Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Sunday, June 29, 2014

SAKATA LA UFISADI AKAUNTI YA ESCROW, ZITTO ALIPUKA, AANIKA KILA KITU, HUKU AKIWASHANGAA WAPINZANI


http://www.fullshangweblog.com/wp-content/uploads/2013/11/ZittoKabwe.jpgSakata la ukwapuaji wa pesa katika akaunti ya ESCROW, lachukua sura mpya, wakati serikali ikesema fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo hazikuwa za umma, wapo wanaodai kuwa fedha hizo zilikuwa za umma, mmoja wa wabunge ambaye wako mstari wa mbele kulishikia bango sakata hilo Zitto Kabwe ameamua kutoka hadharani na kulitolea ufafanuzi sakata hilo huku akiwalaumu wapinzani kukaa kimya kulipigia kelele suala hilo na kumuachia Kafulila, ingawa ushahidi unaonesha kuwa kambi ya upinzani ulilipigia kelele suala hilo hadi kuamua kutoka nje na hata kwa maneno yake mwenyewe Kafulila ndani ya Bunge alisema kuwa yeye na Mnyika walipeleka ushahidi wa sakata hilo kwa Spika.

Yafuatayo ni maelezo ya Zitto Kabwe kuhusu sakata hilo alivyoandika katika ukurasa wake wa facebook.


Kwa mara nyingine serikali kupitia viongozi na watendaji wake akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 zilizopaswa kuendelea kuwapo katika ‘Tegeta Escrow Account’ si mali ya serikali na hivyo si mali ya umma. Akaunti hiyo ilifunguliwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na kampuni ya Independent Power Limited (IPTL).

Kwa bahati mbaya sana viongozi wa serikali wamekuwa wakiendelea kurudia kuueneza huo uongo kwamba fedha hizo si mali ya umma. Inasikitisha pia kwamba vyombo vya habari vimekuwa navyo vikibeba na kusambaza huo uongo bila kuhoji na kuchunguza. Inashangaza sana pia asasi za kiraia nazo zimekaa kimya. Inatisha na kushangaa tena kuona wapinzani wakimwachia suala hili Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, pekee wakati mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda kuu ya wapinzani. Kafulila amekuwa akiendelea kuhoji suala hilo bungeni peke yake bila kupata kuungwa mkono na kupewa msaada wa aina yoyote kutoka kwa wenzake wa kambi ya upinzani bungeni.

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilielekeza kuwapo kwa ukaguzi maalumu kwenye akaunti hiyo ya Tegeta escrow account iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwa ndani yake kulikuwapo fedha za umma. PAC haina sababu yoyote ya kufuatilia fedha za watu binafsi. Mwaka 2009 iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilitoa maelekezo kwa BoT kutothubutu kutoa fedha hizo. Agizo hilo la POAC lilitokana na sababu kwamba fedha hizo zilikuwa ndani ya hesabu za Tanesco.

Akaunti ya ‘Tegeta escrow’ ilifunguliwa kutokana na kuwapo kutoelewana kuhusiana na gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa kwa TANESCO. Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika uamuzi wake wa Februari, 2014 ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL. Kwa uamuzi huo ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye akaunti hiyo maalumu ya escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.

Hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Disemba 2012 za Tanesco zinaonyesha wazi kwamba fedha hizo ni mali ya shirika hilo la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja. Fedha za kampuni ni suala la kisheria kama inavyobainishwa katika sheria ya kampuni ya mwaka 2002.
Kwa maelezo hayo na hoja hizo, inakuaje serikali ianze kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma? Hivi inawezekanaje kwa fedha za mtu binafsi zikaingizwa katika hesabu za shirika la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia 100? Ni lini fedha hizo zimekoma kuwa za umma? Je ni baada ya baadhi ya watendaji wa serikali kula njama za kuzichukua fedha hizo kwa kushirikiana na ‘mwekezaji’ aliyechafuka kwa ufisadi duniani?

Serikali inadanganya waziwazi kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma. Umma una haki ya kukumbushwa kwamba madai hayo yalitolewa pia katika lile sakata la ufisadi maarufu wa EPA unaofanana kwa kila hali na huu wa sasa wa ‘Tegeta Escrow’.

Hoja nyingine ni kwamba, Mbunge Kafulila alisema kwamba Jaji Utamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania hakutoa uamuzi wa kuchukuliwa fedha kutoka akaunti ya ‘Tegeta Escrow’. Nimepitia kwa makini hukumu ya Jaji Utamwa na kubaini kwamba hakuna popote alipotaja akaunti ya ‘Escrow’. Hata hivyo, nilipopitia muhstasari wa kikao kati ya TANESCO, IPTL na Wizara ya Nishati na Madini, ndipo kwa mara ya kwanza nikakuta wametafsiri uamuzi wa mahakama wakidai kwamba fedha zote za ‘Tegeta Escrow’ zipewe kampuni ya PAP (inamilikiwa kwa asilimia 50 na Harbinder Singh na 50% na Simba Trust iliyosajiliwa Australia). Hiki ndicho kikao kilichofanya maamuzi ya kuiba na kugawana wenyewe fedha hizo (Hukumu ya Jaji Utamwa na muhstasari wa kikao vinaambatanishwa).

Wote waliohudhuria kikao hicho kilichojipa mamlaka ya kutafsiri hukumu ya Mahakama Kuu, wanapaswa kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria zilizopo. Inawezekana vipi uamuzi wa mahakama ukatafsiriwa na kikao cha Wizara? Muhstasari wa kikao hicho ndio uliowasilishwa Benki Kuu (BoT) kuhalalisha madai kwamba fedha hizo lazima zitolewa kutoka akaunti ya Escrow.

Fedha zinazohusiana na akaunti ya Escrow ni Dola za Marekani milioni 250, katia ya hizo Dola milioni 122 zilizokuwa BoT zimeshatolewa na kiasi kilichosalia Dola milioni 128 zitalipwa na Tanesco kutokana na fedha zake kwa madai ya kushindwa kulipa kwa wakati. Fedha zilizolipwa ni zile ambazo zimetoka Wizara ya Nishati na Madini ambayo kisheria ndio walipaswa kulipia gharama za uzalishaji umeme (capacity charge) fedha zilizotoka kwa walipa kodi.

Ikumbukwe kwamba uhamishaji wa asilimia 70 ya hisa za IPTL kwenda PAP umeambatana na nyaraka za kughushi kutokana na kutokuwepo kabisa kwa uthibitisho wa cheti halisi cha hisa (share certificate) kutoka kampuni ya Mechmar kwenda kampuni ya Piperlink. Nyaraka za TRA zinaonyesha kwamba hisa hizo (70%) ziliuzwa kwa Shilingi za Kitanzania milioni sita (6) tu. Na bado hakuna ushahidi kuonyesha kwamba uhamishaji huo wa hisa ulipata baraka za mamlaka husika kama inavyotakiwa na sheria za nchi.

Wakati huyo anayejiita mmiliki mpya wa IPTL aliposaini mkataba wa kuchukua fedha kutoka akaunti ya Escrow zilizokuwapo BoT, hakuwa mmiliki halali kisheria kwani kodi ililipwa siku moja baada ya wao kupokea fedha kutoka BoT. Sheria inataka kutolewa kwa cheti na Kamishna wa TRA kama uthibitisho kwamba kodi yote imelipwa ipasavyo (Sheria ya Fedha ya 2012 kifungu cha 29).

Ni nani wamiliki wengine wa kampuni ya PAP? Uchunguzi ni muhimu ukawalenga vigogo na wanasiasa wakubwa wakiwamo watendaji waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini.

Inapaswa tutafakari kuona kwamba Harbinder Singh aliyechukua fedha za Escrow, anamiliki vitalu vya mafuta na gesi kupitia kampuni iitwayo HydroTanz ambayo nayo imesajiliwa nchini Australia, ikiwa na anwani sawa na ya kampuni ya Simba Trust. Kitalu hicho cha mafuta kinaitwa ‘Mnazi Bay North’, jirani kabisa na ugunduzi mkubwa wa hivi karibuni mkoani Mtwara.

Tunatarajia kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), atafichua ukweli wa sakata hili na TAKUKURU itawafikisha mahakamani wahusika bila kujali nyadhifa zao serikalini.

Kauli ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kwamba kuna watu waliokula rushwa na kwamba nyaraka zinazotajwa ni karatasi za kuuzia vitumbua, ni kauli zenye kuonyesha kutapatapa kwa watendaji serikalini. Hakuna hata mahali pamoja ambapo nimemtaja mtu kuwa ni mwizi zaidi ya kuwasilisha hoja zinazohitaji majibu mwafaka na si matusi, vitisho na tuhuma za kuzusha. Nyaraka za TRA haziwezi kuwa za kufungua maandazi kama ambavyo hukumu ya Jaji wa Mahakama Kuu haiwezi kuwa karatasi za kufungia maandazi na badala yake ni nyaraka halali zinazohitaji maelezo kutoka kwa viongozi na watendaji wa serikali badala ya kuropoka na kuporomosha matusi.

Hali kadhalika, Bunge lina kila sababu kupitia sheria yake ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kulinda hadhi yake kutoka kwa watendaji kama Maswi ambao wanatoa matamshi ya kuonyesha kwamba chombo hicho ni chombo cha watu wasiofaa na kwamba watu wanaofaa wanazungumza nje ya Bunge. Maswi na wengine kama wana ushahidi wa rushwa dhidi ya mbunge ama yeyote hawapaswi kupayuka ovyo bali kwa nafasi zao wanaweza kuwasiliana na vyombo vya dola kama TAKUKURU na polisi ili wachunguze na kuchukua hatua kama ambavyo vinawachunguza wao.

Kauli ya Maswi kwamba “wanaume” hawazungumzi ndani ya Bunge si tu udhalilishaji wa chombo hicho bali pia inaashiria ugonjwa wa mfumo dume uliotawala miongoni mwa viongozi wetu kwa maana kwamba wanaume ndio wenye hadhi, uwezo na heshima na wanawake ni dhaifu na wasiostahili heshima. Tufumbue macho tuone na tuondoe hisia binafsi zenye kubebwa na itikadi, chuki na misimamo yetu ya kisiasa. Tuwe   wazi

Wednesday, June 18, 2014

TAARIFA YA UCHAGUZI WA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO 2014

TAARIFA:
Uchaguzi wa wanafunzi wa kuingia Kidato cha Tano katika shule za Serikali na Vyuo vya Ufundi kwa mwaka 2014 umekamilika. Uchaguzi umefanyika kwa kuzingatia takwimu za matokeo ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne Tanzania Bara mwaka 2013.

2.0 WATAHINIWA WALIOFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE, MWAKA 2013

Jumla ya watahiniwa 427,679 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2013, wakiwemo wasichana 199,123 sawa na asilimia 46.56 na wavulana 228,556 sawa na asilimia 53.44. Kati yao watahiniwa 404,083 sawa na asilimia 94.48 walifanya mtihani na watahiniwa 23,596 sawa na asilimia 5.52 hawakufanya mtihani huo.

2.1 Watahiniwa wa Shule (School Candidates)

Kwa Watahiniwa wa Shule, watahiniwa 367,163 walisajiliwa kufanya mithanikati yao wavulana ni 198,099 na wasichana ni 169,064. ambapo watahiniwa 352,614 sawa na asilimia 96.04 walifanya mtihani; kati yao wasichana walikuwa 162,412 sawa na asilimia 96.07 na wavulana 190,202 sawa na asilimia 96.01 . Watahiniwa 14,549 sawa na asilimia 3.96 hawakufanya mtihani kwa sababu mbalimbali.

2.2 Watahiniwa wa Kujitegemea (Private Candidates)

Kati ya watahiniwa 60,516 wa kujitegemea waliosajiliwa kufanya mtihani, watahiniwa 51,469 sawa na asilimia 85.05 walifanya mtihani na watahiniwa 9,047 sawa na asilimia 14.95 hawakufanya mtihani kwa sababu mbalimbali.

Jumla ya watahiniwa 235,227 sawa na asilimia 58.21 ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2013 walifaulu. Mwaka 2012 watahiniwa waliofaulu walikuwa 185,940 kati ya 431,650 waliofanya mitihani; hii ni sawa na asilimia 43.08. Matokeo haya yanaonesha kuwa mwaka 2013 ufaulu umeongezeka kwa asilimia 15.13.

3.1 Ufaulu wa Watahiniwa wa Shule

Mwaka 2013 Watahiniwa wa Shule waliofaulu ni 201,152 sawa na asilimia 57.05 ya watahiniwa 352,614 waliofanya mtihani. Kwa mwaka 2013 kuna ongezeko la ufaulu wa watahiniwa 41,405, sawa na asilimia 25.91 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2012 ambapo watahiniwa 159,747 walifaulu.

3.2 Ufaulu wa Watahiniwa wa Kujitegemea

Takwimu zimeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa watahiniwa wa kujitegemea kutoka 26,193, sawa na asilimia 43.07 mwaka 2012 hadi kufikia watahiniwa 34,075, sawa na asilimia 66.21 kwa mwaka 2013; Kwa kulinganisha na mwaka 2012 lipo ongezeko la asilimia 30.09 kwa ufaulu wa watahiniwa wa kujitegemea.

Ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika madaraja ya I -III umefikia watahiniwa 71,527 sawa na asilimia 20.28 ya watahiniwa waliofanya mtihani Tanzania Bara. Hivyo kuna ongezeko la ufaulu wa asilimia 106.73 ikilinganishwa na matokeo ya ufaulu kwa mwaka 2012, kwa kuwa watahiniwa wa shule waliofaulu katika madaraja I-III kwa mwaka huo walikuwa 34,599 sawa na asilimia 9.67 ya watahiniwa waliofanya mtihani.

5.0 TARATIBU ZA UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO 2014.

Kulingana na utaratibu uliowekwa na Serikali, mwanafunzi anayeomba kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari kidato cha tano na vyuo vya Ufundi, hulazimika kujaza ‘Selform' ambayo ndiyo fomu rasmi ya maombi. Kwa kutumia fomu hiyo, mwanafunzi huchagua maombi matano ya tahasusi (Combinations) za masomo anayotaka kusoma na shule anayotarajia kujiunga nayo kwa kila chaguo. Kamati ya uchaguzi humpanga mwanafunzi katika machaguo yake ya masomo na shule kwa kuanzia na chaguo la kwanza. Kama mwanafunzi atakuwa hana sifa katika machaguo yote aliyoomba, mwanafunzi husika hupangiwa chaguo la somo alilofaulu zaidi na katika shule iliyopo karibu na wilaya yake ya makazi kulingana na tahasusi na nafasi zilizopo katika shule husika.

6.0 IDADI YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHA TANO

Jumla ya Wanafunzi 54,085 sawa na asilimia 75.61 ya wanafunzi 71,527 waliostahili kuingia Kidato cha Tano Tanzania Bara kwa mwaka 2014 wamechaguliwa; hilo ni ongezeko la wanafunzi 20,402 kwa kulinganisha na wanafunzi 33,683 waliochaguliwa mwaka 2013. Kati ya wanafunzi waliochaguliwa 2014 wavulana ni 31,352 na wasichana ni 22,733.

Wanafunzi wamechaguliwa kujiunga kidato cha Tano katika jumla ya shule 241 zikiwemo shule 33 zilizopangiwa wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka 2014.

Nawashukuru sana wadau wote wa elimu katika Halmashauri mbalimbali kwa kuimarisha miundombinu ya shule hizo, ikiwemo maabara.

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano 2014 ni kutoka shule za serikali na zisizo za serikali. Kati yao wavulana 14,826 sawa na asilimia 27.41 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na wavulana 16,526 sawa na asilimia 30.56 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi ya Jamii. Aidha,wasichana 7,859 sawa na asilimia 14.53 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na wasichana 14,874 sawa na asilimia 27.50 wamepangwa kusoma masomo ya Sayansi ya Jamii.

Nawapongeza walimu wote kwa juhudi walizozifanya katika ufundishaji kwa kuzingatia mbinu za ufundishaji walizopata kupitia mpango wa mafunzo kazini (INSET) kwa walimu wa sayansi na lugha (Kiswahili na Kiingereza) unaosimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Ofisi ya WaziriMkuu, Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa. Aidha nawapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi. Hali hiyo inaonesha kuwa jitihada za Serikali za kuhamasisha vijana kusoma masomo ya Sayansi zimeanza kuzaa matunda.

Natoa wito kwa wanafunzi wa jinsi zote kujisomea kwa bidii masomo yote, yakiwemo ya Sayans i na Sayansi ya Jamii , kwani yanategemeana. Walimu wa masomo ya Sayansi, Sayansi ya Jamii na Hisabati wanakumbushwa kutumia mbinu shirikishi za kitaalam na kisaikolojia katika kufundisha ili kuwavutia wanafunzi wengi zaidi kusoma na kufaulu mitihani yao. Aidha walimu wa masomo ya Sayansi, waendelee kuwahamasisha wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi wakiwemo wanafunzi wa kike . Aidha, wanafunzi wa kike wanapaswa kujiamini kuwa wanaweza masomo yote yakiwemo ya Sayansi, kwani siri ya kujifunza ni utayari.

7.0 WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA VYUO VYA UFUNDI, MWAKA 2014

Jumla ya wanafunzi 472 wakiwemo wavulana 355 na wasichana 117 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ufundi. Idadiya wanafunzi hao imepungua kutoka 530 mwaka 2013 hadi 472 mwaka 2014 kwa sababu kwa sasa vyuo hivyo vimeanza kuchukua wanachuo wa shahada ya kwanza. Aidha, kutokana na ufaulu kuongezeka idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na vyuo hivyo imeongezeka kutoka wanafunzi 114 mwaka 2013 hadi wanafunzi 117 mwaka 2014 sawa na ongezeko la asilimia 2.63.

Natoa wito kwa wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii masomo ya sayansi ili mwakani idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya ufundi iongezeke ili Taifa lipate wataalam wa kutosha wa ngazi zote.

8.0 SABABU ZA WANAFUNZI KUKOSA KUCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHA TANO Jumla ya wanafunzi 16,800 wakiwemo watahiniwa wa kujitegemea 10 waliokuwa na sifa za msingi hawakuchaguliwa kwa sababu mbalimbali zikiwemo: ufinyu wa nafasi za shule za Kidato cha Tano (wanafunzi 16,400 ) na kukosa tahasusi - Combination (wanafunzi 400 ).

Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili baada ya kubaini nafasi zitakazokuwa wazi zinazotokana na wanafunzi ambao hawakuripoti awamu ya kwanza. Aidha, Serikali imeweka utaratibu wa kuwapatia nafasi ya kusoma kidato cha Tano na cha Sita kwa pamoja na shahada ya Ualimu wanafunzi wenye sifa.

Shule za Kidato cha Tano na Sita zinatakiwa kuwa na mahitaji ya msingi, ikiwemo miundombinu yenye uwiano sahihi wa vyoo, bafu, vyumba vya madarasa, bweni, jiko, bwalo, maktaba, maabara, chumba cha Jiografia ; pamoja na samani kulingana na idadi ya wanafunzi.

Shule zenye Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne ambazo zinahitaji kuanzisha kidato cha Tano, zinatakiwa kuwa na miundombinu na mahitaji kamilifu yanayotosheleza kidato cha Kwanza hadi cha Nne kabla ya kuanza kujenga miundombinu ya Kidato cha Tano na Sita.

Natoa wito kwa Makatibu Tawala Mikoa wawaelekeze Wakurugenzi wa Halmashauri, Miji na Majiji kuhakikisha azma ya Serikali ya kila Tarafa kuwa na shule ya Kidato cha Tano inatekelezwa ili kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokosa nafasi. Kutokana na ongezeko la ufaulu wa masomo ya sayansi tunahimiza shule zitakazoanza Kidato cha Tano ziwe na maabara ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa tahasusi za sayansi.

Aidha, shule ambazo hazikupangiwa wanafunzi kutokana na mapungufu mbalimbali, Makatibu Tawala wa Mikoa husika wanahimizwa kuwaelekeza Wakurugenzi kusimamia kwa karibu ukamilishwaji wa shule hizo ili ziweze kupokea wanafunzi wa chaguo la pili (Second selection).

Natumia nafasi hii kuwahimiza wadau wote wa Elimu kuhakikisha kuwa shule zote zinazoanzishwa kwa ajili ya kidato cha Tano ziwe za bweni kwa kuwa wanafunzi wa kutwa ni wachache na ni lazima watoke eneo husika. Kwa mfano, mwaka huu shule ya sekondari Buswelu ya mjini Mwanza imekosa wanafunzi kwa kuwa ni ya kutwa na Mwanza kuna shule 3 za kutwa. Hivyo ilikuwa vigumu kupata wanafunzi wa eneo hilo wa kutosheleza shule hizo.

Wakuu wa Shule wahakikishe kuwa wanafunzi wa kidato cha nne wote wanajaza ‘Selforms' kwa umakini na kwa usahihi ili kurahisisha zoezi la uchaguzi. Aidha, wazazi kwa kushirikiana na walimu wawaelekeze watoto wao kuwa na dira , kuwasaidia kusoma kwa malengo na kufanya machaguo ya tahasusi kulingana na dira walizonazo.

10.0 WANAFUNZI KURIPOTI KATIKA SHULE WALIZOPANGWA

Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano mwaka huu 2014,utaanza mwezi Julai tarehe 10 . Wanafunzi wamepangwa katika shule zenye miundombinu na walimu kwa masomo husika. Aidha, iwapo baadae mapungufu yatajitokeza, wakuu wa shule wameelekezwa kutoa taarifa kwa uongozi wa Halmashauri husika kuhusu upungufu huo.

Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano umefanyika kwa kutumia mfumo wa kompyuta kwa kuzingatia machaguo ya wanafunzi pamoja na ufaulu hivyo hakutakuwa na mabadiliko yoyote. Kwa nafasi hii, naagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule walizopangwa tarehe 10 Julai, 2014 . Wanafunzi ambao watashindwa kuripoti shuleni hadi tarehe 30 Julai, 2014 nafasi zao zitajazwa na wanafunzi ambao wamekosa nafasi.

Mwisho ninachukua nafasi hii kuwapongeza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi mwaka 2014, walimu, wazazi, Bodi za Shule, viongozi, jamii na wadau wote wa elimu kwa jitihada za kuwaandaa wanafunzi, na kufanikiwa kuingia Kidato cha Tano. Ushirikiano wa wadau wote unatakiwa ili kuboresha elimu hapa nchini.

Wataalam wa elimu kuanzia ngazi ya shule wawe na utaratibu endelevu wa kuelimisha wadau katika utekelezaji wa malengo yanayopimika. Katika utaratibu wa ”Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now)”; kila mmoja anatakiwa kuacha utendaji wa mazoea na afanye kazi kwa malengo na viwango , kuwa na mipango inayotekelezeka ya muda mfupi na muda mrefu na kuwa na vipindi vya tathmini kwa kila lengo kabla, kati na mwisho wa utekelezaji. Ni matumaini yangu kuwa wakuu wa shule na viongozi wote wa elimu wakizingatia taratibu hizi, elimu inayotolewa hapa nchini itaendelea kuwa bora zaidi.


Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Mhe. Kassim M. Majaliwa (MB)

OFISI YA WAZIRI MKUU - TAMISEMI

MAJINA YA WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO 2014

Wanafunzi waliochaguliwa wanatakiwa kuripoti kwenye shule walizopangiwa kuanzia tarehe 10 Julai 2014 na mwisho wa kuripoti ni tarehe 30 Julai 2014. Aidha, hakutakuwa na mabadiliko ya wanafunzi kubadilishiwa shule walizopangiwa, hivyo wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangiwa kama inavyoonekana katika matokeo haya.


WASICHANA SHULE ZOT BOFYA HAPA
http://www.pmoralg.go.tz/menu-data/adverts/form-five-selection-2014/WASICHANA-SHULE-ZOTE.pdf

WAVULANA KUANZIA HERUFI A-L INGIA HAPA
http://www.pmoralg.go.tz/menu-data/adverts/form-five-selection-2014/WAVULANA-MAJINA-YA-SHULE-A-mpaka-L.pdf

WAVULANA KUANZIA HERUFI M-Z INGIA HAPA

http://www.pmoralg.go.tz/menu-data/adverts/form-five-selection-2014/WAVULANA-MAJINA-YA-SHULE-M-mpaka-Z.pdf

Monday, June 2, 2014

MWALIMU WA SHULE YA SEKONDARI CHIKUYU ATUHUMIWA KUMBAKA MWANAFUNZI WAKE WA KIDATO CHA TATU

ATOKOMEA HAJULIKANI ALIPO

Na: MOSHI LUSONZO- MANYONI
Katika hali ya kutisha, Mwalimu mmoja wa Shule ya sekondari anatuhumiwa kumkamata na kisha kumbaka hadharani mwanafunzi wake wa kike.

Tukio hilo  limetokea Mei 6, mwaka huu katika shule ya Sekondari ya kijiji cha Chikuyu, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, ambapo mwalimu anayehusishwa na tukio hilo ametajwa kwa jina la Chrisant Mpinda.

Taarifa zilizopatikana zinasema mwalimu huyo alimchukua mwanafunzi huyo (Jina linahifadhiwa) anayesoma kidato cha tatu wakati akisubiri kuchukua chakula kisha kumpeleka uwanja wa michezo na kumfanyia unyama huo.

Kutokana na tukio hilo, wazazi wenye watoto wao katika shule hiyo wamekuja juu huku wakihusisha uongozi wa shule hiyo kusaidia kumtorosha mwalimu huyo ili asikamatwe kufikishwa katika vymbo vya sheria.

UBAKAJI
Bibi wa mwanafunzi huyo, Lucy Lumalizo, alisema mjukuu wake baada ya kufanyiwa kitendo hicho ameachiwa majeraha na maumivu makali.

Alisema siku ya tukio, mjukuu wake huyo akiwa na wanafunzi wenzake walikuwa kwenye foleni ya chakula.

Wakati akiendelea kusubiri zamu yake ifike ya kupata chakula, mwalimu huyo alimuita na kumtaka aende ofisini kwake kuna jambo alitaka kumuelekeza.

"Mjukuu wangu alimpatia sahani rafiki yake ili amtunzie na yeye alikwenda moja kwa moja kwenye ofisi ya mwalimu huyo," alisema mama Lumalizo.

Alisema alipofika ofisini kwake, mwalimu huyo alimtaka waongozane ili akampatie simu yake ya mkononi ambayo alinyang'anywa siku tano kabla tukio hilo.

Alimuelekeza waende wote uwanja wa michezo kwa ajili ya kumpatia simu hiyo, lakini walipofika eneo hilo mwalimu huyo alimkamata kwa nguvu na kuanza kumbaka.

Hata hivyo, mwanafunzi huyo alianza kupiga kelele za kuomba msaada kitu ambacho kilipelekea wanafunzi wenzake kukimbilia eneo la tukio na kufanikiwa kushuhudia mwalimu huyo akifanya unyama huo.

Baada ya kuona wanafunzi wamemuona, alimuacha na kukimbilia kusikojulikana.

ALALA BILA MATIBABU
Baada ya tukio hilo, imedaiwa mwanafunzi huyo alilazimika kulala ndani ya bweni bila kupatiwa matibabu kutokana na walimu wa shule hiyo kukataa kutoa ushirikiano.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo (Jina linahifadhiwa) ameliambia NIPASHE kwamba pamoja na kutoa taarifa kwa Mkuu wa shule hiyo Emmanuel Mwarabu, hakuna msaada uliotolewa kwa mwanafunzi huyo kupelekwa hospitali.

"Tulitoa taarifa mapema tukiamini mwenzetu atasaidiwa, lakini hakuna chochote kilichofanyika tulilala naye huku akilalamika maumivu makali hadi asubuhi," alisema mwanafunzi hiyo.

Alisema hata ilipofika asubuhi walimu hawakuchukulia uzito jambo hilo hadi wazazi wake walipokuja na kuamua kumpeleka kituo cha Polisi cha Manyoni.

"Mpaka sasa tunaishi kwa hofu baada ya uongozi wa shule kututaka tutoe maelezo kwa nini tulitoa taarifa kuhusu tukio lile, inaelekea kuna harakati za kuficha ukweli," aliongeza mwanafunzi huyo.

Hata hivyo, mama Lumalizo alisema katika uchunguzi uliofanywa Hospitali ya Manyoni imeonyesha mwanafunzi huyo ameingiliwa kwa nguvu na kumsababishia michubuko sehemu yake ya siri.

Alisema pamoja na ukweli huo, bado kuna hali inayoonyesha kuna vitu vinavyofichwa ili kujaribu kuhakikisha suala hilo linamalizika kimya kimya.

Alihuzunishwa na kitendo cha mwalimu huyo kukimbia  wakati kuna taarifa kuwa siku ya pili baada ya tukio hilo alionekana akiwa na walimu wenzake  wakifanya mkutano.

MKUU WA SHULE AGOMA
Mkuu wa shule hiyo, Mwarabu alipopigiwa simu yake ya mkononi kuelezea tukio hilo, hakuwa tayari kusema chochote kwa maelezo hawezi kuongea na mtu asiyemfahamu kwenye simu.

"Kama ukitaka jambo lolote kuhusu shule yangu, unatakiwa ufike hapa nitakuwa tayari kusema kila kitu na siyo vinginevyo," alisema.

Kwa upande wa Afisa Mtendaji wa kijiji cha Chikuyu, Emmanuel Mdemu, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alikiri kutokea kwa tukio na kusema Polisi wanaendelea kufanya uchunguzi.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo alikutana na pande mbili ikiwamo wazazi na uongozi wa shule na kubainika kuna ukweli wa jambo hilo.

"Kinachofanyika sasa ni kusubiri ripoti ya polisi ikamilike, lakini kitu hicho ni kweli kimefanyika na mwalimu anayehusishwa amekimbia kijiji na hatujui wapi atapatikana,' alisema Mtendaji huyo.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI