Na. Mwl. Venance.
F.K.
Shirika linalowasaidia wanafunzi
wa kike litwalo CAMFED limetoa msaada wa baiskeli na mahitaji mengine kama vile
magodoro, sale za shule, taulo za akina mama, madaftari, taa za sola na viatu
vya shule. Aidha wapo wengine waliopata pesa kwa ajili ya kulipia pango na
matumizi.
Akizungumza katika makabidhiano
mbele ya wazazi na wageni waalikwa hapo jana (tar. 05/03/2018) Mkuu wa Shule Janeth Lubasi alisema
wanafunzi takribani 60 ndiyo wanafadhiliwa na shirika hilo. Ambao kwa utaratibu
kila mwaka wanafunzi wanajaza fomu maalumu kuomba ufadhili kwa kuandika
mahitaji wanayoyahitaji kwa mwaka mzima. Kila mwanafunzi alitakiwa kuomba
mahitaji ya kiasi kisichozidi Tsh. 250,000/=.
“Kati ya wanafunzi 60 wanafunzi
47 waliomba kununuliwa baiskeli, hivyo wazazi msishangae kuona wanafunzi
wengine wanapata baiskeli wengine hapati…kila mwanafunzi amepewa kile
alichoomba.” Alisema mkuu wa shule.
Aidha aliwataka wazazi kuzingatia
kuwa vifaa hivyo ni kwa ajili ya wanafunzi walengwa tu na si vya wazazi. “Hatutegemei
kumkuta mzazi mnadani akiwa na baiskeli ya motto…baiskeli hii ni kwa ajili ya motto
tu…na wazazi ambao watoto wao wamepewa magodoro hairuhusiwi mzazi kumbadilishia
motto kudoro au kulichukua na kulitumia nyie…” alisema mkuu wa shule.
Kabla ya kumkaribisha Mbunge wa
Manyoni Mashariki, Mh. Daniel Mtuka, diwani wa kata ya Manyoni, Mh. Machibula
aliwataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao na kuhakikisha wanasoma
kwa bidii.
Mbunge wa Manyoni Mashariki
Daniel Mtuka alisema kuwa ni jambo la kujivunia sana shule ya Mwanzi kuwa
miongoni mwa shule zinazofadhiliwa na Camfed. “ndani ya mwanamke kuna kitu…ndiyo maana hawa CAMFED wameona umuhimu wa
kuwasaidia hawa watoto wa kike…jambo la muhimu hivi vifaa vitusaidie katika
kufanikisha malengo yetu ya elimu watoto” alisema.
Aidha mmoja wa wazazi ambaye
mwandishi wetu alishindwa kupata jina lake alitoa neno la shukrani kwa niaba ya
wazazi, aliushukuru sana uongozi wa shule na CAMFED kwa kuamua kuwasaidia.
“jamani sisi wengine hata uwezo wa kununua viatu pea mbili hatuna…leo
tumekabidhiwa baiskeli, viatu na vitu vingine tunasema asante asante sana yaani
tunasema asante zaidi ya asante yenyewe.” Alisema.
Nisikuchoshe ungana na mwandishi
wetu katika matukio katika picha hapa chini:
Mh. Diwani wa Kata ya Manyoni akitoa salamu zake
Mh. Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki
akimkabidhi mmoja wa wanafunzi vifaa
Baadhi ya baiskel walizopewa wanafunzi
Mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake ni mnufaika wa Camfed
akitoa neno la shukrani
Mmoja wa wanafunzi akipatiwa godoro na vifaa vingine na Mh. Mbunge
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, Mzee Msongo akitoa neno siku hiyo
Picha zimepigwa na Baba D.