Mkurugenzi Green Acres afichua siri nzito
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mh. Shukuru Kawambwa
WAKATI mjadala wa matokeo mabaya ya kidato cha nne ukiendelea kulitikisa
taifa, kashfa mpya ya matokeo hayo imeibuliwa.
Kashfa hiyo mpya imeibuliwa na Mkurugenzi wa Shule ya Green Acres, Julian
Bujugo, kwamba matokeo ya baadhi ya shule nchini ikiwamo yake
yamechakachuliwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Bujugo alisema kuwa baadhi ya wanafunzi
kwenye shule yake hawakufanya mitihani ya kidato cha nne, lakini matokeo
yanaonesha wamefaulu kwa kupata alama za juu.
Alitaja mfano wa mwanafunzi, Humphrey Sanga, mwenye namba 01197/148, ambaye
hakufanya mitihani hiyo lakini matokeo yanaonesha amefaulu kwa kupata alama
nzuri.
“Huyu mwanafunzi tulimsimamisha na hakufanya mitihani, lakini matokeo yake
yanaonekana amepata hivi; Civics D, Historia D, Jiografia C, Kiswahili D,
English C, Physics D, Chemistry C, Biology C, Basic Mathematics D, ambapo
amepata daraja la tatu pointi 24,” alisema Bujugo.
Alimtaja mwanafunzi mwingine, Martin Rushaigwa, namba 01197/0173, ambaye
alifanya masomo ya ‘Arts’.
Alisema matokeo ya mwanafunzi huyo yanaonesha kuwa ameongezewa alama za
masomo ya biashara ya Bookeeping na Commerce, ambayo hakuyafanya kabisa.
Alimtaja mwanafunzi mwingine aliyefanya mtihani huo lakini matokeo yake
yanaonesha amewekewa ‘absent’ na mwanafunzi mwingine, Mbazi Volta, hakufanya
mitihani lakini amepewa alama za ufaulu.
“Matokeo hayo yananipa wasiwasi kwamba yanaweza kuwa yamechakachuliwa,”
alisema Bujugo.
Mkurugenzi huyo anaiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kurudia
kusahihisha mitihani hiyo ili kuondoa ukungu ulioligubika taifa kwa sasa kuhusu
matokeo ya kidato cha nne.
“Naomba usahihishaji urudiwe, maana huu ni ubabaishaji mkubwa…matokeo hayo
yamewaathiri watoto kisaikolojia na sijui watakwenda wapi?,” alihoji.
Alisisitiza kuwa usahihishaji urudiwe kwani katika shule hiyo wanafunzi wenye
uwezo mkubwa tangu walipoanza kidato cha kwanza ndio waliofanya vibaya wakati
waliokuwa wakifanya vibaya, wameibuka na alama za juu.
Mkurugenzi huyo alisema wazazi wa watoto hao wanatarajiwa kukutana mwishoni
mwa wiki hii kujadiliana kuhusu matokeo hayo na hatua za kuchukua.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Msemaji wa Baraza la Taifa la Mitihani
(NECTA), John Nchimbi, alisema si kweli kuwa matokeo hayo yamechakachuliwa bali
ni matokeo halisi ya shule hiyo.
Alisema iwapo mkurugenzi wa shule hiyo ana shaka na matokeo hayo, alitakiwa
kufika katika ofisi za baraza hilo ili apatiwe taarifa sahihi kabla ya kutoa
taarifa katika vyombo vya habari.
“Mi nimeangalia hayo majina, naona yapo sawa na hata huyo mwanafunzi ambaye
anasemekana hakufanya mitihani na akapewa alama…napenda kusema kuwa alama
alizopewa si zake na hata katika orodha yetu anaonekana kuwa hakufanya
mitihani,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa na
wenzake, wamekuwa bubu kueleza endapo wako tayari kujiuzulu au la.
Tanzania Daima ilifika wizarani hapo jana kutaka kuonana na Waziri Kawambwa
ili atoe msimamo wake, mwandishi alijibiwa kuwa waziri huyo alikuwa kikaoni na
asingeweza kutoka.
Hata waziri alipopigiwa simu pamoja na kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno,
hakupokea wala kujibu ujumbe huo.
Kwa upande wake, katibu mkuu wa wizara hiyo naye hakuwa tayari kuzungumzia
suala hilo kwa madai kuwa alikuwa kikaoni.
Naye Naibu Waziri, Philipo Mulugo, alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi
kueleza msimamo wake, simu yake iliita bila kupokewa na hata hakuwa tayari
kujibu meseji ya ujumbe mfupi.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment