Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Sunday, May 25, 2014

NADHARIA YA FASIHI


                                    

                                                            NADHARIA YA FASIHI

Na: Mwl. Venance F.

                                                 Fasihi ni nini?
Wapo wataalamu mbalimbali ambao wamekuwa na dhana tofauti tofauti kuhusu maana ya istilahi fasihi na wamejaribu kutoa maana mbalimbali, hivyo basi katika sehemu hii tutaangalia baadhi ya maelezo yaliyotolewa na baadhi ya wataalamu wa fasihi kufasili maana ya fasihi:

Ø  Fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha kuwasilisha ujumbe kwa hadhira au jamii iliyokusudiwa.

Ø  Tigiti Sengo na Kiango wanasema, Fasihi ni mwamvuli wa mtu na jamii na utu na maisha wa hadhi na taadhima.

Ø  Fasihi ni kielelezo cha hisia za mwandishi juu ya mambo yanayomwathiri yeye, kikundi au jamii nzima anamoishi na kwamba lengo lake kustarehesha au kufunza wasomaji wake. Fasili hii pia haikidhi maana halisi ya fasihi, je! Kielelezo hicho cha hisia za mwandishi huwasilishwa kwa kutumia nini?

Ø  Fasihi ni maandishi yanayohusu nchi au bara fulani, maandishi hayo sharti yawe ya kubuni. Ukiangalia fasili hii ina upungufu kwani fasihi si lazima yawe maandishi inaweza kuwa ni masimulizi, na si lazima yahusu nchi ama bara fulani, hivyo fasili hii inapotosha ukweli kuhusu fasihi.

Ø  Fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha kuwasilisha ujumbe au fikra za fanani.

Ø  Fasihi ni kitu chochote kilicho kwenye maandishi. Hii fasili ina mapungufu sana, kwani fasihi si lazima yawe maandishi, masimulizi pia yanaweza kuwa ni fasihi, lakini piasi chochote kilichokwenye maandishi ni fasihi kwani fasihi ni lazima kuwa matumizi ya lugha ya kisanaa.

Ø  Fasihi ni sanaa inayoakisi maisha ya jamii.

Ø  Fasihi ni chombo cha utetezi wa maslahi ya tabaka moja au jingine na kwamba mwandishi ni mtumishi wake anayejua au asiyejua, atake asitake mwandishi huyo huwa na lengo au dahamira fulani anayotaka kuionesha,wasomaji wanaweza kuikubali au kuikataa nap engine kutokana na fani, itikadi ya siasa inayotawala au jinsi mwandishi anavyoainisha.

Ø  Fasihi ni sanaa ambayo hutumia lugha teule katika kubuni tungo mbalimbali ambapo lugha hiyo teule yapaswa iwe na ufundi, mvuto wenye kusisimua ili kuwasilisha fikra zilizoko kwenye akili ya binadamu, tungo hizo zaweza kuwa hadithi, ushairi, semi, sanaa za maonesho nakadhalika.


Hivyo basi ukiangalia fasili hizo, sio zote zinazojitosheleza kutoa maana ya fasihi, ingawa fasili nyingine zinajitosheleza, lakini kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, fasihi ni kazi ya sanaa unayotumia lugha mahususi yenye mvuto, mguso wa kusisimua ili kuwasilisha ujumbe, fikra au mawazo ya fanani kwa hadhira aliyoikusudia, fikra au mawazo hayo sharti yawe ya kubuni.

Sanaa imefasiliwa kuwa ni kazi ya mikono na/au akili ya mtu, nayo aghalabu ina umbo dhahiri lenye maana kamili.[Mbunda M.:1992]

Sanaa pia, imefasiliwa kuwa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifiwa, umbo ambalo mtu hutumia katika kuelezaea hisi zinazomgusa au kutoa kielelezo chenye maana maalumu.

Tazama kielelezo Na. 1: Mchoro wa Sanaa na Matawi yake.

