Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Monday, June 2, 2014

MWALIMU WA SHULE YA SEKONDARI CHIKUYU ATUHUMIWA KUMBAKA MWANAFUNZI WAKE WA KIDATO CHA TATU

ATOKOMEA HAJULIKANI ALIPO

Na: MOSHI LUSONZO- MANYONI
Katika hali ya kutisha, Mwalimu mmoja wa Shule ya sekondari anatuhumiwa kumkamata na kisha kumbaka hadharani mwanafunzi wake wa kike.

Tukio hilo  limetokea Mei 6, mwaka huu katika shule ya Sekondari ya kijiji cha Chikuyu, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, ambapo mwalimu anayehusishwa na tukio hilo ametajwa kwa jina la Chrisant Mpinda.

Taarifa zilizopatikana zinasema mwalimu huyo alimchukua mwanafunzi huyo (Jina linahifadhiwa) anayesoma kidato cha tatu wakati akisubiri kuchukua chakula kisha kumpeleka uwanja wa michezo na kumfanyia unyama huo.

Kutokana na tukio hilo, wazazi wenye watoto wao katika shule hiyo wamekuja juu huku wakihusisha uongozi wa shule hiyo kusaidia kumtorosha mwalimu huyo ili asikamatwe kufikishwa katika vymbo vya sheria.

UBAKAJI
Bibi wa mwanafunzi huyo, Lucy Lumalizo, alisema mjukuu wake baada ya kufanyiwa kitendo hicho ameachiwa majeraha na maumivu makali.

Alisema siku ya tukio, mjukuu wake huyo akiwa na wanafunzi wenzake walikuwa kwenye foleni ya chakula.

Wakati akiendelea kusubiri zamu yake ifike ya kupata chakula, mwalimu huyo alimuita na kumtaka aende ofisini kwake kuna jambo alitaka kumuelekeza.

"Mjukuu wangu alimpatia sahani rafiki yake ili amtunzie na yeye alikwenda moja kwa moja kwenye ofisi ya mwalimu huyo," alisema mama Lumalizo.

Alisema alipofika ofisini kwake, mwalimu huyo alimtaka waongozane ili akampatie simu yake ya mkononi ambayo alinyang'anywa siku tano kabla tukio hilo.

Alimuelekeza waende wote uwanja wa michezo kwa ajili ya kumpatia simu hiyo, lakini walipofika eneo hilo mwalimu huyo alimkamata kwa nguvu na kuanza kumbaka.

Hata hivyo, mwanafunzi huyo alianza kupiga kelele za kuomba msaada kitu ambacho kilipelekea wanafunzi wenzake kukimbilia eneo la tukio na kufanikiwa kushuhudia mwalimu huyo akifanya unyama huo.

Baada ya kuona wanafunzi wamemuona, alimuacha na kukimbilia kusikojulikana.

ALALA BILA MATIBABU
Baada ya tukio hilo, imedaiwa mwanafunzi huyo alilazimika kulala ndani ya bweni bila kupatiwa matibabu kutokana na walimu wa shule hiyo kukataa kutoa ushirikiano.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo (Jina linahifadhiwa) ameliambia NIPASHE kwamba pamoja na kutoa taarifa kwa Mkuu wa shule hiyo Emmanuel Mwarabu, hakuna msaada uliotolewa kwa mwanafunzi huyo kupelekwa hospitali.

"Tulitoa taarifa mapema tukiamini mwenzetu atasaidiwa, lakini hakuna chochote kilichofanyika tulilala naye huku akilalamika maumivu makali hadi asubuhi," alisema mwanafunzi hiyo.

Alisema hata ilipofika asubuhi walimu hawakuchukulia uzito jambo hilo hadi wazazi wake walipokuja na kuamua kumpeleka kituo cha Polisi cha Manyoni.

"Mpaka sasa tunaishi kwa hofu baada ya uongozi wa shule kututaka tutoe maelezo kwa nini tulitoa taarifa kuhusu tukio lile, inaelekea kuna harakati za kuficha ukweli," aliongeza mwanafunzi huyo.

Hata hivyo, mama Lumalizo alisema katika uchunguzi uliofanywa Hospitali ya Manyoni imeonyesha mwanafunzi huyo ameingiliwa kwa nguvu na kumsababishia michubuko sehemu yake ya siri.

Alisema pamoja na ukweli huo, bado kuna hali inayoonyesha kuna vitu vinavyofichwa ili kujaribu kuhakikisha suala hilo linamalizika kimya kimya.

Alihuzunishwa na kitendo cha mwalimu huyo kukimbia  wakati kuna taarifa kuwa siku ya pili baada ya tukio hilo alionekana akiwa na walimu wenzake  wakifanya mkutano.

MKUU WA SHULE AGOMA
Mkuu wa shule hiyo, Mwarabu alipopigiwa simu yake ya mkononi kuelezea tukio hilo, hakuwa tayari kusema chochote kwa maelezo hawezi kuongea na mtu asiyemfahamu kwenye simu.

"Kama ukitaka jambo lolote kuhusu shule yangu, unatakiwa ufike hapa nitakuwa tayari kusema kila kitu na siyo vinginevyo," alisema.

Kwa upande wa Afisa Mtendaji wa kijiji cha Chikuyu, Emmanuel Mdemu, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alikiri kutokea kwa tukio na kusema Polisi wanaendelea kufanya uchunguzi.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo alikutana na pande mbili ikiwamo wazazi na uongozi wa shule na kubainika kuna ukweli wa jambo hilo.

"Kinachofanyika sasa ni kusubiri ripoti ya polisi ikamilike, lakini kitu hicho ni kweli kimefanyika na mwalimu anayehusishwa amekimbia kijiji na hatujui wapi atapatikana,' alisema Mtendaji huyo.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment