Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Thursday, February 21, 2013

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 'FEKI'

Mkurugenzi Green Acres afichua siri nzito
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mh. Shukuru Kawambwa
 
WAKATI mjadala wa matokeo mabaya ya kidato cha nne ukiendelea kulitikisa taifa, kashfa mpya ya matokeo hayo imeibuliwa.
 
Kashfa hiyo mpya imeibuliwa na Mkurugenzi wa Shule ya Green Acres, Julian Bujugo, kwamba matokeo ya baadhi ya shule nchini ikiwamo yake yamechakachuliwa.
 
Akizungumza na gazeti hili jana, Bujugo alisema kuwa baadhi ya wanafunzi kwenye shule yake hawakufanya mitihani ya kidato cha nne, lakini matokeo yanaonesha wamefaulu kwa kupata alama za juu.
 
Alitaja mfano wa mwanafunzi, Humphrey Sanga, mwenye namba 01197/148, ambaye hakufanya mitihani hiyo lakini matokeo yanaonesha amefaulu kwa kupata alama nzuri.
 
“Huyu mwanafunzi tulimsimamisha na hakufanya mitihani, lakini matokeo yake yanaonekana amepata hivi; Civics D, Historia D, Jiografia C, Kiswahili D, English C, Physics D, Chemistry C, Biology C, Basic Mathematics D, ambapo amepata daraja la tatu pointi 24,” alisema Bujugo.
 
Alimtaja mwanafunzi mwingine, Martin Rushaigwa, namba 01197/0173, ambaye alifanya masomo ya ‘Arts’.
 
Alisema matokeo ya mwanafunzi huyo yanaonesha kuwa ameongezewa alama za masomo ya biashara ya Bookeeping na Commerce, ambayo hakuyafanya kabisa.
 
Alimtaja mwanafunzi mwingine aliyefanya mtihani huo lakini matokeo yake yanaonesha amewekewa ‘absent’ na mwanafunzi mwingine, Mbazi Volta, hakufanya mitihani lakini amepewa alama za ufaulu.
 
“Matokeo hayo yananipa wasiwasi kwamba yanaweza kuwa yamechakachuliwa,” alisema Bujugo.
Mkurugenzi huyo anaiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kurudia kusahihisha mitihani hiyo ili kuondoa ukungu ulioligubika taifa kwa sasa kuhusu matokeo ya kidato cha nne.
 
“Naomba usahihishaji urudiwe, maana huu ni ubabaishaji mkubwa…matokeo hayo yamewaathiri watoto kisaikolojia na sijui watakwenda wapi?,” alihoji.
 
Alisisitiza kuwa usahihishaji urudiwe kwani katika shule hiyo wanafunzi wenye uwezo mkubwa tangu walipoanza kidato cha kwanza ndio waliofanya vibaya wakati waliokuwa wakifanya vibaya, wameibuka na alama za juu.
 
Mkurugenzi huyo alisema wazazi wa watoto hao wanatarajiwa kukutana mwishoni mwa wiki hii kujadiliana kuhusu matokeo hayo na hatua za kuchukua.
 
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Msemaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), John Nchimbi, alisema si kweli kuwa matokeo hayo yamechakachuliwa bali ni matokeo halisi ya shule hiyo.
 
Alisema iwapo mkurugenzi wa shule hiyo ana shaka na matokeo hayo, alitakiwa kufika katika ofisi za baraza hilo ili apatiwe taarifa sahihi kabla ya kutoa taarifa katika vyombo vya habari.
 
“Mi nimeangalia hayo majina, naona yapo sawa na hata huyo mwanafunzi ambaye anasemekana hakufanya mitihani na akapewa alama…napenda kusema kuwa alama alizopewa si zake na hata katika orodha yetu anaonekana kuwa hakufanya mitihani,” alisema.
 
Katika hatua nyingine, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa na wenzake, wamekuwa bubu kueleza endapo wako tayari kujiuzulu au la.
 
Tanzania Daima ilifika wizarani hapo jana kutaka kuonana na Waziri Kawambwa ili atoe msimamo wake, mwandishi alijibiwa kuwa waziri huyo alikuwa kikaoni na asingeweza kutoka.
 
Hata waziri alipopigiwa simu pamoja na kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakupokea wala kujibu ujumbe huo.
 
Kwa upande wake, katibu mkuu wa wizara hiyo naye hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa alikuwa kikaoni.
 
Naye Naibu Waziri, Philipo Mulugo, alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi kueleza msimamo wake, simu yake iliita bila kupokewa na hata hakuwa tayari kujibu meseji ya ujumbe mfupi.
 
Chanzo: Tanzania Daima

Monday, February 18, 2013

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE HAYA HAPA CHINI



MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012
 
 
 

MAJIBU YA MNYIKA KWA AKINA NAPE NA RIDHIWANI KUHUSU ELIMU YAKE

John Mnyika 17:15 Today
Nilikuwa katikati ya kazi jimboni
nikaambiwa kwamba kuna mwito
humu wa Nape na Ridhwan kutaka
nieleze elimu yangu. WanaCCM
walianza suala hili kwa ari, nguvu
na kasi mpya niliposema kwamba
nchi imefika hapa ilipo kwa
sababu ya udhaifu wa Rais
Kikwete, uzembe wa Bunge na
upuuzi wa CCM.
Nikapuuza, naona sasa limeibuka
tena kwa ari, nguvu na kasi zaidi
baada ya yaliyojiri bungeni kuhusu
hoja binafsi niliyowasilisha
bungeni kuhusu maji na mkutano
wa hadhara wa tarehe 10
Februari 2013 na masuala ambayo
niliipa Serikali wiki mbili
kuyatolea majibu ama sivyo
nitaongoza maandamano ya
wananchi kwenda Wizara ya Maji
kutaka uwajibikaji na hatua za
haraka.
Kwa mara nyingine tena
zinafanyika jitihada za kuhamisha
wananchi kwenye mjadala kwa
kumshambulia mtoa hoja badala
ya hoja, sasa ili turejee kwenye
mijadala ya msingi ni muhimu
niweke kumbukumbu sawa kuhusu
masuala kadhaa kama
yalivyoombwa.
Elimu yangu sio siri, nimegombea
ubunge mara mbili mwaka 2005
na 2010 na mara zote nimeeleza
kuhusu suala hili; Nape na
Ridhwan wangetumia tu elimu yao
wangetafuta kwenye mitandao na
kukuta majibu wanayoyatafuta.
Nieleze kwa muktasari tu;
nimesoma shule ya msingi
Mbuyuni Dar Es Salaam (nilikuwa
mwanafunzi wa kwanza kwa mkoa
wa Dar es Salaam).
Nilichaguliwa kwenda Shule ya
Sekondari ya Ilboru wakati huo
ikiwa ya vipaji maalum, sikwenda;
wito ulinituma kwenda Seminarini.
Nilisoma Franciscan Seminary
Maua (FRASEMA) mpaka kidato
cha nne; nilipata daraja la kwanza;
nikiwa na alama A katika masomo
tisa.
Ningeweza kwenda shule yoyote
ya Serikali ya kidato cha tano na
sita yenye mchepeo ambapo
ningeutaka; lakini niliamua kubaki
Dar es Salaam shule ya Tambaza
kwa sababu nilitaka kusoma huku
nikiendelea na harakati ambazo
nilizianza kabla.
Hapa ndio ilikuwa chanzo cha
mimi kuingia kwenye kazi ya
kuhamasisha mabadiliko kwenye
mimbari nje ya utumishi wa
madhabahuni. Tukio lililobadili
mwelekeo wa maisha yangu,
mwaka 1998 nikiwa kidato cha
nne; nimesoma na tumeanza
mitihani tukatangaziwa kwamba
mitahani yote imefutwa baada ya
kuvujishwa.Tukarudishwa
nyumbani kipindi hicho nikaenda
kwenye mafungo kujitafakari
kwenye mkoa mmoja nikarejea
Dar es Salaam nikakutana na
wanaharakati kadhaa wa asasi
zisizo za kiserikali; maelezo
kuhusu ufisadi yalinifanya nione
nina wajibu kwa nchi yangu,
nikarejea Seminarini kufanya
mitihani nikiwa na fikra tofauti.
Matokeo yakatoka nimefanya
vizuri, kwa mifumo yetu mibovu
ya wakati huo kwa mara ya pili
tena Serikali hii inayoongozwa na
CCM haikutambua vipaji na
nikapaswa niendelee kujilipia ada
mwenyewe kama ilivyokuwa kwa
ngazi nyingine za elimu
zilizotangulia; hapa nikakata shauri
kwamba nitatumia uwezo na
uadilifu wote ambao Mwenyezi
Mungu amenijalia kuwezesha
mabadiliko katika taifa letu.
Nikaamua kuacha kwenda kwenye
shule za bweni mikoani na kubaki
Dar es salaam nisome Tambaza
huku nikiendelea na kazi za
harakati; wakati huo nikihamasisha
masuala ya ukombozi wa vijana
nchini. Pamoja na kusoma kutwa
huku nikifanya kazi nilipata daraja
la pili katika kidato cha sita.
Taasisi nilizoanzisha au
nilizoongoza katika kipindi hicho
na kazi nilizofanya sio siri na
zinapaswa kujieleza zenyewe kwa
matendo badala ya maneno.
Katika kipindi hicho, wakati huo
kukiwa hakuna Mfuko wa Elimu
wala Bodi ya Mikopo nikashiriki
katika ushawishi wa mabadiliko ya
kimfumo; nilikwenda Dodoma,
tukakutana na wabunge na
mawaziri nikawasilisha mada
“Towards a more functional
education in Tanzania”, wakati huo
nikiwa mwanafunzi wa Sekondari.
Kati ya wabunge waliosikiliza mada
niliyoiwaisilisha wakati huo sasa ni
Rais Jakaya Kikwete ( Ridhwan
ukiwa nyumbani unaweza
kumwuliza maoni yake aliyotoa
siku hiyo kuhusu ugharamiaji wa
elimu na suala la mauaji ya
mwanafunzi wa Iyunga Michael
Sikupya). Nilipotoka kwenye
mkutano ule Dodoma mwishoni
wa miaka ya tisini, nilikata shauri
kwamba mwaka 2005 nitagombea
Ubunge hii ni baada ya kushudia
aina ya wabunge waliokuwepo.
Mwaka 2002 nilijiunga na Chuo
Kikuu cha Dar es Es Salaam
kusomea “Bachelor in Business
Administration (BBA) kwenye
programu ya jioni; nilifanya hivyo
kwa kuamua kwa kuwa nilitaka
nisome huku nikiendelea na kazi.
Mkuu wa Programu hiyo wakati
huo alishangaa sana kwa umri
wangu (wakati huo shahada hiyo
walikuwa wakisoma wazee watu
wazima wafanyakazi) na matokeo
yangu (kwa kuwa yaliniruhusu
kwenda kuingia kusoma katika
mfumo wa kawaida). Nikamweleza
akanielewa kwamba sitaki kusoma
kama wanachuo wengine wa
kawaida, uamuzi wangu huo
ulikuwa na gharama kwa
kuwatafsiri yake ni kuwa nilipaswa
kujisomesha binafsi.
Kwa hiyo mimi ni kati ya wale
ambao hatudaiwi na nchi hii kwa
maana ya kwamba sijawahi
kuchukua ruzuku wala
kusomeshwa na Serikali hii
inayoongozwa na CCM; nimesoma
kwa jasho la wazazi wangu na
langu binafsi. Kwa hiyo, nijibu tu
kuhusu elimu yangu ya juu
kwamba nimesoma miaka mitatu
Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam
(mtu aliyosoma kwa kiwango
hicho kwenye baadhi ya vyuo
duniani hupewa associate degree).
Mwaka 2004 ikaanza misukosuko
mbalimbali, mwaka huo ulikuwa
ndio unatungwa muswada wa
Sheria ya Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu, haya matatizo
yanayotokea leo niliyatabiri wakati
huo. Niliwasilisha mada kwa
wanachuo kwenye ukumbi wa
Nkurumah kuchambua udhaifu wa
muswada huo na kupata maoni ya
wanafunzi kuhusu marekebisho
yanayohitajika; wanachuo
wakapitisha azimio la kwamba
muswada huo upingwe.
Kesho yake nikiwa Morogoro
kikazi kukafanyika mgomo
hatimaye wanafunzi wakapigwa na
kukamatwa.Nakumbuka nilikatiza
kazi niliyokuwa nafanya nikarejea
kwa kuwa Chuo kiliweka sharti
kwamba lazima wanachuo waache
mgomo ndio waliokamatwa
waachiwe. Wakati huo Serikali ya
wanafunzi ilikuwa haisikilizwi,
mimi na wengine wachache
tukajitolea kuzunguka kampasi na
hosteli zote kushawishi wanafunzi
kurejea masomoni na wakafanya
hivyo.
Serikali ya CCM ikatoa maelekezo
kwamba kama tumeweza
kuwafanya wanafunzi warudi, hata
kama sikushiriki mgomo na
sihusiki na masuala ya mikopo
kwa kuwa ni mwanafunzi
ninayejilipia mwenyewe lazima
nisimamishwe; nikiwa mwanafunzi
pekee wa BBA niliyesimamishwa
wakati huo.
Nikarejea baada ya muda tayari
kukiwa na mvutano kati yangu na
utawala, mwaka 2005 nikaamua
kugombea Ubunge wakati huo
nikiwa mwanafunzi; mvutano
ukaongezeka zaidi. Na utawala wa
Chuo ukawa unapata mashinikizo
mengi kutoka kwa Serikali na
CCM; wengine wakipendekeza
nifukuzwe, wengine nifelishwe na
wengine nisiruhusiwe kuingia
katika maeneo ya Chuo jioni
masomoni kwa kuwa nitakuwa
nafanya kampeni.
Nikawa katika mtanziko(dilemma)
wa kuchagua ama kuendelea na
masomo na kujitoa au kupunguza
