Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Wednesday, May 30, 2012

UHAKIKI WA RIWAYA YA MFADHILI KIDATO CHA 5 & 6

                                          UHAKIKI WA RIWAYA
                                   JINA LA KITABU: ,MFADHILI.
                                    MWANDISHI:     HUSSEIN TUWA 
   
                                     MHAKIKI: MWL.  FURAHA VENANCE
Mwaka 2012

Utangulizi kuhusu Riwaya.

Mfadhili ni riwaya iliyoandikwa na Hussein Tuwa, ni riwaya inayoongelea juu ya penzi zito baina ya watu wawili, Gaddi Bullah na Dania Theobald na jinsi ambavyo penzi hilo linavyoingiliwa na mitihani,majaribu na misukosuko mikubwa na namna ambavyo kila mmoja anavyojaribu kukabiliana na hiyo misukosuko. Ni riwaya inayogusa moyo na isiyochosha kusomwa na wasomaji wa kila aina.



Mwandishi Hussein Tuwa pamoja na kuandika riwaya hii, pia ameandika riwaya nyingine inayoitwa, Mkimbizi.



Utangulizi kuhusu uhakiki wa riwaya hii.

Tunapofanya uhakiki wa kazi za fasihi huwa tunachambua vipengele mbalimbali  vya fasihi, vipengele hivyo ambavyo huchambuliwa ni fani na maudhui, katika fani huwa tunajishughulisha na Vipengele kama, wahusika, mandhari, mtindo, muundo, matumizi ya lugha, jina la kitabu na jalada, wakati katika maudhui huwa tunashughulika na vipengele kama vile dhamira, migogoro, ujumbe, falsafa ya mwandishi, mtazamo wa mwandishi.



Hivyo basi katika kazi hii, nimeanza uhakiki kwa kuanza na kipengele cha wahusika ambacho ni kipengele cha fani, nimeamua kuanza hivi ili kukupa fulsa msomaji na mtumiaji wa tahakiki hii, uweze kuwajua wahusika katika riwaya hii, na pindi tutakapoanza kuangalia dhamira basi utakuwa unajua ni nani anayehusika na dhamira hiyo. Hivyo basi tuanze kwa kuwaangalia wahusika maana ndio wanaobeba dhamira:



WAHUSIKA

Wahusika ni wakala wa vitendo katika kazi ya fasihi. Wahusika ni watu au viumbe waliokusudiwa na mwandishi wawakilishe tabia za watu katika kazi ya fasihi. Na wahusika katika kazi ya fasihi ni Muhusika/wahusika wakuu na wahusika wasaidizi.



Wahusika wakuu.

Hawa ni wahusika wanaojitokeza mara kwa mara katika kazi ya fasihi na mara nyingi ndio wanaobeba dhamira kuu ya mwandishi lakini pia husaidia kujenga dhamira ndogondogo. Riwaya hii ya Mfadhiri ina wahusika wakuu wawili, Gaddi Bullah na Dania.



1. Gaddi Majid Bullah

Ø      Ni mtu mcheshi na mchangamfu, kama mwandishi anavyothibitisha anaposema, “ Na hii ilitokana na jinsi Gaddi alivyobadilika mara baada ya kukutana na Dania na kurudia ucheshi na uchangamfu wake wa zamani” [Uk 97]

Ø      Ni msomi aliyeajiliwa katika kampuni ya mawasiliano, mwandishi anathibitisha hili anaposema, “….kampuni ile kubwa ya mawasiliano nchini ambayo ilimwajiri mara baada ya kumaliza masomo yake ya elimu ya juu miaka mitano iliyopita.” [Uk 57]

Ø      Anashushwa cheo kutoka Meneja wa mkoa katika tawi la Arusha hadi kuwa Afisa wa kawaida wa kukusanya madeni. Rejea Ukurasa wa 57.

Ø      Kaka pekee wa Bi Hanuna.

Ø      Mume wa Nyambuja ambaye wanakuja kuvunja ndoa yao kutoka na kusalitiwa, kama mwandishi anavyothibitisha anaposema, “Wiki moja baadaye Gaddi na Nyambuja waliachana kisheria….” [Uk 68]

Ø      Anasalitiwa na Mke wake kwa kuanzisha uhusiano na mwanaume mwingine, mwandishi anathibitisha hili kupitia muhusika Nyambuja anaposema katika barua aliyomwandikia Gaddi, “Gaddi nimependana na mtu mwingine, na nimekuwa nikisaliti ndoa yetu kwa muda mrefu.” [Uk. 65]

Ø      Hakufanikiwa kupata mtoto katika uhai wa ndoa yake na nyambuja, kama mwandishi anavyothibitisha hili anaposema, “Gaddi aliguna kwa mshangao, akilini mwake akikumbuka jinsi yeye alivyokuwa akisononeka kwa kutopata mtoto wakati wa ndoa yake...” [Uk. 83]

Ø      Anaanzisha uhusiono wa mapenzi na mwanamke mwingine aitwatae Dania

Anafaa kuigwa



2. Dania Theobald.

Ø      Ni binti wa miaka kama ishirini na nne.

Ø      Ni binti mrembo na wakuvutia.



Ø      Ni binti anayetoka katika familia ya kitajiri, kama mwandishi anavyothibitisha akimtumia muhusika Mama Mlole anaposema, “ Akiwa ni mtoto aliyetoka katika familia ya Kitajiri.” [Uk. 81]



Ø      Ni msichana asiyedanganyika kwa fedha. Mwandishi anathibitisha hili akimtumia muhusika Mama Mlole anaposema, “Sio hivyo tu, bali Dania alikuwa ni binti mwenye uwezo kifedha; kwa hiyo hakuwa msichana aliyeweza kudanganyika kwa fedha kama wengine.” [Uk. 82]



Ø      Ni mwanamke anayehitaji penzi la kweli, rejea mwandishi anaposema “…hakuwa msichana aliyeweza kudanganyika kwa fedha kama wengine. Kwake kilichohitajika ni penzi tu.” [Uk. 82]

Ø      Mpenzi wa Jerry ambaye baadaaye anakuja kusalitiwa na Jerry kwa kuanza uhusiano na mwanamke wa Kizungu huko Marekani, kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika Mama Mallo, “ Mwaka wa pili ulipoisha Jerry alileta barua kuwa alikuwa amepata mwanamke wa kizungu aliyepanga kufunga nae ndoa hukohuko Marekani.” [Uk. 87]



Ø      Alijaribu kujiua baada ya kusalitiwa na Jerry kama mwandishi anavyothibitisha akimtumia muhusika Mama Mallo anaposema, “ …Sasa hili lilkuwa ni pigo la mwisho na Dania alivurugikiwa kabisa….alijaribu kujiua…” [Uk.87]



Ø      Ni mama wa Junior aliyezaa na Jerry.



Ø      Anaanza tabia ya ulevi wa kupindukia. Rejea mwandishi anaposema, “Alianza kunywa pombe kali tena kwa wingi.” [Uk. 87] Pia katika Ukurasa wa 88 mwandishi anaendelea kuthibitisha hili anaposema, ”Akawa mlevi wa kupindukia. Hakuna kilichomzuia kunywa pombe kali…”





Ø      Anaanza uhusiano wa mapenzi na mwanaume mwingine aitwaye Gaddi Bullah baada ya kusalitiwa na Jerry.



Ø      Anapata ugonjwa wa ini kutokana na athari ya pombe kali alizokuwa akinywa kama mwandishi anavyothibitisha akimtumia muhusika Dokta Virani anaposema, “Ini lake la kulia limeathirika kutokana na pombe kali alizokuwa akinywa, wakati wa mfadhaiko wake uliotokana na madhila aliyofanyiwa na Jerry.” [Uk. 105]



Ø      Anafadhiliwa sehemu/kipande cha ini na Gaddi Bullah ili lipandikizwe katika ini lake, mwandishi analithibitisha hili anaposema; "Gaddi Bullah ndiye mfadhiri wako Dania..." [Uk 140]



Ø      Mapenzi yanaathiri utendaji wake kazini kwani hapo awali alikuwa ni mfanyakazi bora, mwenye nidhamu na ushirikiano kazini kama mwandishi anavyosema kupitia mhuhusika Mama Mlole; "Miaka minne iliyopita Dania Theobald alikuwa mmoja kati ya wafanyakazi wenye nidhamu, bidii na ushirikiano mkubwa hapa makao makuu." [Uk 81]

Baadhi ya tabia zake zinafaa kuigwa na jamii.



Ø      Wahusika wadogowadogo.

è    Bi. Hanuna Bint Majid

è     Ni dada pekee wa Gaddi Bullah.

è    Ni mjane, Kama mwandishi anavyosema; “Hanuna Bint Majid Bullah, maarufu kama Bi. Hanuna, ambaye ni mjane.”

è    Anafukuzwa kwenye nyumba

è    Ana mapenzi ya dhati kwa kaka yake Gaddi Bullah.

è     Anawekwa rumande kwa kosa la kumshambulia Dania, kama mwandishi anavyosema, " Hapo Jerry alikuja juu. Alipiga simu polisi na muda si mrefu Bi. Hanuna alikamatwa na kuwekwa rumande kwa kosa la shambulizi." [Uk. 127]   

  

Nunu.

è    Rafiki yake Dania

è    Mpenzi wa Boaz

è    Ni msichana mrembo.

è    MSichana jasiri.



Boaz

è    Mpenzi wa Nunu.

è    Anashirikiana na Nunu kumtafuta Gaddi Bullah

Anafaa kuigwa.



Jerry

è    Msomi na mtaalamu wa kompyuta

è    Alikuwa mpenzi wa Dania kabla ya kumsaliti.

è    Anapata ufadhili wa kwenda kusoma Marekani.

è    Hana mapenzi ya dhati kwa Dania.

è    Anatoweka baada ya kutakiwa kumtolea ini Dania.

è    Baba ya Junior.

Hafai kuigwa



Nyambuja

è    Mke wa kwanza wa Gaddi Bullah

è    Anamsaliti mumewe kwa kuanzisha uhusiano wa mapenzi na mwanaume mwingine.

Hafai kuigwa.

Wahusika wengine ni;

è    Dokta Virani

è    Mama Mlole [Fausta]

è    Junior



DHAMIRA.

Dhamira ni wazo au mawazo yaliyomo katika kazi ya fasihi na kwa kawaida katika kazi ya fasihi huwa tuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo, tukianza na dhamira kuu.



Ø      Dhamira kuu.

