Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Sunday, June 25, 2017

MASUALA YA YA KIDINI KATIKA MASHAIRI YA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA








MASUALA YA YA KIDINI KATIKA MASHAIRI YA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA (BONGO HIP HOP NA BONGO FLEVA)
Furaha Venance
2017
1.0 Utangulizi
Viongozi wa dini, waumini na wanaharakati wengine wa kidini wamekuwa wakiupinga vikali Muziki wa Kizazi Kipya kwa kuhusisha na dhambi, uhuni wengine wanaenda mbali zaidi kuita muziki huu ni muziki wa kishetani. Ni jambo la kawaida kabisa kukuta katika sherehe za kijamii zinazohusisha watu wenye imani kali za kidini kupinga kuchezwa kwa muziki huu katika shughuli hizo. Wazazi wamefikia hadi hatua ya kuwazuia watoto wao kusikiliza, kushiriki au kucheza muziki wa aina hii. Pamoja na upinzani huu ukichunguza mitindo ya uchezaji, uimbaji na hata midundo ya nyimbo nyingi za dini huchota kutoka katika     Muziki wa Kizazi Kipya. Lakini pia ukihudhuria sherehe zao za kijamii kucheza nyimbo za muziki wa Kwaito (Muziki wa Afrika Kusini) ambao kwa hakika hautofautiani sana na Muziki wa Kizazi Kipya. Tofauti ni midundo lakini jumbe zake hazitofautiani sana[1]

Mambo yanayotumiwa kama silaha za kuushambulia muziki huu ni kutokana na kuhusishwa kwake na kubeba dhamira za mapenzi tena zinazozungumzia mambo wazi wazi, kuhamasisha ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, mavazi n.k (rej. Remes, 1999; Chachage, 2002; Perullo, 2005; Suriano, 2006; Omari, 2009 na Mahenge, 2010). hata hivyo vitabu vya dini vinatufundisha mambo mengi kuhusu kuamini kitu au jambo tunaloelezwa, kulisikia au kulisoma lakini tunakatazwa kuamini mambo kijuujuu bila ya kufikiria. Katika Biblia kitabu cha Mithali 14:15,18 tunaelezwa kwamba watu wanaoamini kila wanalolisikia ambalo hawana uzoefu nalo ni wapumbavu. Ieleweke kwamba sina maana wanaoupinga muziki huu ni wapumbavu, la hasha, bali kwa hakika andiko hili linatufundisha jambo moja kwamba si jambo jema kuamini jambo lolote tulisikialo bila kuchunguza ukweli wake.

Hivyo kabla nami sijawa miongoni mwa watu wa kutekwa na hoja namtazamo huo kuhusu muziki huu, nimejiuliza maswali kadha wa kadha. Miongoni mwa maswali hayo; hivi ni kweli muziki huu haufai kiasi cha kupigwa vita hivyo? Hivi watu wa dini hawawezi kujifunza masuala ya dini zao kupitia muziki huu? Makala haya yamegundua kwamba licha ya uwepo wa baadhi ya nyimbo zisizo na maadili katika jamii, hukumu inayotolewa juu ya muziki huu ni wa jumla mno, kwani makala yamebaini zipo nyimbo nyingi za Muziki wa Kizazi Kipya ambazo zina maudhui ya kidini ambayo kwayo jamii inaweza kujifunza, kujirekebisha na kuwa wafuasi wazuri wa dini husika. Makala haya yatajadili namna masuala (dhamira) ya kidini yanavyojitokeza katika mashairi ya Muziki wa Kizazi Kipya. Katika kufikia lengo hili tutachambua mashairi mbalimbali ya Muziki wa Kizazi Kipya kuona jinsi masuala hayo ya kidini yanavyojitokeza.

2.0 Masuala ya Kidini katika Mashairi ya Muziki wa Kizazi Kipya
Dini inafasiliwa kuwa ni imani inayohusiana na mambo ya kiroho baina ya binadamu na Mwenyezi Mungu au njia ya kuhusiana na Mwenyezi Mungu (TUKI, 2004:46). Hivyo dini hutumiwa na binadamu kama njia/daraja la kuwasiliana na kumfikia Mungu. Dini inaonekana kuchukua nafasi kubwa katika maisha ya kila siku ya binadamu. Dini ndiyo hupanga jamii iishije kwa ahadi za kuona pepo baada ya kifo. Kupitia dini binadamu hufundishwa ni mambo gani yakifanywa yanaweza kuwa kikwazo kwake kumfikia muumba wake na ni mambo gani yakifanywa yanaweza kuwa njia bora ya kumfikia muumba wake siku ya mwisho kama dini nyingi zinavyoamini. Kutokana na hali hii dini imekuwa ni muhimu sana katika maisha ya kila siku. Hivyo kutokana na dini kutawala maisha yetu ya kila siku si ajabu kukuta Muziki wa Kizazi Kipya ukisawiri masuala ya kidini katika tungo zake.

Masuala kama uhuru wa kuabudu, kumwabudu Mungu pekee, kuwa na imani thabiti, uvumilivu wa kidini, umuhimu wa kutoa sadaka au dhaka, umuhimu wa kufanya toba na kutenda mambo mema ni baadhi ya masuala ya kidini ambayo tunafundishwa na kuhimizwa kuyatenda katika Muziki wa Kizazi Kipya. Yafutayo ni masuala ya kidini na ufafanuzi wake yanayojitokeza katika muziki huu:

2.1 Uhuru wa Kuabudu
Tanzania ni nchi isiyofungamana na dini yoyote. Licha ya hivyo asilimia kubwa ya watanzania ni waumini wa dini mbalimbali na kila mwananchi ana uhuru wa kuabudu na kujiunga na dini yoyote aipendayo. Uhuru huo unaolindwa na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 19 (1,2). Wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya hawako nyuma katika kuhamasisha watu kuwa huru kuabudu dini yoyote na kuwataka wafuasi wa dini moja kutokashifu dini nyingine. Hili linajitokeza katika wimbo wa Eee Mola wa kundi la Hard Blasters wanasema:

Mbele ya Mungu binadamu si kitu na ni dhaifu,
Kila mtu aabudu anachotaka usikashifu,
Atukuzwe baba, mwana, roho matakatifu,
Mimi ni kiumbe dhaifu Mola twapaswa kukusifu.

Hapa wasanii watuhimiza kwamba kila mtu aabudu ambacho anaona kinafaa kuabudiwa, lakini katika kufanya hivyo hatutakiwa kukashifu upande wa dini nyingine. Kinachosisitizwa hapa ni watu kuwa huru kuabudu dini yoyote. Kwa kuusikiliza wimbo huu ambao unahamasisha uhuru wa watu kuabudu na kutokashifu dini za watu wengine si dhani kama litakuwa jambo ovu na dhambi kwa Mwenyezi Mungu ambaye anaona fahari watu wanapomwabudu yeye. Aidha msanii Roma katika wimbo wake wa 2030 anaieleza jamii kuwa Mkristo anayedhihaki Msaafu (Quran) huenda halijui kanisa kwa maana kwamba kama angekuwa ni muumini wa kweli na anaijua dini yake vizuri hasingewezai kuukashifu Msaafu. Vilevile anaona kuwa Muislamu anayechoma kanisa ni sawa na kuuza Biblia Dubai ambako asilimia kubwa ya wananchi wake ni wafuasi wa dini ya Kiislam. Rejea msanii anaposema:

Anaedhihaki msahafu pengine kanisa halijui,
So kulichoma kanisa ni kuuza Bible Dubai.

Pamoja na kwamba msanii katika mistari hii hajatueleza wazi ni kwa namna gani kulichoma kanisa ni sawa na kuuza Biblia Dubai. Funzo kubwa tunalipata hapa ni kwamba watu wanaoamua kukashifu dini za watu wengine au kuchoma majengo ya ibada ya waumini wa dini zingine wanakuwa ni waumini ambao hawajui vizuri mafundisho ya dini zao. Kwa maana dini zote hizi zinawafundisha waumini wake kupendana (rej. Mathayo, 22:40; Mathayo, 5:17-20; Luka. 6:27-29; Luka. 16:17; Quran, 5:82 na Qur'an 21:107).

2.2 Kumwabudu Mungu wa Kweli
Moja ya amri kumi za Mungu ni kumtaka binadamu kutoabudu miungu wengine isipokuwa yeye tu (rej. Kutoka, 201-17; Mathayo 19:18-22; Quran, 2:163; Quran 17:22; Quran, 20:14 na Quran 26:68-73). Katika Biblia kuna kisa kimoja kinaelezwa kuhusu Yesu kupandishwa juu na ibilisi na kuoneshwa milki zote za ulimwengu ambazo angepewa azimiliki kama tu angekubali kumsujudia ibilisi, jambo ambalo alilikataa. Rejea Luka 4:5-8 maandiko yanaposema:
Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa msujudie Bwana Mungu wako
umwamwudu yeye oeke yake.

Hali kadhalika katika Muziki wa Kizazi Kipya wasanii wanatueleza hili katika wimbo wa Msafiri ulioimbwa na kundi la Kwanza Unit wanaposema:
Naota ndoto za peponi,
Naona shetani aniuliza wewe ni nani?
Na wataka nini, pesa nyumba na magari ya kifahari,
Njoo nifuate mimi, nakuwa makini?

Kama ilivyoelezwa katika Luka 4:5-8 na haya wanayoeleza wasanii katika mistari hii ambayo ni kama wamedondoa katika andiko hilo, tunaona kuwa kikubwa wanachotusisitiza wasanii ni kuwa pamoja na ahadi ya vitu vingi vya kifahari na thamani katika ulimwengu huu binadamu anatakiwa kuwa makini na vitu hivyo bila kuacha kumuabudu Mungu wa kweli. Tunachosisitizwa hapa ni kumwabudu Mungu pekee na si miungu wengine. Kuna dhambi gani kuusikiliza wimbo wa aina hii ambao unatuasa kumwamudu Mungu wa kweli kama vitabu vya dini vinavyotuasa?

2.3 Kuzishika na Kuzifuata Amri Kumi za Mungu
Kati ya mambo yanayosisitizwa na dini ya Kikristo na Kiislamu ni waumini wake kuzishika, kuzitii amri kumi za Mungu. Amri hizo ni; (i) usiabudu miungu wengine, (ii) usilitaje bure jina la Mungu wako, (iii) Shika kitakatifu siku ya Mungu, (iv) Waheshimu baba na mama upate miaka mingi na heri duniani, (v) Usiue, (vi) usizini, (vii) usiibe, (viii) Usiseme uongo, (ix) Usitamani mwanamke asiye mke wako na (x) Usitamani mali ya mtu mwingine (taz. Kutoka, 20:1-17; Mathayo, 19:18-22 na Qur an 7:145; Quran, 17: 22-34). Amri hizi ndizo zinazowafanya binadamu kuwa na mahusiano mazuri na Mungu wao. Kutozifuata amri hizi ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini na maagizo ya Mungu. Kutokana na umuhimu wake katika maisha ya binadamu hapa duniani na baada ya kifo viongozi wa dini, waimbaji wa nyimbo za dini wamekuwa wakizifundisha na kuzisisitiza ili watu wapate kuzifuata. Vivyo hivyo hata wasanii wa muziki wa kizazi wamekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wasikilizaji wa nyimbo zao kuzielewa na kuzishika amri kumi za Mungu ili kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Msanii Dudu Baya anasisitiza jamii yake kuziheshimu na kuzifuata amri kumi za Mungu katika wimbo wake wa Mungu Wangu. Rejea katika wimbo huo anaposema:
Nimeamua kuwatupia kamba
ambayo mtu anatakiwa kuishikiria tu
ndipo aokoke (eeeh Bwana!)
kamba yenyewe ni amri kumi
ukizishika utaokoka milele,
amri zenyewe ndizo hizi,
moja! Mwabudu Mungu wako tu
usiabudu miungu wengine (eeeh Bwana!)
pili! Shika kitakatifu siku ya Mungu wako (eeeh Bwana!)
tatu! Usilitaje bure jina la Mungu wako (eeeh Bwana!)
nne! Waheshimu baba na mama
upate miaka mingi na heri duniani (eeeh Bwana!)
tano! Usiue (eeeh Bwana!)
Sita! Usizini (eeeh Bwana!)
Saba! Usiibe (eeeh Bwana!)
Nane! Usiseme uongo (eeeh Bwana!)
Tisa! Usitamani mwanamke asiye mke wako (eeeh Bwana!)
Kumi! Usitamani mali ya mtu mwingine (eeeh Bwana!)

Msanii hapa anatukumbusha kuwa tukizishika amri kumi za Mungu tutaokoka hivyo kuepuka moto wa jehanamu siku ya mwisho. Anachosisitiza msanii hapa ni kilekile kinachosisitizwa na vitabu vya dini na viongozi wetu wa dini. Kwa kufanya hivi msanii anakuwa ametenda dhambi gani? Anayesikiliza wimbo wa aina hii anakuwa ametenda dhambi gani pia? kwa maoni yangu naona wimbo wa aina hii unafaa kusikilizwa na kila mtu kwa sababu unasisitiza mambo tunayosisitizwa kufanya katika dini zetu na ndivyo Mungu anavyopenda tutende.

2.4 Umuhimu wa Imani katika Dini
Viongozi wa dini kwa kutumia vitabu vya dini wamekuwa wakisisitiza waumini wao kuwa na imani thabiti dhidi ya dini zao, Mungu wao na hata mafanikio wanayohitaji kufikia wanatakiwa kuwa na imani kuwa watafanikiwa. Imani ni kipaji cha kimungu chenye kumwezesha mtu kumsadiki Mungu na ufunuo wake (rej. Katekisimu, 1998:68). Muziki wa Kizazi Kipya pia kwa kutumia tungo zake husisitiza juu ya binadamu kuwa na imani dhabiti ili waweze kuiona pepo siku ya mwisho. Kwa mfano katika wimbo wa Darubini Kali uliombwa na Afande Sele tunaelekezwa hili msanii anaposema:

Hapo ulipo kama unapenda pepo kwanini uogope kifo
Unachekesha ni balaa,
Unafikiri mbinguni utakwenda kwa motokaa!
Ama utapata zali kama Yesu alivyopaa!
Acha kujidanganya kwa Mungu si kwa Mzungu,
Unapokwenda kwa pipa,
Ikibidi kwa njia za panya,
Haiwezekani bila ya imani, unaelipiza baya kwa jema,
We ni shetani haufai msikitini haufai kanisani.

Msanii hapa anatuonesha kuwa Mbinguni hakuendeki kwa njia ya mkato zaidi ya watu kuwa na imani na kutenda matendo mema. Aidha msanii Roma pia anawataka waumini wa dini kuwa na imani thabiti na dini zao na si kuangalia matendo ya viongozi wao ili kuwa wafuasi wa dini husika. Viongozi ambao nao ni binadamu tu wanaoweza kukosea. Msanii analisema hili katika wimbo wa Mathematics:

Imamu akizini nje ya ndoa usiukimbie msikiti
Padri akilala na sista aibadilishi ukatoliki

Anachotufunza msanii hapa ni kwamba inapotokea Imam akazini nje ya ndoa hatupaswi kuukimbia msikiti hali kadhalika Padri akilala (kuzini) na sista usibadili dhehebu lako la Ukatoliki. Kwa maana kwamba matendo yote hayo yanayotendwa na viongozi wa dini si msimamo wa dini bali ni matendo yao binafsi.

2.5 Uvumilivu wa Kidini
Tanzania kuna waumini wa dini mbalimbali dini zenye waumini wengi ikiwa ni dini ya Kikristo na Kiislam. Kumekuwa na matukio ya waumini hasa wa dini hizi kutokea misuguano ya hapa na pale. Mfano ilitokea sintofahamu juu kuchinja, mtoto kukojolea Quran, makisa kuchomwa moto, viongozi wa dini kushambuliwa na kadhalika. Nchi zenye dini tofauti inapohitajika amani ni muhimu kuwa na uvumilivu wa kidini kati ya dini moja na dini nyingine. Muziki wa Kizazi Kipya unalieleza hili katika tungo zake. Mfano msanii Afande Sele katika wimbo wake Dini Tumeletwa anaeleza kuwa kabla ya dini hizi kuingiza Afrika, Waafrika walikuwa na dini zao na walimwabudu mungu na waliishi kama ndugu bila vurugu tofauti na sasa. Anashangaa kwa nini dini hasa dini hizi (za Kikristo na Kiislam) zinatufanya tuchukiane, tukashifiane, tuuane ikiwa tu zilikuja na wageni? Analisema hili katika wimbo huo anaposema: 

Wenyewe kwa wenyewe tunauana kikatili,
Tunaitana makafiri wakati inajulikana sisi ni ndugu wa asili,
Waafrika tunafeli, nako kusoma hatuwezi,
Hata picha hatuzioni,
Ndugu wa baba na mama tunauana kisa dini,
Haingii akilini,
Tofauti za kiimani zilizoletwa na wageni.

Kimsingi hapa msanii anatutaka waumini wa dini tofauti kupendana, kuishi kama ndugu bila kujali tofauti zao za dini. Msanii anaona dini zote hizi ni sawa, ni kama matawi tu ambazo zote zinamwabudu Mungu mmoja kama anavyosema pia katika wimbo huo:

Dini kama matawi lakini Mungu ndiye shina,
Sifa zake zinafanana labda tofauti zake ni majina,
Wapo wanaomwita Bwana, Jehova, Allah, Subhana,
Wengine wanamwita Krishna, Jah, God, Juva, Maulana,
Yote ni majina Mungu ni mmoja.

Hapa msanii anaweka wazi kuwa dini zote zinafanana, zinamwabudu Mungu mmoja isipokuwa tofauti zipo kwenye majina ya Mungu katika dini hizo. Hivyo sisi wote ni ndugu kwanini tugombanie fito wakati tunajenga nyumba mmoja. Jamii inahitaji kuvumiliana kidini ili kudumisha amani ya nchi. Watu waabudu wanachotaka kwa uhuru na amani. Ndiyo maana wasanii wa kundi la Hard Blasters katika wimbo wao wa Eee Mola wanatuasa kila mtu aabudu anachotaka na tusikashifiane. Aidha Roma naye katika wimbo wa 2030 anatueleza kuwa anayedhihaki msaafu pengine kanisa halijui. Kwa maana kama angekuwa analijua akatumbua kuwa kumbe haina haja ya kufanyiana unyama sisi kwa sisi ikiwa wote tunaabudu Mungu Mmoja kwa mawazo ya wasanii. Ikizingatiwa pia dini zote hizi zinasisitiza kupendana (rej. Mathayo, 22:40; Mathayo, 5:17-20; Marko, 12:30-31; Luka, 6:27-29; Luka. 16:17; Quran, 5:82 na Qur'an 21:107).

2.6 Kutoa Dhaka/ sadaka na kusali
Mambo muhimu ambayo waumini wa dini zote husisitizwa katika mafundisho ya dini ni kusali kwa bidii, kutoa dhaka, sadaka na michango mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya dini husika (rej. Hesabu 18:26; 1Wakorintho 16:1-2 na Quran, 2:43). Vitabu vya dini vinasisitiza hivyo na viongozi wa dini pia huwasisitiza waumini wao kufanya hivyo. Hali kadhalika wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya pia huwasisitiza wasikilizaji wao umuhimu wa kufanya hivyo katika tungo zao. Mathalni msanii Roma katika wimbo wa 2030 anasema:

Muislamu gani unahonga Bongo Movie mamilioni,
 mama anakufa mwaisela kakosa dripu ya quinine,
 ni heri ujenge Msikiti tuitukuze mitume,
 anasa za bakulutu unatunza wacheza sebene.

Hapa msanii anamshangaa Muislamu ambaye anahonga ‘Bongo Movie’ (wasichana waigizaji wa Bongo Movie) mamilioni ya pesa na kuwatunza wanamuziki wa dansi (sebene). Msanii anawashauri waumini wa aina hiyo badala ya kufanya mambo hayo ya anasa ni bora watumie fedha zao kujenga misikiti jambo litakalowaongezea thawabu kwa Mwenyezi Mungu. Aidha katika wimbo huo huo anasititiza waumini kutenda mema wakati wote na si katika mfungo wa Ramadhani pekee lakini pia anawasisitiza kusali kwa kwenda msikitini. Hili analisema katika wimbo huo anaposema:

Unamuheshimu ramadhani,
unazini mbele ya shaban,
Kama ilishushwa Quran
Twendeni misikitini.

Kwa hakika kutoa sadaka, Dhaka na kusali na kutenda mema ni njia za kumcha Mungu. Binadamu tunaaswa kumcha Mungu kwa kutenda mema na inapotokea tumeteleza kwa kufanya maovu hatuna budi kutubu makosa yetu (rej. 1Yohana, 1:9 na Quran, 2:54). Katika wimbo wa Eee Mola wa kundi la Hard Blasters tunasisitizwa hili wanaposema:

Njia ni moja tumfuate Yesu,
Eee! Walimwengu tumche Mungu,
Na kutubu makosa yetu.

Kama tunavyoweza kuona katika mistari hii, wasanii wanasisitiza mambo matatu ambayo tunakiwa kama binadamu kuyafanya. Kwanza tunasisitizwa kumfuata Yesu. Kwa imani ya dini ya Kikristo inaelezwa kuwa yeye ndiye njia pekee ya Kweli na uzima ambayo itampeleka binadamu peponi (rej. Yohana. 6:14). Pili tunasisitizwa kumcha Mungu na mwisho wanatutaka tutubu makosa yetu. Pengine swali la kujiuliza kwa kusikiliza na kushabikia muziki wa aina hii unaotuhamasisha kumfuata Yesu (kuokoka), kumcha Mungu na kutubu makosa yetu kwa muumba kuna dhambi gani? Kuna ushetani gani?

2.7 Toba
TUKI (2004:283) inaeleza toba ni majuto kwa matendo yaliyotendwa ambayo ni kinyume cha dini. Dini zote zinasisitiza waumini wake kufanya toba. Katika imani ya kanisa Katoliki toba ama kuungama ni mojawapo ya amri za kanisa ikiwa ni amri ya tatu (rej. Katekisimu, 1998:66). Aidha kwa upande wa dini ya Kiislamu toba pia ni jambo linalosisitizwa na dini hiyo (rej. Quran, 2:54 na Quran, 5:39). Vivyo hivyo wasanii wa kizazi kipya pia hutusisitiza kufanya toba kabla hatujakutwa na mauti ili kujihakikishia pepo. Katika wimbo wa Eee Mola uliombwa na kundi la Hard Blasters wanalisema hili:

Jaribu kufanya masahisho,
Kabla Mungu hajakata pumzi ya mwisho,
Kuna kila dalili za hicho kiyama.

Hapa wasanii wanatueleza kuwa tufanye masahisho ya matendo yetu kabla ya kufa kwetu maana kuna kila dalili za kiyama (siku ya mwisho ambaye watu watahukumiwa kwa matendo yao). Msanii King Crayz GK katika wimbo wa Nitakufanye anajiuliza atakufanye na ikitokea amekufa roho yake itaenda wapi? Ili roho yake iwe salama siku baada ya kufa anatueleza kuwa anahitaji kufanya toba kwa mabaya aliyofanya. Hili anaeleza katika wimbo huo anaposema:

Ningelihonga lakini Mungu hapokei rushwa,
Ili siku yangu ikifika GK niwe tayari,
Kuna mambo mengi nimefanya,
Mabaya nahitaji toba.

Hapa msanii anasisitiza kwamba kama kungekuwa na njia za mkato kuiona pepo angeweza hata kumhonga Mungu ili siku yake ikifika awe salama. Kutokana na ukweli kwamba Mungu hawezi kuhongeka msanii anaona hakuna namna zaidi ya kuungama na kufanya toba kwa mabaya tuliyoyatenda. Ndiyo maana wasanii wa kundi la Daz Nundaz kwa kuona hatari hiyo wanatusihi tuanze kutenda mema kabla kifo hakijatukuta. Rejea katika wimbo wa Kamanda wanaposema:

Anza kutenda mema,
Kabla kifo hakijakukuta.

Aidha msanii Linex katika wimbo wa Wema kwa Ubaya anatupa moyo kuwa Mungu ni mwepesi wa kusamehe makosa yetu pale tunapotubu. Rejea anaposema:
Mungu ni wa ajabu,
hata ukiwa mtenda mabaya,
Ukirudisha moyo wako nyuma,
Anasamehe na kusahau,
Mungu ni wa ajabuuu!
Wa ajabuu ooh! Aah!

Tunaona kwamba kama ambavyo viongozi wetu wa dini na vitabu vya dini kutuagiza kutenda mema na kufanya toba.

3.0 Hitimisho
Tumeona namna ambavyo mashairi ya Muziki wa Kizazi Kipya yanavyozungumzia masuala mbalimbali ya kidini. Masuala ambayo kwa hakika yanaweza kumuongoa mtu na kumfanya kuwa mtu wa kumtegemea Mungu, kusali/swali, kutoa Dhaka na michango mbalimbali katika nyumba za ibada lakini pia mashairi haya yanaweza kutufundisha jinsi waumini wa dini tofauti tofauti wanavyoweza kuvumiliana licha yo tofauti zao za kidini. Kutokana na uchambuzi huu naweza kuhitimisha kwa kusema kuwa wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya wapo ambao wanatufundisha mambo mazuri ya dini kama wafanyavyo viongozi wa dini na wasanii mbalimbali wa nyimbo za dini, tofauti ni kwamba wakati viongozi wa dini wanatumia mimbali za misikitini na makanisani wasanii wa kizazi kipya hutumia jukwa la Muziki wa Kizazi Kipya kufundisha na kuelekeza yale yale yanayosisitizwa na viongozi wa dini. Hivyo pamoja na uwepo wa nyimbo ambazo zinafikirika kwamba zinaweza kupotosha jamii, zipo nyimbo ambazo zinaweza kuwaleta na kuwasogeza watu katika dini au kwa Mungu. Kwani wapo baadhi ya wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya ni mawakala wazuri katika kuhakisha mafunzo haya yanatufikia ili tuweze kumwamudu Mungu wetu pasi na tatizo lolote. Kwa kusikiliza wimbo wenye maudhui ya aina haya licha ya kwamba ni Muziki wa Kizazi Kipya kwa maoni yangu sidhani kama tutakuwa tumetenda dhambi au kumkosea Mungu.

Marejeo
Al-Farsy, A. S. (hm). Qurani Takatifu: Iliyofasiliwa na Marehemu Sheikh Abdullah Salehe Al-Farsy. India.
Bible Society of Tanzania. (1997). Biblia Maandiko Matakatifu. Dodoma: Bible Society of  Tanzania.
Chachage, S. (2002). “Ndani ya Bongo: Utandawazi na Migogoro ya Utamaduni.” Makala iliyowasilishwa katika Mkutano wa Kumi wa Hali ya Siasa Tanzania. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Dar es Salaam.
JMT. (2005). Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Dar es Salaam. Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali.
Katekisimu. (1998). Katekisimu: Katekisimu Ndogo ya Kanisa Katoliki. Songea. Peramiho Printing Press.
Mahenge, E (2010/2011). “Chimbuko la Muziki wa Hip Hop ni Uasi au Sanaa za Maonesho?” Mulika Na. 29 & 30. TATAKI. Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Uk. 2-15.
Mangesho, P. (2003). “Global Cultural Trend. The case of Hip Hop Music in Dar es Salaam”, M.A. Tasinifu. University of Dar es Salaam.
Omari, S. (2009). “Tanzania Hip Hop Poetry Literature”, PhD. Tasinifu, Chuo Kikuu cha
Perullo, A (2005). “Hooligans and Heroes: Youth Identity and Hip-Hop in Dar es Salaam, Tanzania.” Katika Africa Today, No. 76.
Remes, P. (1999). “Global Popular Musics and Changing Awereness of Urban Tanzanian Youth.” Katika Yearbook for Traditional Music, Vol. 31 (1999), uk. 1-26. International Council for Traditional Music.
Samwel, M. (2010). “Masuala ya Kisiasa katika Mashairi ya Mapenzi ya Muziki wa Bongo Fleva”, Mulika Na. 29 & 30. Uk. 16-28. TATAKI. Chuo Kikuu cha Dar es salaam.                  
Suriano, M. (2006). “Hip Hop and Bongo Flavour Music in Contemporary Tanzania: Youth’ Experiences, Agency, Aspirations and Contradictions.” Imepakuliwa kutoka www.ascleiden.nl/pdf/youthconfsuriano1.pdf. tarehe 15 Novemba, 2015
TUKI. (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.

Diskografia
Afande Sele-- Darubini Kali
Afande Sele-- Dini Tumeletewa
Daz Nundaz -- Kamanda
Dudu Baya -- Mungu Wangu
Hard Blasters-- Eee Mola
King Crayz GK -- Nitakufaje
Kwanza Unit -- Msafiri
Linex -- Wema kwa Ubaya
Roma--2030


[1] Kwaito ni sawa na Muziki wa Kizazi Kipya kwa Tanzania, nchini Kenya hujulikana kwa jina la Genge. Hivyo kuupinga muziki wa kizazi kipya na kuukubali muziki wa Kwaito ni jambo la kustaajabisha. Ni muziki ule ule unaotofautishwa na majina na maeneo tu. 

Mwandishi wa makala haya ni Mwalimu katika Shule ya Sekondari Mwanzi (Manyoni DC)
Anapatikana kwa namba 0715 33 55 58/ 0755 44 06 99


No comments:

Post a Comment