Wairaqw ni moja ya
makabila matatu tu Tanzania ambalo ni jamii ya Wakushi au Wahamitiki wenye asili
yao kwenye nchi za Ethiopia tofauti na wengi wanavyoamini kuwa asili yao ni
mesopotamia yaani Iraq ya sasa(mengine ni Wambugu waliopo Tanga na Wagorowa au
wafyomi waliopo Babati). Utafiti wa kiathropolojia na hata vinasaba (DNA)
uliofanyika unathibitisha kuna uhusiano mkubwa kati ya Wairaqw na hao wakushi wa
Ethipia na Eritrea, kuanzia muundo na matamshi ya lugha, miili (body structure),
mavazi na hata shughuli za kila siku ikiwemo hata michezo kwani Wairaqw kama
walivyo waethipia wanasifika kwa riadha na wamefanana katika kila
hali
Kutokana na sababu
ambazo hazifahamiki japo inaaminika kuwa ni kwa sababu ya vita au njaa ya mara
kwa mara inayoikumba eneo hilo la pembe ya Afrika, kundi moja la watu lilihama
kuelekea kusini kufuata bonde la ufa kwa miaka mingi sana. Walipofika kaskazini
kwa Tanzania ya sasa, wakagawanyika makundi mawili ambapo kundi moja dogo
lilielekea mashariki na kundi lingine likaendelea na safari yao wakifuata bonde
la ufa kuelekea kusini. Kundi hilo dogo lilifika mpaka milima ya usambara Tanga
na kukaa huko mpaka leo ambao ndio wanaofahamika kama Wambugu.
Inasemekana kundi
kubwa liliendelea kusonga mpaka kusini mwa Tanzania hadi Iringa wakaishi huko
kwa miongo mingi sana kabla ya kuamua kurudi kaskazini baada ya kuona eneo hilo
haliwatoshi baada ya kustawi sana hapo. Katika thesis yake ya PHD, Dr. Jackson
Makwetta ambaye ni Mhehe aliandika kuwa jina la wahehe limetokana na kabila moja
dogo ambalo liliishi zamani karibu na wahehe ambalo kwa sasa lipo wilayani Mbulu
mkoani Arusha (sasa Manyara) ambalo wao kila wakimwona mtu asiye wa kabila lao
walimwita Hee! Hee!
Lakini pia,
masimulizi ya wazee wa kiiraqw yanaanzia kwenye sehemu inayoitwa Gusir Ma/angwatay, nchi inayoelezwa kuwa ni ya
baridi sana iliyopo kusini, ambapo hawakumbuki wala hakuna masimulizi
yanayoeleza kabla ya kufika hapo walitoka wapi lakini wanajua baada ya kuondoka
hapo wakafika sehemu inayoitwa Gusir Tiwalay yaani
sehemu tuliyopigwa. Hapa ndipo historia ya Wairaqw ilipoandikwa upya
na kuchukua sura nyingine kabisa, eneo hili inasemekana ni kati ya Babati,
Hanang na Kondoa.
Wakiwa hapa,
wairaqw walistawi sana wakiwa na ng`ombe na mazao ya kutosha, wakashamiri katika
michezo na mafunzo ya kivita lakini hawakuwa na watu wa kupigana nao. Masimulizi
yanaeleza kuwa katika kipindi hiki mchezo wa kupigana kwa fimbo yaani Ilgendi
ulishamiri sana ambako kulikuwa na hadi mashindano ya kutafuta bingwa wa mchezo
huo. Vijana wakajawa na kiburi na kuona wao ni wao, wakamshinikiza kiongozi wao
aliyeitwa Haymu Tippe awaletee watu wa kucheza nao (kupigana nao) na kumteka
mtoto pekee wa Haymu na kumtishia kuwa kama hatawaleta watu wa kupigana nao
watamuua huyo mtoto. Japo Haymu Tippe aliwaasa hasa baada ya ramli yake kuonesha
madhara makubwa yatakayotokana na vita hivyo lakini vijana hao waliushikilia
msimamo wao, walidai vita.
Haymu akaenda
akawafuata wadatoga lakini kabla hawajafika, Haymu alitoroka na baadhi tu ya
watu wa ukoo wake (Tippe) na ukoo wa Duwe na Naman
(wengine wanadai ni Masaay) ambao ndio waliomsikiliza. Waliobaki
nyuma na kusubiri vita walimalizwa wote na hakubaki hata mtu moja. Katika
kukimbia huko, Haymu alikuwa na mpwa wake (mtoto wa dada yake) aliyeitwa Gortoo
ambapo katika kukimbia kuelekea ukingo wa bonde la ufa kwa kaskazini
waligawanyika huku Gortoo akiwangoza kundi dogo kuelekea mlima Kwaraa uliopo
Babati na Haymu Tippe na kundi lingine wakielekea mlima Hanang (/Anang) lakini
wakaamua kukimbilia kwenye kingo za bonde la ufa eneo la Madunga na kisha
kufuata kingo hizo kuelekea Kaskazini Mashariki hadi milima ya Tlahhara na Nou
hadi Irqwar Daaw sehemu inayoitwa Mama Isara.
Gortoo na kundi
lake wakakaa huko Kwaraa na maeneo ya Babati na ndio wakawa kabila la Gorowa au
Wafyomi ambao kwa sehemu kubwa wamefanana na wairaqw isipokuwa baadhi ya
matamshi ya maneno kutokana labda na mabadiliko ya mazingira lakini
wanasikilizana.
Wairaqw waliishi
hapo Mama Isara kwa miaka mingi sana na kuanza kuongezeka kutoka hizo koo tatu
tu, wakaanza kupokea watu kutoka koo mbalimbali (assimilation) na kuunda koo
mpya, mfano ukoo wa Bayo uliundwa na Wanyiramba waliofikia kwa mtu anayeitwa
Bayo na kisha kuitwa Manda do Bayo! Aidha ukoo mkubwa kuliko wote wa Wairaqw
ambao ni Sulle asili yao ni Wadatoga na utafiti unaonesha kuwa wadatoga wote
wanaopakana na Wairaqw wanazungumza Kiiraqw na zaidi ya nusu ya hao wadatoga
wanajitmbulisha kama Wairaqw tena wengi wa hao wazazi wote wawili wakiwa
wadatoga.
Baada ya kukaa
Mama Isara kwa miaka mingi na baada ya sera ya serikali ya kikoloni ya
Kiingereza kuamua kufyeka maeneo kuondokana na mbung`o waliokuwa wanasababisha
tauni, Wairaqw walianza kutoka huko milimani na kujaza maeneo ya Karatu, Mbulu,
Babati, Hanang na kusonga magharibi hadi Haydom kote huku wakisonga nyuma ya
Wadatoga ambao huhamahama kutafuta malisho na ndio maana majina karibu yote ya
huku yanaasili ya Kidatoga.
Je! jina Wairaqw ni Wambulu! na nini asili ya jina Mbulu? itaendelea kesho?
No comments:
Post a Comment