunda (1980: 26). Neno Bantu kwa mara ya kwanza lilianza kutumiwa na Dkt. Wilhelm Bleek (1827-1875) katika kitabu chake kilichochapishwa mwaka 1862 kilichopewa jina la Comparative Grammar of South African Languages Collins (1968), Massamba (2002). Bleek alitumia neno Bantu kurejea kundi la lugha alizozilinganisha sarufi za lugha husika hususani kwa kuangalia mfumo wa ngeli za majina na vitenzi na kugundua kuwa lugha hizo zinafanana Massamba (2002:36). Mapunda (keshatajwa, 26-27) anaeleza kuwa, wanahistoria wanaelekea kukubaliana kuwa Wabantu ni jamii ya watu ambao huzungumza lugha zenye asili moja. Aidha, Nurse na Spear (1985:37) wanaeleza kuwa Wabantu ni watu walio na nasaba moja ya Proto-Bantu, waliosambaa labda katika milenia ya pili. Watu hawa wanasadikika kutokea katika kitovu kimoja asili yake ni huko Kameruni na Nigeria ya mashariki. Ama kuhusu madai lao kwamba chimbuko la Wabantu ni huko Kameruni na Nigeria bado wataalamu wanatofautiana kuhusiana na chimbuko la Wabantu.

Aidha, Johnson (1919) katika nadharia yake inayojulikana kama nadharia ya Johnson kuhusu chimbuko la Wabantu na mijongeo yao anaeleza kuwa, mtawanyiko wa Wabantu-Azali ulichukua mwelekeo wa mashariki kuelekea maeneo ya kaskazini ya Maziwa ya Albert na Nyanza ambayo yapo kusini magharibi ya Sudan na kaskazini ya Uganda. Kwa mujibu wa maelezo yake, Maziwa ya Albert na Nyanza kwa maana ya Uganda-Albert-Nile ndiyo kitovu cha chimbuko la Wabantu. Kwa upande wake Greenberg (1955) anatofautiana na Johnson anayedai kuwa, chimbuko la Wabantu ni Uganda-Albert-Nile, kwa maoni yake anadai [1]chimbuko la Wabantu ni mpakani mwa Kameruni na Nigeria na baada ya kutoka maeneo hayo wakaanza kushuka kuelekea kusini mwa Jangwa la Sahara Massamba (2002). Tukiyatazama madai haya tutaona kuwa ndiyo yanayoelekea kuungwa mkono na Nurse na Spear katika fasili yao kuhusu Wabantu na chimbuko lao kama tuliyoitazama hapo juu.

Nadharia nyingine inayozungumzia chimbuko na mtawanyiko wa Wabantu ni nadharia ya Malcom Guthrie (1970). Mtaalamu huyo anaonekana kupinga mawazo yote ya watangulizi wake wanaodai kuwa, chimbuko la wabantu ni Uganda-Albert-Nile (Johnson) na chimbuko la Wabantu kuwa ni mpakani mwa Kameruni na Nigeria (Greenberg). Guthrie anadai kuwa Wazungumzaji wa Kibantu wa mwanzo walikuwa eneo lenye pori kusini mwa msitu wa Ikweta kati ya makutano ya Bahari ya Hindi na Bahari ya Atlantiki. Kwa mujibu wa ramani ya sasa eneo hilo linalotajwa yanasemekana kuwa lipo nchini Zambia Massamba (2007:43-44). 

Kwa kuwa lengo letu si kuzijadili nadharia hizi katika makala haya, itoshe kusema kuwa kwa hakika hatuwezi kupinga ama kukubaliana na akina Nurse na Spear ama nadharia hizo kuhusu hasa chimbuko la Wabantu kwani suala bado linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina zaidi ingawa wanahistoria wengi wanakubaliana kuwa, chimbuko la Wabantu ni huko Afrika Magharibi  inakadiriwa miaka 2500 hadi miaka 3000 iliyopita, Wabantu walianza kusambaa maeneo mbalimbali kutokea Afrika Magharibi hususani mashariki ya Nigeria na    Kameruni.  Wabantu hao waliingia Afrika Mashariki wakitokea huko Katanga,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mapunda (keshatajwa: 27)

Kwa maana hiyo tunaweza sema kuwa, Wabantu ni jamii ya Waafrika wenye nasaba moja na huzungumza lugha zenye asili moja ambazo kwa kiasi kikubwa zinahusiana, wanapatikana kuanzia Afrika Magharibi, Afrika ya Kati hadi kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mtawanyiko wa Wabantu kwa kutumia nadharia inayodai kuwa, chimbuko lao ni Afrika Magharibi hususani maeneo ya Kameruni na Nigeria unaweza kuonekana vizuri katika ramani ifuatayo:


2.0             Kiini cha Makala
2.1  Madai kwamba hadi kufikia miaka 800 BK na 900 BK mijongeo ya Wabantu ilikwishafika maeneo ya mto Juba na Tana kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali.

Kama tulivyokwisha dokeza hapo awali. Katika sehemu tutayatalii mawazo ya baadhi ya wataalamu ambayo kwa hakika yaelekeana kukubaliana na hoja hii kuwa mpaka kufikia miaka hiyo mjongeo wa Wabantu ilikwishafika maeneo ya mto Juba na mto Tana.

Tukiitazama ramani ya sasa ya Afrika Mashariki mto Juba unapatika kusini ya Somalia unakaribia mpakani mwa Kenya upande wa kaskazini na Somalia upande wa kusini (Tazama kielelezo na. 2, uk. 7) wakati mto Tana unapatikana katika nchi ya Kenya. Ama kuhusu mjongeo wa Wabantu mpaka kufikia maeneo hayo yanazungumzwa kwa namna tofauti na wataalamu mbalimbali. Mathalani, Christopher Eheret anatueleza kuwa kufikia karne ya 7 yawezekana Wabantu walifika maeneo ya Mto Tana Massamba (2002:80 ). Kwa maelezo haya ya Eheret ina maana kuwa, mpaka kufikia miaka 600 BK ndiyo kipindi ambacho wabantu walikuwa wamefika mto tana. (karne ya 7 = miaka ya 600 BK).

Aidha, Nurse na Spaer (1985) wanaeleza kuwa hadi kufikia miaka ya 500BK Wabantu walikwisha fika pwani ya kaskazini katika eneo ambalo leo hii ni mpakani mwa pwani ya Kenya kaskazini na pwani ya Somalia kusini Massamba (2002:80). Tukiyachunguza madai haya ya Nurse na Spear bila shaka utaona kuwa, yanawiana na yale ya Eheret tuliyoangalia hapo awali, wakati Nurse na Spear wanataja kuwa kati ya mwaka 500 BK. Wabantu walikuwa wameshatamakani katika pwani ya Kenya kaskazini na pwani ya Somalia kusini ingawa hawataji hasa ni eneo gani, Eheret anatueleza kuwa ni karne ya 7 (miaka ya 600 BK) ndiyo Wabantu walikuwa wameshafika eneo la kaskazini mwa Kenya na anatutajia eneo hilo kuwa ni maeneo ya Mto Tana.

Kwa upande wake, Gonzales (2008) anaeleza kuwa, kwa kutumia ushahidi wa kiisimu kufikia karne 4 BK ( sawa na miaka ya 300 BK) Wabantu walishatamakani katika eneo la pwani ya Afrika Mashariki. Aidha, Jenkins2 anabainisha kuwa Wabantu wa Afrika Mashariki na Somalia inaelekea walihamia maeneo hayo wakitokea Afrika ya kati, anaendelea kueleza kuwa wanahistoria wanakubaliana kuwa Wabantu hao walitamakani eneo la kusini mwa Somalia pengine miaka ya 200 BK. Pamoja na kwamba wataalamu hawa wanatofautiana katika miaka wanayotaja Wabantu kutamakani eneo la upwa wa Afrika Mashariki kimsingi hawa wote wanathibitisha kuwa mpaka kufikia mwaka 800BK na 900BK mjongeo wa Wabantu ulikuwa umeshafika maeneo hayo ya Mto Juba na Mto Tana.

Hata hivyo, kuna madai mengine yanayodai kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili (ama waswahili) ambao kwa asili wataalamu mbalimbali kama vile  Wilhem Bleek (1862), Carl Meinhof (1899), C.M. Doke (1935), Malcom Guthrie (1967,1970,1971), Dereck Nurse na Thomas Spear, Shihabudin Chiraghdin na Mathias Mnyampala (1977), Massamba (2002) kwa kuwataja wachache wanakubaliana kuwa, Kiswahili ni moja wapo ya lugha za  Kibantu. Lugha hii inadaiwa kuwa chimbuko lake ni iliyowahi kuwa himaya ya Shungwaya., Mtetezi wa dai hili ni James Der ver Allen (1993) (Tazama Massamba 2007:51-55). Dai hili laelekea pia kuungwa mkono na Mirikau (2013:14) anaeleza kuwa, baadhi ya Waswahili wametoa maoni yao kwa kusisitiza kwamba Kiswahili kilianza kusemwa na Wabantu wa zamani walioishi Shungwaya. Kwa hakika ingawa dai hili linapingwa na wanazuoni wengine kama vile Greenville (1959) na Massamba kwamba Kiswahili kiliinukia eneo moja mahususi (Tazama Massamba 2002: 85), na bado mpaka sasa kuna utata ama kukubaliana au kutokukubaliana miongoni mwa wanazuoni kama himaya hiyo ilipata kuwepo ama la, Mirikau akijiegemeza katika ushahidi wa fasihi simulizi anaeleza kuwa, eneo la Shungwaya ilikuwa kati ya Mto Juba uliopo nchini Somalia na Mto Tana uliopo nchini Kenya.

Massamba (2002:53) akimnukuu Prins anasema kuwa, Shungwaya ilikuwa himaya kuu ikijumuisha Wasomali, Wakikuyu, Wameru, Watharaka, Wakamba, Wataita, Wapare, Wachaga, Washambaa, Wabondei, Wazaramo na Wagara ilichukua eneo lote la Somalia ya sasa, mashariki ya Kenya na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Tanzania na inakadiliwa kuwa himaya hii ilipata kuwepo hata kabla ya mwaka 800 BK.  Kutokana na maelezo haya na yale ya Mirikau kuwa eneo la Shungwaya lilikuwa kati ya Mto Juba na Mto Tana na madai kuwa, eneo hili lilipata kuwepo hata kabla ya miaka 800 BK kama anavyodai Prins ni wazi kuwa wanatuthibitishia kuwa mjongeo wa Wabantu mpaka kufikia mwaka 800 BK na 900 BK ulikuwa umeshajongea maeneo ya Mto Juba na Mto Tana.

Aidha, Shihabuddin Chiraghdin (1974:57) katika makala yake yenye kichwa cha habari Kiswahili Tokea Ubantu hadi Ki-“standard Swahili.” ingawa haelezi wazi ni mwaka gani, lakini anatuambia kuwa chimbuko la Waswahili (Wabantu) ni huko Ngozini kaskazini ya Kenya pande za visiwa vya Magunyani inayojumuisha Pate, Faza na Lamu na Tikuu na kushukia mpaka mipaka ya Mto Tana. Massamba (2002:84) anaafiki kuwa ,kati ya miaka 400 BK hadi 800 BK upwa wa Mashariki ya Afrika ulikwishakaliwa na Wabantu na Wakushiti yaani Wasomali na Wagalla. Kwa kuwa Chiraghdin anaeleza kuwa Waswahili (Wabantu) walianzia Ngozini na kuenea mpaka mipaka ya Mto Tana ni dhahiri kuwa kwa maelezo yake na tukiyaoainisha na ya Massamba kuwa, kati ya mwaka 400-800BK Wabantu walikwishatamakani upwa wa Afrika Mashariki bila shaka kama tutakubaliana na madai kuwa Wabantu walitokea kusini Somalia na kuteremka mpaka kaskazini ya Kenya, basi watakuwa pia katika kipindi hicho walikuwa wamejongea maeneo ya Juba na kufika huko Ngozini hadi Mto Tana.

Ama kwa hakika, tukiyatalii mawazo ya wanazuoni na wataalamu mbalimbali tuliowaangalia hapo juu tutaona kwamba ingawa wanatofautiana katika miaka na wengine kuonekana kutaja miaka ya kufikirika zaidi, ila kimsingi wote wanaelekea kukubaliana kuwa mpaka kufikia mwaka 800 BK hadi 900 BK Mijongeo ya Wabantu ilikwashafika maeneo ya Mto Juba na Tana. Hivyo basi, katika sehemu inayofuata kwa kutumia nadharia za Turton (1975) na Barker (1848) kuafiki madai haya.

2.2  Nadharia ya Barker (1848) na Nadharia ya Turton (1975)
Katika sehemu hii tutatumia nadharia hizi kutetea ama kuafiki madai kuwa mpaka kufikia mwaka 800 hadi 900BK mijongeo ya Wabantu ilikwishafika na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana kama ambavyo wataalamu wengine wanavyodai. Tukianza na:

2.2.1  Nadharia ya Barker (1848)
Nadharia hii inaeleza kuwa, kwenye karne ya 10 BK Wasomali ambao wapo katika kundi la Wakushiti wa Mashariki walianza kuteremka kusini wakitokea katika ncha ya Kaskazi ya pembe ya Afrika ambako ndipo inapodaiwa kuwa yalikuwa maskani yao.  Inadaiwa kuwa katika kujongea kwao huko kusini waliwakuta Wagalla ambao walikuwa wakiishi katika maeneo ya kaskazini na kati ya Somalia ya sasa na kuwafukuza. Nadharia inaendelea kueleza kuwa, Wagalla nao wakateremka kusini na wakawakuta Wabantu ambao walikuwa wametamakani katika eneo la Webi Shebelle. Wagalla wakaanza kupambana na kuwashinda Wabantu wa taifa la Shungwaya ambao wakawasukuma kusini ya Mto Juba hadi wakafika chini ya Mito Tana na Sabaki Massamba (2002:81)

Ama kwa hakika, tukiichunguza nadharia hii, tunaona kwamba kuna mambo ya msingi matatu yanayotufanya kuafikia kuwa mijongeo ya Wabantu mpaka kufikia mwaka 800 BK hadi 900 BK ilikwishafika na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Jambo la kwanza ni kuwa nadharia inataja kuwa,   kwenye karne ya 10 BK ndipo Wasomali walipoanza kujongea kusini na kupambana na Wagalla. Wagalla nao wakazidi kushuka kusini wakakutana na Wabantu ambao nao walisukumwa kusini ya Mto Juba hadi chini ya Mto Tana na Mto Sabaki. Kimsingi hapa karne ya 10 inayotajwa hapa ni sawa na miaka 900 BK. Kwa maana hiyo basi ni dhahiri kuwa kwa nadharia hii na kwa kutumia sababu hii tunaweza kuafiki kuwa mpaka mwaka 900 BK Wabantu walikuwa wameshafika maeneo ya Mto Juba na mto Tana kwa kusukumwa na Wagalla wakitokea eneo la Webi Shebelle. Ingawa pia dai kwamba Wabantu walifika huko kutokana na kusukumwa na Wagalla ama kwa kushughuli nyingine ni dai ambalo linatakiwa kutazamwa zaidi kwa jicho la kitafiti kwa maana kuwa ni dai ambalo linaweza kusailika kutokana na nadharia hii na ile ya Turton tutakayoenda kuitazama hivi punde kuwa na utata unaosababisha kujiuliza maswali ni nani hasa alipambana na Wabantu kati ya Wagalla au Wasomali? Maana nadharia itakayofuata inaeleza tofauti.

Aidha, jambo la pili tunalolipata katika nadharia hii yanayotusukuma kuafika dai hili ni hoja inayodai kuwa, Wabantu hao waliosukumwa na Wagalla maskani yao ilikuwa Webi Shebelle. Tukiangalia ramani ya sasa ya Afrika Mashariki, eneo la Webi Shebelle linapatikana kusini ya Somalia, yaelekea basi kama madai haya ni ya kweli, inawezekana Wabantu hao walikuwa wakiishi pembezoni ama katikati ya Mto Shebelle na Mto Juba. Mto Shebelle unatokea katika nyanda za juu ya Ethiopia unashuka mpaka maeneo ya pwani ya Somalia na kukutana na Mto Juba na kuingia bahari ya Hindi. Kama ni hivyo basi kuna uwezekano mkubwa kuwa Wabantu pengine walikuwa wameshajongea mpaka eneo la Mto Juba katika karne hiyo ya 10 BK (sawa na miaka ya 900 BK) pengine hata kabla ya kusukumwa na Wagalla.

Jambo la tatu nadharia hii inatueleza kuwa, Wabantu walioshambuliwa na kushindwa na Wagalla ni Wabantu wa Shungwaya pia yanatufanya tuafiki kuwa nadharia hii pia inakubaliana na dai kuwa Wabantu walijongea mpaka maeneo ya Mto Juba na Tana katika mwaka 800 BK hadi 900 BK kutokana na eneo la kijiografia linalotajwa kuwa himaya hiyo ilipata kuwepo. Aidha, Mirikau (keshatajwa) anaeleza eneo la  Shungwaya lilikuwa kati ya Mto Juba na Mto Tana.  Eneo hili linatajwa kuwa lilipata kuwepo hata kabla ya mwaka 800 BK kama anavyodai Prins (keshatajwa) ni wazi kuwa nadharia hii ya Barker inatufanya pia kuafiki kuwa mijongeo ya Wabantu mpaka kufikia mwaka 800 BK na 900 BK ilikuwa imeshajongea na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana kama wanavyodai wataalamu wengine.

2.2.2 Nadharia ya Turton
Tumeangalia nadharia ya Barker (1848), tumeona kuwa, nadharia inaleza kuwa Wasomali walipambana na Wagalla. Wagalla wakazidi kuteremka chini (kusini) wakakutana na Wabantu wakaanza kupambana nao, Wabantu wakaelemewa nao wakasukuMwa hadi kusini maeneo ya Mto Tana. Je, nadharia ya Turton (1975:19) inasemaje?

Turton (keshatajwa) katika makala yake aliyoipa jina la Bantu, Galla and Somali Migrations in the Horn of Africa: A Reassessment of the Juba/Tana Area inayopatika katika Jarida la African History anaeleza kuwa, Wasomali Wahawiya na Wa-kabla ya Wahawiya walitokeo maeneo ya karibu na Merka na kuanza kusambaa kuelekea magharibi na kusini na kulikalia karibu eneo lote la kati ya Mto Juba na Mto Tana mapema kabisa kabla hata Wagalla hawajawasili eneo la pwani. Anaendelea kufafanua kwamba, katika hatua hii ya Wasomali wale wa kundi la Wa-kabla ya Wahawiya kujitanua na kuzidi kusambaa kwa kuelekea kusini waliwakuta Wabantu na kuanza kupambana nao kwa ajili ya kugombea maeneo ya malisho. Wasomali (Wa-kabla ya Wahawiya) wakawasukuma Wabantu kurudi nyuma hadi Mto Tana.

Aidha, Turton anaendelea kutueleza kuwa, baadaye kabisa inakadiliwa pengine kwenye karne ya 16 BK (sawa na miaka ya 1500) Wagalla wenyewe walijongea kuelekea pwani wakifuata uelekeo wa Mto Tana ambako huko waliwakuta watu wa Mijikenda na kuwafukuza (Kumbuka Barker anatueleza kuwa Wagalla walishambuliwa na Wasomali). Watu hao wa Mijikenda kulazimika kuelekea kusini hadi kufikia Mto Sabaki kisha Wagalla wakapamba na kuwaondoa Wasomali katika eneo la Juba na Tana na kuwalazimisha zaidi Wasomali kurudi kaskazini. Aidha, tunaelezwa kuwa, katika karne ya 18 BK (sawa na miaka 1700 BK) Wasomali wakaanza tena kusonga chini na kufikia miaka 1860 Wagalla wakawa wamenyang’anywa eneo lote kati ya Mto Juba na Mto Tana walilolikalia zaidi ya miaka 100. Kwa mujibu wa Turton Wabantu hawakwenda sana kaskazini mwa pembe ya Afrika.

Kwa hakika tukiziangalia nadharia hizi mbili kuhusu mijongeo ya Wabantu katika upwa wa Afrika Mashariki ni wazi kuwa kuna mambo ambayo wataalamu wa nadharia hizi wanapingana. Mathalani, wakati Barker anatueleza kuwa, Wasomali waliwashambulia Wagalla na Wagalla wakawashumbulia Wabantu kwa upande wake Turton anapingana na Barker, yeye anatueleza kuwa Wasomali tena wale Wa-kabla ya Wahawiya ndiyo waliopambana na Wabantu na wala si Wagalla kama anavyodai Barker.

Tofauti nyingine inayojitokeza ni kuwa, wakati Barker anatueleza kuwa Wagalla waliwasukuma Wabantu kusini ya Mto Juba hadi wakafika chini ya mito ya Tana na Sabaki, Turton inaelekea hakubaliani na hili, kwa upande wake anadai kuwa katika mapambano kati ya Wasomali na Wabantu, Wabantu hawakwenda zaidi kaskazini mwa Pembe ya Afrika na kutokana na hoja hii Massamba (2002:82) anaona kuwa nadharia hii hailekei kueleza kwamba Wabantu walivuka Mto Juba kwenda kaskazini zaidi. Dai ambalo kwa hakika ni kweli, hakuna tunakoelezwa katika nadharia hii kuwa Wabantu walifika Mto Juba. Ingawa hatuelezwi hilo ila wote wanakubaliana kwamba mpaka miaka hiyo mjongeo ulishafika na kutamakani mto Tana. Lakini tukichunguza vizuri ramani ya Afrika Mashariki hususani Somalia na Kenya na kama tunakubaliana kuwa himaya Shungwaya kuu ilichukua eneo la Somalia, Kenya na Kaskazini ya Tanzania basi kuna uwezekani mkubwa Wabantu walishafika hadi Mto Juba.

Ama kwa hakika ingawa nadharia hizi zinapingana katika maeneo tuliyoyataja hapo juu, tukizichunguza kwa makini nadharia hizi zote zinaelekea kukubaliana kuwa mpaka kufikia mwaka 800 BK hadi 900 BK Wabantu walikwishajongea maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Hili linathibitishwa na maelezo ya wataalamu wote hawa wawili, ingawa Barker anataja Wabantu walikuwa wamesukumwa kusini ya Mto Juba hadi wakafika chini ya mito Tana na Sabaki, Turton yeye anatueleza kuwa Wasomali waliwalazimisha Wabantu kurudi hadi mto Tana. Kwa maelezo haya ya Turton ni kuwa Wabantu walirudi Mto Tana inaelekea Wabantu walishaanza kuweka maskani maeneo ya Mto Tana na walikuwa wanaelekea Kaskazini ambako ni Somalia kabla ya kukutana na Wasomali.  ingawa haelezi wazi kama walifika Mto Juba ila kimsingi wote wanakubaliana kati ya miaka hiyo Wabantu walikuwa washatamakani maeneo ya Mto Tana.

Si hivyo tu, nadharia hizi pia zaelekea kukubaliana kuwa, Wabantu ndiyo watu wa mwanzo kabisa kufika na kutamakani maeneo hayo kuliko Wasomali ama Wagalla na hii inatokana na ukweli kwamba, tunapoelezwa kuwa, Wagalla waliposhuka chini zaidi waliwakuta Wabantu katika taifa la Shungwa ambalo kama tulivyoelezwa na Mirikau (keshatajwa, uk.14) kuwa eneo la Shungwaya lilikuwa kati ya Mto Juba nchini Somalia na Mto Tana nchini Kenya, ingawa Prins (keshatajwa) anaongezea kuwa eneo la Shungwaya ilichukua eneo lote la Somalia, Kenya na baadhi ya sehemu za kaskazini ya Tanzania.

3       Hitimisho

Kwa hakika, pamoja na kwamba madai ya wataalamu wengi wanakubaliana kuwa hadi kufikia miaka 800BK hadi 900BK mijongeo ya Wabantu na kutamakani kwa Wabantu katika upya wa Afrika Mashariki hususani katika maeneo ya Mto Juba na Mto Tana ilikwishakuwa tayari kuna uwezekano mkubwa pengine Wabantu walishajongea maeneo hayo mapema zaidi kuliko miaka hiyo inayotajwa, tafiti za kiakolojia ingawa zingine hazitaji wazi ni watu wa jamii gani, zinathibitisha kuwa eneo la upwa wa Afrika Mashariki zilianza kukaliwa na watu kuanzia karne ya 3BK. Mathalani Chittick (1975:37) anasema katika maeneo ya unguja Ukuu huko Zanzibar na Manda katika mwambao wa Kenya kulipatikana vifinyange vya zamani sana kati ya vifaa hivyo vimekadiliwa kuwa vilikuwa vya kati ya karne ya tatu hadi karne ya 14 BK Massamba (2002:190). 

Aidha, Massamba anatudokeza utafiti mwingine wa kiakolojia majengo yaliyochimbuliwa Manda, inakadiliwa kuwa mji huo ulijengwa karne tatu na karne ya tisa, na mji wa Kilwa ulijengwa kati ya nne na karne kumi au karne ya tano na karne ya kumi na moja ama karne ya sita na karne ya kumi na mbili. Kutokana na ugunduzi wa kiakiolojia uliofanywa na Wanakiolojia mbalimbali, Massamba anahitimisha kwa kusema kuwa wenyeji wa asili walioanzisha makazi katika maeneo ya pwani walikuwa ni Wabantu.

Aidha, hata huu ushahidi wa kiakiolojia nao hauwezi kuwa ushahidi wa moja moja kuhitimisha kwa kusema kuwa Wabantu walianza kulikalia eneo la Afrika Mashariki kuanzia karne ya tatu kwa kutegemea kugunduliwa kwa majengo au vyombo/vifaa vya kale kwani vifaa ama amajengo hayo kwa hakika yalijengwa na wageni ambao walikuwa na teknolojia bora zaidi iliyowawezesha kujenga majengo yanayoweza kudumu muda mrefu tofauti na Wabantu ambao kutokana na teknolojia duni iliyokuwa ikitumika katika ujenzi wa nyumba za kibantu isingewezekana majengo hayo kudumu kwa miaka mingi kama yalivyobainika majengo ya wageni. Lakini tatizo lingine tunadokezwa na Massamba (2002:utangulizi) ni kuwa vyanzo vingi vya kihistoria na vya kiakiolojia vilivyopo vinaanzia karne ya kumi na kuendelea. Kutokana na hali hii tunashindwa kupata data zaidi za nyuma ya hapo na hii ni kwa sababu Wabantu hawakuwa na utamaduni wa kuandika au taaluma hiyo ilikuwa bado kuvumbuliwa. Ushahidi unaotumika wakati mwingine unatokana na masimulizi jambo ambalo linatufanya kupata ugumu hasa kujua, Wabantu walianza kuishi lini Pwani ya Afrika Mashariki. Hivyo suala la wabantu walianza lini hasa kujongea na kutamakani maeneo ya upwa wa Afrika Mashariki ni jambo ambalo bado linasawilika. Hivyo basi utafiti zaidi unahitajika kufanyika ili kupata taarifa sahihi kuhusiana na mijongeo ya Wabantu katika upwa wa Afrika Mashariki.

MAREJEO
Chiraghdin, S. (1974) “Kiswahili Tokea Ubantu hadi Ki-Standard Swahili.” Katika Mulika.
                  Na. 6 (1974) uk. 57-60.

Charaghdin, S. Na Mnyampala, M. (1977) Historia ya Kiswahili. Nairobi. University Press.

Collins, R.O. (1968) Problem in African History.
Gonzales,R.M (2008) Society, Religion and History: From Hunter land to Motherland, The Northeast-
                  Central Culture Zone. Columbia University Press. Iimepakuliwa kutoka
                   www.guternberg- e.org/gonzales tarehe 05/06/2015.

Jenkins, O.B (HM) Race and Ethnicity in The Horn of Africa. Imepakuliwa kutoka
                     www.orvillejenkins.com/people/race and ethnicity.html

Mapunda, H. (1980) Historia ya Mapambano ya Mtanzania. Dar es Salaam. TPH.

Massamba, D.P.B. (2002) Historia ya Kiswahili50 BK hadi 1500 BK. Nairobi.
                      The Jomo Kenyatta Foundation.

Massamba, D.P.B. (2007) Kiswahili Origins and The Bantu Divergence-Convergence Theory.
                      Dar es Salaam. TUKI.

Mrikau, S.a. (2013) Msururu wa PTE Kiswahili. Nairobi. East African Educational Publishers ltd.
Nurse, D. Na Spear, T. (1985) The Swahili: Reconstructing the History and Language of an African
                        Society, 800 – 1500. University of Pennsylavania Press.

Turton, E.R. (1975) “Bantu, Galla and Somali Migrations in The Horn of Africa: A Reassessment of               the Juba/Tana Area.” Katika Journal of African History. Vol.16. no. 4 (1975) uk.519-537.                   Cambridge University Press. Imepakuliwa kutoka     
            www.jstor.org/stable/1804495?seq=/#page_tab_contents tarahe 05/06/2015



                                                ACHA MAONI YAKO HAPA CHINI

No comments:

Post a Comment