WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa ajira mpya kwa walimu 26,537 wa
shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru
Kawambwa, alisema kuwa utoaji wa ajira hizo haukufanyika kiholela bali ulifuata
tathmini mbalimbali zilizofanyika kubaini maeneo yenye upungufu wa walimu ili
kuwezesha kupeleka walimu kwa wingi katika maeneo hayo.
Waziri Kawambwa alisema kwa sasa taifa lina upungufu wa walimu wa masomo ya
Sayansi na Hesabu na mwaka huu, wameajiri walimu 2,037.
Kwa mujibu wa Waziri Kawambwa, wameajiri walimu 13,568 wa ngazi ya cheti
ambapo walimu 13,527 wamepangwa katika shule za msingi zilizopo kwenye
halmashauri na 41 wamepangwa katika shule za mazoezi zilizo chini yake.
Alisema kwa upande wa wahitimu wa elimu ya shahada na stashahada, wameajiri
walimu 12,893 kufundisha shule za sekondari zilizoko chini ya halmashauri, 59
wamepangwa kuwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu, huku walimu 21 wamepangwa
kufundisha shule za sekondari za mazoezi.
Aliongeza kuwa idadi hiyo ya walimu wenye shahada inajumuisha walimu 188 wa
elimu maalumu ambao wamepangwa katika shule za sekondari na vyuo vinavyotoa
elimu hiyo na kusema kuwa idadi ya walimu walioajiriwa mwaka huu imeongezeka kwa
asilimia 11 sawa na walimu 2,630, ikilinganishwa na walimu 23,907 walioajiri
mwaka uliopita.
Waziri huyo alisema kati ya walimu wa sekondari na vyuo waliochaguliwa,
walimu 1,286 ni wale walioomba ajira serikalini kutoka soko la ajira ambao ni
tofauti na wale wanaotoka vyuoni wakati walimu 841 walioshindwa mitihani mwaka
jana, wamepatiwa ajira baada ya kurudia mitihani yao na kufaulu.
Alisema orodha ya majina na halmashauri walizopangwa, zinapatikana katika
tovuti ya Wizara ya Elimu huku akitoa agizo kwa walimu waliohitimu ambao ni
waajiriwa kurudi katika vituo vyao walivyokuwa wanafanyia kazi kabla ya kwenda
masomoni.
Waziri Kawambwa alisema walimu wapya wanatakiwa kuripoti katika vituo vyao
vya kazi Machi mosi hadi Machi 9, mwaka huu ambapo orodha ya mishahara yao ya
mwezi huo itaingizwa katika utaratibu wa serikali.
“Walimu hao lazima waripoti ndani ya muda uliopangwa ili kuondoa usumbufu wa
ulipaji mishahara na atakayeshindwa kufika, atakuwa amejitoa kwenye ajira hiyo,”
alisema.
Alisema katika ajira hizo walimu wasishangae kupangiwa maeneo ambayo
hawajayachagua kwani uteuzi wao umelenga maeneo yenye uhitaji zaidi huku
akitolea mfano Mkoa wa Lindi ambao walimu wengi hukataa kwenda huko.
“Tumepanga kulingana na uhitaji, huwa tuna weka mwalimu mmoja kwa wanafunzi
46 lakini kwa hapa Dar es Salaam kuna walimu wengi na kufikia uwiano wa mwalimu
mmoja kwa wanafunzi 20,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment