201
Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu, ambazo ni, Utangulizi, katika sehemu hii tutatoa fasili ya nadharia na fasili ya ngano kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali. Sehemu ya pili itakuwa ni kiini cha swali ambapo tutajikita kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya fasihi simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka (1994/1999) na Finnegan (1970). Na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu, ambazo ni, Utangulizi, katika sehemu hii tutatoa fasili ya nadharia na fasili ya ngano kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali. Sehemu ya pili itakuwa ni kiini cha swali ambapo tutajikita kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya fasihi simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka (1994/1999) na Finnegan (1970). Na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Tukianza
na fasili ya Nadharia, Massamba (2009:63) anasema, nadharia ni taratibu kanuni
na misingi ambayo imejengwa katika muundo wa kimawazo kwa madhumuni ya kutumiwa
kama kielelezo cha kuelezea jambo. Sarantakos (1997: 9) amefasili nadharia kama
jambo linalofanywa na kuthibitishwa kwa utaratibu maalum kwa njia ya utafiti
kwa ajili ya kuelezea jambo fulani katika jamii. Martin E. Amini (2005:10)
anasema nadharia ni jumla ya mambo yote ambayo mtafiti amekusudia kuelezea,
kuchambua, kuelewa au hata kutabiri jambo fulani kwa utaratibu maalum.
Hivyo
basi, nadharia huchukuliwa kama dira au muongozo wa kumuongoza mtafiti/mchambuzi
ili kulielezea vema jambo fulani kwa mtazamo unaotarajiwa kuwa imara zaidi
kuliko mtazamo mwingine. Hivyo tunaweza kujumuisha kuwa nadharia ya fasihi
simulizi ni chombo kinachotoa mwongozo kuhusu mwelekeo wa jamii fulani.
Maana ya ngano
Senkoro
(2011:53) anasema, ngano ni utanzu wa kifasihi simulizi ambao
ulipitishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. King’ei (2005:65)
anasema ngano kuwa
ni hadithi fupi
na zenye masimulizi
yasiyo ya kishairi. Kwa upande wake,Wamitila, K.W.
(2003:165) anasema ngano ni hadithi ya kale ambayo ni moja kati ya tanzu maarufu
za fasili simulizi. Ni moja kati ya
vipera au vitanzu vya hadithi au simulizi. Ngano nyingi huwa na mwanzo wa hapo
zamani za kale.
Kwa
fasili yetu, tunaweza kusema kuwa, ngano ni utanzu wa hadithi fupi fupi ambazo
huelezea/kusimulia matukio mbalimbali yanayoleta mafunzo katika jamii husika na
kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Baada
ya kuangalia fasili mbalimbali za nadharia na ngano, sehemu inayofuata ni
kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya fasihi
simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka (1994/1999) na
Finnegan (1970). Tukianza na Okpewho (1992) ameanisha aina sita za nadharia
zinazoelezea asili ya fasihi simulizi/masimulizi ambazo ni, nadharia ya
mabadiliko, nadharia ya msambao, nadharia ya uamilifu, nadharia ya urasimi,
nadharia ya Saikochanganuzi na mwisho ni nadharia ya Umuundo. Kwa upande wake,
Miruka (1994) ameanisha aina tano za nadharia ambazo ni, nadharia ya
Mabadiliko, nadharia ya msambao, nadharia ya urasimi, nadharia ya uamilifu na
nadharia ya umuundo, wakati Finnegan
(1970) ameanisha aina tatu za nadharia ambazo ni nadharia ya Mabadiliko,
nadharia ya msambao na nadharia ya Umuundo.
Tukiangalia
uanishaji wa nadharia hizo za wataalamu hapo juu, tunaona kuwa, wataalamu hao
wanatofautiana katika idadi ya nadharia hizo, lakini kimsingi wataalamu wote
wanakubaliana kuhusu nadharia fulani fulani, mathalani, wote wanakubaliana
uwepo wa nadharia ya mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya umuundo.
Lakini Okpewho na Miruka wanakubaliana juu ya uwepo wa nadharia ya mabadiliko,
nadharia ya msambao na nadharia ya umuundo, nadharia ya urasimi na nadharia ya
uamilifu. Okpewho anainisha aina nyingine ya nadharia ya Saikochanganuzi ambayo
haijitokezi kwa hao wataalamu wengine. Hivyo katika uwasilishaji wetu,
tutazigawa nadharia hizo katika aina sita kama ifuatavyo:
Nadharia ya wanamabadiliko,
nadharia hii iliasisiwa na Charles Darwin ambaye alikuwa mwana bailojia karne
ya 19, alifanya utafiti kuhusu mabadiliko ya viumbe ambao waliishi miaka
mamilioni iliyopita. Katika utafiti wake aligundua kuwa viumbe walioendelea
kuishi imewezekana tu kwa sababu ya
kumudu mapambano dhidi ya uhaba wa vyakula, hivyo Darwin aliita jambo hili kama
“Uhai kwa wanaofaa”. Pia aligundua viumbe walioendelea kuishi kwa sababu ya
maumbo yao na mazingira yaliyosababisha wao kuwepo.
Mawazo
ya utafiti wa Darwin yalishadadiwa na wanazuoni mbalimbali waliokuwa wanachunguza
utamaduni wa binadamu, katika utafiti wao walikusanya simulizi kutoka jamii
mbalimbali za Afrika, Asia na Amerika ambapo baada ya kukusanya simulizi hizo
waligundua zilikuwa na ufanano wa kimaudhui. Wanamabadiliko wanaamini kuwa
ngano/masimulizi tuliyonayo leo yana asili moja isipokuwa zimekuwa zikibadilika
kutokana na mabadiliko ya wakati. Zaidi ya haya wanamabadiliko wanaamini kuwa
viumbe wote tumetokea kwenye asili moja hivyo tuna uwezo wa akili sawa na
maendeleo tutakuwa sawa.
Ubora wa nadharia hii, nadharia
hii ndiyo msingi wa nadharia nyingine zilizofuata kama nadharia ya msambao,
urasimi na uamilifu. Vilevile imesaidia kuelezea asili ya ngano/masimulizi hasa
ngano zinazofanana kimaudhui, na mwisho nadharia imesaidia kuonesha kuwa ngano
zina asili moja isipokuwa zinabadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na
mazingira.
Mapungufu
ya nadharia hii,
wanamabadiliko waliamini kila kilichokusanywa katika fasihi simulizi
kilihesabika kama masalia ya zamani/mabaki ya fasihi zilizotangulia, kwa maana
kwamba kila kitu kilichosalia kitakuwa na dosari hakiwezi kuwa kitu halisi.
Wanamabadiliko pia wameangalia tu upande wa maudhui na kuacha kipengele cha
fani kama vile muundo na mitindo ya fani husika. Mwisho, pamoja na ufanano wa
huo wa kimaudhui kuwa ngano zina asili moja lakini kuna tofauti kubwa hasa
katika utendaji wa fanani hivyo fanani hutofautiana.
Nafasi
ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili,
nadharia hii inahusiana na ngano za Kiswahili katika sanaa za jadi ambayo ni
elimu inayohusu asili ya binadamu pamoja na umuhimu wake ambao ilihusishwa na
usimulizi wa ngano ambayo ilitokana na jamii husika katika shughuli mbalimbali
za jamii kama vile jando na unyago, miviga, vyanzo vya vyakula, sherehe,
matambiko kwa kutaja kwa uchache.
Nadharia ya msambao,
nadharia hii imeasisiwa na wataalamu kama Jacob na Wilhem Grimm, baadaye mawazo
yao yaliendelezwa na Maxmuller na Mmarekani Stere Thomson. Pamoja na kwamba
kulikuwa na tofauti ndogondogo lakini wataalamu wa nadharia hii wanamwelekeo
mmoja ambao wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ni moja lakini kutokana
na maingiliano ya kijamii ndiyo yaliyosababisha kusambaa kwa hii ngano hasa
kutoka katika jamii zilizostaarabika (Ulaya) kuja katika jamii zisizostaarabika
(Afrika).
Okpewho
anasema, wanamsambao walijishughulisha na kuhusianisha ngano za jamii
mbalimbali na kugundua kuwa ngano zina ufanano unaokaribiana sana. Uhusiano huu
unahusishwa na kipindi cha kihistoria ambacho kulikuwa na mawasiliano baina ya
jamii moja hadi nyingine. Katika utafiti wao wanamsambao wamegawanywa katika
shule mbili, kwanza ni kundi la shule ya India, kundi hili lilianzishwa na
Jacob na Wilhelm ambapo walikusanya hadithi mbalimbali huko ujerumani na
kwingineko barani Ulaya na kugundua kuwa ngano hizo zilikuwa na uhusiano na
kuhitimisha kuwa ngano za Ulaya kama zilivyo lugha za Ulaya zimeonekana na
rangi ya nasaba bora iliyopata kuishi huko kati ya kaskazini na Asia, rangi ya
nasaba bora si rangi ya ngozi bali ni familia ya lugha ambayo lugha zote za
Ulaya zinahusishwa nayo. Hivyo aligundua kuwa ngano zilikuwa zinasambaa na
makundi ya wahamiaji. Wao waliona chimbuko la ngano ni huko India na zikafika
huko Magharibi kwa njia ya msambao.
Kundi
la pili ni kundi la shule ya Kifini, shule hii ilianzishwa na Eliasi Lonnrot
ambaye mwaka 1825 alianza kukusanya ngano za mashujaa katika nchi ya Finland,
kupitia maudhui yanayohusiana na kuziweka katika kundi moja.
Ubora
wa nadharia hii, wanamsambao waliipa hadhi fasihi
simulizi kwa kuchunguza muktadha kwa undani, vilevile, nadharia hii ilionekana
kuwa ni ya kisayansi zaidi, hivyo inaweza kuchunguzika tofauti na
wanamabadiliko kwani akili ya mtu haiwezi kuchunguzika.
Upungufu
wa wa nadharia hii,
kufikiria kuwa ngano zimeenea toka kundi moja la watu hadi kundi jingine,
inaonesha kuwa jamii ya Kiafrika haikuwa na ngano. Nadharia hii inaona kuwa
Afrika haikuwa na ngano kwani ngano zilitoka katika jamii zilizostaarabika
(Ulaya) jambo ambalo si kweli kwani hata kabla ya ujio wa wakoloni Waafrika
walikuwa na ngano zao. Vilevile, licha ya kuipa fasihi simulizi upekee katika
kipengele cha muktadha lakini hawakuchunguza kwa undani vipengele vya kisanaa
vya fasihi simulizi, mfano hawakuangalia vipengele muhimu vya fasihi simulizi
ya Kiafrika hususani sanaa ya jadi kama vile, miviga, jando na unyago,
matambiko, n.k.
Nafasi
ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili,
ukiangalia kwa jicho la ndani nadharia hii inasaidia kutambua kuwa mfanano wa
ngano katika jamii nyingi za kiafrika ulitokana na maingiliano ya shughuli za
kijamii kama vile, biashara, kilimo,ufugaji, uwindaji na kazi mbalimbali za
jamii.
Nadharia ya umuundo,
nadharia hii iliasisiwa na Claude Levis Strauses, alidai kuwa utamaduni
unajumuisha vitu mbalimbali vinavyofanana, alichunguza visasili na kusema kuwa
visasili hivyo vinatumika katika kuelezea na kutatua matatizo katika jamii.
Hadithi hizo zilikuwa zinaelezea falsafa ya jamii husika, alidai kuwa visasili
hivyo vilisaidia jamii katika kuyaelewa na kutatua matatizo ambayo yalileta
mtanziko katika maisha ya binadamu, matatizo hayo ni kama vile, uhai na kifo.
Strauses,
alidai kuwa muhusika wa ngano anajengwa katika kupambana na tatiziko ambalo
anashindwa kulipatia majibu. Dominique Zahen aliongeza kuwa ngano zinahusu uhai na kifo na ziishie kwa kuona
kuwa uhai na kifo vimetoka kwa mungu (mfano: ngano inayoelezea namna kifo
kilivyoingia duniani) (rejea Miruka 1994:138)
Ngano
zinatakiwa kutazamwa kama mfumo wenye kanuni zake ambazo kila msanii anatakiwa
kuelewa pia aelewe mfumo unavyoweza kutumiwa katika mawasiliano na hata
kimuundo. Mfano katika ngano lazima kuangalia matumizi ya lugha na kaida
zinazotawala utunzi huo.
Ubora
wa nadharia hii, nadharia hii inasisitiza kuwepo
kwa kanuni/kaida maalumu za kiutambaji, kiutunzi na matumizi ya lugha. Hapa
wanaona kuwa ngano zisichukuliwe kama kitu pekepeke bali ni utanzu unaoongozwa
na kaida maalumu katika uumbaji, kiutambaji na matumizi ya lugha. Hivyo
kutakuwa na sifa zinazofanana katika ngano zote. Vilevile, inasaidia kujua
chimbuko la ngano katika jamii fulani.
Udhaifu
wa nadharia
hii,
kwanza kwa kutumia nadharia hii hatuwezi kupata kanuni rasmi ya kiutambaji,
kiutunzi na matumizi ya lugha toka jamii moja hadi nyingine. Hii ni kutokana na
ukweli kwamba kila jamii ina namna yake ya kuwasilisha ngano zao, kuziumba
ngano zao na matumizi ya tofauti ya lugha. Mfano; maumbo ya ngano
yanatofautiana toka jamii moja hadi nyingine, mfano, muingiliano wa tanzu moja
katika nyingine, utambaji pia hutofautiana, mfano watambaji na tabaka tawala na
watambaji na tabaka duni. Hata wahusika wa ngano pia hutofautina mhusika
anaweza kuwa mtu duni kwenda bora au mtu bora kuwa mtu duni. Nadharia hii pia
inatalia mkazo muundo kuliko dhima ya ngano katika jamii.
Nafasi ya nadharia
hii katika ngano za Kiswahili, nadhairia inasaidia wanafasihi kutambua/kuelewa
ngano kama utanzu wa fasihi una muundo wake rasmi katika uumbaji, kiutambaji na
matumizi ya lugha kiulemwengu lakini muundo huo si wa kimajumui kwa maana
huweza kutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine.
Nadharia ya urasimi,
nadharia hii iliasisiwa na mwanazuoni wa Kinesi Vladimir Propp (1928,1968)
katika chake cha “The Morphology of the
folktale.” Nadharia hii ilizuka ili kupinga mawazo ya wanamsambao hususani
katika ugawaji wa ngano bila kuchunguza kwa umakini sifa ya kila kundi. Propp
anaamini kuwa ili kuchunguza asili ya ngano ni vema kuanza kuchunguza aina za
ngano kwa kuangalia maumbo ya ngano. Hivyo mtazamo huu unaangalia asili ya
ngano kwa kuchunguza maumbo ya ngano husika.
Ubora wa nadhairia
hii, nadharia hii inasaidia kujua aina za ngano kutokana na dhima zake, mfano
ngano za urafiki, miadi, ukatili, ugunduzi na mwisho wa urafiki, (Alan Dunde’s)
Udhaifu wa nadharia,
nadharia hii inaonekana kutomzingatia mtambaji ambaye ni sehemu ya ngano
yenyewe ambaye anaweza kubadilisha umbo la ngano kadri ya utendaji wake.
Nafasi
ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadharia hii inatusaidia kuziweka
ngano katika makundi kutokana na kazi zake. Mfano tunapata ngano zinazohusu
wahusika wajanja mfano sungura na wahusika wasiowaelevu/wajinga mfano fisi.
Nadharia ya saiko-changanuzi,
muasisi wa Nadharia hii ni Sigmund Freud raia wa Australia, mtaalamu huyu
alikuwa tabibu wa magonjwa ya akili, alifanya uchunguzi wa nafsia, alichunguza
hasa sehemu ya nafsi iliyofichika yaani sehemu ya ung’amuzi bwete ili kujua
asili ya tatizo la mgonjwa husika, alieleza kuwa ung’amuzi bwete ni sehemu ya
akili ya binadamu ambayo huhodhi fikra, mawazo, hofu na mitazamo hasi ambayo
haiwezi kukubalika na jamii. Hofu na mawazo hayo hujitokeza kwa ndoto. Pia
ung’amuzi bwete huhusisha matukio yaliyotendeka zamani lakini mgonjwa
huyaingiza katika maongezi yake kama yanatendeka muda huo. Kutokana na utafiti
wake aligundua kwamba ndoto zote husheheni ukweli kuhusu maisha ya mgonjwa.
Freud
anaifananisha kazi ya fasihi na ndoto kwa kuwa visasili huwa ni hadithi za
kubuni basi ubunifu huo unashabihi ndoto kwani wahusika wake na maudhui yake kwa ujumla huwa katika ulimwengu wa kufikirika
ambao ni kama ndoto katika ulimwengu halisi sawa sawa na mgonjwa wa akili
anayeumba ulimwengu wake.
Freud
alisisitiza mambo yote katika akili ya binadamu yanatawaliwa na ngono (libido).
Mawazo yake yaliungwa mkono na mwanafunzi wake Carl Gustav Jung ambaye pia
alifanya kazi pamoja na Freud katika kuwatibu wagonjwa wa akili kwa kutafsiri
ndoto ingawa Gustav alitofautiana na Freud kwa msimamo wake kuwa akili ya
binadamu inatawaliwa na ngono.
Carl
Gustav Jung alifanya utafiti na kuunda dhana ya kikale ambayo ni mtiririko au
picha kongwe inayojitokeza mara kwa mara katika tajriba anayopitia mwanadamu ,
alisema kuna sehemu ndani ya akili isiyokuwa na fahamu ya mtu mwenyewe lakini
ina athira kubwa juu ya mawazo na matendo yake. Alitofautisha sehemu hiyo kama,
sehemu ya kwanza ni sehemu binafsi inayofunza maarifa yaliyokusanywa na kila
mtu katika maisha yake na sehemu ya pili ni sehemu ya kijamii inayofunza
maarifa ya kibinadamu yaliyokusanywa na watu katika historia yao na kuendelezwa
kwa karne nyingi. Anasema sehemu hii husika na matambiko muhimu ambayo mtu
anapitia kama sherehe za kumpa mtu jina, sherehe za kuingia jandoni na
unyagoni, sherehe zinazoigizwa wakati wa ndoa na hatimaye sherehe zinazohusu
maziko ambazo sherehe zote hii ndizo huibua ngano.
Gustav
alifafanua kwa undani masuala ya ngano katika tamaduni mbalimbali za dunia.
Hivyo Freud na Gustav wanasema masimulizi ni kama ndoto au mvurugiko wa akili
kwani picha, taswira na maudhui vyote ni vya kubuni havitoki katika ulimwengu
halisi.
Ubora wa Nadharia hii,
Nadharia hii inaonesha utofauti wa msimulizi mmoja hadi mwingine hutokana na
historia ya mtu binafsi na uwezo wake binafsi hata kama kisa kitakachosimuliwa
ni kimoja, hii imedhihirishwa kwa wagonjwa waliokuwa wanasimulia mambo yao kwa
utofauti kutokana na historia zao. Lakini pia imesaidia kutuonesha chimbuko la
ngano kwa miktadha tofauti tofauti kama sherehe za jando na unyago, sherehe za
kutoa jina, n.k.
Upungufu wa Nadharia
hii, Nadharia hii imesisitiza zaidi masuala ya hisia za kingono katika ubunifu
wa masimulizi kitu ambacho hakina ushahidi wa kutosha kwani siyo kila hadithi
inatarajia kujiridhisha kutoka hali ya ngono iliyofifizwa katika ung’amuzi
bwete kama anavyosema Freud.
Nadharia ya kiuamilifu,
Nadharia hii iliasisiwa karne ya 20 na Poland Bronislav Malinowsk. Uamilifu
uliibuka kama njia yal kuyatazama maisha na utamaduni wa jamii, kwa kuchunguza
dhima za vipengele vya kijamii pamoja na njia ambazo kwazo dhima hizi
zinahakikisha uwepo wa jamii. Malinowsk alifanya utafiti Australia na kugundua
kuwa ngano ni kumbukumbu za kweli za mila na desturi za jamii zilizopita,
unyago, jando, mazishi, harusi, tohara, matambiko, kusalia miungu, n.k.
Ubora wa Nadharia hii,
Nadharia hii imesaidia kuondoa mawazo kuwa chimbuko la fasihi mbalimbali
zikiwemo ngano ni mahali fulani bali ni kila jamii imekuwa na simulizi ambazo
zinasawiri tajriba (uzoefu) wao wa kila siku katika Nyanja mbalimbali kama
vile, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii. Vilevile Nadharia hii,
inatusaidia kujielewa na kuzielewa jamii zetu vizuri, kwa kuyaelewa mazingira
ya mila na desturi zetu katika jimii.
Nafasi ya Nadharia
hii katika ngano za Kiswahili, inatusaidia kujua tamaduni zetu katika somo la
ngano, pia inatusaidia kujua kuwa kila jamii ilikuwa na tamaduni zao zenye
kuwaongoza katika maisha yao ya kila siku kama vile, jando na unyago, harusi,
matambiko, mazishi, miviga, kusalia miungu kuwa ndiyo chimbuko la ngano.
Hitimisho,
kila nadharia tuliyoiangalia ina umuhimu wake katika kujifunza chimbuko la
ngano, hivyo ni muhimu kila mwanataaluma wa ngano kuzisoma na kuzielewa nadharia
zote zinazozungumzia chimbuko la ngano kwa sababu kila nadharia ina misingi
yake ambayo kwa namna moja ama nyingine inatusaidia kujua na kuelewa chimbuko
la ngano, Nadharia hizi ni muhimu pia kujifunza kwa sababu kuanzishwa kwa
nadharia inategemea na upungufu unaojitokeza katika nadharia nyingine. Kwa
ujumla licha ya mtenguo wa nadharia moja dhidi ya nyingine tunaona kuwa
Nadharia hizi zinakamilisha, Nadharia moja inakamilisha Nadharia nyingine. Kwa
maana hiyo, hatuwezi kujua au kuthibitisha chimbuka la ngano kwa kutumia
nadharia moja.
MAREJEO
Finnegan, R. (1976) Oral Literature in Africa. Oxford University Press. Nairobi.
Kingei, K na Kisovi, C (2005), Msingi wa
Fasihi simulizi. Nairobi:
Kenya Literature
Bureau.
Martin E.Amin (2005),Social Science Researc
Conception,Methodology and
Analysis.Makerere
University
Massamba
(2009:63) Kamusi ya isimu na lugha, Falsafa ya Lugha. Dar es salaam.TUKI.
Mhando,J. na Balisidya,
N. (1976) Fasihi , Tanzania
Publishing House, Dar es salaam.
Miruka,
O.S. (1994) Encounter with Oral
Literature, East African Educational
Publisher.Nairobi. Kenya.
Muhando,
P & Balisidya, N (1976) Fasihi na
Sanaa za Maonyesho. Tanzania Publishing
House(TPH)
Dar es Salaam.
Mulokozi,
M.M. (1989:5) “Tanzu za Fasihi Simulizi”
Katika MULIKA Na. 21, D.SM. TUKI
Nkwera,
F.V. (xx) Tamrini za Fasihi Simulizi:
Sekondari na Vyuo, Dar es Salaam: Business Printers Limited
Okpewho, I. (1992) African Oral Literature. Backgrounds,
Character, and Continuity.
Indiana University Press: USA.
Sarantakos. S.(1997), Social Research. (2nd Edition)
Palgrave Publisher Ltd (Formerly
Macmillan
Press Ltd)
Senkoro, F.E.M.K (2011) Fasihi.
KAUTITU Limited. Dar es salaam.
Wamitila.
K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi Istilahi na
Nadharia. Focus Books.Nairobi.
Kazi hii imeandaliwa kwa pamoja na wanafunzi wa mwaka wa kwanza UDSM: M.A. Kiswahili.
2014/2015 wafuatao
VENANCE, Furaha , ASIFIWE, Eliudy Mwagike, FESTUS M.H. Stephano, NGANILE, Kyamba, MARGARETH, Waivyala,PELLA, NATHAN DANIEL na BIBIE MOHAMED NASSOR
Mwandishi anapatikana kwa namba zifuatazo:
0715 33 55 58
No comments:
Post a Comment