VURUGU kubwa za kidini kati ya Waislamu na Wakristo, zimezuka katika kijiji
cha Buseresere, wilaya ya Chato, mkoani Geita, na kusababisha kifo cha Mchungaji
wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God, Mathayo Kachila (45), huku watu
wengine 10 wakijeruhiwa vibaya kwa mapanga.
Mchungaji huyo alichinjwa na watu wanaodaiwa ni kuwa waumini wa Kiislamu
kisha mwili wake kutelekezwa kwenye vibanda vya maduka ambavyo viko jirani na
eneo hilo jana.
Taarifa kutoka eneo la tukio hilo zilisema kuwa tukio hilo lilitokea asubuhi
ambapo chanzo chake kinatajwa kuwa ni watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Kiislamu
kuvamia bucha iliyokuwa ikiwauzia nyama Wakristo wa kijiji hicho waliokuwa
wamepanga foleni kwa wingi kusubiri huduma hiyo.
Wakiristo hao walikuwa wamechinja ng’ombe mmoja na mbuzi wawili eneo la
kanisani kabla ya kuipeleka nyama hiyo katika bucha hiyo iliyoko eneo la
Buseresere Sokoni na ndipo walipokumbana na kadhia.
Mashuhuda walisema kuwa tukio hilo lilianza saa 2:00 asubuhi muda mfupi baada
ya nyama kuwasili katika bucha hiyo ya Wakristo kwa ajili ya kuuzwa, jambo
linalodaiwa kuwakera Waislamu ambao waliivamia bucha hiyo kwa lengo la
kuifunga.
Taarifa ziliongeza kuwa wakati Wakristo wakitafakari uwepo wa Waislamu kwenye
bucha yao, ghafla walishtukia wenzao hao waliokuwa wametapakaa kwa wingi
wakiimwagia nyama hiyo vitu vinavyodaiwa kuwa sumu.
Kutokana na hali hiyo, Wakiristo walioonekana kukerwa na kitendo hicho na
ndipo mapambano yalipoanza kati ya pande hizo mbili huku Wakristo wakitumia mawe
na Waislamu wakitumia mapanga na majambia.
Ilidaiwa kuwa wakati mapambano hayo yakiendelea, mchungaji huyo ambaye kwa
sasa ni marehemu alifika eneo la tukio ili kujua kulikoni na ndipo alipojikuta
akishambuliwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za kichwani na kupoteza maisha
akikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu.
“Yaani ilikuwa kama mzaha tu...baada ya Wakristo kuleta ng’ombe mmoja na
mbuzi wawili kwenye bucha yao, tulishangaa kuona Waislamu wamevamia hiyo bucha
wakati tayari nyama ikiwa inauzwa na Wakristo wakiwa wamepanga foleni wakisubiri
kuhudumiwa,” alisema shuhuda mmoja.
Aliongeza kuwa Waislamu walipofika walitaka kuifunga ile bucha lakini
Wakristo waligoma na ndipo wengine walifika na kuimwagia ile nyama vitu kama
sumu na huo ukawa mwanzo wa machafuko.
“Kwa vile wenzetu walifika eneo hilo wakiwa na silaha tayari walianza
kuwakata Wakristo na kuivunjavunja ile bucha huku Wakristo wakijihami kwa
kutumia mawe lakini walizidiwa nguvu,” alisema shuhuda mwingine.
Waliojeruhiwa ni Saidi Ntahompagaze (45), Sadick Yahaya (40),Yasin Rajab
(56),Vicent Damon (22), wote wakazi wa Buseresere na mtu mmoja aliyefahamika kwa
jina moja la Ramadhan ambaye yuko mahututi katika wodi namba nane katika
hospitali ya wilaya ya Geita.
Hata hivyo watu wengine watano ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara
moja walitibiwa na kuruhusiwa kutokana na hali zao kuwa nzuri.
Polisi kutoka wilaya za Chato na Geita walifika eneo la tukio hilo saa 4:30
na kukuta uharibifu mkubwa umekwishafanyika ikiwa ni pamoja na duka la
Mwenyekiti wa BAKWATA Wilaya ya Chato, Yusuph Idd, linalotumika kwa biashara ya
M-Pesa na vinywaji baridi likiwa linateketea kwa moto.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Ludorick Mpogolo, aliyefika eneo la tukio muda mfupi
baada ya polisi kuwasili, mbali na kusikitishwa na kitendo hicho aliwataka
wananchi kuwa watulivu wakati serikali ikiangalia njia sahihi za kutatua mgogoro
huo ambao unakua kwa kasi kila kukicha.
Hivi karibuni mgogoro huo wa kidini umezidi kukua wilayani humo kwa pande
hizo mbili kila upande ukidai ndiyo wenye haki ya kuchinja nyama inayouzwa
buchani.
Chanzo: www.freemedia.co.tz [Tanzania Daima]
TAZAMA PICHA ZA MAJERUHI WA VURUGU HIZO
No comments:
Post a Comment