     SANAA
USUKAJI
MUZIKI
UWINDAJI
MAONESHO
UWINDAJI
USUSI
FASIHI
UFINYANZI
UTARIZIiiI
UCHONGAJI
 













                                                            
                                                     Mwanzo wa Fasihi
Wanafasihi mbalimbali wa ndani na nje wametoa mawazo yao kuhusu chimbuko/mwanzo wa fasihi, kutokana na mawazo hayo ya wanafasihi kuhusu mwanzo wa fasihi, tunapata mitazamo/nadharia ya namna mbili {2} ambayo ni:

                                                 [i] Mtazamo wa Kidhanifu
                                                 [ii] Mtazamo wa Kiyakinifu

Labda swali la kujiuliza, kwanini, mitazamo hiyo inaitwa, mtazamo wa kidhanifu na kiyakinifu? Jibu ni kwamba watetezi wa mitazamo hiyo hutumia hoja mbalimbali kuthibitisha chanzo au mwanzo wa fasihi, wapo wanaotumia hoja ambazo ni vigumu kuthibika na hivyo kuwa ni hoja zinazotokana na dhana ya kufikirika na ndio maana tunasema mtazamo wa kidhanifu maana hoja zao huwa ni dhana tu. Wakati pia wapo wanaotumia hoja ambazo zinathibitika kisayansi na ndio maana tunasema kuwa ni mtazamo wa kiyakinifu, hivyo basi katika sehemu hii tutajadili mitazamo hiyo kulingana na wataalamu mbalimbali wa fasihi, tukianza na:

[i] Mtazamo wa Kidhanifu
Kama tulivyoweza kuona hapo juu, watetezi wa mtazamo huu, hutoa hoja ambazo ni vigumu kuthibika kisayansi na hivyo kuonekana kama ni dhana tu za kufikirika na ndio maana ukaitwa mtazamo wa kidhanifu. Huu ni mtazamo mkongwe sana kwani ulikuwepo hata kabla ya kuzaliwa Kristo Watetezi wa mtazamo huu wanasema kuwa, fasihi ni zao au kazi ya Mungu na binadamu huiga kazi hiyo kutoka kwa Mungu ambaye ndiye chanzo cha sanaa zote duniani, watetezi wa mtazamo huu wanaamini kuwa sanaa na fasihi kwa ujumla zilitoka kwa Mungu na mwandamu huipokea sanaa hiyo ikiwa imepikwa na kuivishwa na Mungu na hadhira huipokea sanaa/fasihi hiyo ikiwa imechujuka mara tatu [3] yaani inatoka kwa Mungu, inamfikia fanani na fanani huiwasilisha kwa hadhira.

Tazama kielelezo Na. 2 

MUNGU
  MSANII
HADHIRAHIRA HADHIRA
       
                                          


Wayunani na Wagiriki wa kale huko Ulaya walikuwa na miungu ya ushairi na muziki waliowaita Muse ambao walikuwa wakiwaamini kuwa ndio waliokuwa wakiwapa wasanii/watunzi msukumo wa kiroho, kinafsi na kijazba wa kutunga kazi za fasihi, watetezi wa mtazamo huu wanaamini kuwa Mungu ndiye msanii mkuu na na hivyo uwezo wa binadamu kubuni kapewa na Mungu.
      
Mfano wa watetezi wa mtazo huu ni pamoja na Socrates, Plato na Alistotle, hawa ni wanafalsafa wa mwanzo kabisa wa Kigiriki na Kirumi ambao wanaamini kuwa chanzo cha sanaa na fasihi ni Mungu na humfikia mtumiaji ikiwa imechujuka mara tatu kama tulivyoona hapo juu.

Kwa upande wa wataalamu wa fasihi ya kiswahili pia wapo baadhi ya wataalamu wanaokubaliana na akina Plato kuwa chanzo cha sanaa na fasihi ni Mungu, na mfano wa wataalamu hao ni kama vile; F. Nkwera na John Ramadhani, mathalani F.Nkwera katika kuunga mkono mtazamo huu anasema, “…fasihi ni sanaa ambayo huanzia kwa Muumba na hunfikia mtu katika vipengele mbalimbali…” anaendelea kusema kuwa, “Fasihi ni hekima ambayo mtu ameshirikishwa apate kumtambua Muumba wake.”
Hapa anachotuambia Nkwera ni kuwa fasihi huanzia kwa Mungu hivyo chanzo cha fasihi kwa mujibu wa maelezo yake ni Mungu.

Naye John Ramadhani anasisitiza kwa kusema kuwa, “.Zaidi ya kwamba fasihi ni hisi, vilevile kitendo cha mtu cha kubuni kazi ya sanaa ni uigaji wa Mungu ambaye ndiye mfalme wa sanaa zote.”

Vilevile wapo wataalamu wengine wanaounga mkono mtazamo huu, wanaamini kuwa matengenezo ya sanaa huonekana kama kazi ya kiungu yenye kumuiga Mungu ambaye wanaamini kuwa ndiye Msanii wa kwanza kabisa.

Kiufupi F.Nkwera na John Ramadhani wanaami kuwa Mungu ndiye muumba wa fasihi, fasihi hutoka kwa Mungu na kumfikia mtu kwa njia mbalimbali na njia ya mwisho ni darasani.

Hivyo basi ukiangalia hoja zinazotolewa na watetezi wa nadharia hii ni za kidhanifu mno, ni hoja ambazo za kufikirika tu na ambazo haziwezi kuthibitishwa kisayansi kama ni kweli au la! Ni hoja zenye udhaifu mkubwa zinazochanganya taaluma na imani.

Udhaifu wa Mtazamo huu
Ø  Wtaalamu wote wa fasihi wanakubaliana kuwa fasihi ni mwigo, sasa kama fasihi ni mwigo kama fasihi ni huigwa kutoka kwa Mungu, je! Mungu yeye huiga kutoka kwa nani?
Ø  Mungu ni mwenye upendo, na kama Mungu ni mwenye upendo kwanini wengine awapendelee wengine kwa kuwapa hekima ili wapate kumtambua yeye?
Ø  Huu ni mtazamo wa kibinafsi kwani humuweka msanii au fanani kuwa karibu sana na Mungu kuliko watu wengine
Ø  Mtazamo huu pia hukuza hali ya utabaka kati ya msanii/fanani na hadhira yake kwa kujiona kuwa yeye ni bora sana kuliko hadhira yake kwa kuwa amepewa hekima na Mungu.
Ø  Nadharia hii inachanganya taaluma na imani zaidi jambo ambalo halikubariki kabisa katika taaluma na hivyo kuonekana kuwa hoja za mtazamo huu kutokuwa na mashiko zaidi.

Mtazamo wa Kiyakinifu
Fasihi ni sanaa ya lugha. Je! Kama fasihi ni sanaa ya lugha, lugha ilianzaje?
Wanasayansi wenye mtazamo wa kiyakinifu wanaona kuwa chimbuko la lugha linatokana na utumiaji wa dhana za kazi, wanaeleza kuwa, viumbe yaani sokwe walipoanza kubadilika na kuwa watu wakaanza kuwa viumbe wenye hisi, walitoa milio ya uchungu, ya furaha, hasira, tahadhari pamoja na kuonesha hisi hizo walikuwa wanaonesha ishara zao kwa kutumia viungo vyao vya mwili.

Viumbe hawa baada ya kushuka chini na kuanza kusimama wima kwa miguu miwili walianza kutengeneza na kutumia zana kwa mikono yao kwa kushirikiana [kumbuka haya yalikuwa ni mambo ya taratibu na yalichukua muda] kwa maana hiyo ili shughuli za kazi za kijima ziweze kufanikiwa palihitajika chombo cha mawasiliano thabiti, hivyo basi baada ya muda kupita binadamu akaanza kusema na maneno hayo yalikuwa yakiiga sauti za zana katika kufanya kazi {mwigo wa zana za kazi}

Hivyo basi lugha ilizuka katika mazingira hayo ya shuguli za kufanya kazi, na kwa kuwa lugha ni chombo muhimu cha fasihi na ndivyo fasihi ilivyozuka kwa namna hiyo na ushaiti ndiyo fasihi ya mwanzo kabisa.

Hivyo basi kutokana na ushahidi huo, watetezi wa nadharia hii hudai kuwa “Binadamu ndiye alfa na omega wa fasihi”

Baadhi ya wataalamu wa fasihi ambao kwa namna moja ama nyingine hukubaliana na mawazo hayo kuwa binadamu ndiye chanzo cha fasihi, ni kama vile:


1.      Richard, yeye anasema kuwa, Sanaa [ushairi/fasihi] inatokana na mambo makuu manne [4] ambayo ni;
                               {i} Upweke wa binadamu
                               {ii} Ujinga wa binadamu
                               {iii} Nafasi ya binadamu katika upana na wakati
                               {iv} Ukweli kuhusu kifo na kuzaliwa

Hii ina maana kuwa, upweke wa binadamu ulimfanya aanze kutafuta kitu kitakachomuondolea upweke katika mazingira aliyokuwa akiishi na hapo ndipo fasihi ikaziliwa ili kuwa chombo cha kumburudisha binadamu na kumuondolea upweke. Na ujinga wa binadamu unatokana na kuwa kipindi hicho cha ujima hakukuwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia yaani zilikuwa zama za ujinga, kwa maana hiyo zana za kufanyia kazi kipindi hiko zilizobuniwa na binadamu zilikuwa duni mno na hivyo kuanza kutafuta nyenzo itakayomsaidia binadamu kufanya kazi na kuzalisha zaidi na hapo ndipo fasihi ikazaliwa ili kumchochea binadamu kufanya kazi na ndio maana inasemekana kuwa wimbo wa kazi ndio fasihi ya mwanzo kabisa. Pamoja na nafasi ya binadamu katika upana na wakati na ukweli kuhusu kifo na kuzaliwa ndizo shughuli zilizomfikirisha binadamu mpaka akabuni sanaa/fasihi.

2.      Senkoro F.M naye katika kitabu chake cha Fasihi na Jamii katika kuunga mkono mtazamo huu, anasema, binadamu ndiye alfa na omega wa fasihi, na anaendelea kusema kuwa, katika kipindi cha ujima, binadamu alianza kutumia zana kama mawe na mifupa kutumia kama silaha na kufanyia kazi, hisia za kisanaa zilianza kutumika katika kutekeleza kazi kwa nyenzo bora zaidi, wimbo wa kazi ndiyo fasihi ya mwanzo kabisa na ushairi wa mwanzo ulifungamana na nyimbo na ulitungwa kwa kufuata mapigo ya zana za kazi, chanzo cha sanaa ni kazi.

3.      Kezilahabi E. naye anasema, kila binadamu ana uwezo wa kuumba fasihi. Katika kuipa uzito hoja yake, Kezilahabi anatoa mfano wa motto anapozaliwa na kulia kuwa hiyo ndiyo dalili ya fasihi yake ya mwanzo kabisa, yaani shairi lake la kwanza kutunga.

Hizo ndiyo hoja ambazo, wataalamu wengi wa fasihi wanakubaliana nazo kuwa chanzo cha fasihi ni binadamu mwenyewe kuonekana kuwa na mashiko zaidi kuliko ule mtazamo wa kidhanifu  .

Dhima za mtunzi wa kazi za fasihi
  1. Mtunzi wa kazi za fasihi ana dhima ya kuelimisha jamii yake, hii inatokana na ukweli kuwa, katika kazi za fasihi huwa na maudhui mbalimbali ambayo kwayo hadhira huweza kuelimika. Mathalani katika wimbo wa starehe uliotungwa na kuimbwa na msanii Ferouz unaielimisha jamii kuhusiana na ngono zembe kuwa mwisho wake ni kuambukizwa virusi vya ukimwi, na katika riyaya ya Pesa zako Zinanuka iliyoandikwa na Ben Mtobwa anaielimisha jamii juu ya athari ya ufisadi na uhujumu uchumi. Pia zipo kazi nyingine za watunzi wa kazi za fasihi zinazoelimisha juu ya matumizi sahihi ya vyandarua, umuhimu wa kupiga kura n.k

  1. Mtunzi wa kazi za fasihi pia ana dhima ya kuiburudisha jamii yake, hii ina maana kuwa jamii inapokuwa imechoka kutokana na shughuli za uzalishaji mali uhitaji kupumzika na hivyo kazi ya mtunzi wa kazi za fasihi ni kuiburudisha jamii yake, mfano kupitia nyimbo mbalimbali, vichekesho, mathalani vichekesho vinacyooneshwa katika luninga kama vile TBC {Original Comedy}, EATV {The Comedy} na Star tv {Futuhi} huwa na dhima kubwa ya kuiburudisha jamii kwa kiasi kikubwa kwa njia ya kuchekesha lakini wakati huo huo wakitoa elimu.

  1. Dhima nyingine ya mtunzi wa kazi za fasihi ni kuikosoa jamii yake pindi anapogundua kuna maovu yanafanyika katika jamii yake, kwa mfano msanii Mrisho Mpoto kupitia kazi zake amekuwa akiikosoa serikali na jamii kwa ujumla, rejea nyimbo zake za Nikipata Nauli, Asanteni kwa kuja na Adera ambapo katika wimbo wa Nikipata nauli anakosoa urasimu uliopo serikalini, ufisadi na kukumbatia viongozi wasiowaadirifu. Vilevile mwandishi E. Kezilahabi katika tamthiliya yake ya Kaptura la Marx anaikosoa serikali na jamii yake kwa ujumla kukumbatia sera za kigeni pasina kuzifanyia utafiti na matokeo yake kushindwa kuendelea mbele.

  1. Kutia hamasa au kuhamasisha jamii, ni dhima nyingine ya mtunzi wa kazi za fasihi, mtunzi ana dhima ya kuihamasisha jamii kuacha au kufanya jambo fulani kupitia kazi zao, mathalani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 vikundi mbalimbali vya sanaa vilitunga nyimbo zenye lengo la kuhamasisha jamii kukichagua chama fulani na mgombe wake. Kwa mfano kulikuwa na wimbo unaoitwa Anaweza Dr.Slaa uliokuwa ukiwahamasisha wananchi kumchagua Dr. Wilbroad Slaa kuwa Rais lakini pia kulikuwa na wimbo wa Anafaa ulioimbwa na TMK Family uliokuwa ukiwahamasisha wananchi kumchagua Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.

  1. Dhima nyingine ya mtunzi wa kazi za fasihi ni kuionya jamii yake. Kwa mfano msanii 20% katika wimbo wake wa Tamaa mbaya, anaionya jamii yake kuchunga tamaa kwani ni mbaya, lakini pia msanii Profesa J katika wimbo wake wa Bongo Dar es salaam anaionya jamii yake kuwa makini na mji wa Dar-es-salaam kwani umejaa kila aina ya utapeli.

  1. Mtunzi wa kazi zafasihi ana dhima ya kueleza na kuikumbusha jamii historia ya jamii. Mtunzi wa kazi za fasihi wakati mwingine anakuwa na dhima ya kuelezea na kuikumbusha jamii yake ni wapi imetoka, kwa mfano tamthiliya ya Mkwava wa Uhehe kilichoandikwa na M.M. Mulokozi mtunzi anaelezea historia ya Chifu Mkwawa wa Wahehe na mapambano yao dhidi ya uvamizi wa Wajerumani, pia kuna kitabu cha Kinjeketile kilichoandikwa na Hussein kinachoelezea vita vya maji maji.

  1. Mtunzi wa kazi za kifasihi pia ana dhima ya kukuza lugha, hii ina maana kuwa msanii anapoamua kuteua lugha ili kuweza kuwasilisha mawazo au ujumbe wake kwa hadhira hujikuta akiibua msamiati mpya ambao huweza kutumika kama misimu na pindi inapopata mashiko kimatumizi husanifishwa na kuwa msamiati sanifu na hivyo kuchangia lugha kukua kimsamiati, lakini pia kazi zao kusomwa au kusikilizwa na watu wengi pia huchangia lugha kusambaa na kuenea sehemu mbalimbali na kuvuka mipaka kimatumizi.
                                 
Mawasiliano: 0715 33 55 58 (whatsapp)
                       0755 44 06 99
Nifollow instagram: fullraha17
Facebook: Furaha Venance

No comments:

Post a Comment