Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Monday, December 31, 2012

MATOKEO YA SENSA

JK awataka Watanzania kupunguza kasi ya kuzaana
• Watanzania wafikia milioni 44.9
 
 
 
                       
 
MATOKEO ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini Agosti 26 hadi Septemba 8 mwaka jana, yameonyesha kuwa idadi ya Watanzania imefikia milioni 44,929,002.
 
Rais Jakaya Kikwete ndiye alitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam na kuwataka Watanzania kupunguza kasi ya kuzaliana.
 
Akizungumza katika viwanja vya Mnazi Mmoja wakati wa uzinduzi huo, Rais Kikwete ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa, alisema kuwa matokeo ya awali yameonyesha kuwa Tanzania Bara ina idadi ya watu milioni 43,625,434 huku Zanzibar wakiwa 1,303,568.
 
Alisema kuwa matokeo hayo ni ishara kwamba ifikapo mwaka 2016 kuna uwezekano wa idadi hiyo kufikia milioni 51 jambo ambalo linaweza kuwa ni mzigo kwa taifa, jamii na hata katika masuala ya uchumi.
Rais alifafanua kuwa jamii inapaswa kuyachukulia kwa uzito matokeo hayo hasa katika masuala ya kupanga uzazi pamoja na kuongeza bidii ya kufanya kazi.
 
“Mikakati lazima ifanyike sasa kuna umuhimu wa kupanga uzazi; Watanzania wanapaswa kutambua hilo vinginevyo hali ya maisha itashuka,” alisema.
Rais Kikwete alisema kuwa Watanzania wanapaswa kuongeza nguvu ya kufanya kazi zaidi kwa kuwa idadi imekuwa kubwa na inaongezeka kwa kasi kubwa.
 
“Kupanga uzazi ni jambo la msingi sana na tuzingatie hayo ili kuweza kupiga hatua maana matokeo hayo yanaashiria idadi ya watu milioni 10 imeongezeka tangu sensa ya mwaka 2002 kufanyika,” alisema.
 
Alisema kuwa matokeo yatakayofuata yatatangazwa Februari ambapo yatatoa idadi ya wanaume na wanawake na matokeo mengine kutolewa Aprili 2013.
Rais aliongeza kuwa zoezi hilo linagharimu fedha nyingi lakini serikali inalazimika kufanya kutokana na kutakiwa kupanga sera na mikakati ya maendeleo ambapo kwa sensa ya mwaka 2012 imegharimu kiasi cha sh bilioni 140 na zilizotumika hadi sasa ni sh bilioni 124.
 
“Hata hivyo ninapongeza kukamilika kwa zoezi hili la awali kwani kulikuwa na purukushani nyingi na maneno mengi ya kutaka kuvuruga…wapo walioendesha na kuhamasisha wengine wasusie, wapo waliotaka kuendesha maandamano wakati wakijua ni wakati wa sensa lakini pamoja na mitihani yote tumeweza kupata matokeo,” alisema.
 
Alisema sensa hiyo ni ya tano kufanyika tangu Muungano ambapo ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 na idadi ya watu ilikuwa milioni 12,313,469, bara wakiwa milioni 11,958,654 na visiwani 354,400.
 
Alisema kuwa sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1910. Sensa nne za mwisho zilifanyika baada ya Uhuru katika miaka ya 1967, 1978, 1988 na 2002.
 
Kulingana na sensa ya mwisho iliyofanyika Agosti 2002, idadi ya watu nchini ilikuwa 34,443,603.
 
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya sensa, alisema kuwa mchakato huo ulikabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na watu wanne kupoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa.
Alisema kuwa zaidi ya sh bilioni 90 zilitumika kuwalipa vijana walioajiriwa wakati wa sensa ambapo vijana 200,000 waliajiriwa katika kuhesabu na 400 wakati wa uchambuzi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema kuwa hoja aliyoitoa Rais Kikwete ni ya msingi hasa katika suala zima la kupanga uzazi.
 
Profesa Lipumba alisema kuwa matokeo hayo pia yanatoa fursa kwa serikali kuhakikisha inajipanga ili kuhakikisha Watanzania wanapata ajira.
 
Source: Tanzania Daima

'MADUDU' MATOKEO DARASA LA SABA YAFICHULIWA


• Wasiojua kusoma wachaguliwa kujaza shule za kata

WIKI moja tangu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, atangaze matokeo ya darasa la saba na kudai ufaulu umeongezeka, baadhi ya walimu na wazazi wamefichua ‘madudu’ yaliyofanyika kupanga washindi wakidai hatua hiyo itaongeza idadi ya wajinga nchini.
Waziri Kawambwa alisema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao kwa mwaka 2012 kimeongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2011.
Alisema kuwa alama ya juu ya ufaulu kwa wanafunzi wote ni 234 kati ya alama 250 ambapo wasichana wamefaulu kwa wingi zaidi kuliko wavulana kutoka kwenye idadi hiyo ya 865,827 waliofanya mtihani huo.
Hata hivyo, vyanzo vyetu vya taarifa kutoka kwa baadhi ya walimu na wazazi wa wanafunzi hao, vilionyesha kuwa hawakubaliani na maelezo ya Kawambwa ya kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wakati alama zilizotumika kuwachagua washindi zilikuwa chini ya kiwango.
Katika takwimu zilizopatikana kwenye wilaya za Arusha (shule za msingi Kioga na sekondari Ilkiding’a), Sengerema (shule za msingi Buzilasoga, Tamabu Butonga na Buyangu), Bukombe (shule ya msingi Katente), Shinyanga Vijijini, na Singida Mjini (shule za Mungumaji, Mfumbu, Kisasida na Ipungi), kiwango cha ufauli kinatisha.
Akizungumzia matokeo hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Geita (CWT), Dotto Biteko, alihoji ufaulu umeongezeka vipi wakati alama zinazotumika kama vigezo zilishushwa ili kukidhi idadi badala ya kiwango?
Biteko alisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa hawakufikisha alama 100 kati ya 250 kwa masomo yote matano yaliyofanywa na wengi wao wamechukuliwa wakiwa na alama 70 au chini zaidi ya zile zinazohitajika.
Aliongeza kuwa kama waliokuwa wanachagua wanafunzi hao wangezingatia alama 100 zinazohitajika, pamoja na kwamba bado ipo chini ya kiwango cha utahini, shule nyingi za kata zingekuwa na wanafunzi wachache au kukosa kabisa.
“Uteuzi wa wanafunzi ulifanyika kisiasa ili kuziba mapengo shule za kata na kutowavunja moyo wazazi wa watoto,” alisisitiza.
Naye mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Kioga, Vincent Osinga Mollel, alisema kuwa tatizo hilo ni la kweli kwani wanafunzi wamechukuliwa wakiwa na alama 70 badala ya 100.
“Tunashindwa kuelewa vigezo vilivyotumika, hata hivyo kuna wanafunzi wamepata alama 90 wameachwa huku walio na alama hata chini ya 70 wakichukuliwa suala ambalo limetuletea mgogoro na wazazi ambao tayari wana mpango wa kuandamana kupinga matokeo hayo,” alisema.
Pia walimu wengine wa shule za sekondari katika wilaya za Sengerema, Singida na Geita walisema wanasikitika kuwa wanafunzi waliochaguliwa bado wapo ambao hawajui kusoma na kuandika.
Mwalimu wa Taaluma katika shule ya sekondari ya Buyangu wilayani Sengerema, Enock Boniface, alisema ni hali ngumu kwao kwani baadhi ya wanafunzi waliofika kuchukua fomu za kujiunga na shule hiyo hawajui kusoma na kuandika hatua inayowapa shida.
“Tumepokea wanafunzi wenye sifa, yaani waliopata alama 100 kati ya 250 wapo 27, ila wale ambao wamefeli tumeletewa wanafunzi 49, lengo ni kukidhi idadi ya wanafunzi darasani,” alisema.
Naye mwalimu mwingine ambaye hakupenda kutajwa jina, alisema kuwa kuwa wakati wa uteuzi wa wanafunzi hao walifanya uchaguzi wa wanafunzi katika ngazi za wilaya, lakini baadaye zoezi lilirudiwa kimkoa na lilifanyika Ukerewe.
Mwalimu huyo ambaye alishiriki uteuzi, alisema kuwa walipomaliza kuchagua wanafunzi wenye alama 100 walionekana wako pungufu na hivyo kuketi tena kwa siku tatu, wakirudia upya uteuzi huo hadi kufikia hatua ya kuchukua wale wenye alama 70.
“Tutakuwa tumewapatia walimu wa sekondari kazi sana, maana tumechagua watu ambao wamefeli tukawapitisha kwenda sekondari,” alisema.
Baadhi ya walimu wengine walisema kuwa kuna waraka ambao wamepewa na wizara katika kuwatungia mtihani wa kusoma, kuandika na kuhesabu, hata hivyo walilalamika kwamba wale waliosema hawajui kusoma na kuandika mwaka jana hawakuondolewa shuleni na sasa wataingia kidato cha pili.
Gazeti hili lilimtafuta Waziri Kawambwa kuzungumzia suala hilo lakini akasema yuko katika kikao na hivyo kuomba apigiwe baada ya nusu saa, ila alipopigiwa hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu.
Pia Naibu Waziri, Philipo Mulugo, naye alipokea simu na kuomba aandikiwe ujumbe mfupi lakini hakuweza kuujibu.
Source: Tanzania Daima

MAGAZETI YA LEO JUMANNE MWAKA MPYA 01/01/2013





 

             HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI