HOJA binafsi kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu iliyowasilishwa na
mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), ilizua mjadala mzito bungeni
jana.
Mjadala huo ulimfanya Spika wa Bunge, Anna Makinda, kuwa na wakati mgumu
kutumia kanuni ya kuwazuia wabunge wa kambi ya upinzani, Tundu Lissu, Felix
Mkosamali, Mchungaji Peter Msingwa na wengine ambao walikuwa wakiichangia kwa
jazba.
Mjadala huo ulitokana na Mbatia kumaliza hoja yake kwa kulitaka Bunge kuuda
Kamati Teule kuchunguza udhaifu wa mfumo wa elimu nchini.
Wakati wabunge wa upinzani wakichangia kuunga mkono hoja ya kutaka iundwe
Kamati Teule, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alikuja
na mapendekezo ya serikali jinsi inavyoshughulikia suala la kuweka sera mpya ya
mfumo wa elimu nchini.
Hoja ya Waziri Kawambwa iliungwa mkono na Spika na wabunge wengi wa CCM,
lakini wa kambi ya upinzani walipinga wakitaka iundwe Kamati Teule.
Spika Makinda alisema Bunge linaweza kuunda Kamati Teule kwa jambo maalumu,
lakini haliwezi kuunda kamati hiyo kushughulikia hoja ya Mbatia kwani ina
vipengele vingi na ni suala pana.
“Kamati Teule inaundwa kushughulikia jambo maalumu, lakini hoja ya Mbatia ni
pana na inahitaji kuunda Kamati Teule zaidi ya sita, sasa hilo haliwezekani,”
alisema Makinda na kuibua mjadala zaidi.
Hoja hiyo iliamriwa kwa kupiga kura na kukubaliana kutounda kamati teule
badala yake wizara iachiwe ifanyie marekebisho suala la udhaifu wa sera ya elimu
nchini.
Katika hoja yake binafsi, Mbatia alisema pamoja na kazi nzuri inayofanywa na
serikali, elimu itolewayo nchini kwa sasa ina udhaifu mkubwa sana.
Alisema udhaifu huo unajidhihirisha katika sura mbalimbali ambazo miongoni
mwazo ni tabia ya Watanzania wengi kutothamini matumizi ya muda, kupotoka kwa
mila, desturi na utamaduni wa jamii ya Watanzania, kumomonyoka kwa uadilifu
miongoni mwa watumishi wa umma na kada nyinginezo.
“Kuporomoka kwa uwajibikaji, kuporomoka kwa kiwango cha utii wa sheria na
kanuni mbalimbali, kutokuthamini rasilimali za taifa, kukithiri kwa ukiukwaji wa
haki za binadamu, kukua kwa utamaduni wa ukupe, kupungua kwa uzalendo kwa baadhi
ya wananchi, kutojiamini kwa Watanzania wanaohitimu elimu katika ngazi
mbalimbali na kukua na kukomaa kwa migogoro ya mara kwa mara katika sekta ya
elimu,’ alisema.
Alisema uduni wa elimu itolewayo katika ngazi mbalimbali za elimu nchini,
unaojidhihirisha katika viwango vya chini, ufaulu wa wanafunzi katika mitihani,
pamoja na uelewa mdogo wa wahitimimu, huduma mbovu zitolewazo katika sekta
mbalimbali.
Akizungumzia udhaifu katika elimu, Mbatia alisema udhaifu uliopo katika sekta
ya elimu hususan mfumo wa utoaji elimu ndicho kirusi kilichoambukiza udhaifu
kwenye sekta nyingine zote katika taifa.
“Matokeo ya utafiti niliofanya, kwa takriban miaka 18 sasa, yanaonyesha
kwamba udhaifu wa mfumo wetu rasmi wa elimu unatokana na mambo makuu matatu,
ambayo hapa nchini imekuwa ni nadra kuyaangalia kwa undani tunapoendelea
kutafuta ni kwa nini tumekwama katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo,”
alisema.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni sera ya elimu ya taifa ya tangu mwaka 1995 na
sera nyinginezo.
Alisema mitaala ya elimu ya shule za msingi na sekondari na mihtasari ya
masomo na vitabu vya kiada na ziada vitumikavyo katika shule za msingi na
sekondari ina mapungufu.
Alisema tatizo la sera ya elimu ya sasa ni kwamba imetumika kwa muda mrefu,
hivyo kuna haja ya kuifanyia tathmini kubwa.
Alisema sanjari na matatizo ya sera ya elimu nchini, ni jambo la kusikitisha
sana kwamba hadi mwaka 2011, nchi haikuwahi kuwa na mitaala rasmi ya kitaifa kwa
ajili ya elimu ya shule za msingi au sekondari.
Kuhusu udhaifu kwenye vitabu vya kiada, Mbatia alisema kuwa licha ya matatizo
ya kimkakati tuliyonayo, kuna udhaifu mkubwa katika utendaji kiuwezo na
kimaadili.
Chanzo: Tanzania Daima
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment