Mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari Mwanzi iliyoko wilayani Manyoni mkoa wa Singida, amekutwa amefariki kwa kujinyonga. Mwalimu huyo aliyetambulika kwa jina la Godfrey Mtani (33) pichani juu, amekutwa amejinyonga chumbani kwake kwenye nyumba aliyopanga maeneo ya Sayuni huku sababu hasa za kujinyonga kwake zikiwa hazijafahamika wazi.
Godfrey Mtani enzi za uhai wake
Mmoja wa wapangaji mwenzake ambaye hakutaka kutaja jina lake, alidai kuwa, Mtani, alisafiri kwenda Dodoma ingawa hakujua alienda kwa tatizo gani na alirejea hapo kwake majira ya jioni siku ya jumapili ya tarehe 12/01/2014, lakini wao walishangaa kuona tangu aingie ndani siku hiyo ya jumapili hadi leo [jumatano] asubuhi hawajamuona akitoka nje huku wakisikia redio ikilia na kuna muda simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa ndipo wakaingiwa na wasiwasi.
Afisa elimu Sekondari mwenye shati jeupe
akiteta jambo na maafisa wenzake
"Kwakuwa suala la Mtani kujifungia ndani muda mrefu si mara ya kwanza, lakini kwa hili tuliona ni muda mrefu sana, we fikiria tangu jumapili mpaka leo jumatano mtu yuko ndani tu!" Alisema.
HATUA WALIYOCHUKUA WAPANGAJI
Baada ya kuona hali hiyo, wapangaji wenzake wakaamua kwenda kutoa taarifa kazini kwake maana ni jirani na mahali nyumba yao ilipo ili kumtafuta mwalimu ambaye walidhani yuko karibu naye kumjulisha hali hiyo, anasema, "Baada ya wale wenzetu kwenda kutoa taarifa, walirejea na kutujulisha kuwa wametoa taarifa kwa mwalimu mwenzake, baada ya muda kidogo tuliwaona walimu wawili wakiingia na kuelekea moja kwa moja hadi chumba cha marehemu wakiongozana na kijana mmoja wa hapa hapa nyumbani.
Baadhi ya wananchi wakiwa eneo la tukio
ILIKUWAJE WALIPOTOKA NDANI?
"Tuliwaona walimu wale wakitoka huku wakiwa kama watu waliochanganyikiwa hivi, tukawauliza vipi? wakatujibu amejinyonga, ujue tulishangaa sana?" akaendelea, "Basi wakawa kama wanashauriana jambo fulani baada ya hapo wakaondoka na kama nusu saa hivi wakawa wamekuja karibia walimu wote wa Shule aliyokuwa akifundisha."
KATIKA ENEO LA TUKIO
Watu wa maeneo jirani walikuwa wamekusanyika kila mmoja akitaka kushuhudia kilichotokea, baadaye wakawasili Maafisa Elimu Sekondari na Msingi wilaya wakiambatana na Mkaguzi Kanda [Manyoni],
Mwili huo ulichukuliwa na Polisi na kupelekwa kuhifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Manyoni kwa uchunguzi zaidi, juhudi za kumpata OCD kuzungumzia tukio hilo ziligonga mwamba baada ya kuambiwa kuwa alikuwa katika kikao.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, mwili wa marehemu unaweza kusafirishwa kesho alhamisi mkoani Mara wilayani Serengeti baada ya shughuli za kuuaga mwili wa marehemu katika shule ya Sekondari Mwanzi kukamilika.
Marehemu Godfrey Mtani alizawaliwa tarehe 11/04/1980 na mwaka 2011 alihitimu shahada yake ya kwanza katika Chuo cha Elimu (DUCE) na mwaka 2012 mwezi wa pili ndiyo aliajiriwa katika Wilaya hiyo ya Manyoni na kupangiwa Shule ya Sekondari Mwanzi.
No comments:
Post a Comment