MAHAKAMA ya Rufaa Dar es Salaam, imetengua adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na faini ya sh bilioni 22 iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Februari 23 mwaka 2012, dhidi ya raia wa Taiwan na China.
Nahodha wa meli, Hsu Chin Tai, na wakala wa meli ya Tawaliq 1, Zhao Hanquing walikata rufaa baada ya kubaini sheria zilikiukwa wakati wa uendeshwaji wa kesi hiyo katika mahakama za chini.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na jopo la majaji watatu Salum Masati, Semistocles Kaijage ambao walisema dosari ya kwanza ambayo Mahakama ya Rufaa imebaini ni kwamba kesi hiyo ilifunguliwa bila kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Hata hivyo, Mahakama Rufaa imempa ruhusa DPP ya kuwafungulia kesi upya warufani hao na wale walioachiliwa na Mahakama Kuu, kama ataona kuna haja ya kufanya hivyo.
Wakili wa warufani hao, John Mapinduzi, alisema amefurahishwa na hukumu hiyo na kwamba hivi sasa anajiandaa kufungua kesi ya madai dhidi ya serikali kutaka wateja wake walipwe fidia.
Pia alisema ataiomba Mahakama iilipe meli iliyokuwa ikitumiwa na watuhumiwa hao kuvua samaki ambayo kwa sasa imechakaa kutokana na vyuma vyake kukatwa kama chuma chakavu.
Machi 2009 washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kisha kesi hiyo ikahamishiwa Mahakama Kuu wakikabiliwa na makosa ya kuvua samaki bila leseni, kuharibu mazingira katika kina kirefu cha ukanda wa Bahari ya Hindi eneo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Via: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment