Mwaka 2015
Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi, ambapo katika sehemu hii, tutaangalia maana ya sitiari, ishara na maana ya ngano, sehemu ya pili ni kiini cha swali, hapa tutaangalia sitiari na maana zake na ujumbe unaotokana na sitiari hizo, pia tutaangalia ishara maana zake katika ngano na ujumbe unaotokana na ishara hizo. Na sehemu ya mwisho ni hitimisho na kiambatanisho cha ngano tulizozitumia kama mifano katika kazi yetu (kiambatanisho hicho kinapatikana kuanzia ukurasa wa 8-20.
Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi, ambapo katika sehemu hii, tutaangalia maana ya sitiari, ishara na maana ya ngano, sehemu ya pili ni kiini cha swali, hapa tutaangalia sitiari na maana zake na ujumbe unaotokana na sitiari hizo, pia tutaangalia ishara maana zake katika ngano na ujumbe unaotokana na ishara hizo. Na sehemu ya mwisho ni hitimisho na kiambatanisho cha ngano tulizozitumia kama mifano katika kazi yetu (kiambatanisho hicho kinapatikana kuanzia ukurasa wa 8-20.
Utangulizi
Kabla
hatujaingia katika kiini cha swali letu, kwanza tuangalie maana ya istilahi
muhimu katika mada hii. Tukianza na maana ya Sitiari, Mulokozi, M.M. na Kahigi,
K.K. (1979:38) wanasema sitiari ni tamathali ambayo athari yake hutegemea
uhamishaji wa maana na hisi kutoka katika kitu au dhana moja hadi kitu au dhana
nyingine tofauti. Vitu hivyo viwili vyenye kuhusishwa kwa kawaida huwa havina
uhusiano wa moja kwa moja.
Wamitila,
K.W. (2003:202) anasema, Sitiari ni tamathali ya semi ielezeayo sifa za kitu
Fulani kwa kusema kingine anaendelea kufafanua kuwa, sitiari huhusisha vitu
viwili ambavyo ni tofauti kitabia na kimaumbile.
Mulokozi,
M.M. (2002:171) Sitiari ni tamathali ya semi (maneno,kirai au miundo)
inayotumika kuumba picha fulani inayoamsha mwitiko fulani kutoka kwa hadhira.
Method,
S. (2013:97) anasema, tamathali hii ya usemi huitwa pia istiara, istiari au
jazanda. Tamathali hii haina tofauti na tashibiha, kwani kama ilivyo tashibiha,
sitiari pia hulinganisha vitu viwili. Tofauti pekee ni kuwa, katika sitiari,
vitu tofauti hulinganishwa kana kwamba ni vitu vilivyo sawa kabisa.
Hivyo,
kwa ujumla tunaweza sema kuwa, sitiari ni tamathali ya semi inayozungumzia kitu
au dhana moja huku ikimaanisha kitu au dhana nyingine. Mfano wa sitiari ni kama
vile, baba ni simba, juma amepata jiko. Dunia mti mkavu.
Maana
ya ishara
Mulokozi,M.M.(1979:39) wanasema ishara
ni sitiari ambamo kitu kimoja kinawakilisha kitu kingine kwa sababu ya
kuhusiana nacho. Wamitila,K.W. (2003:68) anasema, isharahutumiwa kuelezea kitu
fulani katika kazi ya kifasihi ambacho huwakilisha kitu kingine. Kuwakilisha
huku kuaweza kutokana na uhusiano uliopo kati ya vitu hivyo viwili au uwezo
wake wa kuibua fikra fulani katika akili ya msomaji.
Kwa
ujumla tunaweza sema kuwa, ishara ni matumizi ya kitu, dhana, au kitendo
kuwakilisha jambo au kitu kingine. Mfano wa ishara ni kama vile:
Maji.....................uhai
Damu...................kifo/machafuko
Bundi...................uchuro/mikosi
Paka
mweusi.........ushirikina
Milima
na mabonde.....matatizo au vikwazo
Kitu
muhimu katika ishara ni kuwa, maana ya ishara zinafungamana na utamaduni wa
jamii husika, hivyo ishara huweza kuwa, matendo, vitu au dhana ambazo hutumika
na jamii wa utamaduni fulani kuashiria matendo, vitu au dhana fulani. Kwa maana
hiyo basi ishara za jamii moja zinaweza kutofautiana na ishara za jamii
nyingine. Ikumbukwe kuwa, matendo, dhana au kitu kinapotumika kuwakilisha
matendo, vitu au dhana fulani hiyo ni ishara wakati matendo, vitu au dhana
fulani inapotumika kwa kufananishwa au kuhusishwa na sifa au tabia na dhana,
kitu au matendo mengine hiyo ni sitiari.
Maana
ya ngano
Senkoro (2011:53) anasema, ngano ni utanzu wa kifasihi simulizi ambao
ulipitishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. King’ei (2005:65) anasema
ngano kuwa ni
hadithi fupi na
zenye masimulizi yasiyo
ya kishairi. Kwa upande
wake,Wamitila, K.W. (2003:165) anasema
ngano ni hadithi ya kale ambayo ni
moja kati ya tanzu maarufu za fasili simulizi.
Ni moja kati ya vipera au vitanzu vya hadithi au simulizi. Ngano nyingi
huwa na mwanzo wa hapo zamani za kale.
Kwa
fasili yetu, tunaweza kusema kuwa, ngano ni utanzu wa hadithi fupi fupi ambazo
huelezea/kusimulia matukio mbalimbali yanayoleta mafunzo katika jamii husika na
kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Kiini
cha swali
Tunakubaliana na hoja hii inayosema
kuwa, bila kuelewa sitiari na ishara katika ngano ni vigumu kumuuliza mtoto
hadithi hii amejifunza nini? Ni hii ni kwa sababu ngano/hadithi nzima hujengwa
na sitiari na ishara ambazo kama hazitaeleweka vizuri itakuwa vigumu kuielewa
ngano husika inahusu nini. Hivyo katika sehemu hii tutaangalia baadhi ya
sitiari na ishara zinazojitokeza katika baadhi ya ngano na kuzitolea maana zake
na jinsi tunavyoweza kupata ujumbe kutokana na kuzielewa sitiari na ishara
hizo, lakini kabla hatujajikita huko tuangalie mifano ya ngano tutakazozitumia
katika mjadala wetu. (rejea Kiambatanisho cha ngano kuanzia ukurasa wa 8-20.
Sitiari katika ngano, katika ngano
sitiari huweza kujitokeza kwa namna tatu, kwanza huweza kujitokeza kwa wahusika
wanaotumika kisitiari. Mulokozi na Kahigi (1979:39), wanaziita sitiari za aina
hii kuwa ni istiara, ambapo muhusika au wahusika wakuu katika hadithi huweza
kuwa ni mwakilishi wa tabia na vitendo vya kundi fulani la watu. Njia ya pili
ni kwa njia ya hadithi nzima, hapa ni kwamba hadithi nzima hujengwa kisitiari,
kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho wa hadithi na matukio yanayoambatana na
matendo katika ngano hujengwa kwa kuhusishwa au kufananishwa na matendo au
matukio katika ulimwengu halisi. Na njia ya tatu kwa kwa kutumia matumizi ya
lugha, yaani vitu viwili tofauti hufananishwa au kulinganishwa bila kutumia
maneno ya kuanganisha. Mfano, matumizi ya sentensi kama vile, baba ni simba,
dunia uwanja wa fujo, kilimo ni uti wa mgongo wa taifa, maji ni uhai n.k.
lakini kwa kiasi kikubwa sitiari katika ngano hujitokeza katika njia mbili
yaani njia ya kwanza na njia ya pili ambazo ndizo tutazitumia. Katika mifano
tuliyoitoa (rejea Kiambatanisho cha ngano kuanzia ukurasa wa 8-20.) sitiari
zinazojitokeza hapo ni:
Sungura
amatumika kisitiari kwa kufananiishwa na mtu mwenye tabia za ujanja na hila,
kwa mfano katika hadithi ya CHUI,
PONGO,SUNGURA NA BUIBUI tunamuona Sungura akitumia ujanja kuwaokoa watoto
wa Pongo wasiuwawe na Chui, lakini pia tumwona Sungura akitumia ujanja huo huo
kujinasua kutoka katika hatari ya kukamatwa na Chui. Hadithi nyingine
zinazomtumia Sungura kisitiari kumfananisha na mtu mwenye tabia za ujanja
ujanja ni hadithi ya, Sungura na Fisi,
Sungura Aoa pia angalia hadithi ya
Je, Kuna Wema Duniani?
Funzo:
katika hadithi hizi, kutumika kwa Sungura kisitiari, ukimuuliza mtoto hadithi
hii inatufunza nini? Atakwambia kuwa, tunajifunza kuwa kutumia akili katika
kukabiliana na matatizo katika jamii ni njia bora kuliko kutumia nguvu.
Chui
pia
katika hadithi hiyo ametumika kisitiari kuwakilisha tabia za watu wabinafsi,
wanaotumia nguvu walizonazo kuwaonea watu wanyonge, lakini pia kuwakilisha
tabia za watu wanaotumia nguvu kuliko akili katika kufanya maamuzi. Katika
hadithi hiyo, tunamwona Chui akitumia hila kuwachukua watoto wa Pongo ili
awafanye kitoweo. Lakini pia anaonesha tabia za watu wabinfsi kwani kwa
kumuonesha kuwa anapenda kuwafanyia ubaya wenzake lakini anapofanyiwa yeye huwa
mbogo.
Funzo,
funzo tunalolipata kutokana na Chui kutumika kisitiari, tunajifunza kuwa, ubaya
mwisho wake ni aibu, ujumbe huu tunaupata kutokana na kitendo cha Chui
kumfanyia ubaya Pongo kwa kuwachukua watoto wake kuwa kitoweo lakini mwisho
wake watoto wanaofanywa kitoweo ni watoto wake mwenyewe na hivyo kuishia katika
aibu, lakini pia tunapata ujumbe mwingine kuwa tenda wema kadili na wewe
unavyotaka kutendewa wema, tunamwona Chui akiwatendea wenzake ubaya lakini
anapotendewa ubaya anakuwa mbogo na hii kufanya ionekane kuwa mkuki kwa nguruwe
kwa binadamu mchungu.
Fisi pia ni mnyama
mwingine anayetumika kisitiari katika ngano nyingi za Kiswahili kuwakilisha
tabia za watu waroho, walafi, wajinga au wapumbavu katika jamii, kwa mfano
rejea hadithi ya Sungura Aoa. Katika
hadithi hii tunamwona fisi akiwa na tabia za kiroho na wizi, akiiba mbuzi wa
binadamu na kuwasingizia wenzake lakini kutokana na ujinga wake hila zake hizo
zinagunduliwa na Sungura.
Funzo tunalolipata
kutokana na hadithi hii ni, tama mbele mauti nyuma, tunamwona Fisi tamaa yake
humwingiza katika matatizo na kukosa mke.
Dege
katika hadithi ya DEGE pia ametumika kisitiari katika hadithi hiyo akihusishwa
na watu wenye kukemea uovu unaofanyika sirini, pia kubashiri matukio ya mbele,
pia katika Hadithi ya Mama Mgumba tunamwona
ndege huyo akitoa siri ya Mama Mgumba aliyoitoa kwa rafiki yake jinsi
alivyopata mtoto.
Funzo tunalolipata
hapa, ni kuwa duniani hakuna siri ya watu wawili. Unapokuwa na jambo ambalo
unaona halitakiwi kujulikana na watu wengine ni vema siri hiyo ukabaki nayo
mwenyewe kuliko kumweleza mtu mwingine. Akiingilia mtu wa pili hiyo siyo siri
tena.
Mfalme
katika hadithi ya Saidi na Rafiki yake
Muhamed pia kuna sitiari za wahusika zinajitokeza, kwa mfano, Mfalme,
ametumika kisitiari akihusishwa na viongozi wabinafsi, na wenye tama ya kupata
kila kitu kwa nafasi zao, lakini tabia
yake ya hiyo inamponza mfalme kwa kurubuniwa na Muhamed na hatimaye Mfalme
ananyongwa yeye. Hivyo kutokana na maana hiyo ya sitiari, ukimuuliza mtoto,
hadithi hii inatufundisha nini, atakwambia kuwa, hadithi hii inatufundisha
kuwa, tamaa mbele mauti nyuma. Kwa mfano tunamuona Mfalme, tamaa yake ya kutaka
kwenda peponi kama alivyodanganywa na Muhamed inasababishwa Mfalme ananyongwa
na kufariki.
Muhusika
Kichwa kidogo katika hadithi hiyo hiyo ya Saidi
na Rafiki yake Muhammed pia ametumika kisitiari akihusishwa na watu
wanyonge, watu wanaokandamizwa katika jamii kutokana unyonge wao wa kutokujua
sheria, kwa mfano tunaona Kichwa Kidogo ni mtu mnyonge hana hasiyekuwa na hatia
lakini hakimu anataka kumdhulumu haki yake kwa sababu ya maumbile yake tu.
Lakini Kichwa kidogo hanasi kitanzini anatoka na kuokoka.
Baada
ya kupata maana ya sitiari hii, ukimuuliza mtoto hadithi hii inatufundisha
nini, mtoto atakujibu kuwa hadithi hii inatufundisha, fimbo ya mnyonge hulipwa
na Mungu.
Hakimu
pia katika hadithi hiyo, ametumika kisitiari akihusishwa na mahakimu au
wawakilishi wa mfumo ambao unaendeshwa na watu wasio na elimu na waliojaa inda,
choyo na dhuluma. Kwa mfano katika hadithi hii ya Saidi na Rafiki yake Mohammedi. (Uk. 13-14) hakimu anamuhumu Kichwa
kidogo kunyongwa hadi kufa ili hali hajafanya kosa lolote.
Kwa
sitiari hii ukimuuliza mtoto hadithi hii inatufundisha nini, atakujibu kuwa
hadithi hii inatufundisha kuwa si kila anayehukumiwa kufungwa jela ana hatia,
wengine hufungwa kutokana na uelewa mdogo wa watu waliopewa dhamana ya
kusimamia sheria, lakini inda na dhuluma.
Sitiari
nyingine zinazojitokeza katika ni safari,mabonde, mito, misitu na nyika. Safari
katika ngano hutumika katika ngano kuhusisha na mchakato wa makuzi, yaani
kuzaliwa, kukua hadi kufa, wakati, mabonde, mito, misitu na nyika huusishwa na
matatizo au vikwazo katika maisha, ambavyo binadamu anatakiwa kivivuka ili
kupata mafanio. Kwa mfano rejea hadithi ya “DEGE” (uk. na KAZI KWA MFALME
Kwa
sitiari hizi, ukimuuliza, mtoto hadithi hii imetufundisha nini, atakujibu kuwa
hadithi hii inatufundisha kuwa maisha ni safari ndefu iliyojaa changamoto na
vikwazo vingi ambavyo hatuna budi kupambana navyo ili kufanikiwa katika maisha.
Funzo
lingine tunaloweza kulipata kutokana na sitiari ya safari, mabonde, mito, misitu na nyika ni kuwa, mtaka cha uvunguni sharti ainame, hii ina maana muwa
mtu kama unataka mafanikio katika jambo lolote basi mtu huyo hana budi
kuvumilia shida, matatizo na vikwazo vyote atakavyokumbana navyo na si kukata
tamaa.
Matumizi
ya Ishara.
Baada ya kuzivunja na kuzifafanua
sitiari na jinsi tunavyoweza kupata ujumbe kutokana na sitiari hizo sasa
tuangalie ishara, hapa pia tutaangalia maana ya ishara kama zilivyojitokeza katika
ngano tunazozitumia lakini pia tutaeleza kwa namna gani mtoto anaweza kupata
funzo kutokana na kuzielewa ishara hizo. Tukianza na;
Bundi, bundi hutumika
kiishara kuashiria uchuro, mikosi, ushirikina, kwa mfano katika hadithi ya “Je, Duniani kuna Wema?” tunamuona
muhusika baba mmoja kabla hajaenda kutafuta chakula usiku anasikia sauti ya bundi, ambaye anaashiria
balaa, nuksi au mikosi na huko mbele ya safari huyo baba anakutana na balaa la
kutaka kuuwawa na jinni aliyekuwa amehifadhiwa kwenye chupa.
Matumizi
ya ishara kama hizi, mtoto akizielewa maana yake na ukamuuliza hadithi hii
inatufundisha nini? Atakujibu kuwa hadithi hii inatufundisha kuwa dalili ya
mvua mawingu, hivyo tunapoona dalili fulani ni bora kuchukua hatua mapema kabla
ya hatari kutokea.
Chupa, katika hadithi
hiyo, “Je, Duniani kuna Wema?” imetumika
kiishara kuashiria gereza au kifungo. Na tunamuona jini akiwekwa ndani ya chupa
kutokana na uovu aliomfanyia bosi wake. Lakini jini huyo anapookolewa na
binadamu kwa kutolewa ndani ya chupa jini linataka kumuua binadamu kwa kutaka
kumfanya kitoweo.
Funzo,
matumizi ya ishara ya chupa, na jini kuwekwa ndani ya chupa ni ishara inayotupa
funzo kuwa, dawa ya moto ni moto, ikiwa na maana kuwa haifai kuwahurumia watu
wanaohalifu sheria katika jamii, sharti wapewe adhabu kali kama tulivyoona
adhau aliyopewa jini.
Safari,
katika hadithi ya DEGE na ‘Saidi na
rafiki yake Muhamed’ pia imetumika kiishara, safari imetumika kiishara
kuashiria kuwa maisha ni safari ndefu yenye vingi vikwazo, kwa mfano katika hadithi
ya ‘Saidi na rafiki yake Muhammed’ tunawaona akina Saidi wakisafiri kwa nia ya
kutafuta elimu na katika hadithi ya DEGE tunamwona kijana akitoka nyumbani na
kusafiri kwa lengo la kutafuta binti ampendaye (Kipepeo) .
Funzo,
hadithi hii inatufundisha kuwa, elimu ni ufunguo wa maisha hivyo tunakiwa
kuitafuta popote pale inapoweza kupatikana ili iweze kutusaidia katika maisha
yetu. Lakini pia funzo lingine tunaloweza kulipata hama ni kuwa mtaka cha
uvunguni sharti ainame, ikiwa na maana kuwa jambo lolote tunalolitafuta ili
tuweze kulipata hatuna budi kuvumilia shida, matatizo na vikwazo mbalimbali.
Hadithi nyingine zinazotumia safari kama ishara ni pamoja na Kazi kwa Mfalme, Kitambi cha Pembemauli,
n.k.
Mifupa,
maji na maziwa, pia hutumika kiishara kuashiria uhai,
katika ngano nyingi za Kiswahili mifupa, maji au maziwa ni vitu vinavyotumika
kiishara kuashiria uhai, kwa mfano katika hadithi ya “Mama Mgumba” mama Mgumba anapewa masharti na bibi Kizee ili aweze
kupata mtoto achukue mfupa na kuuweka kwenye chungu na kuumwagilia maziwa, Mama
Mgumba anapofanya hivyo anapata mtoto.
Kilemba pia katika
hadithi ya “Kazi Kwa Mfalme.”
Imetumika kiishara, atakayeweza masharti ya mfalme, mfalme atavua kilemba, hapa
kilemba kinaashiria Utawala au uongozi. Na katika hadithi hiyo, mtoto
anafanikiwa kwenda kuwatafuta ndugu zake na kuweza kujibu vitendawili vyote
alivyotegewa na Mfalme na mfalme kumpa kilemba kama ishara ya kuumpa uongozi.
Funzo:
kama mtoto ataulizwa hadithi hii inatufundisha nini? Anaweza kujibu kuwa hadithi
hii inatufundisha kuwa baada ya dhiki faraja. Pamoja na matatizo ya kuwapoteza
ndugu zake, wazazi kuwapoteza watoto wao hatimaye baadaye familia inaungana na
kuishi maisha ya raha na faraja.
Vilevile
kitendo cha jini kuokolewa kutoka ndani ya chupa na binadamu na kutaka kumuua
binadamu kwa kumfanya kitoweo na kitendo cha binadamu kuokolewa na Sungura
asiuawe na Jini lakini baada ya kuokolewa anaamua kumuua Sungura na kumfanya
kitoewo ni kitendo cha kiishara linachoashiria kutendeana wema na tusifanyiane
ubaya. rejea shairi la “Je, Duniani kuna
Wema?”
Funzo,
funzo tunalolipata hapo ni kuwa shukrani ya punda mateke au tenda wema nenda
zako usingoje shukrani. Na hii inatokana na sababu kuwa Jina anataka kulipa
ubaya kwa wema aliofanyiwa vilevile Sungura anafanyiwa ubaya kwa wema
aliomfanyia binadamu.
Hitimisho
Kama tulivyoona katika sehemu
iliyotangulia, tumeziona sitiari na ishara jinsi zinavyoweza kutumika na maana
zake, na matumizi ya sitiari na ishara katika ngano hutumika ili kuepusha
udhibiti wa jamii, kuepusha migogoro katika jamii ambayo ingeweza kutokea kama
ngano zingekuwa zinaelezea mambo waziwazi, vilevile hutumika kuifikirisha
hadhira iweze kufikiria na kutafakari yale yanayojitokeza katika ngano na hivyo
kukuza uelewa wao na uwezo wa kudadisi lakini pia matumizi ya sitiari na ishara
huijengea jamii utu.
KIAMBATANISHO CHA NGANO
ZILIZOTUMIKA KAMA MIFANO
CHUI,
PONGO,SUNGURA NA BUIBUI
Nakandai!
Nakaicha
Hapo
zamani sana chui, pongo, sungura na buibui walikuwa marafiki, wakubwa. Siku
moja chui alitaka kwenda kuwatembelea wazazi wake. Kabla ya kuondoka lakini
aliwatwaa watoto wa Pongo na kuwafunga katika pakacha. Kasha akawaita Pongo,
Sungura na Buibui na kuwaambia, “Leo ninakwenda kuwaamkia wazazi wangu. Hivyo
ningependa mje pamoja name.” Wote wakakubali.
Wakaanza
safari yao huku Pongo amelibeba lile pakacha.walipokuwa njiani walikutana na
watu, wa wakamsalimia Chui.
“Mama
Chui, HUJAMBO?” Chui akaitika, “Sijambo, wenzangu. Ila ninawadanganya wajinga ,
waliopeleka wenzao kuliwa.” Kusikia jibu hilo Sungura akauliza, “Maana yake
nini Chui kusema hivyo?” basi, akawaomba Pongo na Buibui kwa siri, “Tufungue
pakacha, tuone kilichomo.” Kwa hiyo wamwacha Chui atangulie.
Chui
alipotangulia kidogo kulingana na desturi yake ya kujidai ukubwa, Sungura na
wenzake walifungua pakacha. La haula! Ni watoto wa Pongo ndani: wote hai. Pale
pale Pongo aliwachukua watoto wake na kuwaficha. Kasha aliwaendea watoto wa
Chui na kuwaambia, “Twendeni haraka, mama yenu anawaita.” Akawaleta hadi kwa
Sungura na Buibui. Buibui mara ile akawatia watoto wa chui katika pakacha ,
akalifunga imara kama alivyofunga mama Chui hapo awali.
Kasha
fanya hivyo Pongo, Sungura na Buibui wakapiga mbio hadi kumfikilia Chui.
Wakaendelea na safari huku wanapigiana vitendawili.
Baada
ya muda walikutana tena na watu. Wale watu walipomsalimia chui, mama Chui
aliitikia kwa kauli ile ile yake. “Ninawadanganya wajinga , waliopeleka wenzao
kuliwa .” Watu hao walipomsalimai Sungura, Sungura alijibu, “Nitambua kilichomo
katika pakacha ambalo sikulifunga .” naye Pongo aliposalimiwa alijibu, “Hatua
moja kuficha watoto, ya pili kuchukua watoto, ya tatu kati ya wenzangu.” Naye
Buibui alijibu, “Ninaufunga mzigo kama aliyeufunga.”
Waliendelea
na safari. Jioni jioni walifika nyumbani kwa wazazi wa Chui. Wageni wote
walipokelewa vizuri sana. Wakaonyeshwa kibanda pa kujipumzishia. Alivyojidai ni
mjanja sasa, baada ya kupumzika kidogo tu, Chui alimwambia Sungura, “Nenda kwa
mama yangu na mweleze apike nyama iliyomo katika pakacha bila wasiwasi.”
Mama
chui alipokea pakacha, akasikiliza na maelekezo ya Sungura aliyoagizwa na Chui.
Haraka bila kusita, Chui mzee akalitenga pakacha jikoni. Nyama ikatokota. Kisha
akalifungua pakacha. “Loo!” alishangaa Chui mzee. Akamuliza Sungua, “Mbona hii
nyama inafanana na watoto wa Chui?” Sungura akajibu, “Ndivyo yeye
alivyoniagiza. Pika tu wala usisitesite.”
Hata
chakula kilivyokuwa tayari wageni wote walikaribishwa mezani. Sima na nyama
mbele yao. Baada ya kula tonge mbili tatu Sungura akasema, “Ama kweli watoto wa
Chui watamu sana.” Chui akagutuka, “Umesemaje, Sungura?” Sungura akaitika,
“Nasema hivi: Ama kweli nyama ya chumvi tamu sana.” Wakaendelea kula.
Punde
si punde Sungura akatamka tena, “Utadhani tunakula nyama ya Pongo, kumbe vitoto
vya mama chui.”
Hapo
mama Chui alichukua kipande cha nyama na kukiangalia vizuri. La haula! Ni
kichwa cha mwanaye. Vurumai na rabsha zikaanza mara. Buibui alipanda haraka
kwenye paa la nyumba. Pngo na Sungura wakakurupuka nje, mbio. Chui akawaandama
hawa wawili. Ndipo Pongo akakimbilia upande mmoja na sungura upande wa
pili.Chui akaamua kumfuata Sungura. Sungura alipiga chenga huku na kule mpaka
mwisho akawa karibu akamatwe. Kwa bahati njema Sungura akaona, mara akajitia
ndani.
Karibu
na hilo shimo kulikuwa na mzee Chura. Kuona Chui jinsi alivyohangaika sana,
Chura alimpa Chui ushauri, “Mama Chui, hivi hivi tu huwezi kumpata Sungura .
bali ukalete jembe pamoja na moto kishaye chimba na kulifukizia moshi. Haraka sana moshi
utamtoa Sungura nje.”
Shauri
hili lilimpendeza sana mama Chui. Akamwambia Chura, “Tafadhli nilindie hili
shimo, nikachukue haraka jembe na moto.”
Chui
alipoondoka, Sungura alichungulia mlangoni na kumwangalia Chura. Kisha
akamwambia, “Mzee Chura, kodoa macho nikutupie njugu.” Chura kusikia habari za
njugu akatoa macho pima. Sungura haraka alizoa mchanga na kumtia Chura machoni.
Chura akashindwa kuona. Ndipo Sungura akatoka shimoni na kukimbia kabisa.
Hata
mama Chui aliporudi na jembe na moto, alimwuliza Chura, “Sungura bado angali
ndani?” Chura huku amefikicha macho yake hata yakamvimba mfano wa njugu
alijibu, “Yumo.” Mara kazi ikaanza ya kuchimba shimo na kufukizia moshi ili
kumkamata Sungura.
Alichimba
na kufukua, akafukizia na moshi kufa na kupona. Mwisho akaufikia mwisho wa
shimo, lakini Sungura hayumo.
Mama
Chui alikasirika sana kuona hata Chura amemdanganya. Alimgeukia mara akamkamata
Chura na kumwambia, “sasa hivi
nitakutupa motoni ufe.” Chura akajibu , “Wanyama wote walinichoma moto wala
sikudhurika. Huoni haya malengelenge?”
Mama
chui akaendelea, “Kwanini umenidanganya. Basi nitakuponda ufe.” Chura akajibu
huku ametulia tu, “Oo! Wanyama wote walijaribu kuniponda lakini sikufa.”
Chui
kuona hana la kufanya . akamwuliza Chura, “Basi nifanye nini nikitaka kukuua?”
Mzee Chura akamjibu mara moja, “Sikufichi neno mama Chui. Ukitaka kuniua,
nitupe kwa nguvu zako zote .” hapo Chui alimwinua mzee Chura kwa chuki na
ghadhabu, kwa nguvu zote akamtupa kwenye dimbwi la maji. Kwa furaha kubwa mzee
Chura aliogelea majini hadi ukingo wa pili. Ndipo aliposimama na kumwambia mama
Chui, “Bibi mkuki kwa nguruwe kwa binadamu haramu!
Ndio
mwisho wa hadithi. Chanzo (Nkwera, F.K. (hakina mwaka) uk. 36-39)
SAIDI
NA RAFIKI YAKE MUHAMMED
Paukwa
Pakawa
Mwanangu
mwanasiti
Kijiwe
kama chikichi ehe!
Basi
alikuwepo mtu mmoja, anaitwa Saidi na Muhammed mtu na rafiki yake. Mohammed
akamwambia rafiki yangu Saidi tusafiri tukatafute elimu, Wakakubari wakafanya
safari. Hata wakafika nchi moja ambayo nchi hiyo. Maisha ya pale ni kuwa kila
kitu kinauzwa riale moja. Ukitaka nyumba riale moja, ukitaka owa riale moja,
ukitaka kununua mbuzi riale moja. Ukitaka kununua kuku riale moja, muradi kula
kitu ni riale moja. Kwa hivyo Saidi yule, Muhammed akamwambia la, hapa mie
sipakai, bora mie ntaendelea mbele. Na Saidi yule akasema la, mimi siwezi
kuendelea, ntakaa hapa hapa. Kwa hivyo maisha hapa naona mazuri ntafanya
biashara. Muhammed akafunga safari kuendelea mbele. Saidi yule yue akakaa
akanunua nyumba, akaoa mke, ikawa anafanya biashara, muradi mambo yakamfanikia
vizuri. Pale katika mtaa ule. Palielemewa na mtu na nyumba, palikuwa na nyumba
moja inajengwa , kwa bahati mbaya akafa.ikawa akakatwa yule alojenga yule
tajiri mwenye kujenga nyumba ile, kwamba umemuu mtu. Tajiri yule akasema, la
miye si makosa yangu, nimepata mtu kotrakti, yaani mtu kutengeneza nyumba hii.
Nimempa fundi kwa kazi zote miye juu yangu kutoa fedha basi ikiwa kosa kakosa
huyo fundi. Akakamatwa fundi yule, kashtakiwa. Aliposhtakiwa fundi akasema la,
mie si makosa yangu. Miye ndo niliyetia mafundi wadogo wadogo ili kuitengeneza
nyumba hiyo. Wao ndio waliosababisha ukuta huu kuanguka kumuelemea mtu ukamuua.
Ikenda kesi ikajiri mafundi wale waliojenga wakamatwe. Fundi yule mmoja
alipokamatwa akasema, la si miye Abadan, mimi nilikuwa nikijenga vizuri, lakini
hawa vibarua wakiuponda udongo wakaufanya laini sana. Kwa hivyo udongo ulikuwa
tepetepe nyumba isijiweze hii ikaanguka ikamwelemea mtu.
Sasa
ikawa wakamatwe vibarua wale walioponda udongo, vibarua walipokamatwa kwenda
kwenye kesi wakasema, la, sisi kweli tumeponda udongo lakini alipita mmoja ana kichwa
kidogo. Huyo kichwa kidogo huyo ikawa sote twamtizama na huku twatia maji
twatizama, kutahamaki udongo umekwisha kuwa laini. Kwa hiyo tusiweze kuunanihii tukaupeleka hivo hivo, nyumba
ikawa majenzi yake laini, imeanguka nyumba. Sasa, sasa atafutwe Kichwa Kidogo
yule akatafutwa akakamatwa, ikenda hukumu, akaona sasa lazima Kichwa Kidogo
auliwe, hapana jambo lolote, sasa akatengenezewa kitanzi yule, ikatoka hukumu
kuwa atiew kitanzi, alivyokwenda kwenda tiwa kitanzi yule Kichwa Kidogo kikawa
kitanzi hakikamati, kila akitiwa chatoka. Kila akitiwa akifatuliwa atoka Kichwa
Kidogo. Sasa akenda akaambiwa Hakimu bwana tumejaribu kumuua Kichwa Kidogo
lakini katushinda. Kwa sasa kila
tukimtia kitanzi kichwa chake kinapenya kidogo.
Hakimu
akasema, mtafuteni mtu yoyote mumuue. Kwa bahati akapita Saidi enda sokoni na
Saidi kanenepa alikuwa kibaba. Wakaona huyu ndo anayefaa kuuliw huyu. Huku
maadam jaji kasema auliwe huyu basi auliwe tu hapana maneno yoyote. Akakamatwa,
akasema lakini miye sikufanya kitu, akaambiwa hukumu imekwishatoka uuliwe,
uuliwe tu. Njoo hapa akaona hana njia ya kusema. Lakini akaomba, akasema mimi
naomba, ikiwa mtaniuwa, yuko ndugu yangu Muhammed nimwagize. Maana yake
nikishakufa aweze kwenda kusema kwetu na kuwapa wazee wangu mirathi. Muhammed
akaagizwa yule kwa bahati akaja, alipokuja, akaambiwa Mohammed, huyu bwana
imetoka hukumu hapa auliwe, kwa sababu tumepita mote tumeona hapana mtu wa
kuuliwa isipokuwa yeye. Kichwa Kidogo hakufaa kitu, ambao hukumu ya mwisho
kutoka kwa Kichwa Kidogo, Mohammed akasema miye nataka kuonana na Mfalme,
akaambiwa, jee nini shida yako!
Shida
yangu bwana mimi nna ndugu yangu hapa imetoka hukumu auliwe lakini kwa bahati
naona bora niuliwe miye kuliko yeye. Kwa nini? Akamwambia siri kuwa huyo
akiuliwa atakwendazake peponi. Kwa hivyo fursa hii naitaka miye, unisaidie
niipate miye. Mfalme yule akafikiri akaona bai ikiwa enda peponi moja kwa moja
huyu, bora niuliwe miye nende zangu
peponi. Kwa hiyo akakamatwa mfalme akakubali kwa hiari yake auliwe, mfale
akauliwa. Alipkwishauliwa akamwambia jee si nimwkwambia miye saidi, tusikae
nchi hii! Basi hii salama yetu, hii ni salama yako wewe kuuliwa. Sasa
ninavyokueleza tenzetu unifuate huko niliko miye.
Siku
ile ile wakafungafunga mizigo yao wakasafiri siku ile ile. Akamwambia hii sasa
ndiyo hatari ya kukaa chi ambayo watu hawana elimu. Na hadithi yangu imeishia
hapo. (Chanzo: Gibbe, A.G. na Mvungi, T.A. (1986:16-17)
MAMA
MGUMBA
Hadithi
hadithi1
Hadithi
njoo!
1. Katika
nchi fulani ya mbali paliishi mtu na mkewe. Mama huyo alikuwa mgumba kwa siku
nyingi, wala hakuzaa mtoto hata mmoja. Hali hii iliwahuznunisha sana watu hawa
wawili. Walijaribu kila njia ili wapate watoto lakini hawakufanikiwa kabisa.
2. Siku
moja huyu mama alikwenda mtoni kuteka maji. Njiani alimkuta ajuza mmoja anang’oa
nyasi za kulalia. Ajuza alikuwa amefunga mzigo mkubwa na mzito sana wa nyasi
hata ukamshinda kujitwika peke yake. Akamwomba msaada huyu mama mgumba. Mama
huyu hakusita. Wakaamkiana kiada. Kisha hapo ajuza na mama waliinua mzigo.
Lakini badala ya kumtwika ajuza, mama mgumba akaomba aubebe yeye, kisha
amchukuze walau njia yake. Ajuza akashukuru sana.
3. Wakiwa
njiani, ajuza aliuliza, “Mwanangu, una watoto wangapi?” mama mgumba akajibu,
“Mamangu sina. Sina hata mmoja wa kumtuma maji.” Kusikia vile ajuza alihuzunika
sana moyoni mwake na kumwambia, “Mama kadiri ulivyonitendea wema ndivyo name
nitakufanyia wema. Basi, nenda ukachukue mfupa wowote utakaouona karibu na
nyumba iliyohamwa na wenyeji wake. Ukisha uokota kauweke katika chungu nyumbani
mwako. Kazi yako itakuwa kumwagilia maziwa huo mfupa kila siku. Bora zaidi
uukamulie maziwa yako mwenyewe. Nawe utaona matokeo yake.
4. Mama
mgumba akafurahi sana kupata siri hiyo. Alipofika tu nyumbani kwake kutoka
mtoni, alitua maji yake; mara akaanza kutekeleza agizo la ajuza. Aliokota mfupa
kwenye nyumba iliyohamwa, akauweka ndani ya chungu chumbani mwake, akaukamulia
maziwa kila siku. Baada ya siku saba mama mgumba alisikia mtoto analia ndani ya
chungu. Akafurahi mno. Haraka alikifungua kile chungu akamtoa mtoto wa kiume,
mchanga, mzuri ajabu. Furaha yake nay a mumewe ikawa kubwa sana.
5. Mtoto
alikuwa, naye akaoa.
6. Ila,
pamoja na hiyo siri ya mtoto ajuza alikuwa amemwagiza mama mgumba sharti moja,
“Lolote litakalotokea usimweleze mtu yeyote.” Kumbe, ikaondokea katika furaha
yake kubwa mama mtoto alisahau miko yote. Mama akamweleza jirani yake siri yote
jinsi alivyompata huyo mtoto mzuri. Akiongea naye, mama alimsihi jirani yake,
“Lakini nakuomba usimweleze mambo haya mtu yeyote.”
7. Kumbe
wakati hawa majirani wawili walipozungumza ile siri, kacheche (ndege mdogo
sana) alikuwa ameatamia mayai yake kwenye upenu wa nyumba. Akasikia yote.
Pitepite, kacheche alipomwona yule mtoto mzuri amekaa na mama yeke, akaanza
kumhadithia mtoto mambo yote aliyozungumza mama mtu na jirani yake huku naye
mama mwenyewe anayasikia. Mama akastaajabu sana. Pale pale mtoto wa ajabu huyo
alianza kubadilika rangi na kudidimia ardhini taratibu hadi kutoweka kabisa.
8. Mama
akabaki analia na kufikiria nini atakachomweleza mume wake. Alihuzunika moyoni
n kukumbuka neno la hayati bibi alilomwambia siku moja, “Mjukuu wangu kua
ufikie uzee. Ila hamna siri ya watu watatu.”
(Chanzo:
Nkwera, F.V (xx) uk.14-15)
SUNGURA AOA
Kwali murhu!
Dii!
Hapo kale Sungura, fisi, Chui na
Ngiri waliishi nyumba moja. Walitembea pamoja na kufanya kazi pamoja; kila kitu
walifanya pamoja.
Siku moja katika mazungumzo yao
waliamua waoe mabinti wa watu. Baada ya makelele mengi walishindwa kuafikiana
nani kati yao aanze kuoa. Hatimaye wakaamua, “Wote wane twende pamoja kutafuta
mchumba. Huyo msichana atakayetupendeza sote wane, tumwachia yeye achague yupi
kati yetu apenda kumwoa.
Baada ya makubaliano hayo wote wane
walianza safari ya pamoja katika zunguka yao walikutana na kidosho. Kidosho,
msichana mrembo aliwakata maini wote wanne.
Wote wanne walikaribishwa vizuri
kwao kidosho, wakapikiwa chakula, wakala. Punde si punde wakatoa ombi lao kwa
baba mtu. Baba mtu hakuwakatalia. Aliwaonyesha chumba kizuri ambamo watalala
kwa siku nne; siku ya nne atawapa jibu.
Karibu na chumba walimokaribishwa
wageni kulala, kulikuwa na zizi la mbuzi. Haraka fisi na chui walipata harufu
ya mbuzi, wakawamezea mate. Hata ulipofika usiku wote walikwenda kulala.
Katikati ya usiku mroho wa wote hakuweza kufumba macho zaidi. Fisi aliamka kwa
siri, akaelekea kwenye zizi la mbuzi la yule baba mtu. Akaua mbuzi mmoja na
kumla mzima. Kishaye alitwaa samadi kidogo na kuja nayo chumbani kwao.
Alinyatia taratibu hadi alipolala chui na kumpaka ile samadi miguuni.
Kulipokucha baba mtu alishangaa
kuona mbuzi mmoja ameliwa usiku. Alipowaangalia wageni wake alimwona chui ana
samadi miguuni. Bila hili wala lile baba mtu alishika marungu na kumfukuza
kabisa chui. Maskini chui alitimua mbio za kujisalimisha.
Huku nyuma fisi aliendelea na kazi
yake ya usiku. Siku ya pili ngiri akafukuzwa kwa kosa hilo hilo la wizi. Sasa
wakabaki Fisi na Sungura.
Sungura hakuchelewa. Aling’amua
janja za fisi. Basi naye akabuni hila ya mwaka. Walipokwenda kulala usiku huo
watu wa tatu, sungura alimwambia fisi, “Rafiki yangu, nakupa siri moja. Mimi ni
mtu wa ajabu sana. Usiku nikilala natumbua macho, nikiwa macho nafumba kope!”
Aliposikia habari hiyo fisi
alifurahi sana moyoni mwake. Alidhani
kwamba amefumbuliwa siri kubwa sana itakayomponza sungura.
Basi ilitimu usiku wa manane fisi
akaamka. Kumbe sungura anamsikia, tena amefumbua macho aonekane yuko
usingizini.
Fisi alikwenda zizini, akala beberu
la mbuzi. Hata aliposhiba alirudi chumbani huku amechukua samadi ya kumpaka
sungura . fisi alipomkaribia sungura na kumwona bado amefumbua macho kabisa kwa
furaha alimsogelea ili ampake samadi. Kumbe, ghafula kabisa sungura alikurupuka
na kuanza kumkemea fisi kwa sauti kali, “Fisi mwenzangu unadhani nimelala?
Sikuoni? Nakuona. Wacha mchezo wako.” Basi sungura aliendelea kupiga kelele nay
owe mpaka mwenye nyumba aliamka na kuja chumbani kwa wageni wake.
Ndipo sungura alimshtaki fisi uovu
wake, “Baba mkwe, fisi siye wa kumwacha. Mwana haramu huyu astahili kabisa
kirungu. Mwuaji, mwizi, hakuna alichobakiza.” Bila ya simile baba Kidosho
alimshambulia fisi kwa kishindo kizito. Fisi alinusurika kufa. Alikimbia pasi
na kuona nyuma, huku analia ovyo, “Huuuuuuuuwiii! Nimemkosa Kidosho.”
Huku nyuma, asubuhi na mapema
sungura akapewa mke; akamwoa kidosho.
Mwisho wa hadithi. (Chanzo: Nkwera,
F.V (xx) uk. 65-67)
JE,
DUNIANI KUNA WEMA
Hadithi
hadithi!
Hadithi
njoo
Hapo
zamani za kale palitokea baba mmoja na mkewe ambao walibahatika kuwa na watoto
watatu. Katika nchi ile kulikuwa na neema nyingi yaani ardhi yenye rutuba, watu
walijipatia mazao mengi na mifugo ya kutosha. Basi kiama kikaja bonge la njaa
likaikumba nchi ile watu wakadhoofika kwa kukosa chakula, wanyama wengi wakaffa
na wengine kudhoofika sana. Basi yule bwana akawaza na kuwazua akaona bora
atafute jitihada za kuinusuru familia yake kwa kuwa kazi yake kubwa alikuwa
mwindaji. Akaomba ushauri kwa mkewe naye hakuwa na kipingamizi alimruhusu.
Lakini
kabla ya kuondoka usiku ule wakiwa wamelala yeye na mkewe mara wakasikia mlio
wa bundi juu ya paa lake, uuuuuuuwi! Uuuuuuwi! Uuuuuwi! Basi wakafadhaika sana
kwani walijua kuwa huo ni uchuro mkubwa sana. Mkewe akamwonya mumewe asiende
kwani angeweza angeweza kukumbwa na mabalaa mengi huko aendako. Lakini yule
baba hakuwa na namna ya kufanya kwani aliona hata akikaa na kuacha kwenda
kutafuta chochote familia yake itaangamia.
Basi
siku ya siku ikawadia safari ikaanza, akasafiri kwa masaa marefu sana bila ya
mafanikio, lakini apiga moyo konde. Aliendelea na safari yake ya nyika na
jangwa. Akafika sehemu yenye bonde kubwa sana akawaona wanyama wengi wakila
majani kwa furaha kubwa. Bwana yule akaona atafute mbinu mbadala ya kuwapata,
akaamua kutafuta ulimbo na majani ya miti akajigandisha mwili mzima ili wanyama
wasiweze kujua kuwa ni adui yao. Katika harakati za kuwanyatia akajikuta
katumbukia kwenye shimo, looo! Wanyama wakashtuka na kukimbia yule bwana
akajuta sana kwa uamuzi alioufanya kwani hakuambulia chochote. Lakini hakukata
tama akaendelea mbele na safari yake. Alipofika mbali sana aliona bonge la
chupa ya dhahabu akafurahia sana, akaona sasa umaskini kwa heri na maisha ya
neema yamekaribia. Kasogelea ile chupa akapata shauku ya kulifungua,
alipofungua tu mara zimwi jinni hiloo! Loo! Bonge la jinni akatetemeka sana
lakini hakuwa na ujanja.
Jini
likamshika na kumwambia nashukuru sana kwa kunitoa kifungoni cha miaka saba.
Nilimuuzi tajiri wangu naye akanipa kifungo hiki cha maisha. Sasa nashukuru
sana kwa kunitoa na utakuwa kitoweo change maana sijala muda mrefu. Yule bwana
kajaribu kujitetea lakini jinni halikuelewa somo. Mara Sungura huyo kapita pale
kichakani kasikia mzozo uliopo baina ya binadamu na jinni, sungura akawauliza
kulikoni.
Basi
jini akamweleza sungura kesi yake, na binadamu naye akamweleza mwanzo na chanzo
cha safari yake mpaka kukutana na mkasa huo. Basi sungura akaomba ili kila
mmoja apate haki yake, kila mtu arudi alikotoka ili tuanze upya na utatuzi
utapatikana na kila mmoja ataridhika na matokeo hayo. Basi Sungura akasema
tuanze na wewe jinni urudi kwenye chupa tukufungie na binadamu arudi alikotoka
na mimi nirudi nilikotoka ili tukirudi tutajua la kufanya, Jini akakubali. Mara
tu Jini aliporudi akafungiwa ndani ya chupa, sungura akasema sasa kwa sababu
wewe unajitia jeuri utaendelea kubaki humo humo ndani ya chupa kama tajiri yako
alivyokusudia ufie ndani ya chupa.
Yule
bwana kuona hali ile akamshukuru sana sungura kwa kumwokoa mikononi mwa yule
jinni. Basi wakaagana ili binadamu aendelee na safari zake na sungura ashike
zake. Yule bwna alipopiga hatua mbili akakumbuka kuwa nyumbani watu hawana
kitoweo na anasubiriwa ili ainusuru familia yake, akageuka nyuma na kumwona
mnyama aliyekaribu naye akiwa ni sungura, akampiga mshale pale pale, sungura
akafa, binadamu akamchukua tayari kwa ridhiki ya siku hiyo.
Hadithi
yangu imeishia hapo. (Chanzo: imesimuliwa
na Magreth mwanafunzi wa M.A. Kiswahili 2014)
DEGE
Hapo zamani za kale waliondokea mtu, mkewe na mtoto wao
wa kiume. Watu hao walikuwa na maisha mazuri tu ambayo hayana hitaji
lisilokidhiwa.
Siku moja, majira ya asubuhi sana, yule mtoto mwanamume
alikuwa nje akicheza. Mara hiyo akamwona kipepeo mzuri mmmmmno. Mwenye rangi
mzomzo, zilizooana kwa urembo na ulimbo wa ajabu.
Yule mtoto akawa anajaribu kumkamata yule kipepeo kwa
kuchupa na kumrukia kama sungura na zabibu.
Alichupaaaaaa, akaruka huyooo. Lakini kila akichupa na
kuruka, utadhani waliagana na kipepeo yule, kwani kipepeo pia alichupa na
kuruka. Mtoto alizidi kuchupa na kuruka, akiwa anamfuatia yule kipepeo. Yakawa
ni mashindano ya kuchupa na kuruka. Haooooo! Msitu na nyika, msitu na nyika;
hata kushtukia wako mbaliiii! Mtoto hajui mbele wala nyuma, hajui pa kupata
njia wala pa kupotelea. Mradi tu alijikuta yuko pake yake, kachoka taabani wa
Shaabani, kiu imemkamata kijana, ulimi nje nje kama wa mbwa. Na kipepeo naye
nd'o hivo, haonekani tena.
Basi bwana! Kijana wetu huyo alikaa chini ya mti ambao
ulikuwa umeambatana na mwamba uliokuwa katikati ya njia kubwa. Akawa anawaza ya
nyumbani, lakini afanyeje masikini wa watu. Na jua nalo nd'o hivo linakwenda
kama lilivyopangiwa. Njaa imembana, na kiu kimemkamata; afanye nini?
Ghafla, kijana wetu akaona matone yadondokayo kutoka
kwenye mwamba. Matone yakazidi kudondoka, makubwa hayoo. Kijana akakurupuka
huyoooo! Mbio kama vile kamwona tena yule kipepeo. Akaokota kifuu cha nazi,
akayakinga yale matone. Akakinga weee! Hata wakati maji yale yanakaribia kujaa,
akaona ayanywe kuituliza ile kiu yake kali. Akaelekeza kifuu chenye maji
mdomoni mwake. Lakini, ghafla, likaja dege kubwa hilo! Dege lisilo na mfano. Mbawa zake zilikuwa zikipiga, na
upepo karibu umwangushe kijana wetu. Hilooo, likakipiga kile kifuu na kuyamwaga
yale maji yooote! Halafu likajiendea zake likimwacha kijana anahaha kwa kiu na
woga. Lakini kijana wetu hakukata
tamaa. Alikinga mara
ya pili; tena akawa ameshikilia kifuu imara zaidi ya mara ya kwanza. Alipojaribu
kunywa, lile dege hilooo! Likampokonya
kile kifuu tena.
Mara ya tatu yalipotokea yale, kijana akaamua kwenda juu
ya mwamba kuona kulikoni huko yanakotokea yale maji.Akapanda, akapanda,
akapandaaaa! Halafu hukooo juu kabisa ya ule mwamba, kijana akalikuta joka! Joka joka hasaaa! Limelala utadhania limekufa, ijapokuwa
macho yake makubwa kama nazi yalikuwa yakigeukageuka kama ya kinyonga. Kijana
hakulikaribia dude lile; bali pale akagundua yalikokuwa yanatoka yale maji.
Domo la joka lile lilikuwa wazi, na sumu yalo ikitiririka kama maji mferejini
hadi kule chini ya mwamba. Kijana mwili ulimsisimka, moyo ukamchachatika.
Alijua.
Ghafla, lile dege likaja tena. Mara hii si kwa kasi kama mwanzo. Masikini kijana wetu.
Kule nyumbani wazazi wake wote wawili, wa kuukeni na wa kuumeni walikuwa
wakikata roho kwa huzuni ya kumpoteza mtoto wao.
Lile dege likamjia yule mwanamume na kumchukua
hangahanga, juu kwa juu. Likawa linampepea mwanamume yule asiungue jua.
Lilipaaaaaaa. Halafu ghafla likaanza kushuka. Kijana mwanamume alipoangalia
chini akajua kuwa karudishwa nyumbani kwao. Akafurahi, na hadithi yangu
ikaishia hapo hapo. (Chanzo: Senkoro. F.E.M.K. 2014)
KAZI KWA MFALME
Alikuwepo mtu na mumewe na watoto wao wawili. Kutokana na hali ya maisha waliyonayo mtoto
mkubwa aliamua kuondoka kwenda kutafuta kazi. Aliambiwa na watu kwamba kwa
Mfalme kuna kazi, lakini kuna masharti yake, pindi ukishindwa utafungwa na
ukimshinda mfalme atavua kilemba chake.
Masharti yenyewe ni: Mfalme atatoa vitandawili vyake uvijibu na wewe
utowe vyako avijibu.
Siku ilipowadia mtoto alifika kwa mfalme na akapewa
masharti na akayakubali. Mtoto akaanza
kutoa vitandawili vyake vikajibiwa vyote, zamu ya mfalme mtoto akashindwa na
akapelekwa kufungwa.
Siku zilipita mtoto wa pili naye akaamua kumtafuta kaka
yake. Alipita njia ile ile na kupewa
masharti yale yale. Alishindwa na
akafungwa.
Mama yao alijaaliwa kupata mtoto wa mwisho na kila siku
mtoto yule akifanya kosa mama yake husema, "Wawili wamepotea na kwa hiyo
si kitu."
Yule mtoto yalimuingia ndani ya kichwa maneno yale,
akamuuliza baba yake. Baba yake akamwambia, "Nenda kamuulize mama
yako!" Mama alimuhadithia yote
yale. Mtoto akasema "Kesho kutwa
nitakwenda kuwatafuta." Mama
alimkubalia, lakini baada ya kukaa na mumewe wakashauriana wakaona bora mtoto
afe pale pale kuliko kufa kama walivyokufa wenziwe. Mtoto aliendelea kuwasihi
mpaka wakamkubalia.
Siku ilipowadia mtoto alifunga mizigo yake tayari ili
asubuhi sana aanze safari. Wakati
amelala mtoto alioteshwa kuwa mama yake anataka kumuuwa, ameweka kisu ili
akenda kumuaga amchome nacho. Usiku ule
ule aliamka na kuchonga kisu cha bao na kukibadili na kile ambacho mama yake
angeweza kumuuwa nacho. Kile kisu hasa akakichukua yeye.
Asubuhi alikwenda kumuaga. Alipogeuka nyuma mama
alichukua kisu akamrushia, mtoto aligeuka nyuma na kumuuliza mama yake,
"Nini hicho"? Mama alisema
"Ah nilikuwa nikijaribu tu sababu baba yako eti anataka kwenda
kuwinda". Mtoto kuona vile akavunja
safari akamwambia mama yake kuwa safari itakuwa kesho yake.
Ilipofika usiku alioteshwa tena mama yake kaweka mshale,
alikwenda akauondowa na akauweka wa mbao.
Alipokwenda kumuaga alfajiri alimrushia nao, alipogeuka alimueleza
maneno yale yale, na mtoto alivunja tena safari. Ikawa siku iliyofuatia
usingizini alioteshwa tena, lakini hakujua kuna nini. Alipoamka alimuaga mama
na baba yake. Alipewa chai na mkate na
maandazi. Akanywa na kula, na mengine akafungiwa, mlikuwa mna maandazi yenye
sumu.
Alianza safari yake ya kutwa nzima. Aliposikia njaa
alitoa andazi lile lenye sumu, alitokea paka ikawa analia sana akamkatia andazi
akampa, wakati paka anakula andazi yule mtoto anamtizama. Mara paka akawa
anapepesuka; na mara akafa pale pale.
Akatokea mbwa nae akamla paka. Mbwa baada ya muda akafa. Wakaja nguruwe watatu, wakamla mbwa nao
wakafa. Wakaja wasasi sita nao wakakatiana nguruwe. Watu wawili wakachoma wakala wakafa.
Mambo yote yale mtoto anayatizama akachukua mikuki yao
yote sita na like andazi kipande akenda zake, Alikwenda hadi alipofika kwa
mfalme. Mfalme alimueleza yale yale
aliyowaeleza kaka zake na alikubali.
Mfalme alitoa vitandawili vyake vitatu na mtoto akavijibu.
Zamu ikafika kwa mtoto.
Alikumbuka yaliyomtokea, na baadaye akasema, `Kitandawili!"
Akajibiwa, "Tega!"
"Nusu imeuwa moja, moja imeuwa tatu, tatu imeuwa
sita.'
Mfalme akawaza, hakujuwa la kumjibu. Hivyo alishindwa, na akavua kilemba chake
akampa yule mtoto. Mtoto akashika ufalme
na akawafungua ndugu zake pamoja na wote waliofungwa. Mfalme mpya alikaa na kaka zake kwa raha
zote. (Chanzo: Senkoro. F.E.M.K. 2014)
Kazi imeandaliwa kwa pamoja na Venance, Furaha, Margareth Waivyala na Zuhura Katoto wanafunzi wa mwaka wa kwanza UDSM, M.A.KISWAHILI 2014/2015
No comments:
Post a Comment