nguvu kwenye kampeni (mbinu
nyingi zilitumika wakati huo, sio
sehemu ya majibu yangu ya leo)
au niendelee na kampeni. Nafsi
yangu ikanituma kuamua kuandika
barua yakuahirisha masomo,
baada ya matokeo ya uchaguzi wa
mwaka 2005 mazingira yalikuwa
yamebadilika sana kuweza kurejea
kumalizia mwaka au miezi
michache iliyokuwa imebaki.
Mwaka 2006 nikiwa Marekani
nilitafakari sana na kufikia uamuzi
wa kuendelea na kazi hii ya
kusimamia mabadiliko na
kujiandaa na uchaguzi wa mwaka
2010. Mwaka 2010 niligombea
tena na kushinda wakati huo huo
nikiongoza kazi za kitaifa za
kampeni makao makuu pamoja na
Profesa Baregu na wengine;
hakuna mahali popote
nilipowadanganya wananchi kuhusu
elimu yangu, kama nilivyoeleza
hapo juu.
Naamini wananchi wa Jimbo la
Ubungo walinichagua kwa uwezo
na uadilifu wangu, na walijua pia
kwamba nilikuwa Chuo Kikuu cha
Dar es salaam kwa miaka mitatu.
Naamini elimu ni kitu muhimu
sana kwa kiongozi, lakini wapo
wenye elimu kubwa ya vyeti lakini
hawajaelimika na wapo wenye
elimu ndogo sana ya vyeti lakini
wanaelewa mkubwa wa kutimiza
majukumu yao ya uongozi.
Tangu mwaka 2012 na 2013,
nimekuwa kwenye mtanziko
mwingine na viongozi wangu ndani
ya chama wanafahamu; niliomba
kuachia majukumu mengine yote
katika chama ili nibaki na ubunge
peke yake niweze kuwatumikia
wananchi wakati huo huo
niendelee na masomo zaidi ya
elimu ya juu katika fani
inayoendana na kazi ninayoifanya
ya sasa na matarajio yangu ya
baadaye.
Hata hivyo, kwa mwelekeo huu
wa Serikali na CCM leo nieleze tu
kwamba nikifanya hivyo itakuwa
faida zaidi kwa watawala
tunapoelekea mwaka 2015; hivyo,
nimeamua kama nilivyoamua
mwaka 2005; kwamba nitarejea
masomoni baada ya CCM
kuondoka madarakani na Tanzania
kupata Serikali mpya
itakayoongozwa na CHADEMA. Kwa
sasa nitaendelea kujisomea kila
siku ninapopata wasaa kwa kuwa
elimu haina mwisho.
Wakili Ridhwan katika maandiko
yake amefanya rejea ya suala
Kihiyo wa CCM Temeke, nashauri
arejee kwenye hukumu ya kesi ile
na marekebisho ya sheria
yaliyofanywa na Serikali yaCCM
kuwalinda wabunge wake vihiyo
baada ya hukumu.
Mifano hailingani kwa sababu
mimi sijatoa maelezo ya uongo
popote. Lakini hata kwa wabunge
wa CCM wanaotoa maelezo ya
uongo wa wapiga kura,
marekebisho hayo yamewawekea
wigo wa mianya yakutokea
mahakamani. Zamani fomu
zakuogembea zilikuwa na mahali
pa kujaza elimu ya mgombea,
sasa kipengele hicho
kimeondolewa. Hivyo, suala la
kughushi na kutoa taarifa za uongo
haliko kama ilivyokuwa awali,
isipokuwa kesi inaweza
kufunguliwa ya ukiukwaji wa
kawaida wataratibu za kampeni
kwa kuwashawishi wapiga kura
kwa taarifa za uongo (ndani ya ule
muda wa kisheria wa kesi
kufunguliwa ambao ulishapita).
Halafu ni jukumu la mlalamikaji
sio tu kuthibitisha kwamba uongo
ulitolewa bali uongo umeathiri
vipi matokeo. Ndio maana leo
kuna vihiyo wengi tu wa CCM
ndani ya Bunge lakini ni vigumu
kuwabana kwa mfumo wetu wa
sasa. Baada ya majibu hayo
marefu, naamini sasa Nape
unaweza sasa kurejea kwenye
kujibu; Elimu ya Mnyika ina
uhusiano gani na CCM kuahidi
kwenye ilani yake na kushindwa
kutekeleza kwamba ifikapo mwaka
2010 asilimia 90 ya wananchi wa
mijini ikiwemo Dar essalaam
watakuwa wanapata maji safi na
salama? Ridhwan kwa kuwa
umeweza kufanya rejea unaweza
pia kueleza ni kwanini Rais
Kikwete mwaka 2011 aliahidi kuwa
tatizo la maji Dar es Salaam
litakuwa historia mwezi Februari
2013 lakini mwezi huo umefika na
matatizo bado ni makubwa?
JJ

