Tangu wanachama wachache wa CHADEMA walipoanza kutuhumiana na kushutumiana kupitia JF watoa maoni mbalimbali mmetoa mwito kwa chama kuchukua hatua na wengine mmehitaji majibu kutoka viongozi wengine na kwangu kuhusu hali hiyo iliyojitokeza.

Ifahamike tu kuwa mara baada ya tuhuma na shutuma hizo kuandikwa nimewasiliana na baadhi ya wahusika waliotumia majina yaliyothibitishwa (verified users) ili wawasilishe maelezo navielelezo vyao kwa chama ili hatua ziweze kuchukuliwa. Nimechukua hatua hiyo kwa kuzingatia katiba ya chama ibara ya 5.3 na Kanuni za chama 7.7.5, Maadili yachama 10.0 Itifaki ya chama 12.0.

Aidha, nimewasiliana pia na uongozi wa BAVICHA ili waweze kuagiza viongozi na wanachama wake waliohusika watimize wajibu huo kwa mujibu wa kanuni za kuongoza Baraza la Vijana wa CHADEMA kwa kuzingatia pia katiba, kanuni, maadili na itifaki ya chama.

Pamoja na kusubiri maelezo na vielelezo toka kwa waliotakiwa kuwasilisha, ifahamike kuwa hata kabla ya kuandikwa kwa tuhuma na shutuma za hivi karibuni zilizotolewa na wanachama wenye majina yaliyothibitishwa, chama (kupitia Kurugenzi ya Ulinzi naUsalama) kilishaanza uchunguzi kuhusu madai ya kuwepo kwa baadhi ya wanachama wenye kukichafua chama na viongozi wake katika mitandao ya kijamii na njia nyingine za mawasiliano.

Aidha, ushushushu umekuwa ukiendelea kufuatilia nyendo za wapinzani wa nje ya chama zenye mwelekeo wa kuhujumu kwa kutumia mbinu haramu vuguvugu la mabadiliko nchini linalohamasishwa na CHADEMA.

Hivyo, maelezo na vielelezo vitavyowasilishwa vitashughulikiwa pia kwa kuzingatia ripoti za uchunguzi huo na hatua stahiki kuchukuliwa kwa watakaothibitika kukiuka katiba,kanuni, maadili na itifaki ya chama na pia maamuzi ya ziada yatafanyika juu ya wahujumu wa mabadiliko nchini watakaobainishwa.

Kwa mliohoji kuhusu matakwa ya kanuni za CHADEMA kuhusiana na tuhuma na shutuma zilizojitokeza nawashauri mrejee sura ya kumi ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama hususan kifungu cha 10.0 kinachohusu Maadili ya Viongozi, Sifa mahususi za Viongozi na Maadili ya wanachama.

Maadili ya CHADEMA yanakataza kiongozi kutoa tuhuma zozote dhidi ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizoelekezwa kwenye kanuni za chama. Ni marufuku kwa kiongozi wa CHADEMA kukashifu chama, kiongozi na mwanachama yoyote na viongozi wanapaswa kutofautisha kati ya kashfa na ukosoaji wa kisiasa.

Ni kinyume pia na maadili ya CHADEMA kwa mwanachama kufanya upinzani dhidi ya chama na kujihusisha na makundi ya majungu ya kuchonganisha viongozi na wanachama. Badala yake mwanachama anapaswa kuwa mwanaharakati wa kweli katika kutetea maslahi ya chama na jamii kwa ujumla kwa kuzingatia madhumuni, itikadi na falsafa ya CHADEMA.

CHADEMA imekuwa na kawaida ya kuchukua hatua dhidi ya utovu wa nidhamu kupitia vikao vyake na vyombo vyake vya kikatiba hivyo natoa rai kwa wanachama na watanzania wote wanaounga mkono mabadiliko kuwa wavumilivu na wastahimilivu ili hatua hizo zichukuliwe misingi ya haki na ukweli.

CHADEMA inaendelea na dhima yake kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu; masuala na matukio yanayojitokeza dhidi ya dhamira hiyo yachukuliwe kama changamoto katika kazi ya kuwezesha vuguvugu la mabadiliko.

Kwa sasa kipaumbele ni kusimamia maamuzi ya kamati kuu iliyomalizika karibuni kwa kurejea pia mikakati na mipango ambayo chama kinaendelea kuitekeleza ya kuwaunganisha watanzania kwa falsafa yake ya “Nguvu ya Umma” mpaka kieleweke.