Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Monday, December 31, 2012

'MADUDU' MATOKEO DARASA LA SABA YAFICHULIWA


• Wasiojua kusoma wachaguliwa kujaza shule za kata

WIKI moja tangu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, atangaze matokeo ya darasa la saba na kudai ufaulu umeongezeka, baadhi ya walimu na wazazi wamefichua ‘madudu’ yaliyofanyika kupanga washindi wakidai hatua hiyo itaongeza idadi ya wajinga nchini.
Waziri Kawambwa alisema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao kwa mwaka 2012 kimeongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2011.
Alisema kuwa alama ya juu ya ufaulu kwa wanafunzi wote ni 234 kati ya alama 250 ambapo wasichana wamefaulu kwa wingi zaidi kuliko wavulana kutoka kwenye idadi hiyo ya 865,827 waliofanya mtihani huo.
Hata hivyo, vyanzo vyetu vya taarifa kutoka kwa baadhi ya walimu na wazazi wa wanafunzi hao, vilionyesha kuwa hawakubaliani na maelezo ya Kawambwa ya kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wakati alama zilizotumika kuwachagua washindi zilikuwa chini ya kiwango.
Katika takwimu zilizopatikana kwenye wilaya za Arusha (shule za msingi Kioga na sekondari Ilkiding’a), Sengerema (shule za msingi Buzilasoga, Tamabu Butonga na Buyangu), Bukombe (shule ya msingi Katente), Shinyanga Vijijini, na Singida Mjini (shule za Mungumaji, Mfumbu, Kisasida na Ipungi), kiwango cha ufauli kinatisha.
Akizungumzia matokeo hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Geita (CWT), Dotto Biteko, alihoji ufaulu umeongezeka vipi wakati alama zinazotumika kama vigezo zilishushwa ili kukidhi idadi badala ya kiwango?
Biteko alisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa hawakufikisha alama 100 kati ya 250 kwa masomo yote matano yaliyofanywa na wengi wao wamechukuliwa wakiwa na alama 70 au chini zaidi ya zile zinazohitajika.
Aliongeza kuwa kama waliokuwa wanachagua wanafunzi hao wangezingatia alama 100 zinazohitajika, pamoja na kwamba bado ipo chini ya kiwango cha utahini, shule nyingi za kata zingekuwa na wanafunzi wachache au kukosa kabisa.
“Uteuzi wa wanafunzi ulifanyika kisiasa ili kuziba mapengo shule za kata na kutowavunja moyo wazazi wa watoto,” alisisitiza.
Naye mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Kioga, Vincent Osinga Mollel, alisema kuwa tatizo hilo ni la kweli kwani wanafunzi wamechukuliwa wakiwa na alama 70 badala ya 100.
“Tunashindwa kuelewa vigezo vilivyotumika, hata hivyo kuna wanafunzi wamepata alama 90 wameachwa huku walio na alama hata chini ya 70 wakichukuliwa suala ambalo limetuletea mgogoro na wazazi ambao tayari wana mpango wa kuandamana kupinga matokeo hayo,” alisema.
Pia walimu wengine wa shule za sekondari katika wilaya za Sengerema, Singida na Geita walisema wanasikitika kuwa wanafunzi waliochaguliwa bado wapo ambao hawajui kusoma na kuandika.
Mwalimu wa Taaluma katika shule ya sekondari ya Buyangu wilayani Sengerema, Enock Boniface, alisema ni hali ngumu kwao kwani baadhi ya wanafunzi waliofika kuchukua fomu za kujiunga na shule hiyo hawajui kusoma na kuandika hatua inayowapa shida.
“Tumepokea wanafunzi wenye sifa, yaani waliopata alama 100 kati ya 250 wapo 27, ila wale ambao wamefeli tumeletewa wanafunzi 49, lengo ni kukidhi idadi ya wanafunzi darasani,” alisema.
Naye mwalimu mwingine ambaye hakupenda kutajwa jina, alisema kuwa kuwa wakati wa uteuzi wa wanafunzi hao walifanya uchaguzi wa wanafunzi katika ngazi za wilaya, lakini baadaye zoezi lilirudiwa kimkoa na lilifanyika Ukerewe.
Mwalimu huyo ambaye alishiriki uteuzi, alisema kuwa walipomaliza kuchagua wanafunzi wenye alama 100 walionekana wako pungufu na hivyo kuketi tena kwa siku tatu, wakirudia upya uteuzi huo hadi kufikia hatua ya kuchukua wale wenye alama 70.
“Tutakuwa tumewapatia walimu wa sekondari kazi sana, maana tumechagua watu ambao wamefeli tukawapitisha kwenda sekondari,” alisema.
Baadhi ya walimu wengine walisema kuwa kuna waraka ambao wamepewa na wizara katika kuwatungia mtihani wa kusoma, kuandika na kuhesabu, hata hivyo walilalamika kwamba wale waliosema hawajui kusoma na kuandika mwaka jana hawakuondolewa shuleni na sasa wataingia kidato cha pili.
Gazeti hili lilimtafuta Waziri Kawambwa kuzungumzia suala hilo lakini akasema yuko katika kikao na hivyo kuomba apigiwe baada ya nusu saa, ila alipopigiwa hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu.
Pia Naibu Waziri, Philipo Mulugo, naye alipokea simu na kuomba aandikiwe ujumbe mfupi lakini hakuweza kuujibu.
Source: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment