HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO
KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 31 JANUARY,
2013
Utangulizi
Ndugu
Wananchi;
Kama ilivyo ada naomba tuanze kwa kumshukuru
Mwenyezi Mungu, Mwenye Rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuzungumza
kwa mara nyingine kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina ya
Rais na wananchi wa Tanzania kila mwisho wa mwezi. Siku ya leo nitazungumzia
safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia. Pia nitazungumzia ujenzi wa bomba
la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara kuja Dar es
Salaam.
Safari za Kikazi Nje ya
Nchi
Ndugu
Wananchi;
Safari yangu
ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu.
Nchini Ufaransa licha ya kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya nchi zetu,
tumepata wawekezaji wengi wakubwa wenye nia thabiti ya kuja kuwekeza hapa
nchini. Pia tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa na mpango mwingine wa
ushirikiano. Mpango wetu wa sasa ulioanza mwaka 2006 uliisha mwaka 2010.
Mpango ule ulitusaidia sana kuboresha huduma za maji katika miji ya Utete mkoani
Pwani na Mpwapwa mkoani Dodoma.
Katika mkutano wa Kongamano la Uchumi wa
Dunia uliofanyika Davos, Uswizi, tumehakikishiwa ushirikiano katika kuendeleza
juhudi zetu za kuleta mapinduzi ya kijani ili tujihakikishie usalama wa chakula
na kupunguza umaskini vijijini na kukuza uchumi wa nchi yetu. Aidha, tulipata
bahati ya kushirikishwa katika mjadala wa kuanzishwa kwa programu kubwa ya
kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya upatikanaji wa umeme. Naamini
programu hiyo ikitekelezwa na wakubwa kuheshimu kauli na ahadi zao itakuwa
msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la
Sahara.
Ndugu
Wananchi;
Nchini Ethiopia tulishiriki katika
mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na katika kikao cha
African Peer Review Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya tathmini ya utawala bora
ya Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa. Kwa jumla hatuna mahali
tuliponyooshewa kidole kuwa tunafanya vibaya. Tumepongezwa katika mambo mengi
na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona hatuna budi kuyaboresha.
Nilipata nafasi ya kusema ambayo niliitumia kufafanua baadhi ya mambo
yaliyokuwamo kwenye taarifa. Niliwashukuru na kuahidi kuufanyia kazi ushauri
uliotolewa. Tathmini ya nchi yetu ilipitishwa kwa kauli
moja.
Vurugu za Kupinga Gesi Kusafirishwa
Kutoka Mtwara
Ndugu
wananchi;
Kama mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba, 2012 kule
Kinyerezi, Wilaya ya Ilala hapa Dar es Salaam, niliweka jiwe la msingi la ujenzi
wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es
Salaam. Karibu na mwishoni mwa Desemba, 2012 kukafanyika maandamano mjini
Mtwara kupinga ujenzi wa bomba hilo. Katika maandamano yale na baadaye kwenye
kauli za wanasiasa na wanaharakati yakatolewa madai kuwa gesi hiyo itumike kwa
maendeleo ya Mtwara na kwamba yale yanayotakiwa kufanyika Dar es Salaam
yafanyike Mtwara. Pia, zilitolewa shutuma nyingine dhidi ya Serikali eti kuwa
kwa miaka mingi imewasahau na haiwajali wananchi wa Mikoa ya Kusini na ujenzi wa
bomba hilo ni muendelezo wa hayo. Kauli mbalimbali za wanasiasa na wanaharakati
ni kama vile ziliongeza mafuta kwenye kaa la moto na kuuchochea mpaka kukatokea
matukio yaliyotusikitisha na kutshtua sote. Baadhi ya ndugu zetu wamepoteza
maisha na mali za watu na Serikali
kuharibiwa.
Ndugu
Wananchi;
Katika hotuba yangu ya kuaga mwaka 2012 na
kuukaribisha mwaka 2013, tarehe 31 Desemba, 2012, nililisemea jambo hili. Leo
mwezi mmoja baadae, napenda kusisitiza mambo mawili. Kwanza kwamba, si kweli
kuwa Serikali inapuuza Mikoa ya Kusini. Na pili, kwamba kujenga bomba la
kuipeleka gesi Dar es Salaam hakuinyimi Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa ya
kunufaika na gesi iliyopo Mtwara.
Ndugu
Wananchi;
Serikali imefanya, inafanya na ina
mipango ya kufanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya kuleta maendeleo katika Mikoa
ya Mtwara na Lindi. Ipo mipango ya kuboresha miundombinu, huduma za kiuchumi na
kijamii pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vikubwa na
vidogo. Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa
Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika Mto Rufiji maarufu kama Daraja la Mkapa.
Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya awali katika safari ya kutatua matatizo ya usafiri
ya Mikoa ya Kusini. Serikali ninayoiongoza mie iliachiwa kazi ya kukamilisha
ujenzi wa barabara za lami kufikia darajani na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa
wa Ruvuma. Kazi hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia kuimaliza.
Tulikamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mnazi-Mmoja hadi Nangurukuru. Mwaka
2009 tukaanza ujenzi wa barabara ya kilomita 56 kutoka Somanga
hadi Ndundu (darajani). Ujenzi wa kilometa 36 za mwanzo
ulienda vizuri. Bahati mbaya ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho
umechelewa sana kwa sababu ya mmiliki wa kampuni iliyokabidhiwa kufanya kazi
hiyo kufariki. Kwa sababu hiyo, kampuni ilipata mtikisiko kiasi na kusababisha
kazi kutotekelezwa kwa kasi tuliyoitarajia. Sasa mambo yametengemaa na kazi
inaendelea kwa kasi nzuri. Matumaini yetu ni kuwa ifikapo mwezi Desemba, 2013
kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Hali kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee Benjamin Mkapa
alituachia jukumu la kumaliza ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma na
ujenzi wa barabara ya lami kuanzia Mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Tumelikamilisha
Daraja hilo na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi hadi Mangaka
umekamilika. Mchakato wa kujenga barabara ya kwenda Songea na kwenda Darajani
umefikia mahala pazuri. Tenda ya ujenzi wa barabara kutoka Tunduru hadi
Mangaka mpaka Darajani imeshatangazwa. Kama mambo yataenda sawa miezi mitatu
ijayo mjenzi atapatikana. Wakati huo huo ujenzi wa barabara kutoka Namtumbo
hadi Songea – Mbinga na Namtumbo – Tunduru unaendelea. Hivyo basi, kwa barabara
ya “Mtwara Corridor” kazi iliyobaki ni kutoka Mbinga kwenda Mbambabay
ambayo tutaifanya wenyewe kama tulivyofanya kwa Mnazi Mmoja – Nangurukuru na
Somanga – Ndudu na Daraja la Umoja.
Ndugu
Wananchi;
Ipo pia mipango ya kuipanua na kuijenga upya
bandari ya Mtwara ili iweze kuhudumia mahitaji ya utafutaji na uchimbaji wa gesi
baharini, kuhudumia na kuvifanyia matengenezo vyombo vinavyotumika katika
utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi. Pia iweze kuhudumia shughuli za
kiuchumi zitakazotokana na uchumi wa gesi pamoja na zilizopo sasa.
Nilipozungumza na makampuni ya utafutaji gesi pale Mtwara tarehe 25 Julai, 2011
waliomba nikubali bandari ya Mtwara iwe mahali pa kuhudumia vyombo vyote
vinavyofanya shughuli ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta katika pwani
ya Afrika ya Bahari Kuu ya Hindi. Pia waliomba kuwa sehemu hiyo ya bandari iwe
bandari huru. Niliwakubalia bila ya kusita na tayari eneo la hekta 110
zimeshatengwa na kutangazwa rasmi kuwa bandari huru. Vile vile
waliomba wapewe sehemu ya bandari ya sasa kuendeshea shughuli na eneo la kujenga
kituo cha mitambo ya kuchakata gesi na kusafirisha
nje.
Ndugu
Wananchi;
Baada ya kuzungumza na makampuni ya utafutaji
gesi na mafuta na kuelezwa mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara
inahitaji kupanuliwa na kujengwa upya. Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya
Bandari walikuwepo na walinihakikishia kuwa watafanya
hivyo.
Tayari eneo la bandari limeongezwa kutoka
hekta 70.68 hadi 2,693.68. Eneo la bandari
huru limeshatengwa hivyo hivyo na eneo la kampuni ya Dangote na makampuni ya
gesi yaliyopo. Aidha, mchakato wa kupanua bandari iliyopo, kujenga gati mpya na
kuendelea na ujenzi hadi maeneo ya Msanga Mkuu ipo katika hatua mbalimbali za
matayarisho na utekelezaji.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mkoa wa Lindi mipango ya
kupanua na kuijenga upya bandari ya Lindi imefikia hatua nzuri. Naibu Waziri wa
Uchukuzi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo tarehe 1 Desemba, 2012
nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Lindi ya tarehe 1
mpaka 5 Desemba, 2012. Hali kadhalika mipango ya kujenga bandari ya Kilwa iko
mbioni. Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi moja ya makampuni yaliyogundua gesi
baharini wameamua kujenga bandari na kituo cha kuchakata na kusarifisha gesi nje
ya mkoa huo kama ilivyo kwa Mtwara. Naambiwa wametambua maeneo matatu,
kilichobakia ni kuamua mojawapo ili ujenzi
uanze.
Ndugu
Wananchi;
Nilipotoka bandari ya Mtwara, siku ile
nilitembelea Chuo cha VETA na kuzungumza na viongozi wa VETA taifa na wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa na mitaala ya kutoa mafunzo mahsusi
yanayohitajika na sekta ya gesi na mafuta. Nilisisitiza kwamba tuwapatie vijana
wetu mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni ya gesi na yale
yatakayokuwa yanatoa huduma kwa makampuni hayo. Nilisema tusipofanya hivyo,
makampuni hayo yataajiri watu kutoka nje na hatutakuwa na sababu ya kuwalaumu
wala kulalamika.
Nafurahi kwamba agizo langu hilo limefanyiwa kazi
ipasavyo. Hivi sasa katika chuo cha VETA Mtwara mafunzo hayo yanatolewa.
Kampuni ya PetroBrass ya Brazil inaendesha mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana
25 kutoka mkoani Mtwara. Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana na Kampuni ya
Gesi ya Uingereza (British Gas) na Volunteers Service Overseas ya Uingereza,
kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo Enhancing
Employerbility Through Vocational Training. Programu hii
inalenga kutoa kozi zitakazowafanya wahitimu kuweza kuajiriwa katika sekta ya
gesi. Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed
Gharib Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012.
Ndugu
Wananchi;
Chini ya programu hii, walimu wa masomo
yanayohusiana na gesi wanaongezewa ujuzi ili waweze kufikia viwango vya
kimataifa. Vile vile, Wizara ya Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa
kudhamini wanafunzi 50 kutoka mkoa wa Mtwara kusoma chuoni hapo
ambao tayari wameshahitimu mafunzo ya msingi ya uunganishaji vyuma viwandani.
Mchakato wa kuwapata wanafunzi 50 kwa ajili ya mafunzo kama
hayo kutoka mkoa wa Lindi unaendelea. Nimeambiwa mpaka wameshawapata vijana 25
bado 25.
Hali kadhalika, Wizara ya Nishati na
Madini inadhamini wanafunzi 10 kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Dodoma
ambako kozi za mafuta na gesi zinatolewa. Kipaumbele kwa udhamini huu unatolewa
kwa wanafunzi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za kudahiliwa katika
mafunzo haya. Wamepatikana watatu. Wataalamu hawa na wengine wa fani
mbalimbali za gesi na mafuta watafundishwa kwa kiwango cha shahada ya kwanza na
baadae uzamili na uzamivu ili nchi yetu ijitosheleze kwa wataalamu wa sekta
hii.
Kupanga Mji wa
Mtwara
Ndugu
Wananchi;
Baada ya kutembelea bandari ya Mtwara na
Chuo cha VETA, nilikaa na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Manispaa ya
Mtwara. Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu wa kuwa na mpango
kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango ambao
utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji wa uchumi wa
gesi. Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda, biashara, makazi,
mahoteli, huduma za afya, elimu, mapumziko na burudani, viwanja vya michezo na
kadhalika. Kazi ya kutayarisha Masterplan hiyo imeanza na Manispaa ya
Mtwara inashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Makazi.
Kwa upande wa uwekezaji nafahamu kuwa mpaka sasa
makampuni 51 yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda,
hoteli, shughuli za uchukuzi na huduma hasa kwa sekta ya gesi. Wanachosubiri ni
kutengewa maeneo ya kujenga, waanze. Hivyo kukamilika mapema kwa
Masterplan ya mji wa Mtwara kutasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji huu
kufanyika. Viwanda hivi vyote vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mtwara na
Watanzania kwa jumla. Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi wa kiwanda cha
saruji watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa.
Ndugu
Wananchi;
Kabla hata ya
ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na mipango ya kutumia gesi ya
Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kuzalisha mbolea na kutumika
katika kiwanda cha saruji. Kwa upande wa umeme kulikuwa na mpango wa kujenga
mtambo wa kuzalisha Megawati 300 kwa kushirikiana na mwekezaji
binafsi. Bahati mbaya wakati wa matatizo ya kifedha ya dunia mwaka 2009
mwekezaji huyo akashindwa kupata mkopo, hivyo mradi ukasimama kutekelezwa.
Haukufa wala haukuhamishiwa Dar es Salaam au Bagamoyo kama ambavyo imekuwa
inapotoshwa kwa makusudi. Mradi huo bado upo, tena mpango wa sasa ni kujenga
Megawati 600 zitumike Mtwara na zingine kuziingiza kwenye gridi
ya taifa kupitia Songea.
NduguWananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha mbolea, wawekezaji
wengi wameshajitokeza tangu mwaka 2008 mpaka sasa. Mchakato umefanyika wa
kuchambua wawekezaji wenye sifa na kutambuliwa. Mambo mawili yamechelewesha
utekelezaji kuanza. Jambo la kwanza ni wawekezaji na kampuni ya Artumas
iliyokuwa mbia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (T.P.D.C) wakati ule,
kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya kuwauzia gesi. Wawekezaji walitaka bei
ya gesi ipunguzwe, lakini kampuni ya Artumas na T.P.D.C. hawakuwa tayari
kupunguza zaidi ya kiasi walichopunguza, ambacho wawekezaji bado waliona hailipi
kwa kuzalisha mbolea.
Sababu ya pili ni matatizo ya kifedha
yaliyoikumba kampuni ya Artumas katika kipindi hicho. Kufuatia machafuko ya
masoko ya fedha na mdororo wa uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni ya Artumas
iliathirika na kulazimika kuuza hisa zake kwa wawekezaji wengine. Katika
kipindi hicho ilichopitia kampuni, mazungumzo na uwekezaji wa kiwanda cha mbolea
hayakuweza kupewa kipaumbele. Mtazamo wa sasa wa wabia wapya na T.P.D.C. ni
kuwa wao wenyewe sasa wawekeze katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea. Serikali
imekubali rai yao hiyo na wanaendelea na
matayarisho.
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wa
kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni ya Dangote ucheleweshaji ulikuwa
kwa sababu mbili. Kwanza, kampuni ya Dangote iliomba eneo zaidi ya ililokuwa
imeomba na kupewa. Hoja yao ilikuwa kwamba eneo la ziada walilokuwa wanaliomba
ndilo lenye malighafi nyingi na bora kwa utengenezaji wa saruji. Hivyo,
waliamua kusubiri mpaka watakapopewa eneo
hilo.
Bahati mbaya eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na
mtu mwingine na alikuwa na hati miliki nalo. Halmashauri ya Mtwara iliomba
Serikali eneo hilo litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote. Serikali
ilikubali. Hata hivyo, mchakato ulichukua muda na hata pale ulipokamilika
mwenye eneo aliupinga uamuzi wa Serikali Mahakamani. Kesi ilichukua muda
kusikilizwa na kumalizika. Bahati nzuri Serikali ikashinda na mara baada ya
uamuzi wa Mahakama ndipo kampuni ya Dangote ikamilikishwa eneo
hilo.
Kampuni nayo ilichukua muda kuanza. Hivi sasa,
timu yake ipo kwenye eneo na mradi uko tayari kuanza kutekelezwa. Niliambiwa
kuwa katika magari yaliyopigwa mawe katika fujo za Mtwara ni pamoja na lile la
mradi huu. Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote.
Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya kweli. Ni uzushi wa
makusudi wa watu wenye nia mbaya na Serikali. Huwezi kudai kuwa mtetezi wa
wananchi wa Mtwara kwa hoja za uongo na kufanya upotoshaji wa makusudi
kabisa.
Ndugu
Wananchi;
Ujenzi wa
bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu. Zilijengwa hisia kuwa gesi yote
inapelekwa Dar es Salaam na kwamba Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatayotokana
na gesi hiyo. Na, wengine wakasema gesi inapalekwa Bagamoyo ili kuzidisha
chumvi na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba Rais anapeleka
gesi kwao. Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo. Pili, ukweli ni kwamba
pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya Mtwara, Lindi na Dar es
Salaam na kubaki. Gesi itakayoletwa Dar es Salaam ni asilimia
16 tu ya gesi yote iliyoko Mtwara kwa miaka ishirini ijayo. Hivyo
asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa nje ya
nchi na kupelekwa kwingineko nchini.
Kwa sababu hiyo, ndugu zetu wa Mtwara
hawana sababu ya kuwa na wasiwasi. Ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na
ya miaka mingi ijayo. Viwanda vinavyotumia gesi kama mali ghafi na vile
vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya kutosha. Kwa upande wa
uzalishaji umeme hali kadhalika ipo gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi
zaidi. Hivi sasa tunacho kituo kinachozalisha umeme wa megawati
15 unaotumika Mtwara, Lindi, Tandahimba, Newala, Masasi, Nachingwea,
Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo hautumiki wote hivi
sasa.
Ndugu Wananchi;
Nayaeleza yote
haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa tunawathamini sana na kuwajali.
Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya
Kusini. Aidha, sitakuwa tayari kuwaruhusu watu au mtu ye yote Serikalini
kuwapuuza wananchi wa Mikoa ya Kusini au mkoa wo wote hapa nchini. Hiyo
haitakuwa sawa. Nilishasema siku za nyuma na napenda kurudia tena leo kuwa
kwangu mimi hakuna mkoa ulio bora kuliko mwingine. Ni kutokana na msimamo wangu
huo ndiyo maana tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za Serikali katika mikoa
iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa. Kazi ya ujenzi wa barabara za lami
iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma,
Rukwa, Kigoma na Kagera inajieleza yenyewe. Mipango ya kuboresha Kiwanja cha
Ndege cha Mtwara kufikia hadhi ya kimataifa na uboreshaji wa viwanja vya ndege
vya Lindi na Kilwa ni ushahidi mwingine kati ya mambo mengi tunayoweza kuyataja.
Ndugu
Wananchi;
Haya
niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa na kuelezwa kwa kina na
Mawaziri na Wakuu wa Idara husika za Serikali na Mashirika ya Umma pale Mtwara
katika mkutano wa Waziri Mkuu na viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa na
wazee wa Mkoa wa Mtwara tarehe 29 Januari,
2013.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi
kwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya
kule Mtwara. Uvumilivu wake, usikivu wake na utulivu wake vimesaidia sana
kulivusha taifa katika moja ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta nchi yetu tangu
Uhuru. Nawapongeza Mawaziri na Wakuu wa Mashirika ya Umma na Idara za Serikali
kwa mchango wao muhimu walioutoa, uliosaidia kufafanua masuala ambayo yalikuwa
hayaeleweki vizuri. Kwa wao nawasisitiza na kuwakumbusha wajibu wao wa
kuelimisha jamii kuhusu shughuli wazifanyazo. Wakifanya hivyo mara kwa mara
migongano haitakuwepo na wapotoshaji hawatapata
nafasi.
Ndugu
Wananchi;
Nitakuwa mwizi
wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu
ya dini, viongozi wa jamii, wazee, wana-Mtwara na makundi mbalimbali ya jamii,
kwa muda waliotumia kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza wasaidizi wake
wakifafanua masuala mbalimbali. Uvumilivu wao na uelewa wao npyo vilivyosaidia
kurejesha hali kuwa ya kawaida. Nawaomba nao sasa, wote kwa pamoja washirikiane
na Serikali kuelimisha umma kuhusu ukweli wa mambo. Pia watumie nafasi hiyo
kutahadharisha jamii na kuwataka watu kuwa waangalifu na kupima maneno
wanayoambiwa na watu. Wajiepushe na maneno au vitendo vinavyofarakanisha,
kuchonganisha na kupandikiza chuki dhidi ya watu au Serikali. Waambieni kuwa
ghasia hukimbiza wawekezaji kwani wakipata hofu kuwa hali ya amani na usalama ni
ya mashaka, watatoka kwenda kuwekeza kwingine. Vyema iwe hapa hapa nchini,
lakini wanaweza kwenda nchi nyingine na sisi kupoteza
kabisa.
Ndugu
Wananchi;
Nawapa pole wananchi wa Mtwara na Masasi
kwa usumbufu walioupata kutokana na ghasia zilizofanywa. Nawapa pole waliofiwa
na kujeruhiwa. Nawapa pole waliopoteza au kuharibiwa mali zao. Kwa kweli
inasikitisha na kufadhaisha kuona watu wanafanya vitendo vya kuua, kuchoma moto
nyumba za watu na majengo ya Serikali pamoja na , kuharibu na kuiba mali za
watu. Huu ni uhalifu ambao hauna maelezo na haukubaliki. Tunaviachia vyombo
husika vya dola na sheria kutimiza wajibu wao. Kwa waliohusika iwe fundisho
kwao na kwa wengineo kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wengine siku
zijazo. Sasa wameachwa pekee yao wakati wenzao wako huru na kufaidi
maisha.
Ndugu Wananchi;
Hili sakata la bomba la gesi limefika mahali
pazuri. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Mungu Ibariki
Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania!
Asanteni Sana kwa
Kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment