Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja
Sunday, December 31, 2017
Friday, December 22, 2017
Ajira Mpya Walimu Disemba 2017 majina haya hapa
AJIRA MPYA DECEMBER 2017 SEKONDARI BOFYA HAPA
NAPE KICHWA NGUMU. LICHA YA MKWARA WA MAGUFULI AENDELEA KUMKOSOA VYUMA KUKAZA
Tuesday, December 12, 2017
Saturday, September 16, 2017
Saturday, July 15, 2017
Saturday, July 8, 2017
Monday, July 3, 2017
NIKKI WA PILI AYAKOGA MATUSI. SABABU NI NINI INGIA HAPA
Msanii wa muziki wa Bongo Hip Hop alivuruga katika mitandao ya kijamii. wananchi wamjia juu kutokana na tweet yake aliyoitweet katika akaunti yake. Msanii huyo ambaye kwa siku za hivi karibu amekuwa mtu wa kutoa nukuu mbalimbali katika akaunti zake za tweeter na instagram kuhusiana na masuala mbalimbali ya kijamii. Zamu hii ilikuwa ni katika elimu. Ni kama ameamua kuwashukia walimu juu ya utendaji wake. Hali iliyowaamsha wananchi na kuanza kumshambulia msanii huyo. Kwa lugha ya mtaani tunaweza kusema msanii huyu ni kama 'ameyatimba'.
Balaa lote hili limejitokeza katika ukurasa wa facebook wa Eat African Radio baada ya kuchukua nukuu hiyo na kuiweka katika ukurasa wao. Sasa komenti za wananchi kwa msanii huyo ni balaa. Kwa kifupi tumekuwekea hapa komenti chache.
Sunday, June 25, 2017
MASUALA YA YA KIDINI KATIKA MASHAIRI YA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA
MASUALA
YA YA KIDINI KATIKA MASHAIRI YA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA (BONGO HIP HOP NA BONGO
FLEVA)
Furaha Venance
2017
1.0 Utangulizi
Viongozi
wa dini, waumini na wanaharakati wengine wa kidini wamekuwa wakiupinga vikali Muziki
wa Kizazi Kipya kwa kuhusisha na dhambi, uhuni wengine wanaenda mbali zaidi
kuita muziki huu ni muziki wa kishetani. Ni jambo la kawaida kabisa kukuta
katika sherehe za kijamii zinazohusisha watu wenye imani kali za kidini kupinga
kuchezwa kwa muziki huu katika shughuli hizo. Wazazi wamefikia hadi hatua ya
kuwazuia watoto wao kusikiliza, kushiriki au kucheza muziki wa aina hii. Pamoja
na upinzani huu ukichunguza mitindo ya uchezaji, uimbaji na hata midundo ya
nyimbo nyingi za dini huchota kutoka katika Muziki
wa Kizazi Kipya. Lakini pia ukihudhuria sherehe zao za kijamii kucheza nyimbo
za muziki wa Kwaito (Muziki wa Afrika Kusini) ambao kwa hakika hautofautiani
sana na Muziki wa Kizazi Kipya. Tofauti ni midundo lakini jumbe zake
hazitofautiani sana[1].
Mambo
yanayotumiwa kama silaha za kuushambulia muziki huu ni kutokana na kuhusishwa
kwake na kubeba dhamira za mapenzi tena zinazozungumzia mambo wazi wazi,
kuhamasisha ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, mavazi n.k (rej. Remes, 1999;
Chachage, 2002; Perullo, 2005; Suriano, 2006; Omari, 2009 na Mahenge, 2010). hata
hivyo vitabu vya dini vinatufundisha mambo mengi kuhusu kuamini kitu au jambo
tunaloelezwa, kulisikia au kulisoma lakini tunakatazwa kuamini mambo kijuujuu
bila ya kufikiria. Katika Biblia kitabu cha Mithali 14:15,18 tunaelezwa kwamba
watu wanaoamini kila wanalolisikia ambalo hawana uzoefu nalo ni wapumbavu.
Ieleweke kwamba sina maana wanaoupinga muziki huu ni wapumbavu, la hasha, bali
kwa hakika andiko hili linatufundisha jambo moja kwamba si jambo jema kuamini
jambo lolote tulisikialo bila kuchunguza ukweli wake.
Hivyo
kabla nami sijawa miongoni mwa watu wa kutekwa na hoja namtazamo huo kuhusu
muziki huu, nimejiuliza maswali kadha wa kadha. Miongoni mwa maswali hayo; hivi
ni kweli muziki huu haufai kiasi cha kupigwa vita hivyo? Hivi watu wa dini
hawawezi kujifunza masuala ya dini zao kupitia muziki huu? Makala haya
yamegundua kwamba licha ya uwepo wa baadhi ya nyimbo zisizo na maadili katika
jamii, hukumu inayotolewa juu ya muziki huu ni wa jumla mno, kwani makala yamebaini
zipo nyimbo nyingi za Muziki wa Kizazi Kipya ambazo zina maudhui ya kidini
ambayo kwayo jamii inaweza kujifunza, kujirekebisha na kuwa wafuasi wazuri wa
dini husika. Makala haya yatajadili namna masuala (dhamira) ya kidini
yanavyojitokeza katika mashairi ya Muziki wa Kizazi Kipya. Katika kufikia lengo
hili tutachambua mashairi mbalimbali ya Muziki wa Kizazi Kipya kuona jinsi
masuala hayo ya kidini yanavyojitokeza.
2.0 Masuala ya Kidini
katika Mashairi ya Muziki wa Kizazi Kipya
Dini
inafasiliwa kuwa ni imani inayohusiana na mambo ya kiroho baina ya binadamu na
Mwenyezi Mungu au njia ya kuhusiana na Mwenyezi Mungu (TUKI, 2004:46). Hivyo
dini hutumiwa na binadamu kama njia/daraja la kuwasiliana na kumfikia Mungu.
Dini inaonekana kuchukua nafasi kubwa katika maisha ya kila siku ya binadamu.
Dini ndiyo hupanga jamii iishije kwa ahadi za kuona pepo baada ya kifo. Kupitia
dini binadamu hufundishwa ni mambo gani yakifanywa yanaweza kuwa kikwazo kwake
kumfikia muumba wake na ni mambo gani yakifanywa yanaweza kuwa njia bora ya kumfikia
muumba wake siku ya mwisho kama dini nyingi zinavyoamini. Kutokana na hali hii
dini imekuwa ni muhimu sana katika maisha ya kila siku. Hivyo kutokana na dini
kutawala maisha yetu ya kila siku si ajabu kukuta Muziki wa Kizazi Kipya
ukisawiri masuala ya kidini katika tungo zake.
Masuala
kama uhuru wa kuabudu, kumwabudu Mungu pekee, kuwa na imani thabiti, uvumilivu
wa kidini, umuhimu wa kutoa sadaka au dhaka, umuhimu wa kufanya toba na kutenda
mambo mema ni baadhi ya masuala ya kidini ambayo tunafundishwa na kuhimizwa
kuyatenda katika Muziki wa Kizazi Kipya. Yafutayo ni masuala ya kidini na
ufafanuzi wake yanayojitokeza katika muziki huu:
2.1 Uhuru wa Kuabudu
Tanzania
ni nchi isiyofungamana na dini yoyote. Licha ya hivyo asilimia kubwa ya
watanzania ni waumini wa dini mbalimbali na kila mwananchi ana uhuru wa kuabudu
na kujiunga na dini yoyote aipendayo. Uhuru huo unaolindwa na katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 19 (1,2). Wasanii wa Muziki wa
Kizazi Kipya hawako nyuma katika kuhamasisha watu kuwa huru kuabudu dini yoyote
na kuwataka wafuasi wa dini moja kutokashifu dini nyingine. Hili linajitokeza
katika wimbo wa Eee Mola wa kundi la
Hard Blasters wanasema:
Mbele ya Mungu
binadamu si kitu na ni dhaifu,
Kila mtu aabudu
anachotaka usikashifu,
Atukuzwe baba, mwana,
roho matakatifu,
Mimi ni kiumbe dhaifu
Mola twapaswa kukusifu.
Hapa wasanii watuhimiza kwamba kila
mtu aabudu ambacho anaona kinafaa kuabudiwa, lakini katika kufanya hivyo hatutakiwa
kukashifu upande wa dini nyingine. Kinachosisitizwa hapa ni watu kuwa huru
kuabudu dini yoyote. Kwa kuusikiliza wimbo huu ambao unahamasisha uhuru wa watu
kuabudu na kutokashifu dini za watu wengine si dhani kama litakuwa jambo ovu na
dhambi kwa Mwenyezi Mungu ambaye anaona fahari watu wanapomwabudu yeye. Aidha
msanii Roma katika wimbo wake wa 2030
anaieleza jamii kuwa Mkristo anayedhihaki Msaafu (Quran) huenda halijui kanisa kwa
maana kwamba kama angekuwa ni muumini wa kweli na anaijua dini yake vizuri
hasingewezai kuukashifu Msaafu. Vilevile anaona kuwa Muislamu anayechoma kanisa
ni sawa na kuuza Biblia Dubai ambako asilimia kubwa ya wananchi wake ni wafuasi
wa dini ya Kiislam. Rejea msanii anaposema:
Anaedhihaki msahafu pengine
kanisa halijui,
So kulichoma kanisa ni kuuza
Bible Dubai.
Pamoja na kwamba msanii katika
mistari hii hajatueleza wazi ni kwa namna gani kulichoma kanisa ni sawa na
kuuza Biblia Dubai. Funzo kubwa tunalipata hapa ni kwamba watu wanaoamua
kukashifu dini za watu wengine au kuchoma majengo ya ibada ya waumini wa dini
zingine wanakuwa ni waumini ambao hawajui vizuri mafundisho ya dini zao. Kwa
maana dini zote hizi zinawafundisha waumini wake kupendana (rej. Mathayo, 22:40; Mathayo, 5:17-20; Luka. 6:27-29; Luka.
16:17; Quran, 5:82 na Qur'an 21:107).
2.2
Kumwabudu Mungu wa Kweli
Moja ya amri kumi za Mungu ni
kumtaka binadamu kutoabudu miungu wengine isipokuwa yeye tu (rej. Kutoka,
201-17; Mathayo 19:18-22; Quran, 2:163; Quran 17:22;
Quran, 20:14 na Quran 26:68-73).
Katika Biblia kuna kisa kimoja kinaelezwa kuhusu Yesu kupandishwa juu na
ibilisi na kuoneshwa milki zote za ulimwengu ambazo angepewa azimiliki kama tu
angekubali kumsujudia ibilisi, jambo ambalo alilikataa. Rejea Luka 4:5-8
maandiko yanaposema:
Yesu
akajibu akamwambia, Imeandikwa msujudie Bwana Mungu wako
umwamwudu
yeye oeke yake.
Hali kadhalika katika Muziki wa
Kizazi Kipya wasanii wanatueleza hili katika wimbo wa Msafiri ulioimbwa na kundi la Kwanza Unit wanaposema:
Naota
ndoto za peponi,
Naona
shetani aniuliza wewe ni nani?
Na
wataka nini, pesa nyumba na magari ya kifahari,
Njoo
nifuate mimi, nakuwa makini?
Kama ilivyoelezwa katika Luka 4:5-8
na haya wanayoeleza wasanii katika mistari hii ambayo ni kama wamedondoa katika
andiko hilo, tunaona kuwa kikubwa wanachotusisitiza wasanii ni kuwa pamoja na
ahadi ya vitu vingi vya kifahari na thamani katika ulimwengu huu binadamu
anatakiwa kuwa makini na vitu hivyo bila kuacha kumuabudu Mungu wa kweli.
Tunachosisitizwa hapa ni kumwabudu Mungu pekee na si miungu wengine. Kuna
dhambi gani kuusikiliza wimbo wa aina hii ambao unatuasa kumwamudu Mungu wa
kweli kama vitabu vya dini vinavyotuasa?
2.3
Kuzishika na Kuzifuata Amri Kumi za Mungu
Kati ya mambo yanayosisitizwa na
dini ya Kikristo na Kiislamu ni waumini wake kuzishika, kuzitii amri kumi za
Mungu. Amri hizo ni; (i) usiabudu miungu wengine, (ii) usilitaje bure jina la
Mungu wako, (iii) Shika kitakatifu siku ya Mungu, (iv) Waheshimu baba na mama
upate miaka mingi na heri duniani, (v) Usiue, (vi) usizini, (vii) usiibe,
(viii) Usiseme uongo, (ix) Usitamani mwanamke asiye mke wako na (x) Usitamani
mali ya mtu mwingine (taz. Kutoka, 20:1-17; Mathayo, 19:18-22 na Qur an 7:145; Quran, 17: 22-34). Amri hizi ndizo
zinazowafanya binadamu kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wao. Kutozifuata amri
hizi ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini na maagizo ya Mungu. Kutokana na
umuhimu wake katika maisha ya binadamu hapa duniani na baada ya kifo viongozi
wa dini, waimbaji wa nyimbo za dini wamekuwa wakizifundisha na kuzisisitiza ili
watu wapate kuzifuata. Vivyo hivyo hata wasanii wa muziki wa kizazi wamekuwa
mstari wa mbele kuwahamasisha wasikilizaji wa nyimbo zao kuzielewa na kuzishika amri
kumi za Mungu ili kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Msanii Dudu Baya
anasisitiza jamii yake kuziheshimu na kuzifuata amri kumi za Mungu katika wimbo
wake wa Mungu Wangu. Rejea katika
wimbo huo anaposema:
Nimeamua
kuwatupia kamba
ambayo
mtu anatakiwa kuishikiria tu
ndipo
aokoke (eeeh Bwana!)
kamba
yenyewe ni amri kumi
ukizishika
utaokoka milele,
amri
zenyewe ndizo hizi,
moja!
Mwabudu Mungu wako tu
usiabudu
miungu wengine (eeeh Bwana!)
pili!
Shika kitakatifu siku ya Mungu wako (eeeh Bwana!)
tatu!
Usilitaje bure jina la Mungu wako (eeeh Bwana!)
nne!
Waheshimu baba na mama
upate
miaka mingi na heri duniani (eeeh Bwana!)
tano!
Usiue (eeeh Bwana!)
Sita!
Usizini (eeeh Bwana!)
Saba!
Usiibe (eeeh Bwana!)
Nane!
Usiseme uongo (eeeh Bwana!)
Tisa!
Usitamani mwanamke asiye mke wako (eeeh Bwana!)
Kumi!
Usitamani mali ya mtu mwingine (eeeh Bwana!)
Msanii hapa anatukumbusha kuwa
tukizishika amri kumi za Mungu tutaokoka hivyo kuepuka moto wa jehanamu siku ya
mwisho. Anachosisitiza msanii hapa ni kilekile kinachosisitizwa na vitabu vya
dini na viongozi wetu wa dini. Kwa kufanya hivi msanii anakuwa ametenda dhambi
gani? Anayesikiliza wimbo wa aina hii anakuwa ametenda dhambi gani pia? kwa
maoni yangu naona wimbo wa aina hii unafaa kusikilizwa na kila mtu kwa sababu
unasisitiza mambo tunayosisitizwa kufanya katika dini zetu na ndivyo Mungu
anavyopenda tutende.
2.4
Umuhimu wa Imani katika Dini
Viongozi
wa dini kwa kutumia vitabu vya dini wamekuwa wakisisitiza waumini wao kuwa na
imani thabiti dhidi ya dini zao, Mungu wao na hata mafanikio wanayohitaji
kufikia wanatakiwa kuwa na imani kuwa watafanikiwa. Imani ni kipaji cha kimungu
chenye kumwezesha mtu kumsadiki Mungu na ufunuo wake (rej. Katekisimu,
1998:68). Muziki wa Kizazi Kipya pia kwa kutumia tungo zake husisitiza juu ya
binadamu kuwa na imani dhabiti ili waweze kuiona pepo siku ya mwisho. Kwa mfano
katika wimbo wa Darubini Kali
uliombwa na Afande Sele tunaelekezwa hili msanii anaposema:
Hapo ulipo kama
unapenda pepo kwanini uogope kifo
Unachekesha ni balaa,
Unafikiri mbinguni
utakwenda kwa motokaa!
Ama utapata zali kama
Yesu alivyopaa!
Acha kujidanganya kwa
Mungu si kwa Mzungu,
Unapokwenda kwa pipa,
Ikibidi kwa njia za panya,
Haiwezekani bila ya
imani, unaelipiza baya kwa jema,
We ni shetani haufai
msikitini haufai kanisani.
Msanii hapa anatuonesha kuwa
Mbinguni hakuendeki kwa njia ya mkato zaidi ya watu kuwa na imani na kutenda
matendo mema. Aidha msanii Roma pia anawataka waumini wa dini kuwa na imani
thabiti na dini zao na si kuangalia matendo ya viongozi wao ili kuwa wafuasi wa
dini husika. Viongozi ambao nao ni binadamu tu wanaoweza kukosea. Msanii
analisema hili katika wimbo wa Mathematics:
Imamu akizini nje ya ndoa usiukimbie
msikiti
Padri akilala na sista
aibadilishi ukatoliki
Anachotufunza msanii hapa ni kwamba
inapotokea Imam akazini nje ya ndoa hatupaswi kuukimbia msikiti hali kadhalika
Padri akilala (kuzini) na sista usibadili dhehebu lako la Ukatoliki. Kwa maana
kwamba matendo yote hayo yanayotendwa na viongozi wa dini si msimamo wa dini
bali ni matendo yao binafsi.
2.5 Uvumilivu wa Kidini
Tanzania
kuna waumini wa dini mbalimbali dini zenye waumini wengi ikiwa ni dini ya
Kikristo na Kiislam. Kumekuwa na matukio ya waumini hasa wa dini hizi kutokea
misuguano ya hapa na pale. Mfano ilitokea sintofahamu juu kuchinja, mtoto
kukojolea Quran, makisa kuchomwa moto, viongozi wa dini kushambuliwa na
kadhalika. Nchi zenye dini tofauti inapohitajika amani ni muhimu kuwa na
uvumilivu wa kidini kati ya dini moja na dini nyingine. Muziki wa Kizazi Kipya
unalieleza hili katika tungo zake. Mfano msanii Afande Sele katika wimbo wake Dini Tumeletwa anaeleza kuwa kabla ya
dini hizi kuingiza Afrika, Waafrika walikuwa na dini zao na walimwabudu mungu
na waliishi kama ndugu bila vurugu tofauti na sasa. Anashangaa kwa nini dini hasa
dini hizi (za Kikristo na Kiislam) zinatufanya tuchukiane, tukashifiane, tuuane
ikiwa tu zilikuja na wageni? Analisema hili katika wimbo huo anaposema:
Wenyewe kwa wenyewe
tunauana kikatili,
Tunaitana makafiri
wakati inajulikana sisi ni ndugu wa asili,
Waafrika tunafeli,
nako kusoma hatuwezi,
Hata picha hatuzioni,
Ndugu wa baba na mama
tunauana kisa dini,
Haingii akilini,
Tofauti za kiimani
zilizoletwa na wageni.
Kimsingi hapa msanii anatutaka
waumini wa dini tofauti kupendana, kuishi kama ndugu bila kujali tofauti zao za
dini. Msanii anaona dini zote hizi ni sawa, ni kama matawi tu ambazo zote
zinamwabudu Mungu mmoja kama anavyosema pia katika wimbo huo:
Dini kama matawi
lakini Mungu ndiye shina,
Sifa zake zinafanana
labda tofauti zake ni majina,
Wapo wanaomwita Bwana,
Jehova, Allah, Subhana,
Wengine wanamwita
Krishna, Jah, God, Juva, Maulana,
Yote ni majina Mungu
ni mmoja.
Hapa msanii anaweka wazi kuwa dini
zote zinafanana, zinamwabudu Mungu mmoja isipokuwa tofauti zipo kwenye majina
ya Mungu katika dini hizo. Hivyo sisi wote ni ndugu kwanini tugombanie fito
wakati tunajenga nyumba mmoja. Jamii inahitaji kuvumiliana kidini ili kudumisha
amani ya nchi. Watu waabudu wanachotaka kwa uhuru na amani. Ndiyo maana wasanii
wa kundi la Hard Blasters katika wimbo wao wa Eee Mola wanatuasa kila mtu aabudu anachotaka na tusikashifiane.
Aidha Roma naye katika wimbo wa 2030
anatueleza kuwa anayedhihaki msaafu pengine kanisa halijui. Kwa maana kama
angekuwa analijua akatumbua kuwa kumbe haina haja ya kufanyiana unyama sisi kwa
sisi ikiwa wote tunaabudu Mungu Mmoja kwa mawazo ya wasanii. Ikizingatiwa pia
dini zote hizi zinasisitiza kupendana (rej. Mathayo,
22:40; Mathayo, 5:17-20; Marko, 12:30-31; Luka, 6:27-29; Luka. 16:17; Quran,
5:82 na Qur'an
21:107).
2.6 Kutoa Dhaka/ sadaka
na kusali
Mambo
muhimu ambayo waumini wa dini zote husisitizwa katika mafundisho ya dini ni
kusali kwa bidii, kutoa dhaka, sadaka na michango mbalimbali kwa ajili ya
maendeleo ya dini husika (rej. Hesabu 18:26; 1Wakorintho 16:1-2 na Quran, 2:43).
Vitabu vya dini vinasisitiza hivyo na viongozi wa dini pia huwasisitiza waumini
wao kufanya hivyo. Hali kadhalika wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya pia huwasisitiza
wasikilizaji wao umuhimu wa kufanya hivyo katika tungo zao. Mathalni msanii
Roma katika wimbo wa 2030 anasema:
Muislamu gani unahonga Bongo
Movie mamilioni,
mama anakufa mwaisela kakosa dripu ya quinine,
ni heri ujenge Msikiti tuitukuze mitume,
anasa za bakulutu unatunza wacheza sebene.
Hapa msanii anamshangaa Muislamu
ambaye anahonga ‘Bongo Movie’ (wasichana waigizaji wa Bongo Movie) mamilioni ya
pesa na kuwatunza wanamuziki wa dansi (sebene). Msanii anawashauri waumini wa
aina hiyo badala ya kufanya mambo hayo ya anasa ni bora watumie fedha zao
kujenga misikiti jambo litakalowaongezea thawabu kwa Mwenyezi Mungu. Aidha
katika wimbo huo huo anasititiza waumini kutenda mema wakati wote na si katika
mfungo wa Ramadhani pekee lakini pia anawasisitiza kusali kwa kwenda msikitini.
Hili analisema katika wimbo huo anaposema:
Unamuheshimu
ramadhani,
unazini mbele ya
shaban,
Kama ilishushwa
Quran
Twendeni
misikitini.
Kwa
hakika kutoa sadaka, Dhaka na kusali na kutenda mema ni njia za kumcha Mungu.
Binadamu tunaaswa kumcha Mungu kwa kutenda mema na inapotokea tumeteleza kwa
kufanya maovu hatuna budi kutubu makosa yetu (rej.
1Yohana, 1:9 na Quran, 2:54). Katika wimbo wa Eee Mola wa kundi la Hard Blasters tunasisitizwa hili wanaposema:
Njia
ni moja tumfuate Yesu,
Eee!
Walimwengu tumche Mungu,
Na
kutubu makosa yetu.
Kama tunavyoweza kuona katika
mistari hii, wasanii wanasisitiza mambo matatu ambayo tunakiwa kama binadamu
kuyafanya. Kwanza tunasisitizwa kumfuata Yesu. Kwa imani ya dini ya Kikristo
inaelezwa kuwa yeye ndiye njia pekee ya Kweli na uzima ambayo itampeleka
binadamu peponi (rej. Yohana. 6:14). Pili tunasisitizwa kumcha Mungu na mwisho
wanatutaka tutubu makosa yetu. Pengine swali la kujiuliza kwa kusikiliza na
kushabikia muziki wa aina hii unaotuhamasisha kumfuata Yesu (kuokoka), kumcha
Mungu na kutubu makosa yetu kwa muumba kuna dhambi gani? Kuna ushetani gani?
2.7 Toba
TUKI
(2004:283) inaeleza toba ni majuto kwa matendo yaliyotendwa ambayo ni kinyume
cha dini. Dini zote zinasisitiza waumini wake kufanya toba. Katika imani ya
kanisa Katoliki toba ama kuungama ni mojawapo ya amri za kanisa ikiwa ni amri
ya tatu (rej. Katekisimu, 1998:66). Aidha kwa upande wa dini ya Kiislamu toba
pia ni jambo linalosisitizwa na dini hiyo (rej. Quran, 2:54 na Quran, 5:39).
Vivyo hivyo wasanii wa kizazi kipya pia hutusisitiza kufanya toba kabla
hatujakutwa na mauti ili kujihakikishia pepo. Katika wimbo wa Eee Mola uliombwa na kundi la Hard
Blasters wanalisema hili:
Jaribu
kufanya masahisho,
Kabla
Mungu hajakata pumzi ya mwisho,
Kuna
kila dalili za hicho kiyama.
Hapa wasanii wanatueleza kuwa
tufanye masahisho ya matendo yetu kabla ya kufa kwetu maana kuna kila dalili za
kiyama (siku ya mwisho ambaye watu watahukumiwa kwa matendo yao). Msanii King
Crayz GK katika wimbo wa Nitakufanye anajiuliza
atakufanye na ikitokea amekufa roho yake itaenda wapi? Ili roho yake iwe salama
siku baada ya kufa anatueleza kuwa anahitaji kufanya toba kwa mabaya
aliyofanya. Hili anaeleza katika wimbo huo anaposema:
Ningelihonga
lakini Mungu hapokei rushwa,
Ili
siku yangu ikifika GK niwe tayari,
Kuna
mambo mengi nimefanya,
Mabaya
nahitaji toba.
Hapa msanii anasisitiza kwamba kama
kungekuwa na njia za mkato kuiona pepo angeweza hata kumhonga Mungu ili siku
yake ikifika awe salama. Kutokana na ukweli kwamba Mungu hawezi kuhongeka
msanii anaona hakuna namna zaidi ya kuungama na kufanya toba kwa mabaya
tuliyoyatenda. Ndiyo maana wasanii wa kundi la Daz Nundaz kwa kuona hatari hiyo
wanatusihi tuanze kutenda mema kabla kifo hakijatukuta. Rejea katika wimbo wa Kamanda wanaposema:
Anza
kutenda mema,
Kabla
kifo hakijakukuta.
Aidha msanii Linex katika wimbo wa Wema kwa Ubaya anatupa moyo kuwa Mungu
ni mwepesi wa kusamehe makosa yetu pale tunapotubu. Rejea anaposema:
Mungu
ni wa ajabu,
hata
ukiwa mtenda mabaya,
Ukirudisha
moyo wako nyuma,
Anasamehe
na kusahau,
Mungu
ni wa ajabuuu!
Wa
ajabuu ooh! Aah!
Tunaona kwamba kama ambavyo
viongozi wetu wa dini na vitabu vya dini kutuagiza kutenda mema na kufanya toba.
3.0 Hitimisho
Tumeona
namna ambavyo mashairi ya Muziki wa Kizazi Kipya yanavyozungumzia masuala
mbalimbali ya kidini. Masuala ambayo kwa hakika yanaweza kumuongoa mtu na
kumfanya kuwa mtu wa kumtegemea Mungu, kusali/swali, kutoa Dhaka na michango
mbalimbali katika nyumba za ibada lakini pia mashairi haya yanaweza
kutufundisha jinsi waumini wa dini tofauti tofauti wanavyoweza kuvumiliana
licha yo tofauti zao za kidini. Kutokana na uchambuzi huu naweza kuhitimisha
kwa kusema kuwa wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya wapo ambao wanatufundisha
mambo mazuri ya dini kama wafanyavyo viongozi wa dini na wasanii mbalimbali wa
nyimbo za dini, tofauti ni kwamba wakati viongozi wa dini wanatumia mimbali za
misikitini na makanisani wasanii wa kizazi kipya hutumia jukwa la Muziki wa
Kizazi Kipya kufundisha na kuelekeza yale yale yanayosisitizwa na viongozi wa
dini. Hivyo pamoja na uwepo wa nyimbo ambazo zinafikirika kwamba zinaweza
kupotosha jamii, zipo nyimbo ambazo zinaweza kuwaleta na kuwasogeza watu katika
dini au kwa Mungu. Kwani wapo baadhi ya wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya ni
mawakala wazuri katika kuhakisha mafunzo haya yanatufikia ili tuweze kumwamudu
Mungu wetu pasi na tatizo lolote. Kwa kusikiliza wimbo wenye maudhui ya aina
haya licha ya kwamba ni Muziki wa Kizazi Kipya kwa maoni yangu sidhani kama tutakuwa
tumetenda dhambi au kumkosea Mungu.
Marejeo
Al-Farsy, A. S. (hm). Qurani Takatifu:
Iliyofasiliwa na Marehemu Sheikh Abdullah Salehe Al-Farsy. India.
Bible Society of Tanzania. (1997). Biblia Maandiko Matakatifu. Dodoma:
Bible Society of Tanzania.
Chachage, S. (2002). “Ndani ya Bongo:
Utandawazi na Migogoro ya Utamaduni.” Makala iliyowasilishwa katika Mkutano wa Kumi wa Hali ya Siasa Tanzania.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Dar
es Salaam.
JMT. (2005). Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Dar es
Salaam. Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali.
Katekisimu. (1998). Katekisimu: Katekisimu Ndogo ya Kanisa
Katoliki. Songea. Peramiho Printing Press.
Mahenge, E (2010/2011). “Chimbuko la
Muziki wa Hip Hop ni Uasi au Sanaa za Maonesho?” Mulika Na. 29 & 30. TATAKI. Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Uk.
2-15.
Mangesho, P. (2003). “Global Cultural
Trend. The case of Hip Hop Music in Dar es Salaam”, M.A. Tasinifu. University
of Dar es Salaam.
Omari,
S. (2009). “Tanzania Hip Hop Poetry Literature”, PhD. Tasinifu, Chuo Kikuu cha
Perullo,
A (2005). “Hooligans and Heroes: Youth Identity and Hip-Hop in Dar es Salaam,
Tanzania.” Katika Africa Today, No.
76.
Remes,
P. (1999). “Global Popular Musics and Changing Awereness of Urban Tanzanian
Youth.” Katika Yearbook for Traditional
Music, Vol. 31 (1999), uk. 1-26. International Council for Traditional
Music.
Samwel, M. (2010). “Masuala ya Kisiasa
katika Mashairi ya Mapenzi ya Muziki wa Bongo Fleva”, Mulika Na. 29 & 30. Uk. 16-28. TATAKI. Chuo Kikuu cha Dar es
salaam.
Suriano, M. (2006). “Hip Hop and
Bongo Flavour Music in Contemporary Tanzania: Youth’ Experiences, Agency,
Aspirations and Contradictions.” Imepakuliwa kutoka www.ascleiden.nl/pdf/youthconfsuriano1.pdf.
tarehe 15 Novemba, 2015
TUKI. (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.
Diskografia
Afande
Sele-- Darubini Kali
Afande
Sele-- Dini Tumeletewa
Daz
Nundaz -- Kamanda
Dudu
Baya -- Mungu Wangu
Hard
Blasters-- Eee Mola
King
Crayz GK -- Nitakufaje
Kwanza
Unit -- Msafiri
Linex
-- Wema kwa Ubaya
Roma--2030
[1] Kwaito ni sawa na Muziki
wa Kizazi Kipya kwa Tanzania, nchini Kenya hujulikana kwa jina la Genge. Hivyo
kuupinga muziki wa kizazi kipya na kuukubali muziki wa Kwaito ni jambo la
kustaajabisha. Ni muziki ule ule unaotofautishwa na majina na maeneo tu.
Mwandishi wa makala haya ni Mwalimu katika Shule ya Sekondari Mwanzi (Manyoni DC)
Anapatikana kwa namba 0715 33 55 58/ 0755 44 06 99
Subscribe to:
Posts (Atom)