SERIKALI imeingia katika kashfa nyingine kwenye sekta ya elimu baada ya
kudaiwa kuruhusu vitabu vyenye maelekezo yasiyo sahihi.
Mbunge wa kuteuliwa na rais, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) ndiye aliyeanika
udhaifu uliomo kwenye vitabu vilivyoidhinishwa na serikali kutumika katika shule
za msingi nchini ambapo aliviita ni sumu ya elimu.
Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Mbatia alionesha vitabu
kadhaa bungeni huku akitaja makosa mengi yaliyomo na kuhoji viliidhinishwaje na
Kamati ya Kuidhinisha Machapisho ya Kielimu (EMAC).
“Leo tunavuna tulichokipanda. Serikali imetumia fedha za chenji ya rada
kusaini mikataba na kampuni zaidi ya 10 kwa ajili ya kusambaza vitabu kwenye
shule zetu, lakini vitabu hivyo ni sumu kwa taifa,” alisema.
Alisema kuwa vitabu hivyo vimenunuliwa na fedha hizo sh bilioni 55.2 ambazo
zilitengwa na serikali kwa ajili ya manunuzi ya vitabu na mihutasari.
Alisema kampuni hizo zilipewa mkataba wa zabuni ya kununua vitabu na
mihutasari wa sh milioni 18 na ulisainiwa Machi 18 mwaka huu, huku wakitakiwa
kumaliza ununuzi na usambazaji wake Septemba mwaka huu.
Mbatia alisema kuwa vitabu hivyo vikitumika vitalisababisha taifa kufa
kielimu kwa vile watoto watajifunza mambo ambayo hayana ukweli.
Alitoa mfano wa kitabu cha Jiografia cha darasa la sita kilichoidhinishwa na
EMAC ambacho kimekosewa kwa kuandikwa ‘Jografia’.
Vitabu vingine ni cha Hisabati cha darasa la nne katika ukarasa wa 49, ambapo
imeandikwa sifuri gawanya kwa sifuri jibu lake ni sifuri wakati jibu sahihi ni
haiwezekani.
Pia alisema kitabu cha Hisabati kingine kinaonesha 2x7=15 na kitabu cha Uraia
pia kinaeleza kuwa ‘mtaa unaundwa na vitongoji mbalimbali na kuongozwa na
wenyeviti wa vitongoji.
Mbatia alisema kitabu hicho kinasema kwamba wakazi wengi wa mtaa wameajiriwa
na utumishi wa umma, viwanda na makampuni.
Alisema kampuni za Macmillan na Oxford zilizopewa jukumu la kuleta vitabu
hivyo zimeshafukuzwa nchini Kenya baada ya kugundulika kuwa vitabu vyao havina
ubora wa kitaaluma, lakini Tanzania imeendelea kuzikumbatia.
“Kama Rais Kikwete hivi karibuni akiwa Mbeya alikiri kuwa elimu yetu ina
udhaifu, kwanini wabunge wa CCM hamtaki kukubali hili?” alihoji Mbatia na
kupendekeza iundwe tume ya kudumu ya elimu itakayosimamia maslahi ya walimu,
kasoro za elimu na mengineyo.
CCM wapindisha hoja
Katika hatua nyingine, wabunge wa CCM wamelazimika kupindisha mjadala wa hoja
ya udhaifu wa elimu nchini ili kumwokoa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Dk. Shukuru Kawambwa.
Hatua hiyo imetokea bungeni mjini hapa ambapo Waziri Kawambwa aliwasilisha
hotuba yake ya bajeti kwa mwaka 2013/14 ambayo ilijadiliwa kwa siku mbili.
Kutokana na upinzani mkali ulioonekana tangu mapema kutoka kwa baadhi ya
wabunge hasa wa upinzani, wakitaka Waziri na Naibu wake Philipo Mulugo wajiuzulu
kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012, wabunge wa CCM
walilazimika kukutana kwa dharura juzi.
Katika kikao hicho kilichoketi katika Ukumbi wa Pius Msekwa juzi saa 7:00
mchana, wabunge hao wa CCM walifundana na kuafikiana kumwokoa Waziri Kawambwa
ili bajeti yake iweze kupitishwa.
Licha ya wabunge wawili wa chama hicho, Deogratius Ntukamazina (Ngara) na
Said Mtanda (Mchinga) kuwa wachangiaji wa mapema kabla ya kikao hicho na hivyo
kuishambulia wizara hiyo, waliofuata walikuja na visingizio vya kumwonesha
waziri hana tatizo.
Katika michango yao, wabunge hao walijiegemeza kwenye hoja ya mgawanyo wa
orodha ya shule za sekondari 1,200 zitakazofanyiwa ukarabati wakidai ifumuliwe
kwa vile Mkoa wa Kilimanjaro umependelewa zaidi ya mikoa mingine.
Huku wakiunga mkono hoja ya waziri kwa asilimia mia moja na kisha kuanza
kulalamikia kasoro zilizopo kwenye elimu, wabunge hao walimtetea Kawambwa kuwa
hastahili kujiuzulu kwa vile wizara yake ina majukumu mengi yanayoingilina na
Wizara ya Tamisemi.
“Jamani kusema Waziri Kawambwa ajiuzulu tunamwonea, hii wizara majukumu yake
mengi yako pia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, atawajibikaje
mwenyewe kwa matokeo haya?” walisema.
Katika utetezi huo, waliongeza kuwa bajeti ya wizara hiyo ni ndogo na hivyo
waziri amekwama kutekeleza majukumu yake huku wakilibebesha lawama Baraza la
Taifa la Mitihani (Necta) kuwa ndilo limesababisha matokeo hayo kwa kupanga
madaraja kimakosa.
Katika hatua iliyoibua msigano, wabunge hao walipendekeza serikali iunde tume
nyingine ya wataalamu kuchunguza matatizo ya elimu nchini, jambo lililopingwa
vikali na wapinzani wakihoji kwanini walikataa wazo hilo lilipoletwa na
Mbatia.
Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, aliwaponda wapinzani akisema
kuwa hawatambui kazi kubwa iliyofanywa na CCM na kumtaka Waziri Kawambwa achape
kazi bila kuwasikiliza.
Aliitaka serikali kutowapeleka walimu wapya vituoni pasipo kuwapa fedha zao
za kujikimu kwani inakuwa inatambua idadi yao, lakini akasisitiza kuwa waziri
anakwamishwa na watendaji wake.
Peter Serukamba wa Kigoma Mjini, John Komba wa Mbinga Magharibi, Yahaya
Kassim Issa wa Chwaka, Jason Rweikiza wa Bukoba Vijijini na Lutengano Kigola wa
Mufindi Kaskazini, walilalamikia upendeleo kwenye mgawanyo wa shule, walimu
kutopandishwa madaraja na Tamisemi kuondolewa majukumu ya elimu.
Hata hivyo, utetezi huo ulipingwa vikali na wabunge wa upinzani wakidai kuwa
katika hilo serikali haiwezi kukwepa lawama kwa Waziri Kawambwa na naibu wake
kuwajibika.
“Mimi nilikuwa mmoja wa wabunge waliopinga ugatuaji wa madaraka ya wizara hii
kwenda Tamisemi, lakini wabunge wa CCM walitupinga vikali na kupitisha hoja
hiyo, sasa leo mnatetea nini?
“Tamisemi iko chini ya Waziri Mkuu, kama leo tunamtetea Kawambwa na kuituhumu
Tamisemi ina maana mnataka kusema Waziri Mkuu ndiye hafai,” alisema Mbunge wa
Viti Maalumu Susan Lyimo (CHADEMA).
Mbunge wa Mhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema kuwa hakuna tatizo
jingine katika Wizara ya Elimu bali viongozi wake hawana uwezo wa kuongoza.
“Tunawaambieni kila siku kuwa hawa watu hawana uwezo wa kuongoza hii
wizara…hawawezi, na msipobadilisha hawa watu tutaendelea kuimba nyimbo hizi kila
siku,” alisema.
Alisema kuwa serikali inajenga shule mbovu na kuwataka wananchi wapeleke
watoto wao huko wakati watoto wa viongozi hawasomi katika shule hizo.
Kuhusu Necta, alisema kuwa tangu kuingia kwa Katibu Mtendaji wa sasa, Dk.
Joyce Ndalichako na wasaidizi wake, wameziba mianya yote ya wizi wa
mitihani.
Mkosamali alisema kuwa wanaompiga vita wakitaka aondolewe ni wale wenye shule
binafsi waliokuwa wakisababisha wizi huo ili shule zao zionekane bora.
Joseph Selelasini wa Rombo (CHADEMA) aliwashangaa baadhi ya wabunge
kuibebesha lawama Necta kwa kasoro zilizojitokeza kwenye mfumo uliotumika
kusahisha mitihani ya dini, ya Bible Knowledge na Islamic Knowledge akisema
serikali inaendelea kukiuka katiba kwa kujihusisha na masuala ya dini wakati
nchi haina dini.
Chanzo: Tanzania Daima
|
No comments:
Post a Comment