Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Thursday, March 5, 2015

MAGUFULI AMSIFIA MBOWE. ASEMA ALISTAHILI KUWA MALAIKA. UNAJUA KWANINI?

Hai. Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana aliungana na viongozi wenzake wa Serikali kuwamwagia sifa viongozi wa vyama vya upinzani baada ya kumwelezea Mbunge wa Hai na Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe kuwa ni mpigania maendeleo ya wananchi na kwamba alitakiwa awe malaika.
Dk Magufuli alimuelezea kiongozi huyo wa upinzani bungeni kuwa ni mtu ambaye anafuatilia maendeleo ya watu bila ya kujali itikadi zao.
Waziri huyo ameungana na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusifu utendaji wa viongozi wa upinzani.
Februari 10, Rais Kikwete alisifu utendaji wa meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael wa kuwaletea maendeleo wananchi, na siku 12 baadaye Waziri Pinda alimsifu mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kwa kuwa kiongozi wa kwanza kuchangia vitanda 30 kwenye Hospitali ya Frelimo.
Jana, Dk Magufuli alimmwagia Mbowe sifa hizo katika mkutano wa hadhara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Kwasadala-Masama-Machame katika Jimbo la Hai inayojengwa kwa kiwango cha lami.
“(Mbowe)Unadhihirisha kwamba maendeleo hayana chama na kwa kweli tukienda hivi Tanzania itakuwa ni nchi ya kutolewa mfano. Sincerely (kwa dhati) nakupongeza Mbowe na Mungu akubariki,” alisema.
Kabla ya Dk Magufuli kutoa pongezi hizo, Mbowe aliwataka wanasiasa kutekeleza ahadi zao kwa vitendo kwa kuwa maendeleo hayana itikadi.
“Mimi naamini maendeleo hayana itikadi. Jambo jema likifanywa na chama chochote cha siasa ama kiongozi wa chama chochote au Mtanzania, kama ni jema anastahili kupongezwa,” alisema Mbowe.
“Hakuna aibu ya kukiri pale jambo jema linapofanyika. Ujenzi wa Barabara ya Kwasadala-Mula-Machame ni jambo jema,” alisisitiza Mbowe.
Hata hivyo, alitumia mkutano huo wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Masama kumuomba Dk Magufuli atoe maagizo ya kiserikali baada ya viongozi wawili wa CCM kutishia kuchoma moto greda lake.
“Nimenunua greda ili tusaidiane na Serikali, lakini juzi diwani na mwenyekiti wa kijiji walitishia kuchoma moto greda eti kwa sababu mbunge hajapewa kibali cha kuchimba barabara,” alilalamika.
Mbowe alisema vyama vya siasa ni lazima vifanye pamoja kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo.Akihutubia mkutano huo, Dk Magufuli alisema Mbowe ni kiongozi mpole na mstaarabu na ndiyo maana kila ombi lake analoliwasilisha serikalini kwa ajili ya wananchi wake haligongi mwamba.
“Utapata wapi mtu mpole kama huyu? Alimuomba Rais pale kwamba niongezee kilometa tatu, (Rais) akatoa siku ile ile,” alisema.
“Rais Kikwete ni mwenyekiti wa CCM, lakini ameleta barabara hapa kwa mwenyekiti wa Chadema. Huo ndiyo utanzania na haya ndiyo tunatakiwa viongozi tuige mfano.”
Waziri Dk Magufuli alisema Mbowe ni miongoni mwa wabunge wachache wa upinzani ambao hawamsumbui bungeni na anapokuwa na jambo, huwa wanatoka nje na kuteta.
“Wako wengine wanapigaga kelele, lakini wewe unakuja tunazungumza. Unasema ndugu yangu, brother (kaka). Mbowe weweee! Ulitakiwa uwe malaika,” alisema Dk Magufuli katika mkutano huo.
Hata hivyo, Dk Magufuli aligeukia siasa na kusema ustaarabu na upole alio nao Mbowe unatokana na malezi mazuri ya CCM kwa vile wazazi wake walikuwa wana-CCM na kwamba pongezi anazitoa kwa dhati. Alimpongeza Mbowe kwa kununua greda, akisema fedha hizo angeweza kuzitumia kwa shughuli nyingine lakini akaamua kulinunua ili kusaidia wananchi wake.
Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment