Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Monday, June 27, 2016

UTEUZI WA WAKUU WA WILAYA DK KITILA MKUMBO ATEMA CHECHE


Katika ukurasa wake wa facebook Dk. Kitila ameandika haya kuhusu nafasi za Ukuu wa Wilaya:

Nimekuwa nikipigiwa simu na ndugu zetu waandishi wa habari wakitaka maoni yangu kuhusu walioteuliwa kuwa wakuu wa wilaya. Kimsingi sina maoni kabisa kuhusu walioteuliwa lakini nina maoni kuhusu nafasi yenyewe ya ukuu wa wilaya katika mfumo wa utawala wetu. 

uDC ni nafasi yenye sura nyingi lakini zote za kisiasa. Kwa uzoefu wa nyuma na utaratibu wa serikali ya CCM uDC ni sehemu ya kwapa nafasi ya kukua kisiasa na kikada vijana wa chama tawala kupitia jumuiya yao ya uvccm. Ni nafasi za kuwahifadhi makada wastaafu. Ni sehemu ya kuwasaidia waliogombea ubunge kupitia chama tawala na kushindwa. Hutumika pia kutoa fadhila kwa watu ambao wamekisaidia chama tawala katika kushinda uchaguzi kwa namna mbalimbali. Ni nafasi ambayo hutumika kuandaliwa kuja kuwa Mkuu wa Mkoa. Mpaka hapo utaona kwamba nafasi ya uDC haina tija ya maana kwa taifa. Tija pekee ni kwa chama tawala. Ni mzigo kwa wapiga kura. Ni mzigo kwa taifa na ni mzigo hata kwa Rais mwenyewe, hasa ikiwa Rais aliyejitambulisha kubana matumizi katika utumishi wa umma. Ni mzigo kwa wakurugenzi wa Halmashauri na ni mzigo mzito kwa uendeshaji wa halmashauri zetu. 

Ndiyo maana vyama vyote makini vya upinzani vimeweka katika ilani zao kufuta nafasi ya ukuu wa wilaya kama sera muhimu ya kubana matumizi na kuzipa mamlaka kamili halmashauri zetu zifanye kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo. Siku nikipata nafasi ya kumsogelea mheshimiwa Rais nitamnong’oneza jinsi ambavyo kufuta nafasi ya ukuu wa wilaya ingemrahisishia kazi ya kuwahudumia maskini kama alivyopania. Njia rahisi ya kudhihirisha azma na nia ya kubana matumizi kwa Rais wetu ni kutumia mamlaka yake kikatiba kufuta hii nafasi ya ukuu wa wilaya haraka. Hii ni muhimu zaidi kuliko kufuta/kuahirisha sherehe za Uhuru na Muungano ambazo ndio alama kuu ya Taifa letu tulipendalo. Watanzania wenzangu tumuombee sana Mheshimiwa Rais wetu ili Mungu amfungulie aione busara ya kufuta hii nafasi ya ukuu wa wilaya katika mfumo wetu wa utawala. Hayo ndiyo maoni yangu.

No comments:

Post a Comment