Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Sunday, November 6, 2016

Kauli za Usimulizi na Usimulizi Uliotumika katika Riwaya ya Vuta n'Kuvute.

Na. Furaha Venance
Mwaka 2015

Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo tutatoa fasili  za usimulizi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali na namna wataalamu hao wanavyoainisha aina za usimulizi. Sehemu ya pili ambayo ndiyo kiini cha kazi hii, tutatumia riwaya ya Vuta n’Kuvute iliyoandikwa na Shafi, A. Shafi kubainisha kauli za usimulizi na usimulizi unaojitokeza katika riwaya husika. Sehemu ya mwisho itakuwa ni hitimisho.

Usimulizi umefasiliwa kwa namna mbalimbali na wataalamu tofauti tofauti. Mathalani, Mohochi (2000:50) akiwanukuu Attenbernd na Lewis (1963) anasema, usimulizi ni mkabala ambao hutuwezesha kuyatizama yanayotendeka na kusikia yanayozungumzwa katika kazi ya fasihi. Kanar (2001) akinukuliwa na Burundi na wenzake (2014:74) anasema kuwa, usimulizi ni mtindo wa mpangilio unaotumiwa na mwandishi wa hotuba, habari na utanzu wa kibunilizi kuelezea matukio. Mawazo ya mtaalamu huyo hayapishani sana na mawazo ya Wamitila (2003:325) anayesema kuwa usimulizi ni uelezeaji wa matukio katika hadithi. Hawa wote wanaona kuwa usimulizi ni namna ya kuyaeleza matukio katika habari au hadithi.

Kwa maana hiyo tunaweza kusema, usimulizi ni namna mwandishi anavyotumia kauli mbalimbali za usimulizi na mbinu za usimulizi katika kuelezea visa na matukio kwa jinsi alivyopangilia katika bunilizi yake ya riwaya. Ama kuhusu kauli za usimulizi na mbinu za usimulizi wataalamu mbalimbali wamekuwa wakizitumia dhana hizi kwa namna moja ingawa kiuhalisia kwa mawazo yetu tunaona kama zinatofautiana. Kwa mfano, Mazrui na Syambo (1992) akinukuliwa na Burundi na wenzake (wameshatajwa, 75) wanaeleza aina zifuatazo za usimulizi; Usimulizi wa mwandishi mwenyewe akitumia viambishi nafsi ya tatu, aina ya pili ni usimulizi wa mmoja wa wahusika akitumia viambishi vya  nafsi ya tatu. Aina ya tatu ni usimulizi wa mwandishi akitumia viambishi vya nafsi ya tatu. Wakitofautisha aina hii na ile ya kwanza, wanatueleza kuwa katika aina hii,  msimulizi huwa haelezi yale ambayo wahusika hawayakudhihirisha katika vitendo au maneno, kwa maana kuwa msimulizi anakuwa hayajui yale yaliyofichika ndani tofauti na aina ya kwanza ambapo msimulizi anajua kila kitu hata yaliyo mawazoni mwa mhusika. Na aina ya nne wanatueleza ni usimulizi wa mmoja wa wahusika akitumia viambishi vya nafsi ya kwanza.

Kama tutachunguza vizuri, aina hizi kama zilivyoainishwa na Mazrui na Syambo, tutagundua kuwa, aina hizi zinaangukia katika aina za kauli za usimulizi, wao wamezitaja nne lakini kimsingi zinapaswa kuwa mbili ambazo ni usimulizi wa kutumia viambishi nafsi ya tatu na usimulizi wa kutumia viambishi vya nafsi ya kwanza, kwani aina ya kwanza, ya pili na ile ya tatu wamezitenganisha ili hali zote zina fanana.  Zote zinatumia viambishi nafsi ya tatu hivyo zilitakiwa kuwekwa katika kundi moja kama kauli ya usimulizi nafsi ya tatu.

Mohochi (2000:) anaainisha aina tatu za usimulizi ambazo anaziita kama mitindo ya usimulizi, aina hizo ni, usimulizi maizi pia anauita usimulizi mwakote, aina nyingine ni usimulizi wa nafsi ya tatu na usimulizi wa nafsi ya kwanza. Wamitila (2003:325-328) anabainisha aina zifuatazo za usimulizi, usimulizi anuwai,usimulizi ngazi,usimulizi maizi, usimulizi penyezi au dukizi, usimulizi sawia, usimulizi tangulizi, usimulizi ki-itimamu, usimulizi wa kiutendi, usimulizi kirejeshi, usimulizi wa kiutomaji, usimulizi wa nafsi ya pili na usimulizi wa nafsi ya tatu.

Ama kwa hakika tukiangalia aina hizi za usimulizi kama zilivyoanishwa na wataalamu hao ni wazi kuwa wapo wanaona aina za usimulizi ni zile kauli zinazotumia viambishi vya nafsi na wengine wanachanganya kwa kutumia kigezo cha matumizi ya viambishi vya nafsi na kigezo ambacho kwetu tunaona ni kigezo cha mitindo ya usimulizi au usimuliaji kama inavyojitokeza kwa Mohochi naWamitila.

Katika mjadala huu, tutatumia vigezo vya kauli za usimulizi na mbinu za usimulizi kwa namna tofauti, tukiwa na maana, kauli za usimulizi ni ule usimulizi wa matukio au visa katika bunilizi ya hadithi au riwaya kwa kutumia viambishi vya nafsi. Katika aina hii tunapata kauli zifuatazo za usimulizi, usimulizi kauli nafsi ya kwanza, usimulizi kauli nafsi ya pili na usimulizi kauli nafsi ya tatu, wakati mbinu za usimulizi tunaweza kusema kuwa ni namna mwandishi ama mtunzi anavyotumia mitindo na mbinu mbalimbali za kuyasimulia na kupangilia matukio na visa kwa namna anayoona inafaa katika bunilizi ya hadithi au riwaya. Katika aina hii tunapata aina zifuatazo za usimulizi, usimulizi anuwai, usimulizi ngazi,usimulizi maizi, usimulizi penyezi au dukizi, usimulizi sawia, usimulizi tangulizi, usimulizi ki-itimamu, usimulizi wa kiutendi, usimulizi kirejeshi na usimulizi wa kiutomaji (pia angalia Wamitila uk. 325-328 keshatajwa).

Hivyo basi kwa kutumia riwaya ya Vunta N’kuvute iliyoandikwa na Shafi Adam Shafi tunaweza kuangalia na kubainisha kauli za usimulizi na mbinu za usimulizi zinaojitokeza katika riwaya hii. Tukianza na kauli za usimulizi. Kama tulivyoona hapo awali, kuwa katika kauli za usimulizi kuna aina tatu za usimulizi, aina zinazojitokeza katika riwaya hii ni:

Kwa kiasi kikubwa, riwaya hii inatumia kauli ya usimulizi nafsi ya tatu. Mazrui na Syambo (wameshatajwa,) wanaeleza kuwa, huu ni usimulizi unaomwezesha mtunzi kusimulia matukio yote pamoja na matokeo yake popote. Aina hii ya usimulizi hutumia kiambishi awali cha a katika umoja au wa katika wingi. aina hii ya usimulizi tunaweza kuiona ukurasa wa 1 msimulizi anaposema;
“Mara tu baada ya kuvunja ungo, Yasmin aliozwa mume. Alikuwa mume wa jamii yake ya Ithnasharia ambaye alikuwa akiishi jirani naye hapo Mtendeni.
Alikuwa ni mume asiyelingana naye hata kidogo.”
Hapa mwandishi anatusimulia juu ya binti mdogo kulazimishwa kuolewa na mzee wa miaka 52. Viambishi vilivyoandikwa kwa hati ya kukolezwa ni viambishi vinvyodokeza kuwa kauli husika ni kauli simulizi nafsi ya tatu.
Aidha wakati mwingine  msimulizi anaweza kumwachia mhusika katikati ya usumulizi wake naye akatumia kauli simulizi nafsi ya tatu kama inavyojitokeza katika kazi hii. Mwandishi anapomtumia mhusika Koplo Matata anaposema;
Denge anakwenda kuvua kama kisingizio tu, lakini ana mambo anayoyafanya, tena mambo mabaya sana, mambo ambayo yanaweza kumfanya aende jela, yeye na kila anayemjua kama vile wewe na Mwajuma (Uk. 99-100).

Usimulizi wa kauli nafsi ya kwanza pia unajitokeza katika kazi hii ingawa kwa kiasi kidogo. Wamitila(keshatajwa, uk.327) anaeleza, ni usimulizi wa hadithi unaofanywa na mhusika kwa nafsi ya kwanza. Mhusika huyo anaweza kuwa mshiriki wa matukio au matendo ya hadithi au asiwe mshiriki. Mazrui na Syambo (washatajwa,) wanasema huu ni usimulizi wa mmoja wa wahusika akitumia viambishi vya nafsi ya kwanza. Kwa kuwa kauli usimulizi nafsi ya kwanza Tofauti na Wamitila anavyodai kuwa katika kauli hii, msimulizi anaweza kuwa mshiriki wa matukio au matendo ya hadithi au asiwe mshiriki kwa hakika linahitaji kuangaliwa vizuri. hutumia viwakilishi au viambishi nafsi vya mimi, ni, katika umoja na si, sisi na tu katika wingi ni dhahili kuwa msimulizi ni lazima atakuwa mshiriki wa matendo na matukio katika hadithi husika.

Tukirejea katika riwaya yetu ya Vuta n’kuvute, mwandishi kuna sehemu huwaachia wahusika wake kusimulia au kuelezea na kujieleza ndipo kauli hii nafsi ya kwanza inapojitokeza kama mwandishi anavyotuambia:
Denge alikuwa ametulia kimya, anamsikiliza kwa makini kabisa. “Yasmini mimi najua kama unanipenda, na mimi nakupenda vile vile, lakini kuna kitu kimoja, (Uk. 145).

Hapa tunamwona mwandishi anatumia nafsi ya tatu katika kuelezea matukio na matendo lakini pia anatoa nafasi kwa wahusika kueleza na kusimulia kama tunavyoweza kuona hapo juu mhusika Denge akimweleza Yasmini.

Kwa upande mwingine, usimulizi maizi unapewa nafasi na mwandishi. Mohochi (2000:50) anaeleza kuwa, katika mbinu hii mwandishi huieleza hadithi ambayo mara nyingi yeye haimhusu; yaani haishiriki lakini, akiwa muumbi wake, anaelewa kila kitu kinachotendeka hadithini. Mawazo haya ya Mohochi yanaelekea kuungwa mkono na Wamitila (2003:326) anasema, hii ni aina ya usimulizi unaotambulishwa na ufahamu wa kila kitu. Katika aina hii ya usimulizi, Msimulizi  anakuwa na  uwezo wa kupenya na kuingia katika fikra za wahusika wake na kujua na kutueleza kile wanachowaza, wanachofikiria kukifanya hata kabla hakidhihirika wazi kwa vitendo. Sifa hizi za usimulizi maizi Hawthorn (1985) anaona kuwa, huenda mbinu hii ilikuwa tokeo la mojawapo ya sifa za Mungu ya kujua kila kitu. Usimulizi wa aina hii unajitokeza katika ukurasa wa 17 msimulizi anapotueleza yale yanayowazwa mawazoni na mhusika Yasmin kama anavyotuambi;

Mawazo yake yalikuwa mbali na pale kilipo kiwiliwili chake na alikuwa akiwaza na kujiuliza, “Nende wapi saa hizi?” alijiuliza na kujishauri moyoni mwake, “Nende kwa mama?

Hapa msimulizi ameingia hadi akilini mwa mhusika Yasmin na kujua kile anachowaza, maswali anayojiuliza au yanayomtatiza mawazoni. Aina hii ya usimulizi pia tunaona inajotokeza msimulizi kwa wakati mmoja akisimulia tukio linalotokea Unguja na wakati huo huo anaelezea tukio linalotokea Tanga Rejea ukurasa wa 214 msimulizi anapotupa habari na matendo yanayofanyika unguja na Zanzibar kwa wakati mmoja; katika hali ya kawaida sifa ya mtu kujua mambo yanayotendeka kwa wakati mmoja sehemu mbili tofauti ni jambo ambalo Mungu peke yake ndiye anayeweza.

Aidha usimulizi wa kirejeshi unajitokeza katika riwaya hii, Wamitila (keshatajwa, uk. 327) anatueleza kuwa, usimulizi kirejeshi ni aina ya usimulizi ambao unategemea wakati uliopita hasa kumfanya msimulizi kutafakari kuhusu yaliyotokea na kubainisha tofauti zilizopo kati ya jana na wakati uliopo. Katika sura ya nne mwandishi anatuonesha Denge akiwa Unguja na akiendesha harakati zake za kimapinduzi usimulizi kirejeshi unajitokeza sura ya sita mwandishi anapotusimulia au kuturudisha nyuma matukio ya kutuelezea habari za Denge za huko nyuma ambazo mwanzo hazikuonesha.
“Denge alimaliza darasa la nne skuli ya Gulioni na alifuzu vizuri mtihani wake. Aliingia daraa la tisa Government Secondary School. Alimaliza darasa la 12 na alishinda mtihani wa Cambridge daraja la kwanza.

Hata hivyo usimulizi wa Ki-itimamu pia unajitokeza katika riwaya hii. Wamitila (keshatajwa) anasema usimulizi wa aina hii unaweza kupatikana pale ambapo pana matumizi ya barua hasa katika riwaya za aina hiyo. Riwaya hii si ya kibarua kama ilivyo katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariam Ba. Matumizi ya mbinu hii inajitokeza katika ukurasa 168-169. Mbinu hii imetumika kama mbinu moja wapo ya kuipamba kazi yake na kumchota msomaji kihisia.

Hitimisho, ama kwa hakika tukitaza usimulizi wa kutumia viambishi vya nafsi ya tatu bila shaka utagundua kuwa aina hiyo ya usimulizi kwa kiasi kikubwa huingiliana ama kuhusiana na mbinu ya usimulizi maizi ambayo nayo hutumia viambishi vya nafsi ya tatu katika usimulizi wake. Tofauti yake ni kwamba usimulizi wa nafsi ya tatu kwa mujibu wa mjadala wetu mwandishi si lazima ajue kile kitu hata yale ambayo hayakudhihirishwa na muhusika wakati, katika usimulizi maizi msingi wake mkubwa ni mwandishi kuwa na sifa za kimungu, kujua hata yale ambayo hayakudhihirishwa na muhusika. Kwa hakika, katika riwaya ya Vuta n’kuvute mwandishi ametumia kauli na mbinu mbalimbali za usimulizi, tulizoziangalia hapa ni baadhi tu. Matumizi ya mbinu hizo katika bunilizi ya riwaya nikutupa picha kuwa ni nani anayesimulia, nani anasimuliwa (mhusika), anayesimuliwa anafanya nini, amefanya nini au atafanya nini lini na wapi. Kumbuka mpangilio mzuri wa usimulizi katika bunilizi huweza kuifanya kazi husika kupendeza na kuvutia kwa msomaji.

MAREJEO
Burundi, R.N, Mukuthuria, M. na Matundura, E.S. (2014) “Usimulizi katika Utenzi wa Swifa     
      ya Nguvumali.” Katika Kioo cha Lugha: Jarida la Taasisi ya Taaluma za Kiswahili. Juz 12:
      Uk.73-86.  Dar es Salaam. TATATKI.

Mohochi, E.S. (2000), “Usimulizi wa Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini.” katika Nordic Journal of
            African Studies 9 (2): 49-59.

Shafi, A,S. (1999) Vuta n’Kuvute. Dar es Salaam. Mkuki na Nyota Publisher.

Wamitila, K.W. (2008) Kanzi ya Fasihi: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi.
             Vide-Muwa Publishers Limited.

Wamitila, K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi.Focus Publications  Ltd.

Simu 0715335558 (whatsapp) na 0755440699
Facebook: Furaha Venance
instagram: fullraha17