Dr. Willibroad Peter Slaa
KWA mara ya kwanza, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ameweka bayana chimbuko la mkataba wa makubaliano
kati ya serikali na makanisa, huku akiwasihi Watanzania kujiepusha na malumbano
yenye hisia za udini.
Dk. Slaa alitoa tahadhari hiyo jana katika ufafanuzi wake aliouandika kwenye
mtandao wa kijamii wa Jamii Forum, kuhusu mkataba huo (Memorandum of
Understanding - MOU) kati ya Baraza la Kikristo Tanzania, Baraza la Maaskofu
Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa amelazima kutoa ufafanuzi baada ya kuona mkataba huo umewekwa
kwenye mtandao wa kijamii, huku watu wengi wakiwa wanauzungumzia kwa kupotosha
ukweli wa jambo hilo, na kulihusisha na masuala ya udini.
“Kama mnavyoona, mimi nilikuwa nafahamu historia yote, nafahamu MOU, lakini
sikuwa nayo. Mtu huwezi kujua kila kitu, na au kuwa na kila kitu, ‘we need to
complement each other’.
“Ninarudia kuwaomba wenzangu, tumetumia muda mrefu sana kujadiliana kwa hisia
ya aina mbalimbali. Watanzania hatukuzoea huko nyuma kuulizana dini zetu, wala
kabila, wala ukanda. Haya mambo tukiyaendekeza taifa letu litakuwa hatarini,”
alisema.
Alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa, kubomoa ni kazi nyepesi, lakini
kujenga tena inachukua muda mrefu, na ni kazi ngumu, na wakati mwingine hata
ukifanikiwa huwezi kujenga kama ilivyokuwa.
Akifafanua historia ya jinsi na kwanini MOU hiyo ilizaliwa, Dk. Slaa alisema
kuwa huko nyuma serikali ilitaifisha shule nyingi za madhehebu ya dini.
Kwamba utaifishaji huo uliendana pia na ardhi, hasa ikizingatiwa kuwa wakati
huo shule zilijengwa kwenye maeneo ya madhehebu ya dini na papo hapo kukiwa na
kanisa, nyumba za mapadre na vitu vingine.
Alisema kuwa kwenye miaka ya 1980, madhehebu yakataka warudishiwe ardhi yao,
hasa ambayo ina majengo mengine yasiyohusiana na shule hizo.
Dk. Slaa alifafanua kuwa, mchakato wa mjadala ulishika kasi mwaka 1986 Baraza
la Maaskofu Katoliki (TEC), lilipopitisha azimio rasmi na kumtaka Katibu Mkuu,
awasiliane na serikali kuanzisha mchakato wa kufanya upembuzi na kutenga ardhi
ya shule rasmi, kutoka kwenye ardhi inayotumika kwa huduma nyinginezo za
madhehebu ya dini.
“Wakati huo mimi (Dk. Slaa), ndiye nilikuwa Katibu Mkuu wa TEC baada ya
kupokea rasmi kazi hiyo Desemba1985. Wakati huo madhehebu yaliishakudai
yarudishiwe shule zao kwa kuwa zimegeuka kuwa aibu kwa kukosa ukarabati, na ziko
kwenye hali mbaya sana,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali ilikuwa imekataa ombi hilo kwa lengo la kuwa, shule
hizo zinawahudumia Watanzania wote bila ubaguzi, jambo ambalo ndilo lilikuwa
lengo kuu la utaifishaji, na sababu ya utaifishaji ilikuwa bado
inaendelelea.
Dk. Slaa aliongeza kuwa, mawasiliano yalipoanza na serikali, wakati huo
kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu, serikali iliomba TEC na
madhehebu ya dini kwa ujumla, kama yanaweza kusaidia ukarabati wa shule hizo kwa
kuwa ziko kwenye hali mbaya na hali ya uchumi wa nchi haikuwa nzuri.
“Wakati mchakato huo kwa upande wa elimu umeanza, kulikuwa pia na mgogoro
kati ya serikali na TEC baada ya serikali kuichukua Hospitali ya Bugando kwa
utaratibu huo huo wa kuitaifisha,” alibainisha.
Kwamba hospitali hiyo ilikuwa kwenye awamu ya pili ya ujenzi kwa msaada
mkubwa wa Shirika la la Maendeleo la Baraza la Maaskofu Katoliki la Ujerumani
(Misereor).
Alisema kuwa Katibu Mkuu wa TEC alipowasiliana na wahisani, walikataa
katakata kujihusisha tena na ujenzi au ukarabati wa shule au hospitali, vituo
vya afya na zahanati, kwa kuhofia kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikitaifisha
huduma hizo bila majadiliano ya aina yoyote.
Wahisani hao walisema hawawezi kuwekeza fedha za walipakodi wao (Ujerumani),
lakini walikuwa tayari kuendelea na huduma mbalimbali za kusaidia dawa na elimu
kwa shule ambazo bado ziko chini ya madhehebu ya dini kwa kuwa hawawezi
kuwaadhibu wananchi na watoto.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kwa kuwa shughuli zote za Bugando zilikuwa zinaelekea
kusimama, na kulikuwa na mgomo kila siku kwa madaktari, manesi na watumishi,
serikali ikaomba wajadiliane upya juu ya mambo makubwa mawili.
Mambo hayo ni utoaji huduma katika sekta za huduma za jamii, na kuwa na
chombo cha mawasiliano na majadiliano kati ya Ikulu na madhehebu ya dini.
Lakini kwa kuwa madhehebu ni mengi, wakaomba chombo hicho kiundwe na viongozi
wakuu wa madhehebu yaliyokuwa yanajulikana kwa mujibu wa sheria.
Hivyo, Waislamu wakawakilishwa na Bakwata, TEC na CCT (kwa madhehebu zaidi ya
60 yaliyoko chini ya Christian Council of Tanzania), na baada ya mashauriano
waliunda chombo hicho.
Alifafanua kuwa kutokana na hali mbaya ya shule, serikali iliomba madhehebu
ya dini kusaidia ukarabati kwa zile zilizoonekana zitafungwa kutokana na hali
mbaya.
“Nasi kwa upande wetu, kwa nia njema ya kuisaidia serikali, lakini pia
kuwahudumia Watanzania, tuliwasiliana na wahisani ambao walikazia msimamo wao
kuwa hawako tayari kuingia kwenye shughuli za ujenzi wala ukarabati kwa kukosa
msimamo wa wazi na wa kisheria wa Serikali ya Tanzania kuhusiana na utaifishaji
wa huduma hizo,” alisema.
Katibu huyo aliongeza kuwa, serikali ilipojulishwa ilichukua hatua ya
kuanzisha mchakato mzima wa kupata suluhu ya jambo hilo. Ndipo akapewa jukumu
hilo, Anne Makinda, wakati huo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Hatimaye, serikali ilikubali kuwa haitataifisha tena na kwa kuthibitisha
hivyo, ikawa tayari kuwekeana mkataba na madhehebu ya dini. Ndipo tukaanzisha
mchakato wa majadiliano na wahisani, nao katika umoja wao kati ya dhehebu la
kikatoliki Ujerumani na Kilutheri pia la Ujerumani, tukaanzisha mchakato wa
namna bora ya kutoa huduma za jamii,” alisema.
Hatimaye, makubaliano yalifikiwa na ndipo kikazaliwa chombo kipya, Tume ya
Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), chenye sekretarieti yake, hivyo huduma ya
Christian Medical Board ya TEC na CCT, ikavunjwa na kuwekwa chini ya CSSC.
Dk. Slaa aliongeza kuwa, kwa upande wa serikali aliweka saini Edward Lowassa,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu wakati huo. Kwamba TEC na CCT nazo
zikawekeana na wahisani mikataba yao ya ndani ili kupata misaada ya ujenzi,
ukarabati na uendelezaji wa huduma zote za jamii.
Chanzo: Tanzania Daima au Tembelea www.freemedia.co.tz
No comments:
Post a Comment