Furaha Venance na Nganile Kyamba
(Mwaka: 2015)
Katika
makala haya tunakusudia kujadili namna muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva na
Bongo Fleva) kuonekana kuathiriwa na wanajadi kuliko wanausasa. Hivyo basi ili kukamilisha
hilo, kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni utangulizi
ambapo tutaangalia maana ya istilahi muhimu zinazojitokeza katika mada yetu,
tutaangalia historia ya muziki wa kizazi kipya lakini pia tutaangalia kwa ufupi
wanajadi na wanausasa ni vitu au mambo gani wanayoyasimia. Sehemu ya pili ni
kiini cha swali letu, katika sehemu hii tutaangalia vipengele vinavyoonesha
kuwa wasanii wa kizazi kipya kuathiriwa na wanajadi kuliko wanausasa na sehemu
ya mwisho itakuwa ni hitimisho.
Maana ya Hip Hop na Bongo Fleva.
Wapo
wanaouona muziki wa kizazi kipya yaani Hip Hop na Bongo Fleva kuwa ni kitu
kimoja lakini wapo wanaopinga na kutofautisha kuwa Hip Hop na bongo fleva ni
aina tofauti ya muziki (Omari 2009:5, Samwel 2012:12). Ama kuhusu neno Bongo
Fleva mpaka sasa bado kuna utata kuhusu nani hasa mwasisi wa neno hili,
inaelezwa kuwa, mwanamuziki wa regge, Jah Kimbute ndiye aliyeasisi neno hili
pale alipoamua kuchanganya muziki wa asili na regge na kuziita Bongo Fleva.
Mtayarishaji wa muziki P.Funk anaeleza kuwa mwasisi wa neno Bongo Fleva ni DJ
Bonnie Love ambaye aliliasisi neno hilo mwaka 1998, Omari (keshatajwa, 10-11).
Madai
haya kuhusu waasisi wa neno Bongo Fleva linaonekana kupingwa vikali na
Mtangazaji wa siku nyingi, Michael Mhagama ambaye anadai kuwa yeye ndiye
mwasisi wa neno hilo na aliliasisi katika kipindi chake cha DJ Show kilichokuwa
kinarushwa na Redio One miaka ya 1990 hususani mwaka 1996. katika makala yake,
Mhagama anasema, “Ilipofika dakika 30 za
muziki wa R & B,siku hiyo nilikuwa kwenye usukani na kwa mbwembwe nilicheza
nyimbo ya kundi la R&B lililoitwa 4Krewz Flava na baadaye kuiunganisha na
nyimbo nyingine ya Unique Sistaz.Kwa vile midundo,mpangilio,lugha na utaalamu
wa muziki wenyewe kamwe huwezi kuufananisha na ule wa Soul 4 Real au SWV kutoka
Marekani,tulipenda tutofautishe kidogo kati ya aina hizi mbili na ndipo session
hii niliibatiza jina ambalo lingetofautisha R&B ya Marekani na ile ya kwe
tu….niliipa session hii jina la BONGO FLAVA.” Wengine wanaotajwa kuwa ni
waasisi wa neno Bongo Fleva ni DJ. KBC, DJ. Phat Black, DJ. Venture na Steve B.
(Reaster-Jahn na Hacke, 2014:24).
Ingawa
lengo la kazi hii si kujikita katika mgogoro huo ila tumeona kwa umuhimu wake
tuugusie japo kwa ufupi. Kama tulivyosema hapo awali kuwa wapo watu wanaouona
muziki wa Hip Hop na Bongo Fleva kuwa ni muziki tofauti, Ramadhan Mponjika
akinukuliwa na Samwel na wenzake (2013:55) anasema, muziki wa Bongo Fleva ni
kapu ambamo ndani yake kuna miziki ya aina mbalimbali ikiwemo zouk, rhumba,regge,
RnB, n.k. Kinachoelezwa hapa ni kuwa, muziki wa Bongo Fleva ni aina yoyote ya
muziki wenye asili ya nje lakini unaimbwa kwa mahadhi ya Tanzania (Bongo)
lakini si Hip Hop. Dai hili linaungwa mkono na Michael Muhagama (keshatajwa)
kupitia andiko lake, anasema, “Hii ilikuwa mwaka 1996 na ndio ulikuwa mwanzo wa neno
BONGO FLAVA likiwa na maana muziki wenye mahadhi ya nje lakini wenye vionjo na
ladha ya Tanzania na si vinginevyo lengo kuu ni kuitofautisha na muziki ule wa Marekani.
Hip Hop ya Tanzania ilibaki na itabaki vile vile kama ilivyo, ila muziki
wowote ule wa nje, mbali ya Hip Hop na DANSI ya Tanzania niliuita na
kuufahamishakwa umma wa watanzania kama BONGO FLAVA ndani ya kipindi cha DJ
SHOW cha Radio One.” Hapa maana yake
ni kuwa, jina la Bongo Fleva lilitumika tu, kutambulisha muziki wenye asili ya
nje lakini wenye mahadhi ya Tanzania (Bongo) tofauti na muziki wa Hip Hop na
dansi ambayo yenyewe ilitambulishwa kwa jina la Hip Hop ya Tanzania/Bongo au
Bongo Hip Hop.
Ama kuhusu Hip Hop, Mahenge (2011:8) anasema, Hip Hop ni aina
ya ushairi, usimuliaji au usemaji unaopangwa kivina kwa kufuata mdundo wa ala
za muziki ambao ulisharekodiwa. Pamoja na kwamba fasili hii ya Mahenge inatupa
mwanga kuhusiana na maana ya Hip Hop ambayo kwa kiasi kikubwa tunakubaliana
nayo lakini dai la kusema usimuliaji au usemaji unapangwa kivina kwa kufuata
mdundo wa ala za muziki ambao ulisharekediwa si sahihi kwani sasa hivi wasanii
wengi wa Hip Hop wanaimba juu ya midundo ya muziki ambayo haijarekodiwa vyombo vya
muziki vinapigwa sambamba na wao wakiimba na wakati mwingine hurap kwa mtindo
unaojulikana kama mitindo huru yaani kutoa mashairi ya papo kwa papo kwa
kufuata midundo ya muziki inayopigwa au bila kuwepo kwa midundo ya miziki yaani
akapela.
Kwa maoni yetu, tunaona kuwa Hip Hop na Bongo Fleva ni muziki
tofauti, muziki wa Hip Hop ni utamaduni unaombatana na elementi za, michoro,
rap, Dj, mabreka, ni muziki ambao mashairi yake yanaganwa kwa kutumia mashairi
yenye vina na midundo mizito wakati bongo fleva ni mkusanyiko wa muziki wenye
asili kutoka nje ya Tanzania lakini yenye mahadhi na vionjo vya Tanzania ambayo
hujumuisha Zouk, Kwaito, RnB, Kwaito, n.k. Kwa ujumla muziki huu Hip Hop na
Bongo Fleva huitwa kwa jina la muziki wa kizazi kipya ikiwa na maana ya muziki
unaopendwa na vijana kizazi cha sasa (Omari 2009:5, Samwel 2012:12).
Historia ya muziki
wa kizazi kipya (Hip Hop na Bongo Fleva)
Muziki wa Hip Hop tunaarifiwa kuwa
uliasisiwa na Wamarekani wenye asili ya Kiafrika katika mji wa Bronx huko New
York katika miaka ya 1970 (Omari, keshatajwa:1). Nchini Tanzania unakadiliwa
kuwa uliingia miaka ya 1980 Omari (keshatajwa), Mwanjoka (2011), Mbilinyi
(keshatajwa), Reuster-Jahn (2014). Katika kipindi hiki vijana wengi hususani
wale waliotoka katika familia zenye uwezo walianza kuimba mashairi (muziki) ya
rap kwa kuiga nyimbo zilizokuwa zikiimbwa na wanamuziki wa Marekani wakati huo.
Chachage aliwahi kuandika kuwa, katika mazingira hayo ndipo baadhi ya vijana
waliokuwa wakijitambulisha kwa kusikiliza muziki wa Reggae
wa Bob Marley na kucheza ‘Break
Dance’ katika miaka ya 1980, ili
kujinusuru na kuyasahau matatizo yao, walipoanza kujipambanua na muziki wa Hip Hop (Bongo Fleva). Mwanzoni ulikuwa ni
muziki ulioambatana na kuiga kisisisi muziki huo. Kuiga kisisisi maana yake
kuiga kitu kama kilivyo.
Madai haya ya kuiga muzuki wa Marekani
yanaungwa mkono na Mwanjoka (keshatajwa, 8) anaposema, “Mbali na kuiga nyimbo, vijana hao wa Tanzania waliingiwa na mapenzi ya
ndani zaidi na muziki huo hata kujikuta
wakiiga mavazi, mitindo ya nywele, mienendo hadi kuongea toka kwa wanamuziki
hao wa Marekani na Ulaya.”
Hivyo tunaona kuwa wasanii wa Hip Hop na
Bongo Fleva mwanzoni walianza kuimba kwa kunakiri na kukariri mashairi ya
wasanii hao wa nje na hata midundo waliyokuwa wanaitumia ilikuwa ni midundo
hiyo hiyo ya wasanii wa nje. Mbilinyi (keshatajwa, 32) anaongezea kwa kusema
kuwa, “Kama kulitokea na aliyerap kwa
kutumia lugha ya Kiswahili basi alitumia flow (kutiririka) ya nyimbo za mamtoni zilizokuwa maarufu
kama ambavyo alikuwa anafanya mkongwe Saleh Jabir katika nyimbo kama Ice Ice
Baby ya Vanilla Ice na OPP ya Naught by Nature ilikuwa ndiyo staili ya kipindi
hicho.” Ufafanuzi katika mabano ni wetu.
Lakini baadaye wasanii wakaachana na
uigaji wa muziki wa kimagharibi na kuanza kutunga nyimbo zao binafsi kwa lugha
ya Kiswahili na Kiingereza jambo linaloendelea mpaka sasa ingawa tungo za
Kiswahili ndiyo hupewa nafasi kubwa. Na msanii wa kwanza kabisa kuanza kuandika
na kuimba kwa Kiswahili alikuwa ni Salehe Jabir ambaye kwanza tunaelezwa kuwa
alianza kubadilisha nyimbo za Kiingereza kwa kutumia Kiswahili zilizotamba
kipindi hicho na baadaye akaanza kutunga nyimbo zake mwenyewe. Hapo ndipo
ikachochea wasanii wengi kuona kumbe inawezekana kurap kwa Kiswahili ndiyo nao
wakaanza kujitokeza kutunga na kuimba kwa lugha ya Kiswahili, Mbilinyi
(keshatajwa) na Mwanjoka (Keshatajwa).
Baadhi ya wasanii na makundi ya Hip Hop wanaotajwa
kuwa ni waasisi wa muziki huu walikuwa ni, Fresh XE, BBG, Adili Kumbuka, Salehe
Jabir, KBC, Samia X, The BIG, Rymson, 2 proud (Sugu), makundi ni kama vile,
Kwanza Unit, Deplowmatz, HardBlasterz, Gang Stars With Matatizo (GWM), Wagumu
Weusi Asilia, Young Da Mob, Afro Reign, Jungle Crewz Pose, Bantu Pound,
Hardcore unit kwa kutaja machache. Wasanii na makundi ya kuimba (Bongo Fleva)
ni kama vile, Mawingu Band, Lady Jay Dee, Stara Thomas, Unique Sisters,
Nurueli, 4Kruz kwa kutaja wachache Mhagama (keshatajwa), Mbilinyi (keshatajwa),
Mwanjoka (keshatajwa).
Aidha kabla hatujaingia katika kiini cha
mjadala wetu, tuwaangalie kwanza wanajadi na wanausasa ni mambo gani
wanayoyasimamia na kuyasisitiza katika utungaji wa mashairi. Ushairi wa kijadi
ni ushairi unaozingatia urari wa vina na mizani kuwa ndiyo roho na uti wa mgongo wa mashairi ya
Kiswahili kwao hawataki kukiri kuwa mashairi yalaiyotungwa katika mtiririko
(masivina) ni mashairi (Mulokozi na Kahigi, 1979:1) kwa maana hiyo kwa pamoja
na vipengele vingine katika ushairi wa jadi ni kuzingatia vina kama
anavyotuambia Abeid (1952:viii), “Neno
moja tukumbuke katika utungaji, nalo ni hili ya kuwa mawazo ya mtungaji yazue
vina, siyo vina kuzua mawazo.”
Madai haya yanaonekana kuungwa mkono na
wanajadi wengine kama vile, Chirahdin, Mayoka, Kandoro, Al-amin Mazrui na
Ibrahim Shariff kuwa vina na urari wa mizani ndiyo vitambulisho vya ushairi wa
Kiswahili (Mulokozi na Kahigi, 1979:11). Jambo la msingi hapa ni kuwa wanajadi
wanakumbatia sana suala la vina na mizani katika tungo za mashairi. Ili kuwa na
shairi zuri, mwanajadi Sheikh Amri Abeid anataja mambo manne muhimu yanayopaswa
kuzingatiwa katika ushairi ambayo ni, mizani, vina, kituo na kujitosheleza.
Wanajadi wengine wanaotaja mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa katika ushairi
ni pamoja na, Massamba (1983) anataja vina, mizani, kituo, muwala, Kibao (1983)
naye anataja, mizani, vina, urari, muwala, utoshelevu na kuwa na maana wakati
Komba (1977) anataja, mizani, vina, kituo na utoshelevu. Ama kwa hakika tukiwachunguza
wataalamu hao tutagundua kuwa, wanachosisitiza shairi lenye sifa za ujadi
linatakiwa kuzingatia vipengele vifuatavyo, Mizani, vina, kituo na
kujitosheleza.
Kwa
upande wao, wanausasa wanaona shairi si lazima lifuate urari wa vina na mizani,
Mathalani, Mulokozi na Kahigi (1982;25) wanasema ushairi ni sanaaa
inayopambanuliwa kwa mpangilio maalum wa maneno fasaha na yenye muwala kwa
lugha ya mkato, picha, sitiari au ishara katika usemi maandishi au mahadhi ya
nyimbo, ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisi fulani
kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo. Kwa maoni yao
wanausasa wanaona kuwa shairi ni sanaa yenye mpangilio mzuri wa maneno, lugha
ya mkato na matumizi mengine ya lugha ili kutoa mawazo wao hawasisitizi juu ya
kuzingatia urari wa vina na mizani kama wafanyavyo wanajadi.
Hivyo basi tukiwaangalia mambo yanayosisitizwa
na wanajadi na wanausasa, tunakubaliana na hoja kuwa, muziki wa Hip Hop na
Bongo Fleva unaonekana kuathiriwa zaidi na wanajadi kuliko wanausasa. Na
vipengele ambavyo wanajadi wanasisitiza kuzingatiwa katika ushairi ambavyo
vinaonekana kujitokeza katika mashairi ya Hip Hop na Bongo Fleva kama
tulivyoona hapo awali ni, Mizani, vina, kituo na kujitosheleza. Hebu tuangalie
vipengele hivyo namna vinavyojitokeza katika mashairi ya Hip Hop na Bongo Fleva
ambavyo ndivyo vinavyotufanya kushadidia hoja hii kuwa muziki wa kizazi kipya
unaonekana kuathiriwa na wanajadi kuliko wanausasa tukianza na;
Vina, tunaelezwa na Amri Abeid (1952:4)
kuwa ni silabi za namna moja zinazotokea baada ya kila mizani kadha katika
mstari wa shairi. Kwa upande wake, Wamitila (2003:345) anasema vina ni, dhana
inayotumiwa katika taaluma ya ushairi kuelezea silabi zinazofanana katika
sehemu sawa katika mpangilio wa ubeti wa shairi. Anaendelea kufafanua kuwa
shairi linaweza kugawika katika vipande viwili na kuwa na vina vya kipande
kimoja na kipande kingine. Hiki ndiyo kipengele kinachoonesha kuwa wasanii
wengi wa muziki wa kizazi kipya (Hip Hop na Bongo Fleva) kwa kiasi kikubwa
kuonekana kuathiriwa na ujadi.
Kati ya vitu ambavyo wanajadi
wanasisitiza katika mashairi ni urari wa vina na mizani, kwa mfano Mnyampala
(1962: Dibaji) anasema, Ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale.
Ndicho kitu kilicho bora sana katika maongozi ya dunia kwa kutumia maneno ya
mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina
maalumu kwa shairi. Hapa Mnyampala pamoja na kuongelea suala la shairi kutumia
maneno ya mkato na lugha nzito lakini maneno hayo yanatakiwa kupangwa kwa urari
wa vina na mizani. Suala la urari wa vina pia linashadidiwa na Shabaan Robert (
1958) akinukuliwa na Massamba (1983:54) janaposema, Ushairi ni sanaa ya vina
inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi.Zaidi ya kuwa sanaa ya vina
ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari.
Kama tulivyoona kwa wanajadi, vina ni
kigezo kinachozingatiwa sana na wasanii wa Hip Hop/Bongo Fleva katika tungo
zao. Hiki ndicho kigezo ambacho kwa asilimia kubwa ndicho kinatufanya
kushadidia hoja hii kuwa mashairi ya Hip Hop na Bongo Fleva yanaonekana
kuathiriwa sana na wanajadi kuliko wanausasa. Katika muziki huu, wasanii
wasiozingatia matumizi ya vina katika tungo zao zinaonekana hazina maana kama
wanajadi wanavyoona kuwa mashairi yasiyozingatia vina kuwa si chochote, kama
anavyosema Afande Sele katika wimbo wake wa Mtazamo;
Au wengine mmetumwa kama mamluki,
maana yake hamna maana mnarap mradi rap,
mistari imekosa vina yenye vina haina maana.
Aidha
katika wimbo wake mwingine, Darubini Kali
Afande Sele, anawashangaa wasanii wenzake wanaoimba bila vina kama anavyosema,
Mi
nacheka sana kuna vitu vya kuimba vyenye maana kila kona,
(Sasa)
inakuwa vipi unataja taja majina tu nyimbo nzima
Tena
kwa mistari isiyo na vina!
Kwa mtazamo wa Afande Sele msanii
asipozingatia matumizi ya vina anaonekana kama mamluki na mtu asiye na maana kwenye
sanaa. Kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya hususani wa Hip hop, matumizi ya
vina yanasisitizwa zaidi na hata wengine kujinasibisha kuwa wao ni wataalamu wa
kutumia vina kama anavyojinasibisha Solo Thang katika wimbo wao Tumerudi Tena (Wateule) anaposema, Ona wakali wa vina, ona tumerudi tena...
msanii mwingine Juma Nature katika wimbo alioshirikishwa na Rich One
unaojulikana kwa jina la Hatuna Kitu anajigamba
kuwa yeye ni mkali wa vina anaposema, “...Juma
Nature, Sir Nature a.k.a msitu wa vina, yeah Watanzania mahili tuliokomaa kimashairi...”
Hii yote inaonesha kwa namna gani wasanii wa kizazi kipya (Hip Hop/Bongo
Fleva) wanaonekana kuathiriwa na wanajadi kutokana na kuzingatia matumizi ya
vina katika tungo zao na hata kujinasibisha kuwa ili uwe msanii mzuri lazima
ujue namna ya kuandika na kutunga mashairi yenye vina.
Ama
kwa hakika, wasanii wasanii wa Hip Hop na Bongo Fleva si kwamba wanajigamba tu
kuwa wao ni wataalamu wa kutumia vina, lakini pia vina hiyo vinajidhihirisha
katika tungo zao. Hebu tuangalie baadhi ya tungo kuona jinsi wasanii
wanavyozingatia matumizi ya vina katika tungo zao. Tukianza na msanii Profesa
Jay katika wimbo wake wa Kubwa Kuliko:
Ubeti
wa 1
Yo fani ni fani
muulize, Bishanga Bashaija,
Sanaa ya Bongo
kwa wasanii haina faida,
Ona wenzetu
Mantoni mambo safi kuku kwa mrija,
Na mimi nataka
niishi kama Kadija Kadija,
Wasanii wa Bongo
bado tunakufa maskini,
Nasubiri kiama
changu na sijui kitafika lini,
Wazee wa
serikalini semeni tatizo ni nini?
Mnataka mle
jasho langu nikienda futi sita ardhini,
Hapa jasho la mtu
haliliwi wala mtu haibiwi,
Jay najivinjali
kama kutumia kizizi,
Machozi
yananilenga nikimkumbuka mzee Nyanyusa,
Pamoja na
umuhimu wake wabongo walimsusa,
Baadhi ya mafao
yake wabongo wamefanya asusa,
Kwa mtu mwenye
akili lazima hii itakugusa,
Tunaposema
Watanzania tudumishe sanaa yetu,
Lazima mtuwekee
mazingira safi ya sanaa yetu,
Marijani Rajabu
tulimuita jabali la muziki,
Alifanya
maajabu,alivumilia mikimikiki,
Kinachonipa
ghadhabu, bwana sanaa ya Bongo hailipi,
Tofauti na chati
yake, ndugu yetu amekufa na dhiki,
Sasa kipi ni
kipi maana ufanisi haufanyiki,
Sababu viongozi
wetu mnatamaa hauridhiki,
Wakati ni huu wa
kujifunza watanzania,
Umoja wa wasanii
wa bongo hiyo ndiyo njia.
Kiitikio
Ninaposema Jay
kubwa kuliko,
Siko niliko
ndiko liko zindiko (Yataka moyo)
Ninaposema Jay
kubwa kuliko,
Siko niliko
ndiko liko zindiko (Yataka moyo)
Sanaa yataka
wito (yataka moyo)
Sanaa ya Bongo
nzito (yataka moyo)
Sanaa ujiko
mwiko (yataka moyo)
Sanaa yataka
wito (yataka moyo)
Ubeti
wa 2
Salamu Nicko zingilada popote roho ilipo,
Wasanii wenzako
wa Bongo bado tunafanya zindiko,
Wasalimie sana
kuzimu walio hai na waliolala,
Waambie
tunasuasua tu na akina Mzee Jangala,
Hardblasterz,
Sikinde na Remmy Ongala,
Underground
Soul na Gangwe na Baby Stara,
Uncle Kabaino,
IK pale Kimara,
OTTU Jazz na
Agley Face kule Ilala,
Tunasubiri kudra
za imani kwa Mungu kwa waja wake,
Tunaotafuta
labda tutapata faraja zake,
Mambo si mambo
yameongezeka tu matukio,
Na ajali, rushwa
na UKIMWI tu ndiyo kivutio,
Sanaa imedumaa
najua hiyo huwezi shangaa,
Lakini hali ya
sasa ni mbaya na inatukatisha tamaa,
Soko limekuwa
bovu wasanii hatuungwi mkono,
Wananchi hawana
kitu kila siku wanafanya mgomo,
Kiasi
wanachokipata kinaishia kwenye bia na ngono,
Na kuhusu masoko
ya nje serikali imefungwa mdomo,
Mapromota wengi
matapeli, ukilemaa wanakuacha feli,
Unaangua kilio,
ulichotegemea kinakuwa siyo,
Wepesi kutimua
mbio, wewe linakupitia fagio,
Na sasa
wametuacha na kuleta wasanii wan je,
Hatimiliki ndiyo
kwanza inasua sua ndani ya Bunge.
Kiitikio
Ninaposema Jay
kubwa kuliko,
Siko niliko
ndiko liko zindiko (Yataka moyo)
Ninaposema Jay
kubwa kuliko,
Siko niliko
ndiko liko zindiko (Yataka moyo)
Sanaa yataka
wito (yataka moyo)
Sanaa ya Bongo
nzito (yataka moyo)
Sanaa ujiko
mwiko (yataka moyo)
Sanaa yataka
wito (yataka moyo)
Wasanii wengi wa
bongo bado tunaishi kwenye ujima,
Kiasi
tunachotafuta wenye choyo wanatuzima,
Siyo lazima
tupate tanuzi la kuendesha benzi au bima,
Tunachanga
tuthaminiwe watanzania tupate heshima,
Nje ya mipaka,
tufanye kile tunachokitaka,
Sanaa iwe ajira
tuepushe wimbi la vibaka,
Heri yako Irene
Ngoi milioni hazikupigi chenga,
Nakutakia kila
la heri popote unapokwenda,
Si Mr. Teacher,
GK wala Mzee Jongo,
Anayelidhika na
maslahi ya msanii wa hapa bongo,
Yo Solo Thang,
Simple X hata Onyango,
Yo Mika Mwamba,
Mr Paul sina kinyongo,
Masoud
Kipanya, nathamini unachokifanya,
Oscar Makoye
dodosa kusanya kusanya,
Yo African
Stars, Vijana Jazz, Tatu Nane,
Sisi wote ni
wasanii kwahiyo tushirikiane,
Tusaidiane
kwenye pilika pilika za fani sa tuungane,
Siyo mizengwe
kibao, tuwe pamoja tusitosane,
Mr 2, KU, Fid Q,
TBT Crew,TQ,
Fanya mavitu
kwani wakati ndiyo huu,
Soggy Doggy, Mad
Brain, Eazy Braze, Hard crew,
Heyo, X Plastaz,
Juma Nature na Manzese Crew,
Tuff B, Sos B,
Killa B, Stieve B, Master T, Caz T,
Tukiangalia shairi hili la Profesa Jay,
tunaona kuwa katika ubeti wa kwanza vina vya, a, ni,i,sa,tu, kin a ia na katika
ubeti wa pili tunaona kuwa vina vya, o,la,ra,ke,a,mo,no na e wakati katika
ubeti wa tatu vina vya ma,ka,nga,ngo,nya,ne na u vinajitokeza.
Vilevile
tukimtumia msanii mwingine Diamond Platznum katika wimbo wake wa Kesho tunaona
pia matumizi ya vina yanazingatiwa, hebu tuangalie wimbo wenyewe;
Kiitikio
Minataka kesho twende nikupeleke
nyumbani
Nataka kesho twende ukamuone mama x2
Nataka kesho twende ukamuone mama x2
Ubeti wa 1.
Kwanza kabisa ntanyonga Tai
T"shirt na Jeans ntatupa kidogo..
Unite Nasibu usiniite Dai
Asije kukuona muhuni akapandisha Mbogo...
Naukifika uagize Chai
Savanna Takila uzipe kisogo...
Kuhusu mavazi kimini haifai
Tupia pendeza ila za Hekima Logo...
Even though wanaponda eti we ni kicheche
Waambie ndoo chaguo langu sasa wanicheke x2
Kwanza kabisa ntanyonga Tai
T"shirt na Jeans ntatupa kidogo..
Unite Nasibu usiniite Dai
Asije kukuona muhuni akapandisha Mbogo...
Naukifika uagize Chai
Savanna Takila uzipe kisogo...
Kuhusu mavazi kimini haifai
Tupia pendeza ila za Hekima Logo...
Even though wanaponda eti we ni kicheche
Waambie ndoo chaguo langu sasa wanicheke x2
Kiitikio
Minataka kesho twende nikupeleke
nyumbani
Nataka kesho twende ukamuone mama x2
Ubeti wa 2.
Usilete swaga za Nainai
Ukanyoa kiduku kama Moze Iyobo..
Eti shoping twende Tai
wakati Dadaangu anaduka kigogo..
Ukikuta Nguna usikatae
we zuga unapenda hata kama wa Muhogo..
Kuhusu kabila mbona Sadai
Mama angu hana noma hata kama Mgogo
Even though wanaponda eti we ni kicheche
Waambie ndoo chaguo langu sasa wanicheke x2
Nataka kesho twende ukamuone mama x2
Ubeti wa 2.
Usilete swaga za Nainai
Ukanyoa kiduku kama Moze Iyobo..
Eti shoping twende Tai
wakati Dadaangu anaduka kigogo..
Ukikuta Nguna usikatae
we zuga unapenda hata kama wa Muhogo..
Kuhusu kabila mbona Sadai
Mama angu hana noma hata kama Mgogo
Even though wanaponda eti we ni kicheche
Waambie ndoo chaguo langu sasa wanicheke x2
Vina vinavyojitokeza
katika ubeti wa kwanza wa wimbo huu ni, ai,go na e na katika ubeti wa pili vina
vinavyojitokeza ni ai,o,go na e.
Tukimtumia msanii mwingine Joh Makini
katika wimbo wake wa Najiona Mimi (I
see me) tunaona pia matumizi ya vina yanapewa kipaumbele kama tulivyoona kwa
wasanii wengine, hebu tuangalie shairi lenyewe:
Ubeti wa 1.
Namuona Baba Mmoja Tu Juu Najiona Mimi
Namuona Mama Mmoja Tu Chini Najiona Mimi
Naziona
chuki zao upendo najiona mimi
Mabegani Msalaba Wa Ndoto Mtoto Wa Mageto
Ziwe Kweli Zisiishe Kisongo Segerea Ya Keko
Juu Ya Ukweli Ndo Nifie Steven Biko
Najiona Mimi Yanapoanzia Mabadiliko
Fikra Potofu Badili Hizo
Ndoto Sio Kuzikalia Skani Mkilialia
Ndoto Ni Kuamka Mbio Kuzikimbilia
Mziki Una Hela Mwanzo Unapoingia
Hela Nyingi Zipo Mwishoni Hutozifikia For Real
Hapo Kati Kuna Kisu Siuna Jambia
Wale Papa Wabakaji Mpira Hawatotumia
Ulikuwa Mpaka Powder Utapakwa Rukaria
Na Usiambie Mtu Labda Yesu Na Maria
Baba Nikiwa Club Nakunywa Local Bia
Naomba Mziki Unaopigwa Uwe Ni Local Pia
Nyeusi Kwenye T-shirt Ndo Logo Gear
Makini Joh Na Bado Flow Ni..........Pia
Kiitikio
Ahh Internationally
I See Overtaking Wale
Najiona Mimi
Ahh I See My Sele I See Nobody Nobody Else
Najiona Mimi
Eeh Mungu Bwna Nifanyie Wepesi
I See Me International
I See Me Overtaking Wale
Najiona Mimi Eeh*2
Ubeti 2
Najiona Mimi Na Mitasi To Mary Mary
Utu Ndo Kitu Changu Ni Hery Hery
Maksi Za Show Zangu Ni A Very Very
Natia Neno Halleluya Kwenye Hali Bery
Wametuacha Mbali Na Zao Serikali Wakiunda Magari
Serikali Yangu Bando Inaunda Leseni
Ndo Maana Najiona Mimi Juu Tu Nikiunda Top Ten
Na Amka Na Hangover Ya Hela Siamki Na Deni
Na Amka Na Hangover Ya Hasira Siamki Na Demu
Nakiri Hizi Ndoto Ka Ndoto Si Grammy,BET,MTV NA Channel O
Nawakilisha Daraja Mbili Na Ngalelo
Najiona Mimi Juu Mamileo
Mawazo Juu Ya Pesa Zangu Under My Pilo
Lord Jesus My Hero Ohhh
Naona Injili Ina Shilling Siingilii Kanisani Siitilii Maanani
Sigara Saratani Siingilii Madukani
Nishida Au Umaskinii Ndo Maana Kitaa Inaua
Sugar Mamy Hajuwi Kushika Mooo
Anajuwa Kushika Mua Utashika Hela Ama Dua
Kiitikio
Ahh Internationally
I See Overtaking Wale
Najiona Mimi
Ahh I See My Sele I See Nobody Nobody Else
Najiona Mimi
Eeh Mungu Bwna Nifanyie Wepesi
I See Me International
I See Me Overtaking Wale
Najiona Mimi Eeh*2
Ubeti 3
I See Me International
I See Me Overtaking Walee
Ahh I See My Self I See Nobody Nobody Else
Napiga Goti Eeh Mungu Bwna Anifanyie Wepesi
Mwanzo Na Mwisho Si Niwe Alfa Na Omega Yes
Nalisha Neno Kwa Kila Rika Na Kila Ezi Ahhh
Mm Sio Jino Kwa Jino Nyoka Kwa Kisigino
Zima Ni Lako Neno Makini Joh uwa Simo
Ndoto Zangu Sio Zinoo
Molinge Sokoine All I Do Is Holla Up
All I Do Is Winning Najiona Kwenye Hella Mingi
Chap Chap Shule Mingi Kauli Yangu Mbiu Ni Kauli Kaa Kata Usikate Ringi
Mabegani Msalaba Wa Ndoto Mtoto Wa Mageto
Ziwe Kweli Zisiishe Kisongo Segerea Ya Keko
Juu Ya Ukweli Ndo Nifie Steven Biko
Najiona Mimi Yanapoanzia Mabadiliko
Fikra Potofu Badili Hizo
Ndoto Sio Kuzikalia Skani Mkilialia
Ndoto Ni Kuamka Mbio Kuzikimbilia
Mziki Una Hela Mwanzo Unapoingia
Hela Nyingi Zipo Mwishoni Hutozifikia For Real
Hapo Kati Kuna Kisu Siuna Jambia
Wale Papa Wabakaji Mpira Hawatotumia
Ulikuwa Mpaka Powder Utapakwa Rukaria
Na Usiambie Mtu Labda Yesu Na Maria
Baba Nikiwa Club Nakunywa Local Bia
Naomba Mziki Unaopigwa Uwe Ni Local Pia
Nyeusi Kwenye T-shirt Ndo Logo Gear
Makini Joh Na Bado Flow Ni..........Pia
Kiitikio
Ahh Internationally
I See Overtaking Wale
Najiona Mimi
Ahh I See My Sele I See Nobody Nobody Else
Najiona Mimi
Eeh Mungu Bwna Nifanyie Wepesi
I See Me International
I See Me Overtaking Wale
Najiona Mimi Eeh*2
Ubeti 2
Najiona Mimi Na Mitasi To Mary Mary
Utu Ndo Kitu Changu Ni Hery Hery
Maksi Za Show Zangu Ni A Very Very
Natia Neno Halleluya Kwenye Hali Bery
Wametuacha Mbali Na Zao Serikali Wakiunda Magari
Serikali Yangu Bando Inaunda Leseni
Ndo Maana Najiona Mimi Juu Tu Nikiunda Top Ten
Na Amka Na Hangover Ya Hela Siamki Na Deni
Na Amka Na Hangover Ya Hasira Siamki Na Demu
Nakiri Hizi Ndoto Ka Ndoto Si Grammy,BET,MTV NA Channel O
Nawakilisha Daraja Mbili Na Ngalelo
Najiona Mimi Juu Mamileo
Mawazo Juu Ya Pesa Zangu Under My Pilo
Lord Jesus My Hero Ohhh
Naona Injili Ina Shilling Siingilii Kanisani Siitilii Maanani
Sigara Saratani Siingilii Madukani
Nishida Au Umaskinii Ndo Maana Kitaa Inaua
Sugar Mamy Hajuwi Kushika Mooo
Anajuwa Kushika Mua Utashika Hela Ama Dua
Kiitikio
Ahh Internationally
I See Overtaking Wale
Najiona Mimi
Ahh I See My Sele I See Nobody Nobody Else
Najiona Mimi
Eeh Mungu Bwna Nifanyie Wepesi
I See Me International
I See Me Overtaking Wale
Najiona Mimi Eeh*2
Ubeti 3
I See Me International
I See Me Overtaking Walee
Ahh I See My Self I See Nobody Nobody Else
Napiga Goti Eeh Mungu Bwna Anifanyie Wepesi
Mwanzo Na Mwisho Si Niwe Alfa Na Omega Yes
Nalisha Neno Kwa Kila Rika Na Kila Ezi Ahhh
Mm Sio Jino Kwa Jino Nyoka Kwa Kisigino
Zima Ni Lako Neno Makini Joh uwa Simo
Ndoto Zangu Sio Zinoo
Molinge Sokoine All I Do Is Holla Up
All I Do Is Winning Najiona Kwenye Hella Mingi
Chap Chap Shule Mingi Kauli Yangu Mbiu Ni Kauli Kaa Kata Usikate Ringi
Tukiangalia
shairi hili utaona kuwa msanii pia amezingatia matumizi ya vina, mathalani
katika ubeti wa kwanza, vinajitokeza vina vya, mi, to,ko,zo,ia, katika ubeti wa pili vinajitokeza vina vya ri, ni,o na lo na ua, wakati katika
ubeti wa tatu vinajitokeza vina vya e,si,no,mo,na
ngi.
Aidha wasanii wengine, huandika mashairi
yenye vina vya kati na mwisho vinavyofanana kama wanavyofanya wanajadi, Abedi
(kashatajwa, uk. 5) anasema, baadhi ya watungaji (wanajadi) mwanaweka vina vya
kati vya namna moja katika beti zote. Athari hii, pia tunaweza kuiona katika
shairi lifuatalo kutoka kwa msanii Diamond katika wimbo wa My Nomber One;
Ubeti wa 1
Kwanza mapenzi safari, ujana
ni maji ya moto
Walinenaga zamani...
Pili tumetoka mbali, matatizo
changamoto
tu visa visa fulani...
tatu kidonda chako, kwangu maradhi
Mama tu usononekapo kwangu simanzi..x2
Kwa mahaba uliyonipa nimenogewa
ni vurugu patashika punguza
kidogo..
Na mengine kadharika toto si
unanielewa?
Hapo hapo uliposhika...ukiongeza
kidogo
mi mwenzako ntaumia
Tukiangalia ubeti huu, tutaona kuwa,
katika kila kipande cha mstari cha kwanza ameweka vina vya kati vinavyolingana
rejea silabi zilizokolezwa wino.
Aidha,
Katika shairi hili, ubeti wa
kwanza tunaona vina vya mi,to,ko na ia vimetumika wakati katika ubeti wa pili
vina vya ri, ni mu, o,ni na ua hujitokeza na katika ubeti wa tatu vina vya no
na ngi hujitokeza pia. Hawa ni wasanii wachache tulioamua kuwatumia kuonesha
jinsi wanavyoonekana kutawaliwa na wanajadi hususani katika vipengele vya
matumizi ya vina ama kwa hakika wasanii wengi wa muziki wa Hip Hop na bongo
fleva wameathiliwa na utumiaji wa vina katika mashairi yao kama wanavyosisitiza
wanajadi. Na wakati mwingine wasanii wa Hip Hop na Bongo Fleva huamua kutumia
vifupisho ili mradi tu kuhakikisha kuwa vina vinapatikana katika tungo zao kama
tunavyoweza kuona katika wimbo wa Mathematic
wa Roma Mkatoliki hususani ubeti wa kwanza:
Nimeshatikisa nyavu mi ndo MVP,
Wanakimbia depo hapo nipo CCP,
Niliwapigisha kuruta kwata la JKT,
Nina kipaji mimi kushinda hata THT,
Nawapangisha foleni kama benki ya NMB,
Mi nemesoma PCM siyo PCB,
So hata tufungwe mimi ni Asernal siyo Man U,
Kibonde we ni member wa Loan Board au TCU,
Nchi imeuzwa vigogo wanatuita ATM,
Tuwakemee mafisadi wote wa CCM,
Kuvua gamba haiwasafishi mbele ya CUF,
CHADEMA mwone Makamba, JK kwa TFF,
Sihitaji dancer wala mapanga yale ya TMK,
Show zangu zangu longolongo zile za Y2K,
Na siyo bandia ka kontena lile la BOT,
Situkuzi kilicho feki kama TOT,
Mi ndio Roma ntasimama kaka KKT,
Ahsante Bongo, macho juu, Nyamongo, TBC,
Mistari yangu mitamu kama miwa ya TPC,
Na kwa hizo fomu MC utalazwa KCMC,
Kodi ya walalahoi pombe TRA,
Miili yao ndio biashara ndani ya BBA,
Fataki anatoa mikopo ndani ya TIA,
Licha ya mimba haina uhakika mpaka DNA.
Katika
ubeti huu tunamuona msanii akiamua kutumia vifupisho katika kila mstari na
vifupisho hivyo alivyoviteua kuvitumia vinakamilisha vina katika ubeti mzima.
Vilevile, mtindo wa wasanii kutunga na
kuimba mashairi yao papo kwa papo kwa mtindo ambao wao huuita mitindo huru huku
wakizangatia suala la mizani, ni ushaidi mwingine unaoonesha kuwa muziki huu
unaonekana kuathiriwa na wanajadi zaidi kuliko wanausasa. Samwel na wenzake
(washatajwa, uk. 63-64) wanaeleza kuwa, msanii wa Hip Hop au Bongo fleva
anapotunga papo kwa papo huongozwa na fomula na hasa ile ya urari wa vina na
mizani. Wanaendelea kusisitiza kuwa, fomula hii humfanya (msanii) kila mara
kuhakikisha anapachika maneno ambayo yana vina. Wakimtolea mfano msanii Roma,
wanatueleza kuwa katika tamasha la Epiq Nation jijini Mwanza alitoa ghani za
papo kwa papo ambazo zinaonekana kuzingatia urari wa vina, kama inavyoonekana
hapa chini katika ghani hizo ambap msanii ametumia vina vya ao na to ili hali
mashairi hayo ameyatoa kichwani papo kwa papo;
Mwanza,
msishindane na mwanamke pedeshee atamuhonga noah,
Wanaume
mjitahidi ipo siku mtatoboa,
Mimi ni Rais wa
ghetto,
Sina kabisa
mchecheto,
Na wala sipigi
punyeto,
Namiliki mademu
kwa kipato,
Mwanza sema oyee
kwa Epiq Nation.
Chanzo:
Samwel na wenzanke (washatajwa, uk.64)
Ama kwa hakika, tukiangalia tungo za
wasanii wa muziki wa Hip Hop na Bongo Fleva tutakubaliana kuwa mashairi yao kwa
upande wa kuzingatia vina katika tungo zao inaelekea kuonesha kuwa wasanii wa
muziki huu wanaonekana kuathiriwa sana na wanajadi.
Aidha kipengele
kingine ni mizani, Abedi (keshatajwa) anafasili kuwa,
mizani ni vipimo vinavyopima urefu wa kila mstari, kila silabi moja ni mizani
moja. Yeye anaona shairi zuri ni lile lenye mizani16, lakini anatambua pia kuna
mashairi yasiyotimiza mizani hii, hivyo anatoa maelekezo ya namna ya kuweka kina
cha kati katika mashairi yenye mizani pungufu ya 16. Kupitia maelekezo haya
tunaona hata wasanii wa Bongo Fleva na Hiphop wanazingatia idadi ya mizani na
katika utunzi wao japo hawafuati mizani 16. Mara nyingi wamekuwa wakitumia
mizani pungufu au zaidi ya 16. Mfano katika wimbo wa profesa J ametumia mizani
12. Katika wimbo wake wa kubwa kuliko hasa
katika kiitikio kama inavyojionesha katika ubeti ufuatao;
‘ninaposema jay kubwa kuliko,
Siko niliko ndiko liko zinduko,
Ninaposema jay kubwa kuliko
Tukichunguza mashairi ya Hip Hop na
Bongo Fleva tutaona kuwa hawazingatii ya nane nane kila kipande cha mstari ili
kupata mizani 16, mara nyingi mashairi yao mizani huweza kutofautiana kati ya
mstari mmoja na mstari mwingine katika ubeti mmoja lakini suala la urari wa
vina huzingatiwa kama inavyojionesha katika mfano tulioutoa hapo juu, ambapo
kila mstari unaishia na kina cha ko. Tukiangalia pia mfano ufuatao
kutoka kwa msanii Ali Kiba katika wimbo wake wa Mwana:
Ubeti wa kwanza
Mali ni nyingi
nyumbani, kipi kilichokukimbiza,
Ona babiyo
mamiyo, wote wanakulilia,
Mtoto peke yako
nyumbani, kipi kimekukimbiza,
Ona babiyo
mamiyo, wote wanakulilia,
Ndani ya Dar Es
Salaama, ulikuja bure,
Tena kimwana
kimwana, hujui kuchuna,
Na zile lawama,
za wallokuzoeza,
Ulikuja jana na
leo tofauti sana,
Tena bora yule
wa jana wa leo tofauti sana,
Dakikia mbili
mbele nyuma, kichwa kinauma,
Mbona unawatesa
sana,
Mbona unajitesa
sana,
Ndani ya Dar Es
Salaam mambo matamu hakukuhisha hamu,
We bado mtoto
kwa mama hujayajua mengi,
Mwenda tezi na
omo marejeo ngamani,
Amesema sana
mama, dunia tambara bovu,
Kuna asali na
shubiri, ujana giza na nuru,
We mwana wewe
mwana, mwana jeuri sana,
Ulichokifuata
hukupaa, umekosa ulivyoacha,
Kwa baba yako
mwana, na mama yako mwana,
Kwa vicheche
ulivyotaka, na vingi ulivyoacha,
Tukiangalia wimbo huu, tutaona kuwa
mizani haijazingatiwa sana, kwani kila mstari unaweza kuwa na mizani tofauti na
mstari mwingine ndani ya ubeti huo huo. Kwa mfano mstari wa kwanza una mizani
17 kipande cha kwanza cha mstari kina mizani 8 na kipande cha pili kina mizani
9, wakati mstari wa pili una mizani 16, kipande cha kwanza una mizani 8 na
kipande cha pili una mizani 8. Lakini pamoja na tofauti hiyo, ya mizani, urari
wa vina unazingatiwa kama inavyoonekana katika kila beti, vina vya za, a, na,
cha vimetawala.
Suala lingine ambalo linasisitizwa na wanajadi ni uwepo wa kituo
katika shairi. Abedi (kashatajwa uk.4) anatueleza kuwa, kituo ni mstari wa
mwisho wa kila ubeti. Anaendelea kufafanua kuwa, kutuo huweza kuwa ama kiini
cha habari au kimalizio. Maana hii ya kituo haipishani sana na maana
inayotolewa na Wamitila (2003:93) isipokuwa anaongezea kuwa, wahakiki wengi
hukiita kitua kuwa ni kibwagizo. Wasanii wa Hip Hop na Bongo Fleva hupenda
kutumia istilahi ya kiitikio. Kwa wanajadi kila baada ya ubeti kama ubeti
utakuwa na mistari mine basi mstari wanne ndiyo huwa kiitikio/kituo, na kwa
upande wa mashairi ya Hip Hop na Bongo Fleva huwa na kituo yaani kiitikio
isipokuwa wao hawana mstari maalumu ambao unapaswa kituo kiwepo isipokuwa
kituo/kiitikio huwekwa mara baada ya kukamilika kwa kila ubeti. Hebu rejea
mfano wa wimbo wa Profesa Jay wa Kubwa
Kuliko anatumia kiitikio kifuatacho kila baada ya kukamilika kwa ubeti.
Ninaposema
jay kubwa kuliko,
Siko
niliko ndiko liko zinduko,
Ninaposema
jay kubwa kuliko
Wakati
mwingine kiitikio si lazima kifuate kila baada ya ubeti kwisha, wapo wasanii
wengine ambao hutumia fomula ya kuanza na kiitikio kikifuatiwa na ubeti,
kiitikio ubeti kiitikio, rejea mfano wa Diamond Platznum wimbo wa Kesho, msanii ameanza na kiitikio ndiyo
ubeti unafuata (rejea mfano wetu wa wimbo huo tulioutoa hapo awali, pia rejea
shairi la Joh Makini Najiona Mimi naye kiitikio kinajitokeza kila baada ya
ubeti).
Abeid
(keshatajwa) anatueleza kuwa katika mashairi ya wanajadi, kituo/kiitikio
kinaweza kubadilika badilika, hali hii pia hujitokeza katika mashairi ya
wanamuziki wa Hip Hop na Bongo Fleva, mfano katika shairi la wimbo wa Profesa
Jay Ndiyo Mzee tunaona kiitikio cha
ubeti wa kwanza kinatofautiana na kiitikio cha ubeti wa pili. Kwa mfano ubeti
wa kwanza anatumia kiitikio kifuatacho;
Si mtafurahi Watanzania jamani? (ndiyo mzee)
Si ni kweli nakubalika jamani? (ndiyo mzee)
Basi mimi ni mkombozi wenu jamani (ndiyo mzee)...
Wakati
katika ubeti wa mwisho anatumia kiitikio kingine na kinaimbwa na mtu mwingine
(Juma Nature) anasema;
Je wananchi mmenisikia? (ndiyo mzee)
Kuwa huyu jamaa hatufai (ndiyo mzee)
Na inafaa kumchukia (ndiyo mzee)
Hatumtaki aondoke zake (ndiyo mzee)
Jambo
lingine linalosisitizwa na mwanajadi katika mashairi ya kimapokeo ni
kujitosheleza kwa kila ubeti. Abedi (kashatajwa,uk.4) anaona utoshelevu ni
kipengele cha msingi katika shairi, anasema kuwa, kila ubeti ujitosheleze
kadiri iwezekanavyo, yaani, uwe na maana kamili, na usingoje kutimizwa na ubeti
mwingine. Jambo hili pia linajitokeza katika mashairi ya wasanii wa Hip Hop na Bongo Fleva kila ubeti katika nyimbo zao
huwa na maana inayojitosheleza. Ukiangalia mifano ya nyimbo tulizozitumia hapo
juu ukichunguza kila ubeti utaona kuwa ubeti unajitosheleza na unatoa maana
kamili. Labda kwa mfano mzuri tutumie wimbo wa msanii Jay Mo unaoitwa Story tatu Tofauti, katika wimbo huu
kila ubeti umebeba kisa chake tofauti ambacho kimekamilika na unatoa maana,
hebu hapa tuangalia ubeti wa tatu.
Mariam alikuwa
mtoto aliyekuwa na uzuri wa peke yake,
Mi mwenyewe
mmojawapo kati ya waliotaka ajiweke,
Ili anione
mchumba wake,
Alisimama peke
yake, alilinga kwa uzuri wake,
Tajiri familia
yake, kama hanyi au hali,
Kwa jinsi
alivyojisikia, na vile home kuna mali,
Kiburi alijijengea,
hali iliyofanya wengi waliomjua kumchukia,
Tuliosoma naye
hiyo tabia tulishaizoea,
Wazazi walisoma
ndiyo maana maisha yao ya juu,
Yeye hilo
hakuliona cha maana alichoona ni usister duu,
Pesa zikamtia
udhaifu, za nyumbani akaona hazitoshi,
Shuleni akacheza
rafu, masomo akashindwa pasi,
Alipata zero
kitu ambacho wazazi hawakuamini,
Angekuwa mtoto
wa kiume wangeshamfukuza nyumbani,
Wakaona siyo
mbaya kama atarudia mtihani,
Kitu ambacho
mariam hakikumuingia akilini,
Wakamuuliza
anachotaka, akajibu computer,
Cheti akapata
kwenye stashahada akachemsha,
Baada ya kupewa
ujauzito, inasemekana na kizito,
Ambaye ana mke
na pia nyumbani ana watoto,
Cha moto
kikaanza nyumbani alipofukuzwa,
Kumbe yule
kizito ana ngoma anafanya kuusambaza,
Hakumsikiliza
Jose Mtambo alipoimba kizaazaa,
Yamemwaribikia
mambo na mtoto bado hajazaa.
Katika ubeti huu,
utaona kuwa umebeba kisa kizima kinachojitosheleza na ukisikiliza ubeti wa
kwanza na wa tatu utaona kuwa kila ubeti una kisa chake kinachojitosheleza na
kinachotoa maana iliyokamilika wala ahitaji ubeti mwingine ukamilishe wazo au
maana ya shairi. Katika ubeti huu wa tatu msanii anaelezea tabia za Mariam,
kutowasikiliza wazazi wake, kutozingatia elimu na kujikuta akipewa mimba na
kuambukizwa virusi vya ukimwi.
Hitimisho.
Wasanii wa muziki wa
kizazi kipya yaani Bongo Fleva na Hip Hop kama wamechota baadhi ya sifa katika
ushairi wa kimapokeo katika kutunga
mashairi. Kipengele kikubwa ambacho wana-Hip Hop na Bongo Fleva wanaonekana
kuathiriwa nacho ni kipengele cha matumizi ya vina katika tungo zao ambacho
hasa wanajadi ndiyo wanaona kuwa ni roho ya ushairi. Lakini pamoja na hayo, pia
usasa katika mashairi yao unajitokeza kwa kiasi fulani, kwa mfano yapo mashairi
ya wasanii wa muziki huu ambayo hayazingatii vina lakini yanaimbika. Pia
kutokuwa na idadi maalumu ya mistari katika beti za mashairi yao pia ni sifa za
usasa katika utungaji wa mashairi.. Kwa ujumla hatuweza kusema wazi kuwa
wanajadi ndiyo wamewaathiri wasanii wa Hip Hop na Bongo Fleva au la kwani ni
jambo linalohitaji utafiti wa kina na mjadala mpana, tukiangalia hata namna
muziki huu ulivyoingia nchini kwa kuiga nyimbo za wasanii wa Marekani na Ulaya
ambazo nazo zinaonekana kuzingatia matumizi ya vina, vituo, kujitosheleza n.k.
huenda wasanii hao ndiyo waliowaathiri zaidi. Lakini kwa mujibu wa mjadala wetu
tunasema uwepo wa nduni za kijadi katika mashairi ya Hip Hop na Bongo Fleva
hususani kipengele cha vina washairi hawa inaonekana na hapa tunasisitiza kuwa
inaonekana kama wameathiriwa na wana jadi kwa kuwa jambo kubwa linalosisitizwa
na wanajadi ni matumizi ya vina na mizani ambayo hata wana Hip Hop na Bongo
Fleva nao husisitiza matumizi hayo kama tulivyoona hapo awali.
MAREJELEO
Abeid K.A. (1952) Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri.
Ahmadiyya Printing Press.
Dar
es salaam.
Mahenge, E (2010/2011) “Chimbuko la Muziki wa Hip
Hop ni Uasi au Sanaa za Maonesho?”
Katika
Mulika Na. 29 & 30. TATAKI. Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Mbilinyi,
J (Sugu) (2011) Muziki na Maisha: From the Streets to Parliament.
Mhagama, M (2008) Chimbuko la Muziki wa Kizazi Kipya Tanzania na Maana
Halisi ya Neno
Bongo Fleva. Imepakuliwa kutoka http://richard-mwaikenda.
blogspot.com/2012/03/neno-au-jina-bongo-flavachanzo-chake.html.
tarehe 11/04/2015 saa 4:15.
Mnyampala,
M. (1965) Diwani ya Mnyampala.EAP.
Dar es salaam.
Mulokozi,
M.M na Kahigi, K.K. (1979) Kunga za
Ushairi na Diwani yetu. TPH. Dar es salaam.
Mwanjoka,
G. (2011) Harakati za Bongo Fleva na
Mapinduzi.
Omari, S (2009) Tanzania Hip Hop as Popural Literature. Tasnifu Phd. Chuo
Kikuu cha
Dar
es Salaam.
Reuster-Jahn na Hacke (2014) “The Bongo Fleva Industry in Tanzania and
Artists: Strategies
for Success.” Katika Bongo Media
Words: producing and
Consuming Popular Culture in Dar Es Salaam. (Wahariri)
Krings & Reuster-Jahn. Rudiger Keppe Verlag. Germany.
Samwel, M. (20012) Mabadiliko katika Majigambo: Uchunguzi wa Majigambo
ya Jadi na ya
Bongo Fleva. Tasnifu Phd. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Samwel, M. Selemani, A.J. na Kabiero A.J. (2013)Ushairi wa Kiswahili:
Nadharia, Maendeleo,
Mwongozo kwa Walimu wa Kiswahili na Diwani
ya Mea. Meveli Publishers.
Dar es salaam.
Wamitila, K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi Istilahi
na Nadharia. Focus Publications Ltd. Nairobi.
Hip Hop issue http://cdn.itvs.org/hip_hop-issue-brief-hip-hop.pdf
Mwandishi anapatikana kwa namba zifuatazo:
0715 33 55 558
Mwandishi anapatikana kwa namba zifuatazo:
0715 33 55 558
No comments:
Post a Comment