Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Wednesday, May 30, 2012


MBINU ZA KUZUNGUMZA NA KUSIKILIZA KWA UMAKINI

UWASILISHAJI WA HOJA KWA  NJIA MDOMO [UNENI]

Na. Furaha Venance
Mwaka 2012

Wanafunzi wengi wamekuwa na tatizo la uwasilishaji wa hoja kwa njia ya mdomo mbele ya wanafunzi wenzao, tatizo hili si kwa wanafunzi wa sekondari tu, bali hata wanafunzi wa vyou vikuu pia wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo hili. Lakini pia tunaweza kukubaliana kuwa tatizo hili linawagusa hata watu wa kada nyingine ambao kwa namna moja au nyingine wanajikuta wakitakiwa kutoa hoja au kuchangia hoja kwa kuzungumza.

Tatizo kubwa linalowafanya wanafunzi na watu wa kada nyingine kuwa na tatizo hili ni uoga, wanakuwa na hofu na hii inatokana na kutojiamini kuwa wanaweza. Hivyo basi katika sehemu hii, tutajadili mbinu ambazo tunatakiwa kuzitumia pindi tunapotakiwa kusilisha hoja mbele ya wanafunzi wenzetu, iwe darasani au katika sehemu yoyote ile.

        MBINU ZA UWASILISHAJI WA HOJA KWA  MDOMO [UNENI]
Zifuatazo ni mbinu ambazo zitakusaidia kuondoa uoga na hofu na hivyo kuwa na moyo wa kujiamini pindi unapotaka kuwasilisha hoja yako:

1 Fanya maandalizi
    > Kwanza unatkiwa kuandaa kile unachotakiwa kukiwasilisha au kama umepewa mada basi tafuta maelezo ya kutosha kwa kusoma vitu mbalimbali ambayvyo vitakusaidia kupata maelezo ya kina kuhusiana na kile utakachowasilisha. Andika katika mpangilio mzuri unaoeleweka.

> Pitia maelezo yako.
 Kama tayari umeshaanda kazi yako, jaribu kupitia mara kwa mara, soma upya, tened na tena hadi kiwango cha kujiridhisha kuwa sasa umeelewa vema kile utrakacho wasilisha. kama utagundua kuna dosari ama upungufu wowote ule, ongezea taarifa nyingine ambazo zinahusiana na kile utakachowasilisha ili kuiboresha zaidi kazi yako. Hii itakujengea hali ya kujiamini zaidi kwani utajijua kuwa unajua mambo mengi kuhusiana na mada unayotoa na unataarifa za kutosha.

> Andaa dondoo utakazozizungumzia,
Hapa ina maana kuwa, andaa dondoo ambazo unadhani ndiyo hoja muhimu katika uwasilishaji wako, hoja zako ziwe fupi fupi na rahisi kuzielewa. Pitia hizo dondoo, utazitumia  pindi unapowasilisha hoja zako ili kujikumbusha na kuwasilisha hoja zako kwa mpangilio. Kumbuka hutakiwa kusoma unapowasilisha.

2. Fanya mazoezi
  > Fanya mazoezi binafsi,
Hapa unatakiwa kufanya mazoezi ya kile utakachokiwasilisha, fanya mazoezi kila mara, unaweza kufanya mazoezi ukiwa umesimama mbele ya kioo huku ukijitazama mwenyewe, hata wakati ukiwa bafuni unaoga pia unaweza kufanya mazoezi kwa kuzungumza mwenyewe, pia hata wakati unaelekea darasani unaweza kufanya mazoezi ya kuongea mwenyewe kwa sauti ya chini.

Jaribu kuwasilisha mbele ya hadhira halisi.
Kumbuka mwanzo ulikuwa ukifanya mazoezi mwenyewe mwenyewe, sasa baada ya hapo unatakiwa kufanya majaribio mbele ya hadhila halisi, unaweza kuwaomba rafiki zako, au familia yako nyumbani wakusikilize ukiwasilisha hoja zako mbele yao, na baada ya kukusikiliza waombe watoe tathmini namna ulivyowasilisha sikiliza maoni yao pia kuhusiana na kile ulichowasilisha na namna ya uwasilishaji wako kama utaona inafaa unaweza kufanya marekebisho sehemu ambazo umeshauriwa kufanya hivyo.

3. Unapowasilisha hoja zako darasani.

Usiwe na pupa ya kuwasilisha {kuzungumza}
Kwanza unatakiwa kuvuta pumzi kidogo ili kuondoa hali ya wasiwasi, anza kuwasilisha hoja zako ukianza na swali au maelezo yanayogusa hisia za hadhira yako ili kuwaweka tayari kukusikiliza na kuwavuta wakusikilize kwa makini. Kumbuka kutabasamu unapowasilisha. {Kama unachowasilisha kinasikitisha basi na wewe pia unatakiwa kuonesha hisia za kusikitika.kama la kufurahisha na wewe onesha hisia za kufurahi pia}
> Ongea ana kwa ana na hadhila yako.
Iangalie hadhila yako kwa kuwatazama usoni kama unaongea na mtu ana kwa ana, simama wima, unaweza kutembea tembea lakini katika hali ya kujiamini na si kuashiria hali ya uoga. Tazama mwitikio wa hadhira yako kama ipo pamoja na wewe au umewaacha sehemu au mazungumzo yako yamewachosha, kama unaona umewachosha unaweza kubadili mtindo wa uwasilishaji wako au kuahamia hoja nyingine ili kuwavuta zaidi.

4. Zungumza yale yanayohitajika tu
Hii ina maana kuwa unapowasilisha hoja zako hakikisha unasema yale yanayohitajika tu si zaidi wala pungufu, na katika hatua hii unatakiwa kuzingania kanuni zifuatazo za uzungumzaji:

     1. Ubora/ ukweli
Unapowasilisha hoja zako hakikisha husemi jambo lolote ambalo unaamini kuwa ni uongo na wala usiseme kitu ambacho huna ushahidi nacho yaani huwezi kuthibitisha.

     2. Kuwa na kiasi katika kuzungumza
Hii ina maana kuwa, kwa kawaida mazungumzo yanapokuwa yanashirikisha watu zaidi ya wawili, kila mtu anatakiwa kupata nafasi ya kuchangia na wengine kusikiliza, hivyo unatakiwa kutoa taarifa kwa kiwango cha kujitosheleza, usitoe taarifa nyingi kuliko inavyohitajika, toa taarifa inayohitajika, taarifa nyingine unaweza kuzitoa utakapoulizwa maswali au hadhira kuomba ufafanuzi zaidi kuhusiana na jambo ulilowasilisha.

     3. Uhusiano
Kanuni hii inamtaka mzungumzaji usiseme mambo yaliyokando na mada au shughuli inayofanyika wakati huo, sema mambo yanayohusiana na mada tu.

   4. Njia/ namna ya kuzungumza
Epuka maneno au miundo isiyoeleweka, sema kwa mpangilio, epuka utata wa utakachozungumza kwa hadhira yako, sema kwa kifupi.

5. Uwe na utaratibu wa katika usemaji wako, yaani unatkiwa kuwa na mtindo wako wa uzungumzaji ambao unaweza kuwavutia wasikilizaji wako na hata kukutofautisha na wazungumzaji wengine.

Ø      Hakikisha sauti yako inasikika vizuri na maneno unayatamka vizuri pia.
Ø      Unatakiwa kutumia lugha inayoeleweka, lugha fasaha epuka kutumia lugha za mitaani katika uwasilishaji wako wa hoja.

4. Mwisho, Hitimisha vizuri hoja yako
Unapohitimisha unatakiwa kuelezea kwa ufupi wazo kuu katika hoja yako, fafanua kwa ufupi sehemu ambazo unadhani hukueleweka vizuri, tumia mifano ya ziada ili kuipa nguvu hoa uliwasilisha, baada ya hapo unatakiwa kushukuru hadhira kwa kukusikiliza, lakini pia unaweza kuwauliza wasikilizaji kama wana maswali au ufafanuzi wa ziada kwa kile walichosikia. na hapo utakuwa umewasilisha vizuri hoja yako bila hofu

 Mwandishi ni Mwalimu Shule ya Sekondari Mwanzi-Manyoni (Singida) anapatikana kwa namba zifuatazo:
Mawasiliano: 0715 33 55 58 (whatsapp)
                       0755 44 06 99
Nifollow instagram: fullraha17
Facebook: Furaha Venance                         









No comments:

Post a Comment