Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Thursday, February 14, 2013

KASI YA CHADEMA YAMTISHA KIKWETE: MBOWE ASEMA HAWAHITAJI HISANI YA KIKWETE KUFANYA SIASA

 
 
HARAKATI za kuwaunganisha Watanzania kupitia kampeni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) inayoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), inaonekana kuitia kiwewe serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ambapo ameliagiza Jeshi la Polisi kukabiliana na harakati hizo.
 
Agizo hilo la Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyetiki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), linakuja ikiwa ni miezi michache tangu alipowaonya wafuasi na viongozi wa chama hicho kutotegemea mabavu ya polisi, badala yake wajitokeze kujibu hoja za wapinzani wao.
 
Akifungua mkutano mkuu wa maofisa waandamizi wa jeshi hilo na wakuu wa vituo juzi mjini Dodoma, Rais Kikwete bila kutaja chama lengwa alilitaka Jeshi la Polisi nchini kubabiliana na maandamano na mikutano, kwa madai kuwa ni kati ya vichocheo vya vurugu nchini.
 
Licha ya kutoitaja CHADEMA moja kwa moja, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanasema kuwa alikilenga chama hicho, kwani ndicho kinaendesha harakati mbalimbali mikoani kwa kufanya mikutano na maandamano.                     
 
Hata hivyo, wakati Rais Kikwete akitoa agizo hilo kwa polisi, CHADEMA kupitia kwa Mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Mbowe, kilisisitiza kuwa endapo kitaandamana bila kuingiliwa au kufanyiwa fujo na jeshi hilo hakuna fujo zinazotokea.
 
Kikwete katika hotuba yake, alisema kuwa hivi karibuni suala la maandamano nchini limechukua sura mpya na kuonekana kama la kawaida wakati maandamano hayo yanasababisha uvunjifu wa amani katika baadhi ya sehemu.
Alisema kuwa polisi wanatakiwa kutimiza wajibu wao kuhakikisha wanadhibiti vurugu na maandamano ambayo yamekataliwa.
“Wajibu wa kufanya hivyo umetajwa kisheria, mamlaka hayo mmekabidhiwa na miongozo yake imeandikwa na kufundishwa katika vyuo vyenu ili kuzuia vurugu,” alisema.
 
Alisema kuwa siku za nyuma hapakuwepo na vurugu ambazo zilikuwa zikitokana na maandamano, tofauti na sasa, kwani imegeuka kuwa sehemu ya kazi ya Jeshi la Polisi kupambana pale ambapo kunakuwapo maandamano na mikutano ya vyama vya siasa.
 
“Kwa sasa sisi watu wa vyama vya siasa tunapoomba kibali cha kufanya mikutano na maandamano, Jeshi la Polisi mnajiandaa kupambana na vurugu, kwa kuwa ndicho kinachotazamiwa, kwani ndilo jambo ambalo linaweza kujitokeza tofauti na zamani,” alisema.
 
Alitolea mfano kuwa siku hizi hata mchawi akikamatwa kunafanyika maandamamo ya wananchi kwenda kituo cha polisi wakitaka kufanya vurugu ili wakabidhiwe mtuhumiwa wajichukulie sheria na kuchoma vituo vya polisi.
 
Aliongeza kuwa japo jeshi hilo halikupewa fursa ya kuzuia mikutano wala maandamano lakini limepewa nafasi ya kuweza kutoa maelekezo hususan kwa vyama vya siasa pale ambapo kunatakiwa kufuata maelezo ya njia ya kupita, ambayo haitazuia shughuli za watu wengine.
 
Kikwete alisema kuwa vurugu zinasababishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa ambavyo vinafanya maandamano na mikutano isiyo ruhusiwa kwa muda na wakati ambao wanataka wao.
 
Aliongeza kuwa vipo vyama vya siasa ambavyo vinataka kufanya maandamano kutwa nzima na kutaka kupita maeneo ambayo wakati mwingine Jeshi la Polisi linakuwa limezuia kutumia njia hizo, jambo ambalo linasababisha kuonekana vurugu hizo kuwa uhalifu mpya.
 
Alisema vurugu kwa sasa zimeonekana kuwa mbinu mpya ya uhalifu, hivyo jeshi hilo lazima lihakikishe linajipanga vizuri kukabiliana nao kulingana na jinsi watakavyokuwa wamepanga.
 
Kikwete alifafanua kuwa polisi ielekeze barabara za kupita maandamano na pale ambapo wahusika watashindwa kufuata maelekezo na maagizo hayo wasiwaonee aibu viongozi hao wa kisiasa, kwani wao wanatakiwa kutimiza wajibu wao.
 
Akizungumzia migogoro ya kidini, alisema inatia aibu kutokana na kuwapo kwa baadhi ya watu wengine kufanya fujo hadi kufikia hatua ya kuondoa uhai wa mwanadamu mwingine.
 
Hata hivyo Kikwete alisema kuwa bado Jeshi la Polisi lina changamoto mbalimbali za kuhakikisha linazuia vurugu na maandamano kwa kufanya mazungumzo ya umahili wa kuwashawishi wananchi badala ya kupigana virungu.
 
Mbowe amjibu
Mbowe alisema kuwa maandamano ni haki ya kikatiba na si mapenzi wala hiari ya rais ya kutaka yafanyike au yasifanyike.
 
Alisema rais na chama chake wajue kuwa si kweli kwamba maandamano na mikutano ya vyama vya siasa ndivyo husababisha vurugu.
 
“Tumeshuhudia katika nchi yetu maandamano ya vikundi vya dini ambayo hayakudhibitiwa, serikali inasuasua kuchukua hatua, je, hayo yalisababishwa na mikutano na maandamano ya kisiasa?” alihoji.
 
Alisema kuwa CHADEMA wajue kuwa wakiandamana bila kuingiliwa au kufanyiwa fujo na polisi hakuna vurugu zinazotokea.
 
“Juzi tumeandamana bila kubughudhiwa na polisi tulifanya maandamano ya amani, watu walifika wakasikiliza na tukapeleka ujumbe na wananchi walirudi, hakuna kibanda kilichovunjwa wala mende kuuawa hata simu kuibiwa,” alisema.
 
Alifafanua kuwa maandamano ni njia ya kuonesha kutoridhika na kwamba suluhisho lake si kuyazuia. Hivyo rais asizuie watu wapumue shida zao, kwamba akiwazuia watatafuta mahali pa kuzieleza kwa njia zao.
 
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samuel Ruhuza, alisema kauli ya rais ni ya kushangaza kidogo, kwani yeye aliongoza maandamano ya Chama chake cha CCM mkoani Kigoma halafu leo adai yanaudhi.
 
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema rais amejifanya kuwa katiba ili watu wasikilize maoni yake.
 
Kwamba kama ameamua kuondoa haki ya msingi ya mikutano ya hadhara na watu kujumuika katika maandamano, basi atangaze hali ya hatari katika nchi.
 
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment