HATIMAYE makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaokabiliwa na shtaka la kummwagia tindikali kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wameachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga.
Makada hao ambao wanatetewa na mawakili Prof. Abdallah Safari na Peter Kibatala ni pamoja na Avodius Justinian (Bukoba), Oscar Kaijage (Shinyanga), Rajabu Daniel (Dodoma), Seif Magesa (Mwanza) na Henry Kileo (Dar es Salaam).
Muda mfupi baada ya kuachiwa, vijana hao walifichua jinsi walivyopata mateso makali kutoka kwa maofisa wa jeshi la polisi wakilazimishwa kuwataja viongozi wa juu wa CHADEMA, Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, John Mnyika na Tundu Lissu kuwa wanahusika na ugaidi.
Bila kumung’unya maneno waliwataja vigogo kadhaa wa serikali, CCM na mbunge mmoja wa CHADEMA kuwa ndiyo waratibu wa mikakati hiyo ya kuwabambika CHADEMA kesi za ugaidi.
Vijana hao waliowasili mjini Igunga 12:45 jioni juzi na kupandishwa kizimbani katika mahakama hiyo saa 1:20 usiku na kusomewa shtaka lao la kufanya kitendo kilicholenga madhara mwilini.
Mapema hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Mrakibu Msaidizi, Cosmas Mboya, makada hao walidaiwa kutenda kosa la kummwagia tindikali kada wa CCM, Mussa Tesha, usiku wa Septemba 9, 2011, katika msitu wa Hanihani, Igunga.
Mbela ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ajali Milanzi, ilidaiwa na mwendesha mashtaka kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walimmwagia kada huyo tindikali sehemu za uso, puani, mdomoni na kwenye bega la kulia.
Mwendesha mashtaka alidai kuwa shauri hilo limekwenda wilayani Igunga baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, kuwafutia shtaka la ugaidi na kuamuru kwamba warejeshwe Igunga na kushtakiwa kwa kosa la kumwagia tindikali kisha wapatiwe dhamana.
“Masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama ni kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana kwa ahadi ya sh milioni 10 za maandishi kila mmoja.
Washtakiwa wote walikana shtaka hilo na kutimiza masharti ya dhamana kisha hakimu akaiahirisha kesi Septemba 10 mwaka huu itakapotajwa tena.
Katika hatua nyingine, vifijo, nderemo, vilio vya furaha na shangwe vilitawala mahakamani hapo baada ya makada hao kuachiwa kwa dhamana.
Wafuasi wa CHADEMA walifanya maandamano yaliyoongozwa na msururu wa magari, pikipiki na baiskeli wakitembea umbali wa takriban kilomita tano kutoka mjini Igunga kwa lengo la kuwapokea makada hao.
Akizungumza kwa kifupi, wakili wao Peter Kibatala, aliendelea kuishukuru Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa kuonyesha ujasiri wake na kutimiza majukumu yake ya kutoa haki.
“Namshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Simon Likelerwa, kwa weledi wake wa kutoa uamuzi ulio sahihi kisheria na ulioshiba.
“Pia naipongeza mahakama ya Igunga kwa kuwapatia dhamana washtakiwa kwa masharti yanayoendana na uzito wa jambo lenyewe kwani dhamana ni haki ya msingi kwa mshtakiwa yeyote,” alisema.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Tabora, Kansa Mbaruku, alisema kuwa pamoja na kuridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, pia hiyo ni ishara kuwa haki imezingatiwa kisheria.
Awali makada hao walifutiwa mashtaka na mahakama ya wilaya ya Igunga kisha kukamatwa tena na kupelekwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kusomewa shtaka la ugaidi ambalo hata hivyo lilifutwa na mahakama hiyo.
Mikakati ya hujuma
Wakisimulia kile kilichowapata tangu kukamatwa kwao hadi kufikishwa mahakamani, makada hao walisema kuwa walipata mateso makubwa huku wakilaghaiwa kupewa vyeo serikalini na fedha ili mradi wawahusishe viongozi wa CHADEMA na ugaidi.
Evodius Justinian (Bukoba)
Alisema kuwa alikamatwa Bukoba: “Nikakaa rumande siku tatu kabla ya kusafisirishwa hadi Mwanza. Nikiwa huko niliteswa sana ili nikubali kuwa ninajua ule mkanda wa Wilfred Lwakatare uliokuwa kwenye mitandao.
“Nilikataa, niliteswa sana nikahojiwa kama nilimmwagia Musa Tesha tindikali nilikataa. Nilisafirishwa kwa ndege kuja Dar es Salaam ambako nilipokelewa na polisi.
“Nikiwa uwanja wa ndege niliomba ruhusa kwenda chooni, askari walinifuata huko wakanitesa sana. Nilifanyiwa mahojiano na Advocate Nyombi na afande Pasua. Walinilazimisha nikubali kuwa viongozi wetu huwa wanafanya vitendo vya kigaidi,” alisema.
Alisema kuwa akiwa makao makuu ya jeshi la polisi, aliteswa sana kwa maelekezo ya Afande Pasua na Nyombi katika ghorofa ya nane, jengo la makao makuu ya polisi.
“Niliambiwa nieleze siri za Dk. Slaa, Mbowe, Mnyika na Lissu na niseme kuwa walihusika na vitendo vya utekaji na utesaji, nilipokataa nilipigwa shoti za umeme ili nikubali kusema.
“Walikuwa wametafuta hata waandishi wa habari wakisubiri nikubali ili wanirekodi. Nilitoa maelezo kwa kulazimishwa huku nikiteswa. Nilipata nafuu baada ya wakili wangu, Nyaronyo Kicheere, kuja ndipo nikaeleza nilivyofanyiwa ukatili,” alisema.
Alisema kuwa alisafirishwa toka Dar es Salaam hadi Igunga na kwamba kila walipopita alitambulishwa kwa makamanda wa polisi kuwa ni mtu hatari sana.
Seif Magesa (Mwanza)
Alisema kuwa alikamatwa Mwanza na mabaunsa wa Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, aliyefukuzwa CHADEMA, wakiambatana na Adam Chagulani ambaye pia alifukuzwa pamoja na baadhi ya maafisa wa Usalama wa Taifa.
“Nilipelekwa ofisi za Usalama wa Taifa. Nilihojiwa nikiulizwa mimi ni nani katika CHADEMA na kwa nini huwa nawasiliana na Mbowe, Dk. Slaa, Lissu au Mnyika,” alisema.
Alisema kuwa aliuzwa kama viongozi hao wanahusika na utekaji wa watu mbalimbali unaotokea nchini na alipokataa aliteswa sana kuanzia saa 3 hadi 7 usiku.
“Nilipigwa shoti za umeme kwa maelekezo ya afande Pasua. Yeye alikuwa anakuja kuniaga kuwa anaenda kunywa pombe, vijana watafanya kazi yao. Waliniambia kuwa Lwakatare alikuwa amenitaja kuwa mimi nafanya vitendo vya kigaidi. Nilikataa kata kata,” alisema.
Aliongeza kuwa Aprili 23, mwaka huu, waliwaleta mama yake mzazi, mama mkwe na mkewe huku wakimdhalilisha mbele yao lakini alikataa kubadili maelezo yake.
“Siku moja nikiwa nahojiwa simu ya afande aliyekuwa ananihoji ilikuwa karibu; kiongozi mmoja wa CCM (anamtaja) alipiga simu akisema kama nimekataa kusema lolote nipelekwe Igunga ambako nilipelekwa nikasomewa shtaka la kummwagia tindikali Musa Tesha,” alisema.
Oscar Kaijage (Shinyanga)
“Mimi nilikamatwa, nikaambiwa niwasaidie askari kufahamu wizi wa milioni 100 uliokuwa umefanyika kwa njia ya mtandao kwa kuwa mimi ni wakala wa Airtel.
“Lakini nilipokubali kwenda na askari kituoni nikawekwa chini ya ulinzi. Ghafla nikapelekwa kwa mkuu wa upelelezi akanielekeza kuwa nikapekuliwe nyumbani kwangu kama kuna silaha ya aina yoyote au chupa zenye majimaji. Nilipekuliwa hawakupata kitu. Ilikuwa yapata saa 5 mchana,” alisema.
Aliongeza kuwa ilipofika saa 12 jioni, alipelekwa tena kwenye ofisi ya mkuu wa upelelezi, akakutana na askari alioambiwa wanatoka Dar es Salaam.
“Hapo nikamkuta afande ninayemfahamu, anaitwa Pasua kwa kuwa aliwahi kufanya kazi Shinyanga na Simiyu. Walinihoji kwa nini nina namba za viongozi wa CHADEMA. Nikawaabia, ‘mbona hamuulizi za wale wa CCM?’,” alisema.
Alisema kuwa alijibiwa kuwa wanajua hana kosa ila wanataka ushirikiano aseme kuwa Mbowe, Slaa, Mnyika na Lissu wanahusika na utekaji unaotokea nchini.
“Nilikataa. Afande Pasua nikamwambia anajua kazi yangu na mimi namjua yeye ndipo wakasema sasa kwa kuwa sitoi ushirikiano nitaunganishwa kwenye kesi ya kummwagia Musa Tesha tindikali huko Igunga,” alisema.
Aliongeza kuwa alipelekwa Igunga na wakati wanahojiwa na askari wa kutoka makao makuu, walikuwa wanafanya siri hata OCD wa pale alikuwa haruhusiwi kusikia.
Rajabu Kihawa (Dodoma)
Alidai kuwa alichukuliwa Dodoma baada ya kupigiwa simu na msichana mmoja aliyedai kuwa na maagizo kutoka kwa kaka yake anayesoma naye Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Nilikataa lakini alikuwa anapiga simu kila mara, nikaona ngoja nikamsikilize. Nilipofika kabla sijaongea naye nilikamatwa na maafisa sita wa polisi waliojitambulisha, wakaninyang’anya simu zote na kunipeleka polisi.
“Walinihoji kama najua mkanda wa Lwakatare, nikasema sijui. wakanihoji kama viongozi wa CHADEMA wanahusika na utekaji unaoendelea nchini, nako nikasema sijui,” alisema.
Alisema kuwa baada ya hapo alipelekwa na kufungiwa Chamwino siku mbili bila kupewa chakula kisha askari wakaja wakamuuliza kama amebadili msimamo.
Alitolewa akapelekwa hoteli ya Nam, ambapo aliwakuta vijana waliofukuzwa kwenye uongozi wa Bavicha (anawataja) meya mmoja wa Mwanza na diwani aliyefukuzwa CHADEMA na kijana mwingine wa chama hicho mkoa wa Pwani aliyevuliwa uongozi wa Bavicha.
“Niliombwa nikubali kupewa sh milioni 30 ili nikubali kurekodiwa nikisema kuwa Mbowe, Dk Slaa, Lissu na Mnyika wanahusika na vitendo vya kigaidi na utekaji.
“Nilikataa. Baadaye niliingizwa katika chumba kimoja cha hoteli hiyo nikakuta mbunge mmoja wa CHADEMA kutoka Kanda ya Ziwa (anamtaja) akaniambia, ‘angalia huku’ akinionyesha simu yake kuwa alikuwa akiwasiliana na Rais,” alisema.
Kihawa aliongeza kuwa aliahidiwa kupewa cheo kizuri serikalini na fedha ili mradi akubali kuwa viongozi hao wa CHADEMA wanafanya vitendo vya kigaidi.
“Nilimuuliza kwa nini alikuwa ananishauri hivi wakati yeye ni mbunge wa chama chetu. Akasema mimi nilishinda ubunge sio kwa sababu nipo CHADEMA, bali ni muhimu hata akiondoka CHADEMA.
“Nilikataa kukubali ushauri wao ndio niliambiwa napelekwa Igunga kuunganishwa kwenye kesi ya Musa Tesha,” alisema.
Henry Kileo (Dar)
Alisema kuwa alipigiwa simu na maafisa wa polisi makao makuu Juni 17, mwaka huu, wakimwarifu kuwa wanataka kufanya mahojiano naye lakini hawakusema ni kuhusu nini.
“Juni 21, mwaka huu, wakili wangu Peter Kibatala na John Mnyika (mbunge wa Ubungo) tulienda polisi makao makuu, nilihojiwa mambo mbalimbali likiwemo tukio la kummwagiwa tindikali Musa Tesha.
“Nilicheka sana kwa kuwa kabla ya kuitwa nilipata taarifa za kikao kilichofanyika Dodoma ili kuniunganisha na kesi ya ugaidi. Mahojiano yalifanyika wakati tayari kuna kesi iliyokuwa inaendelea huko Igunga,” alisema.
Kileo alisema kuwa baada ya mahojiano hayo na kuandikisha maelezo saa 11.30 jioni, polisi walimnyima dhamana na kumpeleka rumande ya kituo kikuu cha polisi alikolala.
“Jumamosi ya Juni 22, familia yangu ilikuja kunitembelea ikakatazwa lakini baadaye wakili wangu aliwasiliana na makao makuu ya polisi ndipo wakaruhusiwa kuniona.
“Juni 22, mwaka huu, nilisafirishwa kwa ndege nikapelekwa Igunga kuunganishwa kwenye kesi ya kummwagia tindikali Musa Tesha baada ya kukataa kujibu maswali ya kuwahusisha viongozi wa CHADEMA na vitendo vya utekaji vinavyotokea nchini,” alisema.
Habari kwa hisani ya gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment