Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Monday, February 18, 2013

MAJIBU YA MNYIKA KWA AKINA NAPE NA RIDHIWANI KUHUSU ELIMU YAKE

John Mnyika 17:15 Today
Nilikuwa katikati ya kazi jimboni
nikaambiwa kwamba kuna mwito
humu wa Nape na Ridhwan kutaka
nieleze elimu yangu. WanaCCM
walianza suala hili kwa ari, nguvu
na kasi mpya niliposema kwamba
nchi imefika hapa ilipo kwa
sababu ya udhaifu wa Rais
Kikwete, uzembe wa Bunge na
upuuzi wa CCM.
Nikapuuza, naona sasa limeibuka
tena kwa ari, nguvu na kasi zaidi
baada ya yaliyojiri bungeni kuhusu
hoja binafsi niliyowasilisha
bungeni kuhusu maji na mkutano
wa hadhara wa tarehe 10
Februari 2013 na masuala ambayo
niliipa Serikali wiki mbili
kuyatolea majibu ama sivyo
nitaongoza maandamano ya
wananchi kwenda Wizara ya Maji
kutaka uwajibikaji na hatua za
haraka.
Kwa mara nyingine tena
zinafanyika jitihada za kuhamisha
wananchi kwenye mjadala kwa
kumshambulia mtoa hoja badala
ya hoja, sasa ili turejee kwenye
mijadala ya msingi ni muhimu
niweke kumbukumbu sawa kuhusu
masuala kadhaa kama
yalivyoombwa.
Elimu yangu sio siri, nimegombea
ubunge mara mbili mwaka 2005
na 2010 na mara zote nimeeleza
kuhusu suala hili; Nape na
Ridhwan wangetumia tu elimu yao
wangetafuta kwenye mitandao na
kukuta majibu wanayoyatafuta.
Nieleze kwa muktasari tu;
nimesoma shule ya msingi
Mbuyuni Dar Es Salaam (nilikuwa
mwanafunzi wa kwanza kwa mkoa
wa Dar es Salaam).
Nilichaguliwa kwenda Shule ya
Sekondari ya Ilboru wakati huo
ikiwa ya vipaji maalum, sikwenda;
wito ulinituma kwenda Seminarini.
Nilisoma Franciscan Seminary
Maua (FRASEMA) mpaka kidato
cha nne; nilipata daraja la kwanza;
nikiwa na alama A katika masomo
tisa.
Ningeweza kwenda shule yoyote
ya Serikali ya kidato cha tano na
sita yenye mchepeo ambapo
ningeutaka; lakini niliamua kubaki
Dar es Salaam shule ya Tambaza
kwa sababu nilitaka kusoma huku
nikiendelea na harakati ambazo
nilizianza kabla.
Hapa ndio ilikuwa chanzo cha
mimi kuingia kwenye kazi ya
kuhamasisha mabadiliko kwenye
mimbari nje ya utumishi wa
madhabahuni. Tukio lililobadili
mwelekeo wa maisha yangu,
mwaka 1998 nikiwa kidato cha
nne; nimesoma na tumeanza
mitihani tukatangaziwa kwamba
mitahani yote imefutwa baada ya
kuvujishwa.Tukarudishwa
nyumbani kipindi hicho nikaenda
kwenye mafungo kujitafakari
kwenye mkoa mmoja nikarejea
Dar es Salaam nikakutana na
wanaharakati kadhaa wa asasi
zisizo za kiserikali; maelezo
kuhusu ufisadi yalinifanya nione
nina wajibu kwa nchi yangu,
nikarejea Seminarini kufanya
mitihani nikiwa na fikra tofauti.
Matokeo yakatoka nimefanya
vizuri, kwa mifumo yetu mibovu
ya wakati huo kwa mara ya pili
tena Serikali hii inayoongozwa na
CCM haikutambua vipaji na
nikapaswa niendelee kujilipia ada
mwenyewe kama ilivyokuwa kwa
ngazi nyingine za elimu
zilizotangulia; hapa nikakata shauri
kwamba nitatumia uwezo na
uadilifu wote ambao Mwenyezi
Mungu amenijalia kuwezesha
mabadiliko katika taifa letu.
Nikaamua kuacha kwenda kwenye
shule za bweni mikoani na kubaki
Dar es salaam nisome Tambaza
huku nikiendelea na kazi za
harakati; wakati huo nikihamasisha
masuala ya ukombozi wa vijana
nchini. Pamoja na kusoma kutwa
huku nikifanya kazi nilipata daraja
la pili katika kidato cha sita.
Taasisi nilizoanzisha au
nilizoongoza katika kipindi hicho
na kazi nilizofanya sio siri na
zinapaswa kujieleza zenyewe kwa
matendo badala ya maneno.
Katika kipindi hicho, wakati huo
kukiwa hakuna Mfuko wa Elimu
wala Bodi ya Mikopo nikashiriki
katika ushawishi wa mabadiliko ya
kimfumo; nilikwenda Dodoma,
tukakutana na wabunge na
mawaziri nikawasilisha mada
“Towards a more functional
education in Tanzania”, wakati huo
nikiwa mwanafunzi wa Sekondari.
Kati ya wabunge waliosikiliza mada
niliyoiwaisilisha wakati huo sasa ni
Rais Jakaya Kikwete ( Ridhwan
ukiwa nyumbani unaweza
kumwuliza maoni yake aliyotoa
siku hiyo kuhusu ugharamiaji wa
elimu na suala la mauaji ya
mwanafunzi wa Iyunga Michael
Sikupya). Nilipotoka kwenye
mkutano ule Dodoma mwishoni
wa miaka ya tisini, nilikata shauri
kwamba mwaka 2005 nitagombea
Ubunge hii ni baada ya kushudia
aina ya wabunge waliokuwepo.
Mwaka 2002 nilijiunga na Chuo
Kikuu cha Dar es Es Salaam
kusomea “Bachelor in Business
Administration (BBA) kwenye
programu ya jioni; nilifanya hivyo
kwa kuamua kwa kuwa nilitaka
nisome huku nikiendelea na kazi.
Mkuu wa Programu hiyo wakati
huo alishangaa sana kwa umri
wangu (wakati huo shahada hiyo
walikuwa wakisoma wazee watu
wazima wafanyakazi) na matokeo
yangu (kwa kuwa yaliniruhusu
kwenda kuingia kusoma katika
mfumo wa kawaida). Nikamweleza
akanielewa kwamba sitaki kusoma
kama wanachuo wengine wa
kawaida, uamuzi wangu huo
ulikuwa na gharama kwa
kuwatafsiri yake ni kuwa nilipaswa
kujisomesha binafsi.
Kwa hiyo mimi ni kati ya wale
ambao hatudaiwi na nchi hii kwa
maana ya kwamba sijawahi
kuchukua ruzuku wala
kusomeshwa na Serikali hii
inayoongozwa na CCM; nimesoma
kwa jasho la wazazi wangu na
langu binafsi. Kwa hiyo, nijibu tu
kuhusu elimu yangu ya juu
kwamba nimesoma miaka mitatu
Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam
(mtu aliyosoma kwa kiwango
hicho kwenye baadhi ya vyuo
duniani hupewa associate degree).
Mwaka 2004 ikaanza misukosuko
mbalimbali, mwaka huo ulikuwa
ndio unatungwa muswada wa
Sheria ya Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu, haya matatizo
yanayotokea leo niliyatabiri wakati
huo. Niliwasilisha mada kwa
wanachuo kwenye ukumbi wa
Nkurumah kuchambua udhaifu wa
muswada huo na kupata maoni ya
wanafunzi kuhusu marekebisho
yanayohitajika; wanachuo
wakapitisha azimio la kwamba
muswada huo upingwe.
Kesho yake nikiwa Morogoro
kikazi kukafanyika mgomo
hatimaye wanafunzi wakapigwa na
kukamatwa.Nakumbuka nilikatiza
kazi niliyokuwa nafanya nikarejea
kwa kuwa Chuo kiliweka sharti
kwamba lazima wanachuo waache
mgomo ndio waliokamatwa
waachiwe. Wakati huo Serikali ya
wanafunzi ilikuwa haisikilizwi,
mimi na wengine wachache
tukajitolea kuzunguka kampasi na
hosteli zote kushawishi wanafunzi
kurejea masomoni na wakafanya
hivyo.
Serikali ya CCM ikatoa maelekezo
kwamba kama tumeweza
kuwafanya wanafunzi warudi, hata
kama sikushiriki mgomo na
sihusiki na masuala ya mikopo
kwa kuwa ni mwanafunzi
ninayejilipia mwenyewe lazima
nisimamishwe; nikiwa mwanafunzi
pekee wa BBA niliyesimamishwa
wakati huo.
Nikarejea baada ya muda tayari
kukiwa na mvutano kati yangu na
utawala, mwaka 2005 nikaamua
kugombea Ubunge wakati huo
nikiwa mwanafunzi; mvutano
ukaongezeka zaidi. Na utawala wa
Chuo ukawa unapata mashinikizo
mengi kutoka kwa Serikali na
CCM; wengine wakipendekeza
nifukuzwe, wengine nifelishwe na
wengine nisiruhusiwe kuingia
katika maeneo ya Chuo jioni
masomoni kwa kuwa nitakuwa
nafanya kampeni.
Nikawa katika mtanziko(dilemma)
wa kuchagua ama kuendelea na
masomo na kujitoa au kupunguza
nguvu kwenye kampeni (mbinu
nyingi zilitumika wakati huo, sio
sehemu ya majibu yangu ya leo)
au niendelee na kampeni. Nafsi
yangu ikanituma kuamua kuandika
barua yakuahirisha masomo,
baada ya matokeo ya uchaguzi wa
mwaka 2005 mazingira yalikuwa
yamebadilika sana kuweza kurejea
kumalizia mwaka au miezi
michache iliyokuwa imebaki.
Mwaka 2006 nikiwa Marekani
nilitafakari sana na kufikia uamuzi
wa kuendelea na kazi hii ya
kusimamia mabadiliko na
kujiandaa na uchaguzi wa mwaka
2010. Mwaka 2010 niligombea
tena na kushinda wakati huo huo
nikiongoza kazi za kitaifa za
kampeni makao makuu pamoja na
Profesa Baregu na wengine;
hakuna mahali popote
nilipowadanganya wananchi kuhusu
elimu yangu, kama nilivyoeleza
hapo juu.
Naamini wananchi wa Jimbo la
Ubungo walinichagua kwa uwezo
na uadilifu wangu, na walijua pia
kwamba nilikuwa Chuo Kikuu cha
Dar es salaam kwa miaka mitatu.
Naamini elimu ni kitu muhimu
sana kwa kiongozi, lakini wapo
wenye elimu kubwa ya vyeti lakini
hawajaelimika na wapo wenye
elimu ndogo sana ya vyeti lakini
wanaelewa mkubwa wa kutimiza
majukumu yao ya uongozi.
Tangu mwaka 2012 na 2013,
nimekuwa kwenye mtanziko
mwingine na viongozi wangu ndani
ya chama wanafahamu; niliomba
kuachia majukumu mengine yote
katika chama ili nibaki na ubunge
peke yake niweze kuwatumikia
wananchi wakati huo huo
niendelee na masomo zaidi ya
elimu ya juu katika fani
inayoendana na kazi ninayoifanya
ya sasa na matarajio yangu ya
baadaye.
Hata hivyo, kwa mwelekeo huu
wa Serikali na CCM leo nieleze tu
kwamba nikifanya hivyo itakuwa
faida zaidi kwa watawala
tunapoelekea mwaka 2015; hivyo,
nimeamua kama nilivyoamua
mwaka 2005; kwamba nitarejea
masomoni baada ya CCM
kuondoka madarakani na Tanzania
kupata Serikali mpya
itakayoongozwa na CHADEMA. Kwa
sasa nitaendelea kujisomea kila
siku ninapopata wasaa kwa kuwa
elimu haina mwisho.
Wakili Ridhwan katika maandiko
yake amefanya rejea ya suala
Kihiyo wa CCM Temeke, nashauri
arejee kwenye hukumu ya kesi ile
na marekebisho ya sheria
yaliyofanywa na Serikali yaCCM
kuwalinda wabunge wake vihiyo
baada ya hukumu.
Mifano hailingani kwa sababu
mimi sijatoa maelezo ya uongo
popote. Lakini hata kwa wabunge
wa CCM wanaotoa maelezo ya
uongo wa wapiga kura,
marekebisho hayo yamewawekea
wigo wa mianya yakutokea
mahakamani. Zamani fomu
zakuogembea zilikuwa na mahali
pa kujaza elimu ya mgombea,
sasa kipengele hicho
kimeondolewa. Hivyo, suala la
kughushi na kutoa taarifa za uongo
haliko kama ilivyokuwa awali,
isipokuwa kesi inaweza
kufunguliwa ya ukiukwaji wa
kawaida wataratibu za kampeni
kwa kuwashawishi wapiga kura
kwa taarifa za uongo (ndani ya ule
muda wa kisheria wa kesi
kufunguliwa ambao ulishapita).
Halafu ni jukumu la mlalamikaji
sio tu kuthibitisha kwamba uongo
ulitolewa bali uongo umeathiri
vipi matokeo. Ndio maana leo
kuna vihiyo wengi tu wa CCM
ndani ya Bunge lakini ni vigumu
kuwabana kwa mfumo wetu wa
sasa. Baada ya majibu hayo
marefu, naamini sasa Nape
unaweza sasa kurejea kwenye
kujibu; Elimu ya Mnyika ina
uhusiano gani na CCM kuahidi
kwenye ilani yake na kushindwa
kutekeleza kwamba ifikapo mwaka
2010 asilimia 90 ya wananchi wa
mijini ikiwemo Dar essalaam
watakuwa wanapata maji safi na
salama? Ridhwan kwa kuwa
umeweza kufanya rejea unaweza
pia kueleza ni kwanini Rais
Kikwete mwaka 2011 aliahidi kuwa
tatizo la maji Dar es Salaam
litakuwa historia mwezi Februari
2013 lakini mwezi huo umefika na
matatizo bado ni makubwa?
JJ

No comments:

Post a Comment