WALIOTETEA UCHOTWAJI FEDHA
Pamoja na Kamati ya PAC kuwasilisha ripoti yake juu ya suala hilo
ambapo ilijiridhisha kuwa sehemu ya fedha hizo ni za Serikali, baadhi ya
wabunge na mawaziri walipinga hatua hiyo na kusema kuwa fedha hizo
hazikuwa za umma bali ni mali za IPTL.
Mmoja wa mawaziri waliosimama bungeni kutetea suala hilo ni aliyekuwa
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye
alizungumza kwa kujiamini kuwa fedha hizo si mali ya umma.
LUSINDE
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), akichangia ripoti hiyo ya
PAC bungeni, alisema hata Zitto ambaye ni mwenyekiti wa kamati alipokea
fedha kutoka kwa Sethi.
“Zitto ni rafiki yangu mkubwa na aliwahi kunisaidia nilipokuwa na
tatizo, lakini katika hili lazima niseme kwamba ulipokea fedha kutoka
kwa Sethi, atupe jibu isije kuwa tunakaa hapa kumbe walaji wako wengi.
Kwa nini Tibaijuka anapopewa inakuwa fedha haramu, lakini kwa Zitto ni
halali?
“Na Zitto anahusika, Kafulila naye anakuja hapa ohh eti taarifa ya
siri imevuja tujadili, tujadili kwani ninyi Mungu?” alihoji Lusinde.
MOHAMED CHOMBO
Mbunge wa Magomeni, Zanzibar, Mohamed Chombo (CCM) alisema:
“Nimesikiliza ripoti ya PAC na Serikali, lakini jambo hili lipo wazi
kwamba hizi fedha hazikuwa za umma, zilikuwa za IPTL zimelipwa na
Tanesco.”
RICHARD NDASA
Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alisema kumezuka mtindo wa kusingiziana na kwamba wabunge wa aina wamwogope Mungu.
“Tusiwavunje moyo wizara, wamefanya kazi kubwa, tushauri pale kwenye tatizo tuseme sasa fukuza huyu halafu nini kinafuata?
“Tukiwa na utaratibu wa kufukuzana itaendelea hivyo hivyo, tumwogope
Mungu, lakini nafsi zetu zitatusuta kwa sababu ya matendo yetu. Hivi
sasa kamezuka mtindo wa kusingizia mtu huyu kala, huyu kapewa mtu
akipewa asimame hapa aseme amepewa, lakini tusiwasingizie,” alisema
Ndassa.
MARIAM KISANGI
Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi (CCM), alisema upinzani baada
ya kuona kwamba chama tawala kinapeta wakaamua kuwakoroga na Escrow.
“Tuangalie utendaji wa watu na ninawaambia hatoki Muhongo wala Maswi,
CCM kitapita na hiyo ndiyo njama zenu upinzani kutukoroga. Mmekaa mkao
na CCM inapeta, mkajisemea hawa tuwakoroge na nini ndio mkaja na Escrow
mara EPA, nawaambia njama zenu hazisaidii.
“Zile fedha si za umma. Tanesco ina madeni mengi, inadaiwa Sh bilioni
700. Waziri ameeleza vizuri, kwa hiyo tusipotezeane muda hapa,” alisema
mbunge huyo.
SIMBACHAWENE
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Kibakwe,
George Simbachawene, naye alitumia mbinu zote kutetea ufisadi huo na
wakati mwingine alijenga hoja ili watuhumiwa waweze kupenya.
Chanzo: GAZETI LA MTANZANIA
No comments:
Post a Comment