Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Wednesday, May 14, 2014

MTATIRO AMPA MAKAVU KITILA MKUMBO, ADAI, UKAWA HAINA NIA YA KUVUNJA MUUNGANO



Mwalimu Kitila Mkumbo, UKAWA inapigania na kutetea misingi mikuu ya maoni ya wananchi iliyomo katika rasimu ya katiba. Kabla hatujaenda bungeni hakukuwa na UKAWA, UKAWA ilikuja haraka sana baada ya kuona mbinu chafu za CCM kuzuia maoni halali ya wananchi. Mtikila tunafanya naye kazi kwa sababu pia ameunga mkono kutetea maoni ya wananchi. Kwa kweli kinachotuunganisha sote hivi ss ni kutetea maoni ya wananchi.

Hoja ya nia ya UKAWA kuvunja muungano si kweli, nimeshasema hapo juu kuwa tunataka maoni ya wananchi yaheshimiwa, na wananchi walisema muungano lazima uwepo, wakasema uwe wa serikali tatu. Thats all. Ajenda yetu kuu kwa sasa n kutetea mamlaka, matakwa na maoni ya wananchi. Katika kushirikiana kuwatetea wananchi mambo kadhaa yamejitokeza na nitayataja.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya demokrasia ya vyama vingi Tanzania, viongozi wakuu wa vyama ambao kuna wakati walijiona kama maadui wamepata fursa ya kufanya kazi kwa karibu sana na pamoja, wamejenga njia ya kuanza kuaminiana na kujihakikishia kumbe wanaweza kufanya kazi pamoja. Na hili kwangu mimi ni jambo jema sana. Leo Lipumba, Mbowe, Mbatia na wengine wanaalikaba hadi majumbani na kujadili mwelekeo wa nchi yetu, leo viongozi wamekuwa karibu sana. Mimi naliona kama jambo la heri mno.

Pia, viongozi wameendelea na nia ya kushirikiana katika masuala ya bunge(limefanyika) na wana mipango vyama vishirikiane baadaye hata katika masuala ya uchaguzi(HILI PIA NI TAKWA LA WANANCHI). Mie kama kijana naona siku za usoni panaweza kuwa na ushindani mkubwa zaidi wa kisiasa ikiwa vyama na wadau muhimu watafanya kazi pamoja.

Tuachane na huko, turudi kwenye suala la UKAWA kutaka kuvunja muungano.
Mwalimu wangu, hivi majuzi wewe na wenzio wachache mlikuwa mkipigania mabadiliko makubwa ya kidemokrasia ndani ya CHADEMA, na mlidhani kuwa wanaCHADEMA wengi wangetaka mabadiliko ikiwa yatafanywa kidemokrasia ndani ya chama chao. Je kwa akili za harakaharaka na nyie mlikuwa na lengo la KUIUA na KUIVUNJAVUNJA Chadema? Ikiwa unaamini kuwa UKAWA kupigania maoni ya wananchi yaheshimiwe ni kuvunja muungano, Je unaamini pia wewe na Zitto Kabwe kupigania demokrasia ndani ya CHADEMA ilikuwa ni KUIVUNJA Chadema? Tusipotoshe umma katika masuala ambayo yako wazi. Ndiyo maana mlipotofautiana ndani ya CHADEMA sisi wengine tulijua mna madai ya msingi mno. Hatukutoka hadharani kuja kuwashutumu eti madai yenu ni kuivunja Chadema, japokuwa viongozi mbalimbali wa CHADEMA walisema hadharani kuwa mlikuwa na nia ya kuisambaratisha(SHUTUMA HIZI MLIZOPEWA MIMI SIZIAMINI HATA KIDOGO).

Umemtaja Tundulisu, nakubaliana nawe sana. Kuna wakati aliwahi kuwaponda sana wazanzibari, kuna wakati aliwahi kuwa na ajenda ambayo huwezi kuifahamu, alifanya mambo ya ajabu mno. Wakati ule ulikaa kimya, Hukumkosoa kwa sababu ambazo sizijui, leo wakati mnatofautina kiitikadi unamkosoa.
Nataka tu kusema kwamba, pamoja na madhaifu na mapungufu ya mmoja mmoja kati yetu, pamoja na madhaifu yanayoweza kuwepo katika kundi zima, pamoja na hofu nyingi za watawala juu ya UKAWA. Bado UKAWA haitatoka katika msitari wa ajenda yake. Wananchi waliona tulivyowasilisha maoni ya wachache, wanajua kila tulichosema.

Tunaamini katika muungano wa haki, muungano wa kidemokrasia, muungano uliopendekezwa na wananchi au vyombo vyenye mamlaka kama zilivyowahi kufanya tume za Nyalali, Kisanga, G55, Warioba n.k. Tunaamini kuwa serikali ya Tanganyika ikirudi muungano utakuwa imara zaidi, kama umedumu kwa miaka 50 Zanzibar ikiwepo, hautashindwa kudumu miaka mingine 50 Tanganyika nayo ikiwepo.
Hizi hofu za muungano kuvunjika hazitusaidii. Muungano unahitaji nia ya dhati ya viongozi na hasa utashi wa kuuendeleza, tutumie fursa hii kuwasikiliza wananchi. Sisi hatutarudi nyuma, tutasonga mbele kuhakikisha maoni ya wananchi yanaheshimiwa.

J. Mtatiro

No comments:

Post a Comment