Thursday, February 14, 2013

BREAKING NEWS! GOLDIE WA PREZZO AAGA DUNIA

                                                     Goldie na Prezzo walipokuwa BBA 2012
 
Ni taarifa ambayo kila aliekua karibu na Goldie kwenye page zake za facebook na twitter inakua ngumu kuamini, taarifa rasmi zimeripoti kwamba Goldie ambae ni mwakilishi wa Nigeria kwenye BBA 2012 AMEFARIKI muda mfupi tu baada ya kuwasili Lagos Nigeria akitokea Marekani ambapo bado chanzo cha kifo chake hakijajulikana.
 
Mmoja wa wasaidizi wake amethibitisha kifo cha Goldie kupitia page ya twitter ya Goldi kwa kusema ni kweli msanii huyo amefariki dunia usiku wa february 14 2013 muda mfupi tu baada ya kuwasili Lagos Nigeria, hali yake ya afya ilibadilika ghafla ikabidi apelekwe hospitali ambako hakuchukua muda mrefu akafariki dunia.
Taarifa nyingine nilizozipata kutoka kwa mtu wake wa karibu wanaeshirikiana kimuziki zimeeleza kwamba mpenzi wake Goldie ambae ni Msanii wa Kenya CMB Prezzo ametua Nigeria usiku huu muda mfupi uliopita kwa ajili ya kuendeleza mipango aliyokua nayo na Goldie ikiwemo kutengeneza show ya TV.
 
Prezzo alitakiwa kushiriki katika TV show ambayo yeye na Goldie wangekua moja ya wahusika wakuu ambapo mpango ulikua baada ya mwezi mmoja Goldie na Prezzo wangekuja Tanzania, Uganda na Kenya kwa ajili ya kujitangaza na kuipromote single mpya ya Goldie ya ‘Skibobo’ aliyofanya na Ay.
 
Habari hii kwa hisani ya  http://millardayo.com/kifo-cha-goldie/

MAGAZETI YA LEO ALHAMISI TAREHE 14/02/2013

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
HABARI ZA MICHEZO
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

WALIMU WAPYA 26,537 WAAJIRIWA

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa ajira mpya kwa walimu 26,537 wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu nchini.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema kuwa utoaji wa ajira hizo haukufanyika kiholela bali ulifuata tathmini mbalimbali zilizofanyika kubaini maeneo yenye upungufu wa walimu ili kuwezesha kupeleka walimu kwa wingi katika maeneo hayo.
 
Waziri Kawambwa alisema kwa sasa taifa lina upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hesabu na mwaka huu, wameajiri walimu 2,037.
 
Kwa mujibu wa Waziri Kawambwa, wameajiri walimu 13,568 wa ngazi ya cheti ambapo walimu 13,527 wamepangwa katika shule za msingi zilizopo kwenye halmashauri na 41 wamepangwa katika shule za mazoezi zilizo chini yake.
 
Alisema kwa upande wa wahitimu wa elimu ya shahada na stashahada, wameajiri walimu 12,893 kufundisha shule za sekondari zilizoko chini ya halmashauri, 59 wamepangwa kuwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu, huku walimu 21 wamepangwa kufundisha shule za sekondari za mazoezi.
 
Aliongeza kuwa idadi hiyo ya walimu wenye shahada inajumuisha walimu 188 wa elimu maalumu ambao wamepangwa katika shule za sekondari na vyuo vinavyotoa elimu hiyo na kusema kuwa idadi ya walimu walioajiriwa mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 11 sawa na walimu 2,630, ikilinganishwa na walimu 23,907 walioajiri mwaka uliopita.
 
Waziri huyo alisema kati ya walimu wa sekondari na vyuo waliochaguliwa, walimu 1,286 ni wale walioomba ajira serikalini kutoka soko la ajira ambao ni tofauti na wale wanaotoka vyuoni wakati walimu 841 walioshindwa mitihani mwaka jana, wamepatiwa ajira baada ya kurudia mitihani yao na kufaulu.
Alisema orodha ya majina na halmashauri walizopangwa, zinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Elimu huku akitoa agizo kwa walimu waliohitimu ambao ni waajiriwa kurudi katika vituo vyao walivyokuwa wanafanyia kazi kabla ya kwenda masomoni.
 
Waziri Kawambwa alisema walimu wapya wanatakiwa kuripoti katika vituo vyao vya kazi Machi mosi hadi Machi 9, mwaka huu ambapo orodha ya mishahara yao ya mwezi huo itaingizwa katika utaratibu wa serikali.
“Walimu hao lazima waripoti ndani ya muda uliopangwa ili kuondoa usumbufu wa ulipaji mishahara na atakayeshindwa kufika, atakuwa amejitoa kwenye ajira hiyo,” alisema.
 
Alisema katika ajira hizo walimu wasishangae kupangiwa maeneo ambayo hawajayachagua kwani uteuzi wao umelenga maeneo yenye uhitaji zaidi huku akitolea mfano Mkoa wa Lindi ambao walimu wengi hukataa kwenda huko.
 
“Tumepanga kulingana na uhitaji, huwa tuna weka mwalimu mmoja kwa wanafunzi 46 lakini kwa hapa Dar es Salaam kuna walimu wengi na kufikia uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 20,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima

KASI YA CHADEMA YAMTISHA KIKWETE: MBOWE ASEMA HAWAHITAJI HISANI YA KIKWETE KUFANYA SIASA

 
 
HARAKATI za kuwaunganisha Watanzania kupitia kampeni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) inayoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), inaonekana kuitia kiwewe serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ambapo ameliagiza Jeshi la Polisi kukabiliana na harakati hizo.
 
Agizo hilo la Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyetiki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), linakuja ikiwa ni miezi michache tangu alipowaonya wafuasi na viongozi wa chama hicho kutotegemea mabavu ya polisi, badala yake wajitokeze kujibu hoja za wapinzani wao.
 
Akifungua mkutano mkuu wa maofisa waandamizi wa jeshi hilo na wakuu wa vituo juzi mjini Dodoma, Rais Kikwete bila kutaja chama lengwa alilitaka Jeshi la Polisi nchini kubabiliana na maandamano na mikutano, kwa madai kuwa ni kati ya vichocheo vya vurugu nchini.
 
Licha ya kutoitaja CHADEMA moja kwa moja, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanasema kuwa alikilenga chama hicho, kwani ndicho kinaendesha harakati mbalimbali mikoani kwa kufanya mikutano na maandamano.                     
 
Hata hivyo, wakati Rais Kikwete akitoa agizo hilo kwa polisi, CHADEMA kupitia kwa Mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Mbowe, kilisisitiza kuwa endapo kitaandamana bila kuingiliwa au kufanyiwa fujo na jeshi hilo hakuna fujo zinazotokea.
 
Kikwete katika hotuba yake, alisema kuwa hivi karibuni suala la maandamano nchini limechukua sura mpya na kuonekana kama la kawaida wakati maandamano hayo yanasababisha uvunjifu wa amani katika baadhi ya sehemu.
Alisema kuwa polisi wanatakiwa kutimiza wajibu wao kuhakikisha wanadhibiti vurugu na maandamano ambayo yamekataliwa.
“Wajibu wa kufanya hivyo umetajwa kisheria, mamlaka hayo mmekabidhiwa na miongozo yake imeandikwa na kufundishwa katika vyuo vyenu ili kuzuia vurugu,” alisema.
 
Alisema kuwa siku za nyuma hapakuwepo na vurugu ambazo zilikuwa zikitokana na maandamano, tofauti na sasa, kwani imegeuka kuwa sehemu ya kazi ya Jeshi la Polisi kupambana pale ambapo kunakuwapo maandamano na mikutano ya vyama vya siasa.
 
“Kwa sasa sisi watu wa vyama vya siasa tunapoomba kibali cha kufanya mikutano na maandamano, Jeshi la Polisi mnajiandaa kupambana na vurugu, kwa kuwa ndicho kinachotazamiwa, kwani ndilo jambo ambalo linaweza kujitokeza tofauti na zamani,” alisema.
 
Alitolea mfano kuwa siku hizi hata mchawi akikamatwa kunafanyika maandamamo ya wananchi kwenda kituo cha polisi wakitaka kufanya vurugu ili wakabidhiwe mtuhumiwa wajichukulie sheria na kuchoma vituo vya polisi.
 
Aliongeza kuwa japo jeshi hilo halikupewa fursa ya kuzuia mikutano wala maandamano lakini limepewa nafasi ya kuweza kutoa maelekezo hususan kwa vyama vya siasa pale ambapo kunatakiwa kufuata maelezo ya njia ya kupita, ambayo haitazuia shughuli za watu wengine.
 
Kikwete alisema kuwa vurugu zinasababishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa ambavyo vinafanya maandamano na mikutano isiyo ruhusiwa kwa muda na wakati ambao wanataka wao.
 
Aliongeza kuwa vipo vyama vya siasa ambavyo vinataka kufanya maandamano kutwa nzima na kutaka kupita maeneo ambayo wakati mwingine Jeshi la Polisi linakuwa limezuia kutumia njia hizo, jambo ambalo linasababisha kuonekana vurugu hizo kuwa uhalifu mpya.
 
Alisema vurugu kwa sasa zimeonekana kuwa mbinu mpya ya uhalifu, hivyo jeshi hilo lazima lihakikishe linajipanga vizuri kukabiliana nao kulingana na jinsi watakavyokuwa wamepanga.
 
Kikwete alifafanua kuwa polisi ielekeze barabara za kupita maandamano na pale ambapo wahusika watashindwa kufuata maelekezo na maagizo hayo wasiwaonee aibu viongozi hao wa kisiasa, kwani wao wanatakiwa kutimiza wajibu wao.
 
Akizungumzia migogoro ya kidini, alisema inatia aibu kutokana na kuwapo kwa baadhi ya watu wengine kufanya fujo hadi kufikia hatua ya kuondoa uhai wa mwanadamu mwingine.
 
Hata hivyo Kikwete alisema kuwa bado Jeshi la Polisi lina changamoto mbalimbali za kuhakikisha linazuia vurugu na maandamano kwa kufanya mazungumzo ya umahili wa kuwashawishi wananchi badala ya kupigana virungu.
 
Mbowe amjibu
Mbowe alisema kuwa maandamano ni haki ya kikatiba na si mapenzi wala hiari ya rais ya kutaka yafanyike au yasifanyike.
 
Alisema rais na chama chake wajue kuwa si kweli kwamba maandamano na mikutano ya vyama vya siasa ndivyo husababisha vurugu.
 
“Tumeshuhudia katika nchi yetu maandamano ya vikundi vya dini ambayo hayakudhibitiwa, serikali inasuasua kuchukua hatua, je, hayo yalisababishwa na mikutano na maandamano ya kisiasa?” alihoji.
 
Alisema kuwa CHADEMA wajue kuwa wakiandamana bila kuingiliwa au kufanyiwa fujo na polisi hakuna vurugu zinazotokea.
 
“Juzi tumeandamana bila kubughudhiwa na polisi tulifanya maandamano ya amani, watu walifika wakasikiliza na tukapeleka ujumbe na wananchi walirudi, hakuna kibanda kilichovunjwa wala mende kuuawa hata simu kuibiwa,” alisema.
 
Alifafanua kuwa maandamano ni njia ya kuonesha kutoridhika na kwamba suluhisho lake si kuyazuia. Hivyo rais asizuie watu wapumue shida zao, kwamba akiwazuia watatafuta mahali pa kuzieleza kwa njia zao.
 
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samuel Ruhuza, alisema kauli ya rais ni ya kushangaza kidogo, kwani yeye aliongoza maandamano ya Chama chake cha CCM mkoani Kigoma halafu leo adai yanaudhi.
 
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema rais amejifanya kuwa katiba ili watu wasikilize maoni yake.
 
Kwamba kama ameamua kuondoa haki ya msingi ya mikutano ya hadhara na watu kujumuika katika maandamano, basi atangaze hali ya hatari katika nchi.
 
Chanzo: Tanzania Daima

Wednesday, February 13, 2013

BUNGE KUSITISHA KURUSHA VIKAO VYAKE LIVE



BUNGE linatarajia kufuta utaratibu wa kurusha matangazo ya moja kwamoja kupitia televisheni kwa madai ya kukomesha vitendo vya baadhi ya wabunge kukiuka kanuni za bunge na kuleta vurugu kwa kutafuta umaarufu bila kujua kwamba tabia hiyo inaleta picha mbaya katika jamii.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Bunge Dk.Thomas Kashilila jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa ya mapendekezo ya kuanzisha kamati ya bajeti na kuvunjwa kwa baadhi ya kamati za bunge.


Amesema kuwa ili kuleta maadili kwa baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wanashindwa kufuata kanuni za bunge na kutumia nafasi hiyo kwa kutafuta umaarufu kwa sasa wameomba kufutwa utaratibu wa kurusha matangazo ya bunge ya moja kwa moja badala yake watarekodi ili kuondoa hoja zisizokuwa za msingi.

Ameongeza kuwa kuna idadi kubwa ya wabunge wamekuwa wakikiuka kanuni za bunge makusudi na kusababisha kuleta vurugu bungeni wakati jamii ikiendelea kutazama mabishano yasiyokuwa na hoja za msingi.

Dk Kashilila amesema kuwa kwa sasa kuna baadhi ya kamati za bunge ambazo zimevunjwa kutokana na baadhi ya kamati hizo kuingilia katika utendaji jambo ambalo limekuwa likipoteza maana ya kamati hizo.

Hivi karibuni baadhi ya kamati ikiwemo ile ya Mashirika ya umma POAC zimefutwa na kuacha maswali mengi kwa baadhi ya wananchi juu ya hatua hiyo.
 
Source: Jamii Forums bofya hapa kusoma zaidi
 

HAYA NDIYO MAJIBU YA NAIBU WAZIRI WA ELIMU MH. MULUGO KUHUSU MITIHANI YA KIDATO CHA SITA INAYOENDELEA NCHINI KOTE

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mh. Mulugo alipokuwa akiulizwa na waandishi wa habari kuhusu mitihani ya kidato cha sita inayoendelea nchi kote tangu jumatatu ya tarehe 11/02/2013, haya yalikuwa majibu yake.
 
"Sina taarifa yoyote kuhusiana na kuanza kwa mitihani ya kidato cha sita, kwasasa nipo kwenye kikao cha NEC, labda waulizeni waliopo DSM ofisini. Alipoulizwa zaidi aliendelea kusema mimi sijui kuhsuiana na mitihani ya kidato cha sita.
 
Chanzo: Ukurasa wa Dj Fetty
 

Tuesday, February 12, 2013

MAGAZETI YA LEO JUMATANO TAR 13/02/2013

 
 
 
 
 
 
 
 
HABARI ZA MICHEZO
 
 
 
 
 
 
 

VURUGU ZA KIDINI GEITA, WAKRISTO NA WAISLAMU WAMWAGA DAMU, KISA! KUGOMBEA HAKI YA KUCHINJA


 
VURUGU kubwa za kidini kati ya Waislamu na Wakristo, zimezuka katika kijiji cha Buseresere, wilaya ya Chato, mkoani Geita, na kusababisha kifo cha Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God, Mathayo Kachila (45), huku watu wengine 10 wakijeruhiwa vibaya kwa mapanga.

