BARAZA LA MITIHANI LA TANZANIA
UFAFANUZI KWA UMMA KUHUSU KUTOJUMUISHWA KWA ALAMA ZA MASOMO YA HIARI KATIKA MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA SITA 2014
Baadhi ya wadau wamekuwa wakitaka kujua utaratibu uliotumika kukokotoa pointi za madaraja katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita (ACSEE) 2014. Hii imetokana na kuona kuwa kuna baadhi ya masomo hayakujumuishwa katika kupata idadi ya pointi kwa watahiniwa wa Tanzania Bara na wale wa Zanzibar.
Baraza la Mitihani la Tanzania linapenda kuwajulisha wadau wote kuwa ukokotoaji wa pointi za madaraja kwa watahiniwa wa Mtihani wa Kidato cha Sita huzingatia masomo ya Tahasusi (Subject Combinations) aliyoyasoma mtahiniwa kama ilivyobainishwa katika Kanuni za Mitihani (The Examinations Regulations) Toleo la mwaka 2013 kifungu cha 23(1) kinachosomeka:
“The Advanced Certificate of Secondary Education shall be awarded in four Divisions to both schools and private candidates who have conformed to entry requirements and have fulfilled the conditions of the awards. Calculations of points shall be done based on Subject Combinations approved by the Ministry of Education”,
Masomo ya Tahasusi (Subject Combinations) yanayotumika kukokotoa alama za madaraja yamebainishwa katika Waraka Namba 1 wa mwaka 2006 wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Waraka Kumb. Namba P33/8/53/Vol.I/44 wa mwaka 2012 wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar.
Baadhi ya Tahasusi zinazotumika Zanzibar zinatofautiana na zilizopo Tanzania Bara, ambapo kwa Zanzibar zipo baadhi ya Tahasusi zenye kuhusisha masomo ya hiari. Masomo ya hiari ambayo husomwa na baadhi ya watahiniwa ni pamoja na General Studies (GS), Islamic Knowledge, Basic Applied Mathematics (BAM), Divinity, Computer Studies na Arabic Language. Hata hivyo, Baraza la Mitihani hufanya tathmini na kutunuku ufaulu kwa masomo yote ya hiari ya mtahiniwa katika cheti chake ili kimsaidie katika udahili wa ngazi mbalimbali za mafunzo kulingana na matakwa ya sifa za mafunzo husika.
Taarifa za kina kuhusu utaratibu wa kutunuku matokeo ya Kidato cha Sita zipo katika kitabu cha Mwongozo wa Matumizi ya Viwango vya Ufaulu na Utaratibu wa Kutunuku Matokeo ya Kidato cha Nne na cha Sita kilichotolewa mwaka 2014. Aidha, kitabu hicho kilikabidhiwa kwa Wakuu wa Shule zote za sekondari Tanzania Bara na Zanzibar. Pia kitabu hicho kinapatikana kwenye tovuti ya Baraza la Mitihani la Tanzania (www.necta.go.tz).
Baraza la Mitihani la Tanzania linawaomba wadau wasipotoshwe na taarifa ambazo zinasambazwa katika baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambazo zina lengo la kupotosha Umma.
Imetolewa na,
AFISA HABARI NA UHUSIANO
No comments:
Post a Comment