Wasichana wang'ara
Ufaulu waongezeka kwa asilimia 8.8
WASICHANA
nchini wameng’ara katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, baada
ya kuongoza kwa asilimia 50.20 na kuwapita wavulana waliopata asilimia 49.80.
Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, alitangaza matokeo hayo jana
wizarani kwake na kusema kuwa wanafunzi 560,706 wamechaguliwa kujiunga kidato
cha kwanza katika shule za sekondari za serikali.
Alisema,
kati ya wanafunzi hao wasichana waliochaguliwa ni 281,460, huku wavulana wakiwa
279,246, na hivyo kufanya idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kuongezeka kwa
asilimia 8.8 ikilinganishwa na wanafunzi 515,187 waliochaguliwa awamu ya kwanza
2011.
Kawambwa
alisema, mtihani huo uliofanyika Septemba 19 na 20, kwa mara ya kwanza ulitumia
teknolojia mpya ya ‘optical mark reader’ ambapo mitihani ilisahihishwa kwa
kutumia kompyuta.
Alisema
utumiaji wa teknolojia hiyo mpya umeipunguzia serikali gharama kwa kuwa mwaka
jana walimu 4000 walitumia zaidi ya mwezi mmoja kusahihisha mitihani hiyo nchi
nzima, lakini kwa mwaka huu walimu 285 tu ndio waliotumika kwa siku 15
kukamilisha usahihishaji huo.
“Matokeo
ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yanaonyesha kuwa alama ya juu kabisa
ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana. Matokeo hayo pia yanaonyesha
kuwa jumla ya watahiniwa 3087 walipata alama za daraja la A, wakati wanafunzi
40,683 walipata daraja la B.
“Jumla ya
wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja la C na 526,397 walipata alama za
daraja la D. Waliobaki 73,264 walipata alama E,” alisema Kawambwa.
Hata
hivyo, waziri huyo katika maelezo yake, hakuweza kutaja mikoa iliyofanya vema
na ile iliyoshika nafasi ya mwisho. Kadhalika Waziri Kawamba hakuweza kutoa
nafasi ya kutosha kwa waandishi kuuliza maswali kwa kile alichodai kuwa na
haraka ya majukumu mengine ya kitaifa.
Akizungumzia
udanganyifu katika mtihani alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya
watahiniwa waliofutiwa matokeo kutokana na kujihusisha na vitendo vya
udanganyifu katika mtihani huo imepungua.
Alisema
waliofutiwa matokeo 2012 ni watahiniwa 293 tu ikilinganishwa na watahiniwa 9736
waliofutiwa matokeo kwa undanganyifu mwaka jana.
“Kufuatia
udanganyifu huo, serikali itawabaini wale wote waliohusika katika udanganyifu
huo na kuwachukulia hatua stahiki,” alisema.
kuhusu
tatizo lililojitokeza mwaka jana la wanafunzi kutokujua kusoma na kuandika,
serikali imeanzisha mpango mpya wa kuwachuja wanafunzi hao kwa kufanya mtihani
mwingine kabla ya kuanza kidato cha kwanza.
Alisema,
serikali inafanya hivyo ili kujihakikishia haitarudia kosa la kuwapeleka
wanafunzi wa aina hiyo sekondari, bali endapo watabainika watafutiwa usajili na
kupelekwa kwenye mfumo wa kujifunza kusoma na kuandika.
Wanafunzi
894,839 wa shule za msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo wa kumaliza darasa
la saba, wengine 29,012 sawa na asilimia 3.24 hawakufanya mtihani kutokana na
sababu za utoro, vifo na ugonjwa.
Chanzo:
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment