Watangazaji wawili wa Clouds FM, Ephrahim Kibonde na Gadna Habash wamekamatwa na polisi kwa madai ya kusababisha ajali na kutoa lugha ya matusi kwa polisi.
Kibonde na Gadna wanadaiwa kusababisha ajali hiyo jana katika eneo la Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kibonde ndiye alikuwa dereva wa gari linalodaiwa kusababisha ajali hiyo kwa kugonga gari la raia wa kigeni na kukimbia wakati askari wa usalama barabarani (trafiki) walipofika kupima ajali hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura alithibitisha kukamatwa kwa watangazaji hao, “Ni kweli tunawashikilia watangazaji hao kwa kosa la kukaidi amri ya polisi, bado tunawashikilia mpaka sasa.”
Ilidaiwa kuwa gari la Kibonde iligonga gari hilo kwa nyuma na trafiki walipofika ili kupima alikimbia, ndipo trafiki walipotumia gari lililogongwa kumfukuzia na kufanikiwa kumkamata.
Akisimulia kisa hicho polisi wa kike katika Kituo cha Oysterbay ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema Kibonde alikataa kutii sheria bila shuruti kwa kivuli cha umaarufu alionao.
“Hawa wanashikiliwa kwa kosa la kuvunja sheria za barabarani, Kibonde alikuwa anaendesha akiwa amelewa na kusababisha ajali, kama haitoshi walikimbia na kuwatolea polisi lugha chafu za matusi jambo ambalo ni kinyume na sheria,” alisema askari huyo.
Alisema walipoanza kuwafukuzia waliwakamata Kituo cha Mwenge na trafiki aliingia katika gari lake na kumwomba arudi eneo la ajali ili wakapime ajali. Kibonde aligoma na kumtaka trafiki ashuke katika gari lake, trafiki naye akagoma kushuka.
“Kibonde alikaidi tena na kuondoa gari na kuendelea na safari yake wakati trafiki akiwa ndani ya gari hiyo, aliwasiliana na wenzake ambao walianza kuifuatilia gari hiyo, walipofika eneo la Ubungo mataa, trafiki mwingine aliisimamisha gari na Kibonde alikaidi kusimama, akiwa katika hali hiyo kuna gari ilitokea ikakatisha kati ya trafiki na gari hiyo ndiyo kikawa kigingi cha gari ya Kibonde na kutiwa mbaroni,” alisema polisi huyo.
Baada ya kukamatwa, Kibonde na abiria wake walifikishwa katika Kituo cha Polisi Urafiki Ubungo saa 7:00 asubuhi na baadaye saa 8:00 asubuhi walihamishiwa katika Kituo cha Oysterbay.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Osterbay, Victor Samata aliliambia gazeti hili kuwa suala hilo lipo juu ya uwezo wake kulizungumzia kwani yeye siyo msemaji, hivyo kumtaka mwandishi amtafute msemaji wa kituo hicho.
“Sidhani kama hili ni suala la kulijadili, isitoshe mimi siyo msemaji wa hapa ingefaa atafutwe msemaji kulizungumzia hili,” alisema Samata.
Habari kutoka: www.mwananchi.co.tz picha kwa hisani ya mitandao ya kijamii
No comments:
Post a Comment