Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Friday, January 13, 2017

Rais wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 13 Januari, 2017 ameyaonya magazeti mawili yanayoandika habari za uchochezi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

Simu : +255-22-2114512, 2116898
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA

Rais wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 13 Januari, 2017 ameyaonya magazeti mawili yanayoandika habari za uchochezi na kupotosha wananchi kwa kuwa vinahatarisha amani ya nchini.

Rais Magufuli ametoa onyo hilo wakati akikagua na kufungua Kiwanda cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga.

Rais Magufuli amesema Serikali haitayavumilia magazeti hayo mawili kwa kuandika habari za uchochezi ambazo zinaweza kuhatarisha amani ya nchi kama ilivyotokea katika nchini ya Rwanda na kupelekea mauaji ya kimbari nchini humo.

''Serikali ya kutumbua majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti yanayofanya mambo ya uchochezi hatuwezi kuiacha Tanzania ikawa dampo la eneo la kuweka maneno ya uchochezi chini ya utawala wangu hilo halitakuwepo kuna magazeti mawili tu kila ukisoma wao ni kuchochea tu ikizungumzwa habari hii wao wanageuza hii nasema na nataka wanisikie siku zao zimeshafika kama wanasikia wasikie wasiposikia  wasisikie lakini magazeti mengine na vyombo vyote vingine vinatoa uchambuzi mzuri sana''.

Rais Magufuli amesema Serikali yake haiwezi kuvumilia kuona amani ya nchi inahatarishwa na magazeti mawili kwani amani ndio chimbuko la maendeleo ya taifa lolote duniani.

Amesema bila kuwepo kwa amani hakuna mwekezaji atakayeweza kuja kuwekeza nchi, hata wawekezaji wa ndani watashindwa na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Rais Magufuli amesema uwepo wa amani nchini ndio uliowezesha wawekezaji wa Kiwanda cha Fresho cha kutengenezea mifuko ya kubebea bidhaa za chakula nchini na kiwanda cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga kujengwa mkoani hapo kwani bila amani visingeweza kujengwa.

Aidha ameitaka Benki ya Uwekezaji Nchini TIB na Taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika viwanda badala ya kuwakopesha wanasiasa ambao hutumia fedha wanazokopa kwa matumizi yasiyowanufaisha watanzania waliowengi

Rais Magufuli ameupongeza uongozi wa mkoa wa Shinyanga kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya kutaka Tanzania ya viwanda kwa kujenga viwanda vingi mkoani humo ikiwa ni pamoja na viwanda hivyo viwili alivyovizindua katika siku yake ya mwisho ya ziara mkoani Shinyanga.


Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu
Shinyanga
13 Januari 2017.

No comments:

Post a Comment