Kwa sasa wanachama wa CHADEMA wanaoonekana ni wasaliti wakitimuliwa CHADEMA hujiunga na ACT-Tanzania ambacho kimbatizwa jina la 'Chama cha wasaliti-Tanzania' kwa haliinavyoelekea huenda hawa nao akina Shibuda, Arfi na Leticia wakatimkiwa huko au watakuwa wanachama wa Mahakama.
CHADEMA kuwatosa Shibuda, Arfi, Leticia
- Lissu asema hawavumiliki, CUF yawakana waasi
- Bunge lawatilia shaka, lazuia wasilipwe posho
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kitawafukuza wabunge wake, John Shibuda (Maswa Magharibi), Said Arfi (Mpanda Mjini) na Leticia Nyerere (Viti Maalum) baada ya kujiridhisha kwamba wameshiriki vikao vya Bunge Maalum.
Hatua hiyo inakuja baada ya wabunge hao kuripotiwa kujisajili na kushiriki vikao vya Bunge hilo kinyume na msimamo wa CHADEMA kupitia kundi lao la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambalo wamesusia wakidiai CCM imechakachua rasimu yenye mapendekezo ya wananchi.
Msimamo wa CHADEMA ulitolewa jana na Mwanasheria wake, Tundu Lissu akisema kuwa Kamati Kuu ilishatoa maelekezo kwa wabunge wote, hivyo hawamuogopi wala hawataki kumwonea mtu, kwamba ndio maana wanajiridhisha kwanza.
“CHADEMA kama mshirika wa Ukawa, tuliwazia wabunge wetu wasishiriki Bunge hilo wala vikao vya kamati zake, sasa hawa waliokwenda huko Dodoma lazima waseme wako Ukawa au CCM.
“Hawa watu ni mamluki, kwa hili wala hatutahitaji kuwaita wajieleze. Tulisema wasiende, wao wakaenda. Sasa tutuchukua hatua na kama wanataka ubunge wa mahakama wataupata,”alisema.
Lissu alisisitiza kuwa wabunge hao wameonesha njaa ya ajabu ya kukimbilia posho kwani hata kama ni shida ya kukosa fedha si kwa njia hiyo ya usaliti wanaojaribu kuufanya wakidhani watakidhoofisha CHADEMA.
“Hivi nani asiyemjua Shibuda…nani hamjui Arfi tangu ajiengue umakamu mwenyekiti wa chama au nani asiyejua mwenendo wa Leticia? Sisi hatumwogopi wala hatutamwonea mtu bali siku ya kufanya hesabu ikifika, kila mmoja ataoneshwa zake na kama kuna wengine acha waende tutawashughulikia bila kujali,”alisema
Posho
Bunge Maalum la Katiba, limeamua kuzuia malipo ya posho za kujikimu kwa baadhi ya wajumbe wa Ukawa waliojisajili bila kushiriki vikao.
Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Hamis Hamad, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubaini wajumbe hao wanafanya hila ya kujipatia fedha bila kufanya shughuli inayotakiwa.
Alisema kuwa utaratibu huo wanaufanya kujenga uhalali wa kulipwa posho ya kujikimu ya sh. 230,000 inayotolewa kila siku kwa mjumbe aliyeko Dodoma.
Kwa mujibu wa utaratibu wa malipo ya Bunge Maalum kila siku mjumbe aliyejisajili hulipwa sh. 230,000 na atakayehudhuria kikao hulipwa sh. 70,000, hivyo kufanya sh. 300,000 kwa siku.
Hamad alisema mpaka jana asubuhi wabunge wawili wa CHADEMA, John Shibuda na Leticia Nyerere ndiyo waliojisajili lakini hawakuhudhuria vikao.
Alibainisha kuwa mjumbe mwingine kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Clara Mwaituka naye alijisajili lakini hakushiriki kwenye vikao.
Alisema wamebaini kuwa licha ya wabunge hao kujisajili lakini walikuwa hawajalipwa fedha za siku saba kama walivyolipwa wenzao wanaoshiriki vikao.
Alisema kuwa alipokwenda kwa wahasibu kuangalia walivyolipwa Ukawa, alibaini kutofanyika kwa malipo, hivyo akaagiza yoyote atakayekuja asilipwe mpaka kuwe na uhakika wa kuhudhuria vikao.
“Kwa bahati nzuri watu wa uhasibu waliandika pembeni majina ya wajumbe wa Ukawa….hata Shibuda na Nyerere hawakulipwa, sasa tunataka tubane zaidi kukwepa ujanja ujanja,”alisema.
Katibu aliongeza kuwa Shibuda alitoa taarifa kuwa hatoweza kushiriki kwenye vikao vya kamati kwa madai ana matatizo ya kiafya.
“Shibuda alikuja ofisini kwangu huku mguu wake ukionekana kuwa umevimba hivyo akaomba ruhusa kwenda kupatiwa matibabu, lakini hao wengine wamejiandikisha tu na kuondoka hata hivyo hawajaonekana tena,”alisema.
Hamad aliwataja wajumbe wengine kutoka Ukawa waliojiandikisha na kuhudhuria vikao vya kamati kuwa ni Fatma Mohamed Hasan na Ally Omary Juma aliodai ni wa CUF.
Tanzania Daima, liliwasiliana na mmoja wa wajumbe wa Ukawa, Ismail Jussa Ladhu, ambaye alisema wajumbe waliotajwa na Hamad, hawatoki CUF.
“Mimi naona Katiba hafuatilii vema taarifa za wajumbe wake maana aliowataja mmoja natoka kundi la 201 mwingine anatoka chama kingine cha upinzani kisichokuamo Ukawa,” alisema.
Hamad alimtaja mjumbe mwingine aliyeonekana kuwa na msimamo wa Ukawa akitokea kundi la 201 kuwa ni Jamila Abeid, ambaye hakutaja anawakilisha kundi lipi.
Arfi awasili bungeni
Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi (CHADEMA) jana alijisajili kushiriki vikao vya Bunge Maalum huku akidai amefanya hivyo kwa kutimiza haki yake ya kimsingi.
Arfi aliwasili majira ya asubuhi na mara baada ya kukamilisha taratibu za kujisajili alisema anawawakilisha Watanzania Bara.
Alisema amepata fursa na haki ya kuwemo kwenye Bunge hilo kutokana na kuwa mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Arfi alisema licha ya viongozi wa CHADEMA kuwataka wanachama wake wasihudhurie vikao, yeye ameamua kushiriki kwa lengo la kutimiza wajibu wake kwa wananchi waliomchagua.
Alipinga msimamo wa chama chake huku akidai kuwa vyama vinataka kupokonya mamlaka ya wananchi, kwamba iwapo wataendelea kukubali hali hiyo watakuwa wanawanyima wananchi haki yao ya msingi na kikatiba.
Via: www.freemedia.co.tz
No comments:
Post a Comment