Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Saturday, June 2, 2012

Mfadhili Uamsho Zanzibar mbaroni

Mfadhili Uamsho Zanzibar mbaroni  
  Jumamosi 02 Juni 2012
 
Na Salma Said, Zanzibar

KIONGOZI Mkuu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) ambaye pia anadaiwa kuwa mfadhili wa kundi hilo, Sheikh Azzan Khalid Hamdan amewasili jana jioni katika kiwanja cha ndege cha Zanzibar kutoka nchini Oman alipokwenda kwa ajili ya matibabu, kisha kukamatwa na polisi.

Sheikh Azzan ni miongoni mwa viongoni waliokuwa wakisakwa na polisi akihusishwa na vurugu zilizotokea wiki iliyopita ikiwa pamoja na kufanya maandamano bila kibali.

Baada ya kuwasili katika kiwanja cha ndege, Sheikh Azzan alikwenda moja kwa moja Kituo cha Polisi cha Mfenesini kujisalimisha na kutoa taarifa kuhusu kuvunjwa kwa milango ya nyumba yake wakati akiwa safarini.
Kukamatwa kwake kumekuja siku moja tangu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ally Mohamed Shein atoe ahadi ya wahusikawa vurugu hizo kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.

Sheikh Azzan alisema hakutoa taarifa za ujio wake huo kutokana na kuogopa mkusanyiko usio rasmi ambao ungeweza kusababisha kutokea vurugu nyingine visiwani humo.
“Unajua hamasa za watu ni kubwa hasa vijana wangekuwa wamepata taarifa za kuja kwangu basi wangejaa hapa uwanja wa ndege na jambo hilo lingeweza kuhatarisha shughuli za uwanja huu ndio maana nikaamua kuja kimya kimya,” alisema Sheikh Azzan muda mfupi baada ya kushuka katika ndege ya Shirika la ndege la Oman Air.

Wakati Sheikh huyo akiwa safarini Oman, Zanzibar kulitokea maandamano ambayo yaliandaliwa na viongozi wa jumuiya yake yalioanzia Viwanja vya Shule ya Lumumba kupitia barabara ya Kinazini, Michenzani, Biziredi na kuishia katika viwanja hivyo vya Lumumba, kisha kufanyika mhadhara mkubwa uliozungumzia suala la mfumo wa elimu na matokeo mabovu ya mitihani Zanzibar.

Hata hivyo, maandamano hayo yalibandikwa jina la matembezi ya amani yalikwisha salama na waandamanaji wakarudi majumbani, lakini baada ya muda, kulizuka ghasia muda mfupi baada ya kiongozi na mhadhiri wa Jumuiya ya Uamsho, Sheikh Mussa Juma kukamatwa na polisi kwa ajili ya mahojiano.

Kiongozi huyo alipelekwa katika Kituo cha Polisi Madema Mjini Zanzibar na kusababisha mamia ya vijana kufika katika kituo hicho wakitaka aachiwe, na waliapa kutoondoka kituoni hapo hadi asubuhi, kitendo ambacho kiliwalazimisha polisi kurusha mabomu ya machozi usiku kucha na vurugu hizo kuendelea hadi siku ya pili.

Jeshi la polisi bado linawatafuta viongozi wengine wa jumuiya hiyo walioandaa maandamano hayo akiwamo Katibu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Abdallah Said Madawa, Sheikh Fikirini Majaaliwa Fikirini, Sheikh Suleiman Juma, na Sheikh Sadifa Haji Sadifa.
Katika vurugu hizo makanisa matatu yalichomwa moto na mali kadhaa kuteketea ikiwamo magari na nyumba za watu.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi 02 Juni 2012

No comments:

Post a Comment