 
Mchungaji huyo alichinjwa na watu wanaodaiwa ni kuwa waumini wa Kiislamu kisha mwili wake kutelekezwa kwenye vibanda vya maduka ambavyo viko jirani na eneo hilo jana.

 
Taarifa kutoka eneo la tukio hilo zilisema kuwa tukio hilo lilitokea asubuhi ambapo chanzo chake kinatajwa kuwa ni watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Kiislamu kuvamia bucha iliyokuwa ikiwauzia nyama Wakristo wa kijiji hicho waliokuwa wamepanga foleni kwa wingi kusubiri huduma hiyo.
 
Wakiristo hao walikuwa wamechinja ng’ombe mmoja na mbuzi wawili eneo la kanisani kabla ya kuipeleka nyama hiyo katika bucha hiyo iliyoko eneo la Buseresere Sokoni na ndipo walipokumbana na kadhia.

 
Mashuhuda walisema kuwa tukio hilo lilianza saa 2:00 asubuhi muda mfupi baada ya nyama kuwasili katika bucha hiyo ya Wakristo kwa ajili ya kuuzwa, jambo linalodaiwa kuwakera Waislamu ambao waliivamia bucha hiyo kwa lengo la kuifunga.

 
Taarifa ziliongeza kuwa wakati Wakristo wakitafakari uwepo wa Waislamu kwenye bucha yao, ghafla walishtukia wenzao hao waliokuwa wametapakaa kwa wingi wakiimwagia nyama hiyo vitu vinavyodaiwa kuwa sumu.
Kutokana na hali hiyo, Wakiristo walioonekana kukerwa na kitendo hicho na ndipo mapambano yalipoanza kati ya pande hizo mbili huku Wakristo wakitumia mawe na Waislamu wakitumia mapanga na majambia.

 
Ilidaiwa kuwa wakati mapambano hayo yakiendelea, mchungaji huyo ambaye kwa sasa ni marehemu alifika eneo la tukio ili kujua kulikoni na ndipo alipojikuta akishambuliwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za kichwani na kupoteza maisha akikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu.

 
“Yaani ilikuwa kama mzaha tu...baada ya Wakristo kuleta ng’ombe mmoja na mbuzi wawili kwenye bucha yao, tulishangaa kuona Waislamu wamevamia hiyo bucha wakati tayari nyama ikiwa inauzwa na Wakristo wakiwa wamepanga foleni wakisubiri kuhudumiwa,” alisema shuhuda mmoja.
 
Aliongeza kuwa Waislamu walipofika walitaka kuifunga ile bucha lakini Wakristo waligoma na ndipo wengine walifika na kuimwagia ile nyama vitu kama sumu na huo ukawa mwanzo wa machafuko.
 
“Kwa vile wenzetu walifika eneo hilo wakiwa na silaha tayari walianza kuwakata Wakristo na kuivunjavunja ile bucha huku Wakristo wakijihami kwa kutumia mawe lakini walizidiwa nguvu,” alisema shuhuda mwingine.

 
Waliojeruhiwa ni Saidi Ntahompagaze (45), Sadick Yahaya (40),Yasin Rajab (56),Vicent Damon (22), wote wakazi wa Buseresere na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Ramadhan ambaye yuko mahututi katika wodi namba nane katika hospitali ya wilaya ya Geita.

 
Hata hivyo watu wengine watano ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja walitibiwa na kuruhusiwa kutokana na hali zao kuwa nzuri.

 
Polisi kutoka wilaya za Chato na Geita walifika eneo la tukio hilo saa 4:30 na kukuta uharibifu mkubwa umekwishafanyika ikiwa ni pamoja na duka la Mwenyekiti wa BAKWATA Wilaya ya Chato, Yusuph Idd, linalotumika kwa biashara ya M-Pesa na vinywaji baridi likiwa linateketea kwa moto.

 
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Ludorick Mpogolo, aliyefika eneo la tukio muda mfupi baada ya polisi kuwasili, mbali na kusikitishwa na kitendo hicho aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati serikali ikiangalia njia sahihi za kutatua mgogoro huo ambao unakua kwa kasi kila kukicha.
 
Hivi karibuni mgogoro huo wa kidini umezidi kukua wilayani humo kwa pande hizo mbili kila upande ukidai ndiyo wenye haki ya kuchinja nyama inayouzwa buchani.
 
Chanzo: www.freemedia.co.tz  [Tanzania Daima]
 
TAZAMA PICHA ZA MAJERUHI WA VURUGU HIZO
 
 
 
 
 
 
 
 

MAGAZETI YA LEO JUMANNE TAR. 12/02/2013

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI