MBUNGE wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), amekalia kuti
kavu kutokana na kutajwa kuwa anafadhili baadhi ya viongozi wa Baraza la
Vijana Taifa la CHADEMA (BAVICHA) kuleta mgogoro ndani ya chama hicho.
Siri hiyo ilifichuliwa juzi na baadhi ya vijana hao walipokuwa
wakijitetea mbele ya kikao cha BAVICHA ili kuthibitisha tuhuma zilizokuwa
zikiwakabili za kutumika kuwachafua viongozi wakuu wa CHADEMA.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa mmoja
wa vijana hao, Fred Hatari, ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanachama
wa CHADEMA Vyuo Vikuu (Chaso), alitoa ushuhuda mbele ya Kamati Tendaji ya
BAVICHA kuwa Shibuda amewahi kumwita mara kadhaa na kumpa fedha ili atoe
matamko ya kuchafua viongozi wa chama.
Huku akionesha ujumbe kadhaa wa simu yake ya mkononi (sms) aliyodai
kutumiwa na Shibuda, mwenyekiti huyo aliiambia kamati kuwa amekutana zaidi
ya mara mbili na mbunge huyo na kupewa fedha ili akatoe matamko sehemu
tofauti ya kumpinga Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, na kusema kuwa ana
kadi ya CCM.
“Fred aliamua kusema ukweli mbele ya kamati yetu, akaomba asamehewe
kwa maelezo kuwa alifukuzwa Chuo Kikuu kwa kutetea haki, na kwamba alikuwa
akiishi kwa kutangatanga, ndiyo maana alikubali kupokea fedha ya Shibuda,
lakini alikataa kumkashifu Katibu Mkuu,” kilisema chanzo chetu.
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche, alipoulizwa jana kuhusu
sakata hili, alikataa kusema chochote kuhusiana na kikao chao, akisisitiza
kuwa anapanga mkutano na waandishi wa habari ambao atautumia kuweka wazi
ukweli na ushahidi wote alionao.
BAVICHA iliunda kamati ndogo ya kuchunguza mgongano uliokuwepo baina
ya viongozi wake na hivyo kumteua Mwenyekiti wa baraza hilo Mkoa wa
Singida, Josephat Isango, kuwa mwenyekiti.
Baada ya kamati hiyo kuwasilisha ripoti yake juzi, baraza hilo
lilifanya uamuzi mgumu wa kuwafukuza baadhi ya viongozi wake akiwemo Makamu
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Juliana Shonza na kuwasimamisha baadhi ya
wanachama.
Katika kikao hicho ambacho kilijumuisha wenyeviti wa mikoa yote ya
kichama nchi nzima, Shonza hakuhudhuria badala yake alituma barua akidai
kuwa nje ya Dar es Salaam kwa shughuli za kifamilia.
Makamu mwenyekiti huyo amekuwa akidaiwa kusigana kimaamuzi na
viongozi wenzake, na hivyo kutoa matamko ambayo wakati mwingine yalikuwa
yakikinzana na msimamo wa chama.
Chanzo chetu kilifafanua kuwa, baada ya ripoti ya kamati ya
uchunguzi kusomwa, sekretariati ya BAVICHA ilitoa mapendekezo yake kuunga
mkono mapendekezo ya kamati na kisha wakaletwa mashahidi wengine waliokuwa
nje ya kikao ili kuthibitisha kama yaliyosemwa ni ya kweli au la.
Katika ushahidi uliotolewa, Shonza alibainika kuwa huwa anatumiwa na
Shibuda kutafuta vijana wengine wapokee fedha ili watoe matamko ya
kukifedhehesha chama.
Baada ya tuhuma hizo kuthibitishwa na kujadiliwa na wajumbe, kura
zote ziliazimia kuwa aondolewe uongozi na kusimamishwa uanachama wa
BAVICHA.
Wengine waliotuhumiwa kushirikiana na Shonza ni waliokuwa wagombea
ubunge mwaka 2010 katika majimbo ya Kibaha Mjini (Habib Mchange) na Mbozi
Mashariki (Mtera Mwampamba) ambao pia wamefukuzwa uanachama wa BAVICHA.
Kikao hicho pia kilichukua uamuzi mgumu wa kuwasimamisha uanachama
kwa muda wa mwaka mmoja, Gwakisa Mwakisando (Mbeya), Wilson Makala (Babati)
na Joseph Kasambala (Mbeya).
Alipotafutwa na gazeti hili jana jioni kwa simu, Shibuda alikanusha
kuhusika na tuhuma hizo akisema kuwa hata kijana huyo (Fred) hamfahamu.
“Hivi wewe nikikwambia Shibuda ni baba yako utakubali? Mnapaswa
kujiridhisha na uzushi huo, mimi sijui mambo ya BAVICHA maana si mjumbe
huko na sikuwahi kutumia fedha kumchafua Dk. Slaa kwani sina ugomvi naye,”
alisema.
Aliongeza kuwa hapendi siasa za udaku na chuki, na akaahidi
kulifuatilia suala hilo, huku akidai kuwa kuna watu wanataka kumchafua bila
sababu.
|
No comments:
Post a Comment