Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Tuesday, June 25, 2013

HATIMAYE JOYCE KIRIA AOMBA RADHI

 
Baada ya Jeshi la Polisi kumjibu Joyce Kiria kuhusiana na kuandamana na watoto wake kulitaka jeshi hilo limweleze alipo mume wake Bw. Henry Kilewo hatimaye Joyce aamua kuomba radhi.
 
 
                  TAARIFA YA JOYCE KIRIA KWA VYOMBO VYA HABARI.

YAH; KUOMBA MSAADA WANAWAKE WENZANGU NA WATANZANIA WOTE.

Jina langu ni Joyce Kiria, mke wa Henry Kilewo. Mimi ni mdau wa media, mdau wa Haki za Wanawake. Mume wangu ni mwanasiasa na ni mdau wa Haki za Binadam. Kwa sasa anashikiliwa na jeshi la polisi tangu Ijumaa.

Mume wangu alipigiwa simu kutoka makao makuu ya jeshi la polisi wiki iliyopita. Yeye wakati huo alikuwa safarini kwa shughuli zake za kisiasa, akaniambia ameitwa na akawasiliana na mwanasheria wetu Peter Kibatala, mwanasheria nae alikuwa na shuguli nyingi wakakubaliana wakutane Dar ili waende kuitika wito huo. 21june2013 siku ya ijumaa mume wangu alikwenda makao makuu ya jeshi la polisi kuskiliza wito huo. Mchana nikiwa naendelea na shughuli zangu za kikazi, nikapokea simu toka kwa wakili wetu Peter Kibatala akinijulisha ya kwamba wamemzuia mume wangu wakidai kwamba anahusika na kesi ya 2011 ya uchaguzi huko Igunga.

Baada ya kupokea hizo taarifa binafsi nikaanza kufatilia. Kwanza nikaanzia huko alikokuwa anashikiliwa (makao makuu ya jeshi la polisi) ambapo tulimkuta akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi chini ya askari SSP PASUA na wenzake. Nashukuru nilipata fursa ya kumuona na kumpa chakula ambapo mume wangu alikuwa hajala tangu asubuhi. Ilipofika saa moja jioni mume wangu Henry Kilewo alihamishwa kutoka makao makuu ya jeshi la polisi kwenda central polisi akalala pale.

Siku iliyofata nilidamka asubuhi nikampelekea chai. Chai ikapokelewa na askari akapelekewa akanywa. Baada ya muda mfupi akaingia SSP PASUA kutoka makao makuu ya jeshi la polisi, akazungumza na askari wenzake ndipo niliporuhusiwa kumuona tena. Tukasalimiana kwa dakika mbili baada ya hapo akarudishwa lokap, basi na mimi nikaambiwa nimimi peke yangu naruhusiwa kupeleka chakula chake. Nikatoka kwenda kuandaa chakula cha mchana.

Ilipofika saa sita mchana nikawa nimefika central polisi kumpelekea mume wangu chakula. Nilipata faraja sana baada ya kumkuta mwanasheria wetu Peter Kibatala akiongea na mteja wake ambae ni mume wangu Henry. Mwanasheria aliambiwa ampatie chakula lakini aonje kwanza. Baada ya kula na kuongea na wakili alinisalimia kwa mbali akarudi zake lokap. Wakati naondoka central nikaambiwa na askari wa zamu kwamba chakula cha jioni ni saa kumi na moja kamili mwisho kumi na mbili kamili. Ilipofika muda huo nikawa central cha chakula changu.

Wakati napanda ngazi kuelekea mapokezi ya central polisi, askari mmoja akaanza kusema ya kwamba huyo mnaempelekea chakula kashachukuliwa. Mi nikasogea mpaka mapokezi, nilipofika mapokezi nikamkuta askari ambae alikuwepo tangu asubuhi, nilimueleza ya kwamba nimemletea mume wangu chakula cha jioni. Askari akanijibu ya kwamba ‘’MTU WENU KASHACHUKULIWA’’ nikauliza wamemchukua wamempeleka wapi? Akanijibu ‘’HATA MIMI SIJUI’’

Baada ya kupata hayo majibu toka kwa askari wa zamu, nilimpigia wakili wetu Peter Kibatala kujua mume wangu amepelekwa wapi. Cha ajabu wakili nae alipata mshituko na akaniambia kwamba na yeye hana taarifa zozote na anashangaa kwa nini wamemtoa bila kumpa taarifa yeye kama wakili wake. Ndipo hapo nilipopata maswali mengi ambayo sipati majibu mpaka sasa.

Ndo sababu hasa ya kuita vyombo vya habari mnisaidie, na watanzania pia mnisaie, wanawake wa nchi hii mnisaidie zaidi ya hao Mh Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mh IGP Mwema mnisaidie.

1. kwanza kumuombea mume wangu huko aliko aweze kuwa salama.

2. Ni kweli sijui sheria, lakini inawezekana vipi mtuhumiwa ambae yuko chini ya ulinzi wa jeshi la polisi atoke bila askari wa zamu kujua?

3. Mimi sina tatizo na mume wangu kutuhumiwa, lakini kinachoniuma zaidi ni kwanini inakuwa siri?

4. Mimi ninataka kujua mume wangu yuko wapi? Najua anashikiliwa na jeshi la polisi, nachotaka kujua yuko wapi? Au sina Haki ya kujua?

5. Wanawake wa nchi hii nisaidieni, tunateseka na watoto wangu tukitafuta kujua mume wangu baba yao yuko wapi? Ndugu zake wananiuliza, mama yake, baba yake, marafiki wananiuliza Henry yuko wapi? Kwa nini wananificha mimi mke wake?

6. kuna Agenda gani ya siri, Wanawake wenzangu, yanapotokea matatizo sisi ndiyo wahanga pamoja na watoto wetu, mfano halisi ndo huu kama mnavyoniona na watoto wangu. Kitendo cha kufanya jambo hili siri nimeishiwa maziwa ya kumnyonyesha mwanangu mchanga Linston.

Naomba muungane na mimi katika kipindi hiki kumuombea mume wangu Hanry Kilewo avuke kizingiti hiki kinachomkabili.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA


JOYCE KIRIA
WANAWAKELIVE


 
 




MSEMAJI WA JESHI LA POLISI ALIMJIBU HIVI...


''Inasikitisha kuona kwamba huyu mama Joyce Kiria anaingilia mambo ya kisheria na kutaka kupotosha jamii kwamba hajui mume wake yuko wapi pia nadhani analenga kuichochea jamii kwamba aliyetuhumiwa kutenda uhalifu akikamatwa familia yake iandamane, tendo ambalo pia ni kosa la jinai. Aidha anatakiwa kuheshimu haki za watoto na kuacha kuwatumia katika kinga ya kutetea watu wanaotenda uhalifu (Imetolewa na Advera Senso Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania)''


Maelezo ya Joyce baada ya taarifa ya jeshi.

Binafsi kama JOYCE KIRIA nachukua nafasi hii tena kumuomba msemaji wa jeshi la polisi anisamehe kama nilikosea kudai haki yangu na watoto wangu ya kujua baba yao/ mume wangu yuko wapi! taarifa nilizokuwa nazo hazikuwa na uhakika kwani kuna waliosema kapelekwa Igunga na wengine wakasema kapelekwa Tabora. kwanini niishi kwa mashaka na taarifa zisizo rasmi toka kwa watu baki wakati waliomsafirisha Jeshi la polisi walikuwa na uwezo wa kuitaarifu familia au wakili wake?


Narudia tena kama ni makosa NAOMBENI MSAMAHA KWA MH RAIS, IGP MWEMA, WANAWAKE WA NCHI HII NA WATANZANIA WOTE.

Chanzo: www.joycekiria.com 

Monday, June 24, 2013

CHADEMA TISHIO, MAKADA WAKE WASHTAKIWA KWA UGAIDI AKIWEMO MUME WA JOYCE KIRIA

 
     Kutoka Tanzania Daima
 
KASI ya kuimarika na kushamiri kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kila kukicha kunakotokana na kukubalika kwake kwa wananchi, kumekuwa tishio kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
 
Hali ya mambo inaonesha kuwa, kitisho hicho ndicho kinainyima usingizi CCM na serikali yake, hivyo kupanga na kuibua vituko dhidi ya CHADEMA ili kukidhoofisha na kukipaka matope mbele ya wananchi.
 
 
Vituko na mikakati hiyo imezidi kushika kasi ambapo safari hii, makada watano wa chama hicho wameshtakiwa kwa kosa la ugaidi, ukiwa ni mwendelezo na sehemu ya mkakati huo kwa kutumia njia mbalimbali.
 
 
Kosa kama hilo pia alishtakiwa nalo Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, hivi karibuni, lakini Mahakama Kuu ilimfutia shtaka hilo.
 
 
Wakati makada hao wameshtakiwa kwa ugaidi, kosa ambalo halina dhamana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Tundu Lissu na Godbless Lema wamezuiwa kuingia bungeni.
 
Hata hivyo, matokeo ya kiwewe cha CCM dhidi ya CHADEMA, yamewahi kukipata Chama cha Wananchi CUF kuelekea uchaguzi wa mwaka 2005, baada ya kuonekana ni tishio dhidi ya CCM.
Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Omari Mahita, aliibua tuhuma nzito dhidi ya CUF kuwa waliingiza nchini shehena ya majambia, hivyo ni chama hatari, doa ambalo kwa kiasi kikubwa lilikiathiri chama hicho.
 
 
Safari hii, hila hizo zinaelekezwa kwa CHADEMA kinachoonekana ni tishio kwa utawala wa CCM na serikali yake ambapo jana makada wake wameshtakiwa kwa ugaidi.
 
 
Walioshtakiwa kwa ugaidi
Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo, Evodius Justinian wa Buboka, Oscar Kaijage wa Shinyanga, Seif Magesa Kabuta wa Mwanza, Rajab Daniel Kihawa wa Dodoma, jana wameshtakiwa kwa ugaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora mjini.
 
 
Watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi kwa kumteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.
Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka mawili wote, la kwanza ni la kufanya ugaidi, na la pili ni kummwagia tindikali Tesha.
 
 
Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, ya Tabora mjini, Joktani Rushwera, huku upande wa serikali ukiwakilishwa na Wakili Juma Massanja na Ildefons Mukandara.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Profesa Abdalah Safari, ukiwajumlisha Peter Kibatala na Gasper Mwalyela, uliiomba mahakama hiyo iyafute mashtaka hayo kwa sababu ya kutokuwa na uhai.
 
 
Mawakili wa utetezi walidai kuwa mashtaka hayo hayana uhai kwa sababu yamefunguliwa bila ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
 
Ulidai sheria za uendeshaji wa makosa kama hayo hapa nchini zinadai kuwa mashitaka kama hayo yanapofunguliwa ni lazima ridhaa ya DPP iwepo lakini ridhaa hiyo haipo hivyo yatupwe.
 
Ulitoa sababu ya pili kuwa maelezo hayaoneshi kosa husika ni la kigaidi, tofauti na makosa mengine ya kawaida kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hivyo waliomba yafutwe au yafunguliwe kama kosa la kawaida.
 
 
Upande huo wa utetezi ulidai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, inaelekeza kuwa mshitakiwa ashitakiwe katika mahakama yenye mamlaka na hadhi kama ile waliyopelekwa katika maeneo yale walikokamatwa.
 
 
Ulidai mawakili waliiomba mahakama itupilie mbali shitaka, kwani washitakiwa kama walikuwa na hatia walipaswa kushitakiwa katika maeneo yao walipokamatwa.
Baada ya hoja hizo, mahakama iliahirisha kesi hiyo na itatajwa tena Julai 8, mwaka huu Tabora mjini.
 
 
Hii si mara ya kwanza kwa viongozi au wafuasi wa CHADEMA kufunguliwa kesi zinazohusiana na ugaidi, Machi 18, 2013, Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka manne, yakiwamo ya ugaidi.
 
 
Kosa jingine lililowakabili Lwakatare na Ludovick ni kula njama; kosa ambalo pia linawakabili washtakiwa wote, ambalo ni kinyume cha kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na. 21 ya mwaka 2002.
 
 
Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka Denis Msaki, kinyume cha kifungu cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
 
Katika kosa la tatu, washtakiwa wote wawili wanadaiwa kufanya mkutano wa kupanga kufanya makosa ya ugaidi  kinyume cha kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi.
 
 
Wakili wa serikali alidai kuwa washitakiwa wote Desemba 28, mwaka jana walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyara Msaki kinyume cha kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi.
 
 
Pamoja na tuhuma hizo, Mei 8, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimfutia mashitaka matatu ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Lwakatare.
 
 
Jaji Lawrance Kaduri akitoa uamuzi huo alisema ulitokana na kukubaliana na hoja ya mawakili wa Lwakatare; Tundu Lissu, Peter Kibatara na Mabere Marando na kusema kuwa:
 
“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama inatoa amri ya kumfutia Lwakatare mashitaka matatu, yaani kosa la pili, tatu na la nne kwa sababu Jamhuri imeshindwa kuonesha maelezo yanayotesheleza kumshitaki Lwakatare kwa kesi ya ugaidi.
 
 
“Naamuru jalada la kesi ya msingi lirudishwe Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya mshitakiwa kuendelea kushitakiwa kwa kosa moja la kula njama, ambalo linaangukia katika sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002,” alisema Jaji Kaduri.
 
 
Mbowe, Lissu, wazuiwa
 
Licha ya kanuni za Bunge kuruhusu vazi la safari suti yenye mshono kama kombati zinazovaliwa na baadhi ya wabunge wa CHADEMA, kwa mara ya kwanza Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe na wenzake watatu jana walizuiwa kuingia bungeni.
 
 
Mbowe na Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) walizuiwa na askari kwa madai kuwa wamevalia sera za chama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni katika viwanja vya Bunge, Lissu alisema walishangazwa na uamuzi huo wakati mavazi hayo wamekuwa wakiyavaa na kuingia nayo bungeni kwa miaka mingi sasa.
 
 
Lissu alisema kuzuiwa kwao wanakuchukulia kuwa ni mkakati maalumu wa serikali ya CCM kutaka kuwazima na kuhakikisha hawapati nafasi ya kuingia bungeni ili wasijibu mashambulizi ya tuhuma wazosingiziwa kuhusiana na mlipuko wa bomu jijini Arusha.
 
 
“Sisi hali hiyo tulianza kuishtukia tangu asubuhi tulipoingia kwenye eneo la Bunge, kama mligundua kulikuwa na askari wengi sana kila kona kuliko kawaida kana kwamba nchi imepinduliwa. Kinyume cha utaratibu na kanuni, askari wa kawaida wameingiza hadi bungeni.
 
 
“Tulipofika wakati wa kuingia ukumbini mimi, Mbowe, Lema na Wenje tuliambiwa haturuhusiwi kwa kuwa tumevaa sare za chama. Tulipouliza nani kawapa maagizo hayo walidai ni uongozi wa juu, yaani Spika wa Bunge,” alisema Lissu.
 
 
Aliongeza kuwa kitendo hicho ni kichekesho kwani wakati wote tangu mwaka 2010 Mbowe amekuwa akivalia vazi hilo, achalia mbali wabunge wenzake baadhi ambao mara moja moja nao walikuwa wakivaa suti hizo lakini hawajawahi kuzuiwa.
 
 
Hata hivyo, pamoja na uamuzi huo, kanuni za Bunge hakuna mahali zinazuia mbunge kuvaa sare ya chama chake isipokuwa kanuni limeainisha aina za mavazi ya kuvaliwa na wabunge wanawake na wanaume.
 
 
Kwa mujibu wa kanuni ya 149 (3)(a) Kwa wanawake na (b) Kwa wanaume inasema: (a) Kwa wanawake;- (i) Vazi lolote la heshima yaani ambalo si la kubana mwili, lisiloonesha maungo ambayo kwa mila na desturi za Kitanzania hayapaswi kuoneshwa na ni refu kuvuka magoti.
 
 
(ii) Gauni la kitenge au blauzi inayovaliwa na kitenge au sketi ya rangi yoyote (iii) Kilemba cha kadiri au mtandio (iv) Suti ya kike; au (v) Vazi linalovaliwa wakati wa eda.
 
 
(b) Kwa wabunge wanaume;-(i) Suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia; (ii) Vazi la kimwambao yaani ka nzu rasmi na nadhifu, koti, baraghashia na makubadhi au viatu; (iii) Suti kamili ya Kimagharibi ya rangi kadiri isiyomeremeta; (iv) Koti aina ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au (v) Tarbushi na kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti ya imani au mila.
 
 
Wasusia kupitisha bajeti
 
Akizungumzia kuhusu uamuzi wa wabunge wao kutoingia bungeni kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/14, Lissu alisema baada ya kukutana na kujadiliana kwa kirefu hawakuona sababu ya kuingia.
 
“Tukio la bomu kwa wafuasi wetu jijini Arusha halikuwa la bahati mbaya lakini tumejiuliza ni kwanini Bunge halikuahirishwa walau kwa siku moja kama ilivyo utamaduni ili kushiriki kuomboleza msiba huo,” alisema.
 
 
Alisema kuwa pamoja na kwamba kiongozi wao wa kambi, Mbowe na Lema ndio walikuwa wamelengwa kulipuliwa lakini wakarusurika, Spika wa Bunge na Waziri Mkuu hakuna hata mmoja aliyetuma salamu za pole kwa viongozi hao.
 
 
“Waliolengwa kulipuliwa ni Mbowe, Lema na James ole Millya, lakini hata risasi zilizowaua wale wafuasi wetu wanne zilikuwa zikielekezwa kwa viongozi wetu.
“Sasa tunajiuliza, Bunge limeona waliokufa Arusha ni Watanzania lakini kwa vile walikuwa kwenye mkutano wa CHADEMA haiwahusu, hivyo kama wanajifanya kama hakuna kilichotokea sisi tunaingia ndani kufanya nini?” alihoji.
 
 
Lissu alitaja sababu nyigine kuona siku zote kila unapotokea msiba mkubwa wa wananchi wakati Bunge likiendelea, wamekuwa wakitumwa wawakilishi lakini kwa tukio la Soweto, Arusha Bunge halikutuma mwakilishi.
 
 
Alifafanua kuwa sababu kubwa iliyowafanya wafikie uamuzi huo ni kutokana na hatua ya Spika wa Bunge kupindisha ratiba ya Bunge ili kuwanyima nafasi wasijadili bajeti hiyo, hivyo kuhoji wanakwenda kupitisha kitu gani ambacho hawakushiriki.
 
 
“Hatukuweza kuwasilisha maoni ya kambi kutokana na tukio la Arusha lakini kulingana na ratiba tulimaliza mazishi Ijumaa tukijua kabisa Jumatatu tungepewa muda wetu wa nusu saa kuwasilisha maoni ya kambi.
 
 
“Si hivyo tu, bali hata wale walioomba kuchangia wangepata nafasi ya kuchangia halafu Jumanne bajeti hiyo ingepitishwa kwa mujibu wa ratiba. Lakini kutokana na hofu kuwa tungejibu mapigo kuhusu madai ya Arusha waliamua kufanya mbinu za kutunyima nafasi,” alisema.
 
Chanzo: Tanzania Daima

Sunday, June 23, 2013

Mbowe, Slaa, Lissu, Mnyika waandaliwa kesi ya tindikali Igunga

                                                                 Mh. John Mnyika
 
 
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuna mpango mchafu wa kuwabambikizia viongozi wakuu wa chama hicho kesi ya kumwagiwa Tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Musa Tesha.
 
Viongozi wanaoandaliwa mpango huo ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Mnyika alisema mpango huo unafanyika kwa lengo la kukidhoofisha chama chao kinachowapa wakati mgumu CCM.
 
Alisema hivi sasa baadhi ya makachero wa polisi wamekuwa wakiwakamata vijana na kuwalazimisha kukiri kwa kuandika au kuandikiwa maelezo kuwa viongozi hao waliwatuma kummwagia tindikali Tesha wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
 
 
Mnyika alisema wafuasi wao waliokamatwa na polisi kwa kuhusishwa na tukio hilo wameshinikizwa kusema Mbowe, Slaa, Lissu na yeye ndio waliowatuma kummwagia tindikali Tesha.
 
 
Alisema jambo hilo linaendeshwa kisiasa, ambapo wafuasi wanne wameshatiwa mbaroni na kuwalazimisha kuwataja viongozi wakuu wa CHADEMA kuhusika na uhalifu huo.
Mnyika aliwataja waliokamatwa ni pamoja na Evodius Justinian, aliyeshikiliwa kwa siku mbili mjini Bukoba, na baadaye akapelekwa Mwanza kabla ya kufikishwa Dar es Salaam.
 
 
Alisema zoezi hilo lilifanyika kwa kificho na mtuhumiwa huyo baadae alifikishwa Igunga.
Alibainisha kuwa taarifa za kada huyo kupelekwa Dar es Salaam  zilikuwa za kificho kwani wakili wake, Nyaronyo Kicheere aliyeongozana na ndugu wa mtuhumiwa huyo walipofika Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam walielezwa amepelekwa Makao Makuu.
 
 
Mnyika alisema mara baada ya Evodius kuonana na wakili wake, Kicheere, siku hiyo alieleza unyama aliofanyiwa na jeshi hilo wakati wote wa mahojiano mkoani Mwanza na Dar es Salaam.
Katika maelezo yake yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Advocate Nyombi, Evodius alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa siri bila ndugu zake kujua, alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila kuruhusiwa kuonana na wakili wake.
 
 
Kada huyo akisimulia unyama aliofanyiwa alisema:  “Nimepigwa na polisi Mwanza, nikiwa chooni Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati naletwa huku, polisi wakaniambia mimi ni mtu hatari sana, niseme nilifanya nini Igunga na kama najua mkanda wa Lwakatare.
 
 
“Nikiwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni, waliingia pamoja na mimi wakanipiga sana, nimeshaandika maelezo kwa kulazimishwa, niliomba kuwa na wakili wakanikatalia.”
Aliongeza kuwa akiwa Dar es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video ya Lwakatare. Akawajibu kuwa ilifanyiwa uhariri na Ludovick, lakini akapigwa makofi na askari wakaagiza nyaya za umeme za kutesea.
 
 
“Waliposimama kuleta nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme nikasema hii video ni yangu. Ninaumwa sana tumbo la kuhara damu, natumia dawa nilizonunuliwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kagera tarehe 4 Aprili,” alisema.
 
 
Mnyika alisema mtuhumiwa wa pili aliyeteswa ili akubali kuandika kuwa Mbowe, Slaa, Lissu na Mnyika walimtuma akammwagie tindikali Tesha ni Seif Kabuta aliyekamatwa Mwanza.
 
Alisema Kabuta baada ya kukataa kukiri kuwa viongozi wake wanahusika na matendo hayo, walimfungia katika chumba maalumu wakamleta mke wake, mama yake na mkwe wake na kumtesa mbele yao ili akiri kuwa Mbowe na wenzake walimtuma kummwagia Tesha tindikali.
 
 
Mnyika alisema mtuhumiwa wa tatu aliyekamatwa kuhusishwa na tindikali ni Oscar Kaijage wa Shinyanga mjini, ambaye awali alipokamatwa aliambiwa ni kwa sababu kuna pesa zimepotea kwa njia ya simu, na yeye alikuwa anajishughulisha na uwakala wa pesa kwa njia ya mitandao ya M-pesa na Z-pesa.
 
 
Alisema mtuhumiwa huyo alipokutanishwa na makachero wa polisi makao makuu, naye alilazimishwa aseme kuwa Mbowe, Slaa, Lissu na Mnyika walimtuma akammwagie Tesha tindikali.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa nne ni Rajab Kihawa, aliyetumiwa wasichana kuitwa akiwa Dodoma, ambaye aliombwa akubali kupewa shilingi milioni 30, kama alivyolipwa Ludovick ili aseme kuwa Mbowe na wenzake waliwatuma kummwagia tindikali Tesha.
 
 
Mtuhumiwa wa mwisho ni Henry Kilewo, Katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya Kinondoni, na Katibu wa Makatibu wa CHADEMA Kanda Maalumu ya Dar es Salaam anayeshikiliwa na polisi.
Polisi wanamtuhumu Kilewo kummwagia tindikali Tesha wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
 
 
Kilewo alishikiliwa na polisi kuanzia Ijumaa iliyopita na baada ya kuhojiwa alichukuliwa kwa kificho kupelekwa Mwanza kwa ndege ili aweze kuunganishwa katika kesi hiyo ya Igunga leo.
Mnyika alisema Kilewo amesafirishwa bila wakili wake kuwa na taarifa kuwa amepelekwa Mwanza, wala mke wake aliyeambiwa ampelekee  chakula, lakini alipofika polisi aliambiwa mume wake hayupo.
 
 
Mmoja wa mawakili wanaokwenda Igunga kuwatetea Kilewo na wenzake, Profesa Abdallah Safari alisema wameshitushwa kusikia wateja wao wamelazimishwa kutoa maelezo ili kuwahusisha viongozi wakuu wa CHADEMA.
 
 
Alibainisha kuwa kutokana na kesi hiyo kuonekana kujaa masuala ya kisiasa, atashirikiana na mawakili wenzake ambao ni Peter Kibatala na Gasper Mwalyela na kama itakapolazimika watawaongeza Mabere Marando, Kicheere, Method Kimomogoro na Lissu.
 
 
 
Aliongeza kuwa imefika hatua itabidi atumie kifungu cha sheria cha 102, ili kujenga dhana ya kutiliwa shaka kwani viongozi wote wa CHADEMA sasa wamefunguliwa kesi katika maeneo mbalimbali nchini, huku wale wa CCM wakiachwa.
 
 
Profesa Safari alitolea mfano Mbunge wa Tabora mjini, Ismail Aden Rage, ambaye alipatwa na hatia katika uchaguzi wa Igunga na alipaswa kufungwa miaka mitatu bila fidia, lakini DPP amekalia faili lake hadi sasa.
Aliongeza kuwa mambo hayo yanajitokeza kutokana na CHADEMA kumtaja ofisa wa usalama anayeitwa Shaali Ally kuwa ndiye aliwatafuta vijana wa chama hicho akiwemo Ahmed Sabula na wenzake.
 
 
Alibainisha kuwa Machi 29, mwaka huu vijana hao waliitwa na Shaali katika chumba cha hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam, akiwataka wakubali kutumika kwa kutoa taarifa za vikao vya CHADEMA, kuwasilisha kwake nyaraka za kamati kuu na kueleza mipango ya chama katika kesi ya Lwakatare.
 
 
Kwenye mpango huu, ofisa huyo wa usalama wa taifa ambaye Marando alisema anamfahamu vizuri, alimuahidi Sabula kiasi cha sh milioni 30 na kwamba fedha hizo angelipwa kama ujira kwa kukubali kutoa ushahidi dhidi ya Lwakatare.
 
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima pia waweza lisoma hapa http://www.freemedia.co.tz/daima/

Monday, June 17, 2013

TAZAMA PICHA ZA NDOA YA FURAHA VENANCE NA REGINA MAFFA ILIYOFUNGWA KATIKA KANISA LA ST. MAURUS- KURASINI NA TAFRIJA FUPI ILIYOFANYIKA KATIKA UKUMBI POLICE BAND -KILWA ROAD TAR. 15/6/2013

Mambo ya pete hayo
Tukiweka sahihi kwenye cheti cha ndoa

Mara baada ya kukabidhiwa vyeti vyetu


Tukiwa nje ya Kanisa
Hili ndo gari la kuwabeba maharusi

Tukitoka Kanisani


Tukipata picha ya pamoja na Lena Mwakilembe

Bi harusi huyooooo

Akina mama wakiimba na kucheza ngoma za kinyakyusa

Mzee mzima nilijitutumua kweli

Mzee mzima nilijitutumua kweli




Bi harusi akiwa na shemeji zake, Meshack {kushoto] na Isaya {kulia}

Tukiingia ukimbini

Wazee wa zamani wakitoa burudani

Napenda kuwashukuru wale wote ambao waliniunga mkono kwa hali na mali, kwa michango yenu mliyojitolea kwa ajili ya kufanikisha jambo hili jema, Mungu awabariki sana na awazidishie maradufu kile mlichojitolea kwangu. Na wale walioniunga mkono kwa kuhudhuria katika shughuli hii Mungu awabariki sana.



Thursday, June 6, 2013

SERIKALI YAUMBUKA SEKTA YA ELIMU

 
• Kitabu cha hesabu chaonesha 2x7=15


Mh. James Mbatia


 
SERIKALI imeingia katika kashfa nyingine kwenye sekta ya elimu baada ya kudaiwa kuruhusu vitabu vyenye maelekezo yasiyo sahihi.
 
Mbunge wa kuteuliwa na rais, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) ndiye aliyeanika udhaifu uliomo kwenye vitabu vilivyoidhinishwa na serikali kutumika katika shule za msingi nchini ambapo aliviita ni sumu ya elimu.
 
Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Mbatia alionesha vitabu kadhaa bungeni huku akitaja makosa mengi yaliyomo na kuhoji viliidhinishwaje na Kamati ya Kuidhinisha Machapisho ya Kielimu (EMAC).
 
“Leo tunavuna tulichokipanda. Serikali imetumia fedha za chenji ya rada kusaini mikataba na kampuni zaidi ya 10 kwa ajili ya kusambaza vitabu kwenye shule zetu, lakini vitabu hivyo ni sumu kwa taifa,” alisema.
 
Alisema kuwa vitabu hivyo vimenunuliwa na fedha hizo sh bilioni 55.2 ambazo zilitengwa na serikali kwa ajili ya manunuzi ya vitabu na mihutasari.
 
Alisema kampuni hizo zilipewa mkataba wa zabuni ya kununua vitabu na mihutasari wa sh milioni 18 na ulisainiwa Machi 18 mwaka huu, huku wakitakiwa kumaliza ununuzi na usambazaji wake Septemba mwaka huu.
 
Mbatia alisema kuwa vitabu hivyo vikitumika vitalisababisha taifa kufa kielimu kwa vile watoto watajifunza mambo ambayo hayana ukweli.
 
Alitoa mfano wa kitabu cha Jiografia cha darasa la sita kilichoidhinishwa na EMAC ambacho kimekosewa kwa kuandikwa ‘Jografia’.
 
Vitabu vingine ni cha Hisabati cha darasa la nne katika ukarasa wa 49, ambapo imeandikwa sifuri gawanya kwa sifuri jibu lake ni sifuri wakati jibu sahihi ni haiwezekani.
 
Pia alisema kitabu cha Hisabati kingine kinaonesha 2x7=15 na kitabu cha Uraia pia kinaeleza kuwa ‘mtaa unaundwa na vitongoji mbalimbali na kuongozwa na wenyeviti wa vitongoji.
Mbatia alisema kitabu hicho kinasema kwamba wakazi wengi wa mtaa wameajiriwa na utumishi wa umma, viwanda na makampuni.
 
Alisema kampuni za Macmillan na Oxford zilizopewa jukumu la kuleta vitabu hivyo zimeshafukuzwa nchini Kenya baada ya kugundulika kuwa vitabu vyao havina ubora wa kitaaluma, lakini Tanzania imeendelea kuzikumbatia.
 
“Kama Rais Kikwete hivi karibuni akiwa Mbeya alikiri kuwa elimu yetu ina udhaifu, kwanini wabunge wa CCM hamtaki kukubali hili?” alihoji Mbatia na kupendekeza iundwe tume ya kudumu ya elimu itakayosimamia maslahi ya walimu, kasoro za elimu na mengineyo.
 
CCM wapindisha hoja
Katika hatua nyingine, wabunge wa CCM wamelazimika kupindisha mjadala wa hoja ya udhaifu wa elimu nchini ili kumwokoa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
 
Hatua hiyo imetokea bungeni mjini hapa ambapo Waziri Kawambwa aliwasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka 2013/14 ambayo ilijadiliwa kwa siku mbili.
Kutokana na upinzani mkali ulioonekana tangu mapema kutoka kwa baadhi ya wabunge hasa wa upinzani, wakitaka Waziri na Naibu wake Philipo Mulugo wajiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012, wabunge wa CCM walilazimika kukutana kwa dharura juzi.
 
Katika kikao hicho kilichoketi katika Ukumbi wa Pius Msekwa juzi saa 7:00 mchana, wabunge hao wa CCM walifundana na kuafikiana kumwokoa Waziri Kawambwa ili bajeti yake iweze kupitishwa.
 
Licha ya wabunge wawili wa chama hicho, Deogratius Ntukamazina (Ngara) na Said Mtanda (Mchinga) kuwa wachangiaji wa mapema kabla ya kikao hicho na hivyo kuishambulia wizara hiyo, waliofuata walikuja na visingizio vya kumwonesha waziri hana tatizo.
 
Katika michango yao, wabunge hao walijiegemeza kwenye hoja ya mgawanyo wa orodha ya shule za sekondari 1,200 zitakazofanyiwa ukarabati wakidai ifumuliwe kwa vile Mkoa wa Kilimanjaro umependelewa zaidi ya mikoa mingine.
 
Huku wakiunga mkono hoja ya waziri kwa asilimia mia moja na kisha kuanza kulalamikia kasoro zilizopo kwenye elimu, wabunge hao walimtetea Kawambwa kuwa hastahili kujiuzulu kwa vile wizara yake ina majukumu mengi yanayoingilina na Wizara ya Tamisemi.
 
“Jamani kusema Waziri Kawambwa ajiuzulu tunamwonea, hii wizara majukumu yake mengi yako pia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, atawajibikaje mwenyewe kwa matokeo haya?” walisema.
 
Katika utetezi huo, waliongeza kuwa bajeti ya wizara hiyo ni ndogo na hivyo waziri amekwama kutekeleza majukumu yake huku wakilibebesha lawama Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) kuwa ndilo limesababisha matokeo hayo kwa kupanga madaraja kimakosa.
 
Katika hatua iliyoibua msigano, wabunge hao walipendekeza serikali iunde tume nyingine ya wataalamu kuchunguza matatizo ya elimu nchini, jambo lililopingwa vikali na wapinzani wakihoji kwanini walikataa wazo hilo lilipoletwa na Mbatia.
 
Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, aliwaponda wapinzani akisema kuwa hawatambui kazi kubwa iliyofanywa na CCM na kumtaka Waziri Kawambwa achape kazi bila kuwasikiliza.
 
Aliitaka serikali kutowapeleka walimu wapya vituoni pasipo kuwapa fedha zao za kujikimu kwani inakuwa inatambua idadi yao, lakini akasisitiza kuwa waziri anakwamishwa na watendaji wake.
 
Peter Serukamba wa Kigoma Mjini, John Komba wa Mbinga Magharibi, Yahaya Kassim Issa wa Chwaka, Jason Rweikiza wa Bukoba Vijijini na Lutengano Kigola wa Mufindi Kaskazini, walilalamikia upendeleo kwenye mgawanyo wa shule, walimu kutopandishwa madaraja na Tamisemi kuondolewa majukumu ya elimu.
 
Hata hivyo, utetezi huo ulipingwa vikali na wabunge wa upinzani wakidai kuwa katika hilo serikali haiwezi kukwepa lawama kwa Waziri Kawambwa na naibu wake kuwajibika.
 
“Mimi nilikuwa mmoja wa wabunge waliopinga ugatuaji wa madaraka ya wizara hii kwenda Tamisemi, lakini wabunge wa CCM walitupinga vikali na kupitisha hoja hiyo, sasa leo mnatetea nini?
 
“Tamisemi iko chini ya Waziri Mkuu, kama leo tunamtetea Kawambwa na kuituhumu Tamisemi ina maana mnataka kusema Waziri Mkuu ndiye hafai,” alisema Mbunge wa Viti Maalumu Susan Lyimo (CHADEMA).
 
Mbunge wa Mhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema kuwa hakuna tatizo jingine katika Wizara ya Elimu bali viongozi wake hawana uwezo wa kuongoza.
 
“Tunawaambieni kila siku kuwa hawa watu hawana uwezo wa kuongoza hii wizara…hawawezi, na msipobadilisha hawa watu tutaendelea kuimba nyimbo hizi kila siku,” alisema.
 
Alisema kuwa serikali inajenga shule mbovu na kuwataka wananchi wapeleke watoto wao huko wakati watoto wa viongozi hawasomi katika shule hizo.
 
Kuhusu Necta, alisema kuwa tangu kuingia kwa Katibu Mtendaji wa sasa, Dk. Joyce Ndalichako na wasaidizi wake, wameziba mianya yote ya wizi wa mitihani.
 
Mkosamali alisema kuwa wanaompiga vita wakitaka aondolewe ni wale wenye shule binafsi waliokuwa wakisababisha wizi huo ili shule zao zionekane bora.
 
Joseph Selelasini wa Rombo (CHADEMA) aliwashangaa baadhi ya wabunge kuibebesha lawama Necta kwa kasoro zilizojitokeza kwenye mfumo uliotumika kusahisha mitihani ya dini, ya Bible Knowledge na Islamic Knowledge akisema serikali inaendelea kukiuka katiba kwa kujihusisha na masuala ya dini wakati nchi haina dini.
 
Chanzo: Tanzania Daima

Saturday, June 1, 2013

MAUAJI YA MWANGOSI : KIKWETE ALIKOROGA KUMPANDISHA CHEO KAMUHANDA


•  Wahariri wahoji kumpandisha cheo Kamuhanda
 
 

Na Edson Kamukara, Dodoma
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemvaa Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kumpandisha cheo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, badala ya kumchukulia hatua.


Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kumpandisha cheo Kamuhanda kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) licha ya shutuma kutoka kwa wadau mbalimbali nchini akielezwa kushindwa kuwazuia askari kumuua kikatili mwandishi wa habari wa televisheni ya Chanel Ten, Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012, katika kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.


Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, jana alilieleza gazeti hili mjini hapa jana kuwa uamuzi huo umeonyesha udhaifu mkubwa wa Rais Kikwete.


Alisema Rais Kikwete alipaswa kumchukulia hatua Kamuhanda kufuatia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kumtaja kuwa alikiuka sheria ya vyama vya siasa na kuchangia katika kusababisha mauaji ya Mwangosi.


“Rais Kikwete amefanya hivyo bila kujali kauli iliyotolewa kwa niaba yake na Ikulu kwamba angeeleza hatua yake kuhusu tukio la mauji ya Mwangosi baada ya kupatiwa ripoti ya uchunguzi wa mauji hayo,” alisema.


Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alisema baada ya Rais Kikwete kupatiwa ripoti mbili: ya Kamati ya Jaji mstaafu Ihema, Emmanuel Nchimbi na Tume ya Haki za Binadamu, hajawahi kueleza hatua alizochukua kama ilivyoahidiwa.


“Rais Kikwete kumpandisha cheo Kamuhanda kunaweza kutafsiriwa kuwa ni ‘zawadi’ kwa kazi yake iliyosababisha mauaji, sio tu ya Mwangosi bali yaliyofanywa pia na askari kwa amri yake kwa vijana wa bodaboda mkoani Ruvuma kabla ya kuhamishiwa mkoani Iringa,” alisema.


Alimtaka Rais Kikwete ajitokeze kulieleza taifa vigezo alivyotumia kumpandisha cheo Kamuhanda pamoja na tuhuma zote alizonazo.


Mnyika aliongeza kuwa hatua hiyo ya kumpandisha cheo Kamuhanda na makamanda wengine ambao wamelalamikiwa kuhusu utendaji wao akiwemo Isaya Mungulu na Thobias Andengenye katika matukio mbalimbali ya askari wa chini yao kusababisha mauaji inatoa picha kuwa matendo hayo yalikuwa na baraka ya uongozi wa juu zaidi wa serikali.



“Rais Kikwete kuwapandisha vyeo makamanda hao kumetonesha majonzi ya wote ambao ndugu zao waliuawa kikatili na Jeshi la Polisi, sehemu mbalimbali yakiwemo yale yaliyotokea katika mikutano ya kisiasa,” alisema Mnyika.


Mnyika alisisitiza kuwa Rais Kikwete alipaswa kujitokeza kutoa majibu juu ya barua aliyoandikiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ya kutaka aunde tume huru ya kijamii kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Kwamba badala yake Jeshi la Polisi ambalo makamanda wake ni watuhumiwa liliachwa lijichunguze ili kulindana na kutoa mwanya wa kuhusika kupanda vyeo badala ya kupanda mahakamani.


Jukwaa la wahariri lashangazwa
Jukwaa la wahariri nchini, limepokea kwa mshangao mkubwa kupandishwa cheo kwa Kamanda Kamuhanda, bila kujali kwamba alisukumiwa lawama na tume mbili zilizoundwa kuchunguza mauaji ya Mwangosi.


Akihojiwa na Tanzania Daima Jumamosi, Katibu Mkuu wa TEF, Neville Meena, alisema inasikitisha kuona serikali ikipuuza vilio na malalamiko ya wananchi kuhusiana na tukio hilo.


“Huyu mtu aliondoka mkoani Ruvuma akikabiliwa na tuhuma za askari wa chini yake kuwaua waandamanaji wa bodaboda na kaja Iringa amekutana na janga lingine.
“Tulitegemea katika utawala wa sheria, hata baada ya kelele za watu wengi na kutia doa kubwa katika utendaji wa polisi, angewajibishwa mara moja,” alisema Meena.
“Sehemu nyingine makamanda wengine walipendwa sana kama Gewe na Tibaigana ambao walifanikiwa kuteka nyoyo za watu kwani walijitahidi kufanya kazi kwa uadilifu.


Katibu huyo alisema waandishi wa habari wanamtazama Kamuhanda kama mtu mwenye kasoro katika utendaji kazi wake, sio tu wakiwa ni waandishi wa habari bali hata raia wa kawaida.


“Hata kama hakuua yeye, lakini kwa matukio haya hasa hili la Mwangosi kwa sababu alikuwepo tangu mwanzo hadi mwisho wa tukio, tulitegemea aondoke na si kupandishwa cheo.
“Kuwepo kwake kumeendelea kutuumiza katika tukio zima; hakuchukua hatua kuzuia hata alipoambiwa. Inaonekana kwao ni utendaji kazi bora kulingana na walivyotaka. Wametusaidia kujua sisi waandishi kuwa tuanze kuitazama serikali kwa jicho la namna gani.


Meena alisema kuwa serikali ingetumia busara kubwa katika jambo hilo, maana tafsiri itakayopokelewa na wananchi ni kwamba serikali ilifurahia mauaji haya, na labda inalea ukatili na mauaji.


Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isaac Nantanga, juzi katika taarifa yake alisema kuwa Rais Kikwete amewapandisha vyeo maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi kuwa Makamishna wa Polisi (CP) na Manaibu Kamishna wa Polisi (DCP).
Taarifa hiyo ilieleza kuwa waliopandishwa kuwa Makamishna wa Polisi ni Isaya Juma Mungulu na Suleiman Kova ambao kabla ya vyeo vyao vipya walikuwa Manaibu Kamishna wa Polisi.


Isaya Mungulu yuko Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam, ambapo Suleiman Kova ni Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Dar es Salaam.



Waliopandishwa kuwa Manaibu Kamishna wa Polisi ni Elice Mapunda, Brown Lekey, Hamdani Omar Makame, Keneth Kasseke, Abdulrahman Kaniki, Thobias Andengenye, Adrian Magayane, Sospeter Kondela, Simon Sirro na Ernest Mangu.
Wengine ni Hussein Laisseri, Anthony Joel S. Mwami, Mohamed Mpinga, Adolfina Chialo, Mpinga Michael Gyumi, Ally Mlege, Hezron Gyimbi, Michael Kamuhanda, na Jonas Mugendi.


Kabla ya uteuzi huu, maofisa hao walikuwa Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi. Uteuzi huu umeanza mara moja.

           Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima