Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Sunday, February 10, 2013

CHADEMA WAMBANA SPIKA NA NAIBU WAKE, ZITTO ATOA NJIA/MBINU ZA KUWANG'OA

 
VIONGOZI na mashabiki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana walifanya maandamano na kuhitimishwa kwa mkutano wa hadhara uliofanyika Temeke, jijini Dar es Salaam ambako chama hicho kilitangaza nia ya kuandaa hoja ya kuwang’oa viongozi wa Bunge.

Hoja hiyo itawasilishwa katika mkutano ujao wa Bunge kwa ajili ya kuwapigia kura za kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai kwa madai ya kukwamisha mijadala yenye masilahi ya wananchi bungeni.
 

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Temeke Mwisho, Dar es Salaam, wabunge wa chama hicho wakiwa na uongozi wa juu, waliwataka wananchi waliohudhuria mkutano huo kujiandaa na maandamano ya kuwang’oa spika hao.Kana kwamba hiyo haitoshi, wabunge hao walitangaza namba za simu za viongozi hao wa Bunge ili wananchi wazitumie kuwashinikiza wang’oke.
 

Akihutubia katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Zitto Kabwe alisema Spika Makinda ameshindwa kuwajibika na hivyo anapaswa kung’olewa kutokana na kutaka kuirudisha nchi kwenye kipindi cha kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (Epa).

Akizungumzia kitendo cha Spika Makinda kuifuta Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema imefutwa kwa mbinu za CCM kuzima sauti ya wabunge wa upinzani wanaozungumzia masilahi ya wananchi.
 

Huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo, Zitto alitaja mbinu za kumng’oa Spika Makinda akisema kuwa hoja hiyo imeshakamilika
 
“Kuna njia za kumng’oa Spika Makinda, kwanza kwa kupeleka hoja ya kutokuwa na imani naye na nimeambiwa hapa kwamba imeshakamilika. Au tuandamane hadi pale Shule ya Msingi Bunge… au tutumie namba zake kumpigia na kumtumia ujumbe wa simu za mikononi…” alisema Zitto na kumruhusu Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema kutaja namba za Spika Makinda na Naibu wake.
 

Baada ya kutaja namba hizo wananchi walionekana wakizipiga na wengine kutuma ujumbe wa simu.

Mwananchi lilipompigia simu Spika Makinda, simu yake ilikuwa inaita, kisha inakatika bila kupokewa.
 

Akizungumzia zaidi kuhusu kamati hiyo, Zitto alisema:

“Kamati hii iliundwa mwaka 2008 na aliyekuwa Spika Samuel Sitta kwa ushauri wa kina Dk Slaa (Willibrod, Katibu Mkuu Chadema), waliona kuwa haiwezekani nchi yenye zaidi ya mashirika 200 yenye thamani ya zaidi ya Sh10 trilioni yasidhibitiwe na Bunge…Lakini Serikali ya CCM ikaona upinzani umepata sehemu ya kuzungumzia, sasa wameifuta,” alisema Zitto.
 

Alitaja sababu ya kufutwa kwa kamati hiyo kuwa ni utendaji wa kamati hiyo uliogundua matumizi ya zaidi ya Sh1 trilioni kutoka kwenye mifuko ya pensheni zilizotumika katika kampeni za CCM ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma, Hombolo na Chuo Kikuu cha Arusha.

“Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la Wananchi liitwalo Bunge. Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia,” alisema Zitto.
 

Mnyika alia na Maghembe
 

Katika mkutano huo, Mnyika alitoa wiki mbili kwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kuwa ameshughulikia matatizo ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam.
 

Alisema kutokana na hoja aliyoiwasilisha katika kikao kilichomalizika mwishoni mwa wiki bungeni kuondolewa, analitaka Bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa majitaka katika Jiji la Dar es Salaam.
 
“Natoa wiki mbili kuanzia leo (jana) Waziri wa Maji (Maghembe) awe ameeleza hatua anazochukua kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji kwa Dar es Salaam,” alisema Mnyika na kuongeza:

“Asipofanya hivyo tutaandamana kwenda wizarani kwake kumshinikiza kutekeleza yale ambayo alisema yanaendelea,” alisema.
 

Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa chama hicho, Dk Slaa alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kueleza hatua ambazo amefikia katika ufuatiliaji wa mabilioni yaliyofichwa nchini Uswiss.
 

Alisema watuhumiwa wa fedha hizo ndiyo vigogo katika Serikali, ndiyo maana hakuna jitihada zozote zinazofanyika kuhakikisha fedha hizo zinarudi.
 

Ahadi ya Mbowe
 

Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa ule mtindo wa wabunge wa chama hicho kususia vikao vya Bunge hautakuwepo tena badala yake wataendelea kupiga kelele ndani ya Ukumbi wa Bunge ili mikutano iahirishwe.

“Tulikuwa tunatoka nje ya Bunge, watu wakawa wanasema kuwa hatukuwachagua ili mkatoke nje, kwanza ni sawa na kumwachia nguruwe  shamba la mahindi…Sasa hatutoki, tutakuwa tunakomaa na kupiga kelele hadi hoja zetu zisikilizwe… kama noma na iwe nomaa… kama noma na iwe nomaaa…” alisema Mbowe huku akishangiliwa na wananchi.
Kwa upande mwingine Mbowe aliilaumu Serikali kwa kukusanya kodi nyingi kila mwaka lakini haijali mahitaji ya wananchi.

 
 
“Kwa kipindi cha Desemba 2011 hadi Desemba 2012 Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekusanya kodi ya Sh900 bilioni. Zote wanapeleka hazina, kisha wanakaa vikao Dodoma na kula na kustarehe. Watoto wetu wanashindwa kwenda shule…” alisema Mbowe na kuongeza:

“Kwa upande wa madini, asilimia 60 sawa na Sh256 bilioni iliyokusanywa kama kodi inatokana na wachimbaji wadogo kama ‘Pay as you earn’ (kwenye mishahara), wakati kampuni kubwa zimelipa Sh56,000 bilioni za kodi. Hivi wananchi mnasubiri nini? Mapambano haya hayatoshi bungeni tu, ndiyo maana tumekuja kwa wananchi hadi kieleweke.”
 

Mapokezi ya wabunge


Wabunge wa Chadema wakiongozwa na Mbowe walipokelewa majira ya saa nne asubuhi ambapo magari ya chama hicho na idadi kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam walijikusanya kwa ajili ya kujiunga na msafara ulioanzia maeneo ya Riverside, Ubungo mpaka Uwanja wa Temeke Mwisho.

Shamrashamra za kuwapokea viongozi hao, zilifanyika mpaka majira ya saa 7.00 mchana baada ya kuwasili katika eneo hilo tayari kwa msafara wa kuelekea kwenye uwanja huo.

Magari zaidi ya 70 yaliyokuwa kwenye msafara huo yaliyokuwa yamefurika katika Barabara ya Mandela kwa takriban saa tatu huku magari ya John Mnyika, Tundu Lissu, Zitto Kabwe na Godbless Lema yakivamiwa kwa furaha na wakazi hao katika kona ya kuingia Tandika.
 
 
ANGALIA PICHA ZA MAANDAMANO NA MKUTANO HUO
 

    viongozi wakuu wa chadema wakijiweka sawa kwa maandamano
 


vijana wa ulinzi walihakikisha mambo ya usalama yanakuwa poa

Maandamano yake mabango bwana!
 
Haya sasa! Kushoto Zitto, Dr. Slaa, Mbowe, Mnyika na Lema
 
                              Hiyo ndo Temeke bwana, maandamano hadi kwenye vichochoro
 
                                                   Makamanda wakijiandaa kukaa meza kuu
 
    Meza kuu, kutoka kushoto Dr. Slaa, Mbowe na Zitto
 
Mambo yameanza Lema anamwaga sumu
Haya sasa Katibu Mkuu wa AFP anawakubari sana Chadema
 
Msigwa kama kawa
 
Lisu nae akikandamizia
 
Mnyika akilia na Maghembe
 
Halima Mdee naye alikuwepo
Photo 
 
Dr. Slaa akiwapa somo wakazi wa Dar.

No comments:

Post a Comment