MATOKEO ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini Agosti 26 hadi
Septemba 8 mwaka jana, yameonyesha kuwa idadi ya Watanzania imefikia milioni
44,929,002.
Rais Jakaya Kikwete ndiye alitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam
na kuwataka Watanzania kupunguza kasi ya kuzaliana.
Akizungumza katika viwanja vya Mnazi Mmoja wakati wa uzinduzi huo, Rais
Kikwete ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa, alisema kuwa
matokeo ya awali yameonyesha kuwa Tanzania Bara ina idadi ya watu milioni
43,625,434 huku Zanzibar wakiwa 1,303,568.
Alisema kuwa matokeo hayo ni ishara kwamba ifikapo mwaka 2016 kuna uwezekano
wa idadi hiyo kufikia milioni 51 jambo ambalo linaweza kuwa ni mzigo kwa taifa,
jamii na hata katika masuala ya uchumi.
Rais alifafanua kuwa jamii inapaswa kuyachukulia kwa uzito matokeo hayo hasa
katika masuala ya kupanga uzazi pamoja na kuongeza bidii ya kufanya kazi.
“Mikakati lazima ifanyike sasa kuna umuhimu wa kupanga uzazi; Watanzania
wanapaswa kutambua hilo vinginevyo hali ya maisha itashuka,” alisema.
Rais Kikwete alisema kuwa Watanzania wanapaswa kuongeza nguvu ya kufanya kazi
zaidi kwa kuwa idadi imekuwa kubwa na inaongezeka kwa kasi kubwa.
“Kupanga uzazi ni jambo la msingi sana na tuzingatie hayo ili kuweza kupiga
hatua maana matokeo hayo yanaashiria idadi ya watu milioni 10 imeongezeka tangu
sensa ya mwaka 2002 kufanyika,” alisema.
Alisema kuwa matokeo yatakayofuata yatatangazwa Februari ambapo yatatoa idadi
ya wanaume na wanawake na matokeo mengine kutolewa Aprili 2013.
Rais aliongeza kuwa zoezi hilo linagharimu fedha nyingi lakini serikali
inalazimika kufanya kutokana na kutakiwa kupanga sera na mikakati ya maendeleo
ambapo kwa sensa ya mwaka 2012 imegharimu kiasi cha sh bilioni 140 na
zilizotumika hadi sasa ni sh bilioni 124.
“Hata hivyo ninapongeza kukamilika kwa zoezi hili la awali kwani kulikuwa na
purukushani nyingi na maneno mengi ya kutaka kuvuruga…wapo walioendesha na
kuhamasisha wengine wasusie, wapo waliotaka kuendesha maandamano wakati wakijua
ni wakati wa sensa lakini pamoja na mitihani yote tumeweza kupata matokeo,”
alisema.
Alisema sensa hiyo ni ya tano kufanyika tangu Muungano ambapo ya kwanza
ilifanyika mwaka 1967 na idadi ya watu ilikuwa milioni 12,313,469, bara wakiwa
milioni 11,958,654 na visiwani 354,400.
Alisema kuwa sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1910. Sensa nne za mwisho
zilifanyika baada ya Uhuru katika miaka ya 1967, 1978, 1988 na 2002.
Kulingana na sensa ya mwisho iliyofanyika Agosti 2002, idadi ya watu nchini
ilikuwa 34,443,603.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya sensa,
alisema kuwa mchakato huo ulikabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na
watu wanne kupoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa.
Alisema kuwa zaidi ya sh bilioni 90 zilitumika kuwalipa vijana walioajiriwa
wakati wa sensa ambapo vijana 200,000 waliajiriwa katika kuhesabu na 400 wakati
wa uchambuzi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba,
alisema kuwa hoja aliyoitoa Rais Kikwete ni ya msingi hasa katika suala zima la
kupanga uzazi.
Profesa Lipumba alisema kuwa matokeo hayo pia yanatoa fursa kwa serikali
kuhakikisha inajipanga ili kuhakikisha Watanzania wanapata ajira.
Source: Tanzania Daima
|
No comments:
Post a Comment