MALUMBANO ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanayoonekana dhahiri kuchagizwa na makundi ya urais yameendelea kushika kasi ndani ya chama hicho.
Baada ya jana Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi, Paul Makonda, kumshambulia Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kwamba anawatumia watu kusema hovyo kupitia vyombo vya habari juu ya kazi na juhudi zinazofanywa na sekretarieti, kada mwingine, Richad Kiabo, jana aliibuka kuanika majina ya waasisi wa chama cha siasa cha CCJ kilichokufa hata kabla ya kupata usajili.
Makonda alidai Lowassa anafadhili mikakati ya kupingana na juhudi za sekretarieti ya chama hicho na alipongeza kazi zinazofanywa na sekretarieti chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana na wasaidizi wake akiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, akijibu mapigo ya Makonda, Kiabo aliyekuwa mwenyekiti wa CCJ kabla ya kurejea CCM, aliyataja majina 37 na michango waliyoitoa kwa ajili ya kufanikisha maandamano ya amani ya chama hicho ya kupinga uonevu wa aliyekuwa msajili wa vyama vya siasa nchini wakati huo, John Tendwa.
Kiabo ambaye amekoleza malumbano hayo, alimtaka Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, kuwachukulia hatua wasaliti hao.
Mbele ya waandishi wa habari, Kiabo aliwataja waasisi hao wa CCJ na fedha walizochangia kwenye mabano kuwa ni pamoja na Dk. Harrison Mwakyembe (sh 300,000), Samuel Sitta (sh 500,000), Anne Kilango (sh 400,000), Nape Nnauye (sh 100,000), Paul Makonda (sh 100,000) na James Lembel (sh 400,000) ambao kwa sasa ni miongoni mwa wanachama wa CCM wanaotajwa kuwa na makundi ya urais.
Wengine ni Amina Katemi (sh 300,000), Alex Kisumo (sh 300,000), Baraka Seif (sh 300,000), Sospeter Banigwa (sh 300,000), Saleh Omari (sh 300,000), Sarah Patrick (sh 200,000), Daniel Mwaijojeli (sh 200,000), Dk. Ngonyani (sh 300,000), Elisha Eliya (sh 200,000), Emanuel Magonja (sh 200,000) na Asma Watosha (sh 300,000).
Pia wamo, Kulwa Lulelema (sh 50,000), Hamadi Maduku (sh 100,000), Flavian Nkya (sh 100,000), Gulam kutoka Zanzibar (sh 150,000), Hamad Ferej (sh 200,000), Ally Harun (sh 50,000), Masudi Kangi (sh 100,000), Gumbo (sh 150,000), Idd Kiriwe (sh 100,000), Innocent Makala (sh 200,000), Jacob Msambya (sh 200,000), Ishelula (sh 150,000), Kipute (sh 200,000), Joseph Kashindye (sh 200,000) Kamala Ng’ombe (sh 200,000) na Daniel Malongo (sh 50,000).
Kiabo alisema anashangaa kuona ndani ya CCM bado kuna wanachama na viongozi waandamizi wenye kadi mbili, yaani kadi ya CCJ na CCM na wameshindwa mpaka sasa kuzirudisha na hata kukana, ikiwemo kuwaomba radhi wanachama kwa kitendo cha usaliti.
“Nawashangaa baadhi ya wanachama ambao si waaminifu na wasaliti wa chama baadhi yao wameanza harakati za kugombea urais 2015 ili wapewe ridhaa na chama ambacho tayari walikwisha kisaliti, nami nitakishangaa chama wakati ukifika kama kitawakubalia na kuwapitisha kuwa wagombea watu wenye kadi za vyama viwili,” alisema.
Kiabo alisema watu wenye uwezo wa kuwasema viongozi wenzao mara kwa mara na wao wasijisahau kuwa hawana usafi wowote wa kusema na kuwanyoshea vidole wenzao kwa usaliti walioifanyia CCM.
Aidha, alisema wakati CCM ikielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2015 ni vizuri kikaanza kusafisha nyumba yake ili mamluki waumbuke na wasipewe nafasi ya kugombea wakati ukifika.
Kutoka jijini Morogoro, inaripotiwa kuwa UVCCM Mkoa wa Morogoro imemtaka Makonda kumwomba radhi Lowassa kwa kauli za kichochezi zinazoweza kukigawa chama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii jana, wajumbe hao wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia kundi la vijana, Jonas Nkya na Ramadhani Kimwaga, walisema kauli ya Makonda ni yake binafsi wala haihusiani na UVCCM.
Nkya alisema vijana wa Mkoa wa Morogoro wamehuzunishwa na matamshi ya Makonda akimshutumu Lowassa kuwa hafai kuwa kiongozi wa nchi hii, wala kuwa Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa CCM taifa.
Nkya alisema kuwa umoja huo hautaki kuingizwa katika masuala binafsi ambayo yanaweza kusababisha na kuchangia kukigawa chama na jumuiya zake.
Mnyukano wa sasa miongoni mwa makada wa CCM umekuja baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa Baraza la Mawaziri na kuwarejesha madarakani mawaziri mizigo waliopendekezwa na chama chake watoswe.
Baada ya uteuzi huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alitoa kauli ya kuunga mkono uteuzi huo, lakini akisisitiza chama kitaendelea kuwashughulikia mawaziri mizigo na safari hii wataelekeza mapambano hayo ndani ya Bunge na kwenye mabaraza ya halmashauri.
Kauli hiyo ilimuibua mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, ambaye alimtukana Nape kwamba ameteuliwa kimjombamjomba na hawezi kumchagulia rais majina ya uteuzi.
Kauli ya Guninita ikamuibua Makonda na sasa Kiabo, ambao duru za siasa zinasema wote wanatumiwa kwa malengo ya urais mwaka 2015
VIA: Tanzania Daima