Dhamira kuu ni wazo kuu linalojitokeza katika kazi ya fasihi, dhamira kuu katika riwaya hii ni mapenzi na ndoa, sasa tuangalie ni kwa jinsi gani mwandishi ameijadili dhamira hii;

1. Mapenzi na Ndoa.

 Mwandishi Hussein Tuwa amejadili suala la mapenzi na ndoa katika pande mbili tofauti, kwanza ameonesha mapenzi ya dhati na mapenzi ya ulaghai lakini pia ameonesha ndoa za dhati na ndoa za ulaghai. tukianza na mapenzi ya dhati, mapenzi ya dhati yanajitokeza kwa:



 [a] Gaddi Bullah kwa mke wake wa kwanza anayeitwa Nyambuja,

Mwandishi ameonesha mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo Gaddi Bullah kwa mke wake, Mwandishi anathibisha hili anaposema; "...na mke mzuri aliyempenda sana na aliyeamini kuwa naye alikuwa akimpenda kawa dhati." [Uk 60]

mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo kwa mke wake pia yanajidhihirisha pindi mke wake huyo alivyoanza kubadirika kitabia, Gaddi alipewa ushauri na rafiki yake, lakini kwa kuwa alikuwa akimpenda mke wake hakuukubali ushauri aliopewa. Mwandishi anathibitisha hili anaposema; " ...Lakini kwa maoni yangu naona  bora na wewe ujitafutie nyumba ndogo ujiliwaze..."  mwandishi anaendelea kwa kusema; " ..Lakini hilo Gaddi hakuliafiki." [Uk 64]



 [b] Gaddi Bullah kwa Dania.

 Mapenzi ya dhati pia yanajitokeza kwa muhusika Gddi Bullah kwa Dania, mwandishi anaonesha mapenzi haya ya dhati tangu kuanza kwa uhusiano wa kimapenzi baina ya wawili hawa na hata mara baada ya Dania kumsaliti Gaddi Bullah, bado Gaddi alionesha mapenzi ya dhati kwa Dania na hata Dania alipoanza kuumwa ini Gaddi alijitolea ini lake moja kumsadia Dania ili apone yote haya aliyafanya kwa kuwa Bullah alikwa na mapenzi ya dhati kwa Dania, kama mwansihi anavyothibitisha akiwatumia wahusika ha wote wawili, mathalani Dania anapomuuliza Gaddi; " Umeokoa maisha yangu Gaddi...baada ya yote niliyokufanyia...na hukutaka nijue kuwa ni wewe...kwa nini mpenzi? Gaddi anamjibu kwa kumwambia; " Kwa sababu nakupenda Dania!" [Uk. 144]



[c] Mapenzi ya dhati kati ya Nunu na Boaz

Nunu na Boaz walipendana sana kuonesha mapenzi ya dhati kati, walishirikiana wakati wa shida na raha, na hata wakati Nunu anapewa kazi na Dania ya kumtafuta Daddi Bullah walishirikiana pamoja kumtafuta na wakati mwingine hata kuhatarisha maisha yao. Rejea  Uk 1-56 Nunu na Boaz wanavyoshirikiana kumtafuta Bullah na hadi kuwalazimu kumteka nyara Bi Hanuna ambaye ni dada yake Gaddi.



Tukigeukia katika uhalisia wake, katika jamii yetu wapo watu ambao hupendana sana na wakawa na mapenzi ya dhati na kusaidiana na kushirikiana kwa kila hali na mali kama tulivyoona kwa Nunu na Boaz katika riwaya hii.



[d] Mapenzi ya dhati ya Dania kwa Jerry.

Vilevile tunaona mapenzi ya dhati ya Dania kwa Jerry, pamoja na Jerry kumfanyia Dania kila aina ya vituko, kama vile kuk=mkimbia katikati ya maandalizi ya arusi yao, na kumtumia barua kuwa amepata mchumba mwingine huko Marekani na aliporejea kutoka Marekani na kutaka kurudiana na Dania, Dania anakubali ingawa alikuwa na mwanaume mwingine na hii yote ni kwasababu Dania alimpenda Jerry, kama mwandishi anavyothibitisha akitumia muhusika Dania anaposema; “Nilimuona Jerry ni bora kuliko Gaddi..." [Uk 135]



Tukigeukia katika uhalisia wake, ni wazi kuwa katika jamii zetu, wapo watu wanaoangukia katika mapenzi na watu ambao kiukweli hawawapendi ila kwa kuwa yeye anampenda basi hujikuta anajiingiza katika uhusiano naye matokeo yake ndiyo hayp sasa, usaliti, visa, vitimbi na kuona kuwa ndoa chungu.



[e] Mapenzi ya dhati kati ya Gaddi Bullah na Bi. Hanuna.

Hawa ni ndugu waliopendana sana, na hata katika matatizo yaliyomkuta Gaddi Bullah, Bi. Hanuna alikuwa bega kwa bega na kaka yake, na hakuwa tayari kumsaliti kaka yake kwa kiapo walichopeana pindi akitafutwa na watu ambao hakutaka kuwaona tena katika maisha yake kutokana na unyama aliofanyiwa, kwa mfano Mwandishi anamwonyesha Bi. Hanuna akikataa kata kata kumweleza Nunu mahali alipo Gadii Bullah, kama Mwandishi anvyosema akimtumia Bi. Hanuna mwenyewe; "Na kaniapiza kuwa nisithubutu hata siku moja kuwapeleka au kuwatajia mahala alipo...kwa sababu siwezi kuvunja kiapo changu na kumsaliti mdogo wangu pekee kwa ajili ya mahayawani kama nyinyi!" [Uk. 31-32]

Haya yote bi Hanuna aliyafanya kawa sababu walipendana sana na Gaddi, furaha ya Gaddi ilikuwa furaha ya Bi. Hanuna na kuumia kwa Gaddi kulikuwa ni kuumia kwa Bi. Hanuna na ndio maana kila aliyemuudhi mdogo wake kwake alikuwa adui yake.



Tukigeukia katika uhalisia, katika jamii yetu wapo ndugu ambao wanapendana na kushirikiana kwa kila hali kama wanavyoonekana Gaddi na Bi. Hanuna katika riwaya hii.





[f] Mapenzi ya dhati ya Gaddi Bullah kwa Junior.

Gaddi Bullah alimpenda sana Junior kama mtoto wa kumzaa mwenyewe, na hata Junior alipopata ajali ya kuanguka kutoka kwenye mti ni Gaddi ndiye aliagizwa apelekwe hospitali nae akafuata na alipomrudisha nyumbani hakuweza kumuacha peke yake, kama mwandishi anavyosema; "Gaddi alilazimika kusubiri pale nyumbani hadi atakaporudi, kwanza kwa kuhofia hali atakayokuwa nayo Junior pindi akiamka na kukuta si mama yake wala Gaddi aliyekuwepo pale nyumbani..." [Uk 119]



Na hata wakati anaumwa Gaddi alimwachia husia Dania amtunze vizuri Junior, Mwandishi anathibitisha anapomtumia Gaddi kusema; "Junior Dania... Junior! Mtunze vizuri Junior! Umepewa bahati ya kuu...ndelea kuishi ili umtunze mwan...na...o!"

[Uk 146]



Haya yote Gaddi Bullah aliyanya kwa kuwa alimpenda sana Junior. Na tukigeukia katika uhalisia wake katika jamii zetu, wapo watu au familia ambazo utamkuta baba si mzazi wa mtoto au mama lakini wakaonesha mapenzi ya dhati kwa watoto hao kana kwamba wao ndiyo wamewazaa, upendo ambao hata mzazi husika hawezi kutoa kama tunavyoona kwa Jerry.



[g] Mapenzi ya dhati ya Mama Mlole kwa wafanyakazi walio chini yake.

Mwandishi amemtumia muhusika Mama Mlole [Fausta] kama kiongozi anayewajali na kuwapenda wafanyakazi wake na kuwasaidia pindi wanapopatwa na matatizo, kwa mfano Mama Mlole anaonesha mapenzi ya dhati kwa kumsaidia Dania kurudi kazini licha ya kuwa na matatizo, lakini pia Mama Mlole alimsaidia na Gaddi Bullah ili asifukuzwe kazi kutokana na kutuhumiwa kuhusika na malipo hewa. Mwandishi anathibitisha hili anapomtumia muhusika Mama Mlole anapoongea na Gaddi Bullah; "Ndio... na kwa hatua aliyofikia, ilibidi aachishwe kazi, lakini kwa kumsaidia, nikiwa kama Afisa Utumishi wa kampuni, nilipendekeza apewe likizo.... nilifanya kazi ya ziada kuushawishi uongo wa kampuni juu ya hili, jinsi nilivyofanya kazi ya ziada kulishawishi lile jopo la wakaguzi kule Arusha kukupa wewe nafasi nyingine...badala ya kukufaukuza kazi..." [Uk 88]



Mama Mlole pia alikuwa akimtembelea Dania wakati alipokuwa anaumwa ili kujua maendeleo yake kama anavyosema; "Mimi nilikuwa nikimtembelea mara kwa mara kuona maendeleo yake na kuleta ripoti kwenye uongozi wa kampuni.



Mama Mlole anayafanya yote haya kwakuwa anawapenda wafanyakazi wake, na tukiaangalia katika uhalisia wake, wako mabosi au wakuu ambao huwapenda wafanayakazi waliochini yao na hata wanapokabiliwa na matatizo huwasaidia kama tulivyoona kwa Mama Mlole.



[h] Mapenzi ya dhati kati ya Nunu na Dania.

Nunu alikuwa ni rafiki wa kweli wa Dania, walishirikiana bega kwa bega, wakati wa maadalizi ya arusi ya Dania na Jerry, Nunu alikuwa ndiye mwenyekiti wa kamati, na hata Dania aliposalitiwa na Jerry na Dania kuanza tabia ya ulevi ni Nunu ndiye alikuwa akimsaidia Dania kumlelea mtoto wake na hata Dania alipoanza kuumwa Nunu alikuwa tayari kumtolea ini lake kama mwandishi anavyothibitisha hili anaposema, “Nunu naye alijitolea. Vipimo vilionesha kuwa maini yake yote yalikuwa safi na aliweza kabisa kumtolea Dania ini moja, lakini damu yake ilikuwa haioni kabisa na ile ya Dania." [Uk 132]

Na hata Dania alipompa Nunu kazi ya kumtafuta Gaddi Bullah aliifanya kwa moyo wote kwakuwa alimpenda rafiki yake.



Tukiaangalia uhalisia wake na jamii yetu, wapo marafiki aina ya Dania na Nunu ambao hupendana, husaidiana katika shida na raha, kupeana ushari unaojenga. n.k huu ndio urafiki unaofaa.



[i] Mapenzi ya dhati ya Dania kwa Mtoto wake {Junior]

Vilevile mapenzi ya dhati yanajidhihirisha kwa Dania kwa mtoto wake, Dania alimpenda sana mtoto wake [Junior] mpaka kuamua kurudiana na Jerry ambaye ndiye baba wa wmtoto wake ili mwanae apate malezi ya baba na mama kama mwandishi anavyothibitisha hili akimtumia muhusika Dania anaposema; "Siwezi Nunu, siwezi...nimeshaanza naye uhusiano nadhani Junior anastahili zaidi kulelewa na baba yake mzazi kuliko baba wa kambo." [Uk.115]


Tukigeukia katika uhalisia wake, katika jamii yetu wapo wazazi ambao huwapenda watoto na hata kutopenda kuona watoto wao wanapatwa na matatizo katika makuzi yao.



{j] Mapenzi ya dhati kwa wazazi wa Dania kwa mtoto wao Dania.

Pia mapenzi ya dhati yanajitokeza kwa wazazi wa Dania, kwa mfano baba yake Dania [Mzee Theobald] anamjengea Dania nyumba na hata Dania anapoanza kuumwa ini wazazi wake wanakuwa tayari kujitolea ini moja kwa ajili ya mtoto wao lakini kutokana na uzee na kuumwa kisukari kwa Mzee Theobald inashindikana kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika Mzee Theobald; "Dokta, mimi niko tayari kujitolea ini laangu kwa ajili ya mwanagu!" pia mwandishi anaendelea kusema, "Na wakati huo huo mama naye alijitolea."  [ Uk 132]



Tukiigeukia jamii yetu, wapo wazazi aina ya Mzee Theobald na mkewe, ambao huwapenda watoto wao na kujitoa kwa kila hali ili mradi tu kuona kuwa watoto wao wanaishi maisha mazuri na salama.

[k] Mapenzi ya dhati kati ya Dokta Virani na Gaddi Bullah

Vilevile katika riwaya hii ya Mfadhili mwandishi ameonesha mapenzi ya dhati aliyonayo Dokta Virani kwa Gaddi Bullah, Dania pamoja na Bi. Hanuna. kwa mfano tunamwona Dokta Virani akipigana kufa na kupona kuokoa maisha ya Dania na hata kumuangaikia kumtafutia mfadhili wa kumfadhili ini katika vyombo mbalimbali vya habari, vilevile anamsaidia Dania kumjua mfadhili aliyemfadhili ini jambo ambalo lilikuwa likimsumbua sana Dania, Mwandishi analithibitisha hili akimtumia muhusika Dokta Virani akimw.ambia Dania; "Gaddi Bullah ndiye mfadhili wako Dania..." [Uk 140]



Lakini pia mwandishi ameonesha mapenzi ya dhati ya Dokta Virani kwa Gaddi Bullah na jinsi alivyojitahidi kuokoa uhai wa  Gaddi, lakini Mungu alimpenda zaidi Gaddi, akamtwaa. [Uk 144-148]



Pia mapenzi ya dhati ya Dokta Virani kwa Bi. Hanuna. katika riwaya hii tunaona baada ya Bi. Hanuna kukamatwa na kuwekwa rumande ni Dokta Virani anahangaika na kumtoa kwa dhamana kama mwandishi anavyosema; "Dokta Virani alipopata taarifa alihangaika huku na huko kumpatia dhamana, lakini ilishindikana." Mwandishi anaendelea kusema; "Siku iliyofuata, Dokta Vilani alifanikiwa kumtoa kwa dhamana." [Uk 127]



Hata katika jamii yetu watu jamii ya Dokta Virani wapo, huwajali wateja wao, huwapenda na wakati mwingine kuwa sehemu ya familia hizo kama tunavyomuona Dokta Virani na akina Gaddi Bullah.



Mapenzi ya Ulaghai / Uongo

Pamoja na kuwa mwandishi ameweza kuonesha ni kwa jinsi kuna watu wenye mapenzi ya dhati kwa wenzi wao, ndugu, jamaa na marafiki, mwandishi kwa upande mwingine ameonesha nai kwa jinsi gani katika jamii yake  kuna watu wasio na mapenzi ya dhati kwa watu wanaohusiana nao, kama vile wanandoa, wapenzi, marafiki, ndugu, jamaa na marafiki. Ebu tuangalie sasa jinsi mapenzi ya ulaghai yanavyojitokeza katika riwaya hii;

 

[a] Dania  kwa Gaddi Bullah

Dania hakuwa na mapenzi ya dhati kwa Gaddi Bullah, na ndio maana mara aliporejea mpenzi wake wa zamani aitwaye Jerry ilikuwa ni rahisi kwa Dania kukubali kurudiana nae ingawa alikuwa na mahusiano na Gaddi Bullah mpaka kufikia hatua ya kumfukuza Gaddi nyumbani kwake, kama mwandishi anavyoonesha akimtumia muhusika Dania anapomwambia Gaddi Bullah; "Gaddi samahani sana kwa hili, lakini naomba ujue sitakuwa tayari kumyima mwanangu nafasi ya kuishi na baba yake mzazi kwa ajili ya mtu yoyote! Nakuomba uondoke Gaddi..." [Uk 122]



Hata katika jamii yetu, mapenzi ya aina hii yapo, wapa watu kama Dania ambao hujikuta wakijiingiza katika mahusiano na watu wengine ili kutafuta faraja kutokana na kuachwa au kusalitiwa na wenza wao lakini si kwamba wana mapenzi ya dhati na pindi inapotokea kurubuniwa tena na wenza wao wa zamani inakuwa rahisi kwao kukubali na kuwa chungu kwa yule anayeachwa kama tulivyoona kwa Gaddi Bullah.



[b] Jerry kwa Dania

Jerry hakuwa na mapenzi ya dhati kwa Dania, kwa mfano katika riwaya hii tunamwona Jerry akimkimbia Dania katika hatua za mwisho za maandalizi ya arusi yao na kwenda Marekani kwa ajili ya masomo, na anapofika huko anamwandikia Dania barua kuwa amepata mwanamke mwingi wa kizungu anataka kumuoa kama mwandishi anavyosema; " Mwaka wa pili ulipoisha Jerry alileta barua kuwa alikuwa amepata mwanamke wa kizungu aliyepanga kufunga nae ndoa hukohuko Marekani.” [Uk 87]



Na hata Jerry aliporejea na kuomba msamaha kwa Dania, Dania anamsamehe lakini pindi Dania anapoanza kuumwa na yeye kuombwa ajitolee ini anatoweka kabisa kama mwandishi anavyoonesha; "Baada ya hapo Jerry Gwandume alitoweka. Alitoweka kabisa  siku ya operesheni hakuonekana na kwenye simu akawa hapatikani. Nyumbani kwake hakupatikana..." [Uk 133]

Mwandishi anaendelea kusema; "...na hapo ndipo ilipoeleweka dhahiri kuwa Jerry amekimbia kumtolea ini lake Dania." [Uk 133]



Katika jamii yetu watu aina ya Jerry wapo, ambao huwaraghai wasichana kwa maneno mazuri lakini inapofika wakati wa shida huwakimbia na kutoweka kama tulivyoona kwa Jerry.



[c] Nyambuja kwa Gaddi

Nyambuja hakuwa na mapenzi ya dhati kwa Gaddi Bullah, pamoja na kuwa Nyambuja alikuwa ameolewa lakini bado akawa anaisaliti ndoa yake kwa kuanzisha uhusiano na mwanaume mwingine, na hata barua aliyomwandikia Gaddi Bullah inaonyesha dhahiri kuwa Nyambuja hakuwa na mapenzi ya dhati kwa mumewe. Rejea barua aliyoandika Nyambuja anaposema; “Gaddi nimependana na mtu mwingine, na nimekuwa nikisaliti ndoa yetu kwa muda mrefu.” [Uk 65]



Tukigeukia katika uharia wake, watu kama Nyambuja wapo, zipo ndoa nyingi katika jamii zetu ambazo zimekuwa zikijaa usaliti, dharau. n.k. Katika ndoa mume anaweza kumsaliti mke na mke pia anaweza kumsaliti mume kama tulivyoona kwa Nyambuja.



 [d] Rafiki wa Bullah kwa Bullah.

Rafiki wa Gaddi Bullah pia hakuwa na mapenzi ya kweli na Gaddi Bullah, kwa mfano rafiki huyo anamshauri Gaddi Bullah kutafuta nyumba ndogo wakati akijua kuwa ulimwengu wa sasa umejaa magonjwa ya hatari hususani UKIMWI. Rafiki wa kweli hawezi akatoa ushari kama huo. Rejea Ukurasa wa 67 rafiki huyo anapomshauri Gaddi, anasema; “Gaddi unajua mimi sijaoa. Nitawezaje kutoa ushauri juu ya suala kama hilo?.....Lakini kwa maoni yangu naona bora na wewe ujitafutie nyumba ndogo ujiliwaze…” [Uk 67]



Pia mwandishi anaonesha urafiki huu wa mashaka anaofanyiwa Gaddi na huyo rafiki yake kwa kuamua kumsaliti na kuanzisha uhusiano wa mapenzi na mke wa Gaddi Bullah, Mwandishi anaonesha hili akimtumia Gaddi Bullah anaposema; "Na wewe! Nilidhani kuwa u rafiki yangu! Nilikuwa nakuletea matatizo yangu kumbe ulikuwa ukinilamba kisogo?” [Uk 67]



Hata katika jamii zetu urafiki wa aina hii upo, utakuta mtu anajifanya kuwa ni rafiki wa kweli lakini kumbe ndiye anaekuzunguka na kukuharibia mambao yake kama tulivyoona kwa Gaddi na rafiki yake.

   

Ø      Dhamira ndogo ndogo.

Haya ni mawazo yanayojitokeza ili kujenga dhamira kuu. Dhamira ndogondogo zinazojitokeza katika riwaya hii ni;



1. Usaliti.

Hii ni dhamira nyingine inayojitokeza katika riwaya hii, sasa tuangalie jinsi usaliti huo unavyojitokeza katika riwaya hii;



[a] Nyambuja anamsaliti Gaddi Bullah.

Mwandishi ameonesha katika ndoa kwa kuwatumia wahusika Gaddi Bullah na Nyambuja, kwa mfano nyambuja anaamua kuisaliti ndoa yako kwa kuanza uhusiano wa mapenzi nje ya ndoa na mwanaume mwingine, hili Mwandishi analithibitisha akimtumia Nyambuja mwenyewe anaposema katika barua aliyomwandikia Gaddi Bullah, “Gaddi nimependana na mtu mwingine, na nimekuwa nikisaliti ndoa yetu kwa muda mrefu.” [Uk 65]



[b] Jerry anamsaliti Dania

Usaliti mwingine unaojitokeza katika riwaya hii, ni usaliti unaofanywa na Jerry kwa Dania, kwa mfano Mwandishi anamuonesha Jerry akienda masomoni Marekani kaatika hatua za mwisho za maandalizi ya ndoa yake na Dania, na anapofika huko anamwandikia Dania kuwa amepata mwanamke mwingine wa kizungu anaetaka kumuoa, hili linathibitishwa na Mwandishi anaposema; " Mwaka wa pili ulipoisha Jerry alileta barua kuwa alikuwa amepata mwanamke wa kizungu aliyepanga kufunga nae ndoa hukohuko Marekani.” [Uk 87]



[c] Dania anamsaliti Gaddi Bullah

Mwandishi pia ameonesha usaliti katika mapenzi akimtumia muhusika Dania, kwa mfano Mwandishi anamwonesha Dania akimsaliti mpenzi wake [Gaddi Bullah] kwa kuamua kurudiana na mpenzi wake wa zamani aliyezaa naye mtoto na kuamua kuachana na Gaddi, Mwandishi unaonesha usaliti huu akimtumia Dania anapomwambia Gaddi Bullah;"Gaddi samahani sana kwa hili, lakini naomba ujue sitakuwa tayari kumyima mwanangu nafasi ya kuishi na baba yake mzazi kwa ajili ya mtu yoyote! Nakuomba uondoke Gaddi..." [Uk 122]



[d] Gaddi Bullah anasalitiwa na Rafiki yake.

Mwandishi pia ameonesha usaliti katika urafiki, amemtumia muhusika rafiki yake Gaddi

ambaye anaamua kumsaliti rafiki yake [Gaddi Bullah] wakati akiwa ni rafiki wa karibu wa Gaddi na alimtegemea sana kwa ushauri pindi anapoptwa na matatizo, Mwandishi analionesha hili anaposema; "Baadaye aliamua kwenda kwa rafiki yake kumpasha habari habari juu ya masahibu yake. na huko alipata mshituko mkubwa. Mke wake mwenyewe ndiye aliyemfungulia mlango, tena akiwa khanga moja tu...ilhali rafiki yake akiwa amejitawanya kwenye sofa akiwa kidari wazi na kaptura tu!" [Uk 66]



Tukigeukia katika uhalisia wake, usaliti katika ndoa, mapenzi na hata marafiki wa kawaida tu limekuwa ni tatizo katika jamii na ni suala ambalo linatakiwa kupigwa vita sana katika dunia hii yenye magonjwa ya kila aina.



2. Ulevi.

Mwandishi Hussein Tuwa hakuwa nyuma kujadili suala la ulevi na athari zake kwa afya ya binadamu, katika riwaya yake hii amemtumia muhusika  Dania pamoja na Gaddi Bullah kuelezea dhamira hii. Tukianza na Dania, mwandishi anamwonesha Dania akianza tabia ya ulevi wa pombe kali baada ya kusalitiwa na Jerry ambaye alikwa ni mpenzi wake, kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika Mama Mlole, “Alianza kunywa pombe kali tena kwa wingi.” [Uk 87] mwandishi hakuishia hapo tu bali ameonesha na athari za tabia hiyo ya ulevi kama vile kupata ugonjwa wa ini kama mwandishi anavyothibitisha akimtumia muhusika Dokta Virani anaposema," “Ini lake la kulia limeathirika kutokana na pombe kali alizokuwa akinywa, wakati wa mfadhaiko wake uliotokana na madhila aliyofanyiwa na Jerry.” [Uk 105]



Lakini pia athari nyingine anazozipata Dania kutokana na ulevi wa kupindukia ni kupoteza ufanisi wa kazi, hili pia linathibitishwa na mandishi anaposema; "Na hapo ndipo utendaji wake kazini ulipoathirika vibaya sana. kazi zikawa haziendi kabisa. Alipofikia hatua ya kuja ofisini akiwa amelewa zaidi ilikuwa ni zaidi ya kuvumilika." [Uk 88]



Mwandishi pia amemtumia muhusika Gaddi Bullah kuelezea dhamira hii ya ulevi, tofauti na Dania ambaye yeye ametumiwa kuonesha dhamira ya ulevi wa pombe, Gaddi Bullah ametumika kuelezea dhamira ya Ulevi wa uvutaji wa sigara uliokithiri kama mwandishi anavyothibitisha anaposema, "Alikuwa akivuta sigara mfululizo huku kichwa chake kikiwa kimetawaliwa na mawazo mazito..." [Uk 57]



Mwandishi hakuishia hapo kuonesha tataizo la uvutaji sigara, ameonesha pia athari zake ambapo katika riwaya hii anamtumia muhusika Gaddi Bullah kutokana na uvutaji wa sigara uliokitiri Gaddi anapata matatizo ya mapafu na hatimaye kuaga dunia kutokana na matatizo hayo. Hivyo basi suala la ulevi jamii inatakiwa kuachana nalo kwa ni hatari kwa afya na uhai wa binadamu.



3. Malezi kwa watoto.

Hii ni dhamira nyingine inayojitokeza katika riwaya hii, Mwandishi amemtumia muhusika Dania kuilezea dhamira hii, tunamwona Dania akitaka kurudiana na Jerry ambaye ni baba wa mtoto wake ili kwa pamoja waweze kumlea mtoto wao akiamni kuwa malezi ya mtoto ni ya wazazi wote wawili kama mwandishi anavyothibitisha hili akimtumia muhusika Dania mwenyewe, "Ni kweli kuwa Jerry alinikosea, na nikweli kuwa wewe nilikupenda! Lakini Jerry ni baba wa mtoto wangu! Na naomba uelewe kuwa uamuzi huu ni kwa ajili ya mwanetu..." [Uk 122]



4. Unafiki.

Hii ni dhamira pia inayojitokeza katika riwaya hii, katika kuijadili dhamira hii Mwandishi amemtumia  rafiki yake Gaddi Bullah,  anamwonesha Gaddi Bullah akiomba ushauri kwa rafiki yake huyo kuhusiana na matatizo yake na mkewe, rafiki huyo anamshauri Gaddi atafute nyumba ndogo. Rejea ukurasa wa 64 Mwandishi anaposema, “Gaddi unajua mimi sijaoa. Nitawezaje kutoa ushauri juu ya suala kama hilo?.....Lakini kwa maoni yangu naona bora na wewe ujitafutie nyumba ndogo ujiliwaze…”

Rafiki huyo anashauri hivyo huku kumbe yeye ndiye chamzo anayemsaliti mwenzake kwa kumzunguka kwa mke wake, kama mwandishi anavyothibitisha hili anaposema; “ Na wewe! Nilidhani kuwa u rafiki yangu! Nilikuwa nakuletea matatizo yangu kumbe ulikuwa ukinilamba kisogo?” [Uk 67]



Tukigeukia katika uharisia, tabia hii ya unafiki imeshamiri katika jamii zetu, unaweza ukawa na rafiki au ndugu ambaye akawa mnafiki kwako. Jamii inatakiwa kuondokana na tabia hii kwa haifai kabisa.



5. Ufisadi / Wizi kazini.

Mwandishi pia amejadili suala la ufisadi sehemu ya kazi, amemtumia muhusika Afisa Usafirishaji ambaye anapeleka orodha malipo ya magari saba yaliyofanyiwa matengenezo huku magari matano yakiwa magari hewa kama mwandishi anavyosema, “ Kwani ilionekana kuwa katika magari saba yaliyofanyiwa malipo kwa matengenezo, ni mawili tu ndio hasa yaliyopelekwa matengenezo. Ni wapi pesa za malipo ya yale magari matano mengine zilikwenda?” [Uk 68]



Tukigeukia katika uhalisia wake, suala la ufisadi au wizi sehemu za kazi ni suala ambalo linasumbua sana jamii yetu, si serikalini au katika makampuni binafsi ufisadi kama vile kuandaa vocha za malipo hewa, rushwa tena zile kubwa kubwa, matumizi mabaya ya mali za ofisi. n.k ni tatizo sugu na jamii inatakiwa kuondoka nalo.



6. Elimu.

Mwandishi hakuwa nyuma kujadili suala la elimu na umuhimu wake kwa jamii. Katika kujadili dhamira hii mwandishi anaonesha kuwa elimu ni ufunguo unaoweza kumfunguliwa mtu milango mipya ya maendeleo kielimu na kiuchumi, kama Mwandishi anavyothibitisha hili anaposema akimtumia muhusika Mama Mlole, “ Mke anamtaka, lakini na masomo pia anayataka. Masomo ambayo yangemfungulia milango mipya ya maendeleo kielimu na kiuchumi.” [Uk 84]



Hata katika jamii zetu, jamii imekuwa ikisisitiza sana suala la elimu, watu wengi waliosoma wamepata kazi nzuri na wana maisha mazuri kama tulivyoona kwa Gaddi Bullah, lakini pia wapo vijana waliopata elimu zao nje ya nchi kama tulivyoona kwa Jerry.



7.  Uongozi bora

Vilevile suala la uongozi bora limejitokeza katika riwaya hii, kwa mfano mwandishi anamtumia muhusika Mama Mlole [Fausta] kujadili dhamira hii, tunamwona Mama Mlole jinsi alivyokuwa na upendo kwa wafanayakazi waliochini yake, anawasaidia pindi wanapopatwa na matatizo, mathalani anamsaidia Dania na Gaddi Bullah wasifukuzwe kazi kama mwandishi anavyothibitisha hili akimtumia Mama Mlole mwenyewe; "Ndio... na kwa hatua aliyofikia, ilibidi aachishwe kazi, lakini kwa kumsaidia, nikiwa kama Afisa Utumishi wa kampuni, nilipendekeza apewe likizo.... nilifanya kazi ya ziada kuushawishi uongo wa kampuni juu ya hili, jinsi nilivyofanya kazi ya ziada kulishawishi lile jopo la wakaguzi kule Arusha kukupa wewe nafasi nyingine...badala ya kukufaukuza kazi..." [Uk 88]



Mwandishi pia anasisitiza suala la uongozi, akiwataka viongozi wabadilike wawe viongozi wa kuwajenga watu waliochini yao kitabia na kimaadili kama Mwandishi anavyosema akimtumia Mama Mlole; "Utawala wa kusubiri mfanyakzi akosee ili umuadhibu siku hizi umepitwa na wakati, Gaddi! Utawala wa sasa ni wa kumjenga mfanyakazi kitabia na kimaadili ili asiingie kwenye makosa yatakayosababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Viongozi tunatakiwa tubadilike sasa, Gaddi!" [Uk 93]



Tukigeukia katika uhalisia wake, katika jamii yetu viongo bora kama Mama Mlole wapo lakini pia wapo viongozi ambao wao husubiri wafanyakazi wao wakosee ili wawachukulie hatua kama kuwafukuza kazi au kuwapa onyo kali. Hivyo viongozi wanatakiwa kubadilika na kwenda na wakati.



8.  Nafasi ya mwanamke.

Katika riwaya hii mwanamke amechorwa katika pande mbili, amechorwa katika upande hasi lakini pia mwanamke amechorwa katika upande chanya, upande hasi mwanamke amechorwa kama kiumbe duni na dhaifu wakati katika upande chanya amechorwa kama mtu jasiri, mchapa kazi, mwenye upendo. n.k. Ssasa hebu tuangalie nafasi ya mwanamke katika jamii kama alivyochorwa katika riwaya hii tukianza na upande hasi;



Katika riwaya hii mwanamke amechorwa kama kiumbe duni, dhaifu, katika nafasi mwanamke amechorwa kama;



[A] Chombo cha starehe.

Mwandishi amemchora mwanamke kama chombo cha starehe anayeweza kutumiwa kuwastarehesha wanaume na wakapokeza jinsi wanavyotoka ili mradi kufurahisha nafsi zao, hili linathibitishwa na Mwandishi katika riwaya hii akimtumia muhusika Jerry anapomwambia Gaddi Bullah; "Hakuna haja ya kupoteza muda. Tumeamua kufunga ndoa kwa kuzingatia maslahi ya mwanetu, kwahiyo bwana we kaa pembeni sasa. Muda wako kwa Dania umekwisha." [Uk. 121]



Mwandishi pia amemtumia rafiki yake Gaddi Bullah kumchora mwanamke kama chombo cha starehe kwa kuwa mwanaume anaweza kumtumia kujilawa na kuburudisha nafsi, kama anavyosema; “...Lakini kwa maoni yangu naona bora na wewe ujitafutie nyumba ndogo ujiliwaze…”[Uk 64]



Hata katika jamii yetu inayotuzunguka wanawake kwa kujijua au kutojua wamekuwa wakifanywa kama chombo cha starehe kuwastarehesha wanaume, jamii inatakiwa kubadilika na kuondokana na dhana hii kwani mwanamke pia anastahiri heshima katika jamii.



[B] Mtu asiye na maamuzi katika jamii

Mwandishi amemchora mwanamke kama mtu asiye na maamuzi katika jamii yake, kwa mfano anamtumia muhusika Bi. Hanuna kuthibitisha hili, baada ya Bi. Hanuna kufiwa na mumewe na kwa kuwa hakuzaa nae anakuwa hana maamuzi na haki yoyote kwa mali aliyochuma na mume wake na ndugu wa mume wanaamua kumfukuza katika nyumba aliyojenga na mume wake kama mwandishi anavyosema; " ...ambaye naye hakujaliwa kupata mtoto mpaka mumewe alipofariki, jambo lililowafanya ndugu wa marehemu mumewe kumfukuza kama mbwa kutoka kwenye nyumba ya marehemu mumewe."          [Uk 60]



Hata katika jamii yetu, inawachukulia wanawake kama watu wasio na maamuzi katika familia na pindi inapotokea kufiwa na waume zao huwa wanapata shida na manyanyaso kutoka kwa ndugu wa mwanaume kama vile kufukuzwa kwenye nyumba, kunyang'anywa watoto na mali nyingine alizoshirikiana kuzichuma na mumewe. jamii inatakiwa kumpa nafasi mwanamke na itambue kuwa ana haki sawa kama mwanaume.



[C] Mwanamke amechorwa kama mtu asiye na msimamo katika maamuzi yake.

Hili Mwandishi amelionesha kupitia kwa muhusika Dania, ambaye anaonekana kuwa hana msimamo juu ya kila anachoamua, kwa mfano baada ya Dania kusalitiwa na Jerry na kupata matatizo mbalimbali kutokana na kusalitiwa huko, baadaye tunamwona akianza uhusiano na mwanaume mwingine lakini anaporejea yule aliyemsaliti mwanzo na kumrubuni kwa maneno mazuri anajikuta akirudiana nae kama mwandishi anavyosema; "BIla kujijua, Dania alijikuta akijiingiza tena katika mapenzi na Jerry." [Uk 113]



Hata katika jamii yetu, wanawake wengi kwa kutokuwa na misimamo ya kimaisha hujikuta wakijiingiza katika matatizo mbalimbali kama vile kurubuniwa na wanaume. Hivyo wanawake wenyewe wanatakiwa kujitambua na kubadilika.                



[D] Mwanamke amechorwa kama msaliti.

Hii ni nafasi nyingine ambayo mwandishi amemchora mwanamke, kwa mfano tunaona Nyambuja akiisaliti ndoa yake. Rejea barua aliyoandika Nyambuja kwa Gaddi Bullah anaposema;“Gaddi nimependana na mtu mwingine, na nimekuwa nikisaliti ndoa yetu kwa muda mrefu.” [Uk 65]



vilevile nafasi hii ya usaliti imechorwa kupitia muhusika Dania, ambaye anamsaliti Gaddi Bullah kwa kuamua kurudiana na Jerry ambaye amezaa naye mtoto na kufikia hatua ya kumfukuza Gaddi nyumbani kwake baada ya kuwafumania. Rejea Dania anapomwambia Gaddi Bullah; "Gaddi samahani sana kwa hili, lakini naomba ujue sitakuwa tayari kumyima mwanangu nafasi ya kuishi na baba yake mzazi kwa ajili ya mtu yoyote! Nakuomba uondoke Gaddi..." [Uk 122]



Hivyo ndivyo jinsi mwandishi Hussein Tuwa alivyomchora mwanamke katika upande hasi, yaani kiumbe duni na dhaifu sasa tugeukie upande wa pili, upande chanya, katika upande huu mwanamke amechorwa katika nafasi zifuatazo:



[A] Mwanamke amechorwa kama mtu jasiri.

Mwandishi katika riwaya hii amemtumia muhusika Nunu Mkwanda, tunaona namna nunu anavyojitoa muhanga na kuamua kumteka Bi. Hanuna huku akifahamu kuwa kitendo hicho ni cha hatari, alifanya hivyo kwa kuwa Bi. Hanuna hakuwa tayari kutaja alipo Gaddi Bullah, na allifanya hivyo ili mradi tu lengo  la kumpata Gaddi Bullah kama alivyomuahidi rafiki Dania limitie, Mwandishi anathibisha hili anapomtumia Nunu anaposema; Potelea mbali Bi. Hanuna! Alimradi utakuwa umeona ni kwa nini nimelazimika kufanya hivi baada ya maombi yangu kwako kushindikana, haitakuwa na neno kabisa kwangu." [Uk. 44]



Hata katika jamii zetu wanawake jasiri kama Nunu wapo ambao hujitoa kwa kila hali na wakati mwingine hata kuweza kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya wengine.



[B] Mwanamke amechorwa pia kama kiongozi bora.

Mwandishi amemtumia muhusika Fausta Mlole ambaye wanyakazi wake kutokana uongozi wake mzuri na kuwajali wafanyakazi walikuwa wakimuita kwa jina la Mama Mlole, katika riwaya hii Mama Mlole anawakilisha wanawake viongozi ambao huwaongoza wafanyakazi waliochini yao kwa kufauta taratibu, upendo na kuwasaidia, kuwa karibu nao wakati wa shida na raha kama tunavyomuona Mama Mlole akifanya kwa wafanyakazi wake.



Kwa mfano Mama Mlole kama Afisa Utumishi anamsaidia Gaddi na Dania wasifukuzwe kazi kama anavyosema; "Ndio... na kwa hatua aliyofikia, ilibidi aachishwe kazi, lakini kwa kumsaidia, nikiwa kama Afisa Utumishi wa kampuni, nilipendekeza apewe likizo.... nilifanya kazi ya ziada kuushawishi uongo wa kampuni juu ya hili, jinsi nilivyofanya kazi ya ziada kulishawishi lile jopo la wakaguzi kule Arusha kukupa wewe nafasi nyingine...badala ya kukufaukuza kazi..." [Uk 88]



Hata katika jamii yetu wanawake viongozi kama Mama Mlole wapo, na wanawaongoza vizuri wafanayakazi pengine kuwazidi hata baadhi ya wanaume. hivyo wanawake wakiwezeshwa wanaweza.



Hivyo ndivyo jinsi mwandishi alivyoweza kumchora mwanamke katika nafasi mbalimbali katika jamii yake.



MIGOGORO

Mgogoro wa nafsi.

Gaddi Bullah na nafsi yake

Gaddi Bullah anakuwa na mgogoro dhidi ya nafsi yake, chanzo cha mgogoro huu ni kuanza kubadilika kwa tabia ya mke wake, na kusababisha Gaddi awaze sana na kujiuliza maswali mengi pasina kupata majibu, kama mwandishi anavyoonesha akimtumia Gaddi Bullah; "Kwa nini Nyambuja ananifanyia hivi? Kuna nini anachokosa kwangu? Yaani mambo yote niliyomfanyia huu ndio wema anaonilipa kweli?" [Uk 62] Suluhisho la mgogoro huu ni baada ya Gaddi Bullah kugundua kuwa mke wake alikuwa akiisaliti ndoa wakaamua kuvunja ndoa yao kama mwandishi anavyosema; “ Wiki moja baadaye Gaddi na Nyambuja waliachana kisheria….” [Uk 68]



Pia kuna mgogoro mwingine wa Gaddi Bullah na nafsi yake, chanzo cha mgogoro huu ni baada ya Gaddi Bullah kusalitiwa na Dania, suluhisho la mgogoro huu wa nafsi ni Gaddi kuamua kutoweka na kwenda kuishi Pemba ili kuwa mbali na Dania katika maisha yake yote. kama mwandishi anavyosema akimtumia Bi. Hanuna; "Gaddi Bullah amefanya yote hayo ili awe mbali kabisa na huyo rafiki yako na wote mnayehusiana nae." [Uk 31]

Dania na nafsi yake



Dania na nafsi yake

Chanzo cha mgogoro huu ni baada ya Dania kusalitiwa na Jerry mpaka Dania akataka kujiua kama mwandishi anavyosema; “…Sasa hili lilkuwa ni pigo la mwisho na Dania alivurugikiwa kabisa….alijaribu kujiua…” [Uk 87] Suluhisho la mgogoro huu ni Dania kuanza uhusiano wa kimapenzi na Gaddi Bullah.



Pia mgogoro mwingine wa Dania na nafsi yake unajitokeza baada ya Dania kufadhiliwa ini na hatimaye kupona akawa na mgogoro wa nafsi wa kutaka kujua ni nani hasa mfadhili wake, kama mwandishi anavyosema; "Ila sasa akili yake ikawa inajiuliza swali moja kila siku. Mfadhili wake ni nani?" [Uk 139]

Suluhisho la mgogo huu ni hatua ya Dokta Virani kuamua kumweleza Dania kuwa mfadhili wake ni Bullah. Kama mwandishi anavyosema; "Gaddi Bullah ndiye mfadhili wako Dania..." [Uk 140]



Nunu na nafsi yake

Chanzo cha mgogoro huu ni hatua ya Dania kumsaliti Gaddi Bullah na Gaddi Bullah anaenda nyumbani kwa Nunu anapata mgogoro wa nafsi juu ya nini atakachomweleza Gaddi, kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika Nunu; "Mungu wangu! Nitamueleza nini Gaddi leo? Nitaanzaje? Hivi kwanini Dania ananiweka kwenye mtihani namna hii lakini?[Uk. 123]



Dokta Virani na nafsi yake

Chanzo cha mgogoro huu ni kukaa na siri moyoni mwake ambayo walikubaliana na Gaddi Bullah kuwa asimwambie mtu kuwa yeye ndiye mfadhili wa Dania, Suluhisho la mgogoro huu ni Dokta Virani kuamua kuitoa hiyo siri, kama anavyosema: "Samahani sana Gaddi...imenibidi nifanye hivyo...nadhani Dania alipaswa ajue kuwa ni wewe ndiye uliyejitolea ini lako ili kuokoa maisha yake!" [Uk.144]



Mgogoro kati ya mtu na mtu



Gaddi Bullah na Nyambuja

Gaddi Bullah anakuwa na mgogoro na Nyambuja ambaye ni mke wake, chanzo cha mgogoro huu ni hatua ya Nyambuja kubadilika kitabia kama vile kuanza kuchelewa kurudi nyumbani, majibu ya hovyo na hatimaye kugundua kuwa alikuwa akiisaliti ndoa yao. Suluhisho la mgogoro Gaddi na Nyambuja wanamua kuvunja ndoa yao kama mwandishi anavyosema; “ Wiki moja baadaye Gaddi na Nyambuja waliachana kisheria….” [Uk. 68]



Gaddi Bullah na Dania

Gaddi Bullah anakuwa na mgogoro na Dania, chanzo cha mgogoro huu ni Dania kumkuta Gaddi Bullah akiwa amekaa na kujitau ofisini kwake na pia Gaddi kupewa cheo cha Dania, na kupelekea Dania kutokuwa mttifu kwa Gaddi na kuchelewesha kuandika ripoti jambo linalopelekea Gaddi kumwandikia barua kali ya onyo. Suluhisho la mgogoro huu nia hatua ya Gaddi kuamua kuichoma moto barua ya onyo na kumaliza tofauti zao kama mwandishi anavyosema; "...Hilo suala limeisha kama jinsi hizi barua zinavyomalizwa na huu moto! Tusahau kama lilitokea...tufanye kazi!" [Uk 94]



Mgogoro kati ya Gaddi Bullah na Jerry

Gaddi Bullah na Jerry wanajikuta wakiingia katika mgogoro, chanzo cha mgogoro huu ni Jerry kuingilia penzi la Gaddi Bullah na Dania na kufikia hatua ya kupigana kama mwandishi anavyosema; "Jerry alimtandika ngumi nzito ya taya....Gaddi Bullah alighadhibika. Alimsukuma Dania pembeni na kumkabili adui yake..." [Uk. 121] Suluhisho la mgogoro huu ni Gaddi Bullah kuamua kuondoka na kuachana na Dania. Rejea ukurasa wa 121-123.



Mgogoro kati ya Bi. Hanuna na Dania

Chanzo cha mgogoro huu ni Dania kumsaliti Gaddi Bullah na pia Dania kushirikiana na Jerry kumuweka rumande kama mwandishi anavyosema;"Hapo Jerry alikuja juu. Alipiga simu polisi na muda si mrefu Bi. Hanuna alikamatwa na kuwekwa rumande kwa kosa la shambulizi." [Uk. 127]



Suluhisho la mgogoro huu ni Gaddi Bullah kumuomba Bi. Hanuna amsamehe Dania kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika Gaddi Bullah; "Nakuomba...usimchukie Da...Dania dada...Usimchukie kabisa...si kosa lake." Bi. Hanuna naye anajibu kwa kusema; "Oh! Gaddi...sasa hata nikimchukia itabadilisha nini..." [Uk. 146]



Mgogoro kati ya Bi. Hanuna na Nunu

Chanzo cha mgogoro huu ni Bi. hanuna kukataa katakata kumwambia Nunu mahali alipo Gaddi Bullah, kama mwandhishi anavyosema akimtumia Bi. Hanuna; "Na kaniapiza kuwa nisithubutu hata siku moja kuwapeleka au kuwatajia mahala alipo...kwa sababu siwezi kuvunja kiapo changu na kumsaliti mdogo wangu pekee kwa ajili ya mahayawani kama nyinyi!" [Uk 31-32]



Sulihisho la mgogoro huu ni Nunu kuamua kmchukua kwa nguvu [kumteka] Bi. Hanuna na kumpeleka Bi. Hanuna mahali alipo Dania ili ajionee mwenyewe kwanini Dania anamuhitaji Gaddi Bullah. Rejea Nunu anapomwambibia Bi. Hanuna; "Na hii ndio sababu pekee iliyonifanya nikuchukue kwa nguvu na kukuleta hapa Bi. Hanuna...ili uje ujionee mwenyewe hali hii." [Uk. 55]



Gaddi Bullah rafiki yake

Mgogoro mwingine unaojitokeza katika riwaya hii ni mgogoro kati ya Gaddi Bullah na rafiki yake, chanzo cha mgogoro huu ni hatua ya rafiki yake huyo kumsaliti Gaddi kwa mkewe. Rejea mwandishi anaposema: "Baadaye aliamua kwenda kwa rafiki yake kumpasha habari habari juu ya masahibu yake. na huko alipata mshituko mkubwa. Mke wake mwenyewe ndiye aliyemfungulia mlango, tena akiwa khanga moja tu...ilhali rafiki yake akiwa amejitawanya kwenye sofa akiwa kidari wazi na kaptura tu!" [Uk. 66]



Suluhisho la mgogoro huu ni Gaddi kuamua kuondoka kwa dharau na kuwaacha wasaliti wake kama mwandishi anavyosema; "Alivuta funda kubwa la moshi kutoka kwenye ile sigara na kuwapulizia moshi ule kwa dharau. Kisha aligeuka na kuondoka bila ya kusema neno lolote zaidi!" [Uk. 68]



Mgogoro mwingine unaojitokeza ni mgogoro kati ya kikundi kimoja na kikundi kingine cha watu. Mgogoro huo ni;



Mgogoro kati ya familia ya Dania na familia ya Jerry.

Chanzo cha mgogoro huu ni Jerry kushindwa kutokea katika harusi yake na Dania. Rejea Mama Mlole anapomwambia Gaddi Bullah, "...Lakini Jerry hakupatikana. Ilikuwa kama vile Jerry ameyeyuka ghafla kutoka kwenye uso wa dunia...Uhasama mkubwa ukazuka baina ya familia zao." [Uk. 85]



Suluhisho la mgogoro huu ni Dania anajenga chuki na wanaume wote duniani, anajaribu kujiua na pia anaanza tabia ya ulevi wa kupindukia kama mwandishi anavyosema akimtumia muhuika Mama Mlole; "Na matokeo yake akajenga chuki na dunia na wanaume wote hapa duniani...Alianza kunywa pombe kali tena kwa wingi!" [Uk. 87]



UJUMBE / MAFUNZO

Ujumbe ni yale mafunzo ayapatayo msoamji wa kazi ya fasihi, kwa maana hiyo basi kile ambacho msomaji wa kazi za fasihi amejifunza kutoka na kusaoma kazi husika huo ndio ujumbe. Ujumbe unaojitokeza katika riwaya hii ni;



1. Kikulacho kinguoni mwako.

Huu ni ujumbe ama funzo tunalolipata baada ya kusoma riwaya hii, ujumbe huu tunaupata kupitia muhusika Gaddi Bullah na rafiki yake, Bullah anasalitiwa na rafiki yake  huyo kwa kuamua kuanza mahusiano ya kimapenzi na mke na kupelekea Bullah kuvunja ndoa kisa rafiki yake, ujumbr huu tunaupata kupitia muhusika Bullah anaposema, “Na wewe! Nilidhani kuwa u rafiki yangu! Nilikuwa nakuletea matatizo yangu kumbe ulikuwa ukinilamba kisogo?” [Uk 67]



2. Mapenzi ni kitovu cha uzembe kazini.

Huu pia ni ujumbe mwingine unaojitokeza katika riwaya hii, mwandishi anawatumia wahusika Gaddi Bullah na Dania ambao kutokana na matatizo yanayowasibu katika mapenzi tunawaona wakiathirika kisaikolojia na hatimae kupungukiwa ufanisi wa kazi, kwa mfano tunamwona Gaddi akipitisha malipo hewa kwa kukosa umakini na kusabibisha kushushwa cheo alikadharika Dania nae mapenzi yanamfanya ajitumbukize katika. ulevi uliokithiri na hivyo kusababisha kutokuwa makini ka0zini kama mwandishi anavyosema kupitia muhusika Mama Mlole, "Na hapa ndipo utendaji wake kazini ulipoathirika vibaya sana. Kazi zikawa haziendi kabisa." [Uk 88]



3. Ulevi wa kupindukia ni hatari kwa afya ya binadamu.

Ni ujumbe mwingine tunaoupata katika riwaya hii. Ili kufikisha ujumbe huu mwandishi ame watumia wahusika Dania ambaye kutokana na tabia yake ya ulevi wa pombe kali anajikuta akipata ugonjwa wa ini kama mwandishi anavyothibitisha akimtumia muhusika Dokta Virani anaposema, “Ini lake la kulia limeathirika kutokana na pombe kali alizokuwa akinywa, wakati wa mfadhaiko wake uliotokana na madhila aliyofanyiwa na Jerry.” [Uk 105]



Lakini pia tunaona kuwa ulevi uliokithiri wa uvutaji sigara unaofanya na Gaddi Bullah unamsababishia matatizo ya mapafu na hatimaye anafariki kwa ugonjwa wa mapafu ambao unatokana na uvutaji wa sigara uliokithiri.



4. Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli.

Ni ujumbe unaojitokea pia katika riwaya hii, mwandishi katika kufikisha ujumbe huu amewatumia wahusika Dania, Bullah, Nunu na Boaz. Kwa mfano richa ya Dania kumfanyia unyama Gaddi Bullah kwa kumsaliti lakini anakuja kumfaa wakati wa dhiki yaani wakati Dania anaumwa kwa kumfadhili ini kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika Dokta Virani; "Samahani sana Gaddi...imenibidi nifanye hivyo...nadhani Dania alipaswa ajue kuwa ni wewe ndiye uliyejitolea ini lako ili kuokoa maisha yake!" [UK. 144]



Lakini pia mwandishi amemtumia muhusika Nunu licha ya kumshauri Dania kwa nguvu zake zote asirudiane na Bullah na kutosikilizwa lakini baadaye anakuja kuhangaika kumtafuta Bullah kwa ajili ya Dania, lakini pia Dania alikuwa tayari kujitolea ini kwa ajili ya rafiki yake Dania ila tatizo lilikuwa ni damu kama mwandishi anavyosema, “Nunu naye alijitolea. Vipimo vilionesha kuwa maini yake yote yalikuwa safi na aliweza kabisa kumtolea Dania ini moja, lakini damu yake ilikuwa haioni kabisa na ile ya Dania." [Uk. 132]



Pia Boaz alishirikiana bega kwa bega na Nunu kumtafuta Gaddi Bullah kwa kila hali yote haya yanatupa ujumbe kuwa rafiki wa kweli ni yule akufaaye kwa dhiki na raha.



5. Majuto ni mjukuu.

Ujumbe huu unajitokeza pia katika riwaya hii, mwandishi anamtumia muhusika Dania ambaye kutokana na unyama aliomfanyia Gaddi Bullah na kutomsikiliza rafiki yake Nunu wakati akimhauri kuhusiana na Jerry baadaye anakuja kujuta kutokana na maswahibu yaliyomkuta kama mwandishi anavyosema,  “Nilimuona Jerry ni bora kuliko Gaddi nawe ukaniambia kuwa nilikuwa najidangajnya, sikukusikia. Sasa nimedhihirisha mwenyewe...hii ndio ile ya mkaidi hafaidi mpaka siku ya Iddi. Najuta..." [Uk 135]



6. Elimu ni ufunguo wa maisha.

Mwandishi anatupa ujumbe mwingine kuwa, ili mtu aweze kufanikiwa hana budi kushikiria na kuizingatia elimu kwani elimu ni ufunguo wa maisha, ujumbe huu katika riwaya hii unajitokeza kwa muhusika Gaddi Bullah ambaye kutokana na elimu aliyokuwa nayo anapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri, kama mwandishi anavyosema; “….kampuni ile kubwa ya mawasiliano nchini ambayo ilimwajiri mara baada ya kumaliza masomo yake ya elimu ya juu miaka mitano iliyopita.” [Uk 57]

Ujimbe huu pia unajitokeza mwandishi anapomtumia muhusika Mama Mlole anaposema; “ Mke anamtaka, lakini na masomo pia anayataka. Masomo ambayo yangemfungulia milango mipya ya maendeleo kielimu na kiuchumi.” [Uk 84]



7. Mpende akupendaye asiyekupenda achana nae.

Hussein Tuwa katika riwaya hii anaipa ujumbe jamii yake kuwa penda pale unapopendwa na si kumng'ang'ania tu mtu kwa kuwa moyo wako unataka tu kuwa naye, ujumbe huu tunaupata kupitia kwa muhusika Dania ambaye licha ya kufanyiwa vituko vya kila aina na Jerry yeye bado alimuona kuwa ni mtu wa maana na kuamua kumsaliti Gaddi Bullah mwanaume aliyempenda kwa dhati, lakini baadaye anakuja kung'amua kuwa Jerry hakuwa na mapenzi ya dhati, ujumbe huu unajidhihirisha Dania anaposema; “Nilimuona Jerry ni bora kuliko Gaddi nawe ukaniambia kuwa nilikuwa najidangajnya, sikukusikia. Sasa nimedhihirisha mwenyewe...hii ndio ile ya mkaidi hafaidi mpaka siku ya Iddi. Najuta..." [Uk 135]



8. Uongozi bora ni chachu ya maendeleo na maelewano sehemu za kazi.

Hili ni funzo tunalolipata mara baada ya kusoma riwaya hii, ili kuleta ufanisi wa kazi na maendelea ni wajibu wa viongozi kubadilika na siyo kuwasubiri wanaowaongoza wakosee ndipo wawape onyo kali au kuwafukuza, kama mwandishi anavyotuambia akimtumia muhusika Mama Mlole;"Utawala wa kusubiri mfanyakzi akosee ili umuadhibu siku hizi umepitwa na wakati, Gaddi! Utawala wa sasa ni wa kumjenga mfanyakazi kitabia na kimaadili ili asiingie kwenye makosa yatakayosababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Viongozi tunatakiwa tubadilike sasa, Gaddi!" [Uk 93]











Ø      Matumizi ya Lugha.

è    Misemo / Nahau

1.      Jibu lile lilimkata maini. [Uk 36]

2.      Pale walikuwa wamegonga mwamba. [Uk 33]

3.      Anakuhitaji wewe, radhi zako na kumtia moyo. [Uk. 35]

4.      Dania anamuhitaji.. ni suala la kufa na kupona. [Uk. 26]



·         Methali

ü      Ukiyastaajabu ya Musa utayaona ya Firauni. [Uk. 27]

ü      Hakuna marefu yasiyo na ncha. [Uk.117]

ü      Ni bora nusu shari kuliko shari kamili. [Uk. 127]

ü      Mkaidi hafaidi mpaka siku ya Idi. [Uk.135]

            Tamathari za semi

·         Takriri

Hii ni hali ya kurudiarudia maneno, neon, silabi au sauti zinazolingana katika kazi ya fasihi ili kusisitiza au kutia mkazo jambo fulani. Mfano wa takriri zinazojitokeza katika riwaya hii ni:

            Jjambo lililowafanya ndugu wa mumewe kumfukuza kama mbwa kutoka kwenye nyumba ya marehemu mumewe. [Uk. 60]

            Nimesema sitaki! Sitaki. Sitaki. Sitaki!

Ø       



·         Tashibiha.

Hii ni tamathari ambayo hulinganisha vitu kwa kutumia viunganishi kama, mfano wa, sawa na, mithili ya, kama vile. N.k. baadhi ya tashibiha zinazojitokeza katika riwaya hii ni:

ü      Midomo ilikuwa ikimtetemeka kama mgonjwa wa malaria kali. [Uk 18]

ü      Sasa hapo ilikuwa kama amechokoza nyuki. [Uk 30]



·         Tashititi.

Hii ni aina ya tamathari ya semi ambayo mtu huuliza swali huku jibu lake akilifahamu, mfano wa tashititi zinazojitokea katika riwaya hii ni:

·         Tashihisi.

Tamathari hii hufanya vitu ambavyo havina uhai wa kutenda jambo kama binadamu vitende au vifanye jambo hilo kama binadamu, mfano wa tashihisi zinazojitokeza katika riwaya hii ni:



·         Tanakali sauti [Onomotopeia] na Tanakali lafudhi.

Tanakali sauti [Onomotopeia]

Hii ni aina ya tamathari ambayo sauti ya kitu fulani huigwa ili kwa lengo la kuburudisha au kuipa dhamira uzito falani. Mfano wa tanakali sauti zilizotumika katika riwaya hii ni:



      Tanakali lafudhi.

    







·         Tafsida

Hii ni aina ya tamathari za semi ambazo hutumika ili kupunguza ukali wa maneno, mfano wa tasfida zilizotumika katika riwaya hii ni:



·         Sitiari

·         Mdokezo

           Matumizi ya Taswira.

5.                 Matumizi ya ucheshi.

Ø      Matumizi ya Lugha.



MANDHARI

Kwa kiasi kikubwa riwaya hii imetumia mandhari ya Dar-es-salaam, ambapo ndipo panatajwa kuwa ni makao makuu ya Kampuni ya mawasiliano ambayo Gaddi Bullah na Dania ndipo walipkuwa wakifanyia kazi. Rejea mwandishi anaposema; " Ni mwezi mmoja sasa ulikuwa umepita tangu ahamishwe kwenye ofisi hii iliyopo jijini Dar-es-salaam, ambayo ndiyo makao makuu ya kampuni ile kubwa ya mawasiliano nchini." [Uk. 57]



Katika Jiji hili la Dar-es-salaam pia kuna mandhari nyingine ndogondogo zinajitokeza kama vile Mbezi, Oysterbay, Magomeni, Sinza kwa Remmy, Tabata. n.k

Mbezi, mwandishi anaeleza kuwa ndipo mahali Gaddi Bullah alipojenga nyumba yake ya kifahari na kuiuza baada ya kupatwa na matatizo ya kusalitiwa na mpenzi wake. Rejea mwandishi anaposema; "Alikuwa na miradi iliyomuingizia pesa ya kutosha, ikiwemo nyumba nzuri na ya kifahari maeneo ya mbezi..." [Uk. 58]



Oysterbay, ni mandahri inayotajwa katika riwaya hii ambapo ndipo wanapoishi wa zazi wa Dania yaani Mzee Theobald na mkewe katika nyumba ya kifahari. [Rejea ukurasa 47-49]



Katika riwaya hii maneo ya Mbezi na Oysterbay ni mandhari ambayo mwandishi ameyatumia ili kuonyesha matabaka katika jamii yake kwa kuonesha sehemu na namna ambavyo watu wenye kipato cha juu wanaishi, na hivyo mandhari haya yote mwandishi ameyatumia kufikisha dhamira ya matabaka katika jamii.



Vilevile, Magomeni kumetajwa kama sehemu aliyokuwa akiishi Bi. Hanuna katika nyumba yao ya urithi, lakini pia Tabata imetumika kama sehemu anayoishi Dania katika nyumba aliyojengewa na baba yake, Sinza kwa Remmy ndipo alipokuwa anaishi Jerry katika nyumba ya kupanga.



Arusha pia ni mandhari nyingine inayojotekeza katika riwaya hii, Arusha ndipo alipokuwa akifanyia kazi Gaddi Bullah katika kampuni ya mawasiliano kabla ya kuamishiwa Dar-es-salaam, pia Arusha na huko ndipo Gaddi Bullah alipokutana na Nyambuja na kufunga ndoa kama mwandishi anavyosema; "...Pale mjini Arusha...ndipo Gaddi Bullah alipokutana na binti yule aliyekuwa na sura ya kuvutia, mwili wa kutamanisha na haiba iliyovuta hisia za mapenzi kwa kila rijali..." [Uk. 59]



Sehemu nyingine zinazotajwa katika riwaya hii ni, Mkuranga anakohamia Bi. Hanuna baada ya kuhama kule Magomeni kama mwandhishi anavyosema akimtumia muhusika Boaz; "Bi. Hanuna alijengewa nyumba nyingine na mdogo wake huko Mkuranga..."[Uk. 20]







Lakini pia mandhari ka Pemba imetumika pia ambako ndipo Gaddi Bullah alipokimbilia kujificha huko na ndipo anapofia.[Rejea ukurasa wa 140-148]



Mwandishi pia ametumia Marekani ambako Jerry anaenda kusoma baada ya kupata ufadhili wa shirika fulani, lakini pia inatajwa Afrika ya kusini ambako Dania alienda kutibiwa. [Uk. 83 na 88]



Mandhari nyine zilizotumika ni, nyumbani, ofisini, mgahawani, hospitalini. n.k

Nyumbani tukianzia na kule Arusha, mwandishi anaonyesha matatizo ya kifamilia nyumbani hususani katika ndoa kama tunavyoona kwa Nyambuja na mumewe. pia nyumbani kwa rafiki yake Gaddi Bullah tunaona Gaddi akimfumania mke wake na rafiki yake. [Rejea Uk. 60-68]



Nyumbani kwa Dania, tunaona akifumaniwa na Gaddi Bullah, na vilevile kupigana kwa Gaddi na Jerry.



0fisini, pia imetumika kama mandhari katika riwaya hii, mwandishi ametumia mandhari hii kuonesha wizi unaofanyika katika ofisi mbalimbali, rejea kupitishwa ka vocha ya malipo hewa huko ofisi za Arusha, migogoro kazini kama inavyojitokeza kwa Dania na Gaddi Bullah, lakini pia suala la uongozi bora kama tunavyoweza kuliona kwa Mama Mlole. [Rejea ukurasa wa 68, 71-74 na 93.]



MUUNDO. [Plot]

Muundo ni namna visa na matukio hufuatana kwa mtiririko. Hivyo tunaweza kusema pia muundo ni mfuatano wa masimulizi katika kazi ya fasihi. Katika riwaya hii mwandishi ametumia muundo changamani yaani visa na matukio katika riwaya hii ameanza kati, mwanzo halafu mwisho.



Kwamfano ameanza kati, ambapo tunamwona Nunu na Boaz wakiwa katika harakati za kumtafuta Gaddi Bullah huku msomaji akiwa bado kung'amua ni sababu gani ambayo inawafanya akina Nunu kumsaka Gaddi Bullah? [Angalia kuanzia ukurasa wa 1-56]



Baada ya kuanza na kisa cha katitikati, katika sura ya pili hadi ya tisa mwandishi anaanza kuelezea kisa cha mwanzo na kurudi tena katikati, hapa tunaelezwa habari za Gaddi Bullah na ndipo sababu za Gaddi kutafutwa kinaelezwa. Halafu anamalizia na kisa cha mwisho kujitolea ini kwa Gaddi na kufariki kwake.



Pia katika kuyapanga matukio yake katika riwaya hii, mwandishi ameigawa kazi yake katika sura/sehemu ambazo amezipa namba kuanzia sura/sehemu ya kwanza [1]  hadi kumi [10].



Sura ya 1. Nunu na Boazi wakimtafuta Gaddi Bullah bila mafanikio na hatimaye kumteka dada yake  [Bi. Hanuna] na kumpeleka hadi nyumbani kwa akina Dania. [Uk. 1-56]



Sura ya 2 hadi ya 8. Mwandishi anaanza mwanzo, hapa tunaona kukutana kwa Gaddi Bullah na Nyambuja na kuoana, Gaddi kusalitiwa na huyo mke wake, kuvunja ndoa yake, Kuamishiwa Dar-es-salaam, kukutana na Dania na kuanza uhusiano wa kimapenzi na kusalitiwa na Dania na hatimaye Gaddi Bullah kutoweka. [Uk 57-128]



Sura ya 9 hadi ya 10, Dania anaanza kuumwa ini, Dania anakimbiwa na Jerry kwa mara ya pili, Dania anaandika barua akimuomba Nunu aipeleke kwa Gaddi Bullah, Gaddi anajitolea ini kumfadhili Dania, Gaddi anaanza kuumwa, Dokta Virani anatoa siri juu ya mfadhiri wa Dania, Gaddi anafariki dunia na ndio mwisho wa riyawa hii. [Uk 129-148]



MTINDO [Setting]

Mtindo ni jinsi msanii anavyotumia ufundi, umahiri na hisia zake katika kutenda au kueleza jambo fulani. katika riyawa hii kuna mitindo mbalimbali ambayo mwandishi ameitumia ni kama vile;

Vipengele vya mtindo vilivyotumika katika riwaya hii.



Monolojia [Masimulizi]

Kwa kiasi kikubwa mwandishi ametumia lugha ya masimulizi katika kuelezea visa/matukio, sifa na tabia za wahusika katika kuikamilisha kazi yake.



Diolojia [Majibizano]

Mwandishi katika kazi yake hii ametumia pia lugha ya majibizano, mfano;

 Nunu:          "Aaah Bi. Hanuna, tusamehe...tusaidie tafadhali...ni muhimu sana kwangu

                     kuonana na Gaddi..."

Bi. Hanuna. "Sio juu yangu kutoa msamaha juu ya hilo Nunu! au unataka kuniomba

                       nimsaliti mdogo wangu? Eeenh?  [Uk. 32]



Matumizi ya Barua ndani ya riwaya.

Rejea barua aliyoandika Nyambuja kwa Gaddi anaposema:



     "Kwako Gaddi,

  Samahani sana kwa yote yaliyotokea, na pia kwa huu uamuzi nilioamua   kuchukua...Gaddi nimependana na mtu mwingine na nimekuwa nikisaliti ndoa yetu kwa  muda mrefu....Nakutakia maisha mema katika siku zako zilizobaki ukiwa mbali nami.

                          Kwa heri,

                          Aliyekupenda kwa dhati,

                           Nyambuja."  [Uk.65]



Matumizi ya nafsi.

Mwandishi ametumia nafsi zote tatu, nafsi ya kwanza, pili na tatu.





JINA NA JALADA LA KITABU

Tukianza na jina la kitabu, jina la kitabu ni Mfadhili, kwa mujibu wa Kamusi ya kiswahili Sanifu [1981] nenoMfadhili limefasiliwa kuwa ni, "Mtu anayemfanyia wema mkubwa mtu mwingine" Kwa maana hiyo basi, kwa kiasi kikubwa jina la kitabu linasadifu yale yanayozungumzwa katika riwaya hii. Kwa mfano tunaona baada ya Dania kuanza kuumwa na Daktari kuthibitisha kuwa ana tatizo la ini juhudi za kumtafuta mfadhili atakayejitolea ini lake lipandikizwe kwa Dania zinafanyika kama mwandishi anavyosema; "Hawakuwa na la kufanya zaidi ya kuanza kutangaza kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kuomba wasamaria wema watakaopenda kujitolea sehemu ya ini kumfadhili mgonjwa..." [Uk. 134]



Baada ya Juhudi zote kufanyika za kumtafuta mfadhili kufanyika hatimaye Mwandishi anaonesha kupatikana kwa mfadhili huyo, Mwandishi analithibitisha hili anaposema; "Nina taarifa njema muhimu kwetu sote...hatimaye mfadhili amepatikana!" [Uk 137]



Mwandhishi anamuonesha Gaddi Bullah kuwa ndiye aliyejitolea ini kumfadhili Dania na hivyo kuokoa uhai wa Dania, kama mwandishi anavyothibitisha akimtumia muhusika Dokta Virani anapomwambia Dania; "Gaddi Bullah ndiye mfadhiri wako Dania..." [Uk 140]



Vilevile jina la kitabu linasadifu yale yanayozungumzwa katika riwaya kwa sababu tunamwona Dania baada ya kupona anakuwa akijiuliza kila mara ni nani mfadhili wake? swali ambalo limekuwa likiusumbua moyo wa Dania, kama mwandishi anavyosema; "Ila sasa akili yake ikawa inajiuliza swali moja kila siku. Mfadhili wake ni nani?" [Uk 139]



Pia swala la ufadhili linajitokeza kwa Jerry amabaye anapata ufadhili wa kwenda kusoma Marekani, kama Mwandhishi anavyosema; "...Alikuwa amepata ufadhili wa shirika moja la kimataifa ambalo huwa linapokea maombi mengi sana ya ufadhili kuliko uwezo uliopo..." [Uk 83]



Pamoja na hayo kuna ufadhili mwingine unaofanywa na Dokta Virani kwa Bi. Hanuna, baada ya Bi. Hanuna kukamatwa na polisi na kuwekwa rumande ni Dokta Virani ndiye anayemfadhili kwa kumtoa kwa dhamana kama mwandhishi anavyosema; "Dokta Virani alipopata taarifa alihangaika huku na huko kumpatia dhamana, lakini ilishindikana." Mwandishi anaendelea kusema; "Siku iliyofuata, Dokta Vilani alifanikiwa kumtoa kwa dhamana." [Uk 127]



Ufadhili unaofanywa na Mama Mlole kwa Dania na Gaddi Bullah, licha ya kuwa Dania na Gaddi Bullah kuwa na matatizo ambayo yangeweza kuwafukuzisha kazi, Mama Mlole anafanya juhudi kubwa kushawishi uongozi wa kampuni ili waweze kuendelea na kazi kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika Mama Mlole anaposema; "Ndio...na kwa hatua aliyofikia, ilibidi aachishwe kazi, lakini kwa kumsaidia, nikiwa kama Afisa Utumishi wa kampuni, nilipendekeza apewe likizo....nilifanya kazi ya ziada kuushawishi uongo wa kampuni juu ya hili, jinsi nilivyofanya kazi ya ziada kulishawishi lile jopo la wakaguzi kule Arusha kukupa wewe nafasi nyingine...badala ya kukufaukuza kazi..."   [Uk 88]



Hivyo basi kwa ushahidi huo tunaweza kusema jina la kitabu linasadifu yale yote yanayozungumzwa katika riwaya hii.



FALSAFA YA MWANDISHI.

Mwandishi anaami kuwa katika mapenzi kuna pande mbili, pande hizo ni utamu na uchungu au tunaweza kusema raha na karaha, mara nyingi mapenzi yanapoanza huwa moto moto na yenye furaha kubwa na upendo lakini pindi yanapoanza kupatwa na majaribu ya aina mbalimbali mapenzi hayo hubadilika na kuwa karaha [chungu].



MTAZAMO WA MWANDISHI.

Mwandishi ana mtazamo wa kimapinduzi kwa maana anaihitaji jamii yake kubadilika, ameonesha matatizo mbalimbali katika jamii yake kama vile usaliti, ulevi wa kupindukia,  unafiki, uongozi mbaya, mapenzi ya ulaghai. n.k. ambayo anaitaka jamii yake kubadilika na kuachana nayo.



TATHIMINI

Baada ya kusoma na kuhikiki riwaya hii, kama Mhakiki, inanilazimu kufanya tathimini japo kwa ufupi, katika tathimini nitaelezea mwandishi amefaulu katika mambo gani na wap kuna upungufu katika kazi yake ili iwe msaada kwake na kwa Waandishi wengine mara wasomapo tahikiki hii. Tukianza na:



KUFAULU KWA MWANDISHI.

Tunapoangalia kufaulu kwa mwandishi uwa tunaangalia kufaulu kwa mwandishi katika vipengele vya fani na maudhui, kifani mwandishi amefaulu katika vipengele vifuatavyo, kwanza amefaulu kutumia lugha ambayo ni rahisi na inayoeleweka na watu wengi na hivyo kufanya wasomaji wa riwaya hii kuielewa vizuri na kupata dhamira na ujumbe kwa urahisi kabisa.



Pia mwandishi amefaulu kuwajenga wahusika wake vizuri na kuwatumia wahusika hao katika kufikisha dhamira na ujumbe aliokusudia kwa hadhira yake.

Kwa upande wa mandhari mwandishi pia ameweza amefaulu kutumia mandhari halisi ambazo kwa namna moja ama nyingine mandhari hayo yamesaidia kujenga dhamira mbalimbali zinazojitokeza katika riwaya hii.



Mwandishi amefaulu katika kuyapanga matukio na visa katika mtindo unaomvutia msomaji kuendelea kukisoma kitabu bila kuchoka kwa namna ambavyo matukio yamesukwa na kupangwa vizuri.



Jina la kitabu ni kipengele kingine ambacho mwandishi amefaulu kwani jina la kitabu limeweza kusadifu yale yote yanayozungumzwa katika riwaya hii.



Katika kipengele cha maudhui mwandishi amefaulu kuonesha matatizo mbalimbali yanayoisibu jamii yake na kuenesha njia namna ya kuyamaliza matatizo hayo, matatizo ambayo mwandishi amejaribu kuyaibua ni kama vile usaliti, ulevi, unafiki. n.k. Vilevile tunaona mwandishi amefaulu kuonesha namna migogoro inayoweza kutokea na jinsi migogoro hiyo inavyoweza kutatuliwa kwa kutuo suluhisho kwa mgogo husika.



MAPUNGUFU

Kitu chochote kizuri huwa hakikosi kasoro au mapungufu, hivyo hata riwaya hii pamoja na uzuri wake lakini ina mapungufu yake pia, tukianza na mapungufu hayo, kwa mafano mwandishi ameshindwa kuonesha hatima ya Nyambuja na rafiki yake Bullah walivyofumaniwa kama waliamua kuendelea na uhusiano au ulikoma palepale na hivyo kupelekea jamii kuona kuwa wakati mwingine usaliti ni kitu kizuri katika jamii maana ingekuwa vizuri kama angeonesha madhara au matatizo ya usaliti huo kwao.



Pili, mwandishi pia ameshindwa kuonesha je! Baada ya Jerry kutoweka kwa mara ya pili na Dania kupona na Gaddi kufariki dunia je! alirejea tena na kama hakurejea je! huko alikokwenda yuko salama, kwa hiyo hapa pia mwandishi alitakiwa kuonesha madhara ambayo Jerry anakumbana nayo ili watu wenye tabia kama ya Jerry wajifunze kuwa tabia hiyo siyo nzuri hata kidogo.



MAONI YA MHAKIKI

Hii ni riwaya ya aina yake inayohusu mapenzi na masahibu yanayowapata wapenzi, imejaribu kuelezea kuelezea matatizo mbalimbali kwa wanandoa na hata matatizo kwa  mapenzi ambao hawajaingia kwenye ndoa, ni riwaya nzuri ambayo inafaa kusomwa na mtu yoyote yule na ikaeleweka vema. Matukio na visa vyake vimepangiliwa vizuri kiasi kwamba unapoanza kusoma riwaya hii hutaiweka chini au kuruka kurasa ni riwaya unayotakiwa kuisoma kama hujaisoma.



Mwandishi ni Mwalimu Shule ya Sekondari Mwanzi-Manyoni (Singida) anapatikana kwa namba zifuatazo:
Mawasiliano: 0715 33 55 58 (whatsapp)
                       0755 44 06 99
Nifollow instagram: fullraha17
Facebook: Furaha Venance













No comments:

Post a Comment